Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

UJENZI WA TABIA YA KIROHO

MKWAMO KATIKA UJENZI WA TABIA ZA KIROHO - 1

Mkwamo katika ujenzi wa tabia za kiroho waweza kutokana na kukataa au kutilia shaka nuru na mafunuo mapya kutoka kwa Mungu yanayotokana na hatua ambayo kanisa limeifikia katika wakati husika. Mungu huliongoza kanisa lake kutoka hatua moja hadi nyingine akiongeza nuru ya mambo yanayopaswa kuzingatiwa na wale wanaoukulia wokovu. Mithali 4:18 Bali njia ya wenye haki ni kama nuru ing'aayo, Ikizidi kung'aa hata mchana mkamilifu. 2 Petro 1:19 Nasi tuna lile neno la unabii lililo imara zaidi, ambalo, mkiliangalia, kama taa ing'aayo mahali penye giza, mwafanya vyema, mpaka kutakapopambazuka, na nyota ya asubuhi kuzuka mioyoni mwenu. Kanisa hukoma kukua pale linapoyakataa mafundisho dhahiri ya Neno la Mungu. Isaya 8:20 Na waende kwa sheria na ushuhuda; ikiwa hawasemi sawasawa na neno hili, bila shaka kwa hao hapana asubuhi. Ufunuo wa Yohana 12:17 Joka akamkasirikia yule mwanamke, akaenda zake afanye vita juu ya wazao wake waliosalia, wazishikao amri za Mungu, na kuwa na ushuhuda wa Yesu; naye akasimama juu ya mchanga wa bahari.

Kanisa la kweli linalindwa na Yesu mwenyewe. Mathayo 16:18 Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda. Mwamba ambao juu yake kanisa litajengwa ni Kristo mwenyewe na siyo Petro. 1 Wakorintho 10:4 wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo. Vitisho vinavyoibuka mara kwa mara kuwa kanisa limeuzwa vinapingana na kauli ya Yesu kuwa milango ya kuzimu haiwezi kulishinda kanisa na vina nia ya kuzua hofu na taharuki isiyo na msingi kwa waumini. Kazi hii inafanywa na yule mwovu kwa kuwatumia watu wasio imara waliopo kanisani. Yuda 1:4 Kwa maana kuna watu waliojiingiza kwa siri, watu walioandikiwa tangu zamani hukumu hii, makafiri, wabadilio neema ya Mungu wetu kuwa ufisadi, nao humkana yeye aliye peke yake Mola, na Bwana wetu Yesu Kristo.

Waumini wenye nia ya kweli ya kulisaidia kanisa wamepewa fursa ya kufanya hivyo kupitia taratibu na vikao halali vilivyoainishwa kwenye mwongozo wa kanisa. Kanisa limegawa utaratibu wa ngazi ipi ina haki ya kufanya lipi na hakuna haja ya kuingiliana katika majukumu. Kanisa katika ngazi Mahalia inayo haki ya kumuondoa au kumuingiza mtu katika ushirika wa kanisa bila kushinikizwa na ngazi iliyo juu yake. Hali kadhalika konferensi wana haki ya kumuondoa na kumuingiza mchungaji, na haki ya kuliingiza na kuliondoa kanisa katika ushirika wa makanisa ya konferensi bila kushinikizwa na ngazi iliyo juu au chini yake. Konferensi pia ndiyo yenye wajibu wa kupanga vituo vya makambi na wahudumu wake. Ngazi ya union kwa utaratibu wetu ndiyo yenye wajibu wa kupendekeza na kusimamia Huduma ya kuwekewa mikono wachungaji wakati konferensi kuu inawajibika kutunga sera, na kuibua au kurekebisha misingi ya Imani ya kanisa.

