YESU WOKOVU NA UTII WA SHERIA
Wokovu ni mpango wa Mungu wa kumsaidia mwanadamu kuufikia uzima wa milele bila kutumia njia zake wala jitihada zake mwenyewe kwa kuwa jitihada na njia hizo zisingeweza kumsaidia kuokolewa. Mpango huu unahusisha sheria za Mungu ambazo hutumika kama njia ya kutambulisha uwepo wa dhambi na ubaya wake ingawa sheria hizo hazina uwezo wa kumuokoa mwanadamu. Hapo awali kabla mwanadamu hajaanguka dhambini utii wa sheria za Mungu uliwawezesha wanadamu wa kwanza kudumisha maisha yao ya utakatifu.
Baada ya dhambi uwezo huo wa kudumisha utakatifu kupitia utii wa sheria ulitoweka na maisha matakatifu yakawa hayawezi kudumishwa na mwanadamu kwa njia ya utii wa sheria. (Isaya 64:6) “Kwa maana sisi sote tumekuwa kama mtu aliye mchafu, na matendo yetu yote ya haki yamekuwa kama nguo iliyotiwa unajisi; sisi sote twanyauka kama jani, na maovu yetu yatuondoa, kama upepo uondoavyo.” Mwandishi mmoja maarufu wa vitabu vya Kikristo ajulikanaye kwa jina la Ellen White anasema hivi, “Anayejaribu kufika mbinguni kwa matendo yake mwenyewe katika kushika sheria anajaribu jambo lisilowezekana.”[1] Kauli hiyo haimaanishi kupinga uwepo wa sheria au kupinga hitaji la utii wa sheria. Kauli hiyo inaweka msisitizo kuwa utii wa sheria pamoja na umuhimu wake, usitumike kama njia ya kupatia uzima wa milele.
Kudumisha maisha matakatifu yenye haki kunahitaji njia au utaratibu uliobuniwa na Mungu ukichangamana na uwezo utokao kwa Mungu mwenyewe na utayari wa mwanadamu katika kutii mpango huo kwa imani. (Yeremia 23:6) “Katika siku zake Yuda ataokolewa, na Israeli atakaa salama, na jina lake atakaloitwa ni hili, Bwana ni haki yetu.” Baada ya anguko la mwanadamu haki si ya mwanadamu tena. Haki ni ya Mungu kwa kuwa ndiye anayesimama badala ya mwanadamu yeye akiwa ndani yetu na sisi tukiwa ndani yake.
Katika kulifundisha wazo la wokovu wapo wanaoliwasilisha kama hatua ya Mungu ya kumuondolea mwanadamu haja au ulazima wa kutii sheria na wapo wanaowasilisha utii wa sheria kama sharti la wokovu au la kuokolewa. Makundi yote mawili yanapotosha. Kundi la kwanza halitambui umuhimu wa utii wa sheria wakati kundi la pili halitambui udhaifu na upungufu wa mwanadamu katika kutii sheria. Dini karibu zote zinaangukia katika makundi haya mawili. Kundi la kwanza linawaaminisha watu kuwa kulikuwa na makosa katika kuwaagiza wanadamu watii sheria kwa kuwa jambo hilo halikufanikiwa.
Ni kweli jambo hilo halikufanikiwa lakini sababu ya kutofanikiwa haikutokana na upungufu katika sheria. Ilitokana na upungufu katika wanadamu waliopaswa kutii sheria. (Warumi 8:7) “Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii.” (Wagalatia 3:11) “Ni dhahiri ya kwamba hakuna mtu ahesabiwaye haki mbele za Mungu katika sheria; kwa sababu Mwenye haki ataishi kwa imani.” (Wagalatia 3:12) “Na torati haikuja kwa imani, bali, Ayatendaye hayo ataishi katika hayo.”
Wawasilishaji wa hoja hii wakati fulani wanaonekana kuwalaumu Wayahudi au hata kumlaumu Musa ambaye kwa mtazamo wao hudai ndiye aliyewaamuru Wayahudi kutii sheria ili waokolewe. Wanasahau au wanajisahaulisha kuwa Musa alipokea maagizo ya Torati kutoka kwa Mungu mwenyewe. (Malaki 4:4) “Ikumbukeni torati ya Musa, mtumishi wangu, niliyomwamuru huko Horebu kwa ajili ya Israeli wote, naam, amri na hukumu.” Musa asingeweza kutopokea Torati kutoka kwa Mungu wala asingeacha kuwasisitiza Wayahudi kutii maagizo ya Torati. Wenye madai hayo hata hivyo wanayo mafungu wanayoyatumia kuunga mkono hoja hiyo. (Yohana 1:17) “Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo.” (Kumbukumbu la Torati 4:44) “Na torati Musa aliyowawekea wana wa Israeli ni hii; haya ndiyo mashuhudizo, na amri, na hukumu, Musa alizowaambia wana wa Israeli walipotoka Misri.” (Yoshua 8:32) “Akaandika huko juu ya mawe hayo nakala ya torati ya Musa, aliyoiandika mbele ya wana wa Israeli.”
Ni kweli Musa aliandika torati hata ikajulikana kama torati ya Musa. Lakini mausia yaliyokuwamo kwenye torati hiyo hayakuwa ya Musa. (1 Wafalme 2:1-3) “Basi siku ya kufa kwake Daudi ikakaribia, akamwusia Sulemani mwanawe, akasema, Mimi naenda njia ya ulimwengu wote; basi uwe hodari, ujionyeshe kuwa mwanamume; uyashike mausia ya Bwana, Mungu wako, uende katika njia zake, uzishike sheria zake, na amri zake, na hukumu zake, na shuhuda zake, sawasawa na ilivyoandikwa katika torati ya Musa, upate kufanikiwa katika kila ufanyalo, na kila utazamako.”
Waisraeli au Wayahudi hawakuwa na makosa kutii torati ya Musa maana torati ile ilikuwa ni mausia ya Mungu kwao. Jambo ambalo baadhi ya wafundishaji wa Maandiko au ambalo hata Wayahudi wenyewe hawakulielewa ni kuwa torati iliagizwa kwa Waisraeli wakiwawakilisha wanadamu wote na ilikuwa idumu kwa muda maalum na kufikia mwisho kabla utaratibu mwingine haujachukua nafasi yake. (Wagalatia 3:24) “Hivyo torati imekuwa kiongozi kutuleta kwa Kristo, ili tuhesabiwe haki kwa imani.” (Waebrania 10:1) “Basi torati, kwa kuwa ni kivuli cha mema yatakayokuwa, wala si sura yenyewe ya mambo hayo, kwa dhabihu zile zile wanazozitoa kila mwaka daima, haiwezi wakati wo wote kuwakamilisha wakaribiao.”
Torati inapingana na wokovu?
Je torati ilikuwa inapingana na wokovu? Wokovu ni mpango uliotoka kwa Mungu wa kumsaidia mwanadamu kuufikia uzima wa milele bila kutumia njia zake wala jitihada zake mwenyewe. Torati ni utaratibu uliotoka kwa Mungu wenye kusudi la kumwonyesha mwanadamu ubaya wa dhambi na ilivyo vigumu kufikia wokovu kwa kutii maagizo ya Mungu kwa juhudi za kibinadamu. Hii inatokana na ukweli kuwa mwanadamu aliyeanguka dhambini hawezi kujiokoa kwa kwa kutumia njia anazozibuni au kwa kutumia uwezo wake mwenyewe. Ingawa torati haikubuniwa na watu iliwekwa kwa kusudi la kuwatazamisha kwa Kristo mwenye suluhisho la matatizo yatokanayo na mwanadamu kushindwa kutii ahadi zake. Mungu alipouweka mpango wa wokovu na kuukamilisha kilichokuwa kinahitajika ni mwanadamu kutambua asivyo na uwezo wa kujiokoa na kukubali kutumia njia zinazotolewa na Mungu kama suluhisho la mapungufu yake. Na mara tu mwanadamu anapokubali kufanya hivyo anaingia kwenye mkataba na Mungu mkataba unaotambulika kama agano. Hatua ya kwanza ya agano la Mungu na wanadamu wote lilitokea pale Edeni wakati alipotoa tamko hili la Agano. (Mwanzo 3:15) “Bwana Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha yako; nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino.”
