MASWALI YA KUJADILI: KUTOKA 1:1-22
- Je, Mungu alipanga Yakobo na wanawe wakaishi Misri katika nchi ya ugeni? Unadhani ni kwa nini Waisraeli walizaliana sana katika nchi ya ugeni? Je ni sahihi kuweka makazi yako ya kudumu katika nchi ya ugeni? Unadhani ni rahisi jamaa yako kuishawishi waandamane nawe katika nchi ya ugeni?
- Je wageni wanaweza kuwa na nguvu kuliko wenyeji katika nchi ya ugeni? Kwa nini mara nyingi fursa huwa zinaonekana na wageni zaidi kuliko wenyeji?je ni hatari ya kiasi gani wakati jamii moja inapomtegemea mtu mmoja mwenye ushawishi katika jamii? Kwa nini mtawala anapoondoka madarakani ndugu na watu wake wa karibu hukosa fursa walizokuwa nazo mwanzo?
- Je ukabila na upendeleo kazini una madhara gani kwa ustawi wa jamii husika? Je, katika maisha yako amewahi kuwepo Farao asiyemjua Yusufu? Maisha yako yaliathirikaje kutokana na hali hiyo? Je, hofu juu ya wageni wanaofanikiwa kuliko wenyeji ni hofu inayohitaji kupuuzwa au kuzingatiwa? Kama maendeleo huletwa na wageni kulikuwa na umuhimu wa kuwaacha Waisraeli wastawi katika nchi ya Misri?
- Kwa nini watoto wa kiume wa Waisraeli walionekana kuwa tishio hata kulazimika kuuawa wakati wa kuzaliwa kwao? Je, vita dhidi ya Waisraeli ilikuwa sawa na vita ya kimbari yenye lengo la kulitokomeza taifa zima la Israeli? Unadhani ni nani alikuwa anaichochea vita hiyo? Je, familia na koo zilizoendelea kiuchumi zina kawaida ya kupigwa vita na wasioendelea? Njia sahihi ya kunufaika na walioendelea ni kuwapiga vita au kujifunza kwao?
MASWALI YA KUJADILI: KUTOKA 2:1-25
- Ni maisha gani yalikuwa hatarini zaidi kati ya maisha ya Musa, maisha ya Miriamu, na maisha ya mama yake Musa? Je, binti Farao alikuwa na ulazima wa kuja kuoga mtoni au ilikuwa ni kusudi la Mungu aje akutane na Musa na kumuokoa? Kwa nini Miriamu hakutaka kumtambulisha mlezi wa Musa anayekwenda kumchukua kuwa ni mama yake Musa? Kwa kauli aliyotumia kulikuwa na ukweli aliokuwa anajaribu kuuficha?
- Je kulikuwa na uhali kwa mama yake Musa kulipwa mshahara kwa ajili ya kumyonyesha mwanae? Mungu alimzawadia mama yake Musa mtoto wake aliyekuwa anafichwa mtoni kila siku katika mazingira hatarishi, na kutengeneza mazingira ya mtoto huyo kuhudumiwa kutoka ikulu huku akilipwa mshahara? Hii inatufundisha nini juu ya uthubutu katika maisha?
- Musa alijitambua kuwa Mwebrania ingawa alilelewa katika mila za Kimisri. Hii inakufundisha nini kuhusu mchango wa mama kwa malezi ya mtoto katika miaka ya awali ya makuzi yake? Je, kujitambua na kujikubali ni hatua muhimu kuelekea kukataa unyonge na kushindwa? Kwa nini watu wengine wakiendelea huwasahau na kuwakataa watu wa kwao?
- Je Musa kumuua Mmisri aliyekuwa anamuonea Mwebrania ilikuwa ni dhambi kwa Mungu? (Matendo 7:23-25). Unapohisi Mungu amekutuma Kwenda kuwakomboa ndugu zako lakini wao wanakukataa usiwe kiongozi wao unafanyaje? Je unadhani Musa alikuwa ameiva vya kutosha kuweza kuwaongoza Waisraeli? Mafunzo ya uongozi aliyoyapata kwenye elimu aliyopewa kumuandaa kuwa Farao haikutosha kumsaidia kuwaongoza Waisraeli?
