MASWALI YA KUJADILI: 1 NYAKATI 1:1-54
- Historia ya ulikotoka hadi hapo ulipo ina umuhimu gani katika maisha? Iliwezekanaje kuweka kumbukumbu ya vizazi vya takribani miaka elfu mbili kuanzia Adamu hadi vizazi vya Ibrahimu? Muunganiko huu wa vizazi unakufundisha nini kuhusu jamii ya wanadamu na vinasaba vyao?
- Kushi ambayo ni Ethiopia ya zamani ilimzaa Nimrodi aliyekuwa Hodari wa kuwinda ulimwenguni. Uhodari wa Waafrika ulipotelea wapi hata wakatawaliwa na waarabu na wazungu? Mjukuu wa Nuhu aliyemlaani kwa sababu ya kucheka uchi wake alikuwa na vinasaba vya Kiafrika?
MASWALI YA KUJADILI: 1 NYAKATI 2:1-55
- Hapo awali historia inaonesha kuwa Waarabu (hasa Wamisri) waliwahi kuwa watumwa wa jamii za Waisraeli, ilikuwaje baadaye waarabu hao hao wakawafanya Waafrika kuwa watumwa wao? Kwa nini katika kutaja wazaliwa wa Watoto wa Yakobo hakuanzia kwa Reubeni mtoto wa kwanza na badala yake akaanzia kwa Yuda?
MASWALI YA KUJADILI: 1 NYAKATI 3:1-24
- Daudi alikuwa na Watoto wengi kutokana na kuoa wake wengi. Unadhani alifaa kuongoza taifa la Mungu la Israeli? Migogoro ya vita na mwanae Absalomu na kitendo cha Tamari binti yake kuingiliwa kinguvu na kaka yake Amnoni kinadhihirisha jinsi alivyoshindwa kuonyesha mfano mzuri wa maadili katika familia yake? Unajifunza nini kwa Daudi mtu ambaye Mungu alisema anaupendeza moyo wake? (1 Samweli 13:14).
MASWALI YA KUJADILI: 1 NYAKATI 4:1-43
- Yabesi alimlingana Mungu wa Israeli hata alipomwomba haja zake zilijibiwa. Kumlingana Mungu ni kitu cha namna gani? Leo hii unatakiwa ufanye nini ili haja zako zijibiwe na Mungu?
- Watu wa zamani walikuwa wahamaji wakitafuta mazingira mazuri ya malisho ya mifugo na kilimo. Kwa nini kizazi cha leo hakiendelezi hali hiyo badala yake wanajikusanya kwenye miji isiyo na nafasi ya kutosha hali kuna mapori mengi yenye rutuba huko mikoani? Je, ni waoga wa kuanzisha miji yao wenyewe?
MASWALI YA KUJADILI: 1 NYAKATI 5:1-26
- Kwa nini Reubeni alipoteza haki ya uzaliwa wa kwanza? Kwa nini haki hiyo ilienda kwa Yusufu aliye mdogo sana? Wanadamu watakaokombolewa watatambuliwa kama wazaliwa wa kwanza wa familia ya Mungu. Kwa nini sisi tunaodhaniwa tuliumbwa mwisho na tuliowahi kutenda dhambi tupewe hadhi ya wazaliwa wa kwanza? (Waebrania 12:22-23).
- Kwa nini inatajwa kuwa Yuda alishinda miongoni mwa ndugu zake? (Mwanzo 44:18-34). Kwa nini Yuda alipewa hadhi ya kutoa wafalme na Watawala wa Israeli wakati ambao Yuda alitembea na kuzaa na mkwe wake? (Mwanzo 38:11-30). Kufanya uasherati ni miungu ya kipagani kunafanyikaje? Je ni kushiriki ibada za uongo? (Ufunuo 17:2).
MASWALI YA KUJADILI: 1 NYAKATI 6:1-81
- Musa alitokana na ukoo wa Lawi ambao jukumu lao katika taifa la Israeli lilikuwa ukuhani. Ilikuwaje Musa akapewa kuongoza taifa la Israeli katika safari yake ya kutoka Misri Kwenda Kanani wakati jukumu la uongozi na utawala lilikuwa la kabila la Yuda? Kazi ya kuchagua watu watakaoimba kwenye ibada ya hekaluni ilifanywa na mfalme Daudi. Hii inakuambia nini juu ya umakini katika kuchagua na kupitisha waimbaji wa kwaya makanisani?
