Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

WATAKATIFU WAPENDWAO

WATAKATIFU WAPENDWAO

Mungu alimuumba mwanadamu akiwa mtakatifu. Na ilikuwa mpango wake wa tangu mwanzo kwamba mwanadamu aendelee kuwa katika hali hiyo siku zote. Waefeso 1:4 “Kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo.” Lakini dhambi ilipoingia ulimwenguni ilimfanya mwanadamu aishi maisha ya dhambi yasiyo matakatifu. Maisha ya dhambi humchafua mwenye kuwa nayo na kumfanya aonekane mchafu mbele ya Mungu. Hali hiyo ikawa sehemu ya maisha yake siku zote. Na mtihani ukawa ni namna gani atarejea katika hali ya utakatifu aliyokuwa nayo awali. Mwanadamu akawa katika hali ya kupoteza matumaini. Ayubu 15:14 “Je! Mwanadamu ni kitu gani, hata akawa safi? Huyo aliyezaliwa na mwanamke, hata awe na haki?”

Lakini Mungu akaweka mpango wa kumuokoa mwanadamu. Katika mpango huo alitengeneza mazingira ya kumrejeshea mwanadamu hali yake ya awali ya utakatifu. Katika hatua ya awali, Mungu aliwachagua Waisraeli kama kundi la watu watakaofanyiwa majaribio ya kuwa watakatifu. Mambo ya Walawi 20:26 “Nanyi mtakuwa watakatifu kwangu mimi; kwa kuwa mimi Bwana ni mtakatifu nami nimewatenga ninyi na mataifa, ili kwamba mwe wangu.” Kupitia kwa Waisraeli Mungu alikusudia kuwadhihirishia wanadamu wote kwamba maisha matakatifu yanawezekana. 

Halikuwa jambo jepesi kwa Waisraeli kuacha kufanya yaliyo machafu kwa kuwa asili ya mwanadamu baada ya anguko la dhambi ni ya kupenda kufanya uchafu au yaliyo machukizo mbele ya Mungu. Kila mwanadamu aliyezaliwa alizaliwa akiwa na asili hiyo. Mtunga Zaburi anaielezea hali hiyo ambayo ni fungu la watu wote. Zaburi 51:5 “Tazama, mimi naliumbwa katika hali ya uovu; Mama yangu alinichukua mimba hatiani.” Tangia akiwa tumboni mwa mama yake mwanadamu amekuwa na mwelekeo wa kutenda maovu. Kutenda maovu huwa jambo lililo rahisi kwake kama kunywa maji. Ayubu 15:16 “. . . mtu ambaye ni mwenye kuchukiza na uchafu, Mwanadamu anywaye uovu kama anywavyo maji!”

Hali hiyo ikazalisha matatizo ya aina tatu kwa mwanadamu. Tatizo la kwanza ni la mwanadamu kutamani kufanya uovu tu wakati wote. Mwanzo 6:5 “Bwana akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu sikuzote.” Hiyo ni hali ambayo mtu amepoteza ushawishi wa Roho Mtakatifu maishani. Inafananishwa na dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu ambayo mtu akiifikia hufuatia maangamizo. Mathayo 12:31 “Kwa sababu hiyo nawaambia, Kila dhambi na kila neno la kufuru watasamehewa wanadamu, ila kwa kumkufuru Roho hawatasamehewa.”

Katika hali hii mtu haoni ubaya wa kufanya ubaya wala hajutii makosa anayofanya. Ili asiendelee kujiumiza na kuumiza wengine Mungu huchagua kumpumzisha mtu wa aina hiyo kama alivyofanya kwa wale walioishi kipindi cha Nuhu. Anakuwa amejenga uadui wa kutosha kwa Mungu na nia yake haipo tayari kutii maagizo ya Mungu. Warumi 8:7 “Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii.”

