Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

SAUTI KUTOKA UGHAIBUNI















PITA KOTE KOTE

1.
Ipaze sauti yako, kuihubiri injili,
Wajulishe ndugu zako, wakaribu na wa mbali,
Wasihi jirani zako, Mwokozi wamkubali,
Pita pita kote kote, wafundishe watu wote.

2.
Pita kwenye njia kuu, na pia vichochoroni,
Sauti ipae juu, isikike milimani,
Iwapatie nafuu, waishio mabondeni,
Pita pita kote kote, wafundishe watu wote.

3.
Pita katika vijiji, watembelee mijini,
Hubiri kwenye majiji, wasikie ghorofani,
Kwamba Mungu muumbaji, tawapatia amani,
Pita pita kote kote, wafundishe watu wote.

4.
Pita kote kwa bidii, porini na mashambani,
Wajulishe watalii, na walio viwandani,
Wasifanye usanii, kwenye mambo ya imani,
Pita pita kote kote, wafundishe watu wote.

5.
Pita pita masokoni, ongea na wachuuzi,
Nenda hospitalini, wafundishe wauguzi,
Kwamba hivi karibuni, watamwona Mkombozi,
Pita pita kote kote, wafundishe watu wote.

6.
Vyuoni pia shuleni, kahubiri mabwenini,
Wanafunzi darasani, na walimu ofisini,
Walio maabarani, wote wadumu salani,
Pita pita kote kote, wafundishe watu wote.

7.
Wageni mahotelini, kwenye nyumba za wageni,
Wanasayansi angani, wanaokwenda mwezini,
Warudipo duniani, waonywe kwa umakini,
Pita pita kote kote, wafundishe watu wote.

8.
Danguroni makahaba, wanaoishi gizani
Wasifiao mahaba, kwa kuzini hadharani,
Waoneshwe msalaba, ili warudi mwangani,
Pita pita kote kote, wafundishe watu wote.

9.
Inua paza sauti, isikike gerezani,
Kwa pendo bila shuruti, waelekezwe mbinguni,
Wayakimbie mauti, wakajazwe tumaini,
Pita pita kote kote, wafundishe watu wote.

10.
Haya sasa nenda kote, kwa nguvu zake Mwokozi,
Hubiri kwa nguvu zote, ikibidi kwa machozi,
Ijaze dunia yote, na neno la ukombozi,
Pita pita kote kote, wafundishe watu wote.
---------------------------------------------------
Christopher R. Mwashinga
(Sauti Toka Ughaibuni)


PIGA SIMU JU MBINGUNI


1.
Wasimama dirishani, nje unaangalia,
Moyoni unatamani, kwa makelele kulia,
Kwa kuwa wako mwandani, amekwishakuchunia,
Piga simu ju mbinguni, daima utajibiwa.

2.
Moyoni unahuzuni, jirani kakununia,
Watazama mawinguni, mengi unayawazia,
Ndugu sijione duni, hayo mambo ya dunia,
Piga simu ju mbinguni, daima utajibiwa.

3.
Kila upigapo simu, mwandani kikukatia,
Kukupa maji ya ndimu, matusi kukurushia,
Au kukwita hasimu, uongo kukuzushia,
Piga simu ju mbinguni, daima utajibiwa.

4.
Watu wakikuhujumu, ubaya kukufanyia,
Ukashindwa kujikimu, au kujihudumia,
Jua huo ni msimu, utapita vumilia,
Piga simu juu mbinguni, daima utajibiwa.

5.
Upatwapo na maradhi, kitanda kukilalia,
Watu waovu baadhi, wakakunyanyapalia,
Wakiitamani ardhi, ije kukukumbatia,
Piga simu ju mbinguni, daima utajibiwa.

6.
Ubambikiwapo kesi, kortini ukaingia,
Ukasikia tetesi, hakimu ameridhia,
Uswekwe ndani upesi, upate kuangamia,
Piga simu ju mbinguni, daima utajibiwa.

7.
Usotapo gerezani, usiku kucha kulia,
Kuogelea gizani, nuru kuitamania,
Na huku mwovu Shetani, hofu akikupatia,
Piga simu ju mbinguni, daima utajibiwa.

8.
Mvua igomapo nyesha, mazao yakafifia,
Hadi ukapata presha, kwa uchungu ukalia,
Mungu atakuwezesha, ukimtumainia,
Piga simu ju mbinguni, daima utajibiwa.

