Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

1 PETRO

MASWALI YA KUJADILI: 1 PETRO 1:1-25

  1. Baba, Mwana (Yesu Kristo), na Roho Mtakatifu wameshirikiana kwa karibu sana kuhakikisha ukombozi wa wanadamu unakamilika. Hii inakupa fundisho gani kuhusu thamani ya mwanadamu na gharama ya kumkomboa? Unazipokeaje taarifa kuwa wewe unalindwa na nguvu za Mungu hadi upokee wokovu ulio tayari kufunuliwa?
  2. Unadhani urithi usioharibika, usio na uchafu, usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yako ni urithi wa namna gani? Unadhani baada ya kuupokea urithi huo kitu gani hakitakuwa tena sehemu ya maisha yako? Gharama ya wokovu wetu ina mchango gani katika kutuzuia tusiendelee kuishi maisha ya dhambi? Je kuzaliwa mara ya pili ni kwa lazima ili kuishi maisha yenye ushindi dhidi ya dhambi?

MASWALI YA KUJADILI: 1 PETRO 2:1-25

  1. Kama Yesu alikuwa jiwe lililo hai, teule, na lenye heshima, kwa nini Wayahudi na wanadamu walimkataa? Kama wangemkubali wokovu wa wanadamu ungekuwaje? Maziwa yasiyoghoshiwa ambayo watoto wachanga wa kiroho wanashauriwa kuyatumia ni yapi? Hadhi ya watakaokombolewa inajumuisha cheo cha ukuhani na ufalme. Hii inaashiria kuwa ukuhani utaendelea mbinguni?
  2. Je ukuhani huo utawahusu wanawake pia? Je ufalme wa waliokombolewa utahusika kutawala hata viumbe wengine wasio binadamu? Yesu alizichukuaje dhambi zetu katika mwili wake? Iliwezekanaje kwa Yesu kutotenda dhambi wakati ambao yeye alikuwa na mwili unaojaribiwa kama sisi?
  3. Maziwa ya akili yasiyogoshiwa ni yapi? Kugoshiwa ni kufanyaje na kwa nini maziwa yanagoshiwa? (1 Wakorintho 3:1-2; Waebrania 5:12-13). Kwa nini masomo kama ya Unabii na Haki kwa Imani hayajadiliwi sana na badala yake mambo mepesi yasiyohusu wokovu yanapewa nafasi zaidi? Kama Yesu ni jiwe lililo hai kwa nini alikataliwa na wanadamu?
  4. Kwa nini Mungu aliruhusu jambo hilo litokee? Kwa nini wanaomwamini Yesu nao wanaitwa mawe yaliyo haì? Dhabihu za roho zinazokubaliwa na Mungu ni zipi? Kwa nini wanaomwamini Yesu wanatambuliwa kama mzao mteule? Kwa nini hapa ukuhani umeunganishwa na ufalme wakati katika Agano la Kale hizi zilikuwa ofisi mbili tofauti?
  5. Watu wa milki ya Mungu maana yake ni wanaomiliki na Mungu au wanaomilikiwa na Mungu? Je ni Waisraeli tu waliopata fursa ya kuwa taifa takatifu au mtu yeyote anayo fursa ya kuwa taifa takatifu? Kujihesabu kama mpitaji na msafiri hapa duniani kuna faida gani kiroho? Kutenda mema kunawezaje kuziba vinywa vya ujinga vya watu wapumbavu?
  6. Unawezaje uwe huru bila kutumia uhuru huo kusitiri ubaya? Yesu aliwezaje kuishi bila kutenda dhambi licha ya kuwa alijaribiwa kama sisi? (Waebrania 4:15). Yesu aliwezaje kuzichukua dhambi zetu mwilini mwake? Iliwezekanaje kupigwa apigwe yeye na kupona tupone sisi?

