Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

WARUMI 9

UCHAMBUZI WA KITABU CHA WARUMI

SURA YA TISA

Kitabu cha Warumi sura ya tisa kinafafanua kwa nini wokovu umekuwa wa wote (hata wale wasio na agano na Mungu) na kwa nini Waisraeli licha ya kuwa kwenye agano na Mungu wameonekana kuachwa nyuma kwenye mpango wa wokovu. Yesu anatambulisha kuwa wokovu watoka kwa Wayahudi. (Yohana 4:22) “Ninyi mnaabudu msichokijua; sisi tunaabudu tukijuacho; kwa kuwa wokovu watoka kwa Wayahudi.” Watoka watoka kwa Wayahudi kwa kuwa wao ndiyo waliopewa wasia na maelekezo juu ya utaratibu wa kuufikia wokovu. (Warumi 3:1-2) “Basi Myahudi ana ziada gani? Na kutahiriwa kwafaa nini? Kwafaa sana kwa kila njia. Kwanza kwa kuwa wamekabidhiwa mausia ya Mungu.”

Ibrahimu aliye baba wa taifa la Israeli alikuwa wa kwanza kuahidiwa wokovu. (Mwanzo 12:1-3) “Bwana akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha; nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka; nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa.” Ibrahimu aliahidiwa kutendewa hayo si kwa kuwa alitenda lolote la kumfanya astahili. Ibrahimu alimwamini Mungu na kuhesabiwa haki. (Yakobo 2:23) “Maandiko yale yakatimizwa yaliyonena, Ibrahimu alimwamini Mungu, ikahesabiwa kwake kuwa ni haki; naye aliitwa rafiki wa Mungu.”

Mungu alipanga kutumia kigezo hicho hicho kilichomstahilisha Ibrahimu kuhesabiwa haki kuwahesabia haki watu wa mataifa. (Wagalatia 3:8) “Na andiko, kwa vile lilivyoona tangu zamani kwamba Mungu atawahesabia haki Mataifa kwa imani, lilimhubiri Ibrahimu habari njema zamani, kusema, Katika wewe Mataifa yote watabarikiwa.” Kwa bahati mbaya Waisraeli walidhani mibaraka ya Mungu ilikuwa iwatoshe wao peke yao.

Mibaraka ya Mungu haijui kutindikiwa. Yenyewe huwa inajaa kusukwa sukwa na kumwagika. (Luka 6:38) “Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa.” Mungu ameahidi kutupatia utajiri wa kutosha. (1 Petro 1:3-4) “Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu; tupate na urithi usioharibika, usio na uchafu, usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu.”

Licha ya mibaraka hiyo ya utajiri Mungu anakusudia kutupatia au kuturithisha ufalme utakaodumu milele sisi tukiwa watawala. (1 Petro 2:9) “Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu.” Yesu anathibitisha ukweli wa sisi kuzawadiwa ufalme dhambi itakapokoma. (Mathayo 25:34) “Kisha Mfalme atawaambia wale walioko mkono wake wa kuume, Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu.” Ahadi hii inawahusu wote waliotahiriwa na wasiotahiriwa. Inawahusu walio chini ya sheria na walio chini ya neema.

Ukweli huu ulikuwa mchungu kwa Wayahudi kwa sababu wao walijihesabia kuwa ndiyo pekee wanaostahili kwa kuwa wanalo agano na Mungu. Paulo alikuwa na wakati mgumu kuwafunulia siri Wayahudi ya kuwa wamataifa ni wenzetu. (Waefeso 3:5-6) “Siri hiyo hawakujulishwa wanadamu katika vizazi vingine; kama walivyofunuliwa mitume wake watakatifu na manabii zamani hizi katika Roho; ya kwamba Mataifa ni warithi pamoja nasi wa urithi mmoja, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja nasi wa ahadi yake iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili.”

Paulo kwa mara nyingine tena anakiri kuwa Wayahudi walitoa Mwokozi wa ulimwengu kutoka katika taifa lao na ya kwamba Yesu ana vinasaba na jamii ya Kiyahudi. (Warumi 9:4-5) “Ambao ni Waisraeli, wenye kule kufanywa wana, na ule utukufu, na maagano, na kupewa torati, na ibada ya Mungu, na ahadi zake; ambao mababu ni wao, na katika hao alitoka Kristo kwa jinsi ya mwili. Ndiye aliye juu ya mambo yote, Mungu, mwenye kuhimidiwa milele. Amina.”