MASWALI YA KUJADILI: 1 NYAKATI 7:1-40
- Wana wa Isakari wanasifiwa kuwa walikuwa “watu wenye akili za kujua nyakati, kuyajua yawapasayo Israeli wayatende.” (1 Nyakati 12:32). Unadhani sifa hii ina umuhimu wowote kwa watu wa Mungu leo? Kujua nyakati maana yake ni nini?
MASWALI YA KUJADILI: 1 NYAKATI 8:1-40
- Mfalme Sauli alitoka kwenye ukoo wa Benjamini na siyo kwenye ukoo wa Yuda ambao ulikuwa katika utaratibu wa kutoa wafalme. Unadhani hiyo pia ndiyo sababu ya Sauli kufanya vibaya katika muhula wake wa uongozi? Je uongozi unatokana na vinasaba au ni jambo ambalo mtu yeyote anaweza kulifanya?
MASWALI YA KUJADILI: 1 NYAKATI 9:1-44
- Je tunao utaratibu wa kuandika historia ya uanzishwaji wa kazi ya injili katika maeneo yetu? Wanaoijua historia hiyo wanaonwa ili kupata kumbukumbu ya matukio ya nyuma kabla ya kufariki kwao? Je unao uwezo wa kuelezea vinasaba vya familia yako vizazi kadhaa vya huko nyuma? Je, jambo hilo bado lina umuhimu hata katika kizazi cha leo?
- Walinzi, mabawabu, na wafanya usafi hekaluni wote walitoka kabila la Lawi nao walichaguliwa na mfalme. Unauonaje utaratibu huo ukilinganisha na utaratibu wa sasa ambapo watu huchaguliwa kwa sifa zao bila kuzingatia koo zao na huchaguliwa na kibaraza cha uchaguzi?
MASWALI YA KUJADILI: 1 NYAKATI 10:1-14
- Sauli alikufa kifo cha kishujaa au kifo cha kizembe? Askari wamefundishwa kutii na kutekeleza maagizo wanayopewa na wakuu wao bila kuhoji wala kusita. Kwa nini mlinzi wa mfalme Sauli alikataa kutekeleza agizo la kumuua Sauli alilopewa na Sauli? Je kuna haja ya kupima maagizo unayopewa ili kuona kama yanafaa kutekelezwa? Je, alifanya vizuri naye kujiua?
- Mashujaa wa Yabeshi-gileadi waliokuja kufuata mabaki (mifupa) ya miili ya Sauli na wanawe walistahili kuitwa mashujaa? Je, kitendo cha Wafilisti kupeleka kichwa cha Sauli na silaha zake kwenye masanamu yao kiliashiria ushindi wa miungu yao dhidi ya Mungu wa Israeli?
- Kosa kubwa lililosababisha kifo cha Sauli ni nini? Je, ni halali kwa viongozi wa nchi, na viongozi wa kiroho kwenda kwa wenye pepo wa utambuzi na waganga wa kienyeji ili kutafuta msaada wa kuendelea kuwapo madarakani? Mungu aliruhusu Wafilisti kuwashambulia Waisraeli na kuwashinda vitani. Kwa nini Mungu aliruhusu jambo hili kutokea?
- Wakati Waisraeli wakimshambulia mfalme wa Israeli, Manabii na Kuhani Mkuu walisaidia nini kuliepushia taifa la Mungu aibu hii? Je unadhani mfalme Sauli alikuwa mtu wa kushaurika?Je kiongozi akipotoka kuna uwezekano wa anaowaongoza kupotoka na kupotea? Kwa nini mtumishi wa mfalme alipoona mfalme amejiua naye akaamua kujiua?
- Je kujiua ni kosa mbele ya Mungu hata pale unapoona hali iliyo mbele yako ni ngumu kuikabili? Je anayejiua anafanya dhambi isiyosameheka kwa Mungu? Je aliyejiua anastahili mazishi yanayowastahili waliokufa kifo cha kawaida?Je Sauli na wanawe walikufa kama mashujaa au walikufa kifo cha kujitakia? Je kupeleka kichwa cha Sauli hadi kwa miungu yao kulikofanywa na Wafilisti kulikusudia kutambua uwezo wa miungu hiyo katika vita waliyoshinda?
