Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

DHANA YA UTATU HAIEPUKIKI

DHANA YA UTATU HAIEPUKIKI

Unaweza kuwa umesikia dhana yaa utatu ikisemwa vibaya kiasi kwamba nawe umeanza kuitilia shaka. Huenda kinachofanya uitilie shaka zaidi ni vile inavyohusianishwa na dhana za kipagani zilizoingizwa kwa hila kwenye kanisa la Mungu ili kuwapotosha wanadamu. Kama tuhuma hiyo ina ukweli au haina ukweli ni jambo jingine. Jambo moja lililo Dhahiri ni kuwa dhana ya utatu haikuibuka bila kuwepo kwa hoja zenye mantiki zipatikanazo ndani ya Biblia. Na kwa sababu hiyo dhana ya utatu hata ichukiwe vipi ni dhana isiyoepukika.

Mtu yeyote mwenye akili ya kawaida angetamani tafsiri ya Mungu isiwe na utata au ugumu katika kuielezea. Yaani iwe rafiki na uelewa wa mwanadamu. Yaani kama Mungu ni mmoja basi ibaki hivyo hivyo na wala kusiwepo tafsiri zingine za kuwepo kwa nafsi tatu jambo linaloweza kumaanisha kuna miungu watatu. Na kama Mungu si mmoja basi isemwe waziwazi kuwa kuna miungu watatu yaani Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu. Mungu hawezi kutafsiriwa kwa namna itakayomwia rahisi mwanadamu kuelewa huku ikipotosha maana yenyewe halisi ya Mungu. Mungu mwenyewe amechagua kujifunua kwa namna hiyo ambayo kwa watu wengine imewafanya kuchanganyikiwa na kuhisi kuwa Mungu hatendewi haki.

Je, Mungu ni mmoja?

Wakati Mungu anajitambulisha kwa Waisraeli alikuta dunia ikiwa na miungu wengi wanaoaminiwa na kuabudiwa. (Kumbukumbu la Torati 6:14-15) “Msifuate miungu mingine katika miungu ya mataifa wawazungukao; kwani Bwana, Mungu wako, aliye katikati yako ni Mungu mwenye wivu; isije ikawaka juu yako hasira ya Bwana, Mungu wako, akakuangamiza kutoka juu ya uso wa nchi.” (Waamuzi 10:6) “Kisha wana wa Israeli walifanya tena yaliyo maovu mbele za macho ya Bwana, wakawatumikia Mabaali, na Maashtorethi, na miungu ya Shamu, na miungu ya Sidoni, na miungu ya Moabu, na miungu ya wana wa Amoni, na miungu ya Wafilisti; nao wakamwacha Bwana, wala hawakumtumikia yeye.” Wazo la kuwepo Mungu mmoja lilikuwa la kigeni sana nyakati hizo. Ilidhaniwa kuwa kuna miungu wengi wanaopishana kwa uwezo na hata wakati mwingine kwa mitazamo hivyo hufikia wakati hata wakagombana. Waliamini kuwa mungu mmoja peke yake hatoshi kufanikisha mambo yaliyo juu ya uwezo wa mwanadamu. (Kutoka 32:7-8) “Bwana akamwambia Musa, Haya! Shuka; kwa maana watu wako uliowatoa katika nchi ya Misri wamejiharibu nafsi zao, wamepotoka upesi kuiacha ile njia niliyowaamuru, wamejifanyizia ndama ya kuyeyusha wakaiabudu na kuitolea dhabihu, wakasema, Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyokutoa katika nchi ya Misri.” Ili kuondoa dhana hiyo kwa wanadamu akaweka bayana kuwa yupo Mungu mmoja anayestahili kuaminiwa na kuabudiwa. Kuamini kuwa kuna Mungu zaidi ya mmoja kukawa ni kukiuka amri ya kwanza ya Mungu.  (Kutoka 20:3) “Usiwe na miungu mingine ila mimi.”

Miungu hiyo mingine ilihusika katika kuleta ustawi katika maisha ya mwadamu. Alikuwepo Mungu wa kuleta uzazi, Mungu wa kuleta mvua, Mungu wa kustawisha chakula na kadhalika. Na wanadamu walikuwa na uwezo wa kuitengeneza miungu hiyo kwa kuichonga kwa kutumia madini, mawe, mbao na njia zinginezo. (Kutoka 20:23) “Msifanye miungu mingine pamoja nami; miungu ya fedha, wala miungu ya dhahabu, msijifanyie.” Kazi ya kwanza ya Waisraeli ilikuwa kuiangamiza miungu hiyo isiyo na uwezo wa kujitetea. (Kutoka 23:24) “Usiisujudie miungu yao, wala kuitumikia; wala usitende mfano wa matendo yao; bali utaiangamiza kabisa, na nguzo zao utazivunja vipande vipande.”