Ni ukweli kuwa kabla sisi wote hatujafanywa wana na wazaliwa wa kwanza Wayahudi ndiyo walioipokea hali hiyo kwanza. (Mwanzo 17:7) “Agano langu nitalifanya imara kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, na vizazi vyao, kuwa agano la milele, kwamba nitakuwa Mungu kwako na kwa uzao wako baada yako.” (Kutoka 4:22) “Nawe umwambie Farao, Bwana asema hivi, Israeli ni mwanangu mimi, mzaliwa wa kwanza wangu.” (1 Yohana 3:2) “Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo.”

Waisraeli au Wayahudi pia ndiyo waliotangulia kuingia kwenye maagano. (Kutoka 19:8) “Watu wote wakaitika pamoja wakisema, Hayo yote aliyoyasema Bwana tutayatenda. Naye Musa akamwambia Bwana maneno ya hao watu.” Agano hilo halikudumu kwa sababu badala ya kutegemea uwezo wa Mungu kulishika walilishika kwa kutumia juhudi zao. (Warumi 10:1-2) “Ndugu zangu, nitakayo sana moyoni mwangu, na dua yangu nimwombayo Mungu, ni kwa ajili yao, ili waokolewe. Kwa maana nawashuhudia kwamba wana juhudi kwa ajili ya Mungu, lakini si katika maarifa.” Hii ndiyo iliyokuwa tabia ya Paulo kabla hajakutana na injili ya Yesu. (Wafilipi 3:6) “Kwa habari ya juhudi, mwenye kuliudhi Kanisa, kwa habari ya haki ipatikanayo kwa sheria sikuwa na hatia.”

Wayahudi walijizima data wasitambue kuwa agano hilo la Sinai liliishia Kalvari. (Waebrania 8:9) “Halitakuwa kama agano lile nililoagana na baba zao, Katika siku ile nilipowashika mikono yao niwatoe katika nchi ya Misri. Kwa sababu hawakudumu katika agano langu, Mimi nami sikuwajali asema Bwana.” Wayahudi walipewa pia ibada. Wao ndiyo wameendelea kuidumisha ibada ya Sabato iliyotolewa na Mungu mwanzo wa uumbaji. Kama si Wayahudi leo tusingejua kuwa siku ya ibada iliyoasisiwa na Mungu ni Sabato ya siku ya saba ya juma yaani Jumamosi. Lakini yote hayo hayana tija kwa Paulo kama utambuzi kuwa wokovu unapatikana bure kwa watu wote. (Warumi 9:3) “Kwa maana ningeweza kuomba mimi mwenyewe niharimishwe na kutengwa na Kristo kwa ajili ya ndugu zangu, jamaa zangu kwa jinsi ya mwili.” Anawaona Wayahudi amba oni ndugu zake wa damu wakipotea kwa sababu ya kushindwa kuitambua neema ya Mungu.

Leo hii historia kama hii inaweza kujirudia hasa kwa kanisa langu. Waadventista wa Sabato wanakidhi vigezo vya kutambuliwa kama kanisa la Mungu la kweli liishilo siku za mwisho. (Ufunuo 14:12) “Hapa ndipo penye subira ya watakatifu, hao wazishikao amri za Mungu, na imani ya Yesu.” Lakini hatari inayowakabili haina tofauti na ile iliyokuwa ikiwakabili Wayahudi nyakati za Paulo. Wao wanaendelea kuzitunza Amri Kumi za Mungu kama walivyofanya Wayahudi ikiwepo na ibada ya Sabato ambayo karibu ulimwengu wote umeitupilia mbali.

Tofauti kubwa iliyopo kati ya Waadventista na Wayahudi ni kuwa Waadventista hawatunzi sheria na maagizo ya torati hasa yale yaliyokuwa kivuli cha mambo yajayo yaliyokomea pale msalabani. Na linguine kubwa ni kuwa Waadventista wana imani kama ile aliyokuwa nayo Yesu. Waadventista wanabatizwa kama Yesu alivyobatizwa. Hawali vyakula najisi kama ambavyo Yesu hakula na wanahesabiwa haki kwa imani kama Yesu alivyoelekeza. Hata hivyo wapo ambao kwa kujua au kwa kutojua wana nadharia kuwa wokovu haupatikani kwa neema peke yake bali juhudi ya mwanadamu inahitajika ili mtu ahesabiwe haki na kurithi uzima.

