Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

AMOSI

MASWALI YA KUJADILI: AMOSI 1:1-15

  1. Amosi aliyekuwa mchungaji wa mifugo alifaa kutumika kuchunga watu wa Mungu? Kuna ulinganifu gani kati ya kazi yake ya kwanza ya kuchunga wanyama na ile ya pili ya kuchunga watu? Kuchunga kunaenda sambamba na kutafuta malisho mazuri ya wanyama na kuwawekea ulinzi na maadui na wanyama hatari. unauona wajibu huo kwa kazi ya wachungaji wa watu? Je Mungu anaweza kukutumia kazini mwake hata kama watu wanakuona hufai?
  2. Manabii wa Yuda na Israeli kabla hawajachukuliwa utumwani na kusambaratishwa walitumwa kuwaonya watawala na raia wake. Unadhani nini kilifanya wasisikie ujumbe huo wa maonyo na kuangamia? Je ni rahisi kuuonya ulimwengu juu ya maangamizo yanayokuja ikiwa hautatubu? Nini kingepaswa kufanyika na manabii ili kuwaaminisha watu kuwa maoyo wanayotoa ni kweli yametoka kwa Mungu? Ni njia ipi kati ya ukali na upole inafikisha ujumbe vizuri?

MASWALI YA KUJADILI: AMOSI 2:1-16

  1. Wamoabu na Waamoni asili yao ni moja na hawakupaswa kuwa na uhasama mkubwa kiasi cha kuchomeana mabaki ya mifupa hata ikawa chokaa. (Mwanzo 19:30-38). Nini kifanyike ili kuondoa uhasama wa ndugu wa damu moja? Je Mungu anapendezwa ndugu wanapogombana?
  2. Mazoea haya ya mtu na baba yake kumwendea mwanamke mmoja hutokana na nini? Nani mwenye makosa kati ya hao watatu? Je. kuwaambia manabii wasifanye unabii hutokeaje? Je kuwapangia wahubiri cha kuhubiri ni sawa na kuwaambia manabii wasifanye unabii?

MASWALI YA KUJADILI: AMOSI 3:1-14

  1. Ni vigumu watu wawili kutembea pamoja hali ya kuwa hawajapatana. Unadhani Israeli na Mungu walikuwa wamepatana? Nikitambua ninayetembea naye hatupatani, nimuache na kuchagua mwingine au niangalie namna ya kuondoa hizo tofauti?
  2. Mungu hatafanya jambo bila kutujulisha kupitia kwa manabii wake. Je Mungu alishawahi kututahadharisha juu ya fundisho la utatu au kuwepo kwa idara ya wanawake? Kwa nini watu wanatumia nguvu nyingi juu ya jambo ambalo Mungu hakuwahi kulisemea?

MASWALI YA KUJADILI: AMOSI 4:1-14

  1. Kwa nini baada ya kukutwa na majanga mfululizo Israeli hawakujihoji na kumrudia Mungu? Je baadhi ya majanga yanayotukuta yanaweza kuwa yamechangiwa na matendo yetu na mahusiano yetu mabaya na Mungu?
  2. Ni nini kinachokuja akilini mwako Mungu anaposema jiandae kukutana naye? Unadhani unapaswa kujiandaaje unapoenda kukutana na Mungu? Unadhani Mungu anapanga kumtenda nini Israeli?
  3. Je, ni busara kufanya toba kabla ya kuanza msimu wa kilimo ili Mungu asije akazuia mvua kwa sababu ya maovu yetu? Je kuomba kwa ajili ya nchi kwaweza kuiponya nchi hiyo?