Mungu anajitofautisha na miungu mingine kwa uwezo wa kuumba na kuokoa. (2 Wafalme 18:34-35) “Iko wapi miungu ya Hamathi, na ya Arpadi? Iko wapi miungu ya Sefarvaimu, na ya Hena, na ya Iva? Je! Imeuokoa Samaria na mkono wangu? Katika miungu ya nchi hizi zote, ni miungu gani iliyookoa nchi yao na mkono wangu, hata Bwana auokoe Yerusalemu na mkono wangu?” (1 Mambo ya Nyakati 16:26) “Maana miungu yote ya watu si kitu; Lakini Bwana ndiye aliyezifanya mbingu.” (Yeremia 10:11) “Mtawaambia hivi, Miungu hiyo isiyofanya mbingu na nchi, hiyo itaangamia katika nchi, nayo itatoweka chini ya mbingu.” Kupitia uzoefu wa Waisraeli ilikuja kuaminika kuwa yupo Mungu mmoja aliye mkuu kuliko miungu yote ya wamataifa. (Danieli 2:47) “Mfalme akajibu, akamwambia Danieli, Hakika Mungu wenu ndiye Mungu wa miungu, na Bwana wa wafalme, awezaye kufumbua siri, kwa kuwa wewe uliweza kuifumbua siri hii.” Musa alipotaka kujua namna atakavyomtambulisha Mungu huyu kwa wale aliokuwa anamtuma kwao alijitambulisha kama Mungu mmoja. (Kutoka 3:14) “Mungu akamwambia Musa, MIMI NIKO AMBAYE NIKO; akasema, Ndivyo utakavyowaambia wana wa Israeli; MIMI NIKO amenituma kwenu.” Wala hakumwambia miungu imenituma au UTATU umenituma kana kwamba ni wengi.

Kama Biblia yote ingebaki na uelewa huu kusingekuwa na dhana ya UTATU kama ilivyo leo. Kusingekuwepo Yesu na Roho Mtakatifu wanaopewa hadhi ya Uungu hata kufanya watu wengine wadhanie kuna miungu watatu. Tungekuwa tunasemakuna Mungu mmoja mwenye nafsi moja. Lakini wazo la nafsi linakuja pale Uungu unapotajwa katika uwingi. (Mwanzo 1:26) “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.” Sentensi hii inaleta dhana kuwa kuna ushirika au ushirikishwaji katika utendaji wa Mungu. Wala si ushirika kati ya Mungu na miungu wengine bali ni ushirika ndani ya taasisi ya Mungu mmoja. Kuna namna ambayo huyu Mungu mmoja katika kurahisisha au kufanikisha utendaji wake amejiweka katika mafungu mtatu lakini ni Mungu yule yule mmoja. Kuhakikisha ni Mungu yule yule mmoja anaanza kwa kusema ‘Mungu akasema’. Lakini kuthibitisha kuwa kuna nafsi zaidi ya moja katika huyo Mungu mmoja anabainisha akisema, ‘tumfanye mtu.’

Hali hii ya kutoa kauli yenye umoja na uwingi ndani yake inaonekana tena pale Mungu alipokuwa anakusudia kusambaratisha ujenzi wa mnara wa Babeli. (Mwanzo 11:5-7) “Bwana akashuka ili auone mji na mnara waliokuwa wakiujenga wanadamu. Bwana akasema, Tazama, watu hawa ni taifa moja, na lugha yao ni moja; na haya ndiyo wanayoanza kuyafanya, wala sasa hawatazuiliwa neno wanalokusudia kulifanya. Haya, na tushuke huko, tuwachafulie usemi wao ili wasisikilizane maneno wao kwa wao.” Aliyeshuka ili auone ujenzi wa mnara wa Babeli ni mmoja yaani Mungu au kama lilivyotumika hapa Bwana. Na mwenye kutoa kauli ya kile kinachokusudiwa kufanyika ni Mungu mmoja na wala si wawili au watatu.  Lakini inapokuja kwenye utekelezaji wa kilichoazimiwa nafsi zaidi ya moja zinajitokeza, ‘tushuke.’ Hii inatoa majumuisho kuwa Mungu mmoja aliye juu ya miungu yote ya wanadamu anapatikana katika nafsi zaidi ya moja hasa linapokuja swala la utendaji. Huo ndio ukweli ambao haupingiki hata kama huupendi.