9.
Kadi tama narudia, piga simu usichoke,
Mungu atakusikia, takwondolea upweke,
Yeye ukishamwambia, inabaki kazi kwake,
Piga simu ju mbinguni, daima utajibiwa.
-------------------------------------------------------------
Christopher R. Mwashinga
(Sauti Toka Ughaibuni)








MTI USIO NA TUNDA

1.
Pole nimekusikia, machozi nimeyaona,
Watu wamekununia, moyoni unasonona,
Watamani kukimbia, huzuni imekubana,
Mti usio na tunda, kamwe haupigwi mawe.

2.
Kama unapigwa mawe, usiku pia mchana,
Watu wenye chuki nawe, watamani kukuchana,
Jua mambo yako wewe, sasa yamekwisha fana,
Mti usio na tunda, kamwe haupigwi mawe.

3.
Kama watu wakusema, japo huna konakona,
Hiyo ni dalili njema, sali mshukuru Bwana,
Matunda yako ni mema, wengi wameshayaona,
Mti usio na tunda, kamwe haupigwi mawe.

4.
Kama wanaleta visa, matusi kukutukana,
Wakija kukutikisa, kwa yasiyo na maana,
Jua hayo kwako tisa, cheza piga danadana,
Mti usio na tunda, kamwe haupigwi mawe.

5.
Kama wakikusudia, kukufanyia hiyana,
Kutangazia dunia, kwamba wewe huna mana,
Ndugu yangu vumilia, jiepushe kuzozana,
Mti usio na tunda, kamwe haupigwi mawe.

6.
Kama hilo jua lako, liangazalo mchana,
Lamulika njia yako, tangu siku za ujana,
Hapo jua fyucha yako, ina upepo mwanana,
Mti usio na tunda, kamwe haupigwi mawe.


7.
Kama unapigwa mawe, kamshukuru Rabana,
Shukuru usichelewe, usianze kutukana,
Kwani mti wako wewe, wapendeza kwa shehena,
Mti usio na tunda, kamwe haupigwi mawe.

8.
Kama watupiwa mawe, na wazee na vijana,
Usiingie kiwewe, na kuanza kubishana,
Bali kwepa kila jiwe, kwa hekima yake Bwana,
Mti usio na tunda, kamwe haupigwi mawe.

9.
Beti tisa zinatosha, sihitaji sema sana,
Njia nimekuonesha, wewe mtu wa maana,
Watu wanapokutisha, wambie leo si jana,
Mti usio na tunda, kamwe haupigwi mawe.
----------------------------------------------------
Christopher R. Mwashinga
(Sauti Toka Ughaibuni)

JUA ZURI LITUALO
1.
Mchana ulipoanza, kwa radi nyingi na mvua,
Wenyeji walojibanza, walianza kutimua,
Wageni wakajifunza, kwa chozi kuomba dua,
Jua zuri litualo, kulitazama ni kheri.
2.
Tufani kila upande, imegoma kupungua,
Waipende wasipende, watu waweza ugua,
Wafanyaje wajilinde, na ugonjwa wa mafua?
Jua zuri litualo, kulitazama ni kheri.
3.
Mchana hadi jioni, hatukuliona jua,
Kisha pepo za kusini, zikavuma kwa hatua,
Zikaondoa tufani, mambo yakawa murua,
Jua zuri litualo, kulitazama ni kheri.
4.
Ni jioni ona jua, magharibi linatua,
Rangize kama maua, mwangaza unachanua,
Hali ya hewa murua, koti la mvua navua,
Jua zuri litualo, kulitazama ni kheri.
5.
Anga la kisamawati, hakuna wingu la mvua,
Huu sasa ni wakati, mandhari kufurahia,
Na kuweka mikakati, ubunifu kuibua,
Jua zuri litualo, kulitazama ni kheri.
6.
Mdomoni ninakiri, moyoni nimetambua,
Mambo yaliyo mazuri, yote ukiyachungua,
Mungu wetu mashuhuri, ndo aliyoyavumbua,
Jua zuri litualo, kulitazama ni kheri.
7.
Mambo mengi yapendeza, kama upinde wa mvua,
Hata mwenye makengeza, akiona atajua,
Ya kwamba Mungu muweza, apanga na kupangua,
Jua zuri litualo, kulitazama ni kheri.
8.
Wavaao nguo chafu, mambo wakishatibua,
Kwa matendo ya uchafu, maovu wakitubia,
Mungu wetu mtukufu, nguo zao atafua,
Jua zuri litualo, kulitazama ni kheri.
9.
Kama ua la waridi, furaha itachanua,
Na kama zabarijadi, Mungu atawachukua,
Kuwapatia zawadi, wokovu kufurahia,
Jua zuri litualo, kulitazama ni kheri.
10
Hivyo wewe mwenye dhambi, kwa nini wajisumbua?
Njoo na yako mavumbi, Mungu hatokuumbua,
Atakusafisha dhambi, nawe utashangilia,
Jua zuri litualo, kulitazama ni kheri.
11.
Akishafuta adhabu, juu akikuinua,
Utapendeza ajabu, zidi mwangaza wa jua,
Kwani yazidi dhahabu, bei alokununua,
Jua zuri litualo, kulitazama ni kheri.
----------------------------------------------------------
Christopher R. Mwashinga
(Sauti Toka Ughaibuni)


