Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

ELDAD MULWAMBO

Mulwambo , Eldad Jeremia (1948–2013)

Mhudumu, mwalimu, mwinjilisti, mpanda makanisa, na msimamizi wa kazi nchini Tanzania.

Maisha ya siku za awali"

Eldad Jeremia Mulwambo alizaliwa mwaka 1948 katika Kisiwa cha Ukerewe, Mkoa wa Mwanza, nchini Tanzania. Wazazi wake wote wawili, Jeremia Mulwambo Sakara na Perusi, walikuwa wenyeji wa Ukerewe na Waadventista wa Sabato waliojitoa sana kwa kazi. Waliongokea kwenye Uadventista baada ya mafundisho ya Waadventista kuletwa kijijini kwao na wamishionari wenyeji kutoka Majita. Jeremia Mulwambo alikuwa na watoto tisa: wavulana watatu na wasichana sita ambapo Eldadi Mulwambo alikuwa wa pili katika kuzaliwa kwenye familia yao. Baba ya Eldadi aliishi maisha ya kielelezo yaliyojenga msingi thabiti katika kumwogopa Mungu kwa wana familia wengine.

Elimu:

Eldad Mulwambo alipata elimu yake ya msingi katika Shule ya Kati ya Tangaza. Baada ya hapo, alienda kwa elimu ya sekondari nchini Uganda. Ingawa shule hizi hazikuwa za Waadventista, imani ya Eldad Mulwambo iliimarika licha ya changamoto kadhaa alizokumbana nazo katika shule hizo. Kutoka hapo, Eldad alihudhuria Chuo cha Waadventista cha Ikizu mnamo 1975, ambapo alipata mafunzo ya uchungaji. Mchungaji Mulwambo alipambania elimu na maendeleo yake. Kutokana na shauku yake ya kuwa na elimu ya juu, alihudhuria Chuo cha Memorial Spicer kwa shahada yake ya kwanza ya theolojia. Mara tu baada ya kuhitimu mwaka wa 1984, alijiunga na shahada ya uzamili katika historia katika Chuo Kikuu cha Poona na baadaye shahada ya uzamili katika sosholojia katika Taasisi za Kijamii za Nehru nchini India.
Mafanikio yake ya kielimu yaliwatia moyo wahudumu vijana wa siku zake, kama vile Mchungaji Herry Muhando na Mchungaji Jacob Gagi, kwenda kwa masomo zaidi. Ikumbukwe kwamba wakati huo, kanisa barani Afrika lilikuwa na Waafrika wachache wenye elimu ya uzamili.

Uchungaji wa Mapema:

Mchungaji Mulwambo alijiunga na huduma ya kichungaji katika Kanisa la Waadventista mwaka 1972 akiwa mwinjilisti wa vitabu wilayani Ukerewe. Alifurahia kufanya kazi hiyo hadi alipoitwa kuwa mchungaji wa mtaa wa Kisoria wilayani Bunda mkoani Mara. Wakati huo, Mchungaji Mulwambo alijishughulisha na uinjilisti na upandaji wa makanisa. Alikuwa mchungaji kijana mwenye maono na shauku ya huduma. Alijitolea kumtumikia Mungu na kanisa lake. Baada ya kazi kubwa aliyoifanya Ukerewe na Mkoa wa Mara, Mchungaji Mulwambo alihamishiwa Shule ya Sekondari ya Parane na kuwa Mlezi wa kiroho wa shule (Chaplain). Alihudumu kama Chaplain kuanzia 1976 hadi 1979. Akielezea huduma ya Mchungaji Mulwambo huko Parane, Mchungaji Jacob Gagi, ambaye pia alifundisha katika shule hiyo, anasema kwamba Mulwambo alikuwa mchungaji mwenye bidii. Alijichanganya na wanafunzi katika shughuli mbalimbali, kama vile kulima na kutafuta kuni msituni na kuzikata. Wakati wa uchungaji wake katika Shule ya Sekondari ya Parane, roho yake ya uinjilisti iliwashwa. Katika kipindi cha miaka minne, aliendesha mikutano miwili ya hadhara ya uinjilisti (effort). Tangu wakati huo, Parane haijaacha kufanya kampeni za uinjilisti. Baada ya elimu yake nchini India, Mchungaji Mulwambo alihudumu tena huko Parane kuanzia 1986 hadi Desemba 1988.

