KUCHAMBUA KITABU CHA WARUMI
SURA YA KWANZA
Kitabu cha Warumi ni muhtasari wa kile Mtume Paulo alichotaka kukiwasilisha kwa watu wa Rumi kama angefanikiwa kuzuru maeneo yao. (Warumi 1:13) “Lakini, ndugu zangu, sipendi msiwe na habari, ya kuwa mara nyingi nalikusudia kuja kwenu, nikazuiliwa hata sasa, ili nipate kuwa na matunda kwenu ninyi pia kama nilivyo nayo katika Mataifa wengine.” Hapa anawasilisha mpango wa wokovu kwa namna aliyofunuliwa na Mungu. Kwake mpango wa wokovu unahusu uwezo wa Mungu uletao wokovu kwa watu wote bila kubagua utaifa wao, dini zao, jinsia au uelewa wao wa mambo ya kiroho. (Warumi 1:16) “Kwa maana siionei haya Injili; kwa sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia.”
Hii inaondoa dhana inayowafanya Wayahudi kuonekana bora zaidi kuliko wa mataifa mengine ambao hawakubahatika kufahamu mengi kuhusu mpango huo. Kwa upande mmoja Paulo anakiri kuwepo kwa faida ya mtu kuwa Myahudi kwa sababu ya kukabidhiwa yale mausia ambayo watu wa mataifa mengine hawakupewa. (Warumi 3:1-2) “Basi Myahudi ana ziada gani? Na kutahiriwa kwafaa nini Kwafaa sana kwa kila njia. Kwanza kwa kuwa wamekabidhiwa mausia ya Mungu.”
Lakini kule kukabidhiwa mausia hakuwafanyi wao kuwa bora kama hawatatambua kuwa changamoto zinazowapata watu wa mataifa mengine katika kuwa wenye haki mbele za Mungu zinawakabili na wao pia. (Warumi 3:9-12) “Ni nini basi? Tu bora kuliko wengine? La! Hata kidogo. Kwa maana tumekwisha kuwashitaki Wayahudi na Wayunani ya kwamba pia wamekuwa chini ya dhambi; kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Hakuna mwenye haki hata mmoja. Hakuna afahamuye; Hakuna amtafutaye Mungu. Wote wamepotoka, wameoza wote pia; Hakuna mtenda mema, la! Hata mmoja.”
Ukweli huu kwa kiasi fulani ulikuwa mchungu kwa Wayahudi waliojihesabu kuwa wenye haki zaidi kuliko watu wa mataifa mengine waliowaita najisi. Paulo alikuwa muumini wa dhana hii hapo mwanzo hadi alipoongoka baada ya kukutana na Yesu kwenye njia ya kwenda Dameski. (Matendo 10:28) “Akawaambia, Ninyi mnajua ya kuwa si halali mtu aliye Myahudi ashikamane na mtu aliye wa taifa lingine wala kumwendea, lakini Mungu amenionya, nisimwite mtu awaye yote mchafu wala najisi.” Uelewa huu mpya haukuwa rahisi kupokelewa na Wayahudi kiasi cha kumjengea Paulo chuki na ndugu zake wa Kiyahudi. (Matendo 21:28) “Wakapiga kelele, na kusema, Enyi wanaume wa Israeli, tusaidieni. Huyu ndiye mtu yule afundishaye watu wote kila mahali kinyume cha taifa letu na torati na mahali hapa. Tena, zaidi ya haya, amewaingiza Wayunani katika hekalu, akapatia unajisi mahali hapa patakatifu.”
Ujumbe wa Paulo katika kitabu cha Warumi unawahusu watu wote kwa kuwa wote wanakabiliwa na tatizo moja la kuwa chini ya dhambi. Kuwa chini ya dhambi ni sawa na kuwa chini ya sheria au chini ya torati. (Warumi 3:19-20) “Basi twajua ya kuwa mambo yote inenayo torati huyanena kwa hao walio chini ya torati, ili kila kinywa kifumbwe, na ulimwengu wote uwe chini ya hukumu ya Mungu; kwa sababu hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki mbele zake kwa matendo ya sheria; kwa maana kutambua dhambi huja kwa njia ya sheria.”