KUNA SIKU UTAVUNA

( A )

1.
Kila nipandapo mbegu, kwenye msimu wa mvua,
Nikatazamia njugu, nivune zikikomaa,
Watu wenye matendegu, wanakuja kuzing’oa,
Je nizidi panda mbegu, hata kama sitovuna?

2.
Kila ninapobandika, wao huja kubandua,
Na kila nikiandika, hufuta kwa kusugua,
Uchafu wameushika, mavazi hawajafua,
Je nizidi panda mbegu, hata kama sitovuna?

3.
Kila ninaposafisha, wao huja kuchafua,
Hata nikitakatisha, matope wanatupia,
Wajinga wasikitisha, akili zimedumaa,
Je nizidi panda mbegu, hata kama sitovuna?

4.
Kila ninapoanika, wao huja kuanua,
Na ninapovipachika, wao huja kupachua,
Kweli wamefilisika, wamekaushwa na jua,
Je nizidi panda mbegu, hata kama sitovuna?

5.
Kila nijengapo ghala, wao huja kubomoa,
Akili zao za swala, vitasa wanaving’oa,
Kama mchwa wanakula, kwa kweli wananiboa,
Je nizidi panda mbegu, hata kama sitovuna?
6.
Niendelee kupanda, kisha waje kuving’oa?
Au nijenge kibanda, na upanga kuunoa?
Vitu vyangu kuvilinda, waovu kuwatoboa?
Je nizidi panda mbegu, hata kama sitovuna?

( B )
7.
Pole sana mwanakwetu, hao wanakuzuzua,
Hao ni pepo si watu, umekwishawagundua,
Wakemee hao chatu, wachukulie hatua,
Panda mwanakwetu panda, kuna siku utavuna.

8.
Nasema usikubali, kamwe kuwasujudia,
Wakabili kwa maswali, lima na kupalilia,
Ukiimba na kusali, Mungu takupigania,
Panda mwanakwetu panda, kuna siku utavuna.

9.
Panda bila ya kuchoka, panda bila kuugua,
Wanenapo we ondoka, kula chako kitumbua,
Chakula unachopika, watashindwa kupakua,
Panda mwanakwetu panda, kuna siku utavuna.

10
Bandika kwa ujasiri, usijali wenye ngoa,
Ujinga wataukiri, watapovuna mabua,
Wavivu wa kufikiri, bure wanajiumbua,
Panda mwanakwetu panda, kuna siku utavuna.

11.
Anika usiogope, hakuna wakuanua,
Wakiyarusha matope, kwepa kwa sala na dua,
Zifungue zako kope, njia umeshaijua,
Panda mwanakwetu panda, kuna siku utavuna.

12.
Safisha na kusafika, watashindwa kuchafua,
Watasita kukushika, ukizungukwa na jua,
Mwisho wataaibika, nuru itawafichua,
Panda mwanakwetu panda, kuna siku utavuna.

13.
Pika chakula kitamu, kunywa juisi ya mua,
Jiandalie karamu, pamba meza kwa maua,
Harufu ya marhamu, itawale kila pua,
Panda mwanakwetu panda, kuna siku utavuna.

14.
Uliwazalo moyoni, lifanye kwa kuamua,
Wenye wivu hawaoni, heshima wamejivua,
Wamefika ukingoni, jua lao linatua,
Panda mwanakwetu panda, kuna siku utavuna.

15
Tamaa usikatishwe, na wasiojitambua,
Simama upendezeshwe, ukang’are kama jua,
Waovu waaibishwe, wabaki kusuasua,
Panda mwanakwetu panda, kuna siku utavuna.