Kanisa la Mungu limekuwa likipitia mabadiliko kadhaa tangu lilipoanzishwa nyakati za Agano la Kale. Zilikuwepo nyakati ambazo ubatizo unaomuingiza muumini kanisa ulikuwa kwa njia ya kutahiriwa lakini utaratibu huo ulikoma na utaratibu unaotumika kwa sasa ni wa kubatizwa kwa maji mengi. Mabadiliko haya yanapotokea wapo wasioridhika nayo na hao wamekuwepo katika vizazi vyote. Wayahudi walilisumbua sana kanisa la awali kwa sababu walitaka kanisa la kikristo lifanane na kanisa la kiyahudi. Matendo ya Mitume 15:1 Wakashuka watu waliotoka Uyahudi wakawafundisha wale ndugu ya kwamba, Msipotahiriwa kama desturi ya Musa hamwezi kuokoka. Upinzani haukuishia katika swala la tohara bali ulihusu pia swala la ni nani anastahili kuingia hekaluni. Paulo alishutumiwa kuwa amelinajisi hekalu kwa kuingiza Wayunani watu wasio wa taifa la Israeli ambao kwa mujibu wa sheria ya hekalu hawakupaswa kuingia. Hoja kama hiyo bado ingali inalisumbua kanisa la Mungu leo. Inadhaniwa kuwa majengo ya ibada ya leo ni mahekalu kama yale ya Agano la Kale ambapo kuna maeneo ndani yake asiyopaswa mwanamke kusimama au kukanyaga. Dhana hii ni potofu. Kama nyumba za ibada za leo ni sawa na hekalu inakuwaje watu wa makabila yasiyo wayahudi wanaruhusiwa kuingia ndani yake? Je huko siko kulinajisi hekalu?

Huduma ya hekalu la Agano la Kale ilikomea Yesu alipokufa pale msalabani wakati pazia la hekalu lilipopasuka. Mathayo 27:51 Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka. Huduma ya hekalu la duniani kuanzia wakati huo ilikoma na Huduma ya hekalu la mbinguni ikaanza. Waebrania 9:24 Kwa sababu Kristo hakuingia katika patakatifu palipofanyika kwa mikono, ndio mfano wa patakatifu halisi; bali aliingia mbinguni hasa, aonekane sasa usoni pa Mungu kwa ajili yetu. Aliingia chumba cha kwanza alipopaa mbinguni na chumba cha pili mwaka 1844. Hapa dunia ambapo Yesu Mwanakondoo alichinjwa panatambulika kama nje ya lango la hekalu la mbinguni. Waebrania 13:12 Kwa ajili hii Yesu naye, ili awatakase watu kwa damu yake mwenyewe, aliteswa nje ya lango. Hekalu pekee lililobakia leo duniani ni hekalu linalotembea ambalo ni mimi na wewe. 1 Wakorintho 3:16 Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?

Hili ndilo hekalu pekee la hapa duniani ambalo Mungu analitambua na kuliheshimu kwa kuwa halijajengwa kwa mikono ya wanadamu. Ni dharau kubwa kwa Mungu kumzuia mwanamke aliyeumbwa na Mungu asiingie mahali palipojengwa na mikono ya wanadamu. Mahali pa ibada huwa patakatifu kutegemeana na wale wanaoabudu hapo kama ni mahelu yanayotembea yenye Roho Mtakatifu. Ndiyo maana wakati mwingine tumeshuhudia mahali pa ibada pakigeuzwa ulingo wa ngumi na hao hao wanaotetea kuwa ni mahali patakatifu!

 

MKWAMO KATIKA UJENZI WA TABIA ZA KIROHO – II

Mkwamo wa ujenzi wa tabia za kiroho waweza kutokana na nuru mpya katika mafundisho ya Biblia. Wakati mmoja Yesu alileta mada iliyoleta utata kwa wasikilizaji wake hata wengi wakarudi nyuma. Yohana 6:66-68 “Kwa ajili ya hayo wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma, wasiandamane naye tena. Basi Yesu akawaambia wale Thenashara, Je! Ninyi nanyi mwataka kuondoka? Basi Simoni Petro akamjibu, Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.” Hali hii ilijitokeza mara nyingi katika historia ya kanisa la Mungu hasa kanisa la awali (Matendo 15:1 – kuhusu tohara, na Matendo 21:28 – kuhusu wanaostahili kuingia hekaluni.

