Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

KUNA NINI BAADA YA KUFA

KUNATOKEA NINI MTU ANAPOKUFA?

Zipo nadharia nyingi juu ya kile kinachotokea mtu anapokufa. Watu wamekuwa wakitaka kujua nini kinamtokea mtu mara tu anapokufa na upi ukweli kati ya dhana kuwa anabaki pale pale alipofia au alipozikiwa na dhana kuwa huenda mahali pengine? Katika kujibu hoja hizo mbili wengine wamekuja na nadharia kuwa mtu anapokufa anakuwa hajafa moja kwa moja bali anabadilisha aina ya kuishi na anakuwa katika mfumo tofauti na awali kwa kiasi fulani lakini akiwa na uwezo wa kuwasiliana na kutambua yanayotokea kwa walio hai, wakati wengine huamini mtu akifa anaendelea kuoza na hawezi kuishi tena isipokuwa kwa miujiza ya Mwenyezi Mungu.

Juu ya dhana ya wapi mtu huenda akisha kufa wapo wanaoamini kuwa hubaki pale pale alipofia au alipozikiwa hadi hapo itakapoamuliwa vinginevyo na Mungu mhukumu wa wote, na wapo wanaoamini kuwa mtu akifa huenda kwenye mateso ya moto kama atapatikana kuwa na hatia ama huenda kwenye raha ya milele (peponi) ikiwa atapatikana kuwa hawana hatia. Ili kuondoa utata huu tutatumia Maandiko Matakatifu katika kujibu swali “Kunatokea nini mtu anapokufa?”

Juu ya wafu huenda wapi baada ya kufa, jibu lake linatolewa na Yesu mwenyewe katika Yohana 5:28; “Msistaajabie maneno hayo; kwa maana saa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake. Nao watatoka; wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima, na wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu.” Yesu hapa anasema watu waliokufa wanabakia hapo hapo walipofia (kama haikuwezekana kuwazika) ama wanabakia makaburini (kama iliwezekana kuwazika) hadi yeye mwenyewe atakaporudi, bila kujali kama wanastahili hukumu ama wanastahili uzima wa milele.

Hakuna kinachofanyika sasa kwa watu waliokufa. Wanapumzika wakisubiri kufufuliwa siku ya mwisho. Siku hiyo Mungu atakaposhuka maiti zote zitainuka na kutoka makaburini na watakaotangulia kutoka watakuwa wale wenye haki. “Wafu wako wataishi, maiti zangu zitafufuka; amkeni, kaimbeni, ninyi mnaokaa mavumbini, kwa maana umande wako ni kama umande wa mimea, nayo ardhi itawatoa waliokufa.” (Isaya 26:19) “Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza.” (1 Wathesalonike 4:16)

Baada ya wenye haki kufufuliwa ndipo watafuatia waovu (au wale ambao hawakumwamini Yesu). Hawa watafufuliwa kwa ajili ya kupokea hukumu yao ambayo Yesu aliwalipia pale msalabani lakini hawakutaka kuipokea kwa imani. “. . . Wakati wa kufunuliwa kwake Bwana Yesu kutoka mbinguni pamoja na malaika wa uweza wake katika mwali wa moto; huku akiwalipiza kisasi wao wasiomjua Mungu, na wao wasioitii Injili ya Bwana wetu Yesu; watakaoadhibiwa kwa maangamizi ya milele, kutengwa na uso wa Bwana na utukufu wa nguvu zake.” (2 Wathesalonike 1:7-9). Sababu ya waovu kuangamizwa inatajwa hapa kuwa ni kutomjua Mungu, na kutotii injili ya Bwana Yesu.

Hakuna atakayeangamizwa kwa sababu ya uwingi wa dhambi zake maana Yesu alizilipia dhambi hizo pale msalabani.Kristo alikuja duniani kulipa adhabu ya kifo kile kitakachowapata watakaokataa kumwamini. Na kwa kuwa Mungu hana sera ya kulazimisha viumbe wake kukubali anachowafanyia atakubaliana na uchaguzi wao wa kutengwa naye milele kwa maangamizo yale makuu ingawa alilipa kila kitu kwa ajili yao.

Juu ya hoja kuwa wenye waliokufa wanaendelea kuishi katika mfumo fulani unaowawezesha kuwasiliana na walio hai au kujua kinachoendelea katika maisha ya wanadamu, Maandiko Matakatifu yanapinga dhana hiyo. “Kwa sababu walio hai wanajua ya kwamba watakufa; lakini wafu hawajui neno lo lote, wala hawana ijara tena; maana kumbukumbu lao limesahauliwa.” (Mhubiri 9:5). Na kwa kuwa Yesu alisema waliokufa wanaendelea kukaa makaburini hiyo inaondoa uwezekano wa wao kuendelea kuishi. Ili binadamu aweze kuishi kunatakiwa muunganiko wa vitu viwili; kiwiliwili na pumzi ya Mungu. “Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.” (Mwanzo 2:7). Kifo kinapotokea pumzi hutoka na kiwiliwili kukosa uhalali wa kuendelea kuishi. “Pumzi yake hutoka, huurudia udongo wake, Siku hiyo mawazo yake yapotea.” (Zaburi 146:4)

Dhana kuwaa mtu anapokufa anaendelea kuishi zinalenga kuwafariji wafiwa kwa kuwapunguzia uchungu, ama zinalenga kuwahadaa wanadamu. Maana wengine kwa kutumia dhana hizo wamewatoza wafiwa wakiwaahidi kuwaombea marehemu wao na kuwatoa sehemu ya mateso. Njia sahihi ya kukabili uchungu wa kuondokewa na marehemu ni kukubali kuwa amekufa na hajui lolote na Mungu ndiye atakayeamua pa kumweka siku hiyo ya mwisho anapokuja kuhukumu wanadamu.