- Je kila tunapoanguka dhambini tunathibitisha na kutambua uwezo wa Shetani juu yetu? Je tunaposhinda vishawishi na mitego ya dhambi tunamrudishia Mungu sifa na shukrani? Je katika vita yetu dhidi ya dhambi na dhidi ya Shetani kuna tumaini la kupata ushindi? Sauli alishindwa kwa sababu alielemewa na nguvu za Shetani au kwa kuwa alitumaini kumshinda Shetani kwa nguvu zake bila kumtegemea Mungu?
- Je Sauli na wanawe walikufa kama mashujaa au walikufa kifo cha kujitakia na cha kizembe? Je kupeleka kichwa cha Sauli na silaha zake hadi kwa miungu yao kulikofanywa na Wafilisti kulikusudia kutambua uwezo wa miungu hiyo katika vita waliyoshinda? Je kila tunapoanguka dhambini tunathibitisha na kutambua uwezo wa Shetani juu yetu?
- Kwa nini hapakuwepo watu waliokumbuka kutwaa miili ya Sauli na wanawe ili izikwe kwa heshima na badala yake kuruhusu waidhihaki miili hiyo kwa kuifanyia ibada za kipagani? Kwa nini ilimchukua Mungu muda mrefu tangu kumtawaza Daudi kuwa mfalme na kumuingiza madarakani (Ikulu)?
- Je Sauli ndiye aliyekuwa kikwazo au ni kwa kuwa wakati wa Mungu ulikuwa haujafika? Tunawasaidiaje wenye migogoro ya kiroho na Mungu kama alivyokuwa Sauli migogoro inayoweza pelekea msongo na kutamani kujiua? Je ni nini dawa ya msongo wa mawazo?
MASWALI YA KUJADILI: 1 NYAKATI 11:1-47
- Daudi alitiwa mafuta na Samweli ili awe mfalme wa Israeli wakati Sauli akiwa anatawala (1 Samweli 16:1-13). Inakuwaje Daudi anatiwa mafuta tena ya kutawazwa kuwa mfalme? (1 Nyakati 11:3). Daudi alikuwa na ushawishi mkubwa kwa watu hata wakati alipokuwa hana nafasi ya ufalme. Hii huashiria kuwa mtu aliyeitwa kwa nafasi ya uongozi huonekana hata kabla ya kuchaguliwa kwake?
- Je, inawezekana kuwaongoza watu ukiwa hauna nafasi yoyote ya kuchaguliwa? Ikiwa una ushawishi mkubwa kuliko aliye madarakani unafanyaje ili hali hiyo isilete chuki kwa kiongozi wako? Ili uendelee kuwa mkuu unahitaji Mungu aendelee kuwa upande wako. Unadhani nini humzuia Mungu asiendelee kuwa na viongozi wake mara wanapoanza kutekeleza majukumu yao?
- Mafanikio ya uongozi hutegemea wanavyothamini na kudumisha moyo wa kufanya kazi kama timu. Unaiona hali hiyo katika utawala wa Daudi? Je, kutambua mchango wa wasaidizi wako huwaongezea ari ya kukuunga mkono na kufanya kazi kwa ufanisi zaidi? Je, mnao utaratibu katika kanisa lenu wa kutambua watu waliojitoa zaidi kwa mali na hali hata kukaribia kuhatarisha maisha yao kwa kazi ya Mungu?
- Je, kufanya hivyo hakuwezi kuwavunja moyo wale wasiotambuliwa? Je zoezi hilo linahitaji tahadhari ili lisiwafanye waliopongezwa kuvimba vichwa na wasiotambuliwa kuvunjika mioyo? Mashujaa watatu waliomletea Daudi maji kutoka ngome ya adui walifanya hivyo kwa kujipendekeza kama wafanyavyo machawa leo au walikuwa na nia ya dhati ya kumhudumia kiongozi wao bila kutarajia ujira?
- Nidhamu ya namna hiyo unaishuhudia kanisani kwako? Umepanga kufanya nini kwa watu waliotumika kwa dhati mwaka huu unaoisha kanisani kwako? Je, Uria Mhiti alistahili kuwamo kwenye orodha ya mashujaa wa Israeli? Unadhani Daudi alijihisi vipi alipokuwa anamuorodhesha Uria kama shujaa wakati akijua aliamrisha kuuawa kwake kwa hila? Unadhani Daudi alijutia dhambi hiyo?
