Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

WAGALATIA

MASWALI YA KUJADILI: WAGALATIA 1:1-24

  1. Mitume waliotumwa na Mungu wanatofautianaje na mitume waliotumwa na wanadamu? Kwa nini ilikuwa muhimu kwa Paulo kujitambulisha kama mtume aliyetumwa na Mungu? Kwa kuwa Baba alimfufua Yesu kutoka kwa wafu, Je hiyo inadhihirisha kuwa Yesu alikuwa mdogo kwa Baba? (Yohana 10:17-18). Kwa nini Paulo anawatakia neema wasomaji wake? Neema ina nafasi gani katika kuufanya ujumbe ueleweke na kupokelewa? (Matendo 17:11; 1 Wathesalonike 2:1.
  2. Yesu alitumwa na nani kutoa nafsi yake kwa ajili ya dhambi zetu? Kwa nini Baba hakuja yeye mwenyewe kutoa nafsi kwa ajili ya dhambi zetu badala yake akamtuma Yesu? (Yohana 3:16; Wafilipi 2:5-8). Kujitoa kwa Yesu kulituokoaje na dunia hii mbovu iliyopo sasa? Kama injili ni habari njema kwa nini wanadamu wana kawaida ya kusukumilia mbali injili na kugeukia injili nyingine ya imani kwa matendo?
  3. Kwa nini Mungu alimchagua Sauli mtu aliyeliudhi kanisa la Kristo na kulihubiri awe mtume kwa kanisa hilo? Kwa nini dini ya Kiyahudi ilikuwa inaona fahari kufanya vitendo vya kikatili kwa watu wanaotofautiana nao misimamo ya kidini? (Wafilipi 3:4-9) Je watu wenye tabia hizo leo wapo? (1 Wakorintho 3:1-3). Ikiwa watu huchaguliwa kuwa watumishi wa Mungu wakiwa matumboni mwa mama zao inawezekana kuikataa kazi hiyo baada ya kuzaliwa? Kwa nini kama Paulo alichaguliwa kuifanya kazi ya Mungu tangu akiwa tumboni alianza kwa kuliudhi na kulitesa kanisa? (2 Wakorintho 9:7; Filemoni 2:14).
  4. Kungetokea shida gani kama Paulo angeenda kujitambulisha kwa mitume waliokuwa kabla yake huko Yerusalemu? Miaka 3 aliyokaa Arabuni ilikuwa ya kujifunza nini? Makanisa ya Uyahudi yaliyokuwa katika Kristo ni makanisa gani hayo? Kwa nini Paulo hakujulikana na makanisa hayo?

MASWALI YA KUJADILI: WAGALATIA 2:1-21

  1. Kwa nini Mungu alimtuma Paulo kuiburi injili kwa mataifa kwanza kabla hajamfunulia kuihubiri kwa walio Yerusalemu? Kwa nini walio Yerusalemu waliofunuliwa mwisho kuhubiriwa injili wanaitwa "walio wenye sifa?" Je unadhani injili inapokelewa kwa shukrani na wale wanaojihisi ni wenye sifa au wanaostahili?
  2. Je, unaweza kuihubirii injili kama hujafunuliwa? Je kitendo cha Tito asiye Myahudi kuwa mshirika katika utumishi wa kuhubiri injili akiwa hajatahiriwa lilikuwa halali? (Warumi 2:26-27; Warumi 15:8; 1 Wakorintho 7:18; Wagalatia 5:6). Je kweli ya injili inakuwa hatarini kiasi gani kama wanaoihubiri wakijitia chini ya wale wanaoshikilia mapokeo ya kidini?
  3. Kwa nini kulikuwa na mgawanyiko katika kuhubiri wengine wakielekezwa kuwaendea wamataifa wasiotahiriwa na wengine wakielekezwa kuwaendea watu wa tohara na mapokeo ya kidini? Je injili za watu hawa huwa zinafanana? Kwa nini kuwakumbuka maskini katika kuhubiri injili ni kwa muhimu? (Luka 6:36; Luka 7:11-13; 1 Yohana 3:17). Je ni watu gani walio hodari kufanya unafiki baina ya watu wa mataifa na washika dini?
  4. Kwa nini washika dini huwabagua na kutamani kujitenga na wamataifa hasa wanapokuwa mbele ya waumini wenzao? (Luka 18:10-14). Ni kwa namna gani Kefa alikuwa anafuata desturi za Mataifa na si za Wayahudì? Kwa nini Wayahudi walihesabiwa kuwa ni watu wasiokosa kama wa Mataifa? Tunajuaje kuwa mwanadamu hahesabiwi haki kwa matendo ya sheria?
  5. Kama mwanadamu hahesabiwi haki kwa matendo ya sheria kwa nini Mungu aliagiza wanadamu washike sheria? (Warumi 3:19-20; Wagalatia 3:24). Kama tunahesabiwa haki kwa imani ya Kristo, Je wale walioishi kabla ya Kristo walihesabiwaje haki? Kwa nini anayetafuta kuhesabiwa haki katika Kristo anaonekana kuwa mwenye dhambi? (Wafilipi 3:3). Mtu anaifiaje sheria kwa njia ya sheria ili amwishie Mungu? (Warumi 7:1-6; 2 Wakorintho 5:14)