Wengine katika kulikataa wazo la kuwepo kwa nafsi zaidi ya moja katika Mungu mmoja wamedai ule uwingi unaoonekana kwenye sentensi za ‘tumfanye’ na ‘tushuke’ Mungu alikuwa anaongea na Malaika au mwanadamu. Ugumu katika kuipokea tafsiri hiyo unatokana na ukweli kuwa kitendo cha kumfanya mtu au kushuka Babeli kinafanywa na Mungu na anayeweza kushirikishwa katika matendo hayo lazima awe ana hadhi kama ya Mungu mwenyewe. Kulitolea ufafanuzi hilo Biblia inatambulisha kuwepo kwa Neno kama nafsi iliyofungamanishwa na Mungu. (Yohana 1:1) “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.”

Huyu Neno anayetajwa hapa amefafanuliwa kwenye fungu la 14 kama Mwana au Yesu. (Yohana 1:14) “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.” Hapa kunaibuka dhana ya kuwepo nafsi mbili zote zikiwa na hadhi ya Uungu. Je, ni kusema kuna Mungu wawili? Hapana. Biblia imesisitiza mara nyingi kuwa Mungu ni mmoja. Hata Yesu mwenyewe alikazia jambo hilo. (Marko 12:32-33) “Yule mwandishi akamwambia, Hakika, Mwalimu, umesema vema ya kwamba Mungu ni mmoja, wala hakuna mwingine ila yeye; na kumpenda yeye kwa moyo wote, na kwa ufahamu wote, na kwa nguvu zote, na kumpenda jirani kama nafsi yako, kwafaa kuliko sadaka nzima za kuteketezwa na dhahibu zote pia.”

Sasa mtu anaweza kujiuliza, kama Mungu ni mmoja inakuwaje wawili wenye hadhi ya Mungu wasiwe miungu wawili? Hawawi miungu wawili kwa sababu hao ni nafsi mbili za Uungu zinazounda Mungu mmoja. Mfano rahisi juu ya hilo unaupata pale wawili wanapoungana katika ndoa. Wakishaungana hawawi wawili tena bali mwili mmoja. (Marko 10:6-8) “Lakini tangu mwanzo wa kuumbwa ulimwengu, aliwafanya mume na mke. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja; hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja.” Hatujui mengi juu ya chanzo cha Mungu. Kwamba ilitokeaje Neno kuweko kwa Mungu na Yeye mwenyewe akiwa Mungu? lakini hiyo haituzuii kujua kuwa angalao kuna nafsi zaidi ya moja ya Uungu.

Je nafsi zinazounda Uungu ni mbili au tatu?

Kwa mujibu wa Yohana 1:1-3 tunajua kuna nafsi mbili za Uungu. Nafsi moja inaitwa Neno au Mwana au Yesu na nafsi nyingine inaitwa Baba. (1 Wakorintho 8:6) “Lakini kwetu sisi Mungu ni mmoja tu, aliye Baba, ambaye vitu vyote vimetoka kwake, nasi tunaishi kwake; yuko na Bwana mmoja Yesu Kristo, ambaye kwake vitu vyote vimekuwapo, na sisi kwa yeye huyo.” Hapa usipokuwa mwangalifu unaweza kudhani nafsi hizi mbili; ya Baba na ya Yesu zinatofautiana kwa hadhi. Lakini ukiangalia kwa kina nafsi zote zimepewa uwezo wa kuumba usiotofautiana. Baba ambaye vitu vyote vimetoka kwake na Yesu ambaye kwake vitu vyote vimekuwapo. Hapa hakuna utofauti wa hadhi bali kuna utofauti wa majina. 

Kuna hatari nyingine ya kudhani majina haya yamebeba hadhi hasa pale nafsi moja inapoitwa Baba na nafsi nyingine inapoitwa Mwana. Majina haya ni ya kimkakati yakilenga jambo ambalo kila nafsi italitekeleza katika uumbaji na ukombozi wa mwanadamu. Utaratibu wa majina na majukumu ya kutekeleza katika ukombozi viliafikiwa kwa ridhaa ya kila nafsi na haikutolewa na nafsi moja yenye mamlaka kuliko zingine. Ilikuwa lazima nafsi moja iitwe Baba na nafsi nyingine iitwe Mwana kwa kuwa kulikuwa na wazo pana la kumfanya mwanadamu atakayeanguka dhambini awe mtoto wa Mungu mwenye kustahili kurithi kiti cha enzi cha Mungu na mamlaka yake. Ili hilo lifikiwe lazima nafsi mojawapo ya Mungu ifanyike Mwana ili kuwakilisha wanadamu watakaokombolewa ili kupitia kwake wanadamu wahesabiwe kustahili kuurithi ufalme.