MASWALI YA KUJADILI: 1 NYAKATI 12:1-40
- Rafiki wa kweli ni wale wakukimbiliao katika dhiki na kukusaidia. Kwa nini ni rahisi kuwasahau watu wa namna hiyo unapofikia mafanikio? Je, ilikuwa rahisi kwa Daudi kuwasahau waliomsaidia alipokuwa akiandamwa na adui wa ndani na nje ya nchi? Daudi alisema, "kama mmekuja kunisaliti Mungu alitazame neno hili na kulikemea." Kauli hii inaonesha Daudi ni mwenye kupenda ugomvi au kisasi?
- Je, kuna uwezekano watu wanaoonesha kukusaidia wakawa wanafanya hivyo wakikusudia kukusaliti? Hii inakueleza nini kuhusu tabia ya wanadamu? Abishai, mkuu wa wale thelathini aliwahi kumwambia Daudi, "Akusaidiaye ndiye Mungu wako." Je usemi huu una ukweli wa kiasi gani? Kwa nini aseme ndiyo Mungu wako na asiseme ndiyo ndugu yako?
- Wana wa Isakari walikuwa watu wenye akili za kujua nyakati, na kuyajua yawapasayo Israeli kutenda. Je karama hii ni ya muhimu katika kuliongoza kanisa la Mungu leo? Je, mtu aweza kumuomba Mungu ampatie karama hii? Kwa nini karama hii ikawa kwa wana wa Isakari peke yao?
- Wana wa Zabuloni walikuwa hodari wa kupanga vita na wenye zana za vita za kila namna. Inatokeaje watu wa kabila moja au kikundi kimoja kikawa na mwelekeo wa tabia unaofanana? Je, mgawanyiko wa idara za kanisani una mwelekeo huo? Je, kuna kikundi (idara) katika kanisa ambacho ni bora kuliko kingine?
- Je, ikitokea mkuu wa idara anaipigia debe idara yake kuwa ndiyo bora atakuwa anasema ukweli au anapotosha? Je, ipo haja ya kufanya sherehe ya vyakula na vinywaji siku ya kusimikwa uongozi wa kanisa? Je, tukio hilo linapaswa kushuhudiwa na waumini wote au si lazima lishuhudiwe na waumini?
MASWALI YA KUJADILI: 1 NYAKATI 13:1-14
- Kiongozi mwenye mafanikio hushauriana na wasaidizi wake kabla ya kutoa maagizo. Je, unadhani swala la kuleta Sanduku la Agano lilihitaji kushauriana? Kwa nini hata baada ya kushauriana, uletaji wa Sanduku ulileta maafa makubwa ya kifo cha Uza? Ni tahadhari gani ilihitaji kuchukuliwa ili kuepusha kifo hicho?
- Kuna umuhimu gani wa kuwapa watu unaowaongoza uhuru wa kupima mapendekezo unayowapa? Kuna shida gani ikiwa watu wamechagua kutoa uhuru huo kwa kiongozi wao na wao wakajibakishia wajibu wa kupokea maelekezo na kuyatekeleza? Utajuaje kama mashauri yanayotolewa na viongozi wako yametoka kwa Mungu?
- Je, kucheza kwa nguvu zote kwa nyimbo, na kwa vinubi, na kwa vinanda, na kwa matari, na kwa matoazi, na kwa tarumbeta, kulikofanywa na Daudi na Israeli yote kulifanywa kwa utukufu wa Mungu na kwa kuzingatia falsafa sahihi ya muziki wa kiroho?
- Je, kuonesha furaha kwa matendo makuu ambayo Mungu amekutendea kuna ubaya wowote? Uza alifanya kosa gani lililomkasirisha Mungu? Je, unadhani Daudi alielewa sababu ya Mungu kumwadhibu Uza?
- Je, kama Daudi angelitambua kukaa na Sanduku la Bwana ni mbaraka angeagiza likatunzwe kwa Obed-edomu Mgiti? Je kile kinachoweza kuwa laana kwa wengine chaweza kuwa mbaraka kwako?
NILICHOJIFUNZA NA KUGUNDUA: 1 NYAKATI 14:1-17
- Mungu anapomwinua mtu huibuka watu wanaomuunga mkono na kumtegemeza na wale wanaompiga vita.
MASWALI YA KUJADILI: 1 NYAKATI 15:1-17
- Pamoja na kuwa Daudi alikuwa kiongozi mkuu wa taifa la Israeli alijua kutofautisha majukumu yanayomhusu na yasiyomhusu. Aliwahimiza Walawi wachukue jukumu la kulibeba sanduku la Agano ambalo hawajapewa wengine. Unadhani leo kuna watu wanaojiona kuwa na wajibu wa kupanda vichwani mwa wazee wa kanisa na wachungaji wao?
