Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

KRISTO HAKI YETU

HAKI IPATIKANAYO KWA IMANI

Hii ni makala inayoochambua namna haki ipatikanavyo kwa imani. Haki ni kiwango ambacho mwanadamu yoyote anapaswa kukifikia ili kustahili kuokolewa. Kiwango hicho cha haki kiko juu kiasi cha mwanadamu yoyote wa kawaida kutoweza kukifikia. Adamu na Hawa waliwahi kukifikia kiwango hicho mara tu baada ya kuumbwa kwao, kabla hawajaanguka dhambini. Baada ya kuanguka dhambini mwanadamu mwingine aliyewahi kukifikia kiwango hicho ni Yesu. Yesu alikuwa na asili zote mbili. Alikuwa mwanadamu asilimia mia moja na Mungu asilimia mia moja. Yesu hakutumia uungu kufikia kiwango hicho cha haki. Alitumia ubinadamu ule ule upatikanao kwa mwanadamu yeyote. Tofauti ni kuwa yeye alimtegemea Mungu asilimia mia moja kinyume na wamadamu wengine wanaomtegemea Mungu kwa kiasi fulani na kwa kiasi kingine wakijitegemea wenyewe.

HAKI NI NINI?

Kwa kawaida haki ni kile unachostahili baada ya kutekeleza wajibu fulani. Haki ya mfanyakazi baada ya kufanya kazi ni ujira. Haki ya mwanariadha ni kutunukiwa taji baada ya kufikia viwango vya kukimbia vinavyohitajiwa. Haki ya mwanafunzi ni kutunukiwa cheti baada ya kufikia viwango vya ufaulu vilivyowekwa. Haki ni matokeo ya kutimiza makubaliano fulani. Kwa upande wa kiroho haki ni ya Mungu tu. Ndiyo maana waswahili wana usemi ambao kwa bahati mbaya hutumika katika kuapa usemao ‘Haki ya Mungu’ Pengine nia ya kutumia usemi huo kwenye kiapo ni kudhihirisha kuwa mwenye haki ni Mungu tu. Haki ni ya Mungu kwa sababu ni yeye tu ndiye anayeweza kufikia viwango vya haki vinavyokubalika.

MWENYE HAKI NI MUNGU PEKEE

Haki ni hali ya kutodaiwa chochote kwa mujibu wa makubaliano. Mungu ni mtakatifu. Utakatifu ni hali ya kutokuwa na dhambi. Kipimo cha kutambua kuwa mtu hana au ana dhambi ni kuangalia kama anaenenda sawa sawa na Amri Kumi za Mungu, kwa sababu Amri Kumi za Mungu  ni kipimo cha haki. Mtu akifanya kinyume cha Amri za Mungu anakuwa mdhambi na akifanya sawa sawa na Amri Kumi anakuwa mtakatifu na mwenye haki. Mungu anayo sifa ya kutokwenda kinyume cha Amri au Sheria zake wakati wowote. Ndiyo maana yeye anatambulika kama mtakatifu au mwenye haki. Yeye hafanyi mabaya yoyote wakati wowote. Hana ubaya katika sura zote tatu za ubaya. Kwanza hawazi wala kunia mabaya kama wanadamu. Pili haneni neno lolote baya kama wanenavyo wanadamu. Na tatu hatendi tendo lolote baya kama wanadamu watendavyo. Mungu hajawahi kufanya lolote katika hayo. Yeye hujua mema na mabaya lakini hajawahi kutumia uhuru alionao kuchagua kufanya mabaya. Hajawahi kunia au kuwazia mabaya, kunena neno baya au kutenda tendo baya. Hakuwahi kufanya hayo pale alipokuwa na asili ya uungu na hakuwahi kufanya hayo hata pale alipochukua ubinadamu!

YESU HAKUWAHI KUTENDA DHAMBI!