- Usomi wa Musa ulimfanya afikirie namna ya kutatua changamoto za jamii yake hata kama itamsababisha kufanya shughuli duni kama za kufuga na kusaidia wanawake kuchota maji. Unadhani elimu yetu inayotoa wasomi wasioweza kuziona fursa za kutatua changamoto za jamii inakwama kwenye mtaala uliopo au kwenye kushindwa kujitambua kwa wasomi wetu? Je ni kipi kinapaswa kutangulia kati ya kuoa na kupata kazi? Je Musa alikuwa na kazi wakati alipooa?
- Baada ya mfalme wa Misri kufa Mungu akawaona Waisraeli na kuwaangalia. Kuna tofauti gani kati ya kuona na kuangalia? Je, wewe ungekuwa baba wa Sipora ungeridhia aolewe na mtu asiye na kazi tena muuaji? Kitu muhimu cha kupima utayari wa kijana anayetaka kuoa leo ni nini? Ilikuwaje Waisraeli hawakuonyesha shukrani kwa Musa alipowapigania kwa Mmisri lakini mabinti wa Midiani walionesha shukrani kwa Musa? Kwa nini walimtambulisha Musa kama Mmisri?
MASWALI YA KUJADILI: KUTOKA 3:1-22
- Kuwaka moto bila kuteketea ni kanuni ya Mungu na wale wanaomwamini kama Daniel aliyetupwa katika tanuru la moto. Je unawafahamu watu waliokuwa wakiungua bila kuteketea maishani mwako? Umejifunza nini juu ya upendo wa Mungu kupitia uzoefu wao? Je unafahamu ni kwa nini kijiti anachoruhusu Mungu kiungue huwa hakiteketei?
- Je yule aliyetambulishwa kama malaika wa Bwana katika fungu la 2 ndiye huyo huyo aliyejitambulisha kama Mungu katika fungu la 4? Wale wanaomkaribia Mungu katika ibada bila kuvua viatu wanakosea? Je kubaki na viatu mguuni kunakwamishaje ibada kwa Mungu? Ni uchafu gani mwingine ambao hautakiwi kwenye ibada? Je ni eneo gani katika nyumba ya ibada lililo takatifu zaidi?
- Musa alienda kuishi Midiani kwa mkwewe akichunga kondoo badala ya kuchunga kondoo wa Mungu yaani Waisraeli. Je unailinganisha au kuitofautisha hali yake na ya Yona aliyekimbilia Tarshishi kujiepusha na uso wa Bwana? Je kama umekimbia kazi ya Mungu utakuwa na amani moyoni? Kwa nini Mungu hakutafuta mwingine wa kuwaongoza Waisraeli badala ya Musa?
- Kwa nini Mungu hachukui hatua ya kukomesha mara moja mateso ya watu wake na badala yake huruhusu muda mwingi kabla hajachukua hatua? Je inawezekana mara nyingi tunapofikiria Mungu ametuacha huwa hajatuacha ila anaangalia wakati bora zaidi wa kuingilia na kutuokoa? Je ipo haja ya kuendelea kumlilia Mungu hata kama vilio vyetu vya nyuma hajavijibu?
- Je ni jambo la hakika na la kuaminika kuwa Mungu anakuwazia mema na siku zako njema ziko mbele zinakuja? Viongozi wazuri wa kiroho ni wale wanaobaini kutokufaa au kutotosha katika jukumu walilopewa. Unaiona hali hiyo wakati Mungu alipompa agizo la kwenda kumuona Farao? Je wakati alipomuua Mimisri akimtetea Mwebrania mwenzake alijiona hafai kama anavyojiona sasa baada ya miaka 40 ya kuchunga kondoo wa mkwe wake? Ni nini kimeleta mabadiliko hayo?