Torati au sheria ilitambulishwa ili kuongeza uelewa wa ubaya wa dhambi na kuthibitisha ilivyo vigumu kwa mwanadamu kuitii sheria hiyo. (Warumi 8:7) “Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii.” Faida aliyonayo Myahudi kwa kupokea maagizo ya torati kinyume na watu wa mataifa mengine ilipaswa iwe utambuzi wa ubaya wa dhambi na jinsi ilivyo vigumu kwa mwanadamu kuitii sheria hiyo kutokana na mapungufu yatokanayo na mwili wa dhambi. (Warumi 7:14) “Kwa maana twajua ya kuwa torati asili yake ni ya rohoni; bali mimi ni mtu wa mwilini, nimeuzwa chini ya dhambi.”
Agano la mlima Sinai lililojengwa juu ya ahadi zisizo bora zaidi lilikusudiwa kuwa la mpito huku Agano lililo bora zaidi likiandaliwa. (2 Wakorintho 3:7-9) “Basi, ikiwa huduma ya mauti, iliyoandikwa na kuchorwa katika mawe, ilikuja katika utukufu, hata Waisraeli hawakuweza kuukazia macho uso wa Musa, kwa sababu ya utukufu wa uso wake; nao ni utukufu uliokuwa ukibatilika; je! Huduma ya roho haitazidi kuwa katika utukufu? Kwa maana ikiwa huduma ya adhabu ina utukufu, siuze huduma ya haki ina utukufu unaozidi.” Huduma ya Agano la kale inafananishwa na huduma y amauti au huduma ya adhabu kwa sababu haitoi suluhisho la utumwa wa dhambi n amauti vinavyomkabili mwanadamu.
Ujumbe katika kitabu cha Warumi unajikita zaidi kwenye tatizo la mwili wa dhambi na suluhisho lake. Paulo anafunua kuwa mwanadamu alipoanguka dhambini pamoja na kujipatia uhalali wa kuingia mautini alipoteza pia uwezo aliokuwa nao mwanzo wa kutenda mema na wa kutii maagizo ya Mungu. Mwili ukawa katika hali ambayo isingeweza kurekebika. (Yeremia 13:23) “Je! Mkushi aweza kuibadili ngozi yake, au chui madoa-doa yake? Kama aweza, ndipo na ninyi mwaweza kutenda mema, ninyi mliozoea kutenda mabaya.” Ule mwili wa asili ukapotea na badala yake mwili wa dhambi ukaanza kutawala katika maisha ya mwanadamu na kuizalia mauti mazao. (Warumi 7:5) “Kwa maana tulipokuwa katika hali ya mwili, tamaa za dhambi, zilizokuwako kwa sababu ya torati, zilitenda kazi katika viungo vyetu hata mkaizalia mauti mazao.”
Wayahudi hawakuwa wameipokea dhana hii na kupitia uzoefu wao wakawa wanajidanganya kuwa kwa namna fulani wangeweza kuutiisha mwili ili utii maagizo ya Mungu kwa uwezo wao bila kuhitaji kusaidiwa na Mungu. (Kutoka 19:8) “Watu wote wakaitika pamoja wakisema, Hayo yote aliyoyasema Bwana tutayatenda. Naye Musa akamwambia Bwana maneno ya hao watu.” (Kutoka 24:3) “Musa akaenda akawaambia watu maneno yote ya Bwana, na hukumu zake zote; watu wote wakajibu kwa sauti moja, wakasema, Maneno yote aliyoyanena Bwana tutayatenda. (Kutoka 24:7) “Kisha akakitwaa kitabu cha agano akakisoma masikioni mwa watu; wakasema, Hayo yote aliyoyanena Bwana tutayatenda, nasi tutatii.”
Jaribio la Wayahudi kutaka kutii maagizo ya Mungu kwa juhudi zao wenyewe liligonga mwamba baada ya agano walilofanya na Mungu pale mlima Sinai kutodumu. (Waebrania 8:9) “Halitakuwa kama agano lile nililoagana na baba zao, Katika siku ile nilipowashika mikono yao niwatoe katika nchi ya Misri. Kwa sababu hawakudumu katika agano langu, Mimi nami sikuwajali asema Bwana.” Hata baada ya Yesu kuja duniani na kuuweka wazi zaidi mpango wa wokovu, bado Wayahudi walikuwa wazito kutambua udhaifu wa mwili wa dhambi katika kumfanya mwanadamu kuwa mwenye haki kwa njia ya kutii maagizo.
