Mungu ameijalia familia ya wanadamu kuwa sehemu ya familia yake. (Ayubu 2:1) “Tena kulikuwa na siku hao wana wa Mungu walipokwenda kujihudhurisha mbele za Bwana, Shetani naye akaenda kati yao, ili kujihudhurisha mbele za Bwana.” Wanadamu walipoteza hadhi ya kuwa wana wa Mungu na ndipo ikamlazimu Yesu kufanyika mwanadamu ili aturejeshee hadhi ya kuwa wana wa Mungu. Wakolosai 1:12-14 “Mkimshukuru Baba, aliyewastahilisha kupokea sehemu ya urithi wa watakatifu katika nuru. Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi.”
Hadhi yetu kabla ya dhambi ilikuwa chini ya hadhi ya Malaika. (Waebrania 2:6-9) “Mwanadamu ni nini hata umkumbuke, Ama mwana wa binadamu, hata umwangalie? Umemfanya mdogo punde kuliko malaika, Umemvika taji ya utukufu na heshima, Umemtawaza juu ya kazi za mikono yako; Umeweka vitu vyote chini ya nyayo zake. Kwa maana katika kuweka vitu vyote chini yake hakusaza kitu kisichowekwa chini yake. Lakini sasa bado hatujaona vitu vyote kutiwa chini yake. Ila twamwona yeye aliyefanywa mdogo punde kuliko malaika, yaani, Yesu, kwa sababu ya maumivu ya mauti, amevikwa taji ya utukufu na heshima, ili kwa neema ya Mungu aionje mauti kwa ajili ya kila mtu.”
Hapa twajifunza mambo mawili. Mwanadamu alikuwa na hadhi ya chini kuliko Malaika. Lakini alipoumbwa kwa sura na mfano wa Mungu akapewa hadhi ya utawala. (Mwanzo 1:26) “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.”
Mungu aliona anguko la mwanadamu kabla halijatokea na hivyo akaamuru aokolewe. (Zaburi 71:3) “Uwe kwangu mwamba wa makazi yangu, Nitakakokwenda sikuzote. Umeamuru niokolewe, Ndiwe genge langu na ngome yangu.” Mungu aliona uwezo wetu wa kutenda mema umepotea. (Yeremia 13:23) “Je! Mkushi aweza kuibadili ngozi yake, au chui madoa-doa yake? Kama aweza, ndipo na ninyi mwaweza kutenda mema, ninyi mliozoea kutenda mabaya.” Hata tukijaribu kutenda mema yale tutendayo yamejaa udhaifu, ubinafsi na upungufu mwingi. (Isaya 64:6) “Kwa maana sisi sote tumekuwa kama mtu aliye mchafu, na matendo yetu yote ya haki yamekuwa kama nguo iliyotiwa unajisi; sisi sote twanyauka kama jani, na maovu yetu yatuondoa, kama upepo uondoavyo.” (Yeremia 10:23) “Ee Bwana, najua ya kuwa njia ya mwanadamu haimo katika nafsi yake; kuelekeza hatua zake si katika uwezo wa mwanadamu.”
Mungu alimtuma Yesu duniani kwenye himaya ya Shetani na kwenye utumwa wa dhambi kama alivyomtuma Yusufu kwa ndugu zake na kama alivyomtuma Musa kuwakomboa Waisraeli. (Yohana 3:16) “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.” Yesu alikuwa mwana wa pekee wa Mungu kwa sababu kimsingi hakuwa mwanae hapo kabla. (Yohana 1:1-3,4) “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika. Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.”
Yesu ndiye mzaliwa wa kwanza aliyekuwepo kabla ya Adamu aliye mbali na asili ya wanadamu. (Waebrania 1:5-6) “Kwa maana alimwambia malaika yupi wakati wo wote, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa? Na tena, Mimi nitakuwa kwake baba, Na yeye atakuwa kwangu mwana? Hata tena, amletapo mzaliwa wa kwanza ulimwenguni, asema, Na wamsujudu malaika wote wa Mungu.” Alihitajika Mungu mwenyewe afanyike mzao wa Adamu ili awakomboe wote wa uzao wa Adamu kutoka utumwa wa dhambi. (Warumi 5:12) “Kwa hiyo, kama kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi.”
Tulihesabiwa kuwa tu wenye dhambi si kwa sababu tulishiriki kufanya hiyo dhambi bali tulifanywa wenye dhambi kupitia Adamu. (Warumi 5: 19) “Kwa sababu kama kwa kuasi kwake mtu mmoja watu wengi waliingizwa katika hali ya wenye dhambi, kadhalika kwa kutii kwake mmoja watu wengi wameingizwa katika hali ya wenye haki.” (Wakolosai 1:15) “Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi; naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote.”
Yesu alipofanyika mwanadamu aliendelea kuwa Mungu. (Tito 2:11-14) “Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa; tukilitazamia tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa Kristo Yesu, Mungu mkuu na Mwokozi wetu; ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe na maasi yote, na kujisafishia watu wawe milki yake mwenyewe, wale walio na juhudi katika matendo mema.” (1 Timotheo 2:5) “Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu.”
Kupitia Yesu tunafanyika wana wa Mungu na wazaliwa wa kwanza kama yeye alivyo. Akiwa katika hali ya ubinadamu aliendelea kushikilia Uungu wake kwa upande mmoja na ubinadamu wake kwa upande mwingine. Kama Mungu aliweza kusamehe dhambi, kusoma mawazo. (Mathayo 9:4) “Naye Yesu, hali akijua mawazo yao, akasema, Mbona mnawaza maovu mioyoni mwenu?” (Waebrania 2:17) “Hivyo ilimpasa kufananishwa na ndugu zake katika mambo yote, apate kuwa kuhani mkuu mwenye rehema, mwaminifu katika mambo ya Mungu, ili afanye suluhu kwa dhambi za watu wake.” Baada ya kupoteza hadhi hiyo Yesu akairejesha kwa yeye mwenyewe kufanyika mdogo kuliko Malaika. Yesu alifanyika mdogo kuliko Malaika pale alipofanyika mwanadamu. Akawa mzaliwa wa kwanza wa viumbe wote mwenye sifa ya Uungu na ubinadamu.