Katika tamko hili la agano Mungu anaahidi kutuma yule anayemwita uzao kuja kukamilisha yote yanayohitajika kwenye agano hilo kwa niaba ya mwanadamu. Agano hili ndilo la milele linalohakikisha dhambi na mapungufu mengine yote ya wanadamu yanatafutiwa ufumbuzi wa kudumu. Agano ambalo Mungu alilifanya na Ibrahimu linaakisi kwa karibu agano hili lililofanyika Edeni. (Mwanzo 17:7) “Agano langu nitalifanya imara kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, na vizazi vyao, kuwa agano la milele, kwamba nitakuwa Mungu kwako na kwa uzao wako baada yako.” Agano hili tofauti na mtazamo wa Waisraeli na waelimishaji wengine halikuwa linamlenga Isaka kama mzao aliyeahidiwa kwenye Agano la Edeni licha ya kuwa Mungu mwenyewe alidokeza Isaka kuwa ndiye angekuwa utimizo wa mzao aliyeahidiwa. (Mwanzo 21:12) “Mungu akamwambia Ibrahimu, Neno hili lisiwe baya machoni pako, kwa ajili ya huyo mwana, na huyo mjakazi wako. Kila akuambialo Sara, sikiza sauti yake, kwa maana katika Isaka uzao wako utaitwa.”
Hata hivyo mzao aliyekuwa analengwa kwenye agano la Mungu na Ibrahimu alikuwa ni Kristo. (Wagalatia 3:16) “Basi ahadi zilinenwa kwa Ibrahimu na kwa mzao wake. Hasemi, Kwa wazao, kana kwamba ni wengi, bali kana kwamba ni mmoja, Kwa mzao wako, yaani, Kristo.” Huyu ndiye aliyekuwa anatarajiwa kukamilisha agalo na ahadi iliyotolewa pale Edeni na kurejelewa kwenye agano alilolifanya Mungu kwa Ibrahimu. Yesu anakamilisha agano la awali kwa kukidhi vigezo vyote vinavyokamilisha agano hilo ambavyo Isaka wala torati haikuwa navyo. (Waebrania 8:6) “Lakini sasa amepata huduma iliyo bora zaidi, kwa kadiri alivyo mjumbe wa agano lililo bora, lililoamriwa juu ya ahadi zilizo bora.”
Agano la msalabani lilikuwa bora zaidi kuliko agano la kale ambalo Mungu alilifanya baina yake na Waisraeli pale Sinai ingawa maagano yote yalifanyika mlimani. Kwenye agano la Sinai Waisraeli wakiwawakilisha wanadamu wote wanaahidi kutenda yote yaliyoagizwa kwenye torati wakati kwenye agano la msalaba mzao mmoja anaahidi kutenda yote kwa niaba ya wanadamu. (Kutoka 24:6-7) “Musa akatwaa nusu ya ile damu, akaitia katika mabakuli; na nusu ya ile damu akainyunyiza juu ya madhabahu. Kisha akakitwaa kitabu cha agano akakisoma masikioni mwa watu; wakasema, Hayo yote aliyoyanena Bwana tutayatenda, nasi tutatii.”
Mungu anapozindua agano jipya la msalaba anataja sababu za kuondokana na Agano la Kale la mlima Sinai. (Waebrania 8:8-9) “Maana, awalaumupo, asema Angalia, siku zinakuja, asema Bwana, Nami nitawatimizia nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda agano jipya; Halitakuwa kama agano lile nililoagana na baba zao, Katika siku ile nilipowashika mikono yao niwatoe katika nchi ya Misri. Kwa sababu hawakudumu katika agano langu, Mimi nami sikuwajali asema Bwana.” Anachosema hapa mtumishi wa Mungu ni kuwa agano la Sinai lilikuwa na mapungufu. Na mapungufu haya hayakutokana na Musa aliyeandika torati wala mapungufu haya hayatokani na kuwepo kwa sheria ndani ya agano hilo.
Kimsingi agano hili la Sinai linaitwa pia agano la Amri Kumi. (Kumbukumbu la Torati 4:13) “Akawahubiri agano lake, alilowaamuru kulitenda, yaani, zile amri kumi; akaziandika juu ya mbao mbili za mawe.” Hivyo Mungu ndiye aliyeagiza kuwapo kwa amri kumi kwenye agano la Sinai. Upungufu wa agano hili ulikuwa kwa wanadamu walioahidi kufanya wasicho na uwezo nacho na siyo amri wala sheria zilizokuwemo ndani ya hilo Agano. Sheria zinabaki kuwa sehemu ya agano katika agano jipya kama zilivyokuwa sehemu ya agano la Sinai au agano la kale. Hazikubadilika. Kilichokuwa kimebadilika ni mahali zinapoandikwa. Katika agano la Sinai ziliandikwa kwenye mbao mbili za mawe lakini katika agano jipya zinaandikwa mioyoni mwa washiriki wa agano. (Waebrania 8:10) “Maana hili ndilo agano nitakaloagana na nyumba ya Israeli Baada ya siku zile, asema Bwana; Nitawapa sheria zangu katika nia zao, Na katika mioyo yao nitaziandika; Nami nitakuwa Mungu kwao, Nao watakuwa watu wangu.”
Torati haikuingizwa kupitia agano lenye ahadi zilizo bora zaidi zinazotimizwa na mzao aliyeahidiwa kwenye agano jipya ambalo Mungu anaagana na wanadamu wote. Torati iliingizwa ili kulifanya kosa la mwanadamu kuwa kubwa na kujenga mazingira ya kumhitaji mkombozi atakayewatoa kwenye madhila hayo. (Wagalatia 3:17) “Nisemalo ni hili; agano lililothibitishwa kwanza na Mungu, torati iliyotokea miaka mia nne na thelathini baadaye hailitangui, hata kuibatilisha ile ahadi.” Agano la ahadi ya kuwepo mzao atakayemponda kichwa Shetani halioani na agano ambapo mwanadamu mwenyewe kwa kutumia jitihada zake anamponda kichwa shetani kwa kutii sheria.
Sababu ya kuwepo kwa torati si kuendeleza ahadi iliyotolewa ya Mungu kumsaidia mwanadamu kuirejea hali ya kuwa na haki aliyoipoteza kwa njia ya yeye mwenyewe kujitahidi awezavyo kutii maagizo ya torati. Bali torati iliingizwa ili kukuza utambuzi wa tatizo la dhambi na umuhimu wa kuwepo kwa mzaliwa aliyeahidiwa. (Wagalatia 3:19) “Torati ni nini basi? Iliingizwa kwa sababu ya makosa, hata aje huyo mzao aliyepewa ile ahadi; iliamriwa kwa utumishi wa malaika kwa mkono wa mjumbe.” Torati inaposhikwa nje ya matarajio ya mzao aliye ufumbuzi kamili wa dhambi inakwenda kinyume na makusudio ya kuingizwa kwake.
Kuishika torati hakukuwa kunamhesabia mtu haki bali kulikuwa kunamwonyesha alivyo na mapungufu yanayohitaji Mwanakondoo wa Mungu azichukuaye dhambi zote za dunia achinjwe ili kuwahesabia haki wale waishikao torati. Sheria zote zilizoagizwa na kuamuriwa katika torati hazikuwa na uwezo wa kumhesabia haki mwanadamu. (Wagalatia 3:21) “Basi je! Torati haipatani na ahadi za Mungu? Hasha! Kwa kuwa, kama ingalitolewa sheria iwezayo kuhuisha, yakini haki ingalipatikana kwa sheria.” Ahadi za Mungu zililenga kuhuisha yaani kumrejesha mwanadamu pale alipokuwapo kabla ya dhambi. Na ahadi hizi zilikuwa zitekelezwe na Yesu aliye mzao aliyeahidiwa na hazikulenga kutekelezwa na torati. Kuwepo kwa torati hakusitishi wala kuondoa kuwepo kwa ahadi. Torati inatumika kama Daraja ya kutuleta kwa Ahadi pale tutakapotambua tusivyoweza kutii maagizo ya torati.
Yesu ndiye aliyechinjwa wakati wa kuweka misingi ya dunia akiwakilisha Wanyama wote watakaochinjwa katika maagizo ya torati kama ishara ya ondoleo la dhambi. (Ufunuo wa Yohana 13:8) “Na watu wote wakaao juu ya nchi watamsujudu, kila ambaye jina lake halikuandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo, aliyechinjwa tangu kuwekwa misingi ya dunia.” Kuwepo kwa huduma ya kuchinja Wanyama kama ondoleo la dhambi kulikofanyika wakati wa Agano la Kale kulikuwa kivuli cha kuchinjwa kwa Mwanakondoo kulikofanyika wakati wa kuwekwa misingi ya dunia na ambako kulikamilika pale msalabani. Wanyama wale waliochinjwa kwa kufuata maagizo ya torati hawakuwa na uwezo wa kuondoa dhambi. (Waebrania 9:9) “Ambayo ndiyo mfano wa wakati huu uliopo sasa; wakati huo sadaka na dhabihu zinatolewa, zisizoweza kwa jinsi ya dhambi kumkamilisha mtu aabuduye.”