- Je, kulikuwa na umuhimu kwa Musa kujua jina la Mungu aliyemtuma kabla ya kufikisha ujumbe aliotumwa kwa Waisraeli? Hilo jina la Mungu la MIMI NIKO linaleta ujumbe gani kwa Waisraeli walioteseka kwa muda mrefu? Je, kuna jambo linaloweza kutokea wakati wowote ambalo Mungu halioni?
- Kwa nini ikuwa lazima kuomba ruhusa kwa Farao ili awaruhusu Waisraeli waende kule ambako Mungu ameagiza wakamwabudu? Kwani Mungu angeshindwa kuwatoa hata bila kibali cha Farao? Ni Mungu yupi mkuu kati ya yule aliyewatumikisha Waisraeli utumwani na yule aliyewatoa utumwani? Je kulikuwa na haja ya kutambulisha ni Mungu yupi mkuu kati ya hao wawili?
MASWALI YA KUJADILI: KUTOKA 4:1-31
- Je ni muhimu kuwa na hakika kama ni Mungu kweli amekutuma yale uyafanyayo ili watu waikubali huduma yako? Je kufanya ishara na miujiza ni dalili kuwa Mungu amekutuma? Unaelewaje pale Mungu anapojitambulisha kuwa ndiye awafanyaye watu kuwa bubu, viziwi au vipofu? Je Mungu aweza kuondoa ulemavu wako unaodhani umeshindikana?
- Kwa jinsi Musa alivyokuwa na madai mengi kwa Mungu ni dalili kuwa yeye mwenyewe alikuwa na shida ya kumwamini Mungu au alitaka kazi anayoikubali ikafanyike kwa ufanisi? Musa aliambiwa arudi Misri maana waliotaka kumuua wamekufa na wazazi wa Yesu wakiwa Misri waliambiwa warudi Nazareth maana waliotaka kumuua mtoto wamekufa.
- Kwa nini ilikuwa lazima watu hao wafe ili uhakika wa amani upatikane? Je ni sahihi kumuombea adui yako afe? Kwa nini taifa la Israeli linatambuliwa kama mzaliwa wa kwanza wa Mungu? Kwa nini Mungu anaufanya moyo wa Farao mgumu asiwaruhusu Waisraeli kuondoka?
- Sipora mke wa Musa anaonekana kuipokea haraka desturi ya Waisraeli ya kutahiri na kwa ujasiri anamtahiri kijana wake kwa jiwe. Unajifunza nini juu ya wale Mungu aliowaita kutoka jamii zingine za kipagani na kujiunga na watu wa Mungu? Kwa nini kutahiriwa kulikuwa kwa lazima hivyo? Leo nini kinasimama badala ya kutahiriwa?
MASWALI YA KUJADILI: KUTOKA 5:1-23
- Ilikuwaje Mungu anaenda kuomba ruhusa kwa watawala wa dunia kwa ajili ya watu wake Kwenda kumtumikia? Je Farao alionyesha kiburi kwa kusema hamjui Mungu wa Waebrania au ni kweli alikuwa hamjui? Kwa nini Mungu aliruhusu watu wake wawe watumwa? Kama Waisraeli ndiyo waliokuwa wanafyatua matofali na kjenga Mapiramidi kwa nini Farao aliwaita wavivu?
- Kwa nini mtu anapoomba ruhusa kwa kiongozi wake ili aende ibadani siku za Sabato nao huonekana kama wavivu wanaokwepa kazi? Kwani Mungu aliruhusu kuongezeke ugumu kwenye kazi ya utumwa wakati akiwa anakaribia kuwatoa Misri? Unajisikiaje wakati unaowaongoza wanapotilia shaka uongozi wako?
MASWALI YA KUJADILI: KUTOKA 6:1-30
- Kwa nini Mungu aliwatwaa Waisraeli wawe watu wake kati ya mataifa yote ya dunia (Kumb.7:6-8). Kwa nini Waisraeli hawakuzipokea kwa furaha taarifa kuwa Mungu anakusudia kuwapigania? Je, wokovu wetu unategemea agano au unategemea utii kwa sheria? Ikiwa watu watatilia shaka agano na ahadi Mungu alizotoa kwa wanadamu je kuna njia nyingine inayoweza kutumika?