Hata kama watu kama hao watakuwapo hiyo itakuwa haikutokana na maelekezo ya kanisa hilo. Kanisa la Kikristo lilipitia wakati mgumu lilipokuwa linajadili vigezo vinavyopewa kipaumbele ili mtu atambulike kama ni muumini halali wa kanisa hilo. (Matendo 15:1-2) “Wakashuka watu waliotoka Uyahudi wakawafundisha wale ndugu ya kwamba, Msipotahiriwa kama desturi ya Musa hamwezi kuokoka. Basi baada ya Paulo na Barnaba kushindana na watu hawa na kuhojiana nao sana, ndugu wakaamuru kwamba Paulo na Barnaba na wengine miongoni mwao wapande kwenda Yerusalemu kwa mitume na wazee kwa habari ya swali hilo.”

Ili kujiunga na kanisa la Waadventista wa Sabato mtu anatakiwa kutoa ahadi kumi na tatu au ahadi tatu zilizofupishwa. Katika ahadi hizo msisitizo mkubwa umewekwa kwenye dhana ya kuhesabiwa haki kwa imani na kuokolewa kwa neema. Nitakutajia baadhi ya ahadi hizo ili kujionea ukweli huo. Ahadi ya pili kati ya zile 13 inasema, “Je, unakikubali kifo cha Yesu Kristo pale Kalvari kama dhabihu ya upatanisho kwa ajili ya dhambi zako, na unaamini kwamba, kwa neema ya Mungu, kwa kuiamini damu yake iliyomwagika, umeokolewa kutoka katika dhambi pamoja na adhabu yake?”

Ahadi hii inakiri kuwa kwa neema ya Mungu, kwa kuiamini damu ya Yesu iliyomwagika, mtu huokolewa kutoka katika dhambi pamoja na adhabu yake. Kimsingi ahadi hii inakubaliana na mafungu haya. (Warumi 8:1) “Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu.” (Yohana 5:24) “Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani.”

Ahadi ya tatu inasema, “Je, unamkubali Yesu Kristo kama Bwana wako na Mwokozi wako mahususi ukiamini kwamba, Mungu amekusamehe dhambi zako na kukupa moyo mpya katika Kristo, na unazikataa njia za dhambi za ulimwengu?” Ahadi hii inatambua kuwa mtu kabla hajampokea Yesu kwa njia ubatizo anakuwa amesamehewa dhambi zake na kupewa moyo mpya baada ya mwili wa dhambi kusulubishwa na Yesu pale msalabani. (Warumi 6:6) “Mkijua neno hili, ya kuwa utu wetu wa kale ulisulibishwa pamoja naye, ili mwili wa dhambi ubatilike, tusitumikie dhambi tena.”

Ahadi ya nne inasema, “Je, unaikubali kwa imani haki ya Kristo, ambaye ni Mwombezi wako katika patakatifu pa mbinguni, na unaikubali ahadi ya kukupatia neema ibadilishayo na uwezo wa kuishi maisha ya upendo yaliyojengwa katika Kristo nyumbani kwako na mbele za ulimwengu?” Ahadi hii inatambua kuwa tunahesabiwa haki kwa imani na Kristo ndiye anayetuhesabia haki na wala si matendo yetu. Tena ahadi hii inatambua kuwepo kwa neema ibadilishayo inayotuwezesha kuishi maisha ya ushindi na kwamba hali hiyo huletwa na Roho wa Mungu aishiye ndani yetu. (Wafilipi 2:13) “Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema.”

Ahadi ya sita inasema, “Je, unazikubali Amri Kumi kuwa ni andiko la tabia ya Mungu na, ufunuo wa mapenzi yake? Je, unakusudia kuishika sheria hii kwa uwezo wa Kristo aliye ndani yako, ikiwa ni pamoja na amri ya nne inayoagiza kuiadhimisha siku ya saba ya juma kama Sabato ya Bwana na kumbukumbu ya Uumbaji?” Ahadi hii inatambua umuhimu wa kushika sheria na Sabato baada ya kuokolewa na si kabla ya kuokolewa. Tena inatambua jinsi isivyowezekana kuishika sheria bila kusaidiwa na uwezo wa Kristo aliye ndani yetu. 

