Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

BARUA YA MFALME

BARUA KUTOKA KWA MFALME
 
Maandiko Matakatifu yanatujulisha kuwa hakuna utawala wa kidunia uwe wa kisiasa au wa kidini utakaotawala dunia nzima kwa wakati huu. Utawala wa mwisho uliotawala dunia nzima ulikuwa wa Kirumi na sasa utawala huo haupo duniani na jitihada zozote za kuuibua utawala huo kwa njia yoyote hautafanikiwa, maana utawala pekee unaongojewa kwa sasa ni utawala wa Kristo unaofananishwa na jiwe lisilochongwa na binadamu. "Ndipo kile chuma, na ule udongo, na ile shaba, na ile fedha, na ile dhahabu, vilivunjwa vipande vipande pamoja vikawa kama makapi ya viwanja vya kupepetea wakati wa hari; upepo ukavipeperusha hata pasionekane mahali pake; na lile jiwe lililoipiga hiyo sanamu likawa milima mikubwa, likaijaza dunia yote." (Danieli 2:35)
 
BARUA YA MFALME KWA RAFIKI ZAKE

Kila binadamu ana shauku ya kujua alikotoka. Ukijikuta ukiishi bila baba au mama na kisha ukadokezwa kuwa wazazi wako hao wawili au mmojawapo yupo hai, utafanya kila jitihada kufahamu alipo ili ukutane naye. Ukiangalia ulimwengu huu ulivyoratibiwa ni rahisi kujua kuwa kuna aliyeuratibu. Katika jamii nyingi huyu aliyeuratibu aliitwa kwa majina mbalimbali kadri walivyosukumwa mioyoni mwao. "Kwa sababu nilipokuwa nikipita huko na huko na kuyaona mambo ya ibada yenu, naliona madhabahu iliyoandikwa maneno haya, KWA MUNGU ASIYEJULIKANA. Basi mimi nawahubirini habari zake yeye ambaye ninyi mnamwabudu bila kumjua." (Matendo 17:23). Mungu huyu amejifunua kupitia vitu vya asili. Lakini amejifunua kikamilifu zaidi kupitia Maandiko Matakatifu yaani Biblia. Kupitia Maandiko Matakatifu tunaweza kufahamu tutokako, tulipo, kule tuendako na kwa nini tupo hapa. Hii ndiyo barua yako kutoka kwa mfalme.
 
BIBLIA NI KITABU CHA NAMNA GANI?

Biblia ni neno ambalo kwa asili linatokana na lugha ya Kiyunani na Kilatini likimaanisha kitabu au mkusanyiko wa vitabu. Kitabu hiki kimegawanyika sehemu kuu mbili; sehemu ya kwanza iitwayo Agano la Kale ikizungumzia kisa cha taifa la Israeli na sehemu ya pili iitwayo Agano Jipya ikizungumzia habari za mtu mmoja aitwaye Yesu Kristo. Biblia yenye vitabu 66 imegawanyika sehemu mbili; ile ya kwanza inaitwa Agano la Kale na ile ya pili inaitwa Agano Jipya. Agano Jipya ina vitabu 39 na Agano Jipya 27

UMUHIMU WA BIBLIA
 
Ndani ya Biblia Mungu amempatia mwanadamu maarifa yaliyo ya lazima kwa ajili ya wokovu. “Na ya kuwa tangu utoto umeyajua maandiko matakatifu, ambayo yaweza kukuhekimisha hata upate wokovu kwa imani iliyo katika Kristo Yesu. Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki.” (2 Timotheo 3:15) Ni kweli kuwa hata leo yapo mambo ambayo wanadamu tungetamani tuyajue lakini kwa hekima yake Mungu amezuia tusiyajue kwa kuwa hayana umuhimu kwa wokovu wetu. “Mambo ya siri ni ya Bwana, Mungu wetu; lakini mambo yaliyofunuliwa ni yetu sisi na watoto wetu milele, ili tuyafanye maneno yote ya sheria hii.” (Kumbukumbu 29:29)
 
