Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

MAWASILIANO KATIKA NDOA

MAWASILIANO KATIKA FAMILIA

FAMILIA, MAWASILIANO, NA UREJESHWAJI.
Familia ilianza na mtu mmoja. “Adamu akawapa majina yao kila mnyama wa kufugwa, na ndege wa angani, na kila mnyama wa mwituni; lakini hakuonekana wa kumsaidia Adamu aliyefanana naye." (Mwanzo 2:20) Hata katika hatua hiyo ya binadamu mmoja bado yalikuwapo mawasiliano. Familia kwa maana hii inahusisha na mazingira yanayomzunguka mtu. Kuna familia zenye mbwa, paka, ngombe, na mifugo mingine ambayo ina nafasi katika bajeti ya kifamilia na hata wana majina waliyopewa na familia. Mtu aliye mmoja kwa hiyo anatambulika kuwa yupo kwenye familia. Hata hivyo ni ukweli usiopingika kwamba familia inakuwa imekamilika zaidi ikiwa ina mume na mke.

Hali hiyo ya familia kuwa na mtu mmoja haikumvutia Mungu na hivyo akaitafutia majibu. “Bwana Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye.” (
Mwanzo 2:18) Mungu hakustukizwa na hali hiyo ya upungufu katika familia ya Adamu, bali aliijua tangu awali kuwa angehitaji mwenzi wa maisha. Umuhimu wa familia kuwa na zaidi ya mtu mmoja imefafanuliwa katika kitabu cha Mhubiri. Mhubiri 4:9-10 “Afadhali kuwa wawili kuliko mmoja; Maana wapata ijara njema kwa kazi yao. Kwa maana wakianguka, mmoja wao atamwinua mwenzake; lakini ole wake aliye peke yake aangukapo, wala hana mwingine wa kumwinua!”

Lakini dhambi imetengeneza mazingira ambayo wakati fulani huwa ni vema kwa mtu kukaa peke yake bila kuoa au kuolewa. “Wanafunzi wake wakamwambia, Mambo ya mtu na mkewe yakiwa hivyo, haifai kuoa. Lakini yeye akawaambia, Si wote wawezao kulipokea neno hili, ila wale waliojaliwa. Maana wako matowashi waliozaliwa hali hiyo toka matumboni mwa mama zao; tena wako matowashi waliofanywa na watu kuwa matowashi; tena wako matowashi waliojifanya kuwa matowashi kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Awezaye kulipokea neno hili, na alipokee.” (
Mathayo 19:10-12)

Kabla ya dhambi familia ilikuwa mahali bora pa kuishi. Watu walielewana na kupendana kila mmoja akitumikia furaha ya mwenzake. Dhambi ikaleta tatizo kubwa katika mawasiliano na mahusiano ya mume na mke.  Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala." (
Mwanzo 3:12) Hali ya kulaumiana iliharibu uhusiano kati ya mume na mke na kati yao na Mungu wa mbinguni. Hali hiyo ilivuruga uhusiano baina yao na mazingira yao na viumbe vilivyowazunguka. "Michongoma na miiba itakuzalia, nawe utakula mboga za kondeni." (Mwanzo 3:18)

Hali hiyo iliendelea kuiathiri familia kwa vizazi vyote vilivyofuata. Mtoto wa kwanza wa Adamu aitwaye Kaini alimuua mdogo wake Habili baada ya kutofautiana katika maswala ya ibada hapo nyumbani kwao. Mwanzo 4:8 “Kaini akamwambia Habili nduguye, Twende uwandani Ikawa walipokuwapo uwandani, Kaini akamwinukia Habili nduguye, akamwua.” Hata mahusiano ya wazazi na watoto yaliendelea kuzorota.  Mwanzo 9:22-23 “Hamu, baba wa Kanaani, akauona uchi wa baba yake, akawaeleza ndugu zake wawili waliokuwa nje. Shemu na Yafethi wakatwaa vazi, wakalitanda mabegani mwao wote wawili, wakaenda kinyumenyume, wakaufunika uchi wa baba yao; na nyuso zao zilielekea nyuma, wala hawakuuona uchi wa baba yao.”

Hali hii ya kurejeshwa kwa mawasiliano na mahusiano katika familia iliyooneshwa na Shemu na Yafeti kwa baba yao, imetabiriwa kutokea katika siku za usoni karibu na kufungwa kwa historia ya dunia. Malaki 4:5-6 “Angalieni, nitawapelekea Eliya nabii, kabla haijaja siku ile ya Bwana, iliyo kuu na kuogofya. Naye ataigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto wao, na mioyo ya watoto iwaelekee baba zao, ili nisije nikaipiga dunia kwa laana.”