- Je, watu wasiostahili wanapofanya majukumu ambayo Mungu hajawapangia Kundi zima laweza kufikwa na hasira ya Mungu na kupokea mapigo? Kitendo cha mfalme Daudi kucheza mbele ya sanduku la Agano kulikofanya mkewe Milka kumcheka kulikuwa sahihi machoni pa Mungu? Je, Daudi alifanya hivyo kwa kumheshimu Mungu? Je. wenzi wetu wa maisha wanaweza kutushawishi tusijishushe sana katika kutekeleza majukumu yetu ya kiroho?
MASWALI YA KUJADILI: 1 NYAKATI 16:1-17
- Je kuna uwezekano wa mtu kumtaka Mungu bila nguvu zake? Je kumtaka Mungu na nguvu zake kunafanyikaje? Uso wa Mungu unatafutwaje kila siku? Agano la milele alilolifanya kwa Ibrahimu na kulithibitisha kwa Yakob oni lipi? Je una ushuhuda wa namna ambavyo Mungu hajaacha watu wakuonee maishani mwako? Unaweza kutoa mifano inayothibitisha kuwa Mungu hakuacha watu wawaonee Israeli?
- Ni nini kinachofanya BWANA awe mkuu kuliko miungu mingine yote? Kwa nini wokovu unatakiwa kutangazwa siku kwa siku? Mada kuu katika kutangaza huo wokovu ni nini? Kuzikumbuka nyakati ulizokuwa huwezi kuhesabiwa kunasaidiaje kukupa matumaini ya kule unakoelekea?
MASWALI YA KUJADILI: 1 NYAKATI 17:1-17
- Kuna shida yoyote ikiwa hadhi ya nyumba za waumini inazidi hadhi ya nyumba ya Mungu kule wanakofanyia ibada? Kwa nini nyumba za ibada zina hadhi duni kuliko nyumba za waumini? Ikiwa mtu atafikiria kujenga peke yake nyumba ya ibada kwa nini waumini wenzake huweza kupinga hatua hiyo kwa madai mbalimbali?
- Je ni sahihi mtu kabla hajafikiria kujenga au kuboresha nyumba yake afikirie kujenga au kuboresha nyumba ya wazazi wake? Nathani alitoa wapi majibu aliyompa Daudi kuwa asonge mbele na mpango wa kumjengea Mungu nyumba wakati usiku uliofuata Mungu alimpa Nathani ujumbe kuwa Daudi asijenge hiyo nyumba kwa hajawahi kutoa hitaji hilo kwa viongozi wote waliotangulia?
- Je ni kweli Mungu hahitaji kujengewa nyumba yake na wanadamu? Je kuna wakati wa kukataa msaada kutoka kwa watu wanaotaka kumjengea Mungu nyumba? Kwa nini Mungu anaahidi kumjengea Daudi nyumba wakati Daudi ndiye aliyetangulia kuweka ombi la kumjengea Mungu?
- Ujenzi wa nyumba ya Mungu unaweza kukwama ukimsubiri mtu ambaye Mungu amepanga kumtumia kujenga? Je, ni kweli kuwa Mungu amewafanya Israeli kuwa watu wake milele? Kwa nini Daudi baada ya kukataliwa kumjengea Mungu nyumba anamsifu kwa matendo yake makuu badala ya kuonyesha kinyongo?
1 NYAKATI 18:1-17
- Je, Mungu anapompa mtu kushinda huyo mtu hutambua kuwa amesaidiwa au huwa hajui? Je kitendo ambaccho Daudi aliwafanyia farasi kwa kuwakata mshipakilikuwa ccha kikatili na kisichokubalika au kilikuwa ni halali kwa kuwa ni mbinu mojawapo ya kumshinda adui yako?
Watumwa wanawezaje kuleta zawadi kwa bwana wao wakati zawadi ni tendo la hiyari linalofanywa baada ya kuridhishwa na unayemzawadia?
1 NYAKATI 19:1-17
1 NYAKATI 20:1-17
1 NYAKATI 21:1-17
MASWALI YA KUJADILI: 1 NYAKATI 22:1-19
- Je, nyumba ya ibada ni lazima iwe nzuri mno, yenye sifa, na yenye fahari? Ujenzi wa nyumba ya ibada unahitaji kukusanya vifaa vyote vinavyohitajika kwa ujenzi? Je, mtu mmoja peke yake au familia yake au kikundi cha watu waweza kutoa gharama zote za ujenzi wa kanisa na kusimamia ukamilikaji wake?