Biblia ni ufunuo wenye mamlaka juu ya mafundisho ya imani. Kila imani ya kweli ni lazima ijikite kwenye kile kilichofunuliwa na Maandfiko Matakatifu. “Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.” (Warumi 10:17). Maandiko Matakatifu yanamfunua Yesu Kristo na kupitia kwake watu wanapata uzima wa milele.  “Mwayachunguza maandiko, kwa sababu mnadhani kwamba ninyi mna uzima wa milele ndani yake; na hayo ndiyo yanayonishuhudia." (Yohana 5:39)
 
Biblia imejaa kumbukumbu za kuaminika za matendo ya Mungu katika historia.  "Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli." (Yohana 17:17). Ukweli kuhusu mwanadamu ametokana na nini na ulimwengu huu ulitokeaje zipo ndani ya Biblia. “Mungu aliyeufanya ulimwengu na vitu vyote vilivyomo, yeye, kwa kuwa ni Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika hekalu zilizojengwa kwa mikono; wala hatumikiwi kwa mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji kitu cho chote; kwa maana ndiye anayewapa wote uzima na pumzi na vitu vyote. Naye alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika mmoja, wakae juu ya uso wa nchi yote, akiisha kuwawekea nyakati alizoziamuru tangu zamani, na mipaka ya makazi yao; ili wamtafute Mungu, ingawa ni kwa kupapasa-papasa, wakamwone, ijapokuwa hawi mbali na kila mmoja wetu.” (Matendo 17:24-27).
 
Biblia pia ni taa iangazayo gizani. “Neno lako ni taa ya miguu yangu, na mwanga wa njia yangu.” (Zaburi 119:105). Maisha ya mwanadamu yamejaa changamoto nzito zinazohitaji ufumbuzi kama mtembezi wa usiku anavyohitaji taa kumulikia njia yake. Kwa msaada wa Neno la Mungu mtu huweza kuishinda dhambi. “Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi.” (Zaburi 119:11). Kama dunia ingeifanya Biblia kuwa kitabu muhimu kinachosomwa na kueleweka na wote, ujinga, umaskini, na maradhi vingeweza kutokomezwa kwa kiasi kikubwa. Biblia ina uwezo wa kuhekimisha kuliko kitabu kingine chochote. "Na ya kuwa tangu utoto umeyajua maandiko matakatifu, ambayo yaweza kukuhekimisha hata upate wokovu kwa imani iliyo katika Kristo Yesu." (2 Timotheo 3:15)
 
NENO LA MUNGU NI KAMILIFU:

Maandiko Matakatifu huitwa pia Neno au Neno la Mungu. Neno hili limehakikishwa ili watumiaji wake wasipotoshwe. “Kila neno la Mungu limehakikishwa; Yeye ni ngao yao wamwaminio.” (Mithali 30:5). Vitabu vinavyopatikana katika Neno la Mungu vimethibitishwa kuwa vinatokana na uvuvio wa Mungu na kazi hiyo ilifanywa na watu waaminifu waliozingatia vigezo mbalimbali. Baada ya kufanyiwa mchujo vitabu 66 vilipasishwa na vingine 6 kukataliwa. Maandiko hayahitaji nyongeza au kupunguza kwa maneno. “Usiongeze neno katika maneno yake; Asije akakulaumu, ukaonekana u mwongo.” (Mithali 30:6)
 
MUNGU SI KIGEUGEU:

Mungu ndiye mwandishi wa Maandiko Matakatifu. Anakuwa mwandishi kwa sababu mawazo yaliyopo katika kitabu kizima ni yake, ila aliwatumia wanadamu kuandika kwa lugha na mtazamo wao wa kibinadamu. Mungu kupitia Roho Mtakatifu aliwavuvia wanadamu mawazo yake, na waliojaliwa kuvuviwa ambao Biblia huwaita manabii wakayasema ama kuyaandika mawazo hayo kwa wanadamu wenzao. “Maana unabii haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu.” (2 Petro 1:21). Kawaida ya Mungu ni kutokosea na kutobadilika katika kauli zake. “Mimi sitalihalifu agano langu, Sitalibadili neno lililotoka midomoni mwangu.” (Zaburi 89:34). Yeye ni mwangalifu katika kutoa matamko yake, kiasi ambacho haiwezekani matamko yake yapishane au kupingana. Yeye hana kigeugeu kama wanadamu ambao hubadilisha kauli zao kila wanapohisi maslahi yao fulani yapo hatarini. “Mungu si mtu, aseme uongo; Wala si mwanadamu, ajute; Iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena, hatalifikiliza?” (Hesabu 23:19). Faida kubwa ya kuamini Maandiko Matakatifu ni kwamba yana kauli za kuaminika zisizobadilika badilika. “Kwa kuwa mimi, Bwana, sina kigeugeu; ndio maana ninyi hamkuangamizwa, enyi wana wa Yakobo.” (Malaki 3:6). Mungu ameahidi kutolibadili neon lililotoka midomoni mwake. “Mimi sitalihalifu agano langu, Sitalibadili neno lililotoka midomoni mwangu.” (Zaburi 89:34)
 