Ndoa na Familia:

Mchungaji Mulwambo alimuoa Lucy Nyabweke Murusuri mnamo 1976. Walienda pamoja kama timu katika huduma kutokea Kisoria hadi Parane, na kutoka India kurudi Parane kwa miaka miwili. Baada ya hapo walihamia sehemu mbalimbali zikiwemo Arusha, Morogoro, Kigoma, Dar es Salaam na hatimaye kurudi Morogoro kwenye makazi yake ya kustaafia ambako umauti ulimkuta. Mchungaji Edad Jeremia Mulwambo alizikwa hapo Morogoro akisubiri ahadi ya ujio wa pili wa Bwana.

Bibi Mulwambo alifanya kazi katika nyadhifa mbalimbali katika Kanisa la Waadventista Wasabato. Akiwa Parane, alifanya kazi kama mwalimu. Katika Seminari na Chuo cha Waadventista Wasabato Tanzania, alifanya kazi kama mwalimu na meneja wa mgahawa. Katika Fildi ya Tanzania Mashariki ya wakati huo, alikuwa katibu muhtasi wa ofisi ya makao makuu ya Fildi. Pia alikuwa mkurugenzi wa Huduma za Wanawake na Watoto katika Fildi ya West Tanzania. Alikuwa mchapakazi, mshauri wa Mchungaji Mulwambo, mama mwenye upendo kwa watoto watano, mwalimu, na mtunzaji katika shamba la mizabibu la Mungu. Mchango wake kwa Kanisa la Waadventista hautasahaulika kamwe. Bibi Mulwambo alilala katika Bwana Aprili 23, 2017. Alizikwa katika makaburi ya Mlima Kora kwenye manispaa ya Morogoro.

Mchungaji Mulwambo na mkewe Lucy walijaliwa watoto watano, wavulana wawili na wasichana watatu: Mark, Mugara, Maradufu, Maria, na Mwasi. Watoto wa Mchungaji Mulwambo wanamkumbuka baba yao kama baba mwenye upendo na anayejali licha ya kuwa na shughuli nyingi za kiutawala. Kila mara alipata muda na watoto wake, kwa kuwashauri na kwa mafunzo, na alikuwa shujaa kwao.

Majukumu ya Utawala:

Safari ya uongozi ya Mchungaji Mulwambo ilianza mwaka 1988 alipoitwa kuwa mkuu wa Tanzania Adventist Seminary and College Arusha. Katika mwaka huo huo, aliwekewa mikono ya kichungaji na kuwa mhudumu wa injili katika Kanisa la Waadventista. Wakati akiwa mkuu wa shule, seminari hiyo iliongeza kozi mbali mbali kando ya ile ya mafunzo ya uchungaji, kama vile cheti cha huduma za ukatibu, diploma ya usimamizi wa biashara, na diploma ya elimu. Mbali na maendeleo hayo ya kitaaluma, baadhi ya miundombinu ilianzishwa, ikiwa ni pamoja na mabweni ya wanawake na wanaume na nyumba moja ya wafanyakazi. Kutokana na awamu hii ya maendeleo, Tanzania Adventist Seminary and College ilianza safari iliyoifanya kusajiliwa kama Chuo Kikuu cha Arusha.

Mwaka 1991 Mchungaji Mulwambo aliitwa kuhudumu kama Mwenyekiti wa Fildi ya Tanzania Mashariki, yenye makao yake makuu mjini Morogoro. Kufikia wakati huo, Fildi hiyo ilikuwa ikijumuisha mikoa ya kiutawala ya serikali ya Mtwara, Lindi, Pwani, Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, na visiwa vya Unguja na Pemba na Visiwa vya Zanzibar. Wakati huu, kazi ya umishionari ya Waadventista ilikuwa bado katika mwanzo wake katika sehemu nyingi za hayo maeneo. Mchungaji Manento anaelezea miaka hii kama miaka ya taabu, jasho na joto. Kulikuwa na uhaba wa rasilimali fedha na watu. Pamoja na changamoto zote hizo, Kanisa hilo katika Fildi ya Tanzania Mashariki lilifanikiwa kuanzisha zahanati katika Kisiwa cha Pemba ambacho kina Waislamu wengi.