MASWALI YA KUJADILI: WAGALATIA 3:1-29

  1. Kuwaambia watu unaowalea kiroho hawana akili ni halali kwa mtumishi wa Mungu? Paulo kwa kuwaita watu wa Galatia wamelogwa alikuwa anamaanisha au anawadhihaki? Je watu wa Mungu wanalogeka? (Hesabu 23:23). Je, ni njia ipi iliyo sahihi ya kupokea Roho Mtakatifu? Je, ni kwa njia ya matendo ya sheria au ni kwa njia ya kusikia kunakotokana na imani? Je, mtu aliyeanza katika Roho anaweza kukamilishwa katika mwili? Kwa nini ndiyo au kwa nini hapana?
  2. Kwa nini watu wa imani wanatambulika kama wana wa Ibrahimu? Je wana wa Ibrahimu wa asili (wa kinasaba) wasipokuwa na imani hawatambuliki kama wana wake? Ni andiko gani lililoona tangu zamani kwamba Mungu atawahesabia haki Mataifa kwa njia ya imani? Kwa nini tamko la Mungu kwa Ibrahimu kwamba kupitia kwake mataifa yote yatabarikiwa linachukuliwa kama habari njema? Kwa nini wanaotafuta kuhesabiwa haki kwa matendo wanachukuliwa kuwa wapo chini ya laana? Kwa nini kuishi kwa imani kunamfanya mtu kuwa mwenye haki?
  3. Kwa nini inasemwa torati haikuja kwa imani? Na kama haikuja kwa imani kwa nini ililetwa? Kristo alitukomboaje kwenye laana ya torati? Je, Yesu aliangikwa juu ya mti au aliangikwa juu ya msalaba? Baraka ya Ibrahimu iliwafikiaje mataifa? Kwa nini agano ambalo Mungu aliagana na Ibrahimu linaitwa agano la mwanadamu? Agano hilo lilithibitikaje? Je ni kweli kuwa agano hilo halikubatilishwa wala kuongezwa neno? Kwa nini ahadi zilizonenwa kwa Ibrahimu zilinenwa kwa mzao wake na si kwa wazao wake?
  4. Ni kipi kipo juu ya kingine kati ya Ahadi na Torati iliyotokea miaka mia nne na thelathini baadaye? Je urithi hupatikana kwa njia ya sheria (torati) au hupatikana kwa njia ya ahadi? Kwa nini inasemwa torati iliingizwa kwa sababu ya makosa? Je torati iliamriwa kuwepo na nani? Kwa nini torati haipatani na ahadi za Mungu? Kwa nini sheria haiwezi kuhuisha? Je sheria ingeweza kuhuisha haki ingewezekana kupatikana kwa njia ya sheria? Kwa nini?
  5. Hayo yote ambayo andiko limeyafunga chini ya nguvu ya dhambi kusudi waaminio wapewe ile ahadi kwa imani ya Yesu Kristo ni nini? Kwa nini ilikuwa ni lazima tuwekwe au tufungwe chini ya sheria mpaka ije ile imani itakayofunuliwa? Hiyo imani itakayofunuliwa ni ipi? Je kufanyika kwetu wana kuliwezekana kwa njia ya imani au kwa njia ya matendo? Kwa nini waliobatizwa katika Kristo wanatambulika kama waliomvaa Kristo? Vazi hapa lina umuhimu gani?
  6. Kristo amewezaje kuondoa tofauti na tabaka baina ya wanaume na wanawake, baina ya Wayahudi na Wayunani na baina ya mtumwa na aliye huru? Je kabla ya hapo makundi hayo yalikuwa yanahasimiana? Je sababu ya mgogoro wao hasa ilikuwa nini? Kwa nini kila aliye wa Kristo ni mzao wa Ibrahimu na mrithi sawasawa na ahadi

