ASILI YA MWANADAMU
Asili ya mwanadamu kabla hajatenda dhambi ilikuwa ya ukamilifu. Alikuwa mwenye haki kwa kuwa alimwamini Mungu kwa asilimia zote na bila kumtilia mashaka yoyote. Alipotenda dhambi alipoteza vazi la haki na kuanzia wakati huo mwili ukawa mtumwa wa dhambi ukitumikishwa katika dhambi. Jitihada zozote za kuirudia asili ya mwanadamu ya awali nje ya majaliwa ya Mungu haziwezi kufanikiwa na badala yake zinakuwa machukizo.
- Nani aliitumbukiza jamii ya wanadamu kwenye dhambi kati ya Adamu na Hawa?
Yakobo 4:17 “Basi yeye ajuaye kutenda mema, wala hayatendi, kwake huyo ni dhambi.”
Warumi 5:12 “Kwa hiyo, kama kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi.”
1 Timotheo 2:14 “Wala Adamu hakudanganywa, ila mwanamke alidanganywa kabisa akaingia katika hali ya kukosa.”
Mwanzo 3:6-7 “Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala. Wakafumbuliwa macho wote wawili wakajijua kuwa wa uchi, wakashona majani ya mtini, wakajifanyia nguo.”
- Kwa nini dhambi ya Adamu iliathiri jamii yote ya wanadamu hata wale ambao hawakuwepo kwenye tukio la kwanza?
Dhambi ilipoingia kwa Adamu iliharibu vinasaba vya Adamu na Hawa na kufanya watoto wanaozaliwa wazaliwe wakiwa na vinasaba vyenye uraibu wa uovu.
Warumi 5:13-14 “Maana kabla ya sheria dhambi ilikuwamo ulimwenguni, lakini dhambi haihesabiwi isipokuwapo sheria; walakini mauti ilitawala tangu Adamu mpaka Musa, nayo iliwatawala hata wao wasiofanya dhambi ifananayo na kosa la Adamu, aliye mfano wake yeye atakayekuja.”
Zaburi 51:5 “Tazama, mimi naliumbwa katika hali ya uovu; Mama yangu alinichukua mimba hatiani.”
Warumi 3:23 “Kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu.”
- Mwili wa dhambi unakabiliwa na changamoto zipi ambazo hauwezi kuzikwepa?
Mwili wa dhambi unakabiliwa na ugumu katika kutii maagizo na hasa sheria kwa kuwa nia yake ipo kinyume chake.
Warumi 7:14-15 “Kwa maana twajua ya kuwa torati asili yake ni ya rohoni; bali mimi ni mtu wa mwilini, nimeuzwa chini ya dhambi. Maana sijui nifanyalo, kwa sababu lile nilipendalo, silitendi; bali lile nilichukialo ndilo ninalolitenda.”
Warumi 8:7 “Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii.”
Warumi 7:19-20 “Kwa maana lile jema nilipendalo, silitendi; bali lile baya nisilolipenda ndilo nilitendalo. Basi kama lile nisilolipenda ndilo nilitendalo, si mimi nafsi yangu nilitendaye, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu.”
- Je katika mazingira hayo ambayo sheria ya dhambi inafanya kazi mwilini na kuitawala nia kuna matarajio ya mtu kufanikiwa kutenda jema?
Yeremia 13:23 “Je! Mkushi aweza kuibadili ngozi yake, au chui madoa-doa yake? Kama aweza, ndipo na ninyi mwaweza kutenda mema, ninyi mliozoea kutenda mabaya.”
Warumi 3:12 “Wote wamepotoka, wameoza wote pia; Hakuna mtenda mema, la! Hata mmoja.”
Luka 18:19 “Yesu akamwambia, Mbona unaniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, naye ndiye Mungu.”
Waebrania 4:15 “Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi.”
- Je mwanadamu akiongeza jitihada aweza kuwa mwenye haki hapa duniani?