Tatizo la pili lililozalishwa na uovu ni la mwanadamu kutamani kufanya mema na kujikuta akiishia kutenda mabaya. Hii kwa lugha nyingine ndiyo inayoitwa dhambi. Yakobo 4:17 “Basi yeye ajuaye kutenda mema, wala hayatendi, kwake huyo ni dhambi.” Wanadamu wote wapo katika hali hiyo ya kujikuta wakiwa na ujuzi wa mema na mabaya lakini wakishindwa kujizuia kutenda mabaya.

Mtu atendaye dhambi ni tofauti na atendaye kosa. Atendaye kosa ni yule asiyejua kama alitendalo ni kosa. Kwa kawaida atendaye kosa huwa hana hatia kwa kuwa hakufanya kwa kukusudia. Hata hivyo aliyefanya dhambi na aliyefanya kosa wote waweza kujikuta wakiadhibiwa. Warumi 2:12 “Kwa kuwa wote waliokosa pasipo sheria watapotea pasipo sheria, na wote waliokosa, wenye sheria, watahukumiwa kwa sheria.” Kile kinachoitwa hapa kama sheria ni ile sauti unayoisikia moyoni ikikutahadharisha kabla hujatenda dhambi na ile inayokusuta baada ya kuwa umetenda dhambi.

Tafsiri iliyo bayana kuhusu dhambi na makosa tunaiona kwa Adamu na Hawa. Adamu alifanya dhambi na Hawa alifanya makosa. Hawa alidanganywa maana hakujua kama anatenda kosa lakini Adamu hakudanganywa kwa kuwa alikuwa anajua madai ya Shetani na mkewe ni ya uongo na bado akala tunda lililokatazwa na Mungu. 1 Timotheo 2:14-15 “Wala Adamu hakudanganywa, ila mwanamke alidanganywa kabisa akaingia katika hali ya kukosa. Walakini ataokolewa kwa uzazi wake, kama wakidumu katika imani na upendo na utakaso, pamoja na moyo wa kiasi.” Kwao wote Adamu na Hawa na kwa waliofanya dhambi na makosa; ahadi inatolewa ya kuokolewa na mzao wa mwanamke utakaokuja kumponda kichwa Shetani. Mwanzo 3:15 “Nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino.”

Hali ya kujisikia hatia inawahusu hata wale wanaodhaniwa kuwa hawana taarifa za kipi ni kibaya na kipi ni chema. Katika dhamira zao upo mwongozo unaowaelekeza kutofautisha jema na baya. Warumi 2:14-15 “Kwa maana watu wa Mataifa wasio na sheria wafanyapo kwa tabia zao yaliyo ndani ya torati, hao wasio na sheria wamekuwa sheria kwa nafsi zao wenyewe. Hao waionyesha kazi ya torati iliyoandikwa mioyoni mwao, dhamiri yao ikiwashuhudia, na mawazo yao, yenyewe kwa yenyewe, yakiwashitaki au kuwatetea.”

Hali hii inaashiria kuwepo kwa ushawishi wa Roho Mtakatifu maishani. Wagalatia 5:17 “Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka.” Hali hii inaleta matumaini kuwa angalau nia ya mwanadamu inatamani kumtii Mungu. Warumi 7:15-17 “Maana sijui nifanyalo, kwa sababu lile nilipendalo, silitendi; bali lile nilichukialo ndilo ninalolitenda. Lakini kama nikilitenda lile nisilolipenda, naikiri ile sheria ya kuwa ni njema. Basi sasa si mimi nafsi yangu ninayetenda hilo, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu.” Mwanadamu aliye katika hatua hii yupo katika hatua ya kukua akizoezwa kuongozwa na Roho Mtakatifu badala ya kuongozwa na mwili.

Kwa bahati mbaya hali hii inaweza kuzalisha tatizo la kukata tamaa kwa sababu ya kukerwa na hali ya kurudia rudia kufanya makosa yale yale na lawama za watu zinazoelekezwa kwa mkosaji. Ndiyo maana Paulo analalamika akisema, Warumi 7:24 “Ole wangu, maskini mimi! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti?” lakini katika fungu linalofuata anajipa faraja akisema, “Namshukuru Mungu, kwa Yesu Kristo Bwana wetu. Basi, kama ni hivyo, mimi mwenyewe kwa akili zangu naitumikia sheria ya Mungu, bali kwa mwili wangu sheria ya dhambi.”