MASWALI YA KUJADILI: WAGALATIA 4:1-31

  1. Kwa nini mrithi wakati wote awapo mtoto, hana tofauti na mtumwa? Mrithi anayetajwa katika aya ya kwanza ni nani? Alikuwa katika hali ya utoto wakati gani? Utimilifu wa wakati unamaanisha nini? Je hii inamaanisha kulikuwa na ratiba ya matukio inayoonyesha tukio gani litatokea wakati gani? Je, Yesu alikuja duniani kulingana na ratiba iliyowekwa? Kungekuwa na mtatiziko gani kama Yesu angezaliwa nje ya ratiba ya matukio?
  2. Mwanae ambaye Mungu alimtuma ili awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria ni nani? Je anaitwa mwanae kwa sababu alimzaa? Je mtu aweza kuwa mwanao hata kama hujamzaa? Kama Yesu ni mwana wa Mungu kwa nini anatambulishwa kama amezaliwa na mwanamke? Je Mungu aweza kuzaa na mwanamke? Kuzaliwa chini ya sheria maana yake nini? Kwa nini Yesu anatambulishwa kama amezaliwa chini ya sheria?
  3. Kulikuwa na umuhimu gani kwa Yesu kuzaliwa chini ya sheria? Kuwakomboa walio chini ya sheria kulihitaji nini? Kuzaliwa kwa Yesu aliye mwana wa Mungu chini ya sheria kulitupatiaje hali ya kuwa wana? Kwa nini Roho wa mwanae aliye ndani yetu analia Baba? Kwa nini anaitwa Roho wa Mwanawe na si Roho wa Mungu? Kwa nini Mungu alituondolea hadhi ya kuwa watumwa na kutufanya wana?
  4. Je kuwatumikia wale ambao kwa asili si miungu kunatokana na kutokumjua Mungu? Mungu anahakikishaje watu hawatumbukii katika kosa hilo? Je, kuna mtu atakayehukumiwa kwa kutokumjua Mungu? Mafundisho ya kwanza na yenye upungufu ambayo watu walitaka kuyatumikia tena ni yapi? Kwa nini mafundisho hayo yanaitwa manyonge na yenye upungufu?
  5. Kushika siku, miezi, na nyakati na miaka kulikuwa na tatizo gani kwa wale waliopokea hali ya kuwa wana? Kwa nini Paulo anatamani macho ya waumini wake yangeng'olewe ili apewe yeye? Je kusema kweli kunaweza kumtengenezea mtu maadui? Hatua ya ukuaji ambayo Kristo anaendelea kuumbika ndani ya muumini huitwaje? Je kuna wakati katika makuzi yake ya kiroho muumini hutamani kuwa chini ya sheria?
  6. Kwa nini wana wawili wa Ibrahimu wanafananishwa na maagano mawili? Kwa nini Ishmaili anafananishwa na agano lililozaliwa kwa mwili na Isaka anafananishwa na agano lililozaliwa kwa agano? Kwa nini watoto wake aliyeachwa pekee ni wengi kuliko wa huyo aliye na mume? Je kuna wakati katika makuzi yake ya kiroho muumini hutamani kuwa chini ya sheria? Kwa nini wana wawili wa Ibrahimu wanafananishwa na maagano mawili?
  7. Kwa nini Ishmaili anafananishwa na agano lililozaliwa kwa mwili na Isaka anafananishwa na agano lililozaliwa kwa ahadi? Kwa nini watoto wake aliyeachwa pekee ni wengi kuliko wa huyo aliye na mume? Je, mtoto wa ahadi katika kusanyiko la waumini utamtambuaje? Je inatokeaje watoto wasiozaliwa kwa ahadi wawaudhi wale waliozaliwa kwa ahadi? Je, kwa mujibu wa Maandiko wale watoto waliozaliwa kwa mwili kuna wakati watakuja kuliacha kanisa au watafukuzwa?