Mafungu hayo yanatabiri kuwapo kwa watu watakaohubiri injili ya milele yenye kuinua haki ya Kristo itakayolegeza mioyo ya wazazi iwaelekee watoto nay a watoto iwaelekee wazazi wao. Jambo moja unalilisikia mara nyingi ni wazazi kuwalalamikia watoto wao na watoto kuwalalamikia wazazi wao kuwa hawawapi muda wao. Kuna msemo kwa wazazi kuwa watoto wanapokuwa watoto wanatukanyaga miguuni lakini wakiwa wakubwa wanatukanyaga mioyoni. Lakini watoto nao wanalalamika kuwa wazazi hupenda kujigamba kuwa walipokuwa watoto hawakuwa wajinga wala hawakufanya yale maovu watoto wanayotenda jambo ambalo watoto wamekuwa wakitilia mashaka.

Watoto wanadai wanajua kinachoendelea kwa wazazi wao kuliko wazazi wanavyojua kinachoendelea kwa watoto wao. Watoto wanasema ni rahisi kupata ushauri kutoka kwa wale wa rika lao (maana wanapatikana) kuliko kupata ushauri kutoka kwa wazazi wao – kwa kuwa ama hawapatikani ama hawana ushirikiano (ni wakali). Njia ya kulisuluhisha hilo ni kwa wazazi kutowachokoza watoto na watoto kutokosa kuwatii wazazi wao. Wakolosai 3:21 “Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, wasije wakakata tamaa.” Wakolosai 3:20 “Ninyi watoto, watiini wazazi wenu katika mambo yote; maana jambo hili lapendeza katika Bwana.”

Nyumbani ni mahali pa kuvutia kwa kuwa kila mmoja huweza kutekeleza jukumu lake na lile la mwanafamilia mwingine bila kushurutishwa wala manung’uniko. Baba anaweza kubeba mtoto mgongoni mama anapokuwa hayupo nyumbani na mama kujaribu kubadilisha balbu iliyo juu sana baba anapokuwa nyumbani. Nyumbani ndipo mahali ambapo havikomi vitu vya kuwafanya mcheke na kufurahi. Nyumbani ndipo mahali ambapo watu husahihishana kwa upendo. Waefeso 4:31 “Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya.” Wakolosai 3:8-9 “Lakini sasa yawekeni mbali nanyi haya yote, hasira, na ghadhabu, na uovu, na matukano, na matusi vinywani mwenu. Msiambiane uongo, kwa kuwa mmevua kabisa utu wa kale, pamoja na matendo yake.”

Kutoambiana uongo ni kumaanisha ulichosema, na kusikia kilichomaanishwa. Wataalam wa mawasiliano wanatuambia kuwa kuna ngazi tano za mawasiliano. Mawasiliano ya mtu mmoja. Mawasiliano ya watu wawili, mwasiliano ya kikundi, mawasiliano ya halaiki, na mawasiliano ya umma. Katika hatua ya somo la leo ambapo tunajielekeza katika kuboresha mawasiliano nyumbani tutaangalia hatua ya kwanza na ya pili na kidigo hatua ya tatu.

Mawasiliano ni kitu kisichoepukika na kinachofanyika wakati wote (hata unapokuwa umelala), kwa sababu unawasiliana hata pale unapokuwa hujakusudia kuwasiliana. Ili ujumbe uwe na ufanisi ni lazima uwe wazi (usio na uwezekano wa kuleta tafsiri isiyokusudiwa), sahihi (si habari zisizothibitishwa), unaohitajika na mpokeaji, na unaofaa kwa wakati husika.

Kwa kawaida tunawasiliana ili kupashana mawazo, hisia, taarifa, uzoefu, na maarifa. Ili tuwasiliane tunatumia maneno (ya kuandikwa ama kutamkwa), lugha ya mwili, picha, na ishara zinginezo zenye uwezo wa kufikisha ujumbe uliokusudiwa. Katika hali ya kawaida mawasiliano yanahitaji mtoaji, ujumbe unaotumwa, njia inayotumika kuutuma, mpokeaji, na mrejesho. 
Kuwasiliana ni tofauti na kushauri. Kushauri ni kumsaidia mteja kufanya maamuzi yake mwenyewe kwa kumpatia taarifa zisizoegemea upande mmoja na kwa kumuuliza mteja anachotaka na anachoweza kufanya kukabili hali iliyopo.

(Intrapersonal Communication): Mawasiliano binafsi
Haya ni mawasiliano yanayofanyika kwenye akili yako mara nyingi kimya kimya ingawa wakati fulani hufanyika kwa sauti. Hapa ndipo kituo cha hisia zetu, imani zetu,  misimamo yetu na maamuzi yetu. Luka 15:18 “Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako.”
Interpersonal Communication): Mawasiliano ya wawili
Haya ni mawasiliano baina ya watu wawili. Katika mawasiliano haya kuna uwezekano wa maana iliyokusudiwa kupotoshwa. Mwanzo 3:10 Akasema, Nalisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha.