Yesu hapo mwanzo alikuwa Mungu. Lakini akaona kule kuwa sawa na Mungu kuwa si kitu cha kushikamana nacho sana. Akatwaa kwa hiari yake asili ya mwanadamu ili amkomboe mwanadamu. Na hata alipokuwa mwanadamu akawa mtii. Akiwa katika ubinadamu ule, Yesu alitii kikamilifu. Yeye alitii Amri Kumi za Mungu kikamilifu, kuliko alivyowahi kufanya mwanadamu mwingine yeyote. Yeye ndiye mwandamu mtakatifu kuliko yeyote aliyewahi kuishi duniani. Yeye alishuhudiwa na walioishi katika kizazi chake kuwa hakuwa na dhambi. Aliwahi kuwauliza wasikilizaji wake wakati fulani kuwa ni nani kati yao aliyemshuhudia kuwa ni mwenye dhambi, (Yoh. 8:46). Hakuna aliyejitokeza kuthibitisha kuwa Yesu alikuwa na dhambi. Kijana mmoja tajiri alidiriki kumwita ‘mwalimu mwema’ kwa kuwa hivyo ndivyo alivyokuwa anatambuliwa na wengi. Yeye alishinda dhambi si kwa sababu aliishi kwenye maisha yasiyo na majaribu kama wengine wadhaniavyo. Yeye alijaribiwa sawa sawa na sisi bila kutenda dhambi. (Waebrania 4:15).

KWA NINI NI VIGUMU KWA MWANADAMU KUWA MWENYE HAKI

Iliwezekana mwanadamu kuwa mwenye haki pale kabla hajaanguka dhambini. Baada ya kuanguka dhambini mwanadamu alipoteza uwezo wa kutenda mema. Hakuwa na uwezo tena wa kutenda yale yanayohitajiwa na sheria ya Mungu. Jitihada zake za kutenda mema zilimwezesha kufikia kiwango fulani cha chini cha matakwa ya sheria ambacho hakikumpa uhalali wa kutambuliwa kuwa ni mwenye haki. Kiwango hicho cha chini nabii Isaya anakiita nguo iliyotiwa unajisi. Nguo iliyotiwa unajisi anayoilinganishia matendo yetu ya haki yanayotokana na jitihada zetu ni kama ile ilyotumiwa na mwanamke aliyekuwa kwenye siku zake. Ambayo si tu haitamanaki bali ilikuwa ni mwiko kwa myahudi kuisogelea au kuigusa maana ilikuwa imenajisika. Ndivyo yalivyo matendo yetu ya haki tujaribuyo kuyafanya kwa jitihada zetu wenyewe yanavyoonekana mbele ya Mungu.

HUWEZI KUTENDA MEMA KAMA WEWE SI MWEMA

Ni vigumu kwa mwanadamu kutenda mema kwa kuwa yeye si mwema tena. Tabia ya wema ilipotea pale tulipotenda dhambi. Moja ya madhara makubwa yaliyoletwa na dhambi ni kutupotezea uwezo wa kutenda mema. Madhara mengine yaliyoletwa na dhambi ni kupoteza uzima wa milele, kupoteza amani moyoni, kupoteza urithi na umiliki wa kifalme tuliopewa, kupoteza uwezo wa kutambua unyonge wetu, kupoteza uwezo wa kutambua nguvu iliyo karibu yetu tunayopaswa kuing’ang’ania, kupoteza uwezo wa kutumia uhuru wetu vizuri, na kupoteza haki mbele za Mungu. Katika kitabu hiki tutajadili kila tulichokipoteza kama matokeo ya dhambi na namna Mungu kupitia kwa Yesu Kristo alivyoturejeshea vyote tulivyokuwa tumevipoteza! Katika hatua hii hebu tujadili namna tulivyopoteza uwezo wa kutenda mema.