Torati iliingizwa ili kuonesha nguvu ya dhambi na jinsi mwanadamu asivyoweza kushindana na dhambi bila msaada wa Mungu. (1 Wakorintho 15:56) “Uchungu wa mauti ni dhambi, na nguvu za dhambi ni torati.” Hapa tunajulishwa kuwa chimbuko la mauti ni dhambi na chimbuko la dhambi ni torati. Huwezi kushughulikia mauti bila kushughulikia dhambi na huwezi kushughulikia dhambi bila msaada wa torati inayoifunua dhambi. torati inamsaidia mwanadamu ambaye mara nyingi ana kawaida ya kujihesabia haki. Torati inamkanya mwanadamu asithubutu kujiona asiye na dhambi kwa kuwa kazi ya ukombozi ni ngumu kwa asiyejitambua alivyo mdhaifu.
Torati iliingizwa ili kuwaadabisha wanadamu wasijione kuwa wana uwezo wa kujihesabia haki. (Warumi 3:19-20) “Basi twajua ya kuwa mambo yote inenayo torati huyanena kwa hao walio chini ya torati, ili kila kinywa kifumbwe, na ulimwengu wote uwe chini ya hukumu ya Mungu; kwa sababu hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki mbele zake kwa matendo ya sheria; kwa maana kutambua dhambi huja kwa njia ya sheria.” Midomo kufumbwa ni kwa muhimu ili ukombozi wa mwanadamu uchukue nafasi yake. Hata wanaofanyiwa upasuaji wanakuwa katika hali ya kufa ili kufanikisha upasuaji. Kushindwa kwa Waisraeli kuitii torati ni Ushahidi kuwa wanadamu wote ni wadhaifu wanaohitaji msaada kutoka nje kwa aliye na uwezo zaidi yao.
Torati iliingizwa ili kuwaonyesha wanadamu ilivyo vigumu kutii maagizo yake katika mwili wa dhambi na ilivyo muhimu mwili huu wa dhambi uhukumiwe kwa njia ya kifo cha Kristo ili kuwawezesha wanadamu kuitii torati kikamilifu ingawa si kwa nia ya kununua wokovu au uzima wa milele. (Warumi 8:3-4) “Maana yale yasiyowezekana kwa sheria, kwa vile ilivyokuwa dhaifu kwa sababu ya mwili, Mungu, kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe katika mfano wa mwili ulio wa dhambi, na kwa sababu ya dhambi, aliihukumu dhambi katika mwili; ili maagizo ya torati yatimizwe ndani yetu sisi, tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali mambo ya roho.”
Miongoni mwa mambo muhimu Yesu aliyoyafanya kwa kufa kwake msalabani ni kuwarejeshea wanadamu uwezo wa kutii sheria uliopotea baada ya anguko la dhambi. Uwezo huo ulipotea pale mwili uliposhindwa kutii au kutimiza maagizo ya sheria kwa kuwa ulikuwa hauwezi kustahimili maagizo hayo. Na mwili ulishindwa kustahimili maagizo hayo kwa sababu ulikuwa na udhaifu. Udhaifu huo sasa umeondolewa. Kutii sheria badala ya kuwa jambo la kuhuzunisha limebadilika na kuwa jambo liletalo furaha. (Zaburi 119:165) “Wana amani nyingi waipendao sheria yako, Wala hawana la kuwakwaza.” Baada ya mabadiliko haya yaliyoletwa na kifo cha Kristo, mwanadamu anaipenda sheria ya Bwana vizuri sana maana Kristo amempatanisha nayo. (Zaburi 119:97) “Sheria yako naipenda mno ajabu, Ndiyo kutafakari kwangu mchana kutwa.”
Ugomvi na sheria uliisha pale madai ya sheria yalipotimizwa katika maisha ya Kristo. (Warumi 7:1) “Ndugu zangu, hamjui (maana nasema na hao waijuao sheria) ya kuwa torati humtawala mtu wakati anapokuwa yu hai?” Hoja anayoileta Paulo hapa ni kuwa Yesu alipochukua mwili wa kibinadamu alifanya hivyo ili madai yote ya torati yaelekezwe kwake kwa niaba ya wanadamu wote. Na alipokufa pale msalabani alikuwa anakufa kwa niaba ya wanadamu wote walioshindwa kutimiza madai ya torati. (Wagalatia 3:10) “Kwa maana wale wote walio wa matendo ya sheria, wako chini ya laana; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu asiyedumu katika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha torati, ayafanye.”
Waisraeli ama Wayahudi walikuwa wanawakilisha jamii yote ya wanadamu waliokuwa chini ya sheria. Kuwa chini ya sheria au kuwa watu wa matendo ya sheria kama ilivyotumika hapa kunamaanisha waliokuwa wanadaiwa kuonyesha utii kwa sheria. Wanadamu kwa uwakilishi wa Waisraeli waliposhindwa kuonyesha utii kwa sheria wakawa chini ya laana ya torati. Yesu kupitia mwili wake wa kibinadamu unaowakilisha wanadamu wote akafanyika laana maana aliwakilisha wanadamu walioshindwa kutii maagizo ya torati. (Wagalatia 3:13) “Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti.”
Kiteondo hicho cha kufanyika laana na kulipa madai ya torati kwa kifo chake, alikomesha uwezo wa torati kumtawala mtu kwa kuwa adhabu ya torati imetimizwa na wanadamu waliotakiwa kuhukumiwa kwa kushindwa kutimiza madai ya torati wamehukumiwa kupitia kifo cha mmoja aliyefanyika laana ingawa yeye mwenyewe hakuwahi kupingana na maagizo ya torati. Torati haikufikia ukomo wake kwa sababu ilikosewa ilifikia ukomo wake kwa kuwa madai yake yalitimizwa na mmoja aliyewawakilisha wanadamu aliuawa kwa sababu aliowafia walishindwa kutimiza maagizo ya torati. Sasa torati haimtawali tena mwanadamu maana hadaiwi nayo.
Yesu ndiye utimilifu wa torati. Waisraeli na Wayahudi walitakiwa wamuone Yesu katika maagizo yote ya torati. Wayahudi walioshindwa kumuona Yesu katika maagizo yote ya torati ndiyo hatimaye waliomkataa Yesu alipokuja kuitimiliza torati. (Yohana 12:34) “Basi mkutano wakamjibu, Sisi tumesikia katika torati ya kwamba Kristo adumu hata milele; nawe wasemaje ya kwamba imempasa Mwana wa Adamu kuinuliwa? Huyu Mwana wa Adamu ni nani?” Lakini wale waliomuona Kristo katika maagizo yote ya torati waliweza kumpokea kama masihi na mzao aliyeahidiwa katika agano la kwanza. (Yohana 1:45) “Filipo akamwona Nathanaeli, akamwambia, Tumemwona yeye aliyeandikiwa na Musa katika torati, na manabii, Yesu, mwana wa Yusufu, mtu wa Nazareti.” (Mathayo 5:17) “Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza.” (Luka 24:44) “Kisha akawaambia, Hayo ndiyo maneno yangu niliyowaambia nilipokuwa nikali pamoja nanyi, ya kwamba ni lazima yatimizwe yote niliyoandikiwa katika Torati ya Musa, na katika Manabii na Zaburi.”
Hoja kuwa torati haikufuata mtiririko wa ahadi za wokovu zilizowekwa kwenye agano ambalo Mungu alilifanya na wanadamu pale Edeni ina ukweli unaoungwa mkono na Maandiko kadhaa. Agano la Kale kwa njia ya torati badala ya kuja na ufumbuzi wa tatizo la mwanadamu kama ilivyoahidiwa kule Edeni likatumika kama njia ya kuonyesha ukubwa wa tatizo. Wanadamu wote walio Wayahudi na wasio Wayahudi walikabiliwa na madai ya torati. (Warumi 2:14-15) “Kwa maana watu wa Mataifa wasio na sheria wafanyapo kwa tabia zao yaliyo ndani ya torati, hao wasio na sheria wamekuwa sheria kwa nafsi zao wenyewe. Hao waionyesha kazi ya torati iliyoandikwa mioyoni mwao, dhamiri yao ikiwashuhudia, na mawazo yao, yenyewe kwa yenyewe, yakiwashitaki au kuwatetea.” Torati badala ya kuja na mtiririko wa ahadi ilikazia umuhimu wa utii, ubaya wa dhambi, na jinsi mwanadamu asivyoweza kujiokoa kwa jitihada zake.