Wayahudi waliendelea kuamini kuwa mwili wa dhambi bado unao uwezo wa kuzalisha matendo mema yawezayo kumwingizia mwanadamu haki kama ukitiishwa na kuzoezwa kutenda matendo mema. (Luka 18:10) “Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru. Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang'anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote. Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi. Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.”
Kwa nini aliyekiri kuwa ni mwenye dhambi ndiye aliyehesabiwa haki kuliko yule aliyejigamba kuwa na matendo mema? Aliyejigamba kuwa ana matendo mema alisahau au hakutaka kukubali kwamba mwanadamu mwenye mwili wa dhambi hana uwezo wa kuzalisha matendo mema na kwamba yale anayodhani ni matendo mema yamejaa kujitukuza, dharau na kujihesabia haki. Tendo jema huamuliwa na nia iliyolizalisha. (Mathayo 6:1) “Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya kama hayo, hampati thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni.”
Paulo anaanza kitabu cha Warumi kwa kujitambulisha kama mtumwa na si Farisayo. (Matendo 23:6) “Paulo alipotambua ya kuwa sehemu moja ni Masadukayo, na sehemu ya pili ni Mafarisayo, akapaza sauti yake katika ile baraza, Ndugu zangu, mimi ni Farisayo mwana wa Farisayo; mimi ninahukumiwa kwa ajili ya tumaini la ufufuo wa wafu.” Paulo hakubaki kuwa Farisayo maisha yake yote. Alibadilika baada ya kukutana na injili ya Yesu. (Wafilipi 3: 3-6) “Maana sisi tu tohara, tumwabuduo Mungu kwa Roho, na kuona fahari juu ya Kristo Yesu, wala hatuutumainii mwili. Walakini mimi ningeweza kuutumainia mwili. Mtu ye yote akijiona kuwa anayo sababu ya kuutumainia mwili, mimi zaidi. Nalitahiriwa siku ya nane, ni mtu wa taifa la Israeli, wa kabila ya Benyamini, Mwebrania wa Waebrania, kwa habari ya kuishika torati, ni Farisayo, kwa habari ya juhudi, mwenye kuliudhi Kanisa, kwa habari ya haki ipatikanayo kwa sheria sikuwa na hatia.”
Lakini kwa neema ya Mungu Yesu alimpa mafunuo kuwa njia aliyochagua isingemfikisha kokote. (Waefeso 3:7-9) “Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo. Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo; tena nionekane katika yeye, nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani iliyo katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu, kwa Imani.”
Paulo sasa anajitambulisha kama mtumwa aliyetengwa aihubiri injili iliyokuwa imeahidiwa katika Maandiko iliyotimia katika Yesu Kristo aliye Mwana wa Mungu. Baada ya anguko la dhambi Mungu aliahidi kutuma mzao utakaosaidia kuondoa changamoto zilizoletwa na nyoka yaani Shetani. (Mwanzo 3:15) “Nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino.” Mzao huo ulioahidiwa hakuwa Isaka ingawa kwa kiasi kikubwa Isaka alikuwa anamuwakilisha Mzao huo. (Wagalatia 4:22-24, 31) “Ibrahimu alikuwa na wana wawili mmoja kwa mjakazi, na mmoja kwa mwungwana. Lakini yule wa mjakazi alizaliwa kwa mwili, yule wa mwungwana kwa ahadi. Mambo haya husemwa kwa mfano; kwa maana hawa ndio kama maagano mawili, moja kutoka mlima Sinai, lizaalo kwa utumwa, ambalo ni Hajiri. Ndiposa, ndugu zangu, sisi si watoto wa mjakazi, bali tu watoto wa huyo aliye mwungwana.”
Ahadi ya Mungu pale Edeni ilitimizwa kupitia Yesu Kristo aliye Mwana wa Mungu. (Wagalatia 3:16) “Basi ahadi zilinenwa kwa Ibrahimu na kwa mzao wake. Hasemi, Kwa wazao, kana kwamba ni wengi, bali kana kwamba ni mmoja, Kwa mzao wako, yaani, Kristo.” Yesu alifanyika Mwana wa Mungu ili atukomboe sisi wanadamu na nguvu za Ibilisi. Kama wanadamu tulihitaji mtu mwenye asili moja na sisi asiye na mwili wenye dhambi ili kupitia kwake turejeshwe kwenye hali yetu ya asili ya mwanzo. (1 Yohana 3:8) “Atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi.”