Leo tutaangalia ni nani walistahili kuingia hekaluni wakati wa Agano la Kale na nani wanastahili kuingia hekaluni wakati huu wa Agano Jipya. Hekalu la Agano la Kale liliruhusu watu wenye sifa maalumu kuingia hekaluni. Wahudumu wa hekalu la Agano la Kale walitoka kabila la Lawi. Hesabu 18:6 “Nami, tazama, nimewatwaa ndugu zenu Walawi miongoni mwa wana wa Israeli; kwenu ninyi watu hao ni kipawa alichopewa Bwana, waufanye utumishi wa hema ya kukutania.” Yoshua 3:3 “Wakawaamuru watu wote wakisema, Mtakapoliona sanduku la agano la Bwana, Mungu wenu, na makuhani Walawi wakilichukua, ndipo mtakapoondoka hapa mlipo na kulifuata.” Utaratibu huu wa kufanya kabila moja miongoni mwa watu wa taifa la Israeli haukuwa mpango wa awali wa Mungu kwa kuwa kimsingi Mungu alikusudia taifa zima la Israeli liwe makuhani kwa ajili ya ulimwengu mzima. Kutoka 19:6 “Nanyi mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani, na taifa takatifu. Hayo ndiyo maneno utakayowaambia wana wa Israeli.”

Kulikuwa na aina mbili za makuhani; makuhani wahudumuo kila siku kutoka kabila zima la Lawi na Kuhani Mkuu aliyetoka mlango (familia ya) Haruni na wanawe aliyehudumu mara moja kwa mwaka. Hesabu 3:10 “Nawe utawaweka Haruni na wanawe, nao wataushika ukuhani wao, na mgeni atakayekaribia atauawa.” Paulo akiielezea hali hiyo kwa mapana anasema, “Basi hata agano la kwanza lilikuwa na kawaida za ibada, na patakatifu pake, pa kidunia. Maana hema ilitengenezwa, ile ya kwanza, mlimokuwa na kinara cha taa, na meza, na mikate ya Wonyesho; ndipo palipoitwa, Patakatifu. Na nyuma ya pazia la pili, ile hema iitwayo Patakatifu pa patakatifu, yenye chetezo cha dhahabu, na sanduku la agano lililofunikwa kwa dhahabu pande zote, mlimokuwa na kopo la dhahabu lenye ile mana, na ile fimbo ya Haruni iliyochipuka, na vile vibao vya agano; na juu yake makerubi ya utukufu, yakikitia kivuli kiti cha rehema; basi hatuna nafasi sasa ya kueleza habari za vitu hivi kimoja kimoja. Basi, vitu hivi vikiisha kutengenezwa hivyo, makuhani huingia katika hema hiyo ya kwanza daima, wakiyatimiza mambo ya ibada. Lakini katika hema hiyo ya pili kuhani mkuu huingia peke yake, mara moja kila mwaka; wala si pasipo damu, atoayo kwa ajili ya nafsi yake na kwa dhambi za kutokujua za hao watu.” Waebrania 9:1-7

Pamoja na makuhani (ambao wote walikuwa wa jinsia ya kiume), kulikuwako pia wahudumu wengine wasio makuhani waliokuwa wanahudumu katika hekalu la Agano la Kale, waliokuwa wakitumika mlangoni pa hema ya kukutania. Kutoka 38:8 “Kisha akafanya hilo birika la shaba, na tako lake la shaba; shaba hiyo ilikuwa ni ya vioo vya wanawake wenye kutumika, waliokuwa wakitumika mlangoni mwa hema ya kukutania.” 1 Samweli 2:22 “Basi Eli alikuwa mzee sana; naye alisikia habari za mambo yote ambayo wanawe waliwatenda Waisraeli; na jinsi walivyolala na wanawake waliokuwa wakitumika mlangoni pa hema ya kukutania.”