MASWALI YA KUJADILI: WAGALATIA 5:1-26

  1. Wagalatia wakiwawakilisha wanadamu wote wanahimizwa kusimama ili wasinaswe tena chini ya kongwa la utumwa. Ilitokeaje hata wakanaswa katika kongwa la utumwa? Kwa nini kutahiriwa kunawafanya watu wasifaidiwe na neno? Kwa nini kutahiriwa kunakuwa hakuna umuhimu tena? (Matendo 15:1; Matendo 7:51; Warumi 2:26). Kwa nini inampasa kila atahiriwaye kuitimiza torati yote? Ni nini huwa kinawapunguzia mwendo Wakristo katika kukua kwao?(Marko 4:18-19).
  2. Kwa nini kutaka kuhesabiwa haki kwa sheria kunamtenga mtu na Kristo? Kwa nini kutaka kuhesabiwa haki kwa sheria kunamfanya mtu kuanguka kutoka katika hali ya neema? Je tumeitwa katika Ukristo ili tupate uhuru? Je uhuru huo ni upi ni ule wa kutotii sheria au wa kutohesabiwa haki kwa sheria? Je, kumpenda jirani yako kama nafsi yako kunatimilishaje torati yote? (Mathayo 22:36-42). Kwa nini kuenenda katika Roho kunazuia tamaa za mwili? Kwa nini mwanadamu mwenye asili ya dhambi hawezi kufanya anayotaka? (Warumi 7:15-24).
  3. Kwa nini wanaoongozwa na Roho hawapo chini ya sheria? Kuwa chini ya sheria maana yake ni nini? Je, kutii Amri 10 za Mungu ni kuwa chini ya sheria? Kwa nini watendao matendo ya mwili hawatarithi ufalme wa Mungu? Kwa nini matendo hayo yanaitwa matendo ya mwili? Je, mwili ndiyo unaozalisha matendo hayo? Kwa nini matendo yanayozalishwa na Roho yanaitwa tunda na si matunda? Je, kama matendo yote ni tunda kuna uwezekano wa kua na tabia moja ya Roho na usiwe na tabia nyingine ya Roho yule yule? Ni nini tofauti baina ya tunda la Roho na karama za Roho?
  4. Kwa nini hakuna sheria kwa mtu aonyeshapo tunda la Roho? Je, hiyo inamaanisha kuwa sheria hazina umuhimu tena? Kuusulubisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake hufanywa na mwongofu mwenyewe au na Roho aliye ndani yake? Je, mawazo mabaya yanaweza kusulubishwa? Kwa nini kitendo cha kuondokana na mawazo mabaya kinaitwa kusulubisha? Je anayeishi katika Roho anaweza kubadilika na kuanza kuishi katika mwili? Mtu afanyeje ili kuzuia jambo kama hilo lisitokee?

MASWALI YA KUJADILI: WAGALATIA 6:1-18

  1. Kughafilika ni nini? Je kughafilika ni sawa na kupitiwa? Je, muumini wa Kristo aweza kughafilika? Kwa nini inashauriwa mtu aliyeghafirika arejeshwe na mtu aliye wa Roho? Mtu aliye wa Roho ni mtu wa namna gani? Unamrejezaje upya mtu aliyeghafilika? Katika kumrejeza mtu aliyeghafilika kuna uwezekano wa kujaribiwa? Unaweza kujaribiwa kufanya nini?
  2. Ni sheria gani ya Kristo ambayo kwa kuchukuliana mizigo tunakuwa tunaitimiza? Kuchukuliana mizigo maana yake ni nini? Je, ni kutambua mapungufu aliyonayo mwenzako na kuyavumilia? (2 Wakorintho 11:1,19-20). Je, ni rahisi kwa anayejiona bora kuchukuliana na walio dhaifu? Kwa nini anayejiona kuwa kitu anajidanganya mwenyewe? (1 Wakorintho 10:12).
  3. Je, ni salama kujipima ulivyo kiroho na watu wengine? Kwa nini katika kujipima kiroho mara nyingi watu hujilinganisha na walio dhaifu kwao badala ya kujipima kwa Yesu? Je kujisifu ndani ya nafsi bila kuwaambia wengine ni jambo linalowezekana? Kwa nini jambo hilo huwa haliwavutii watu wengi?
  4. Kwa nini Maandiko yanasema kila mtu atalichukua furushi lake mwenyewe wakati mafungu mengine yakisema Yesu ametubebea mizigo? (Mathayo 11:28; Isaya 53:4). Je kila mtu akilichukua furushi lake kuna uwezekano wa kupona? (1 Timotheo 5:24). Sisi tunamshirikishaje mkufunzi wetu katika mema yote? Msemo wa "kila apandacho mtu ndicho atakachovuna" una maana gani? Je kutenda mema kunalipa? (1 Samweli 25:21; Mathayo 5:16; Mathayo 6:11).
  5. Kwa nini kuwatendea mema jamaa ya waaminio kunasisitizwa sana? (1 Timotheo 5:8). Kwa nini wasiotaka kuudhiwa na msalaba wa Kristo wanawashurutisha watu kutahiriwa? Kutahiriwa kunawafanyaje waonekane wazuri? Waliotahiriwa wanapataje kuona fahari miilini mwao wanapoona watu waetahiriwa kutokana na shurti zao? Kuna uthibitisho gani kuwa waliotahiriwa nao pia hawaishiki sheria? Msalaba wa Yesu Kristo unamletea fahari gani muumini? Msalaba unamfanyaje mtu asulubishwe kwa ulimwengu?