Samsoni anajua vizuri maana ya kupoteza uwezo. Alikuwa mtu mwenye nguvu aliyeishi kipindi cha Agano la Kale katika taifa la Israeli. Mtu huyu aliyejaliwa nguvu zisizo za kawaida alifanya kosa la kueleza asili ya nguvu zake kwa mwanamke kahaba aitwaye Delila. Delila baada ya kuambiwa kuwa asili ya nguvu za samsoni ni nywele zake ambazo zilikuwa hazijakatwa tangu kuzaliwa, alitumia fursa ile Samsoni alipokuwa usingizini kuzinyoa nywele zake zote. Ndipo kwa ghafla Samsoni alipoamshwa ajitetee na dui zake waliokuwa wamezingira aligundua nguvu zake, uwezo wake umeondoka na hakuwa tena na zile nguvu zake za awali. Samsoni alijaribu kupambana na adui zake lakini alishindwa na kufungwa kamba na hatimaye kutobolewa macho yote mawili! Samsoni ambaye hapo mwanzo alikuwa tishio akawa si tishio tena! Alipoteza asili yake. Wanadamu walipotenda dhambi walipoteza asili yao. Ule uwezo wa kutenda wema uliokuwa ndani yao ukatoweka. Wakabaki wasio na uwezo kabisa wa kutenda mema. Ulemavu fulani ukawaingilia. Ulemavu ambao haukuruhusu uzalishaji wa matendo mema. Ulemavu ulioingilia utendaji bora wa mfumo uliokuwa ukiuendesha mwili hapo mwanzo. Uingiliaji huo unafanan na ule unaotokea wakati kompyuta inapoingiliwa na virusi, au mwili wa binadamu unapoingiliwa na virusi vya UKIMWI. Mfumo wa awali hufanywa mtumwa wa mfumo mpya unaojichukulia mamlaka ya kuongoza kila kinachotakiwa kufanyika. Kuanzia wakati wa uingiliaji kati wa mfumo huu mpya wa kigeni usio na nia njema kunazaliwa mgongano na wa kudumu baina ya mifumo hii miwili. Mfumo wa awali ukitaka kuendesha utendaji unaohitajika na ule mfumo adui wa kigeni ukitaka kuzuia ufanisi wa utendaji wa mfumo ule wa awali. Mgogoro huu unatajwa na Mtume Paulo kwa maelezo yafuatayo. “Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, Roho kushindana na mwili, kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka.” (Wagalatia 5:17)

KICHAFU HAKIWEZI KUTOA KISAFI

Yesu alipokuwepo hapa duniani aliwahi kuongelea tatizo hili. Yeye alisema wazi kuwa mwanadamu hawezi kutenda mema kwa kuwa yeye si mwema. “Enyi wazao wa nyoka, mwawezaje kunena mema, mkiwa wabaya? Maana, kinywa cha mtu huyanena yaujazayo moyo wake. Mtu mwema katika akiba njema hutoa mema; na mtu mbaya katika akiba mbaya hutoa mabaya.” (Mathayo 12:34, 35. Katika maelezo haya Yesu anafafanua kwa nini mwandamu hawezi kunena mambo mema. Kosa halipo mdomoni au kwenye maneno yake. Kosa lipo kwenye asili au kule kunakozalishwa yale maneno ambako ni kubaya. Na kitu kibaya kwa kawaida, hakiwezi kutoa kitu kizuri. Ukweli huu unaelezwa na mwandishi wa kitabu cha Ayubu pale anapoiweka hoja hii katika muundo wa swali. “Ni nani awezaye kutoa kitu kilicho safi kitoke katika kitu kichafu? Hapana awezaye.” (Ayubu 14:4)

Ulemavu huo wa kushindwa kutenda mema unawapata wanadamu wote kwa kuwa wanaupata kwa njia ya kuurithi. Kila aliyezaliwa na mwanamke anakuja duniani akiwa na udhaifu huu mwilini mwake. Jamii yote ya wanadamu bila kujali tofauti za jinsia, utaifa, rangi, kabila, lugha au jamaa. Kama ilivyo vigumu kwa mwandamu kubadili asili ya utaifa au jinsia yake ndivyo pia ilivyo vigumu kwa mwandamu kubadili asili yake ya ulemavu wa kutoweza kutenda mema. Nabii Yeremia analiweka hilo katika maelezo yafuatayo: “Je! Mkushi (Mwafrika mwenye asili ya Ethiopia) aweza kuibadili ngozi yake, au chui madoa-doa yake? Kama aweza, ndipo na ninyi mwaweza kutenda mema, ninyi mliozoea kutenda mabaya” (Yeremia 13:23)