Torati ya Musa ilisheheni maagizo yahusuyo ibada za hema takatifu au hekaluni zilizoandamana na uchinjaji wa Wanyama kwa ajili ya ondoleo la dhambi zilizokuwa zinamlenga Kristo. Uchinjaji wa Wanyama ulihusika pia katika kumbukumbu la kutoka utumwani lililojulikana kama pasaka ya wayahudi ambapo Wanyama pia walichinjwa wakiwakilisha kifo cha Kristo atakayechinjwa ili kuwaweka huru wanadamu kutoka kifungo cha dhambi. (1 Wakorintho 5:7 Basi, jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya, kama vile mlivyo hamkutiwa chachu. Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo.”
Torati ilisheni pia sheria na maagizo ya uadilifu yaliyokuwa yanaainisha na kuratibu mahusiano ya wanadamu kwa wanadamu wenzao na mahusiano ya wanadamu kwa Mungu wao. (Mathayo 22:35-40) “Mmoja wao, mwana-sheria, akamwuliza, akimjaribu; Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu? Akamwambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii.” Amri mbili Kristo anazozitaja hapa ni ufupisho wa maagizo na maamrisho yote yaliyopo kwenye torati. Kama tulivyosema awali maagizo ya Amri Kumi za Mungu yalikuwako kwenye torati na kwenye agano la Sinai. Amri hizi tofauti na maagizo mengine ya sheria yaliyopo kwenye torati yaliwahusu wanadamu wa mahali pote na wa nyakati zote. Maagizo ya Amri Kumi hayakulenga kuishia msalabani kama madai mengine yaliyopo kwenye torati. Ndiyo maana kijana Tajiri aliyetaka kujua afanye nini ili akolewe alikumbushwa kuzishika Amri za Mungu. (Marko 10:17-20) “Hata alipokuwa akitoka kwenda njiani, mtu mmoja akaja mbio, akampigia magoti, akamwuliza, Mwalimu mwema, nifanye nini nipate kuurithi uzima wa milele? Yesu akamwambia, Kwa nini kuniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu. Wazijua amri, Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo, Usidanganye, Waheshimu baba yako na mama yako. Akamwambia, Mwalimu, haya yote nimeyashika tangu utoto wangu.”
Pamoja na kujua kwamba wanadamu hawakuwa na uwezo wa kuzishika amri za Mungu bila msaada wa Mungu bado Kristo yeye mwenyewe alizishika amri hizo na kuwahimiza watu kuzishika pia. (Yohana 15:10) “Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake.” Yesu haagizi tu watu kuzishika amri za Mungu bali pia anaagiza wazifundishe. (Mathayo 5:19) “Basi mtu ye yote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni.” Tena wale wanaojihusisha katika kuzishika na kuzifundisha haahidi tu kuwaita wakubwa, bali pia anaahidi kuwaita rafiki zake. (Yohana 15:14) “Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo.”
Kimsingi hakuna mgogoro kati ya sheria au amri na wokovu ulioletwa na Kristo. Maana wokovu ni kuhesabiwa haki na kuhesabiwa haki huja baada ya kutambua mapungufu yako yaliyofunuliwa na sheria. (Warumi 7:8) “Lakini dhambi ilipata nafasi kwa ile amri, ikafanya ndani yangu kila namna ya kutamani. Kwa maana dhambi bila sheria imekufa.” (Warumi 4:15) “Kwa sababu sheria ndiyo ifanyayo hasira; maana pasipokuwapo sheria, hapana kosa.” Wokovu ni njia iliyowekwa na Mungu kushughulikia dhambi. Ili mtu aokolewe ni lazima kwanza asaidiwe kutambua kuwa ni mwenye dhambi. Mwanadamu anatakiwa kujitambua kuwa ni mwenye dhambi kwa sababu moyo wake una kawaida ya kumdanganya kwamba hana tatizo. (Yeremia 17:9) “Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua?”
Moyo huweza kumfanya mtu ajisikiye hana dhambi na hivyo hahitaji kuokolewa. Ili kuusaidia moyo usimdanganye mwanadamu Mungu aliweka sheria mioyoni ili wanapoikiuka wasikie hatia na haja ya kutubu. (Warumi 2:14-15) “Kwa maana watu wa Mataifa wasio na sheria wafanyapo kwa tabia zao yaliyo ndani ya torati, hao wasio na sheria wamekuwa sheria kwa nafsi zao wenyewe. Hao waionyesha kazi ya torati iliyoandikwa mioyoni mwao, dhamiri yao ikiwashuhudia, na mawazo yao, yenyewe kwa yenyewe, yakiwashitaki au kuwatetea.” Pamoja na kuwa katika Agano la Kale sheria ziliandikwa kwenye mbao za mawe Mungu hakusahau kuziandika mioyoni. Unapohisi moyo kuuma baada ya kutenda dhambi hiyo ni sheria iliyoandikwa moyoni iliyowekwa hapo ili ikukoseshe amani unapotenda dhambi. Hayo maumivu unayoyasikia ni hatia inayotoka kwenye dhamira, inayotokana na kuvunja sheria.
Kama ambavyo mchakato wa matibabu kwenye vituo vya afya mara nyingi huanzia maabara ndivyo ambavyo mchakato wa wokovu huanzia kwenye matumizi ya sheria ambayo kazi yake kubwa ni kuitambulisha dhambi. (Warumi 3:20) “Kwa sababu hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki mbele zake kwa matendo ya sheria; kwa maana kutambua dhambi huja kwa njia ya sheria.” Kwa hiyo kutotambua sheria ni kutotambua chombo kinachoitambulisha dhambi ndani ya maisha yako. Ni kutotoa ushirikiano kwa vyombo vinavyotambulisha kuwepo kwa dhambi, aina ya dhambi, na ukubwa wa dhambi yenyewe, ili iwe rahisi kutoa msaada unaohitajika kwa mwathirika. Na mtu asiyetaka kutambua kama ana dhambi hana nia ya dhati ya kuokolewa.
Ni kawaida ya sheria kumkera aliyeikosea. Kero hiyo yaweza kuzalisha unyenyekevu au kuzalisha kiburi na jeuri. Hali hiyo ya kukera kwenye Maandiko inatambuliwa kama kuchomwa moyo. Neno la Mungu na sheria vina kawaida ya kuchoma moyo. (Yeremia 36:23) “Hata ikawa, Yehudi alipokuwa amekwisha kusoma kurasa tatu nne, mfalme akalikata kwa kijembe, akalitupa katika moto wa makaa, hata gombo lote likawa limekwisha kuteketea katika huo moto wa makaa. Mtu wa kawaida huwa hana ustahimilifu na mtu au kitu kinachoweka wazi mapungufu yake. (Matendo ya Mitume 5:33) “Petro na mitume wakajibu, wakisema, Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu. Mungu wa baba zetu alimfufua Yesu, ambaye ninyi mlimwua mkimtundika katika mti. Mtu huyo Mungu amemtukuza kwa mkono wake wa kuume, awe Mkuu na Mwokozi, awape Waisraeli toba na msamaha wa dhambi. Na sisi tu mashahidi wa mambo haya, pamoja na Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wote wamtiio. Wao waliposikia wakachomwa mioyo yao; wakafanya shauri kuwaua.”
Neno la Mungu kama ilivyo sheria yake vinapomkera mtu huweza kuinua vita na mapambano makali kutoka kwa mtu huyo. Ni vita kama ile inayoibuka mtu anapopewa matokeo ya vipimo vya afya vinayothibitisha kuwa ana ugonjwa ambao asingependa kuwa nao. Sheria ya Mungu na Neno la Mungu vimekuwa kwa muda mrefu wahanga wa wanadamu vikipigwa vita ili visifanye kazi yake ya kuibua mapungufu ya wanadamu. (Danieli 8:12) “Na jeshi likatolewa kwake pamoja na sadaka ya kuteketezwa ya daima, kwa sababu ya makosa; nayo ikaiangusha kweli hata chini; ikatenda ilivyopenda, na kufanikiwa.” Kweli iliyoangushwa chini hapa ni Neno la Mungu (Yohana 17:17) kwa kuwa ilionekana ikiwakera watendao maovu. Yohana alifungwa kisiwa cha Patmo kwa sababu ya kutetea Neno la Mungu (Ufunuo 1:9).
Hii ndiyo sababu Shetani anafanya vita na wote wapendao kusisitiza umuhimu na nafasi ya sheria au amri katika mpango wa wokovu. (Ufunuo wa Yohana 12:17) “Joka akamkasirikia yule mwanamke, akaenda zake afanye vita juu ya wazao wake waliosalia, wazishikao amri za Mungu, na kuwa na ushuhuda wa Yesu; naye akasimama juu ya mchanga wa bahari.” Hataki watu watambue makosa, dhambi na uovu wao vinavyofunuliwa na sheria ya Mungu. anataka wabaki katika dhambi zao huku wakijifariji kuwa hawana hatia. Pamoja na kuwa sheria haiokoi lakini kuiondoa kwenye mchakato wa wokovu kunafanya wanadamu wasinufaike na wokovu huo. Sawa na vile ambavyo maabara haiponyi ugonjwa lakini kuiondoa kwenye mchakato wa matibabu kunaweza kusimnufaishe mgonjwa na huduma bora za tiba zilizo kwenye hospitali husika kwa kuwa wahudumu wale watashindwa kutambua ugonjwa unaomsumbua mgonjwa na hivyo kushindwa kumsaidia kikamilifu.