Mhubiri 7:20 “Bila shaka hakuna mwanadamu mwenye haki hapa duniani, ambaye afanya mema, asifanye dhambi.”
Ayubu 9:2 “Kweli najua kuwa ndivyo hivyo; Lakini mtu huwaje mwenye haki mbele za Mungu?”
Warumi 5:19 “Kwa sababu kama kwa kuasi kwake mtu mmoja watu wengi waliingizwa katika hali ya wenye dhambi, kadhalika kwa kutii kwake mmoja watu wengi wameingizwa katika hali ya wenye haki.”
- Mtu mwenye asili ya dhambi anapoweka jitihada katika kutenda mema au anapotaka hadhi au daraja aliyojipatia katik jamii ya kidini vimpe uhalali wa kuhesabiwa haki matokeo yake huwa ni nini?
Isaya 64:6 “Kwa maana sisi sote tumekuwa kama mtu aliye mchafu, na matendo yetu yote ya haki yamekuwa kama nguo iliyotiwa unajisi; sisi sote twanyauka kama jani, na maovu yetu yatuondoa, kama upepo uondoavyo.”
Wafilipi 3:4-7 “Walakini mimi ningeweza kuutumainia mwili. Mtu ye yote akijiona kuwa anayo sababu ya kuutumainia mwili, mimi zaidi. Nalitahiriwa siku ya nane, ni mtu wa taifa la Israeli, wa kabila ya Benyamini, Mwebrania wa Waebrania, kwa habari ya kuishika torati, ni Farisayo, kwa habari ya juhudi, mwenye kuliudhi Kanisa, kwa habari ya haki ipatikanayo kwa sheria sikuwa na hatia. Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo.”
Luka 18:11-14 “Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang'anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote. Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi. Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.”
- Je, mwanadamu mwenye asili ya dhambi aweza kuhesabiwa haki kwa matendo ya sheria au kwa kushika sheria?
Wagalatia 2:16 “Hali tukijua ya kuwa mwanadamu hahesabiwi haki kwa matendo ya sheria, bali kwa imani ya Kristo Yesu; sisi tulimwamini Kristo Yesu ili tuhesabiwe haki kwa imani ya Kristo, wala si kwa matendo ya sheria; maana kwa matendo ya sheria hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki.”
Warumi 2:13 “Kwa sababu sio wale waisikiao sheria walio wenye haki mbele za Mungu, bali ni wale waitendao sheria watakaohesabiwa haki.”
Warumi 3:28 “Basi, twaona ya kuwa mwanadamu huhesabiwa haki kwa imani pasipo matendo ya sheria.”
Warumi 4:13 “Kwa maana ahadi ile ya kwamba atakuwa mrithi wa ulimwengu alipewa Ibrahimu na uzao wake, si kwa sheria bali kwa haki aliyohesabiwa kwa imani.”
Wagalatia 3:17 “Nisemalo ni hili; agano lililothibitishwa kwanza na Mungu, torati iliyotokea miaka mia nne na thelathini baadaye hailitangui, hata kuibatilisha ile ahadi.”
- Kama Mungu alikuwa na agano na mwanadamu lililojengwa juu ya ahadi ya urithi ilikuwaje akafanya naye agano linguine lililojengwa juu ya sheria na torati?
Agano la kwanza ambalo ni la milele lilikuwa ni lile lililotolewa bustanini lililotimizwa wakati wa agano jipya lilipohitimishwa pale msalabani. Agano la amri liliingizwa kwa ajili ya kukuza makosa na ili kulipa agano la kwanza na agano jipya umuhimu unaostahili.
Wagalatia 3:19 “Torati ni nini basi? Iliingizwa kwa sababu ya makosa, hata aje huyo mzao aliyepewa ile ahadi; iliamriwa kwa utumishi wa malaika kwa mkono wa mjumbe.”
Waebrania 9:15 “Na kwa sababu hii ni mjumbe wa agano jipya, ili, mauti ikiisha kufanyika kwa kukomboa makosa yaliyokuwa chini ya agano la kwanza, hao walioitwa waipokee ahadi ya urithi wa milele.”