16.
Beti hizi zakutosha, ugomvi acha kuzua,
Wanataka kukuchosha, upate kujilipua,
Kwako Yesu anatosha, kesho yako ni murua,
Panda mwanakwetu panda, kuna siku utavuna.
-------------------------------------------------------
Christopher R. Mwashinga
(Sauti Toka Ughaibuni)





















MWANAMKE NDO KIPIMO

1.
Kama wataka kujua, jamii yako ilipo,
Kama inaendelea, kwa mapato na malipo,
Au inasuasua, kwa kudhani nayo ipo,
Mwanamke ndo kipimo, cha ukuu wa taifa.
2.
Ukiona mwanamke, mapato yake madogo,
Na pia elimu yake, imezungukwa na zogo,
Jua hiyo nchi yake, uchumi wake mdogo,
Mwanamke ndo kipimo, cha ukuu wa taifa.
3.
Ukiona mwanamke, atembea kwa miguu,
Kabeba watoto wake, pamoja na wajukuu,
Jua usafiri kwake, ndo tatizo lake kuu,
Mwanamke ndo kipimo, cha ukuu wa taifa.
4.
Ukiona mwanamke, anabebwa machelani,
Na kujifungua kwake, siku zote ni nyumbani,
Jua hiyo afya yake, ndiyo kero ya moyoni,
Mwanamke ndo kipimo, cha ukuu wa taifa.
5.
Ukiona mwanamke, anabeba zake kuni,
Pamoja na maji yake, mgongoni na kichwani,
Jua familia yake, haina raha nyumbani,
Mwanamke ndo kipimo, cha ukuu wa taifa.
6.
Ukiona mwanamke, pekupeku atembea,
Mavumbi kichwani mwake, huku anachechemea,
Ujue uchumi wake, umekwishatokomea,
Mwanamke ndo kipimo, cha ukuu wa taifa.
7.
Ukiona mwanamke, mdomowe umezibwa,
Makovu mwilini mwake, kila siku anazabwa,
Jua maishani mwake, haki zake zimeibwa,
Mwanamke ndo kipimo, cha ukuu wa taifa.
8.
Ukiona mwanamke, machozi tele shavuni,
Kapoteza sura yake, kwa kutopata sabuni,
Ujue moyoni mwake, mwisho uko karibuni,
Mwanamke ndo kipimo, cha ukuu wa taifa.
9.
Mwanamke ndo kipimo, cha nchi ilositawi,
Kama shina kwenye shimo, na matunda kwenye tawi,
Mwanamke ni kipimo, cha nchi ilositawi,
Mwanamke ndo kipimo, cha ukuu wa taifa.
10
Kamwe nchi haikui, kumpita mwanamke,
Na hata kama hajui, yeye ndo kipimo chake,
Mawingu hayapungui, mpaka apate chake,
Mwanamke ndo kipimo, cha ukuu wa taifa.
11.
Kaditama namaliza, kompyuta naweka chini,
Uanze kujiuliza, yatafakari moyoni,
Kisha ukisha maliza, jadili mtandaoni,
Mwanamke ndo kipimo, cha ukuu wa taifa.
---------------------------------------------------------
Christopher R. Mwashinga
(Sauti Toka Ughaibuni)