Kwa upande mwingine Sheria ya Mungu, au Neno la Mungu huweza kupokelewa vizuri licha ya tabia yake ya kukera wanaoibuliwa mapungufu yao. (Matendo ya Mitume 2:36-39) “Basi nyumba yote ya Israeli na wajue yakini ya kwamba Mungu amemfanya Yesu huyo mliyemsulibisha kuwa Bwana na Kristo. Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu? Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu. Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie.”
Wayahudi waliamini kuwa hawakuwa na hatia mbele za Mungu kwa kitendo cha cha kumsulubisha Yesu. Hata hivyo kwa ujasiri Paulo alipowadhirishia makosa yao mioyo yao ilichomwa na wakatambua kuwa walikosea na kutubu. Hapa lengo la kuwepo kwa sheria iliyoandikwa mioyoni likawa limetimia. Ili kidonda kipone kinahitaji kusafishwa na wakati mwingine kisuguliwe ili kuondoa uchafu na utando wa usaha. Zoezi hilo husababisha maumivu lakini huharakisha uponyaji. Ndivyo ilivyo sheria ya Mungu inapotumika kuleta toba kwa mwanadamu. Kila sheria iliyovunjwa hurejeshwa kupitia toba. Na hapa ndipo unapokuja umuhimu wa kuwa na sheria au neno lisilogoshiwa. (1 Petro 2:2) “Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu.”
Kughoshiwa ni kupunguzwa nguvu au viwango kwa kitu kunakofanya kitu kile kisiwe na uwezo uliokuwa umekusudiwa hapo awali. Neno au sheria ya Mungu iliyoghoshiwa huipunguzia uwezo wake wa kuponya. Hivyo shetani kama atashindwa kuiondoa kabisa sheria au neno la Mungu atajitahidi kupunguza nguvu au kughoshi sheria na neno la Mungu ili visiwe na nguvu ile ile iliyokusudiwa hapo mwanzo. Jambo hilo limefanyika kwa sheria za Mungu na neno lake. Matokeo yake ni kuwa wale wanaorekebisha mienendo yao kwa msaada wa sheria inayofunua mapungufu yao hushindwa kupata badiliko lililokusudiwa kupitia sheria zilizobadilishwa au zilizoondolewa. (Yakobo 2:10-11) “Maana mtu awaye yote atakayeishika sheria yote, ila akajikwaa katika neno moja, amekosa juu ya yote. Kwa maana yeye aliyesema, Usizini, pia alisema, Usiue. Basi ijapokuwa hukuzini, lakini umeua, umekuwa mvunja sheria.”
Kuukulia wokovu ni kurekebisha makosa yaliyotokana na uvunjaji wa sheria. Ni sawa na kushona suti mpya kwa kulinganisha na suti uliyonayo ili mtu anayeiangalia suti ya pili asione tofauti yoyote na suti ya kwanza. Katika hali hiyo kama mhusika ataleta kwa fundi suti ambayo mkono wake mmoja ulikatwa kimakosa suti ya pili itaendeleza kosa hilo hilo. Ndiyo maana sheria au amri kumi zilizotolewa Sinai zinapaswa kufanana na na Amri Kumi zinazotumika leo na Wakristo. Zisibadilike yodi au sentensi yoyote maana hali hiyo itaakisiwa kwenye tabia ya yule anayetumia sheria hiyo mpya katika kuukulia wokovu wake.
Amri kumi au sheria za Mungu ndizo zinazowatambulisha wale walio kwenye mchakato wa wokovu kwa kuwa huakisi tabia zinazokubaliana na matakwa ya sheria zilizozalishwa na nguvu ya Mungu iliyo ndani ya yule anayefanyiwa mchakato wa wokovu. (Ezekieli 20:12) “Tena naliwapa sabato zangu, ziwe ishara kati ya mimi na wao, wapate kujua ya kuwa mimi, Bwana, ndimi niwatakasaye.” Amri ya nne ya Mungu inaonekana kubeba utambulisho wa watu wanaoukulia wokovu. Kwamba Mungu analo kundi la watu anaowapitisha kwenye mchakato wa wovu na namna mojawapo ya kuwatambua watu hao ni kwamba watakuwa wanatunza Sabato. (Ufunuo wa Yohana 14:12) “Hapa ndipo penye subira ya watakatifu, hao wazishikao amri za Mungu, na imani ya Yesu.” (Yohana 14:15) “Mkinipenda, mtazishika amri zangu.”
Mungu alipokuwa anaunda utaratibu wa utii wa sheria hakukukusudia mwanadamu ajitwishe jukumu la kuzishika sheria hizo kwa juhudi zake mwenyewe kwa lengo la kujipatia wokovu kwa kuwa ni jambo lisilowezekana. (Warumi 8:7) “Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii.” (Wagalatia 5:17) “Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka.” Mungu alikuwa ameandaa utaratibu ili nguvu yake atakayoiweka ndani yetu ituwezeshe kutii amri na maagizo mengine yote. (Wafilipi 2:13) “Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema.” (Waefeso 3:20) “Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu.”
Mwanadamu aliye kwenye mchakato wa wokovu anaposhika amri za Mungu kwa msaada wa nguvu iliyomo ndani yake jambo hilo halimuongezei uwezekano wa kuokolewa maana alishaokolewa tayari bali humuongezea amani na furaha kwa kuwa amri zilizokuwa ngumu hapo mwanzo sasa zimekuwa si nzito tena. (Zaburi 119:165) “Wana amani nyingi waipendao sheria yako, Wala hawana la kuwakwaza.” (1 Yohana 5:3) “Kwa maana huku ndiko kumpenda Mungu, kwamba tuzishike amri zake; wala amri zake si nzito.” Mwanadamu asiyetumia nguvu za Mungu kushika sheria hutumia nguvu zake mwenyewe na kitendo hicho huifanya sheria kuwa ngumu na mzito. Katika kujaribu kupunguza ugumu na uzito huo watu hawa hujaribiwa kuzipunguzia makali sheria hizo kwa kuzitafsiri kinyume, kwa kuzibadilisha, ama kwa kuziondoa kabisa.
Yesu alilipinga wazo la kuziondoa amri au kuzipunguzia makali ama kwa lengo la kujipatia unafuu wa kuzishika ama kwa lengo la kujiongezea umaarufu kwa wanadamu. Wayahudi walizishika amri zote bila kupunguza mojawapo kama ilivyofanyika katika kipindi cha Ukristo ambao walibadilisha amri ya nne na kuondoa amri ya pili. Wayahudi waliamini kuwa kushika sehemu ya sheria huku ukiziacha zingine ilikuwa ni jambo lisilokubalika na lisilo na manufaa. (Yakobo 2:11) “Kwa maana yeye aliyesema, Usizini, pia alisema, Usiue. Basi ijapokuwa hukuzini, lakini umeua, umekuwa mvunja sheria.”
Kosa la Wayahudi lilikuwa katika kuzipunguzia uzito amri ya tano hadi ya kumi zilizokuwa zinaratibu mahusiano ya wanadamu na kuziongezea uzito amri ya kwanza hadi ya nne zilizokuwa zinaratibu uhusiano wa Mungu na wanadamu na maagizo ya torati yaliyokuwa yanahusu usafi wa mwili. Wayahudi waliweza kumleta mwanamke aliyefumaniwa kwenye uzinzi apigwe mawe hadi kufa hata kama mioyoni mwao walikuwa wanamtamani. Kule kumtamani wao hawakuona kama ni kuzini. Yesu alirekebisha mtazamo huo potofu. (Mathayo 5:27-28) “Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini; lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake.”
Yesu alikusudia kuzifanya sheria kuwa za rohoni kuliko kuzifanya za mwilini kama Wayahudi walivyokuwa wanafanya. Kwa asili sheria zote hata zile za torati ni za rohoni kwa maana ya kuwa uvunjaji wake unatathminiwa katika hatua zake za awali wakati wazo na nia inapozaliwa. (Warumi 7:14) “Kwa maana twajua ya kuwa torati asili yake ni ya rohoni; bali mimi ni mtu wa mwilini, nimeuzwa chini ya dhambi.” Kwa kuwa kuithibiti dhambi hasa ya uzinzi katika hatua zake za awali wazo linapoundwa huwa ni jambo gumu kwa sababu ya udhaifu wa mwili wa mwanadamu, Wayahudi walijiwekea utaratibu kuanza kuithibiti katika hatua ya matendo inayoonekana na watu.