Yesu alikubali kuchukua nafasi hiyo kwa hiyari yake na si kwa kulazimishwa na Baba. (Wafilipi 2:6-8) “Ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; 7 bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.” Baada ya kuikamilisha kazi hiyo kwa kifo chake msalabani mwanadamu alihitaji nafsi nyingine itakayofanya kazi ndani yake ili kuondoa tabia na mazoea ya dhambi ili kumuandaa kuwa raia mwema wa mbinguni na mtawala wa malimwengu. Kazi hiyo isingeweza kufanywa na Baba au Mwana isipokuwa na Roho Mtakatifu. (Wafilipi 1:6) “Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu.” Ingawa yeye haonekani kazi yake inaonekana na kupitia kwa kazi zake watu wengi wamebadilishwa. (Yohana 3:8) “Upepo huvuma upendako, na sauti yake waisikia, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda; kadhalika na hali yake kila mtu aliyezaliwa kwa Roho.”

Siku Yesu anabatizwa Nafsi hizi tatu zilishiriki tukio hilo. (Mathayo 3:16-17) “Naye Yesu alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake; na tazama, sauti kutoka mbinguni ikisema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye.” Kama ambavyo Baba na Mwana walivyo na sifa ya kuumba ambayo miungu wengine wa mataifa hawana, Roho Mtakatifu anayo sifa ya kuumba. (Ayubu 33:4) “Roho ya Mungu imeniumba, Na pumzi za Mwenyezi hunipa uhai.”

Kumekuwepo ugumu katika kumkubali Roho Mtakatifu kama nafsi na kumkubali kama ana hadhi sawa na Baba na Mwana. Hii imetokana kwanza na Jina analobeba na namna ambavyo kwa nyakati mbalimbali Baba na Mwana wamekuwa wakimtuma kiasi cha kudhaniwa kuwa anamilikiwa na nafsi hizo mbili. Roho Mtakatifu ameitwa pia Roho wa Mungu na Roho wa Kristo. (Warumi 8:9) “Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake.” Katika mpango wa kumuokoa mwanadamu Baba ndiye anayemtuma Mwana kuja duniani na ndiye pia anayempeleka Roho Mtakatifu kuja kuchukua nafasi ya Mwana aliyekamilisha awamu yake. (Yohana 14:26) “Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.” Roho Mtakatifu anakuja akiwa na maagizo ya Baba na anakuja ili kumtukuza Kristo yaani kumfanya Kristo na kafara yake vikubalike kwa wanadamu. (Yohana 16:13-14) “Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake. Yeye atanitukuza mimi, kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari.”

Hii ndiyo maana ya kuitwa Roho wa Mungu au Roho wa Kristo kwa kuwa anakuja kuhitimisha kile kilichoanzwa na Baba kupitia matamko na maagizo na kile kilichotekelezwa na Kristo kupitia kafara yake. Kazi hii haimfanyi kuwa duni bali inamuweka katika nafasi ya juu kwa vigezo vya mbinguni. (Mathayo 20:26-28) “Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu ye yote anayetaka kuwa mkubwa kwenu, na awe mtumishi wenu; na mtu ye yote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu; kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.”

Roho Mtakatifu haonekani kupewa heshima ya juu na wanadamu kwa sababu ya mtazamo wao wa kumthamini zaidi yule anayeonekana kutumikiwa kuliko yule anayetumika. Yesu anamuona Roho Mtakatifu kwa jicho tofauti. (Mathayo 12: 32) “Naye mtu ye yote atakayenena neno juu ya Mwana wa Adamu atasamehewa, bali yeye atakayenena neno juu ya Roho Mtakatifu hatasamehewa katika ulimwengu wa sasa, wala katika ule ujao.”

Roho Mtakatifu ni nafsi yenye uwezo wa kuamua na kutenda bila kutegemea nafsi ya Baba au ya Mwana. (1 Wakorintho 12:8-11) “Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo Roho yeye yule; mwingine imani katika Roho yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika Roho yule mmoja; na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha; lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye.” Kwa uelewa huu mtu hawezi kutilia shaka juu ya Uungu wa Roho Mtakatifu na mamlaka yake.