TUMEITWA TUWE TOFAUTI
1.
Tumeitwa na Mwokozi, ili tuwe tofauti,
Ili tuwe mabalozi, tupaze zetu sauti,
Tutangaze ukombozi, kwa walio mahututi,
Tumeitwa na Mwokozi, ili tuwe tofauti.
2.
Tumeitwa na Mwokozi, tukatembee nuruni,
Ili tuwe viongozi, kuelekeza mbinguni,
Tuwaonye wachokozi, wasiilete huzuni,
Tumeitwa na Mwokozi, ili tuwe tofauti.
3.
Tumeitwa naye Bwana, tuongee kwa hekima,
Usiku pia mchana, tuioneshe heshima,
Matusi kwetu hapana, hayo hayana uzima,
Tumeitwa na Mwokozi, ili tuwe tofauti.
4.
Tumeitwa naye Yesu, tufundishe neno lake,
Tuwaonye mahabusu, waume na wanawake,
Dunia yote si nusu, waamini jina lake,
Tumeitwa na Mwokozi, ili tuwe tofauti.
5.
Tumeitwa kwa pamoja, tuwapende watu wote,
Rangi zao sio hoja, tuwahudumie wote,
Tuache kungojangoja, tuwape huduma zote,
Tumeitwa na Mwokozi, ili tuwe tofauti.
6.
Tumeitwa naye Mungu, tuepuke ufisadi,
Tusiyalete machungu, kwa kutotunza ahadi,
Kuwapiga watu rungu, ili kupata miradi,
Tumeitwa na Mwokozi, ili tuwe tofauti.
7.
Tumeitwa na Mwokozi, kuishi maisha safi,
Kuuepuka ulozi, ngono chafu na ulafi,
Kukataa udokozi, kuiba samaki chafi,
Tumeitwa na Mwokozi, ili tuwe tofauti.
8.
Tumeitwa na Mwokozi, wenye njaa tuwalishe,
Wagonjwa wa kikohozi, maji safi tuwanyweshe,
Wasokuwa na mavazi, walo uchi tuwavishe,
Tumeitwa na Mwokozi, ili tuwe tofauti.
9.
Tumeitwa naye Bwana, tuhudumiye yatima,
Wajane walojazana, kwenye bonde na milima,
Wasichana wavulana, wapewe zote huduma,
Tumeitwa na Mwokozi, ili tuwe tofauti.
10
Tumeitwa kuwa chumvi, kuinusuru dunia,
Na wazee wenye mvi, tupate wahurumia,
Tuwapatie majamvi, mazuri yakulalia,
Tumeitwa na Mwokozi, ili tuwe tofauti.
11
Tumeitwa na Mwokozi, ili tuwe tofauti,
Tueneze hii njozi, imara na madhubuti,
Watu wafutwe machozi, kwa pendo bila shuruti,
Tumeitwa na Mwokozi, ili tuwe tofauti.
12
Kaditama namaliza, nampigia saluti,
Bwana alotuagiza, tuishi kitofauti,
Tuwe nuru siyo giza, kumfata hatujuti,
Tumeitwa na Mwokozi, ili tuwe tofauti.
-------------------------------------------------------
Christopher R. Mwashinga
(Sauti Toka Ughaibuni )

SIRI SI SIRI TENA

1.
Siri sii siri tena, itokapo kwa mmoja,
Jambo ukishalinena, hata kwa mtu mmoja,
Hilo sii siri tena, tayari limeshavuja,
Siri sii siri tena, itokapo mdomoni.
2.
Mwingine ukimwambia, hapo siri imekufa,
Hata kama ukilia, umeshaupata ufa,
Na usipoangalia, utayapata maafa,
Siri sii siri tena, itokapo mdomoni.
3.
Aweza kuwa rafiki, pale unapomwambia,
Akakufaa kwa dhiki, huduma kukupatia,
Maneno kama muziki, sikioni kukwambia,
Siri sii siri tena, itokapo mdomoni.
4.
Siku akibadilika, utaisoma nambari,
Juani takuanika, bila kujali hatari,
Wewe ukihangaika, yeye taona fahari,
Siri sii siri tena, itokapo mdomoni.
5
Siri ukishaitoa, rafikiyo kumwambia,
Aweza kukutoboa, huwezi kumzuia,
Nyundo ya kukubomoa, umekwishampatia,
Siri sii siri tena, itokapo mdomoni.
6.
Kumdhibiti huwezi, umeshampa upanga,
Umejipa utelezi, umeshafanya ujinga,
Akikwita mtembezi, ni vigumu kumpinga,
Siri sii siri tena, itokapo mdomoni.
7.
Aweza kukutangaza, kila kona ya dunia,
Chini kukugaragaza, bila kukuhurumia,
Hata ukimkataza, hawezi kukusikia,
Siri sii siri tena, itokapo mdomoni.
8.
Hivyo hiyo siri yako, ukipenda iwe siri,
Itunze moyoni mwako, kamwe usiihubiri,
Leo umakini wako, kesho utakusitiri,
Siri sii siri tena, itokapo mdomoni.
9
Kushindwa kutunza siri, ni ugonjwa wa mauti,
Kama unao tayari, wewe sasa mahututi,
Wahitaji daktari, mwenye nguvu madhubuti,
Siri sii siri tena, itokapo mdomoni.
10.
Mwombe Mungu wa mbinguni, ushindi akupatie,
Uiepuke huzuni, mauti uyakimbie,
Uwapo ulimwenguni, maisha ufurahie,
Siri sii siri tena, itokapo mdomoni.
----------------------------------------------------------
Christopher R. Mwashinga
(Sauti Toka Ughaibuni)