Ahadi hizo chache zinathibitisha kuwa kanisa la Waadventista linatambua kuwa tunaokolewa kwa neema na haitokani na matendo yetu mema. (Waefeso 2:8-9) “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu.” Kama kuna Mwaadventista atashindwa kuuelewa ukweli huu hiyo itakuwa haijatokana na fundisho la kanisa huenda itakuwa imetokana na uelewa mdogo.

Paulo anathibitisha kuwa upotofu wa Wayahudi haukutokana na kile Mungu alichowafunulia bali kutoongoka. (Warumi 9:6-8) “Si kana kwamba neno la Mungu limetanguka. Maana hawawi wote Waisraeli walio wa uzao wa Israeli. Si kana kwamba neno la Mungu limetanguka. Maana hawawi wote Waisraeli walio wa uzao wa Israeli. Wala hawawi wote wana kwa kuwa wazao wa Ibrahimu, bali, Katika Isaka wazao wako wataitwa; yaani, si watoto wa mwili walio watoto wa Mungu, bali watoto wa ile ahadi wanahesabiwa kuwa wazao.”

Kwa hiyo kama kuna Wakristo wanaotafuta kuhesabiwa haki kwa matendo hao wanaangukia katika fungu la Waisraeli wasio wa uzao wa Israeli. Hawa ni Waisraeli wa kimwili ambao siku zote huwasumbua watoto wa ahadi. (Wagalatia 4:22-23, 29) “Kwa maana imeandikwa ya kuwa, Ibrahimu alikuwa na wana wawili mmoja kwa mjakazi, na mmoja kwa mwungwana. Lakini yule wa mjakazi alizaliwa kwa mwili, yule wa mwungwana kwa ahadi. Lakini kama vile siku zile yule aliyezaliwa kwa mwili alivyomwudhi yule aliyezaliwa kwa Roho, ndivyo ilivyo na sasa.”

Siku zote kuna mpambano kati ya wale wanaotamani kuthihirisha namna wanavyostahili na walivyo na haki kuliko wengine. Kwao kuokolewa kwa neema kusikochangiwa na matendo hakuna mvuto maana hakutoi nafasi ya kufurahia na kujivunia matunda ya kazi zao. Hawa ni watu wa mwilini ambao hawakui. (1 Wakorintho 3:1-2) “Lakini, ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama na watu wenye tabia ya rohoni, bali kama na watu wenye tabia ya mwilini, kama na watoto wachanga katika Kristo. Naliwanywesha maziwa sikuwalisha chakula; kwa kuwa mlikuwa hamjakiweza. Naam, hata sasa hamkiwezi.”

Kuna uwezekano wa kuhama kutoka kuwa mtu wa mwilini na kuwa mtu wa rohoni kama Paulo alivyofanya. (Wafilipi 3:4-7) “Walakini mimi ningeweza kuutumainia mwili. Mtu ye yote akijiona kuwa anayo sababu ya kuutumainia mwili, mimi zaidi. Nalitahiriwa siku ya nane, ni mtu wa taifa la Israeli, wa kabila ya Benyamini, Mwebrania wa Waebrania, kwa habari ya kuishika torati, ni Farisayo, kwa habari ya juhudi, mwenye kuliudhi Kanisa, kwa habari ya haki ipatikanayo kwa sheria sikuwa na hatia. Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo.”

Mojawapo ya faida anayoipata mtu wa rohoni ni kupokea hadhi ya kuwa mwana. Hadhi hii huja kwa njia ya ahadi na si kwa njia ya matendo. (Warumi 9:8-9) “Yaani, si watoto wa mwili walio watoto wa Mungu, bali watoto wa ile ahadi wanahesabiwa kuwa wazao. Kwa maana neno la ahadi ni hili, Panapo wakati huu nitakuja, na Sara atakuwa na mwana.” Ili kuwa wana hapakutakiwa tendo lolote kwetu liwe jema au baya bali kulitegemea nia yake yeye anayetuchagua. (Warumi 9:10-11) “Wala si hivyo tu, lakini Rebeka naye, akiisha kuchukua mimba kwa mume mmoja, naye ni Isaka, baba yetu, (kwa maana kabla hawajazaliwa wale watoto, wala hawajatenda neno jema wala baya, ili lisimame kusudi la Mungu la kuchagua, si kwa sababu ya matendo, bali kwa sababu ya nia yake aitaye).”