MASWALI YA KUJADILI: AMOSI 5:1-15

  1. Mungu anasema nitafuteni mimi nanyi mtaishi. Je inawezekana kuishi bila kutegemea msaada wa Mungu? Ni mambo gani ambayo ukiyafanya yanaonesha kuwa unamtafuta Mungu? Kwa nini ni busara kunyamaza katika wakati mbaya? Kwa nini ni rahisi kutafuta mabaya ya mtu kuliko kutafuta mema yake?
  2. Kwa nini hatupaswi kutamani wakati uliotabiriwa kwenye unabii uje? Unajifunza nini kwa wale ambao muda wote wanazungumzia mateso ya watu wa Mungu yanayoandaliwa na mtesi wao yaani Mpinga Kristo badala ya kumzungumzia Mkombozi wao? (Ufunuo 13:15; Danieli 12:1)
  3. Kwa nini Mungu anachukizwa na sikukuu zetu na mikutano yetu ya dini? Je Mungu hataki tuwe na sikukuu au hataki tuwe na mikusanyiko ya kidini? Je kinanda kina uwezo wa kutoa sauti isiyompendeza Mungu? (Amosi 5:23). Tutafanyaje ili kuhakikisha kinanda hakitoi mlio isiyompendeza Mungu? Je kuna uwezekano wa kukosa kwenda mbinguni kwa sababu ya matumizi mabaya ya kinanda?

MASWALI YA KUJADILI: AMOSI 6:1-14

  1. Kula wana-kondoo wa kundi, na ndama waliomo zizini kunamaanisha nini kwa viongozi wa kiroho wa leo? Sauti za upuuzi na sauti za vinanda zvinavyomkera Mungu ni zipi? Je, ala za muziki zaweza kuwa laana badala ya kufanyika baraka? Je kuna haja ya kuwa na mwongozo wa matumizi sahihi wa ala za muziki?

MASWALI YA KUJADILI: AMOSI 7:1-17

  1. Yakobo atasimamaje kwa maana ni mdogo? Umewahi kumuombea mtu ambaye umejiridhisha kuwa anaadhibiwa na Mungu kwa makosa yake? Unadhani maombezi kama hayo yana nafasi katika wakati wetu?
  2. Kubaki mwaminifu katika wakati ambao watawala wameanguka na kuyaacha maadili ni jambo linaloweza kugharimu uhai. Ni namna gani mtu afanye ili kujipunguzia maadui anapoifanya kazi ya Mungu au anapokuwa mzalendo kwa nchi yake? Je ni rahisi kumchukulia Amosi kuwa ni jeuri kwa viongozi wake?

MASWALI YA KUJADILI: AMOSI 8:1-14

  1. Mungu analalamikia maisha ya wanadamu yaliyojaa unafiki hata katika mambo nyeti ya ibada. Ni kwa kiasi gani unamaanisha kile unachokisema na unachokifanya? Kungekuwa na matokeo gani mazuri kama vile unavyotaka watu wakutambue ungekuwa ndivyo ulivyo hasa? Njaa ya Neno la Mungu iliyotabiriwa na Amosi imeshatokea duniani?
  2. Je unadhani kasi ya kutafuta Neno la Mungu inaendana na kasi ya kutafuta mafanikio ya muda ya maisha haya? Kwa nini Mungu asababishe njaa ya kukosa Neno lake? Je, hataki watu waokolewe? Kwa nini kusikia Neno la Mungu kuwekewe ukomo? Nini kitawafanya watu walitafute Neno la Mungu katika wakati huo wa mwisho?
  3. Je kudanganya watu kwa mizani ya udanganyifu kunakofanywa na baadhi ya wafanyabiashara kumeweza kuwatajirisha? Kama takataka za ngano zaweza kuuzwa na kujipatia kipato takataka gani zingine zaweza kuwa chanzo cha mapato? Kwa nini nyimbo za hekaluni zitageuzwa kilio siku ya hasira ya Mungu? Nchi kutiwa giza wakati wa nuru ya mchana maana yake nini?

MASWALI YA KUJADILI: AMOSI 9:1-15

  1. Kwa nini Mungu hataiangamiza Israeli kabisa licha ya maovu yake kukithiri? Kwa nini Mungu anawaona wana wa Waisraeli kama wana wa Kushi kwake? Mungu anakusudia kuipepeta Israeli ili kutenga ngano safi na makapi. Kwa nini katika upepetaji huo hakuna hata chembe moja iliyo ndogo haitaanguka chini?