Warumi 5:20 “Lakini sheria iliingia ili kosa lile liwe kubwa sana; na dhambi ilipozidi, neema ilikuwa nyingi zaidi.”
Warumi 4:13 “Kwa maana ahadi ile ya kwamba atakuwa mrithi wa ulimwengu alipewa Ibrahimu na uzao wake, si kwa sheria bali kwa haki aliyohesabiwa kwa imani.”
Warumi 4:14 “Maana ikiwa wale wa sheria ndio warithi, imani imekuwa bure, na ahadi imebatilika.”
Wagalatia 3:18 “Kwa maana urithi ukiwa kwa sheria, hauwi tena kwa ahadi; lakini Mungu alimkirimia Ibrahimu kwa njia ya ahadi.”
- Kama mwanadamu mwenye mwili wa dhambi asingeweza kushika sheria ilikuwaje Mungu akampa mwanadamu huyo sheria ili aishike?
Mungu alimpa mwanadamu sheria kabla ya dhambi ili aishike lakini alimpa mwanadamu huyo huyo sheria baada ya dhambi ilia aone ilivyo vigumu kuishika bila msaada wa Mungu na matokeo mabaya ya kuishika sheria hiyo bila msaada wa Mungu.
Warumi 3:19-20 “Basi twajua ya kuwa mambo yote inenayo torati huyanena kwa hao walio chini ya torati, ili kila kinywa kifumbwe, na ulimwengu wote uwe chini ya hukumu ya Mungu; kwa sababu hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki mbele zake kwa matendo ya sheria; kwa maana kutambua dhambi huja kwa njia ya sheria.”
Warumi 2:25 “Kwa maana kutahiriwa kwafaa kama ukiwa mtendaji wa sheria, lakini ukiwa mvunjaji wa sheria kutahiriwa kwako kumekuwa kutokutahiriwa.”
Warumi 4:15 “Kwa sababu sheria ndiyo ifanyayo hasira; maana pasipokuwapo sheria, hapana kosa.”
Warumi 5:13 “Maana kabla ya sheria dhambi ilikuwamo ulimwenguni, lakini dhambi haihesabiwi isipokuwapo sheria.”
Warumi 7:7-8 “Tusemeje, basi? Torati ni dhambi? Hasha! Walakini singalitambua dhambi ila kwa sheria; kwa kuwa singalijua kutamani, kama torati isingalisema, Usitamani. Lakini dhambi ilipata nafasi kwa ile amri, ikafanya ndani yangu kila namna ya kutamani. Kwa maana dhambi bila sheria imekufa.”
- Yesu alifanya nini kumwezesha mwanadamu kuhesabiwa haki bila kushika sheria?
Warumi 8:2-4 “Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti. Maana yale yasiyowezekana kwa sheria, kwa vile ilivyokuwa dhaifu kwa sababu ya mwili, Mungu, kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe katika mfano wa mwili ulio wa dhambi, na kwa sababu ya dhambi, aliihukumu dhambi katika mwili; ili maagizo ya torati yatimizwe ndani yetu sisi, tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali mambo ya roho.”
Warumi 7: 1-4 “Ndugu zangu, hamjui (maana nasema na hao waijuao sheria) ya kuwa torati humtawala mtu wakati anapokuwa yu hai? Kwa maana mwanamke aliye na mume amefungwa na sheria kwa yule mume wakati anapokuwa yu hai; bali akifa yule mume, amefunguliwa ile sheria ya mume. Basi wakati awapo hai mumewe, kama akiwa na mume mwingine huitwa mzinzi. Ila mumewe akifa, amekuwa huru, hafungwi na sheria hiyo, hata yeye si mzinzi, ajapoolewa na mume mwingine. Kadhalika, ndugu zangu, ninyi pia mmeifia torati, kwa njia ya mwili wa Kristo, mpate kuwa mali ya mwingine, yeye aliyefufuka katika wafu, kusudi tumzalie Mungu matunda.”