- Je kuna wakati uongozi wa kanisa unapaswa kutambua uwezo wake mdogo katika kukamilisha miradu iliyoanzisha hivyo kuomba msaada kwa wenye uwezo huo hata kama siyo waumini? Mara kadhaa Daudi alimwaga damu katika vita alizopigana. Je, Mungu alikuwa akiridhia umwagikaji huo wa damu?
- Je, kuna uwezekano wa uongozi wa kanisa kutoa adhabu kwa namna ambayo Mungu hajaridhika nayo? Nini kufanyike kuepuka hali hiyo? Kuna wakati ujenzi wa Kanisa waweza kusimama kwa muda ili mtu maalum aliyeandaliwa na Mungu aje aukwamue?
- Je ujenzi na usimamizi wa ujenzi wa nyumba ya ibada ni karama ambayo wengine hawakujaliwa nayo? Je ipo haja ya kumbadilisha mtu ambaye amefanikiwa sana katika kusimamia ujenzi wa nyumba ya ibada? Je ni kipi sahihi ujenzi wa miradi ya kanisa ufanywe na makandarasi wenye ujuzi na kazi na wanaolipwa au ufanywe na waumini wote kwa njia ya kujitolea?
MASWALI YA KUJADILI: 1 NYAKATI 23:1-32
MASWALI YA KUJADILI: 1 NYAKATI 24:1-29
MASWALI YA KUJADILI: 1 NYAKATI 25:1-31
MASWALI YA KUJADILI: 1 NYAKATI 26:1-32
MASWALI YA KUJADILI: 1 NYAKATI 27:1-34
MASWALI YA KUJADILI: 1 NYAKATI 28:1-21
NILICHOGUNDUANA KUJIFUNZA: 1 NYAKATI 29:1-30
- Utambuzi kuwa Mungu peke yake amekuchagua kuongoza watu wake huleta faraja unapokutana na changamoto. Mungu ana uwezo wa kumchagua hata aliye mwororo kwenye nafasi kubwa ya uongozi. Kufanikiwa katika uongozi hakutegemei misuli. Wala ushindi wa kiroho hautegemei mabavu. Kama ingekuwa hivyo Samsoni asingetobolewa macho. Mungu anatujua tulivyo. Tukikubali kutumika naye atatupa nguvu za kushinda.
- Uongozi unaokumbukwa kwa muda mrefu ni ule unaofanya uwekezaji wa miundombinu kama wa Daudi na Sulemani. Mafanikio ya miradi kama hiyo ya kitaasisi inahitaji utengwaji wa mafungu ya fedha kabla ujenzi haujaanza ili kuepuka kukwama. Miradi ya Mungu inayokwama kwa kukosa fedha za kuiendeleza inaliabisha Jina la Mungu. Imani kwa Mungu kisiwe kisingizio cha kukosa mipango.
- Moyo wa kutoa na kujitoa kwa hiari huchochewa na mwamko wa viongozi wanaohamasisha kujitoa huko kwa sababu maneno yana ushawishi mdogo kuliko vitendo. Binadamu ana kawaida ya kufanya kitu anachokipenda na kukielewa hata kama kigumu. Kwa kiasi kikubwa maendeleo ya jamii nyingi yanategemea viongozi wanaoshawishi kuliko watawala wanaoamrisha.
- Siri ya mafanikio ya kweli ipo katika kutambua ukuu wa Mungu na asivyo na wa kufanana naye. Daudi licha ya kutukuzwa kwa mafanikio ya kipindi cha uongozi wake hakuwa mbinafsi bali alielekeza sifa hizo kwa Mungu anayezistahili. Kwa kawaida wanadamu wote hupokea sifa wasizostahili. Wanasifiwa kwa kile walichowezeshwa na Mungu. Mwenye kustahili sifa ni Mungu peke yake
- Daudi alitumia mali alizojikusanyia maishani kutegemeza kazi ya Mungu lakini hakufa maskini. Kutegemeza kazi ya Mungu ndiyo njia bora zaidi ya uwekezaji wa mali. Kufilisika hakuwahusu wanaotumia mali na Mungu. Wao wana uhakika wa kufa wenye umri mwema, wameshiba siku, wakiwa na mali na heshima.