Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

ZEPHANIA BINA

 

Sefania Bina, (1919 – 1987)

Zephaniah Bina alikuwa mwalimu wa Kiadventista, mchungaji, shujaa wa maombi, na msimamizi nchini Tanzania.

Maisha ya Awali na Elimu

Zephaniah Bina alizaliwa mwaka 1919 huko Kibumaye, Wilaya ya Tarime, katika mkoa wa Mara uliopo karibu na Ziwa Victoria nchini Tanzania. Kabla ya kuwa Muadventista, Bina alifuata dini ya mapokeo ya Kiafrika, na baadaye Ukatoliki wa Kirumi. Akawa Muadventista mwaka wa 1934.

Mnamo 1933, akiwa na umri wa miaka 14, alipokuwa akihudhuria parokia ya Kikatoliki ya Isbania, Bina alimwomba babu yake ruhusa ya kuhudhuria shule. Babu yake alikataa na kumwambia ikiwa ataacha kuchunga ng'ombe ili aende shule hatapewa mahari ya kuoa. Bina alichagua kujitoa mhanga kwa kuacha kuchunga ng’ombe wa babu yake na hivyo kukosa mahari ili ajiunge na shule. Alienda shule ya wamishonari ya Kikatoliki, iliyokuwa karibu na Isbania. Siku moja baada ya kujifunza kusoma na kuandika, alimwomba baba mmoja Mkatoliki amruhusu asome Biblia. Baba alimpiga kofi kwa namna ambayo hakuwahi kuisahau maisha yake yote. Kutokana na kipigo hicho, aliamua kuacha shule.

Bina alimuona kaka yake Samson Chacha Mwita akiwa na kitabu cheusi alipokuwa akitoka shuleni. Hiyo ikamhamasisha kutamani kusoma, na hatimaye akakusudia kwenda shule moja huko Kibumaye. Mnamo mwaka wa 1935, Bina alijiunga na Shule ya Msingi ya Kisu Seventh-day Adventist Upper Primary School na hatimaye kufuzu kama mwalimu, kwenye miaka ya 1942. Kwa sababu ya umbali mrefu kati ya shule na nyumbani, kaka yake hakumruhusu kuwa anakwenda likizo nyumbani hadi alipomaliza shule. Nyakati za likizo akiwa shuleni, alifanya kazi ya misheni ili kujipatia ada ya masomo yake.

Mafunzo ya Kichungaji na Ndoa

Mnamo 1946, Bina alimuoa Bathsheba Bhoke Sabai katika sherehe iliyosimamiwa na Mchungaji Paulo Kilonzo. Baadaye walibahatika kuwa na watoto saba, binti wanne na watoto wa kiume watatu. Kwa kufuata umri, watoto hao ni Joyce Robhi, Elizabeth Nyakorema, Tabitha Nyanswi, Joseph Mwita, Steven Magesa, Lucas Mogonche na Weirungu Eliada. Kuanzia mapema 1959 hadi 1960, Bina alisoma kozi ya uchungaji katika Chuo cha Waadventista cha Bugema. Mnamo 1962, alijisajili kwa kozi ya mwaka mmoja ya afya ya umma katika Chuo cha Heri Hospital.

Uchungaji

Bina aliajiriwa kama mwinjilisti mwalimu mara baada ya kuhitimu masomo yake. Katika miaka ya mapema ya kuajiriwa kwake, yaani 1946 hadi 1950 – mara tu baada ya Vita ya Pili ya Dunia – nchi ilikuwa bado maskini na ambayo haijastaarabika sana; katika baadhi ya maeneo ilikuwa ni kawaida kwa watu kutembea uchi. Mnamo 1947, mara baada ya ndoa yake, Bina alihamishiwa mahali paitwapo Bukenye, kuchukua nafasi ya mtu mwingine ambaye alikataa nafasi hiyo. Mke wa Bina pia hakufurahishwa na kazi hii, lakini baada ya majadiliano na kushauriwa, alikubali kuhama. Huko Bukenye, juhudi za Bina zilichangia kuongezeka kwa waumini, kujengwa vizuri kwa shule, na mahusiano bora ya jamii.

Mnamo 1950 – 1951, Bina alihamishiwa shule ya Minigo Shirati, ambapo kwa mara nyingine, yule aliyeombwa kuhamia huko kwanza alikataa kwa sababu hofu ya kupata malaria ilikuwa kubwa na hospitali ilikuwa mbali. Kule Minigo Shirati, Bina alipendwa sana na watu, akapata sifa ya kuwa mtu wa mfano, mcha Mungu aliyeishi imani yake kwa matendo.

