MASWALI YA KUJADILI: ZEKARIA 1-1-21
- Maneno mazuri na yenye faraja yana msaada gani kwa aliyeumia na aliye katika hali ya kukata tamaa? Je utulivu katika jamii, familia, na katika taifa ni wa muhimu ili kuwa na maendeleo ya kweli? Huwa si gharama kubwa kumsamehe unayempenda. Mungu amelithibitisha hilo mara nyingi kwako na kwangu. Je kusamehe waliokukosea ni sehemu ya maisha yako?
- Je, mtu aweza kuathirika ikiwa Mungu atawakasirikia baba zake? Ni mambo gani yanayoweza kusababisha Mungu kukasirikia baba za watu? Mtu ana wajibu gani kwa baba waliokasirikiwa na Mungu? Kati ya Mungu na wale waliotanga mbali na Mungu ni yupi anayepaswa kutangulia kumrudia mwenzake? (Yohana 6:64-65)
MASWALI YA KUJADILI: ZEKARIA 2:1-13
- Mungu anaahidi kuwa ukuta wa moto na kuuzunguka Yerusalemu pande zote. Unapata faraja gani unapojua kuwa Mungu amezungushia ukuta wa aina hiyo hiyo wale wamchao? (Zaburi 34:7). Wale wawagusao watu wake wanagusa mboni ya Mungu. Umewahi kushuhudia watu waliowagusa watu wa Mungu na wakapata madhara makubwa sana? Je unajisikia salama zaidi kumtumikia Mungu?
MASWALI YA KUJADILI: ZEKARIA 3:1-10
- Kuna nyakati katika maisha yako umewahi kuhisi Shetani akiwa mkono wako wa kuume akijaribu kushindana nawe? Ni kipi hutokea mara nyingi kati ya hisia za uwepo wa Mungu na hisia za uwepo wa Shetani maishani mwako? Kwa nini BWANA aliingilia kati ugomvi baina ya Shetani na Yoshua? Nguo chafu za Yoshua zinawakilisha nini? (Isaya 64:6). Mavazi ya thamani aliyovikwa Yoshua yanawakilisha nini? (Ufunuo 19:8).
- Kwa nini Shetani anashindana na Kuhani Mkuu? Kuna nini anachofanya Kuhani mkuu kinachomkera Shetani? Kwa nini Mungu aliingilia kati ugomvi kati ya Shetani na Joshua? Kipi sahihi kati ya kumkemea Shetani na kumtaka Mungu amkemee? Kwa nini nyakati fulani Yesu alimkemea Shetani na nyakati zingine alitaka Mungu ndiyo amkemee? (Mathayo 17:18; Yuda 1:9).
- Kazi ya ukuhani anayofanya Yesu sasa ina umuhimu gani katika ukombozi wa wanadamu? (Waebrania 2:17). Nguo chafu sana alizokuwa amevaa Yoshua zinawakilisha nini kiroho? (Isaya 64:6). Je mavazi ya thamani aliyovikwa Yoshua yanawakilisha nini? (Ufunuo 19:8). Je, mtu mwenye tabia mbaya ya dhambi anasimamaje mbele ya Mungu aliye mtakatifu sana? Je anaweza kuwa salama? Nafasi ya kuhani katika mazingira hayo ni nini?
- Je haki ya Kristo ni vazi lenye thamani nyingi? (Wailipi 3:9). Haki ya Kristo inamuokoaje mdhambi? (Warumi 5:19). Je, baada ya kuhesabiwa haki ya Kristo mwanadamu anapaswa kuendelea kuishi maisha ya dhambi? (Warumi 6:1-2). Je aliyehesabiwa haki ana haki ya kujitangaza kuwa amekamilika? Je kuenenda kwa kufuata maagizo ya Mungu ni sehemu ya kuukulia wokovu?
MASWALI YA KUJADILI: ZEKARIA 4:1-14
- Mungu amekusudia ufanye mambo makubwa ya kubariki watu yatakayoacha alama duniani. Je jambo hilo linawezekana kwa kila mtu au kwa wale wenye uwezo tu? Ili moto unaowaka kwenye taa usizimike unahitaji mafuta. Ili moto wa injili usizimike unahitaji mafuta gani? Nini kinazuia moto huo kuwaka sasa kwa viwango vya kanisa la awali?
- Je, umewahi kuamshwa kwenye usingizi na Mungu kama mtu aamshwavyo kwenye usingizi wake? Uliamshwa ili uombe au ujihadhari na hatari inayokukaribia? Je ulikubali kuamka au ulikaidi? Unahitaji kumwambia nini ili uwe miongoni mwa wale wanaoamshwa ili kiomba au kujihadhari na hatari inayokunyemelea?
- Je umekuwa ukitumainia uwezo wako kutii maagizo ya Mungu au kufanikisha mipango yako? Je Mungu anakusudia kufanikisha mipango yako kwa nguvu zako au kwa uwezo wa Roho wake? Je, kuna wakati tumeshiriki kumsaidia Mungu pale ambapo hajatutaka tumsaidie?