Matakatifu hayana kawaida ya kujipinga hasa katika mambo ya msingi. Hata zile tofauti ndogo ndogo zinazoweza kujitokeza zinatokana na watu zaidi ya mmoja kulielezea jambo moja katika mitazamo tofauti ama zinatokana na msomaji kushindwa kuulewa ujumbe uliokusudiwa katika fungu husika kutokana na kutozingatia kanuni za kutafsiri Maandiko. Biblia inatudokezea njia salama ya kusoma maandiko ili kuepuka kupata tafsiri potofu ni kwa kupima kama uelewa wa fungu husika haupingani na uelewa wa mafungu mengine ya Biblia? “Kwa sababu hiyo neno la Bwana kwao litakuwa hivi, amri juu ya amri, amri juu ya amri; kanuni juu ya kanuni, kanuni juu ya kanuni; huku kidogo na huku kidogo; ili waende na kuanguka nyuma, na kuvunjwa, na kunaswa, na kuchukuliwa.” (Isaya 28:13)
 
TUMIA NENO LA MUNGU KWA HALALI:

Neno la Mungu lisipotumiwa kihalali laweza kuleta maana isiyokusudiwa na kupotosha watu. Hivyo kila anayelifundisha Neno la Mungu ni sharti ajiridhishe kuwa analitumia neno hilo kihalali. “Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli.” (2 Timotheo 2:15). Kujua kuwa unatumia Neno la Mungu kihalali ni kujiridhisha kama imeelewa maana iliyokusudiwa. Ili kuelewa maana iliyokusudiwa mtu anapaswa kujiuliza mswali kadhaa. Je, maneno hayo yalitolewa kwa watu gani hapo mwanzo (walengwa wa kwanza wa maneno haya walikuwa nani?). Pili ni lazima msomaji na mfundishaji ajiridhishe kuwa wazo kuu katika ujumbe uliokusudiwa ilikuwa nini? Ikiwa bado maana iliyokusudiwa itakuwa haijaeleweka msomaji anapaswa kufuatilia kusoma kuanzia mwanzo wa mjadala ili kujiridhisha na mtiririko wa mazungumzo, na pia kujua angalu wakati husika ujumbe ulipotolewa na mazingira ya walengwa wa ujumbe. Mambo haya ni muhimu ili kupata tafsiri iliyokusudiwa na mwandishi. Watu wengi wanaokosea kutafsiri nyaraka za Paulo wanakosea kutokana na kutozingatia kanuni hizo za kutafsiri Maandiko. “Vile vile kama katika nyaraka zake zote pia, akitoa humo habari za mambo hayo; katika nyaraka hizo yamo mambo ambayo ni vigumu kuelewa nayo; na mambo hayo watu wasio na elimu, wasio imara, huyapotoa, kama vile wayapotoavyo na maandiko mengine, kwa uvunjifu wao wenyewe.” (2 Petro 3:16). Maneno ya Mungu yakipokelewa kwa tafsiri yake sahihi yana uwezo wa kuwapa watu msaada mkubwa kama maziwa yasiyoghoshiwa (yasiyochakachuliwa) yawezavyo kumsaidia mtoto anayekua. “Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu.” 1 Petro 2:2
 
UDANGANYIFU WA SHETANI:

Neno la Mungu ni upanga ukatao kuwili kwa wenye dhambi. Unaibua uwepo wa dhambi na kuzihukumu. “Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.” (Waebrania 4:12). Mwadamu mdhambi hawezi kusikia amani anapokuwa mbele ya Neno la Mungu. Kwake linakuwa kama nyundo iumizayo au moto uunguzao. “Je! Neno langu si kama moto? Asema Bwana; na kama nyundo ivunjayo mawe vipande vipande?” (Yeremia 23:29). Kutokana na ukweli huo, Neno la Mungu limekabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa wale linaowaumbua akiwemo shetani mwenyewe, tangu lilipoanza kuwepo duniani. Wakati fulani mfalme mmoja wa Israeli aliwahi kuagiza Neno la Mungu lichomwe moto. “Hata ikawa, Yehudi alipokuwa amekwisha kusoma kurasa tatu nne, mfalme akalikata kwa kijembe, akalitupa katika moto wa makaa, hata gombo lote likawa limekwisha kuteketea katika huo moto wa makaa.” (Yeremia 36:23). Pamoja na kuwa jitihada hizo hazijawahi kufanikisha kutokomeza Neno la Mungu, jitihada zingine za kuingiza udanganyifu kwenye mafundisho ya dini kwa kisingizio kuwa ni maagizo ya Neno la Mungu zimekuwa yakiendelea kwa kasi kubwa. Wakati fulani jitihada hizo zimeonekana kufanikiwa na watu wengi kupotoshwa. “Na katika moja ya pembe hizo ilitokea pembe ndogo, iliyokua sana, upande wa kusini, na upande wa magharibi, na upande wa nchi ya uzuri. Nayo ikakua, kiasi cha kulifikilia jeshi la mbinguni; ikaangusha chini baadhi ya jeshi lile, na ya nyota, ikazikanyaga. Naam, ikajitukuza hata juu yake aliye mkuu wa jeshi hilo, ikamwondolea sadaka ya kuteketezwa ya daima, na mahali pa patakatifu pake pakaangushwa chini.Na jeshi likatolewa kwake pamoja na sadaka ya kuteketezwa ya daima, kwa sababu ya makosa; nayo ikaiangusha kweli hata chini; ikatenda ilivyopenda, na kufanikiwa.” (Danieli 8:9-12)
 
MAFUNDISHO YA UONGO:

Yesu alipokuja duniani, alikuta hali hii ya kutukuza mafundisho ya kibinadamu yanayopingana na Maandiko Matakatifu na akatumia muda mwingi kuikemea. “Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu”. (Mathayo 15:9). Mpango huu wa kuudanganya ulimwengu kwa mafundisho ya uongo unaasisiwa na shetani mwenyewe. “Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo.” (Yohana 8:44). Amekuwa akitumia silaha hiyo tangu alipotimuliwa kule mbinguni. “Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye.” (Ufunuo 12:9)
 
MANABII WA UONGO:

Biblia inatahadharisha kuwa udanganyifu mkubwa utatokea duniani watu wakijitambulisha kuwa wametumwa na Mungu nao watatoa maneno mengi yanayopingana na Neno la Mungu kwa nia ya kuwapotosha wanadamu. “Kwa maana wataondoka Makristo wa uongo, na manabii wa uongo, watatoa ishara na maajabu, wapate kuwadanganya, kama yamkini, hata hao wateule.” (Marko 13:22). Hawa watakuwa mawakala wa yule mwovu ambao kwa kujua au kwa kutokujua watajivalisha muonekano wa watumishi wa nuru. “Maana watu kama hao ni mitume wa uongo, watendao kazi kwa hila, wanaojigeuza wawe mfano wa mitume wa Kristo. Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru.” (2 Wakorintho 11:13-14). Mungu anawaita watu watoao mawazo yao na kuyawasilisha kana kwamba ni ya Mungu kuwa ni manabii wa uongo kwa sababu wanawapa watu faraja ya uongo. “Na manabii wake wamewapakia chokaa isiyokorogwa vema, wakiona ubatili, na kuwatabiria maneno ya uongo, wakisema, Bwana MUNGU asema hivi; iwapo Bwana hakusema neno.” (Ezekieli 22:28). Mungu anatoa tahadhari kwetu sote kuwa makini na watu hao. “Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani.” (1 Yohana 4:1). Neno la Mungu ni silaha tosha. Hata Yesu alitumia silaha alipokabiliwa na uongo wa aina hiyo kutoka kwa shetani mwenyewe. “Yesu akajibu akamwambia, Imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake.” (Luka 4:8)
 