Yeremia anafafanua kuwa sisi tumezoea kutenda mabaya kwa kuwa asili yetu inaturuhusu tu kutenda mabaya kama ambavyo chui analazimishwa na asili yake kuwa na madoa doa na si jambo linalotokana na hiari yake. Huwi mbaya kwa sababu umechagua kuwa mbaya. Hata wale wanaochgua kuwa wema hujikuta wakitenda mabaya kinyume na dhamira zao. Mtume Paulo alikabiliana na hali hiyo. Katika kitabu cha Warumi sura ya saba anaijadili hali hii. “Maana sijui nifanyalo, kwa sababu lile nilipendalo, silitendi; bali lile nilichukialo ndilo ninalolitenda. Kwa maana najua ya kuwa ndani yangu, yaani, ndani ya mwili wangu, halikai neno jema; kwa kuwa kutaka nataka, bali kutenda lililo jema sipati. Kwa maana lile jema nilipendalo, silitendi; bali lile baya nisilolipenda ndilo nilitendalo.” (Warumi 7:15, 18, 19)

ALIYEZALIWA NA MWANAMKE AWEZA KUWA NA HAKI?

Wanadamu wote ukiondoa wale wawili wa kwanza (Adamu na Hawa) huja duniani kupitia mwanamke. Wote hukaa tumboni mwa mwanamke kwa miezi tisa na kuzaliwa akiwa na vinasaba vya mume aliyetoa mbegu za kiume na mama aliyetoa yai lililounganika na mbegu na kuunda mwanadamu. Kwa kawaida mtoto licha ya kuchukua vinasaba vya wazazi hawa wawili huchukua madhaifu mengine atakayokuwa nayo mama. Mfano mama mwenye upungufu wa kinga mwilini (UKIMWI) ana uwezekano mkubwa wa kumsababisha mtoto wake kuzaliwa akiwa na virusi vya UKIMWI kuliko kutoka kwa baba mwenye virusi, kwa kuwa ni yeye anayekilisha kile kitoto katika kipindi chote kitakapokuwa tumboni. Mama anayevuta sigara, tunaambiwa na wataalamu wa afya ana uwezekano mkubwa wa kuzaa kitoto njiti kwa sababu zile zile za UKIMWI. Kwa hiyo mchango wa mama kwa ulemavu wowote wa mtoto ni mkubwa kuliko wa baba. Ndiyo sababu Ayubu anashangaa ingewezekanaje mwanamke mdhambi na mwenye mapungufu mengine azae kitoto ambacho hakina athari hizo ila kikawa kikamilifu kama Mungu alivyo. “Basi mtu awezaje kuwa na haki mbele ya Mungu? Au awezaje kuwa safi aliyezaliwa na mwanamke?” (Ayubu 25:4). Tena anaongeza. “Je! Mwanadamu ni kitu gani, hata akawa safi? Huyo aliyezaliwa na mwanamke, hata awe na haki?” (Ayubu 15:14).

ONYO KWA WANAUME

Katika jamii nyingi wanaume huchukuliwa kuwa ni bora kuliko wanawake. Hata jamii ya Kiyahudi ilikuwa na kawaida ya kuwaona wanawake kuwa ni duni. Sababu za kufanya hivyo wakati mwingine hutolewa kwenye vitabu vitakatifu kama Biblia na Kurani ikidaiwa kuwa mwanamke hakuumbwa kwa mfano wa Mungu maana alitolewa kwenye ubavu wa mwanaume. Sababu hiyo na sababu nyingi nyingine zina lengo la kumtofautisha mwanaume na mwanamke katika viwango vya ubora kabla na baada ya dhambi. Lakini hoja inayotolewa na Mwandishi wa kitabu cha Ayubu ingepaswa iwape tahadhari wale kupendeea msimamo huo wa kutoa majumuisho ya jumla jumla.

PASIPO MIMI NINYI HAMWEZI NENO LOLOTE

Wanadamu wote ni wabaya bila kujali kama wamefanya baya au hawajafanya. Ni wabaya si kwa sababu ya mabaya wanayofanya bali ni wabaya kwa sababu wana asii ya ubaya ambao hata kama haujaonekana kwa nje upo ndani yao ukisubiri nafasi nzuri ili utokee nje. Yesu akiitambua hali hiyo alituonea huruma akasema: “Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote.” (Yohana 15:5). Yesu pekee ndiye awezaye kutufanya tuweze kutenda mema. Anatuwezesha kutenda baada ya kutufanya wema kama yeye mwnyewe aivyo. Muujiza unaotubadilisha tuliokuwa wabaya kuwa wema ni muujiza upitao miujiza yote ambayo Yesu amewahi kuifanya.

