Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

MZAO MTEULE

SIFA ZA KUWA MZAO MTEULE

Unaposikia neno Mzao Mteule mambo ambayo huenda utatamani kufahamu ni kuwa nani huyo aliye mzao mteule, sifa gani zilizingatiwa katika kumfanya mzao mteule, ni lini alipofanywa mzao mteule na nani alikuwa na mamlaka hayo ya kumfanya mzao mteule, kabla ya kupewa hadhi ya mzao mteule hapo mwanzo alikuwa na hadhi gani, na haki na stahiki gani zinaandamana na huko kuwa mzao mteule?

Fuatana nami katika makala haya upate majibu ya maswali hayo yote. Petro alipokuwa akiwaandikia watu wote alidokeza kuwepo kwa dhana ya mzao mteule. (1 Petro 2:9) “Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu.”

Kinachosewa hapa ni kuwa sisi yaani mimi na wewe na binadamu wote tumekirimiwa hadhi ya mzao mteule na Mungu aliye asili ya uhai wote aliye muumbaji wa mbingu na ardhi na vyote vinavyoonekana na visivyoonekana. Alituchagua tuwe mzao mteule kabla ya kuwekwa kwa misingi ya dunia. (Waefeso 1:4) “Kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo.”

Mungu anapoteua hafanyi hivyo kutokana na sifa za anayeteuliwa. Yeye huangalia utayari wa mhusika katika kushirikiana naye kufanikisha mpango unaowekwa mbele yake. Nuhu hakuwa mkamilifu sana kwa kuwa hata baada ya gharika kwisha yeye na familia yake (jumla ya watu wanane) waliopona kati ya mabilioni walioteketea na maji alikunywa pombe na kufanya mambo ya aibu. (Mwanzo 9:20-26).

Mungu alimchagua Nuhu kwa kuwa alikuwa tayari kujenga safina katika kipindi ambacho mvua hazinyeshi naye akaamini kuwa dunia itagharikishwa na maji na watu wataokolewa kwa Safina ambayo Mungu anamwagiza kuijenga. Jambo muhimu ni kuwa Nuhu aliamini kuwa mvua itanyesha kama Mungu alivyosema na kuwa wale watakaokubali kuokolewa wataokolewa ili kuhifanyi jamii ya mzao mteule ulioteuliwa kabla ya kuwekwa kwa misingi ya dunia. Hakutilia shaka maagizo ya Mungu. (Mwanzo 6:22) “Ndivyo alivyofanya Nuhu, sawasawa na vyote alivyomwamuru Mungu, hivyo ndivyo alivyofanya.”

Mpango wa kuokoa mzao mteule kwa Safina uliratibiwa na Mungu ili kuzima jaribio la Shetani la kuangamiza mzao mteule wa Mungu jaribio ambalo halikufanikiwa licha ya kuleta hasara ya vifo vya watu wanaokadiriwa kuwa bilioni kumi na moja. Jaribio hili halikuwa la kwanza kufanywa na Shetai hapo nyuma alimwongoza Kaini kukaidi mpango wa ibada ya Mungu uliohusisha kafara ya wanyama kuwakilisha mpango mkubwa wa kuokoa mzao mteule utakaotekelezwa na Yesu mwenyewe aliye mzao mteule halisi (Mwanzo 4:3-5). Uzao wa Kaini uliokataa hadhi ya mzao mteule ukaendelea kuasi maagizo ya Mungu hadi ulipoangamizwa kwenye gharika.

Mzao mteule ulikuwa uwe na sifa pia ya kuwa taifa takatifu la Mungu ukiwakilisha tabia yake ya upendo na utakatifu katika jamii iliyopotoka. (Wafilipi 2:15) “Mpate kuwa wana wa Mungu wasio na lawama, wala udanganyifu, wasio na ila kati ya kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka; ambao kati ya hao mnaonekana kuwa kama mianga katika ulimwengu.”

Kwa bahati mbaya wateule wa Mungu walishindwa kuwa mabalozi sahihi wa tabia ya Mungu na hivyo Mungu akalazimika kila uasi ulipotokea kuchagua wateule wapya kuwakilisha tabia ya Mungu na kuendeleza mbegu ya mzao mteule. Baada ya Nuhu Mungu alimchagua Ibrahimu na baadaye wazao wake walioitwa Waisraeli. Lengo likibaki kuwa watu watakaounda taifa takatifu, wakitangaza matendo yake ya ajabu kwa wanadamu bila kubagua. Hawakuchaguliwa kwa sababu ya wema wao au uwingi wao. 

(Kumb. 7:6-8). “Kwa maana wewe u taifa takatifu kwa BWANA, Mungu wako; BWANA Mungu wako, amekuchagua kuwa watu wake hasa, zaidi ya mataifa yote walioko juu ya uso wa nchi. BWANA hakuwapenda ninyi, wala hakuwachagua ninyi, kwa sababu mlikuwa wengi kuliko mataifa yote, maana mlikuwa wachache kuliko watu wote; bali kwa sababu BWANA anawapenda, na kwa sababu alitaka kuutimiza uapo wake aliowaapia baba zenu, ndiyo sababu BWANA akawatoa kwa mkono wa nguvu, akawakomboa katika nyumba ya utumwa, katika mkono wa Farao, mfalme wa Misri.”

Mungu anapoteua watu wa kumwakilisha atakaowatambua kama mzao mteule huangalia utayari wao wa kutumika na kile alichopanga kukifanya juu ya watu hao tangu milele. Mungu alituchagua sisi si kwa kuwa tulikuwa wema sana kwake. (Waefeso 2:4-6) “Lakini Mungu, kwa kuwa ni mwingi wa rehema, kwa mapenzi yake makuu aliyotupenda; hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu; alituhuisha pamoja na Kristo; yaani, tumeokolewa kwa neema. Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu.”