Mgogoro wa kushindwa kutii maagizo ya Mungu unatokana na mwili uliolemazwa na uovu na wala mwanadamu hana sababu ya kuiona hali hiyo kama ya kukatisha tamaa. Yesu anaijua hali hiyo na ameitafutia ufumbuzi. Hapaswi mtu kujilaumu au kumlaumu Mungu kutokana na hali hiyo. Mungu anajua sisi wenyewe kwa uwezo wetu hatuwezi kuibadili hali hiyo. Yeremia 13:23 “Je! Mkushi aweza kuibadili ngozi yake, au chui madoa-doa yake? Kama aweza, ndipo na ninyi mwaweza kutenda mema, ninyi mliozoea kutenda mabaya.”

Uwezo wa kutenda mema unakuzwa na kazi ya Roho Mtakatifu inayofanywa ndani ya mwanadamu aliyemwamini Yesu. Yeye huwaongoza wanadamu ili kutaka kwao na kutenda kwao kuenende sawasawa na mapenzi ya Mungu. Wafilipi 2:13 “Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema.” Mungu kupitia nafsi ya Roho Mtakatifu huteka akili zetu na kuziongoza ili kuutiisha mwili. Na ingawa mchakato huo huonekana kuchukua muda mrefu kwa baadhi ya watu lakini kukamilika kwake ni jambo la hakika. Wafilipi 1:6 “Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu.”

Katika hali ya kawaida isingetarajiwa Mungu afanye uingiliaji kati wa kiwango hiki kwa tatizo la uovu wa mwanadamu. Kwa kuwa mwanadamu alipoteza uwezo wa kutenda mema kutokana na asili yake kushindwa kuendana na matakwa ya Mungu, hapakuwa na uwezekano tena wa yeye kuwa msafi. Ayubu 14:4 “Ni nani awezaye kutoa kitu kilicho safi kitoke katika kitu kichafu? Hapana awezaye.” Lakini Mungu ameweza kutoa kitu kisafi kutoka kwa kitu kichafu kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Waefeso 3:20 Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu.”

Tatizo la tatu ni lile la kujaribu kufanya mema kwa juhudi zetu bila kutegemea msaada wa Mungu. Mwanadamu akisukumwa na nia ya kutotaka vya bure na kujaribu kuonyesha uwezo wake wa kujiokoa anajaribu kufanya yale yasiyotekelezeka kutokana na udhaifu wa mwili. Analazimisha kutenda mema huku nia yake ikiwa na uadui na Mungu. Kinachotokea ni kuzaliwa kwa matendo ya haki yaliyojaa unajisi kwa kuwa yamechangamana na kiburi na majivuno. Isaya 64:6 “Kwa maana sisi sote tumekuwa kama mtu aliye mchafu, na matendo yetu yote ya haki yamekuwa kama nguo iliyotiwa unajisi; sisi sote twanyauka kama jani, na maovu yetu yatuondoa, kama upepo uondoavyo.”

Paulo alikuwa mtu wa kuutumainia mwili kabla hajakutana na Yesu. Wafilipi 3:4 Walakini mimi ningeweza kuutumainia mwili. Mtu ye yote akijiona kuwa anayo sababu ya kuutumainia mwili, mimi zaidi. Nalitahiriwa siku ya nane, ni mtu wa taifa la Israeli, wa kabila ya Benyamini, Mwebrania wa Waebrania, kwa habari ya kuishika torati, ni Farisayo, kwa habari ya juhudi, mwenye kuliudhi Kanisa, kwa habari ya haki ipatikanayo kwa sheria sikuwa na hatia.” Haikumchukua muda mrefu kugundua hatimaye kuwa mfumo huu wa kujaribu kuufikia utakatifu kwa juhudi za kibinadamu ni wa kuchosha usioweza kumpatia furaha wala amani mwenye kuufanya.