KITU KISAFI KUTOKA KWENYE KITU KICHAFU

Yesu ndiye aiyembadiisha Rahabu kutoka kuwa kahaba hadi kuwa miongoni mwa mashujaa wa imani walioorodheshwa kwenye waebrabia kumi na moja. Yesu ndiye aiyembadilisha mtesaji wa wakristo wa kanisa la kwanza; Sauli (ambaye baadaye aliitwa Pauo) na kumfanya mtume aliyepeleka Injii kwa nguvu kubwa na kuchangia kuwepo kwa ongezeko kubwa la waumini waliojiunga na kanisa. Mtu mbaya anaweza kuwa mzuri kwa njia ya Roho Mtakatifu aliye na uwezo wa kuondoa ile asili ya ubaya kwa kuitiisha isiwe na uwezo wa kuzalisha mawazo, maneno na matendo mabaya. Roho huuteka moyo na kuuendesha apendavyo wakati mtu anapoisalimisha nia yake kwa Mungu  kwa hiari. Kile kilichoonekana pale mwanzo kuwa ni kitu kisichowezekana; yaani kitu kisafi kutoka kwa kitu kibaya kwa njia ya Roho Mtakatifu, sasa kinawezekana. Hata Yesu (mwanadamu aliyekuwa mwema kuliko wote) alizaliwa kutoka kijiji kilichodhaniwa kuwa hakingeweza kutoa lolote jema. “Filipo akamwona Nathanaeli, akamwambia, Tumemwona yeye aliyeandikiwa na Musa katika torati, na manabii, Yesu, mwana wa Yusufu, mtu wa Nazareti. Nathanaeli akamwambia, Laweza neno jema kutoka Nazareti? Filipo akamwambia, Njoo uone.”   (Yohana 1:45, 46) Ndiyo! Mtu mwema aweza kutoka kwa mtu mbaya kama ambavyo neno jema liliweza kutoka Nazareti. Twende pamoja nami kwenye karakana ya Yesu ukajionee mwenyewe namna hilo linavyowezekana.

KUZALIWA MARA YA PILI

Nikodemu alikuwa mwalimu wa dini ya kiyahudi aliyeheshimika sana tena aikuwa kiongozi. Walimu hawa wa dini walichukua muda wao mwingi kujifunza maandiko na hasa sheria za torati na kanuni zingine zingine ili kujaribu kujiingizia sifa zitakazowastahilisha kuwa wenye haki mbele za wanadamu wenzao na mbele za Mungu. Lakini pamoja na jitihada hizo zote waalimu hawa wa dini walihisi kupungukiwa na kitu fulani. Kutokana na hali hiyo, Nikodemu alimtafuta Yesu aiyemtambua kuwa ni binadamu wa pekee mwenye uwezo wa kiungu ili amsaidie. Lakini kwa sababu ya kuogopa watu wasimuone mnyonge alimwendea Yesu usiku wakati kuna kiza. Yohana anaandika hivi kuhusiana na tukio hilo. “Basi palikuwa na mtu mmoja wa Mafarisayo, jina lake Nikodemo, mkuu wa Wayahudi. Huyo alimjia usiku, akamwambia, Rabi, twajua ya kuwa u mwalimu, umetoka kwa Mungu; kwa maana hakuna mtu awezaye kuzifanya ishara hizi uzifanyazo wewe, isipokuwa Mungu yu pamoja naye.” (Yohana 3:1-3). Yesu alilijua hitaji lake na moja kwa moja akampa njia sahihi ya kufikia viwango vya haki ni kwa yeye kukubali kubadilishwa moyo wake kwa njia ya kuzaliwa upya kwa msaada wa Roho Mtakatifu. “Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu. Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa? Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu. Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho. Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia, Hamna budi kuzaliwa mara ya pili.” (Yohana 3: 4-7)