MASWALI YA KUJADILI: 1 PETRO 3:1-22

  1. Kwa nini wake wanatakiwa kuwatii waume zao? Je, ni halali kwa mke kuishi na mume asiyeliamini Neno? Je mke mtii humvutia mumewe kiasi cha kubadilisha mtazamo wake usiofaa? Je, mwanamke anayejitambua kuwa yupo kwenye dini sahihi kuliko ya mume wake anaweza kuwa na mwenendo safi na wenye hofu? Je, mwanamke anastahili kujipamba? Katika waraka huu Petro anakataza wanawake kujipamba au anaelekeza kujipamba kuliko kwa thamani kuu mbele za Mungu?
  2. Je, kujipamba kwa nje kuna umuhimu wowote? Aliyeanza kwa kujipamba ndani kisha akamalizia kujipamba kwa nje ana tatizo lolote? Je waraka huu umekataza kujipamba kwa kusuka nywele? Roho ya upole, utulivu na utu wa ndani usioonekana ni mapambo yamfaayo mwanamke? Mapambo haya ya ndani ni matokeo ya kazi fanywayo na mtu au Roho Mtakatifu? Mapambo haya ya nje ni matokeo ya kazi fanywayo na mtu au Roho Mtakatifu?
  3. Wanawake watakatifu wa zamani waliomtii Mungu walijipamba kwa mapambo ya nje zaidi au mapambo ya ndani zaidi? Wanawake watakatifu wa leo hujipamba kwa mapambo ya ndani zaidi au ya nje zaidi? Kuna Ushahidi gani kama Sara alijipamba kwa mapambo ya ndani zaidi? Je, kuna wakati utii wa Sara kwa mumewe ulizidi mipaka? Kumwita mumewe Bwana ile inayotumika kwa Mungu ilikuwa sahihi? (Waefeso 5:22).
  4. Kwa nini waume wanashauriwa kukaa na wake zao kwa akili? Kuna shida gani itatokea kama hawatakaa nao kwa akili? Je, mwanamke ni Chombo kisicho na nguvu? Unadhani nini kitatokea Ikiwa nguvu kubwa itatumika kuishi na mwanamke ambaye ni Chombo kisicho na nguvu? Kwa nini wanaume hupendelea kukaa na wake zao kwa kutumia nguvu badala kutumia akili? Je, kuishi kwa akili kinakozungumzwa hapa kunahusisha kujua walivyo na mabadiliko wanayoyapitia nyakati mbalimbali?
  5. Je, wanawake ni warithi wa uzima kama walivyo wanaume? Urithi huu wa uzima utazingatia jinsia au kila mmoja bila kujali jinsia yake atapewa urithi sawa? Je, wanawake nao watatawala katika ule ufalme Mungu aliokwenda kuuandaa? Je kuna wakati maombi yetu kwa Mungu hukosa kujibiwa kwa sababu ya ukatili tunaowafanyia wake zetu majumbani?
  6. Kwa nini ili turithi baraka tunatakiwa kuwa watu wenye kubariki? Kwa nini unapolaumiwa hutakiwi kulaumu? Unadhani kuhurumiana kukiwepo magomvi yataepukwa kwenye mahusiano? Kwa nini kuhurumiana kumepungua? Kwa nini mtu asiyeuzuia ulimi wake usinene mabaya na midomo yake isiseme hila hawezi kuwa na siku njema? Je, mtu anaweza kuteswa kwa sababu ya haki au kwa sababu ya kutenda mema?
  7. Kwa nini kumjibu mtu tumaini lililo ndani yako kunahitaji hofu na upole? Je, kuna uwezekano wa kulalamikiwa kwa jambo ulilolifanya kwa dhamira njema? Roho wa Kristo aliyehuishwa aliwaendeaje roho waliokaa kifungoni akawahubiri? Uvumilivu wa Mungu ulikuwa unangoja nini wakati Safina ilipokuwa inatengenezwa? Je, ubatizo unaokoa?