Mpango wa Mungu wa kumuokoa mwanadamu ulitokana na wazo lake ambalo halikutoa nafasi ya kutushirikisha kwa sababu hakuhitaji mchango wowote kutoka kwetu. Mungu alituchagua kisha akatuahidi kutusaidia kufikia makusudi yake. Wengine wanataka kuamini kuwa mpango huu una ubia ambapo mwanadamu anaonyesha kujali kwake kwa kuchangia kitu kidogo ili Mungu amsaidie kukamilisha hiyo sehemu iliyobakia. Ikiwa hivi ndivyo basi mpango huu una ati ati ya kukamilika kama Mungu anavyokusudia. Vipi kama wanadamu wote wakishindwa kutimiza maeneo waliyoachiwa kuchangia matokeo ya mwisho yatakuwa vile Mungu alivyokuwa amekusudia? Na vipi ikiwa watakuwepo waliochangia kikamilifu maeneo waliyoachiwa kuchangia hawatajivuna na kuibua uasi mwingine?

Mpango wa Mungu wa wokovu haumtegemei anayeokolewa bali anayeokoa. (Warumi 9:15-17) “Maana amwambia Musa, Nitamrehemu yeye nimrehemuye, nitamhurumia yeye nimhurumiaye. Basi, kama ni hivyo, si katika uwezo wa yule atakaye, wala wa yule apigaye mbio; bali wa yule arehemuye, yaani, Mungu. Kwa maana maandiko yasema juu ya Farao, ya kwamba, Nilikusimamisha kwa kusudi hili, ili nionyeshe nguvu zangu kwako, jina langu likatangazwe katika nchi yote.” Mungu ndiye anayeruhusu kuwepo kwa mazingira ya ugumu na mazingira ya wepesi. Mungu kama amekusudia tushinde dhambi tutashinda tu hakuna la kumzuia. (Ayubu 4:18) “Tazama, yeye hawategemei watumishi wake; Na malaika zake huwahesabia upuzi.”

Kusudi la Mungu la kutuokoa ni lazima litimie. Yeye huwa hafanyi biashara kichaa. Watu pekee anaoweza kuwapoteza ni wale watakaokaidi hadi mwisho kuukubali mpango kama ulivyopangiliwa. (Warumi 9:19) “Basi, utaniambia, Mbona angali akilaumu? Kwa maana ni nani ashindanaye na kusudi lake?” Katika kuwaita wale aliowachagua aliwaita wote na katika hilo hastahili kulaumiwa au kupangiwa. Mungu anawafananisha wanadamu kama udongo wa mfinyanzi. Yupo karakana akiwa anawarekebisha ili wafikie kusudi lake. (Warumi 9:20-21) “La! Sivyo, Ee binadamu; wewe u nani umjibuye Mungu? Je! Kitu kilichoumbwa kimwambie yeye aliyekiumba, Kwani kuniumba hivi? Au mfinyanzi je! Hana amri juu ya udongo, kwa fungu moja la udongo kuumba chombo kimoja kiwe cha heshima, na kimoja kiwe hakina heshima?” Aliyewaumba Wayahudi ndiye huyo huyo aliyewaumba wamataifa.

Habari njema ni kwamba sisi sote tuliumbwa na Mungu ili kutimiza kusudi lake. (Warumi 9:23-24) “Tena, ili audhihirishe wingi wa utukufu wake katika vile vyombo vya rehema, alivyovitengeneza tangu zamani vipate utukufu; ndio sisi aliotuita, si watu wa Wayahudi tu, ila na watu wa Mataifa pia?” Mungu alitukusudia sote tangu zamani tupate utukufu. Fungu letu ni katika kuitikia mpango huo katika namna ulivyobuniwa na kujiepusha kuufanyia maboresho. (Warumi 9:25-26) “Ni kama vile alivyosema katika Hosea, Nitawaita watu wangu wale wasiokuwa watu wangu, Na mpenzi wangu yeye asiyekuwa mpenzi wangu. Tena itakuwa mahali pale walipoambiwa, Ninyi si watu wangu, Hapo wataitwa wana wa Mungu aliye hai.” Mungu ni wa mataifa yote ni wa madhehebu yote. Usimkatie mtu tamaa. Kwa Mungu wake huyo ni mwenye thamani kuu.