Shetani alijua kuwa Mwana wa Mungu atakuwa na uwezo zaidi yake ndiyo maana ujio wake ulimwogopesha. (Mathayo 4:3) “Mjaribu akamjia akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, amuru kwamba mawe haya yawe mikate.” Huyu ndiye Mwana wa Mungu asiyeshindwa ambaye kama tutatoa ushirikiano kwake ushindi wetu juu ya dhambi utakuwa wa hakika. Tatizo walilonalo Wayahudi lipo katika muamini huyu ambaye ni mzao aliyeahidiwa kuwa ndiye hasa Mwana wa Mungu. Hata Kuhani Mkuu alipata wakati mgumu kumtambua kama ndiye Mwana wa Mungu. (Mathayo 26:63) “Lakini, Yesu akanyamaza. Kuhani Mkuu akamwambia, Nakuapisha kwa Mungu aliye hai, utuambie kama wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu.”
Utambuzi kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu katika nyakati za Yesu hata katika nyakati hizi huja tu kwa njia ya mafunuo. Inaonekana Ibilisi hakutaka na bado hataki Yesu ajulikane kuwa ni Mwana wa Mungu kwa kuwa inahatarisha usalama wake na wa himaya yake na inawafungulia siri ya kuuteka ufalme wake. (Mathayo 16:15-17) “Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani? Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni.” (Marko 3:11) “Na pepo wachafu, kila walipomwona, walianguka mbele yake, wakalia wakisema, Wewe ndiwe Mwana wa Mungu. (Marko 15:39) “Basi yule akida, aliyesimama hapo akimwelekea, alipoona ya kuwa alikata roho jinsi hii, akasema, Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu.”
Tunatakiwa kumfahamu Yesu kama Mwana wa Mungu kwa sababu ya uzito uliobebwa na wadhifa huo. (Waefeso 4:13) “Hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo.” Yesu kabla hajawa Mwana wa Mungu alikuwa nafsi ya Uuungu iitwayo Neno. (Yohana 1:1-3, 14) “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. uyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika. Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.”
Kufanyika kwake kuwa Mwana wa Mungu kulitokana na uhitaji uliojitokeza baada ya Mwana wa Mungu aliyekuwepo kupoteza hadhi hiyo na kuitumbukiza jamii ya wanadamu kwenye anguko la dhambi. Alihitajika Mwana wa Mungu mwenye asili ya Uungu mwenye uwezo wa kuzishinda hila zote za yule mwovu. Yesu kwa hiyari akakubali kuwa Mwana wa Mungu. Kitendo cha Yesu kukubali kuwa Mwana wa Mungu kulilazimisha nafsi moja kati ya mbili zilizobaki itambuliwe kama Baba. Mwana wa Mungu alipatikana kwa tamko na si kwa kuzaliwa. (Waebrania 1:1-5) “Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, wake aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu. Yeye kwa kuwa ni mng'ao wa utukufu na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu; amefanyika bora kupita malaika, kwa kadiri jina alilolirithi lilivyo tukufu kuliko lao. Kwa maana alimwambia malaika yupi wakati wo wote, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa? Na tena, Mimi nitakuwa kwake baba, Na yeye atakuwa kwangu mwana?”
Yesu ndiye kiumbe pekee mwenye asili mbili yaani Uungu na ubinadamu. Kuwa kwake Mwana wa Mungu kunampa hadhi iliyo bora kuliko ya Malaika kwa kuwa hilo jina alilolirithi linampa uhalali wa kuwa mrithi wa yote, kuwa mng'ao wa utukufu na chapa ya nafsi ya Mungu, kuvichukua vyote kwa amri ya uweza wake, na kuketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu. Ndiyo maana Shetani anaposikia jina la Mwana wa Mungu anakosa amani. (Marko 3:11) “Na pepo wachafu, kila walipomwona, walianguka mbele yake, wakalia wakisema, Wewe ndiwe Mwana wa Mungu.”