MASWALI YA KUJADILI: KUTOKA 12:1-51
- Kwa nini kuondoka kwa Wisraeli nchini Misri kuliandamana na uchinjanji wa wanyama wa kafara, kunyunyiza damu kwenye miimo, na kula mikate isiyochachwa? Wangeondoka bila kufanya Huduma hiyo kungekuwa na upungufu gani?
Ahadi za Mungu kuwa hazichelewi wala haziwahi unajidhihirishaje katika utimizo wa miaka 430 ya kukaa utumwani? Unadhani hujafikia matarajio yako kwa kuwa ratiba ya Mungu haijafika au kwa kuwa hujaweka juhudi ya kutosha au vyote?
- Waisraeli walisherehekea Pasaka kukumbuka siku waliyotolewa utumwani. Je, sisi leo tunasherehekea pasaka kukumbuka nini? Je, tarehe ya tukio letu la pasaka inawiana na tarehe halisi ya tukio lenyewe?
- Wale watakaokuwemo kwenye kundi la watakaookolewa kutoka dunia hii ya dhambi watakuwa ni wale walioandikwa kwenye kitabu cha Mwanakondoo (Ufunuo 21:27). Kuna ulinganifu gani na wale waliookolewa kutoka Misri?
- Kufuata maelekezo kulikuwa kwa muhimu sana ili kupata kuokolewa kutoka utumwani kwa Waisraeli. Kuna ukweli gani kwa wale wanaodai si lazima kuzingatia maagizo ya kuokolewa yaliyotolewa kwenye Biblia wakidai kuwa neema pekee inatosha?
- Kutahiriwa kulikuwa kwa lazima ili kuwemo katika kundi la wanaookolewa kutoka Misri. Je, ni lazima leo kutahiriwa ili kuhesabiwa miongoni mwa wanaookolewa. (Kut.12:48) Nini kinasimama leo badala ya tohara?
MASWALI YA KUJADILI: KUTOKA 16:1-36
- Inaelekea Waisraeli waliishiwa chakula na ndiyo maana Mungu aliwapatia kware na mana. Kwa nini njia ya kunung’unika waliyoitumia kufikisha hitaji lao haikuwa njia bora? Kuna tofauti gani kati ya kuomba na kunung’unika? Kwa nini Mungu aliwabadilishia Waisraeli aina ya vyakula walivyozoea kuvila wakiwa Misri?
- Je, unapookolewa ni lazima ubadilishiwe aina ya vyakula, vinywaji na mtindo mzima wa maisha? Je, ni sahihi kusema kila unapomnung’unikia mtumishi wa Mungu unamnung’unikia Mungu mwenyewe? Kwa nini kanuni ya ukusanyaji wa mana iliwasumbua baadhi ya Waisraeli kwa kukusanya kingi kuliko mahitaji au kwa kwenda kukitafuta siku waliyotakiwa kupumzika?
- Unadhani tatizo hilo lipo kwa wanadamu hata leo? Kitendo cha Mungu kuwapatia Waisraeli chakula cha bure kwa miaka 40 kinaelezea nini juu ya upendo wake kwa wanadamu? Je, unadhani kula kwako, kuvaa kwako, kusoma kwako, na mafanikio yako mengine ya maisha vinafadhiliwa na Mungu au ni juhudi yako mwenyewe?
- Je, agizo la kutunza Sabato liliwahusu Waisraeli tu au linawahusu wanadamu wote hata waishio leo? Nini kinathibitisha kuwa agizo hilo ni la Waisraeli au ni la wanadamu wote?
- Kwa nini mana iliyotunzwa hadi siku ya pili iliharibika lakini ile iliyowekwa kwenye kopo na Haruni ilidumu kuwa salama kwa siku nyingi? Neno la Mungu ni mana iliyoshuka toka mbinguni. Unachukua muda wa kutosha kuila (kusoma)?