Kwa upande wa pili, Wayahudi walizikuza amri zinazoratibu mahusiano ya Mungu na wanadamu kwa kufanya zaidi ya vile ilivyotakiwa. Walithamini Sabato kuliko mwanadamu jambo ambalo Kristo alilikemea. (Marko 2:27) “Akawaambia, Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, si mwanadamu kwa ajili ya sabato.” Wayahudi walizuia uponyaji wa wanadamu siku ya Sabato kinyume na mtazamo wa Mungu. (Luka 13:14) “Basi mkuu wa sinagogi alikasirika kwa sababu Yesu amemponya mtu siku ya sabato, akajibu, akawaambia mkutano, Kuna siku sita zifaazo kufanya kazi, basi njoni mponywe katika siku hizo, wala si katika siku ya sabato.” Lakini Yesu alikemea unafiki huo kwa kuwa alijua ng’ombe wao akitumbukia shimoni siku ya Sabato walikuwa wanamtoa kwa kuhofia hasara ya kiuchumi. (Mathayo 12:11) “Akawaambia, Ni mtu yupi miongoni mwenu mwenye kondoo mmoja, na yule kondoo ametumbukia shimoni siku ya sabato, asiyemshika akamwopoa?”
Wote wazishikao sheria za Mungu kimwili wana kawaida ya kuongeza au kupunguza madai yake. Wayahudi waliongeza madai ya amri ya nne inayowaagiza wanadamu wote kutunza Sabato kwa kukataza shughuli yoyote ya uponyaji kufanyika siku hiyo. (Luka 6:6-7) “Ikawa siku ya sabato nyingine aliingia katika sinagogi akafundisha; na mlikuwamo mtu ambaye mkono wake wa kuume umepooza. Na waandishi na Mafarisayo walikuwa wakimvizia, ili waone kwamba ataponya siku ya sabato; kusudi wapate neno la kumshitakia.”
Miongoni mwa madai ya Wayahudi dhidi ya Yesu ilikuwa ni uvunjaji wa siku ya Sabato uliofanywa na yeye mwenyewe na wanafnzi wake. Walidai Yesu anayejinasibu kama mwasisi au Bwana wa Sabato ndiye kinara wa kuivunja Sabato. (Yohana 5:18-19) “Basi kwa sababu hiyo Wayahudi walizidi kutaka kumwua, kwa kuwa hakuivunja sabato tu, bali pamoja na hayo alimwita Mungu Baba yake, akijifanya sawa na Mungu. Basi Yesu akajibu, akawaambia, Amin, amin, nawaambia, Mwana hawezi kutenda neno mwenyewe ila lile ambalo amwona Baba analitenda; kwa maana yote ayatendayo yeye, ndiyo ayatendayo Mwana vile vile.” (Marko 2:23-24) “Ikawa alipokuwa akipita mashambani siku ya sabato, wanafunzi wake walianza kuendelea njiani wakivunja masuke. Mafarisayo wakamwambia, Tazama, mbona wanafanya lisilokuwa halali siku ya sabato?”
Wayahudi hawa walikuwa wanataka kujionyesha kuwa wanaijua na kuithamini Sabato kuliko yeye anayejitambulisha kwao kama Bwana wa Sabato. Ni kawaida ya watu wa mwilini kujitambulisha kama wenye kuwa na mamlaka kuliko Mungu aliyeitoa sheria na kwamba uchungu wao kwa madai ya sheria unavuka ule uchungu alionao Mungu kwa sheria yake. Watu wenye madai haya katika kipindi cha Yesu waliitwa Mafarisayo na sehemu kubwa ya waliokuwa viongozi wa dini ya Kiyahudi. Walikuwa wanautumainia mwili. Paulo hapo mwanzo kabla hajakutana na Yesu alkuwa katika kundi hili. (Wafilipi 3:4-6) “Walakini mimi ningeweza kuutumainia mwili. Mtu ye yote akijiona kuwa anayo sababu ya kuutumainia mwili, mimi zaidi. Nalitahiriwa siku ya nane, ni mtu wa taifa la Israeli, wa kabila ya Benyamini, Mwebrania wa Waebrania, kwa habari ya kuishika torati, ni Farisayo, kwa habari ya juhudi, mwenye kuliudhi Kanisa, kwa habari ya haki ipatikanayo kwa sheria sikuwa na hatia.”
Leo hii watu hao wa mwilini ambao wangependa madai ya Sabato yasitambue umuhimu wa kutenda mema kwa watu siku hiyo bado wapo. Wanakataza kununua, kuuza, kupika, au kumfanyia jema mhitaji aliye katika hatari ya kupoteza maisha kwa kuwa tu siku hiyo ya uhitaji wake ni siku ya Sabato. Kwao Sabato ni kitu chenye thamani kuliko thamani aliyonayo mwanadamu. Kwa mujibu wa Yesu thamani ya Sabato haiwezi kuizidi thamani ya mwanadamu. (Marko 2:27) “Akawaambia, Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, si mwanadamu kwa ajili ya sabato.” Utunzaji wa Sabato haupaswi ufikie hatua ya kutotambua thamani ya mwanadamu.
Lakini watu wengine wa mwilini ni wale wanaoondoa umuhimu wa madai ya sheria kwa maelezo kuwa hayawahusu tena walio kwenye mchakato wa wokovu. Madai yao kwa namna fulani yanaonekana kama kuungwa mkono na Maandiko hasa nyaraka za Paulo. (Warumi 6:14) “Kwa maana dhambi haitawatawala ninyi, kwa sababu hamwi chini ya sheria, bali chini ya neema.” Kauli hii ya kutokuwa chini ya sheria imetafsiriwa vibaya. Kauli hii haina maana ya kuwa sheria haitakuwa na nafasi kwenye mchakato wa wokovu kama wengine wanavyodai. Mchakato wa wokovu unategemea kuwepo kwa sheria inayoitambulisha dhambi na kudhihirisha mwanadamu asivyoweza kujiokoa. Kinachosemwa hapa ni kuwa ule utaratibu wa kutafuta kuokolewa kwa kushika sheria kwa juhudi za kibinadamu ambao haukutoa suluhisho kwa dhambi umefikia ukomo kwa kifo cha Yesu msalabani aliyeanzisha utaratibu mpya wa kuokolewa kwa neema.
Kwa hiyo wale wanaoendelea kushika sheria kimwili yaani kwa kutumia jitihada zao wenyewe badala ya kutegemea uwezo wa Mungu na kwa kutumia tafsiri zao badala ya tafsiri ya Mungu iliyokusudiwa kwenye sheria husika ndiyo walio chini ya sheria na hawa hawawezi kunufaika na neema ya Mungu maana hawapo chini ya neema. Kinyume cha kuwa chini ya sheria ni kuwa chini ya neema na siyo kutokuwa na sheria. Wale wote walio chini ya neema ni wale waliohama kutoka kutafuta kuokolewa kwa kushika sheria kwa juhudi zao (watu wa mwilini) na kuingia katika kundi la wanaotafuta kuokolewa kwa neema (watu wa rohoni). Walio chini ya sheria ni wale Wayahudi waliojitaabisha kuzisha sheria kwa juhudi na tafsiri zao, waliojaribu kuzipunguza makali kwa kuzipa tafsiri nyepesi kwa lengo la kujipatia unafuu wa kuzishika na na wale waliozipa tafsiri ngumu na kuzitii kimwili badala ya kuzitii kiroho kwa lengo la kujiongezea umaarufu.
Historia ya Ukristo ina kumbukumbu ya watu waliobadilisha amri za Mungu kutoka zilivyokuwa wakati zinatolewa pale mlima Sinai na kuwa vile zinavyosomeka sasa katika makanisa mengi ya Kikristo. Watu hao waliiondoa amri ya pili inayokataza watu kuabudu sanamu na kubadilisha amri ya pili iliyokuwa inaagiza kuitunza Jumamosi kama siku ya ibada iliyowekwa na Mungu na kuhamishia ibada hiyo siku ya Jumapili. Mabadiliko hayo yalipunguza idadi ya amri kutoka kumi na kuwa tisa. Ili kuzifanya ziendelee kusomeka kama zipo kumi ile amri ya kumi iligawanywa vipande viwili na kutimiza idadi ya amri kumi kama ilivyokuwa mwanzo. Huu ulikuwa uasi mkubwa kupata kufanyika chini ya jua na katika malimwengu yote kwa kuwa haionyeshwi mahali popote katika Biblia ambapo Mungu aliridhia mabadiliko hayo makubwa.