Kuonyesha uzito jina la Mwana wa Mungu alilolirithi Yesu, wakati wa ubatizo wake, nafsi zote mbili zilikuwepo kuthibitisha ukuu huo. (Marko 1:9-12) “Ikawa siku zile, Yesu alikuja kutoka Nazareti ya Galilaya, akabatizwa na Yohana katika Yordani. Mara alipopanda kutoka majini, akaona mbingu zinapasuka, na Roho, kama hua, akishuka juu yake; na sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe. Mara Roho akamtoa aende nyikani.” Upendo wa Mungu kwetu unapimwa kupitia kitendo cha kumtoa huyo Mwanae mpendwa awe fidia ya makosa yetu! (Warumi 8:32) “Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye?”
Hata ibrahimu alipoambiwa amtoe mwanae wa pekee Isaka alikuwa anaonyeshwa thamani ya mwanadamu na ilivyomgharimu Mungu kumuokoa. (Mwanzo 22:2) “Akasema, Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia.” Mungu alistahimili kumtoa mwanae mpendwa kwa kuwa hiyo ndiyo njia pekee iliyokuwa imebaki ya kutatua tatizo lililoletwa na dhambi. Ndiyo njia pekee ya kumrejeshea mwanadamu yote aliyopoteza baada ya anguko la dhambi. Kurejeshewa mwili usio wa dhambi wenye uwezo wa kutenda mema ambayo Mungu alipanga yawe sehemu ya maisha yake. (Waefeso 2:10) “Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo.”
Paulo anaonyesha kuwa Wayahudi walikuwa na angalau unafuu katika kuzishika amri nne za kwanza zinazoshughulikia ibada ya kweli ya Mungu aliyeziumba mbingu na nchi. Wayahudi kupitia Maandiko Matakatifu walifunuliwa kuwa Mungu aliyeumba mbingu na nchi ndiye mwenye kustahili kuabudiwa. Walielekezwa kuwa ibada yake hufanyika kila siku ya saba ya juma kukumbuka uumbaji na kwamba kusiwepo na kawaida ya kuabudu sanamu iliyozoeleka na mataifa yanayowazunguka. Miongoni mwa mataifa yanayowazunguka waliokuwa wapinzani wakubwa wa dhana ya Mungu waliyokuwa nayo Wayahudi ni Wayunani waliosifika nyakati hizo kama watu wenye hekima kuliko wote.
Hata hivyo hekima yao inaonekana kutowasaidia kwa sababu walikuwa hawamfahamu Mungu aliyeumba mbingu na dunia licha ya kujifunua kupitia vitu vya asili. (Warumi 1:22-23) “Wakijinena kuwa wenye hekima walipumbazika; wakaubadili utukufu wa Mungu asiye na uharibifu kwa mfano wa sura ya binadamu aliye na uharibifu, na ya ndege, na ya wanyama, na ya vitambaavyo.” Hali ilikuwa hiyo hiyo pia kwa Wayahudi. (Warumi 1:21) “Kwa sababu, walipomjua Mungu hawakumtukuza kama ndiye Mungu wala kumshukuru; bali walipotea katika uzushi wao, na mioyo yao yenye ujinga ikatiwa giza.” Kutokana na hali hiyo Paulo anaonyesha injili inawahusu wote. (Warumi 1:14) “Nawiwa na Wayunani na wasio Wayunani, nawiwa na wenye hekima na wasio na hekima.”
Paulo anabainisha kuwepo kwa njia moja tu ya kunufaika na wokovu inayopatikana katika Kristo nayo ni njia ya Imani. Wayahudi, Wayunani, na wanadamu wa mataifa yote walipaswa kumwamini Yesu kama njia pekee ya wokovu. Kwa Bahati mbaya Yesu alikuwa ni kikwazo kwa Wayahudi na upuzi kwa Wayunani. (1 Wakorintho 1:22-24) “Kwa sababu Wayahudi wanataka ishara, na Wayunani wanatafuta hekima; bali sisi tunamhubiri Kristo, aliyesulibiwa; kwa Wayahudi ni kikwazo, na kwa Wayunani ni upuzi; bali kwao waitwao, Wayahudi kwa Wayunani, ni Kristo, nguvu ya Mungu, na hekima ya Mungu.”