KUYAKATAA MAFUNDISHO YA UZIMA:

Mungu ana ujumbe muhimu kwa kila mmoja wetu ambao ameuweka kwenye Maandiko Matakatifu. Ni ujumbe muhimu kwa mustakabali wa maisha yetu. Mashauri yaliyomo kwenye ujumbe huo yalikuwa yanatosha kutuondolea shida nyingi tunazopambana nazo sasa bila mafanikio. Kwa kadri tunavyochelewa kuufikia ujumbe huo na kuusoma ndivyo tunavyoendeleaa kupoteza fursa muhimu ya mafanikio kwa maisha ya sasa na ya baadaye. Shetani anaongeza juhudi zake za kuwashawishi wanadamu wasiyapokee mafundisho yenye uzima. “Maana utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima; ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe watajipatia waalimu makundi makundi, kwa kuwa wana masikio ya utafiti; nao watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za uongo.” (2 Timotheo 4:3-4). Watu wanavutiwa na uongo kuliko ukweli na wanavutiwa na hadithi kuliko maneno ya uzima. “Nao watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za uongo.” (2 Timotheo 4:4) Kuna wimbi kubwa la watu wanaogeukia majumba ya ibada kwa ajili ya kukidhi mahitaji yao ya kiuchumi na kiafya tu na siyo mahitaji ya kiroho. Watu huja kwenye mikutano ya kiroho na majumba ya ibada kama waendao kwenye vikundi vya ujasiriamali kutafuta namna ya kuboresha maisha yao kiuchumi. Watu hawasukumwi na Neno la Mungu ili liwabadilishe kiroho bali wanasukumwa na faida za kitambo tu.
 
KUPENDA MANENO LAINI:

Kuna ongezeko la waendao nyumba za ibada wakitaka wahubiriwe maneno laini. “Wawaambiao waonaji, Msione; na manabii, Msitoe unabii wa mambo ya haki, tuambieni maneno laini, hubirini maneno yadanganyayo.” (Isaya 30:10). Wahubiri nao kwa kutaka kuwaridhisha wafuasi wao wamepunguza ukali wa Neno la Mungu kwa kutogusa dhambi zao zinazowatenga na Mungu wao na kuwapa ahadi za uongo. Ni kama waaabuduo wamejitengenezea wahubiri wanaowataka na wahubiri nao kwa kufuata maslahi manono ya muda mfupi wameridhia kufanya huduma ya uongo inayotakiwa na waabuduo wao. Ni ndoa ya ajabu baina ya wadanganyaji na wadanganywaji. “Lakini watu wabaya na wadanganyaji wataendelea, na kuzidi kuwa waovu, wakidanganya na kudanganyika.” (2 Timotheo 3:13). Hawa ndiyo wachungaji wa mishahara ambao wamegeuza matumbo yao kuwa miungu yao. “Kwa sababu walio hivyo hawamtumikii Bwana wetu Kristo, bali matumbo yao wenyewe; na kwa maneno laini na ya kujipendekeza waidanganya mioyo ya watu wanyofu.” (Warumi 16:18)
 
USHAURI WA WA MUHIMU:

Nakupa shauri uchukue nafasi kusoma na kusikiliza Maandiko Matakatifu kila unapopata nafasi. Mungu ametengeneza mazingira mazuri leo kiasi kuwa Neno la Mungu linapatikana katika Redio, televisheni, simu ya mkononi, mtandaoni, hata kwa kutumia memory card na flush. Mungu amelisogeza karibu zaidi na wewe kwa gharama nafuu unayoweza kuimudu. Weka kipaumbele katika kusoma ama kusikiliza nini Mungu ameweka hapo kwa ajili yako. Mungu anataka kusema nawe. Lishike Neno la Mungu maana ni uzima wako. “Kumpenda Bwana, Mungu wako, kuitii sauti yake, na kushikamana naye; kwani hiyo ndiyo uzima wako, na wingi wa siku zako; upate kukaa katika nchi Bwana aliyowaapia baba zako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kuwa atawapa.” (Kumbukumbu 30:20)