Hawa walikuwa watu wa mwilini kama walivyokuwa Wayahudi. Huku wakiwa na nuru kubwa kuliko waliyokuwa nayo Wayahudi kuwa sheria haiokoi bali ipo kwa ajili ya kutusaidia kutambua dhambi walifanya mabadiliko hayo makubwa kwenye amri za Mungu. Hapa lengo lilikuwa kuondokana na kero waipatayo kwa madai ya amri ya pili na amri ya nne. Hawakupenda sheria iwahukumu wanapoabudu sanamu na hawakupenda ionekane wanaungana na Wayahudi kwa kutunza Sabato. Hawana tofauti na yule anayeichoma moto Biblia kwa kuwa inafunua madhaifu yake, au anayeondoa alama za barabarani ili awe huru Kwenda kwa mwendo anaoutaka.
Wangekuwa watu wa rohoni wangetambua kuwa sheria vile ilivyokuwa kabla ya kubadilishwa na vile ilivyo sasa baada ya kufanyiwa mabadiliko haina uwezo wa kumuokoa mwanadamu. (Wagalatia 2:16) “Hali tukijua ya kuwa mwanadamu hahesabiwi haki kwa matendo ya sheria, bali kwa imani ya Kristo Yesu; sisi tulimwamini Kristo Yesu ili tuhesabiwe haki kwa imani ya Kristo, wala si kwa matendo ya sheria; maana kwa matendo ya sheria hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki.” Unahangaikiaje kitu kisichoweza kukusaidia kwa wokovu wako? Katika hali ya kawaida mtu angetarajia wenye uelewa huu wasijaribu kuifanya sheria isomeke tofauti kwa kuwa mabadiliko hayo yasingeongeza chochote katika wokovu wake.
Wangekuwa watu wa rohoni wangetambua kwamba unaposhika kwa uaminifu amri zile zilizobaki baada ya zingine kuondolewa na kubadilishwa unahesabiwa hujashika amri yoyote. (Yakobo 2:10-11) “Maana mtu awaye yote atakayeishika sheria yote, ila akajikwaa katika neno moja, amekosa juu ya yote. Kwa maana yeye aliyesema, Usizini, pia alisema, Usiue. Basi ijapokuwa hukuzini, lakini umeua, umekuwa mvunja sheria.” Kama lengo ni kuondokana na sheria wangeziondoa zote. Lakini kuchagua baadhi zenye kukera hakukuzingatia busara wala mantiki.
Yesu anafafanua kuwa amri ya kwanza hadi ya nne inazungumzia kumpenda Mungu na amri ya tano hadi ya sita inazungumzia kumpenda jirani kama nafasi yako. (Marko 12:28-31). “Na mmojawapo wa waandishi akafika, akawasikia wakisemezana naye, akatambua ya kuwa amewajibu vema, akamwuliza, Katika amri zote ni ipi iliyo ya kwanza? Yesu akamjibu, Ya kwanza ndiyo hii, Sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja; nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote. Na ya pili ndiyo hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi.” Akili ya kawaida itajiuliza, kwa nini sheria zilizobadilishwa na kuondolewa ni zile zinazozungumzia upendo kwa Mungu tu na zinazozungumzia upendo kwa mwanadamu hazikuguswa? Je, aliyekuwa nyuma ya mabadiliko haya alikuwa adui mkuu wa Mungu na hivyo alikuwa anakereka na kitendo cha Mungu kupewa heshima?
Je, waliofanya mabadiliko haya hawakujua katika Agano Jipya Mungu anakwenda kuandika sheria alizoziandika kwenye mbao mbili za mawe mioyoni mwa wale atakaofanya nao agano la msalaba? Je, sheria hizo zinazoandikwa mioyoni zitakuwa na hayo mabadiliko yaliyofanywa na wanadamu au zitakuwa sawa na zile Musa alizopokea kutoka Sinai? (Waebrania 10:16-17) “Hili ni agano nitakaloagana nao baada ya siku zile, anena Bwana, Nitatia sheria zangu mioyoni mwao, Na katika nia zao nitaziandika; ndipo anenapo, Dhambi zao na uasi wao sitaukumbuka tena kabisa.” Kwa vyovyote vile mabadiliko hayo ya sheria yaliyofanywa na wanadamu yatakuwa na athari kubwa kwa wokovu wa wanadamu.
Ni vigumu mtu kutambua kuwa anafanya dhambi ya kuvunja sabato wakati amri aliyofundishwa ilisema shika kitakatifu siku ya Bwana bila kufafanua huko kushika kunafanyikaje na hiyo siku ya Bwana ni ipi? Uwezekano ni kuwa hatasikia hatia yeyote ya kuvunja sabato kwa kuwa amri ambayo ingemtambulisha kuwa anafanya dhambi ilibadilishwa. Huyu anaweza kupokea maonyo kwa uvunjifu wa sheria zingine na kufanikiwa kwa msaada wa Mungu kuziishi kama zinavyotaka lakini akaendelea kuwa mvunjaji wa amri ya nne bila kusikia hatia moyoni. Hali kadhalika yule ambaye hakufundishwa kuwa kuabudu sanamu ni kinyume na sheria za Mungu ana uwezekano wa kuendelea kuivunja amri hiyo bila kusikia hatia.
Sheria ya Mungu haipo tu kwa ajili ya kuitambulisha dhambi, lakini ipo pia kwa ajili ya kuwatambulisha wafuasi wa kweli wa Mungu. Wafuasi wa kweli wa Mungu watajitambulisha kwa kumwamini Yesu na kutii sheria zake kwa neema itokayo kwake mwenyewe. Wanaompenda Yesu wanazipenda pia sheria zake na kuzishika. (Yohana 14:15) “Mkinipenda, mtazishika amri zangu.” Kule kusema unampenda Yesu na huku huzithamini na kuzishika amri zake ni unafiki uliopitiliza. (Luka 6:46) “Na kwa nini mnaniita, Bwana, Bwana, walakini hamyatendi nisemayo?” (Yohana 15:14) “Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo.” Kuna njia moja tu ya kuwatambua walio rafiki za Yesu. Wanayapokea maagizo yake na kuyatii bila kuyafanyia masahihisho au maboresho.
Kundi hili la wale wanaotaka kumfurahisha Yesu kwa kila anachokiagiza ni vinara wa kufundisha umuhimu wa kubaki na zile amri za Mungu kama zilivyotolewa na yeye mwenyewe hapo mwanzo. (Mathayo 5:19) “Basi mtu ye yote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni.” Licha ya kupewa majina mabaya kwamba kwa kufanya hivyo wanadhihirisha wapo chini ya sheria na chini ya torati na kuwa wanaziinua hizo sheria wakiamini zina uwezo wa kumpa mtu wokovu, bado kundi hilo halijatetereka kwa sababu madai hayo yote hayana ukweli.
Uadui unaolekezwa kwa kundi hili hautoki kwa wanadamu bali unatoka kwa yule aliyewashawishi wanadamu kufanya mabadiliko kwenye sheria ya Mungu isiyobadilika. “Ufunuo wa Yohana 12:17) “Joka akamkasirikia yule mwanamke, akaenda zake afanye vita juu ya wazao wake waliosalia, wazishikao amri za Mungu, na kuwa na ushuhuda wa Yesu; naye akasimama juu ya mchanga wa bahari.” Kwa nini wazishikao amri za Mungu wanaandamwa na Shetani na wale wasiozishika amri za Mungu wakiwa hawaandamwi? Ni kwa sababu mabadiliko yale ya sheria yalisimamiwa na kuchochewa na Shetani. Yeye hakutaka Mungu aabudiwe. (2 Wathesalonike 2:3-4) “Mtu awaye yote asiwadanganye kwa njia yo yote; maana haiji, usipokuja kwanza ule ukengeufu; akafunuliwa yule mtu wa kuasi, mwana wa uharibifu; yule mpingamizi, ajiinuaye nafsi yake juu ya kila kiitwacho Mungu ama kuabudiwa; hata yeye mwenyewe kuketi katika hekalu la Mungu, akijionyesha nafsi yake kana kwamba yeye ndiye Mungu.”