- Kudharau siku ya mambo madogo ni nini? Kwa nini mlima mkubwa mbele ya Zerubabeli huwa tambarare? Je tunahitaji uwezo wa Roho Mtakatifu kuifanya milima mikubwa kuwa tambarare? Milima mikubwa maishani mwetu hufananishwa na nini? Matawi mawili ya mizeituni yanawakilisha nini?
- Mungu amekusudia ufanye mambo makubwa ya kubariki watu yatakayoacha alama duniani. Je jambo hilo linawezekana kwa kila mtu au kwa wale wenye uwezo tu? Ili moto unaowaka kwenye taa usizimike unahitaji mafuta. Ili moto wa injili usizimike unahitaji mafuta gani? Nini kinazuia moto huo kuwaka sasa kwa viwango vya kanisa la awali?
MASWALI YA KUJADILI: ZEKARIA 5:1-11
- Gombo la chuo lirukalo linaashiria nini? Kitu gani hupelekea eneo fulani la dunia kulaaniwa? Je eneo lililolaaniwa au mtu aliyelaaniwa ana uwezekano wa kutoa jambo lolote lililo jema? Je laana ikishatolewa ina uwezekano wa kubatilishwa? Gombo la Chuo lirukalo lina uhusiano gani na injili inayowaendea watu kupitia malaika watatu warukao katikati ya mbingu? (Ufunuo 14:6-7).
- Ni nani walio na jukumu la kupeleka ujumbe huo leo hii? Je hii inaashiria kuwepo kwa teknolojia ya mawasiliano itakayorahisisha kazi hiyo? Ujumbe utokao kwenye Gombo la chuo unaoruka katikati ya mbingu utahusisha kushika Amri Kumi za Mungu? Unadhani ni Amri gani katika zile kumi zilizokanyagwa zinazohitaji kuhubiriwa sana?
MASWALI YA KUJADILI: ZEKARIA 6:1-15
- Farasi wa kitabu cha Zekaria 6:2-8 wana mfanano na tofauti gani na farasi wa Ufunuo 6:2-8? Pepo zinazotajwa katika Zekaria 6:5 zinafananaje na pepo za Ufunuo 7:1?. Yesu ni Kuhani mkuu ajetiye juu ya kiti cha enzi. Je wewe na mimi ni makuhani tutakaojeti juu ya kiti cha enzi?
- Kutakuwa na kuhani kwenye kiti chake cha enzi. Kwa nini ofisi ya uuhani na ofisi ya kifalme zinaunganishwa pamoja? Kulikuwa na mapungufu gani wakati ofisi ya ukuhani ilivyotenganishwa na ofisi ya kifalme? Shauri la amani linalotajwa hapa ni lipi? Shauri hili litakuwa baina ya nani na nani?
- Kuna mfanano gani kati ya farasi wanaotajwa hapa na wale wa Ufunuo 6:2-8? Kuhani atakayekaa kwenye kiti cha enzi anayetajwa hapa ni nani? Kwa nini katika mbingu mpya na nchi mpya cheo cha ukuhani na ufalme vitaunganishwa? (Ufunuo 16:17) hao wawili waliofanya shauri walikuwa nani na nani?
MASWALI YA KUJADILI: ZEKARIA 7:1-14
- Jibu la Mungu kwa watu wa Betheli juu ya kufunga kwao linaonyesha kutotambuliwa juu ya kufunga kwao. Inakuwaje mtu anafunga kwa ajili ya Mungu lakini Mungu hatambui na wala hamjulishi mfungaji mpaka pale anapokuja kuuliza? Je, kuna uwezekano wa kufanya matendo ya dini yasiyo ya kiroho? Unapofanya matendo mema kwa lengo la kujipatia sifa hiyo huwa ni dhambi? Matendo kama hayo Mungu anayapokeaje?
MASWALI YA KUJADILI: ZEKARIA 8:1-23
- Je, Mungu asipokuwapo katikati ya jambo lolote la kidini jambo hilo linakuwa na thamani yoyote? Utajuaje kama Mungu yupo kwenye jambo unalofanya au la. Kwa nini Mungu anawahimiza Yuda mikono yao iwe hodari ili yale mema anayoyatabiri kwa ajili yao yatimie? Kuna uhusiano gani kati ya kupokea mibaraka na kuwa hodari? Je Mungu aweza kubadilisha laana iliyo juu yetu iwe baraka?
- Kuwa watu wa Mungu katika kweli na katika haki kunawezeshwa na nini na nani? Je, Mungu ana mchango katika kuifanya ardhi itoe rutuba na mazao? Je unauona unabii wa watu kumi wa lugha zote za mataifa wakiushika upindo wa Myahudi kwa kuwa imethibitishwa kuwa Mungu yupo Pamoja nao? Nini kifanyike ili kuleta uamsho wa kweli kwa watu wa Mungu?
MASWALI YA KUJADILI: ZEKARIA 9:1-17
- Mungu ana mapambano yasiyokoma kati yake na kiburi cha Mwanadamu. Unadhani kwa nini anakiandama sana kiburi cha Mwanadamu? Huyu mfalme mnyenyekevu na mwenye haki anayetajwa katika fungu la 9 ni nani? Je, watu wenye kiburi wanahitaji mfalme au mtawala mnyenyekevu au mtawala mbabe? Je kuna tumaini la Ushindi mnapoongozwa na mtu mnyenyekevu?