Huduma za hekalu la Agano Jipya ziliishia pale msalabani Yesu alipokata roho na pazia la hekalu kupasuka.  Mathayo 27:50-51 “Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake. Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka.” Huduma ya hekalu ilipokoma na wahudumu wa hekalu pia walibadilishwa na majukumu yao pia yakabadilishwa. Kuhani mkuu badala ya kuwa Haruni na watu wa mlango wake kama ilivyokuwa katika hekalu la Agano la Kale, sasa katika Agano Jipya Kuhani Mkuu anakuwa Yesu ambaye kimsingi hatoki katika kabila la Lawi. Yesu anakuwa Kuhani Mkuu kutoka kabila la Yuda ambalo Biblia haikuwa imesema lolote kuhusu ukuhani. Kabila la Yuda lilikuwa kwa ajili ya kutoa watawala au wafalme katika Israeli. Mwanzo 49:10 “Fimbo ya enzi haitaondoka katika Yuda, Wala mfanya sheria kati ya miguu yake, Hata atakapokuja Yeye, mwenye milki, Ambaye mataifa watamtii.”

Ni Dhahiri kuwa haya yalikuwa mafunuo mapya. Waebrania 7:12-14 “Maana ukuhani ule ukibadilika, hapana budi sheria nayo ibadilike. Maana yeye aliyenenwa hayo alikuwa mshirika wa kabila nyingine, [Yesu] ambayo hapana mtu wa kabila hiyo aliyeihudumia madhabahu. Maana ni dhahiri kwamba Bwana wetu alitoka katika Yuda, kabila ambayo Musa hakunena neno lo lote juu yake katika mambo ya ukuhani.” Mtu aweza kujiuliza kulikuwa na haja gani sheria ya ukuhani ibadilike? Waebrania 7:11 Basi, kama ukamilifu ulikuwapo kwa ukuhani wa Lawi; (maana watu wale waliipata sheria kwa huo); kulikuwa na haja gani tena ya kuhani mwingine ainuke, kwa mfano wa Melkizedeki, wala asihesabiwe kwa mfano wa Haruni?”  Sababu ya msingi ni kuwa Huduma ya ukuhani ilikuwa ni kivuli cha mambo yajayo. Ilikuwa inawakilisha Huduma kamilifu ya kuwakomboa wanadamu ya Yesu pale msalabani na huduma ambayo Yesu anaifanya sasa huko mbinguni. Waebrania 4:14 “Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungamo yetu.”

Kristo kwa sasa anahudumu kwenye hekalu la mbinguni. Waebrania 9:24-26 “Kwa sababu Kristo hakuingia katika patakatifu palipofanyika kwa mikono, ndio mfano wa patakatifu halisi; bali aliingia mbinguni hasa, aonekane sasa usoni pa Mungu kwa ajili yetu; wala si kwamba ajitoe mara nyingi, kama vile kuhani mkuu aingiavyo katika patakatifu kila mwaka kwa damu isiyo yake; kama ni hivyo, ingalimpasa kuteswa mara nyingi tangu kuwekwa msingi wa ulimwengu; lakini sasa, mara moja tu, katika utimilifu wa nyakati, amefunuliwa, azitangue dhambi kwa dhabihu ya nafsi yake.” Yesu alifanyika kuhani mkuu kwa kuwa ndiye pekee aliyekidhi vigezo vya kuhani mkuu. Waebrania 7:26 “Maana ilitupasa sisi tuwe na kuhani mkuu wa namna hii aliye mtakatifu, asiyekuwa na uovu, asiyekuwa na waa lo lote, aliyetengwa na wakosaji, aliyekuwa juu kuliko mbingu.”