Shetani anapenda kuabudiwa. Alitamani kuabudiwa hata na Yesu huku akijua yeye mwenyewe aliumbwa na Yesu. (Yohana 1:3) “Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika.” Tamaa yake ya kutaka kuabudiwa ni ya kiwango cha juu nayo ilianzia mbinguni. (Isaya 14:13-14) “Nawe ulisema moyoni mwako, Nitapanda mpaka mbinguni, Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu; Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano, Katika pande za mwisho za kaskazini. Nitapaa kupita vimo vya mawingu, Nitafanana na yeye Aliye juu.” Hata Yesu alipokuja duniani kumyang’anya mamlaka alifanya jaribio jingine la kutaka kuabudiwa. (Mathayo 4:8-9) “Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mlima mrefu mno, akamwonyesha milki zote za ulimwengu, na fahari yake, akamwambia, Haya yote nitakupa, ukianguka kunisujudia.” Baada ya kushindwa jaribio la kuabudiwa na Yesu amefanikiwa kuabudiwa na wanadamu kwa kuanzisha utaratibu wa ibada ulio tofauti na ule ulioelekezwa na Mungu ili ibada zote zinazofanyika badala ya kumwelekea Mungu zimwelekee yeye.
Yesu anailalamikia hali hiyo kwa maumivu makubwa. (Marko 7:7-8) “Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu, Ninyi mwaiacha amri ya Mungu, na kuyashika mapokeo ya wanadamu.” Wakristo walipoacha utaratibu wa kuabudu siku ya Sabato uliowekwa na Mungu na kuhamishia siku ya kwanza ya juma walifanikisha tamanio la Shetani la siku nyingi la kutaka kuabudiwa. Sasa heshima iliyokuwa inaelekezwa kwa Mungu inaelekezwa kwake. Ibada ile inayofanyika nje ya utaratibu wa Mungu ni ibada ya bure yaani isiyo na faida kwa anayeabudu. Kwa kuwa aliye tayari kuipokea ibada kama hiyo ni Shetani na si Mungu kama waabuduo wanavyojifariji.
Taratibu za ibada zilizovurugwa ili kumkasirisha Mungu na kumtengenezea Shetani mazingira ya kuzipokea ni pamoja na kuwa na masanamu kwenye nyumba za ibada. Mungu alizikataa hizo sanamu. (Kutoka 20:4-6) “Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu.” Zinapotumika hizo sanamu kwenye ibada, Shetani ndiye hupokea heshima zote zinazoelekezwa kwa sanamu hizo.
Taratibu nyingine ya ibada iliyovurugwa inahusu kukosekana kicho na utulivu katika nyumba za ibada. Mungu anasisitiza haja ya kuwepo kwa utulivu na amani katika nyumba za ibada. (1 Wakorintho 14:33) “Kwa maana Mungu si Mungu wa machafuko, bali wa amani; vile vile kama ilivyo katika makanisa yote ya watakatifu.” Utaratibu huu umekiukwa na baadhi ya Wakristo kwa kisingizio cha kutoa mapepo na kunena kwa lugha na kusababisha vurugu na kelele kwenye nyumba za ibada, kiasi cha kuwafanya wanaoabudu waonekane kama wana wazimu na kumvunjia Mungu heshima. (1 Wakorintho 14:23) “Haya! Ikiwa kanisa lote limekusanyika pamoja, na wote wanene kwa lugha, kisha ikawa wameingia watu wajinga au wasioamini, je! Hawatasema ya kwamba mna wazimu?” Kama kuna anayenufaika sana na hali hii ni Shetani aliye mwasisi wa vurugu hizo.
Unenaji kwa lugha una utaratibu wake. (1 Wakorintho 14:27) “Kama mtu akinena kwa lugha, wanene wawili au watatu, si zaidi, tena zamu kwa zamu, na mmoja na afasiri.” Kama ushauri huu ungezingatiwa vurugu tunazozishuhudia leo makanisani zisingekuwepo. (1 Wakorintho 14:40) “Lakini mambo yote na yatendeke kwa uzuri na kwa utaratibu.” Vurugu hizi zimeondoa utukufu uliostahili kuwepo kwenye nyumba za ibada. Wanadamu wamemvunjia Mungu heshima. Hakuna ulazima wa kuwa na lugha maalum ya kuongea na Mungu. Mungu ana uwezo wa kusikia mahitaji yoyote yanayotolewa kwa lugha yoyote. Hakuna sababu ya kujisumbua kuongea kwa lugha usiyojua tafsiri yake kwa madai kwamba ndiyo lugha pekee Mungu anayopokelea maombi ya wanadamu. (Wafilipi 4:6-7) “Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.”
Kilicho muhimu ni haja zako zijulikane na Mungu. Kama Mungu ana uwezo wa kujua haja za bubu asiyejua kusema atashindwaje kujua haja zilizotamkwa kwa lugha ya wanadamu? (Mathayo 12:22) “Wakati ule akaletewa mtu mwenye pepo, kipofu, naye ni bubu; akamponya, hata yule bubu akanena na kuona.” Mungu anataka tutoe hoja zenye nguvu tunapowasilisha maombi yetu kwake. (Isaya 41:21) “Haya, leteni maneno yenu, asema Bwana; toeni hoja zenu zenye nguvu, asema mfalme wa Yakobo.” Utafiti umeonyesha wanafunzi wengi hushindwa mitihani kwa kukosa kutoa hoja zenye nguvu kwa kuwa lugha ya kiingereza wanayotumia kujibia mitihani si rafiki kwao. Je ni watu wangapi wameshindwa kupeleka haja zao na hoja zao zenye nguvu kwa Mungu kutokana na kutumia lugha isiyowapa uhuru wa kujieleza? Je, kama hoja na haja zao zimeshindwa kumfikia Mungu kwa sababu ya changamoto ya lugha ya mawasiliano ni nani amefaidika kati ya Shetani na Mungu?
Mabadiliko ya sheria za Mungu yaliyofanywa na wanadamu bila ridhaa yake yalilenga kukwamisha mchakato wa wokovu. Hata hivyo Mungu amefanikiwa kubaki na kundi linalozidi kuongezeka la watakatifu wazishikao amri za Mungu. (Ufunuo wa Yohana 14:12) “Hapa ndipo penye subira ya watakatifu, hao wazishikao amri za Mungu, na imani ya Yesu.” Sifa za watakatifu wa Bwana ni mbili. Kwanza wanazishika amri za Mungu na kuzifundisha. Sifa ya pili ni kuwa wanamtegemea Yesu katika kuzishika hizo amri hizo na wanaamini juu ya mpango wa wokovu. Wanaamini kuwa wokovu ni mpango wa Mungu wa kumsaidia mwanadamu kuufikia uzima wa milele bila kutumia njia zake wala jitihada zake mwenyewe kwa kuwa jitihada na njia hizo zisingeweza kumsaidia kuokolewa. Hawashiki amri za Mungu ili wahesabiwe haki. Wanategemea neema ya Mungu ili kuhesabiwa haki.
Kundi hili la watakatifu wanatambua pia kuwa hii ni neema ibadilishayo, na kwamba mojawapo ya matokeo ya neema hii ni kuleta badiliko la tabia ili maisha yaakisisi maagizo yaliyo kwenye sheria za Mungu. (Tito 2:11-14) “Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa; tukilitazamia tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa Kristo Yesu, Mungu mkuu na Mwokozi wetu; ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe na maasi yote, na kujisafishia watu wawe milki yake mwenyewe, wale walio na juhudi katika matendo mema.”
Kuwa na juhudi katika kutenda mema baada ya kuokolewa kwa neema ni jambo lililo sahihi ambalo Mungu analitarajia. Tofauti ya juhudi hii na ile ya kifarisayo aliyokuwa nayo Paulo (Wafilipi 3:6) ni kwamba juhudi hii ya baada ya kuokolewa inawezeshwa na Roho Mtakatifu (ya rohoni) na haitokani na jitihada za kibinadamu (ya mwilini). Kwa kuwa matendo haya hayatokani na juhudi za kibinadamu yanaweza tu kupimwa na Mungu mwenyewe. Wakati mchakato wa mabadiliko ya tabia ukiendelea mtu wa rohoni hawezi kudai kuwa amefikia ukamilifu. (Wafilipi 3:12-14) “Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake nimeshikwa na Kristo Yesu. Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele; nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu.”
Wakati watakatifu hawa wakisita kujiona wamekamilika Mungu kwa upande wake hasiti kuwaita watakatifu. (Wakolosai 3:12) “Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi.” Salamu hii inaashiria kuwepo kwa mambo yanayoendelea kukamilishwa kwa watakatifu hawa. Mungu ana kawaida ya kuwatambua walio kwenye mchakato wa kutakaswa kama waliokamilika ndiyo sababu anawaita watakatifu. Hata hivyo watu wa rohoni hawana kawaida ya kujitutumua kama ni watu wema au wakamilifu. (Luka 18:13-14) “Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi. Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.”
Ni mimi mchambuzi wako
Mchungaji Stephen Julius Letta
Ukihitaji ufafanuzi niandikie au nipigie:
+255764600362 – Mlandizi – Tanzania