USIACHE MBACHAO

1.
Mambo unayotafuta, si muhimu udhanivyo,
Kuna siku utajuta, kuacha uviachavyo,
Pale utapojikuta, yakienda ndivyo sivyo,
Ndugu siache mbachao, kwa msala upitao.
2.
Uyaachayo muhimu, kuliko utafutayo,
Usikimbiliye simu, picha nzuri itumayo,
Na kuidharau simu, nyumbani itumikayo,
Ndugu siache mbachao, kwa msala upitao.
3.
Usimdharau mtu, unayejuana naye,
Kwa sababu hana kitu, ukafata apitaye,
Anayetamani vitu, hatamwona afaaye,
Ndugu siache mbachao, kwa msala upitao.
4.
Usikimbile-kimbile, kumtukana swahibu,
Kwa kuwa lake umbile, linamwitaji tabibu,
Kwa sababu apitile, mwenye bawa la dhahabu,
Ndugu siache mbachao, kwa msala upitao.
5.
Ukidharau mzazi, kwa sababu hajasoma,
Au avaa mavazi, ya mgonjwa wa ukoma,
Utapigwa kiangazi, cha jua lisilokoma,
Ndugu siache mbachao, kwa msala upitao.
6.
Ukimwacha mwenzi wako, kwa kufata mpitaji,
Asojua moyo wako, atafutaye mtaji,
Tapoteza njozi yako, na kunywewa kama maji,
Ndugu siache mbachao, kwa msala upitao.
7.
Vitu unavyoviona, vingi vyapita upesi,
Ukizidisha kutuna, kama mtungi wa gesi,
Mwishowe utafanana, na mti wa mafenesi,
Ndugu siache mbachao, kwa msala upitao.
8.
Wachumao watachuma, faida hutoiona,
Utapoteza heshima, utabaki kusonona,
Tumia yako hekima, kumtegemea Bwana,
Ndugu siache mbachao, kwa msala upitao.
9.
Beti tisa namaliza, nimekwisha kukuonya,
Kisasi ukilipiza, huko ni kujidanganya,
Hayo ni mambo ya giza, bure yatakuchanganya,
Ndugu siache mbachao, kwa msala upitao.
---------------------------------------------------------
Christopher R, Mwashinga
(Sauti Toka Ughaibuni)

AKILI BILA HEKIMA

1. 

Mwanakwetu sikiliza, neno langu zingatia,
Swali wakikuuliza, jibu kwa kufikiria,
Hekima ishinde giza, nuru ijaze dunia,
Akili bila hekima, ni jua bila mwangaza.
2.
Kunena kwa mhemko, bila ya kufikiria,
Kunaleta machafuko, kila kona ya dunia,
Usifanye matamko, yanayoleta udhia,
Akili bila hekima, ni jua bila mwangaza.
3.
Mwache anayeropoka, aropoke kwa hisia,
Naye anayecharuka, azunguke kama pia,
Lakini wewe kumbuka, nuru ishakuzukia,
Akili bila hekima, ni jua bila mwangaza.
4.
Mwache anayepayuka, huku akijisifia,
Bure anabwabwajika, nuruye imefifia,
Huyo ameshachachuka, busara zimemwishia,
Akili bila hekima, ni jua bila mwangaza.
5.
Mwache anayetangaza, walimwengu kuwambia,
Mambo yanayodumaza, anayoyakumbatia,
Maneno akisambaza, watu watamkimbia,
Akili bila hekima, ni jua bila mwangaza.
6.
Maneno yako yapime, kwa makini fikiria,
Kama mashamba yalime, palizi kuyapatia,
Kwa kisu au kwa sime, yachonge yawe sawia,
Akili bila hekima, ni jua bila mwangaza.
7.
Mdomoni yakitoka, kwa makumi na mamia,
Yapoze waliochoka, na wote wanaolia,
Na waliokasirika, wacheke kupindukia,
Akili bila hekima, ni jua bila mwangaza.
8.
Maneno yawe machache, ongea kwa kutulia,
Wabishibishi waache, huo ni wangu wosia,
Wote wamekuwa kwache, mambo yanawarudia,
Akili bila hekima, ni jua bila mwangaza.
9.
Beti tisa naishia, mkono nakupungia,
Kazi ukiyafanyia, mambo niliyokwambia,
Hutachoka kumwimbia, Mungu ukishangilia,
Akili bila hekima, ni jua bila mwangaza.
-------------------------------------------------------------------
Christopher R. Mwashinga
(Sauti Toka Ughaibuni)