Yeye aliyemwagiza Kristo awe kuhani mkuu wa Agano Jipya kwa mfano wa Melkizedeki ndiye aliyewaagiza wanadamu wote kuwa makuhani. 1 Petro 2:9 Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu. Ukuhani wa Agano Jipya inawahusisha watu wote wa kutoka katika mataifa yote na makabila yote na jinsia zote. Haubagui kama ulivyokuwa ukuhani wa Agano la Kale ambao ulihusu wanaume wa kabila la Lawi pekee. Hawa wanaotambuliwa kama ukuhani wa kifalme katika fungu la hapo juu ni wale wote walioitwa na Yesu kutoka katika jamii zote za wanadamu. Matendo ya Mitume 2:39 “Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie.” Leo hii kila anayemuamini Yesu ni kuhani. Mungu amerejea kusudi lake la awali la kuwafanya taifa zima la Israeli kuwa makuhani. Kutoka 19:6 “Nanyi mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani, na taifa takatifu. Hayo ndiyo maneno utakayowaambia wana wa Israeli.”

Kuhani mkuu wa Agano Jipya haendelezi huduma zilizokuwa zinafanyika kwenye hekalu la Agano la Kale maana huduma hizo zinafanyika sasa na kuhani mkuu Yesu kwenye hekalu la kule mbinguni. Ufunuo 1:12-16 “Nikageuka niione ile sauti iliyosema nami. Na nilipogeuka, niliona vinara vya taa saba vya dhahabu; na katikati ya vile vinara nikaona mtu mfano wa Mwanadamu, amevaa vazi lililofika miguuni, na kufungwa mshipi wa dhahabu matitini. Kichwa chake na nywele zake zilikuwa nyeupe kama sufu nyeupe, kama theluji; na macho yake kama mwali wa moto; na miguu yake kama shaba iliyosuguliwa sana, kana kwamba imesafishwa katika tanuru; na sauti yake kama sauti ya maji mengi. Naye alikuwa na nyota saba katika mkono wake wa kuume; na upanga mkali, wenye makali kuwili, ukitoka katika kinywa chake; na uso wake kama jua liking'aa kwa nguvu zake.”

Makuhani wa leo huendeleza majukumu ya ukuhani kwa njia ya kutangaza fadhila zake yeye aliyewaita watoke gizani. 2 Wakorintho 5:18-19 Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho; yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu neno la upatanisho. Huduma ya upatanisho tuliyopewa inahusu kutangaza habari njema ya wokovu na uwezo wa Yesu kuokoa wenye dhambi. Ufunuo 14:6-7 Kisha nikaona malaika mwingine, akiruka katikati ya mbingu, mwenye Injili ya milele, awahubiri hao wakaao juu ya nchi, na kila taifa na kabila na lugha na jamaa, akasema kwa sauti kuu, Mcheni Mungu, na kumtukuza, kwa maana saa ya hukumu yake imekuja. Msujudieni yeye aliyezifanya mbingu na nchi na bahari na chemchemi za maji. Huduma hii huwanyenyekesha wanadamu kwa kuwasaidia kutambua jinsi wasivyoweza kujiokoa na namna wanavyohitaji msaada wa Mungu kuokolewa.

Kazi hii hufanywa kupitia huduma za uinjilisti binafsi, mahubiri na mafundisho ya Neno la Mungu, kwa njia ya mikutano ya hadhara, mikutano ya redioni na kwenye runinga, na kwa njia ya huduma za matendo ya huruma. Kupitia huduma hii wengi huokolewa na wengine huweza kupoteza fursa hizo na kuangamia. Marko 16:15-16 “Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.” Ukuhani huu hahuhitaji mavazi maalumu ili kutekeleza majukumu yake kama ilivyokuwa kwenye Agano la Kale. Mambo ya Walawi 16:4 “Ataivaa ile kanzu takatifu ya kitani, atakuwa na zile suruali za kitani mwilini mwake, atafungwa ule mshipi wa kitani, naye atavaa ile kofia ya kitani; hayo ndiyo mavazi matakatifu, naye ataoga mwili wake majini, na kuyavaa.”