Kusikiliza ni fani inayohitaji umakini
Kusema siyo jambo la kukimbilia kulifanya kwani linahitaji ustadi na weledi. Ubora wa kilichosema hupimwa kwa matokeo yake. Hivyo kilichosemwa kitakuwa na umuhimu pale kitapoweza kufikisha ujumbe uliokuwa umekusudiwa. “Hayo mnajua, ndugu zangu wapenzi. Basi kila mtu na awe mwepesi wa kusikia, bali si mwepesi wa kusema; wala kukasirika.” (Yakobo 1:19) Yesu anasema “Mtu akiwa na masikio ya kusikilia, na asikie.” (Marko 4:23). Yesu hapa anamaanisha si kila mwenye masikio aweza kusikia kwa kuwa kusikia huja pale masikio yanapopewa uwezo wa kusikia kile kisichosikiwa na masikio mengine. Kile kilichobebwa na ujumbe na ambacho hakionekani wazi wazi kwa msikilizaji wa juu juu.

Kusikia na kusikiliza:
Kusikiliza ni kujaribu kuzielewa hisia za mwingine. Ni kukubali kile kinachosemwa bila kuhukumu mantiki yake ama namna kinavyosemwa. Kukubali haimaanishi kukubaliana moja kwa moja na msimamo wa msemaji bali ni kutambua na kuelewa kuwa kilichosemwa ndicho msemaji anachokihisi na anachomaanisha. Kusikiliza pia humaanisha uwezo wa kurudia kilichosemwa katika jitihada za kujiridhisha kama ulichoelewa ndicho kilichokusudiwa na kilichokuwa kwenye hisia za mzungumzaji. Ni lazima ujiridhishe kama kile unachokusudia kukiweka kwenye kumbukumbu zako ni kile kilichomaanishwa na mzungumzaji au ni tafsiri yako tu isiyo sahihi.

Wataalam wa mawasiliano wanadai kuwa, ujumbe unaotumwa na mwanadamu yeyote unabebwa na vitu vitatu. Asilimia 7 ya ujumbe inabebwa na sauti, asilimia 38 inabebwa na mkao wa sauti, wakati asilimia 55 inabebwa na lugha ya mwili. Tunatakiwa tusikilize kile kilicho nyuma ya maneno ambacho ndicho hubeba ujumbe wenyewe – yaani mkao wa sauti na lugha ya mwili. Kusikia ni tofauti na kusikiliza. Kusikia ni kutambua kinachoendelea kwenye akili ya mzungumzaji na utayari wa kukipokea kwa utekelezaji wakati kusikiliza ni vile akili yangu inavyokipokea inachosikia na inavyoathirika nacho. Kwenye kusikia tunatafsiri na kujaribu kuelewa kile tulichosikia.

Wakati fulani kukaa kimya ni njia bora zaidi ya kuonesha unasikia. Mithali 17:27-28 “Azuiaye maneno yake ni mwenye maarifa; Na mwenye roho ya utulivu ana busara. Hata mpumbavu akinyamaza, huhesabiwa hekima; Akifumba midomo yake, huhesabiwa ufahamu.” Mithali 21:23 “Mtu azuiaye kinywa chake na ulimi wake, Atajilinda nafsi yake na taabu.” Mithali 26:20 Moto hufa kwa kukosa kuni; Na bila mchongezi fitina hukoma.

Usitarajie ukamilifu kwenye familia yako,
kwa kuwa hapo ndani hayupo mkamilifu. Na kama unataka kubadilisha hali hiyo anzia kwako wewe mwenyewe. Mhubiri 7:20 “Bila shaka hakuna mwanadamu mwenye haki hapa duniani, ambaye afanya mema, asifanye dhambi.” 1 Yohana 1:8 “Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu.” Zaburi 14:3 “Wote wamepotoka, wameoza wote pamoja, Hakuna atendaye mema, La! Hata mmoja.” Warumi 7:18 “Kwa maana najua ya kuwa ndani yangu, yaani, ndani ya mwili wangu, halikai neno jema; kwa kuwa kutaka nataka, bali kutenda lililo jema sipati.” Luka 18:19 “Yesu akamwambia, Mbona unaniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, naye ndiye Mungu.”

Shughulikieni tofauti zenu mapema.
Wakolosai 3:19 “Ninyi waume, wapendeni wake zenu msiwe na uchungu nao.” Waefeso 4:26 “Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka.”

Msikumbushane dhambi mlizosameheana.
Isaya 43:25 “Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe, wala sitazikumbuka dhambi zako.” Luka 23:34 “Yesu akasema, Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo. Wakagawa mavazi yake, wakipiga kura.”

Msilipize kisasi.
Warumi 12:19 “Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana.

Kumbukeni Mungu anawapenda wadhambi.
Marko 2:17 Yesu aliposikia aliwaambia, Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi; sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi. Warumi 5:8 “Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi.” 1 Yohana 3:1 “Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye.” Warumi 8:32-33 “Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye? Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki.” Tumeokolewa kwa neema kwa njia ya imani. Waefeso 2:8-9 “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu.”