Sisi tumekuwa wateule wa Mungu kutokana na ahadi na uapo aliouweka Mungu juu yetu. Mungu aliahidi kututumia mzao halisi ambaye ni Yesu Kristo ambaye angehakikisha tunashinda dhidi ya njama za adui za kutaka tusiwe mzao mteule wala tusiwe taifa takatifu. (Mwanzo 3:15) “Nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino.” Hapa anatabiriwa mzao mteule aliyesheni sifa za kuwa Mzao mteule yaani Kristo atakayetusaidia kushinda dhambi. 

Hata Ibrahimu alipohidiwa kuwa jamaa yake itakuwa taifa kubwa lililobarikiwa ahadi hiyo ilijengwa juu ya ahadi ile ya mwanzo iliyotolewa Edeni. (Mwanzo 12:1-3) “BWANA akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesh, nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka; nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa.”

Kusudi la Mungu lilikuwa kubariki mataifa yote ya dunia kupitia taifa la Israeli lakini kwa bahati mbaya Waisraeli wakajiona kuwa bora kuliko mataifa mengine. (Matendo 13:46) “Paulo na Barnaba wakanena kwa ushujaa wakasema, Ilikuwa lazima neno la Mungu linenwe kwenu kwanza; lakini kwa kuwa mnalisukumia mbali, na kujiona nafsi zenu kuwa hamkustahili uzima wa milele, angalieni, twawageukia Mataifa.”

Katika mazingira hayo Mungu akifanyika mwanadamu akaja kwa njia ya Yesu Kristo kutimiza ahadi ya Mungu aliyoitoa Edeni na kwa Ibrahimu. (Wagalatia 3:16) “Basi ahadi zilinenwa kwa Ibrahimu na kwa mzao wake. Hasemi, Kwa wazao, kana kwamba ni wengi, bali kana kwamba ni mmoja, Kwa mzao wako, yaani, Kristo.” Yesu alitwaa mwili wa dhambi ili avunje nguvu za dhambi iliyokuwa imetamalaki hata kutufanya mateka wa dhambi. Mwili wa dhambi akaufisha pale msalabani na alipofufuka tukafufuka naye na alipoketi kwenye kiti cha enzi akatuketisha pamoja naye. (Waefeso 2:6) “Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu.”

Kupitia maisha, mauti, na ufufuo wake Kristo, pakapatikana mzao mteule haisi ambapo kila amwaminiye hupokea hali hiyo hiyo ya kufanyika mtoto mpya wa Mungu na kuwa mzao mteule. (Yohana 1:12) “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake.” Kufayika kuwa watoto wa Mungu ni kufanyika kuwa mzao mteule, taifa takatifu na watu wa milki yake Mungu. Ni kufanyika kuwa wazaliwa wa kwanza na warithi wa ufalme. (Waebrania 12:22-23) “Bali ninyi mmeufikilia mlima Sayuni, na mji wa Mungu aliye hai, Yerusalemu wa mbinguni, na majeshi ya malaika elfu nyingi, mkutano mkuu na kanisa la wazaliwa wa kwanza walioandikwa mbinguni, na Mungu mwamuzi wa watu wote, na roho za watu wenye haki waliokamilika.”

Hadhi ya mzao mteule inampa anayeipokea uwezekano wa kutoishi maisha ya dhambi kwa kuwa mzao mteule halisi anakaa ndani yake. (1 Yohana 3:9) “Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu.” Hali hii ya kuachana na dhambi haitokei kufumba na kufumbua ingawa lingekuwa jambo jema kama ingekuwa hivyo.

Kutokana na kiwango cha ushirikiano kinachotolewa, Roho Mtakatifu aliyepewa dhamana ya kutubadilisha, aweza kudumu kwa muda mrefu au mfupi na muumini akibadilishwa kutoka utukufu hadi utukufu. (2 Wakorintho 3:18). “Lakini sisi sote, kwa uso usiotiwa utaji, tukiurudisha utukufu wa Bwana, kama vile katika kioo, tunabadilishwa tufanane na mfano uo huo, toka utukufu hata utukufu, kama vile kwa utukufu utokao kwa Bwana, aliye Roho.” Mchakato huu utakamilishwa pale tutakapofikia kimo cha Kristo kwa msaada wa Roho Mtakatifu na kuiwakilisha kikamilifu tabia ya Mungu hapa duniani. (Waefeso 4:13) “Hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo.”

Yesu ndiye mzao mteule halisi. Yeye ndiye aliyeahidiwa pale Edeni wakati Mungu akifunua kwa wanadamu nia yake ya kuwasaidia katika vita yao dhidi ya dhambi na dhidi ya Shetani. (Mwanzo 3:15) “Nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino.” Yeye ndiye mwanadamu pekee aliyewahi kuishi duniani akaishinda dhambi na kumshinda Shetani na hila zake zote. (1 Petro 2:22) “Yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana kinywani mwake. Yeye alipotukanwa, hakurudisha matukano; alipoteswa, hakuogofya; bali alijikabidhi kwake yeye ahukumuye kwa haki. Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa kupigwa kwake mliponywa.” (Yohana 14:30) “Mimi sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu.”

Na kwa sababu hiyo uteule wetu unaandama na sifa ya kuwa watawala watakaotawala pamoja na Yesu milele zote tukishiriki majukumu ya ukuhani. (1 Petro 2:9) “Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu.”