Warumi 6:5-7 “Kwa maana kama mlivyounganika naye katika mfano wa mauti yake, kadhalika mtaunganika kwa mfano wa kufufuka kwake; mkijua neno hili, ya kuwa utu wetu wa kale ulisulibishwa pamoja naye, ili mwili wa dhambi ubatilike, tusitumikie dhambi tena; kwa kuwa yeye aliyekufa amehesabiwa haki mbali na dhambi.”
Warumi 5:18-19 “Basi tena, kama kwa kosa moja watu wote walihukumiwa adhabu, kadhalika kwa tendo moja la haki watu wote walihesabiwa haki yenye uzima. Kwa sababu kama kwa kuasi kwake mtu mmoja watu wengi waliingizwa katika hali ya wenye dhambi, kadhalika kwa kutii kwake mmoja watu wengi wameingizwa katika hali ya wenye haki.”
- Kama haki, urithi, na uzima havipatikani kwa kushika sheria hii ni kumaanisha aliyehesabiwa haki hahitajiki kushika sheria?
Warumi 6:15-16 “Ni nini basi? Tufanye dhambi kwa sababu hatuwi chini ya sheria bali chini ya neema? Hasha! Hamjui ya kuwa kwake yeye ambaye mnajitoa nafsi zenu kuwa watumwa wake katika kumtii, mmekuwa watumwa wake yule mnayemtii, kwamba ni utumishi wa dhambi uletao mauti, au kwamba ni utumishi wa utii uletao haki.”
Yohana 15:10 “Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake.”
Yohana 14:15 “Mkinipenda, mtazishika amri zangu.”
1 Yohana 5:3 “Kwa maana huku ndiko kumpenda Mungu, kwamba tuzishike amri zake; wala amri zake si nzito.”
Warumi 8:3-4 “Maana yale yasiyowezekana kwa sheria, kwa vile ilivyokuwa dhaifu kwa sababu ya mwili, Mungu, kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe katika mfano wa mwili ulio wa dhambi, na kwa sababu ya dhambi, aliihukumu dhambi katika mwili; ili maagizo ya torati yatimizwe ndani yetu sisi, tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali mambo ya roho.”
- Kwa nini Shetani anazichukia Amri za Mungu na wale wanaozifundisha na kuzishika?
1 Yohana 2:4 “Yeye asemaye, Nimemjua, wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake.”
Mathayo 5:19 “Basi mtu ye yote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni.”
Ufunuo 12:17 “Joka akamkasirikia yule mwanamke, akaenda zake afanye vita juu ya wazao wake waliosalia, wazishikao amri za Mungu, na kuwa na ushuhuda wa Yesu; naye akasimama juu ya mchanga wa bahari.”
- Ni Amri ipi hasa ambayo Shetani anaichukia na kwa nini?
Shetani anazichukia amri zote zinazomtambulisha Mungu anayestahili kuabudiwa na zinazoelekeza anavyostahili kuabudiwa. Amefanya majaribio ya kuziondoa au kuzibadili amri ya pili inayokataza ibada ya sanamu na amri ya nne inayoelekeza siku ya kumwabudu Mungu na namna anavyopaswa kuabudiwa na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa. Katika majaribio hayo hakubadili wala kuondoa amri ya tano hadi ya kumi zinazoratibu mahusiano ya wanadamu.
Danieli 8:12 “Na jeshi likatolewa kwake pamoja na sadaka ya kuteketezwa ya daima, kwa sababu ya makosa; nayo ikaiangusha kweli hata chini; ikatenda ilivyopenda, na kufanikiwa.”
Danieli 7:25 “Naye atanena maneno kinyume chake Aliye juu, naye atawadhoofisha watakatifu wake Aliye juu; naye ataazimu kubadili majira na sheria; nao watatiwa mikononi mwake kwa wakati, na nyakati mbili, na nusu wakati.”