MASWALI YA KUJADILI: KUTOKA 17:1-16
- Nini huja mawazoni mwako unapokuta hali usiyoitarajia kama ile waliyoikuta Waisraeli ambapo hapakuwa na maji ya kunywa? Unaikabilije hali hiyo ili kutojiletea matatizo ya kisaikolojia yanayowakuta wengi siku hizi?
- Kwa nini kitendo cha Waisraeli kumsuta Musa (kuteta) alikilinganisha na kumjaribu Bwana. Bwana anaingiaje katika malumbano haya? Unapotatizika na jambo ni vyema kuwaona wazee kwa ushauri na majadiliano. Unadhani wazee wa leo wana busara na hekima ya kutoa mashauri ya kufaa?
- Waamaleki ni uzao wa Esau (Mwanzo 36:1) nduguye Yakobo, kwa nini waliamua kuwashambulia Waisreali ambao ni watoto wa baba yao mdogo? Je, unafanyaje kuepuka ugomvi wa ndugu?
- Kuna fundisho gani katika ushindi unaotokana na kuinuliwa kwa mikono ya Musa? Je, ushindi wa kiongozi unategemea pia msaada kutoka kwa anaowaongoza?
MASWALI YA KUJADILI: KUTOKA 26:1-37
- Maelekezo ya ujenzi wa hema ya kukutania ulihitaji umakini na weledi. Unadhani hii inaashiria kuwa Mungu hupenda vitu vyake vifanywe kwa mpangilio nzuri na wa kuvutia? Unadhani kulikuwa na ulazima wa kufuatilia vipimo vyote kama vilivyoelekezwa?
- Juu kufuatilia maelekezo ya ujenzi wa hema ya kukutania kulihitaji kiwango fulani cha elimu au weledi na unadhani Musa alikidhi vigezo hivyo? Je, kuna umuhimu wowote wa viongozi wa kidini kuwa na kiwango cha kuridhisha cha elimu na weledi ili kutekeleza kwa ufanisi majukumu yao?
- Una maoni gani juu ya wale wanaodhani kuwa elimu au ujuzi havina umuhimu katika kufanikisha majukumu ya uongozi wa kiroho?
MASWALI YA KUJADILI: KUTOKA 28:1-43
- Kwa nini makuhani wa Agano la Kale walikuwa wanaume kutoka familia ya Haruni na ukoo wa Lawi. Kwa nini makuhani wa Agano Jipya hutoka jinsia yoyote na kabila lolote? (1Petro 2:9; Ufunuo 20:6). Kulikuwa na mavazi maalum kwa wahudumu wa hekaluni wakati wa Agano la Kale. Kwa nini leo wahudumu hawalazimiki kuvaa mavazi yoyote ya kuwatambulisha kwenye ibada?
- Kwa nini ilikuwa ni lazima kwa Kuhani kubeba kifuani mwake majina ya makabila ya Israeli? Je unajisikia faraja unapotambua wako wa kiroho anakufahamu na anakuombea ufanikiwe? Je waumini wana thamani gani ukilinganisha na mali zingine zinazomilikiwa na kanisa? Njuga zilizovaliwa na makuhani zilikuwa na umuhimu gani katika kulinda usalama wao wanapohudumu hekaluni?
- Viongozi wa kiroho wanapoteuliwa kushika wadhifu wao kwenye Agano la Kale walifanyiwa mambo mazito ya kuwaweka wakfu. Unadhani jambo hilo linachukuliwa kwa uzito unaostahili?
MASWALI YA KUJADILI: KUTOKA 30:1-38
- Kuhesabu watu kwa lengo la kukusanya sadaka zao kuliwezekana wakati wa ujenzi wa hekalu. Kwa nini jambo hilo lisifanyike leo ili kuhakikisha kila mmoja anashiriki ujenzi wa nyumba ya ibada?
- Kwa nini palihitajika manukatko yaliyokolea kwenye huduma za hema takatifu? Je kujipulizia au kujipaka manukato kwa wale wanaokuja kuabudu kunaenda sawa na Maandiko?
- Harufu ya wanyama wanaotolewa kafara ilikuwa inatoa ujumbe gani kwa waabuduo ikilinganishwa na harufu za uvumba na manukato? Je harufu ya manukato ilileta ujumbe wowote wa matumaini kwa mdhambi?