Aliitikia wito wa Yesu wa kuwataka wanadamu kutoiga mfumo wa kujipatia haki uliokuwa unafuatwa na Mafarisayo. Mathayo 5:20 “Maana nawaambia ya kwamba, Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.” Paulo aliubwaga chini mfumo huo wa kujipatia haki kwa juhudi za kibinadamu na kukubali kuhesabiwa haki ya Kristo. Wafilipi 3:8-9 “Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo; tena nionekane katika yeye, nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani iliyo katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu, kwa imani.”

Kuna uwezekano wa mtu kupoteza muda mwingi ukijaribu kuishi Maisha matakatifu yasiyotokana usaidizi wa Roho Mtakatifu ukiamini kuwa matendo yako yana mchango kwa wokovu wako. Huu ndiyo udanganyifu mkubwa wa Shetani. Kwa nje mtu wa aina hiyo aweza kuonekana ni mwenye kukua kiroho wakati ambapo kimsingi kile akifanyacho ni maigizo tu yasiyotoka ndani. Matendo hayo siku ya mwisho yatapimwa na endapo yataonekana hayakutokana na kazi ya Roho yatatupiliwa mbali na mhusika atakabili adhabu. 1 Wakorintho 3:14 “Maana msingi mwingine hakuna mtu awezaye kuuweka, isipokuwa ni ule uliokwisha kuwekwa, yaani, Yesu Kristo. Lakini kama mtu akijenga juu ya msingi huo, dhahabu au fedha au mawe ya thamani, au miti au majani au manyasi, kazi ya kila mtu itakuwa dhahiri. Maana siku ile itaidhihirisha, kwa kuwa yafunuliwa katika moto; na ule moto wenyewe utaijaribu kazi ya kila mtu, ni ya namna gani. Kazi ya mtu aliyoijenga juu yake ikikaa, atapata thawabu.”

Lakini wale watakaochagua kuwa chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu wakipokea kwa unyenyekevu maonyo yanayofunua mwenendo wao usiofaa, watapata ondoleo la dhambi na kupewa uwezo wa kuishi maisha matakatifu kwa utukufu wa Mungu. Matendo ya Mitume 2:37-39 “Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu? Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu. Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie.”

Mchakato huu wa kubadilisha nia na asili ya dhambi ya mwanadamu ni wa kudumu kwa kadri mwanadamu anavyoendelea kuwa hai. Kukamilika kwa mchakato huu wa mabadiliko ya tabia, kunategemea namna mwanadamu husika anavyotoa ushirikiano kukubali mapungufu aliyonayo kwa kadri yanavyoibuliwa na vyanzo mbalimbali vyenye kumtakia mema na namna anavyoruhusu mabadiliko kutokea maishani mwake.

Moyo wa mwanadamu ni mdanganyifu. Yeremia 17:9 “Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua?” Na kwa kuwa moyo wa mwanadamu ni mdanganyifu Mungu amemuwekea mwanadamu mfumo wa kumwezesha kujikagua mwenyewe na kujithibitisha kama yupo sahihi au la ili asiingie hatarini kizembe. Neno la Mungu lililo kwenye mfumo wa sauti au maandishi laweza kumpa tahadhari mwanadamu anapoelekea kutenda kosa au dhambi. Na Neno la Mungu laweza kumsaidia mtu asiingie kwenye mazingira hatarishi ya dhambi.  Zaburi 119:11 “Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi.” Neno la Mungu likiwa sehemu ya Maisha ya mwanadamu humfanyia ulinzi na kumkumbusha kimpasacho kutenda. Waebrania 4:12 “Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.”

Kazi hii ya utakaso nay a kufua mavazi ya binadamu kwa kuondoa tabia ya ubinafsi ya dhambi na kuweka tabia ya Mungu ya upendo. Tabia hii ya upendo wa Mungu inaakisi tabia yake ya utakatifu kama ilivyofunuliwa kwenye Amri zake Kumi takatifu. Amri zile kwa muhtasari zinazungumzia upendo kwa Mungu na upendo kwa wanadamu. Wagalatia 5:14 “Maana torati yote imetimilika katika neno moja, nalo ni hili, Umpende jirani yako kama nafsi yako.”