Wanadamu huanza maisha baada ya kuzaliwa na mwanamke. Kwa bahati mbaya amaisha hayo yamejaa masumbufu mengi ukiwepo utumwa wa dhambi ambapo mtu hujikuta amefungwa asiweze kutenda mema anayoyatamani. Hakuna anayeweza kuyajia maisha kwa njia nyingine tofauti na hiyo ya kuzaliwa na mwanamke. Hali kadhalika ili mtu ayajie maisha ya kiroho yenye ushindi juu ya dhambi ni azima kwanza aifie ile hai yake ya mwanzo ya dhambi na kuzaliwa upya katika maisha ya ushindi dhidi ya dhambi. Mabadiliko hayo ni ya lazima ambayo hufnywa kwa hiari na Yule anayejisikia kutoridhika na maisha ya kitumwa.

MAISHA YA KITUMWA

Mwanadamu aliumbwa awe na uwezo wa kutumia uhuru wake kuchagua alipendalo. Uwezo huo alipewa na Mungu. Mungu alikusudia mwanadamu afaidi uhuru wa kujiamulia mambo yake bila kushurutishwa, kama ambavyo yeye Mungu  amekuwa akifaidi uhuru huo tangu milele hapo alipoanza kuwepo. Mwanadamu aliumbwa kwa mfano wa Mungu  awe mtawala mwenye kuvitawala vyote Mungu  alivyoviweka katika ulimwengu huu. Na ili ajue kujitawala alipaswa yeye mwenyewe ajue kujitawala. Ajue mipaka ya uhuru wake. Kwa kuwa kila uhuru ni lazima ukomee pale uhuru wa mwnigine unapokuwa hatarini kuhujumiwa. Lakini dhambi ilimuondolea mwanadamu uhuru huu. Na kielelezo sahihi cha kutambua madhara ya kupoteza uhuru huo ni pale wanadamu walionekana kuwa wanyonge kuliko wenzao waipofanywa watumwa wa kutumikishwa bila hiari na bila malipo. Kwa bahati mbaya waafrika walijikuta wakiangukia katika kundi la watu waliofanywa watumwa kwenye karne ya 15 na 16. Watumwa walifanyishwa kazi ngumu bila kupewa ajira yoyote. Walitumiwa kama vitumikavyo vifaa na nyenzo zingine za kiuchumi kama matrekta, majembe, mapanga n.k. Hawakuwa na hiari ya kukataa kufanya kazi hata pale walipokuwa wamechoka au kuumwa! Hiyo ndiyo hali anayokuwa nayo mdhambi yeyote. Anatumikishwa na dhambi. Hafaidiki chochote yeye mwenyewe, ila anafanya kwa kuwa bwana wake anamuamurisha afanye. Bwana anayewaamurisha wanadamu kufanya dhambi ni nani? Ni Shetani

SHETANI NDIYE MUASISI WA DHAMBI

Shetani ni muasisi wa dhambi. Yesu anasema “Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo.” (Yohana 8:44). Kwa kweli Shetani hakuumbwa akiwa na dhambi wala hakuumbwa akiwa anaitwa Shetani. Yeye aliumbwa akiwa mkamilifu, na akiitwa Lusifa jina lenye maana ya nyota ya alfajiri. “Ulikuwa mkamilifu katika njia zako tangu siku ile ulipoumbwa, hata uovu ulipoonekana ndani yako. Kwa wingi wa uchuuzi wako watu walikujaza udhalimu ndani yako, nawe umetenda dhambi; kwa sababu hiyo nimekutoa kwa nguvu katika mlima wa Mungu, kama kitu kilicho najisi; nami nimekuangamiza, Ewe kerubi ufunikaye, utoke katika mawe hayo ya moto. Moyo wako uliinuka kwa sababu ya uzuri wako; umeiharibu hekima yako kwa sababu ya mwangaza wako; nimekutupa chini, nimekulaza mbele ya wafalme, wapate kukutazama.” (Ezekiel 28:15-17). Hata leo haijulikani dhambi iliwezekanaje kutokea kwa kiumbe mkamilifu, tena kwenye makao ya amani mbinguni. Lakini ukweli ni kuwa Malaika yule aiyependeewa sana alilea mawazo ya kutoridhika na kile alichopewa na kutamani kile ambacho Mungu kwa hekima yake alikizuia asiwe nacho. Yeye na malaika wengine walioshawishiwa na uongo wake walitimuliwa kutoka mbinguni nao wakaja duniani na kufanikiwa kuwashawishi wanadamu wale wa kwanza na udanganyifu wake na hivyo dunia yote ikaingia kwenye dhambi. Malaika hao waovu wamewekwa kifungoni wakingojea hukumu yao. Mwandishi wa kitabu cha Yuda anatutahadharisha tusije tukakutwa na hayo yaliyowakuta malaika wale wasioridhika. “Na malaika wasioilinda enzi yao wenyewe, lakini wakayaacha makao yao yaliyowahusu, amewaweka katika vifungo vya milele chini ya giza kwa hukumu ya siku ile kuu.” (Yuda 1:6).