Kufikia 1955, Bina alikuwa akifundisha shule ya sekondari katika Shule ya Ualimu ya Ikizu huko Musoma ambako alikaa hadi mnamo 1958. Kufikia 1963, alikuwa mchungaji katika Fildi ya Ziwa Mashariki. Kuanzia 1964 hadi 1967, alikuwa katibu wa uchapishaji, huduma ya televisheni na redio, na huduma ya vijana ya fildi. Bina alikua mchungaji katika Fildi ya Nyanza Mashariki mnamo 1968. Mnamo 1969, alikuwa Mwenyekiti wa Fildi ya Nyanza Mashariki. Kufikia 1975, alikuwa amechaguliwa na Fildi ya Nyanza ya Kati. Bina akawa Mwenyekiti wa Tanzania General Field mwaka 1977 na Central Tanzania Field mwaka 1983, ambako alihudumu hadi alipostaafu mwaka 1985.

Kama Mwenyekiti wa Fildi, Bina alikuwa kiongozi wa kiroho aliyeamini katika uongozi wa kitumishi. Alikuwa mnyenyekevu na aliongoza kwa ushauri. Baraka Muganda anakumbuka kuwa alikabidhiwa kuendesha gari binafsi la Bina wakati wa kusafiri naye kote katika eneo lote la Fildi. “Sisi watu wa idara…tulimtazama, jinsi alivyokuwa akiongoza, na jinsi alivyozungumza na washiriki wa kanisa.” Alisema, William Daniel Tieng’o, aliyekuwa mfanyakazi kijana aliyemjua Bina, aliyemzungumzia kama kiongozi wa ajabu aliyependa alichokifanya. Bina aliamini pia katika uwazi, uwajibikaji, na kujitolea kwa kazi ya injili. Aliamini katika uongozi wa pamoja, kufanya maamuzi ya pamoja, na alikuwa mwaminifu sana kwa Kanisa. Nakumbuka alinipigia simu mara nyingi sana kwa maombi binafsi ofisini kwake. Hakuwahi kuwaongelea viongozi wenzake vibaya mbele yetu.” Alisema.

Bina aliwapenda vijana, wale waliofanya kazi chini yake hasa. Alikuwa akiwapa ushauri wa wazazi na wa kiroho kwa uhuru bila kukoma. Wafanyakazi wengi katika Union ya Tanzania waliokwenda nje ya nchi kwa masomo zaidi mwishoni mwa miaka ya 1970 na 1980 ni wale waliofanya kazi chini yake na kukubali ushauri wake. Bina alikuwa tayari kusaidia watu wote. Katika vituo vya misheni, yeye peke yake ndiye aliyekuwa na gari, lakini hakuna aliyenyimwa huduma ya gari hilo. Aliweza kuwafikisha wachungaji wageni kutoka stendi ya basi hadi kituo cha mkutano na baadaye kuwarudisha kwenye stendi ya basi. Alipenda kuhubiri kila Sabato, na mara chache alihudhuria ibada bila kuhubiri. Alipenda kazi ya uchungaji. Bina alikuwa makini na mwenye kipawa cha kutatua matatizo. Ni mara chache, kama ilitokea, mtu yeyote alimlaumu kwa kutendewa vibaya.

Maisha ya Baadaye na Mchango wake

Mapema mwaka wa 1985, afya mbaya ilimlazimu Bina kustaafu. Aligunduliwa na ugonjwa wa kisukari, ugonjwa ambao ulisababisha kifo chake. Baada ya kustaafu, Bina alipambana na ugonjwa huo kwa miaka miwili; hata hivyo, ugonjwa uliizidi tiba na kufariki mwaka 1987.

Sefania Bina alitambuliwa kwa mambo mawili: alitambuliwa kwanza kama shujaa wa maombi na pili alitambuliwa kama mshauri bora. Pia alikuwa na ufanisi katika kufundisha mazoezi ya afya bora. Sehemu ya urithi alioiachia jamii ni yale aliyoyafanya mkoani Mara. Alianzisha mafunzo ya afya kuhusiana na ukeketaji. Alipotoka Heri mnamo 1962 (baada ya kuhitimu kozi ya afya ya umma), watu wengi walikuwa hawana uelewa juu ya suala la usafi. Watu hawakuwa na vyoo, hawakuwa wanaoga, hawakuwa wakichemsha maji ya kunywa, na kadhalika. Bina alianza kuwaelimisha Waadventista Wasabato kuhusu umuhimu wa afya na watu wakabadilika.