Upendo utakaodhihirishwa na wale walioruhusu mabadiliko ya tabia kutokana na kazi inayofanywa na Roho Mtakatifu, utawavuta watu wengine nao kuchagua kuokolewa. Kazi ya mabadiliko ya tabia ni ya muhimu kwa ajili ya kuwa ushuhuda kwa walio nje na siyo njia ya kujipatia wokovu. Yohana 13:35 “Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi.”

Wakati mchakato huu ukiendelea Mungu ameonesha nia ya kuwatambua wanaohudumiwa na mchakato huu wa marekebisho ya tabia kama watakatifu. Wanaoishi kwa mfumo huu wa kuwakilisha tabia ya Mungu ya upendo kama inavyowasilishwa kwenye Amri Kumi huitwa watakatifu. Ufunuo wa Yohana 14:12 “Hapa ndipo penye subira ya watakatifu, hao wazishikao amri za Mungu, na imani ya Yesu.” Utakatifu wao unatokana na kukubali mapungufu yanayobainishwa na amri hizo maishani mwao na kukubali marekebisho yanayopendekezwa na Roho mtakatifu kwao yatakayozifanya tabia zao kuakisi tabia zinazodhihirishwa na amri kumi.

Sababu nyingine ya wale walioanza marekebisho ya tabia kutambuliwa kama watakatifu ni utayari wao wa kumkubali Yesu kuwa Mwokozi wa Maisha yao. Waefeso 1:1 “Paulo, mtume wa Kristo Yesu, kwa mapenzi ya Mungu; kwa watakatifu walioko Efeso wanaomwamini Kristo Yesu.” Kumwamini Kristo Yesu kunampa mtu hadhi ya kutambuliwa kama mtakatifu. Kuwa kwao watakatifu hakumaanishi wamekuwa wakamilifu. Waefeso 4:12 “Kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe.” Hawa ni watakatifu wanaoendelea kukamilishwa huku wakitambuliwa kama watakatifu. Wala kuitwa kwao watakatifu hakutamatishi mchakato wa marekebisho ya tabia.

Ni jambo la hatari katika hatua yoyote ya mchakato wa marekebisho ya tabia kudhani kuwa umekamilika. Paulo anaweka bayana kuwa hajafikia hatua ya ukamilifu na hivyo yeyote asije akaingiliwa na udanganyifu wa Shetani kuwa amefikia hatua asiyoweza kurudi nyuma. Wafilipi 3:12-14 “Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake nimeshikwa na Kristo Yesu. Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele; nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu.”

Mungu ana hakika kuwa kazi aliyoianza ndani yetu itakamilika nasi tutakuwa wakamilifu. Waefeso 5:25-27 “Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno; apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa.” Wakati kazi hiyo ikiendelea anaona sababu ya kutuita watakatifu ili tuondokane na ile dhana ya kujiona watu duni kwa kujiangalia tulivyo sasa badala ya kujiangalia tutakavyokuwa hapo baadaye.

Mungu anataka tusijiangalie tulivyokuwa bali vile tutakavyokuwa. Wakolosai 3:5-13 Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu; kwa ajili ya mambo hayo huja ghadhabu ya Mungu. Katika hayo ninyi nanyi mlitembea zamani, mlipoishi katika hayo. Lakini sasa yawekeni mbali nanyi haya yote, hasira, na ghadhabu, na uovu, na matukano, na matusi vinywani mwenu. Msiambiane uongo, kwa kuwa mmevua kabisa utu wa kale, pamoja na matendo yake; mkivaa utu mpya, unaofanywa upya upate ufahamu sawasawa na mfano wake yeye aliyeuumba. Hapo hapana Myunani wala Myahudi, kutahiriwa wala kutokutahiriwa, mgeni wala mshenzi, mtumwa wala mwungwana, bali Kristo ni yote, na katika yote. Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi.”