Wakati wa kikao cha uchaguzi cha Union kilichofanyika kuelekea mwisho wa mwaka wa 2000, Mchungaji Mulwambo alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Fildi ya Magharibi mwa Tanzania. Fildi ya Magharibi mwa Tanzania ulihusisha mikoa ya utawala ya serikali ya Kigoma, Kagera, Tabora, Singida na Wilaya ya Mpanda, ambayo wakati huo ilikuwa katika mkoa wa utawala wa Rukwa. Siku hizo, kusafiri kwa barabara lilikuwa jambo la hatari sana. Lakini Mchungaji Mulwambo alisafiri katika eneo la West Tanzania Field bila woga. Mchungaji Mngwabi, ambaye aliwahi kufanya kazi naye West Tanzania Field, alitoa ushuhuda kuhusu namna alivyokuwa mmoja wa abiria wake pale majambazi wenye silaha walipowavamia na kuwatishia kuwaua walipokuwa wakisafiri kwenda kutembelea makanisa. Lakini Mungu alikuwa mwema, kwani Mchungaji Mulwambo na wao hawakudhurika.

Akiwa Mwenyekiti wa West Tanzania Field, Mchungaji Mulwambo na timu yake walianza kujenga jengo jipya la ofisi. Mradi huu ulianzishwa kwa imani kwa sababu hapakuwa na fedha. Lakini alifaulu kuwahamasisha waumini, nao wakaanza kujenga jengo jipya. Kufikia mwisho wa 2005, jengo la ofisi, ingawa lilikuwa halijakamilika kabisa, lilikuwa na vyumba vya kutosha kuruhusu wafanyakazi wote wa West Tanzania Field watumie kama mahali pao papya pa kufanyia kazi. Alipata fursa adimu ya kuwa mjumbe wa Kikao cha Konferensi Kuu cha 2005 ambacho kilifanyika huko Saint Louis, Missouri, Marekani. Zaidi ya hayo, Mchungaji Mulwambo alihudumu katika Halmashauri Kuu ya Union ya Tanzania kwa miaka 21 mfululizo. Hili liliwezekana kwa sababu, kwa miaka hiyo yote, aliwahi kuwa Mwenyekiti wa fildi fulani au mkuu wa taasisi ya union. Kulingana na taratibu za kanisa, nyadhifa zote mbili zilimstahilisha kuwa mshiriki wa vikao vya union.

Akiwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Union ya Tanzania, alihudumu pamoja na wenyeviti wa union wafuatao: Dk. Robert Taylor, Mchungaji Yohana Lusingu, Mchungaji Lameck Mwamukonda, Mchungaji Geoffrey Mbwana, Mchungaji Magesa Bina, na Mchungaji Joshua Kajula. Pia alifanya kazi kwa karibu na Mzee Eliamani Kachua, meneja biashara wa Tanzania Adventist Seminary and College; Mchungaji Mangi Fadhili Manento, katibu-mweka hazina wa fildi ya Tanzania Mashariki; Bw. Mathias Mavanza, katibu-hazina wa Fildi ya Tanzania Mashariki; Mzee Julius Rulanyaga, katibu-hazina wa Fildi ya Magharibi mwa Tanzania; Mchungaji Joseph Mngwabi, katibu wa West Tanzania Field; na Denis Wairaha, mweka hazina wa Ukanda wa Magharibi mwa Tanzania.

Miaka ya Baadaye ya Huduma na Kifo

Baada ya kuhudumu kama mwenyekiti wa West Tanzania Field (2001–2010), Mchungaji Mulwambo aliitwa kuhudumu kama mchungaji wa mtaa wa Ilala jijini Dar es Salaam mwaka 2011. Kufikia wakati huu, Wilaya ya Ilala ilikuwa na makanisa manne, likiwemo kanisa la Mzizima, ambalo halikuwa na jengo la ibada la kudumu. Mchungaji Mulwambo aliona kuwahudumia waumini wa kanisa hili ni changamoto ya kipekee. Waumini wa kanisa hili walijumuisha wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, Chuo cha Ufundi Dar es Salaam, na Taasisi ya Usimamizi wa Fedha pamoja na waumini wa kawaida wa kanisa waliotoka katika jiji zima la Dar es Salaam.

Kabla ya kulala katika Bwana, Mchungaji Mulwambo alihamishiwa Morogoro, Mtaa wa Misufini, ambako alichunga makanisa sita. Miaka yake ya mwisho ya huduma ilijaa tumaini la kurudi kwa Kristo upesi. Alilala katika Bwana mnamo Septemba 26, 2013.

Urithi

Mchungaji Eldad Jeremia Mulwambo atakumbukwa kwa ucheshi wake, uchapakazi, usimamizi mzuri, na kujitolea katika uinjilisti na moyo wa upandaji wa makanisa.