MASWALI YA KUJADILI: ZEKARIA 10:1-12
- Shughuli za kilimo kwa sehemu kubwa zinategemea kuwepo kwa mvua za kutosha zisizo na madhara. Kwa nini Mungu huwanyeshea mvua yake wema na waovu? Je ipo haja ya kumrudishia Mungu kwa mazao ya mashambani tuyapatayo mwaka kwa mwaka?
MASWALI YA KUJADILI: ZEKARIA 11:1-17
- Yesu ndiye mchungaji mwema ayatoaye maisha yake kwa ajili ya kondoo wa malisho yake. Je alistahili kupewa huo ujira wa vipande thelathini vya fedha? Je unapoona dhuluma ya aina hiyo hiyo ikitendwa katika jamii yako unachukua hatua gani?
MASWALI YA KUJADILI: ZEKARIA 12:1-14
- Je, Mungu ameahidi kuwamwagia watu wake Roho ya neema na kuomba? Unadhani watu wa Mungu wanaihitaji Roho hiyo wakati huu? Dalili ya kuwa umemwagiwa Roho ya kuomba ni ipi? Je kumwagiwa Roho huandamana na kumtazama yeye ambaye walimchoma? (Yohana 7:39). Huyo waliyemchoma ni nani? (Yohana 19:37).
- Uamsho ni lazima uandamane na kutubu na kuungama dhambi? Maombi ya Pamoja yanatofautianaje na maombi ya mtu mmoja mmoja? Je wakati wa maombi ya kuutafuta uso wa Bwana ipo haja ya kuwatenga wanaume peke yao na wanawake peke yao?
- Kwa nini Mungu anakusudia kuifanya Yerusalemu kuwa kikombe cha kuyumba-yumba kwa watu wa kabila zote? Yerusalemu inawakilisha nini? Kwa nini wakuu wa Yuda wamefananishwa na kinga cha moto katika miganda? Je ili Yerusalemu ikae mahali pake inatakiwa itendewe nini? Unaiona hali hiyo ikitokea katika kanisa lako? Ni nini ambacho Mungu anakusudia kukiteketeza kwenye kanisa la Kikristo ili kanisa hilo likae mahali pake?
- Je, ni sahihi kusema wenyeji wa Yerusalemu ni nguvu zangu? Je kuna ubaya kuwatukuza waumini wa kanisa kuliko kanisa na Mungu? Onyo kwa Laodikia linalenga kushusha kiburi cha wanadamu na kumwinua Mungu? Je tabia ya kuabudu watu kuliko Mungu unaiona ikishamiri katika kanisa lako? Je kuikemea tabia hiyo ni sawa na kuwasha moto msituni?
- Je ushindi wa kanisa la Mungu unategemea wanavyopokea maonyo? Je kanisa linahitaji sasa Roho ya neema na Roho ya kuomba ili liwe na nguvu ya kukabili changamoto zijazo? Je kupokea maonyo ni njia ya kumwagiwa Roho hiyo? Huyo tuliyemchoma tunayepaswa kumwangalia ni nani? Je wanadamu wote wanahusika na kile kitendo cha kumchoma Yesu mkuki ubavuni kilichofanywa na Askari wa Kirumi? (Yohana 19:33-34).
- Je kuna uhusiano gani kati ya kumtukuza Yesu na kupokea nguvu za Roho Mtakatifu? (Yohana 7:39). Je, kumwangalia Yesu ni kutafakari juu ya wokovu aliotununulia? (Waebrania 12:2-3). Maombi ya faragha yana nguvu na nafasi kiasi gani katika maisha yako?
MASWALI YA KUJADILI: ZEKARIA 13:1-9
- Huyo mwenye jeraha za mikononi alizotiwa kwenye nyumba ya rafiki zake ni nani na kisa cha kutiwa jeraha hizo ni nini? Kwa nini alama za majeraha ya Yesu za mikononi na miguuni zitabaki bila kufutika milele zote? Mafungu matatu yanayotajwa katika fungu la tisa yana uhusiano wowote na siku tatu za ibada za Ijumaa, Jumamosi, na Jumapili?
MASWALI YA KUJADILI: ZEKARIA 14:1-9
- Siku ambayo mfalme juu ya nchi yote atakuwa mmoja na Yerusalemu utakaa salama inakaribia. Huyo mfalme atakayesababisha amani ya kweli na ya kudumu atatokea wapi? Unafanyaje ili kuwa raia wa ufalme huo? Unajisikiaje kuwepo kwenye ufalme huo kama raia na mtawala katika ikulu ya mfalme?
- Je sikukuu ya vibanda au makambi bado ina umuhimu leo? Mojawapo ya faida ya sikukuu za vibanda ni nini? Je kuwa na sikukuu ya vibanda bila kuwa na vibanda kwa ajili ya malazi na shughuli za mkutano ni kuitendea haki sikukuu hiyo? Je wageni wana umuhimu wa kuhudhuria Makambi?