2 Wathesalonike 2:3-4 “Mtu awaye yote asiwadanganye kwa njia yo yote; maana haiji, usipokuja kwanza ule ukengeufu; akafunuliwa yule mtu wa kuasi, mwana wa uharibifu; yule mpingamizi, ajiinuaye nafsi yake juu ya kila kiitwacho Mungu ama kuabudiwa; hata yeye mwenyewe kuketi katika hekalu la Mungu, akijionyesha nafsi yake kana kwamba yeye ndiye Mungu.”
Ufunuo 13:4-7 “Wakamsujudu yule joka kwa sababu alimpa huyo mnyama uwezo wake; nao wakamsujudu yule mnyama, wakisema, Ni nani afananaye na mnyama huyu? Tena ni nani awezaye kufanya vita naye? Naye akapewa kinywa cha kunena maneno makuu, ya makufuru. Akapewa uwezo wa kufanya kazi yake miezi arobaini na miwili. Akafunua kinywa chake amtukane Mungu, na kulitukana jina lake, na maskani yake, nao wakaao mbinguni. Tena akapewa kufanya vita na watakatifu na kuwashinda, akapewa uwezo juu ya kila kabila na jamaa na lugha na taifa.”
Ufunuo 13:13-15 “Naye afanya ishara kubwa, hata kufanya moto kushuka kutoka mbinguni uje juu ya nchi mbele ya wanadamu. Naye awakosesha wale wakaao juu ya nchi, kwa ishara zile alizopewa kuzifanya mbele ya huyo mnyama, akiwaambia wakaao juu ya nchi kumfanyia sanamu yule mnyama, aliyekuwa na jeraha la upanga naye akaishi. Akapewa kutia pumzi katika ile sanamu ya mnyama, hata ile sanamu ya mnyama inene, na kuwafanya hao wote wasioisujudu sanamu ya mnyama wauawe.”
Ufunuo 15:2 “Tena nikaona kitu kama mfano wa bahari ya kioo iliyochangamana na moto, na wale wenye kushinda, watokao kwa yule mnyama, na sanamu yake, na kwa hesabu ya jina lake, walikuwa wamesimama kando-kando ya hiyo bahari ya kioo, wenye vinubi vya Mungu.”
Ufunuo 19:20 “Yule mnyama akakamatwa, na yule nabii wa uongo pamoja naye, yeye aliyezifanya hizo ishara mbele yake, ambazo kwa hizo aliwadanganya watu wale walioipokea ile chapa ya huyo mnyama, nao walioisujudia sanamu yake; hao wawili wakatupwa wangali hai katika lile ziwa la moto liwakalo kwa kiberiti.”
- Je Mungu ana mpango wowote wa kuzirejesha amri hizo zilizoondolewa au kubadilishwa na Shetani?
Marko 7:6-9 “Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu, Ninyi mwaiacha amri ya Mungu, na kuyashika mapokeo ya wanadamu. Akawaambia, Vema! Mwaikataa amri ya Mungu mpate kuyashika mapokeo yenu.
Mathayo 15:12-13 “Ndipo wanafunzi wake walipomwendea, wakamwambia, Wajua ya kuwa Mafarisayo walipolisikia neno lile walichukizwa? Akajibu, akasema, Kila pando asilolipanda Baba yangu wa mbinguni litang'olewa.”
Matendo 17:23 “Kwa sababu nilipokuwa nikipita huko na huko na kuyaona mambo ya ibada yenu, naliona madhabahu iliyoandikwa maneno haya, KWA MUNGU ASIYEJULIKANA. Basi mimi nawahubirini habari zake yeye ambaye ninyi mnamwabudu bila kumjua.”
Yohana 4:22 “Ninyi mnaabudu msichokijua; sisi tunaabudu tukijuacho; kwa kuwa wokovu watoka kwa Wayahudi.”
Yohana 4:23 “Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu.”