MASWALI YA KUJADILI: KUTOKA 31:1-18
- Mungu anapokuagiza kazi ya kufanya atakupa na watu wa kukusaidia na kuitegemeza kazi hiyo. Je unaiona hali hiyo katika kazi aliyompa Haruni. Ukweli huo unakupa faraja gani wewe unayehisi umeachwa peke yako katika kuifanya kazi ya Mungu?
- Mungu hugawa vipawa vyake na kuwapa majukumu wanadamu bila kupendelea kabila la mtu au eneo analotokea kama alivyofanya kwa Bezaleli na Oholiabu. Je kanisa hupata hasara gani hupata hasara gani linapoacha kutambua watu hao na kuchagua watu kwa vigezo vingine vya kibinadamu?
- Fundi wa ujenzi stadi anapojitolea kupaua jengo la Kanisa bila kuwatoza chichote Kanisa linapaswa kumfanyia nini mtu huyo? Kwa nini hutokea Waumini wakatoa gharama kubwa ya huduma zinazohitajika kanisani kuliko walio nje?
- Je ni sahihi kazi inayohitaji ustadi kufanywa na watu wote kwa njia ya kujitolea na kuleta matokeo dhaifu ya ubora? Je, ni makosa kwa mtu kudai kulipwa kwa kazi aliyoifanya kwa kanisa kwa kuwa naye ni muumini?
- Kwa nini Mungu alikazia maagizo ya kutunza Sabato kwa Waisraeli kupitia kwa Musa? Je utunzaji wa Sabato ulikusudia kuitambulisha siku maalum ya ibada katika juma kuwa Jumamosi? Je madai haya yanawahusu hata watu wa mataifa mengine yaishiyo leo?
- Je mbao mbili za mawe zilizoandikwa Amri Kumi za Mungu alizopewa Musa na Mungu pale mlima Sinai zinawakisha Agano alilolifanya Mungu na wanadamu kupitia kwa Waisraeli? (Kutoka 38:24)
MASWALI YA KUJADILI: KUTOKA 32:1-35
- Je, ni Musa aliyewatoa Waisraeli Misri au ni Mungu? Kuna ,hatari gani watu wanapomwekea tumaini kiongozi aliyechaguliwa na Mungu awaongoze kuliko kumwekea tumaini Mungu mwenyewe?
- Je subira inahitajika ili viongozi walete mabadiliko yanayotarajiwa? Je kutowaamini viongozi ni sababu mojawapo ya taasisi nyingi zikiwepo jumuiya za kidini kuwa na migogoro isiyoisha?
- Waisreli waliopendekeza kufanyiwa miungu ya kuwaongoza walikuwa na imani na Mungu aliyewatoa Misri? Kuna ukweli wowote kuwa wengi wa wale wanaodai kuwa Wanamwamini Mungu na kuacha imani za kipagani huwa hawajaziacha kabisa,?
- Je Haruni alifanya sawa kuwakubalia watu wake kutengeneza ndama wa kumuabudu? Kiongozi anayependa kuwafurahisha watu wake wakati wote hata pale wanapomtaka avunje miiko ya taasisi anayoiongoza anafaa kuwa kiongo,zi?
- Je Musa alikuwa sahihi kumwambia Mungu aache uovu wake wa kufikiria kuwaangamiza Wamisri kwa uasi waliofanya? Je viongozi wanaopendelea wenye dhambi wasemehewe wanaonekana wana sifa za kuwa viongozi?
MASWALI YA KUJADILI: KUTOKA 33:1-23
- Mungu ana deni la kututimizia yale aliyomwapia Ibrahimu zamani kwamba atatupatia nchi ya maziwa na asali. Ukweli huo unakusaidiaje kuamsha matumaini pale unapojikuta umekata tamaa?
- Je leo inawezekana kuongea na Mungu uso kwa uso kama Musa alivyokuwa anafanya? Kama kwa Musa iliwezekana kwa nini Mungu asifanye hivyo kwa wanadamu wote?