MASWALI YA KUJADILI: 1 PETRO 4:1-19

  1. Kuteswa katika mwili kunamfanyaje mtu kuachana na dhambi? Je dhambi ipo mwilini? Je, tamaa za wanadamu zinapingana na mapenzi ya Mungu? Je, kuna mambo yasiyofaa ambayo watu wa jamii yako huyatenda na huona ajabu kuwa wewe huyafanyi? Je huo ni ushuhuda wenye nguvu juu ya Imani yako kuliko kutegemea kuwafundisha Neno? Kama Wakristo wangeishi yale wanayofundisha Ukristo ungepokelewa kwa kiasi gani? Kwa nini Maisha yetu hayamwakilishi Kristo?
  2. Je walioshuhudiwa kwa matendo mema ya waumini watatoa hesabu siku ya mwisho kwa nini hawakuamini? Kwa nini akili inayohitajiwa wakati mambo yanapokuwa yamekaribia mwisho ni kukesha katika sala? Upendano unasitirije wingi wa dhambi? Je, kupendana kunahitaji juhudi? Je, ukarimu unaofanyika kwa kunung’unika unatambuliwa kama ukarimu? Kwa nini?
  3. Je, karama zilitolewa kwa kusudi la kuhudumiana? Je, kuna namna gani nyingine isiyofaa ambayo karama hutumika? Je, kuna uwezekano wa watu kuhudumu kwa nguvu wasizojaliwa na Mungu? Watu wasipohudumu kwa nguvu wanazojaliwa na Mungu ni nani anatukuzwa? Kwa nini majaribu yanatakiwa kuchukuliwa kama jambo la kawaida kwa watu wa Mungu?
  4. Ufunuo wa utukufu wa Yesu Kristo ambao tutaushiriki ni wa namna gani? Je utukufu huo unafanana na mateso ya Kristo tunayoyashiriki sasa? Je, kulaumiwa kwa ajili ya Kristo ni dalili kuwa unakaliwa na Roho Mtakatifu? Je, kujishughulisha na mambo ya watu wengine ni dhambi? Ni lini hukumu ilipoanza katika nyumba ya Mungu? Je hukumu ya wale wasio kwenye nyumba ya Munu inaanza lini? Kwa nini hukumu ya walio kwenye nyumba ya Mungu inatangulia?

MASWALI YA KUJADILI: 1 PETRO 5:1-14

  1. Kwa nini Petro anajiita mshiriki wa utukufu utakaoonekana baadaye? Je ni halali kwa mfuasi wa Yesu leo kujitambulisha kama mshiriki wa utukufu utakaoonekana baadaye? Kwa nini wazee wanaombwa kulichunga kundi lililo kwao kwa hiyari na kwa moyo na si kwa kujifanya mabwana? Je, kulisimamia kundi ni sawa na kuliongoza? Je kusimamia kundi kunahitaji upole?
  2. Je kuna uwezekano wa kuifanya kazi ya Mungu kwa kutaka fedha ya aibu? Inakuwaje hata fedha ikaitwa ya aibu? Mshahara wa watumishi wa Mungu upo kwenye fedha au kwenye taji ya uzima? Mchungaji mkuu ni nani naye atadhihirishwa lini? Hiyo taji ya utukufu isiyokauka ipoje? Je kuhudumiana kunahitaji unyenyekevu? Mtu anajifungaje unyenyekevu?
  3. Kiongozi anayeongoza kwa kuonyesha mfano hufanikiwaje katika uongozi wake? Kwa nini Mungu anawapinga wenye kiburi na kuwapa wanyenyekevu neema? Je Mungu anayo ratiba ya kutuinua wakati Fulani? Kama Munu anajua wakati atakaotuinua ipo haja ya kumwomba?
  4. Nitajuaje kama nimenyenyekea chini ya mkono wa Mungu ulio Hodari? Tunamtwikaje Mungu fadhaa zetu zote? Kama Mungu amejitolea kuchukua fadhaa (misongo) yetu yote kuna haja ya kuishi Maisha ya msongo? Kama hata baada ya kumkabidhi Mungu fadhaa zako unahisi hali ya kukosa amani unatakiwa kufanyaje?
  5. Kwa nini shetani anaitwa mshitaki wetu? Anatushitaki kwa nani na wakati tunapofanya nini? Shetani anawamezaje watu? Maeneo anayozungukia ni yapi? Je, inawezekana kumpinga shetani? Mungu ametuitaje kuingia katika utukufu wake wa milele? Yesu anatutengeneza, kututhibitisha, na kututia nguvu kwa namna gani? Kusalimiana kwa busu takatifu kunafanyikaje?