Huduma hii ya kikuhani inayofanywa na wanaume na wanawake waliompokea Yesu kama Bwana na Mwokozi wao, haishii hapa duniani bali itaendelea hata baada ya kufika mbinguni. Huduma ya Yesu ya kuupatanisha ulimwengu na Mungu itaendelea pale wakati waliokombolewa watakaposhuhudia viumbe wasioanguka dhambini juu ya upendo wa Mungu. Ufunuo 20:6 Huo ndio ufufuo wa kwanza. Heri, na mtakatifu, ni yeye aliye na sehemu katika ufufuo wa kwanza; juu ya hao mauti ya pili haina nguvu; bali watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, nao watatawala pamoja naye hiyo miaka elfu. Sisi tutakaokombolewa tutakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo kwa kipindi cha miaka elfu moja kwa mujibu wa Maandiko. Ukuhani huo kama ulivyokuwa ukuhani wa hapa duniani utawahusu waliokombolewa wa jinsia zote. Huduma hiyo itaendelea hata katika nchi mpya ambapo waliokombolewa watafanya kazi ya kikuhani huku wakitimiza na shughuli za kifalme. Ufunuo wa Yohana 5:10 ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi.”

Wale wanaohoji uhalali wa wanawake kuwa makuhani wakati wa Agano Jipya wakati hawakuwa makuhani wakati wa Agano Jipya wanasahau ukweli kuwa kwa kadri kanisa linavyokuwa nuru nayo inaongezeka. Mungu ambaye hakuruhusu wanawake wawe makuhani katika Agano la Kale, ndiye aliyeruhusu wawe makuhani katika Agano Jipya, na ndiye aliyeruhusu wawe makuhani mbinguni na katika nchi mpya. Hii inatokana na kubadilika kwa sheria ya ukuhani kulikowapa uhalali watu wa mataifa mengine yasiyo ya Israeli kuingia hekaluni kama ilivyotokea katika kanisa la awali. Matendo ya Mitume 21:28 wakapiga kelele, na kusema, Enyi wanaume wa Israeli, tusaidieni. Huyu ndiye mtu yule afundishaye watu wote kila mahali kinyume cha taifa letu na torati na mahali hapa. Tena, zaidi ya haya, amewaingiza Wayunani katika hekalu, akapatia unajisi mahali hapa patakatifu.” Kama ilivyodhaniwa kuwa watu wa mataifa mengine waingiapo hekaluni hulinajisi hekalu ndivyo na leo baadhi ya watu wanavyodhani mwanamke anapotangaza habari njema kwa kusimamama mimbarani kanisani naye analinajisi hekalu au kanisa la Mungu. Jambo la kujiuliza ni hili; inawezekanaje yule anayedhaniwa kuwa ni najisi hapa duniani anaruhusiwa kuwa kuhani wa mbinguni na wan chi mpya? Je wanadamu wanajali mahekalu waliyoyatengeneza wenyewe kwa mikono yao kuliko Mungu anavyothamini mbingu na nchi mpya alivyoviumba? Je siyo yeye aliyedai kitu kinyonge hakitaruhusiwa mbinguni? Ufunuo 21:27 Na ndani yake hakitaingia kamwe cho chote kilicho kinyonge, wala yeye afanyaye machukizo na uongo, bali wale walioandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo.

Wale wanaopingana na fundisho kuwa wanawake nao ni sehemu ya makuhani wa hapa duniani, wa kule mbinguni, na wa nchi mpya, wanasababisha mkwamo katika ujenzi wa tabia za kiroho. Mkwamo huo waweza kusababisha kutopokea nuru nyingine muhimu zaidi kwa wokovu wao. Mungu anapokusudia kuwatumia wale ambao huko nyuma hakuwahi kuwatumia hahitaji kushauriana na mtu sawa na mwalimu wa timu anapoongeza mchezaji wa akiba. Kwa kuwakataa wale ambao Mungu amewakubali watumike siyo tu kwamba tunaingilia majukumu yake bali tunajionesha kuwa sisi tuna hekima zaidi kuliko Mungu wetu. Mungu atusaidie kujua hatari ya kupinga nuru mpya na atupe roho ya kuwa tayari kujifunza na kutii.