YESU ATUWEKA HURU

Yesu alikuja ulimwenguni ili atuweke huru mbali na utumwa wa dhambi. Alikuja aturudishie uwezo wa kuchagua kile tukijuacho kuwa ni chema, ili tusitumikishwe na dhambi tena bila hiari yetu. Alikuja atupatie uwezo wa kusema HAPANA! Alikuja aturejeshee uwezo wa kujitawala. Alikuja ili atupe fursa nyingine ya pili ya kuchagua kati ya Mungu na Shetani; kati ya wema na ubaya; na kati ya kuokolewa na kupotea. Jambo gumu katika kumuweka mtu huru, ni pale atakaposhindwa kuona umuhimu wa kuwekwa huru na kukataa kushirikiana katika jaribio lolote la kumuweka huru. Watumwa wakati wa agano la kale waikuwa na hiari ya kuachiliwa huru baada ya miaka sita ya utumishi. “Ukimnunua mtumwa wa Kiebrania, atakutumikia muda wa miaka sita; mwaka wa saba atatoka kwako huru bure.” (Kutoka 21:2) Lakini wapo waliochagua kuendelea na utumwa hata muda wa kuachiliwa ulipokuwa umewadia. Walikuwa wameuzoea utumwa kiasi cha kutoamini kama wangeweza kufurahia maisha mengine kando ya yale ya utumwa. “Lakini huyo mtumwa akisema waziwazi, Mimi nampenda bwana wangu, na mke wangu na watoto wangu; sitaki mimi kutoka niwe huru; ndipo hapo huyo bwana wake atamleta mbele ya Mungu na kumleta mlangoni, au penye mwimo wa mlango; na bwana wake atalitoboa sikio lake kwa uma; ndipo atamtumikia sikuzote.” (Kutoka 21:5, 6) Ndivyo ilivyokuwa vita ya kupambana na utumwa katika karne ya 15 na 16. Haikuwa rahisi. Haikuwa rahisi kwa kuwa si mabwana wa watumwa tu waliolipinga zoezi hilo bali hata baadhi ya watumwa wenyewe hawakuwa tayari kuachwa huru. Waliuzoea utumwa.

Yesu ameahidi kutuweka huru. “Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli.” (Yohana 8: 36). Yeye anajua kutakuwa na kipingamizi kutoka kwa wale waliozoelea utumwa. Kwao hii haitakuwa habari njema. Watajaribu kuzuia ili wasiwekwe huru. Lakini kama watashirikiana na Roho wake atakayewadhihirishia namna walivyo watumwa wa dhambi kwa njia ya maandiko wataitumia fursa hiyo vizuri na kuchangamkia taarifa hizo za kuwekwa huru. Mungu  hulitumia neno kuwadhihirishia walio utumwani juu ya hali yao isiyo na matumaini na kuwaonyesha namna Mungu  alivyotafuta ufumbuzi wa tatizo lao. Somo la namna Mungu anavyotusaidia tujitambue tulivyo wanyonge na namna tunavyopaswa kung’a ng’ania uwezo ulio juu yetu utokao kwa Mungu, litakuja hapo baada