Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

2 PETRO

MASWALI YA KUJADILI: 2 PETRO 1:1-21

  1. Tunakuwaje washirika wa tabia ya Uungu kupitia ahadi kubwa za Mungu? Ahadi hizo kubwa mno ni zipi? Ahadi hizo zinatusaidiaje kuokolewa na uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa.
  2. Kwa nini upendo umekuwa hatua ya mwisho katika kumjua Mungu na kuzaa matunda? Kwa nini upendo ukikosekana sifa nyingine zote za ukristo zinapoteza maana? (1Wakorintho 13:1-2). Jitihada zinazotakiwa ili kufanya uteule wetu na kuitwa kwetu imara ni zipi? Mbona mahali pengine jitihada kama hizo zinaonekana kutohitajika? (Zekaria 4:6; Waefeso 2:8-9)
  3. Yesu alipata heshima gani na utukufu alipoletewa sauti iliyotoka kwa Baba alipoambiwa huyu ni mwanangu mpendwa wangu, ninayependezwa naye? Kwani kuna heshima na utukufu ambao hakuwa nao mwanzo? Yesu aliambiwa maneno hayo akimwakilisha Mungu au akimwakilisha mwanadamu?
  4. Kwa neno la unabii halijifunui lote kwa wakati mmoja bali hatua kwa hatua hadi kufikia mchana mkamilifu? Kwa nini hata ule unabii uliofunuliwa hupokelewa kwa shida na walio wengi? (Luka 13:34).
  5. Je unabii waweza kuwa na tafsiri mbili tofauti? Je, lipo kanisa linaloaminika kuwa mstari wa mbele katika karama hiyo ya unabii kuliko mengine? Vigezo vya kulitambua kanisa hilo ni vipi?

 

MASWALI YA KUJADILI: 2 PETRO 2:1-22

  1. Je, kuna uwezekano wa kujipatia faida kupitia upotoshaji wa Neno la Mungu? Uharibifu unaoweza kuwapata watu wa aina hiyo ni upi? Mojawapo ya uzushi wa kupoteza ulioingizwa kwa werevu ni upi? Kwa nini panahitajika werevu ili kuingiza uzushi wa kupoteza? (Mwanzo 3:1).
  2. Malaika walio kwenye vifungo vya giza wanaolindwa hadi ije hukumu ni nani? Malaika hao wanalindwa na nani? Je wenyewe wanatambua kuwa wanasubiri hukumu? (Ufunuo 12:12). Kwa nini Lutu anaitwa ni mwenye haki naye alishindwa kuokoa nyumba yake isipokuwa mabinti wawili ambao alizini nao baadaye. Je, hata wasio wakamilifu wanaweza kuwa wenye haki?
  3. Watu wenye macho yajaayo uzinzi utawatambuaje? Kwa nini ulevi wakati wa mchana si anasa? Kwa nini watu wenye kujikinai hawatetemeki wanapoyatukana mambo matukufu? Kwa nini walioyakimbia machafu ya dunia wakirudi nyuma hali yao huwa mbaya kuliko ya kwanza?
  4. Je wanaowafundisha watu kuwa chini ya neema ni kuwa huru kuvunja sheria za Mungu wanawaahidia watu uhuru wao wenyewe wakiwa watumwa wa uharibifu? Kwa nini tabia za mbwa na nguruwe zinalinganishwa na mtu aliyerudia maisha ya dhambi? Je, hii ni kudhihirisha kuwa Wanyama hawa wapo kwenye kundi la Wanyama najisi?

 

MASWALI YA KUJADILI: 2 PETRO 3:1-18

  1. Je, dunia imefanyizwa katika maji na ndani ya maji? Kufanyizwa katika maji kuna tofauti ani na kufanyika ndani ya maji? Mbingu na nchi za sasa zimewekwaje akiba hadi zitakapoangamia? Tangu zamani za mababu zetu dunia imeendelea kubaki hali ile ile. Je huu ni ushahidi tosha kuwa yale yanayotabiriwa kuwa yataupata ulimwengu si ya kweli?
  2. Ukweli kuwa dunia ilifanyizwa kutoka ndani ya maji kunathibitishaje kuwa yaliyotabiriwa yatakuwa? Dhana kuwa dunia yote iliwahi kugharikishwa na maji inaungwaje mkono na somo la historia inakinzanaje jiografia? Je wanasayansi wanaelewa zaidi umri wa dunia kuliko wanazuoni wa Biblia? Miaka alfu moja inakuwaje sawa na siku moja?
  3. Mungu anaonekana kukawia kutimiza ahadi yake kwa kuwa hapendi mtu yeyote apotee. Ikiwa wanadamu wataendelea kuwa wagumu wa kutubu ataendelea kuwasubiri? Tunaihimiza siku ya Bwana kwa kufanya nini? Je, kosa la wanadamu watakaoangamizwa ni kutokumcha Mungu pekee? (2 Wathesalonike 1:8). Yesu anakuja mara ya pili duniani ili atukuzwe katika watakatifu. Jambo hilo la kutukuzwa kwa Yesu lina umuhimu gani?
  4. Nyaraka za Paulo ni ngumu kueleweka kwa watu wenye tabia gani? Je kuyaelewa Maandiko kunahitaji elimu? Ni mambo gani muhimu kuyazingatia ili kuelewa andiko? Kwa nini watu wenye dhihaka wanakuja siku za mwisho? Kwa nini inasemwa wenye dhihaka wanafuata tamaa zao wenyewe? Je ni kweli kuwa ahadi ya kuja kwa Yesu imecheleweshwa? Je dunia hii imefanyizwa kutoka kwenye maji na ndani ya maji? Jambo hilo liliwezekanaje?
  5. Kwa nini dunia ya zamani ilipofanya uasi iliangamizwa na gharika lakini dunia ya sasa imewekwa tayari kwa moto? Kwa nini Mungu anaangamiza wanadamu wasiomcha kwenye gharika lakini hakufanya hivyo kwa Shetani? Siku moja inakuwaje sawa na miaka elfu moja? Kwa nini nyaraka za Paulo zinapotoshwa? Wenye tabia ya kupotosha nyaraka za Paulo wana sifa gani zinazowatambulisha?