Machukizo yanayofanywa na watu wa mataifa yanatokana na kumkataa Mungu Fulani na nguvu ya kuzalisha dhamb iliyo ndni ya mwili wa dhambi. (Warumi 1:24-27) “Kwa ajili ya hayo Mungu aliwaacha katika tamaa za mioyo yao, waufuate uchafu, hata wakavunjiana heshima miili yao. Kwa maana waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakakisujudia kiumbe na kukiabudu badala ya Muumba anayehimidiwa milele. Amina. Hivyo Mungu aliwaacha wafuate tamaa zao za aibu, hata wanawake wakabadili matumizi ya asili kwa matumizi yasiyo ya asili; wanaume nao vivyo hivyo waliyaacha matumizi ya mke, ya asili, wakawakiana tamaa, wanaume wakiyatenda yasiyopasa, wakapata nafsini mwao malipo ya upotevu wao yaliyo haki yao.”
Kuwalaumu wanaofanya vitendo hivyo vinavyokiuka maadili hakutoshi kama tatizo la kuwa na mwili wa dhambi unaozalisha hali hiyo halitafutiwi ufumbuzi. Ndani ya Kristo tatizo hilo lina ufumbuzi. (Wakolosai 3:5, 10-11) “Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu. mkivaa utu mpya, unaofanywa upya upate ufahamu sawasawa na mfano wake yeye aliyeuumba. Hapo hapana Myunani wala Myahudi, kutahiriwa wala kutokutahiriwa, mgeni wala mshenzi, mtumwa wala mwungwana, bali Kristo ni yote, na katika yote.”
Dunia ya leo kama ilivyokuwa ya wakati ule ilijawa na watu waliodhaniwa kuwa wenye hekima lakini walishindwa kutawala tamaa za mwili kwa kuwa walikuwa hawajamkaribisha mwenye kutawala mwili. Paulo katika sura ya kwanza ya Warumi anataka kuweka mzani sawa kwamba hakuna mdhambi mwenye nafuu. Kama Myunani anavyomhitaji Kristo vivyo hivyo Myahudi naye anamhitaji Kristo kama mpatanishi wao na Mungu. Injili ya Yesu Kristo ni ya watu wote kwa sababu wote wamepungua na wanahitaji neema yake ili kuokolewa. Ujio wa Yesu atakayekomesha utumwa wa dhambi ndilo lilikuwa tumaini la vizazi vyote. (Luka 2:10-11) “Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana.”
Mungu alitangulia kuwadhihirishia wanadamu wote juu ya kuwepo kwa dhambi na hatia na kuwepo kwa haki ipatikanayo kwa kumwamini Yesu. Licha ya hali zao kukosa sifa za utakatifu Paulo anawathibitishia kuwa wao Wayahudi na wasio Wayahudi ni wateule walioitwa ili wawe watakatifu. (Warumi 1:5-7) “Ambaye katika yeye tulipokea neema na utume ili mataifa yote wapate kujitiisha kwa imani, kwa ajili ya jina lake; ambao katika hao ninyi mmekuwa wateule wa Yesu Kristo; kwa wote walioko Rumi, wapendwao na Mungu, walioitwa kuwa watakatifu. Neema na iwe kwenu na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo.”
Paulo anapenyeza uzoefu mpya wa kuhesabiwa haki kwa imani ulio tofauti na ule uliozoeleka na dini ya Kiyahudi na dini ya kipagani wa kutegemea matendo ya kidini. (Warumi 1:17) “Kwa maana haki ya Mungu inadhihirishwa ndani yake, toka imani hata imani; kama ilivyoandikwa, Mwenye haki ataishi kwa imani.” Hii tafsiri yake ni kuwa Mungu hatakuwa akimhesabia hatia na hukumu mtu yoyote kwa kuangalia amefanya nini bali atamhukumu mtu kulingana na kiasi gani alimwamini au hakumwamini Yesu. Hii ni kutokana na kuwa Yesu alikidhi matakwa yote ambayo wanadamu wamekuwa wakishindwa kuyaishi na hivyo kumuondolea mwanadamu hatia na hukumu iliyokuwa inamkabili. (Warumi 5:19) “Kwa sababu kama kwa kuasi kwake mtu mmoja watu wengi waliingizwa katika hali ya wenye dhambi, kadhalika kwa kutii kwake mmoja watu wengi wameingizwa katika hali ya wenye haki.”