MASWALI YA KUJADILI: 2 TIMOTHEO 1:1-18
- Paulo alikuwa mtume wa Yesu Kristo kwa mapenzi ya Mungu. Unadhani mitume wanaoibuka kila uchao leo hii wapo kwa mapenzi ya Mungu? Paulo alikuwa akimwabudu Mungu kwa dhamira safi. Nitatambuaje kama namwabudu Mungu kwa moyo safi? Paulo anamsiffia Timotheo kuwa alikuwa na imani isiyo na unafiki. Imani isiyo na unafiki unaitambuaje? Paulo anadai imani ya Timotheo ilikuwapo kwanza kwa mama yake na bibi yake. Je imani inarithishwa?
- Karama ya Mungu inachochewaje? Je unaweza uwe na karama na usiitambue? Yesu alituokoa kisha akatuita kwa wito wake mkuu? Kati ya kuitwa na kuokolewa ni kipi huwa kinatangulia? Je matendo yetu yana nafasi gani katika kuokolewa kwetu? Yesu alibatilisha mauti na kuufunua uzima wakati gani na kwa kitendo gani? Je mtu aweza kwa wakati mmoja kuwa mhubiri, mtume, na mwalimu? Paulo anasema anamjua yeye aliyemwamini. Je ni muhimu kumjua uliyemwamini?
MASWALI YA KUJADILI: 2 TIMOTHEO 2:1-26
- Moja ya wajibu wa kiongozi wa kiroho ni kuwakabidhi watu waaminifu walio chini yake mambo ambayo watayafundisha kwa waumini. Je katika mazingira ambayo kila mmoja anajiona anajua jambo hili linawezekana? Ikiwa Bwana awajua walio wake ni kusema pia kuwa anawajua watakaopotea?
- Kama Bwana anawajua watakaochagua kupotea hiyo ni kusema hao watu hawawezi kubadilisha mtazamo na kuchagua kuokolewa? Mtumishi wa Mungu ajuaye kufundisha ana uwezekano wa kiasi gani wa kupunguza magomvi kwa watu anaowaongoza? Wateule wanaahidiwa kupewa wokovu na utukufu wa milele. Huo unaoitwa utukufu wa milele ni kitu gani?
- Hatua ya kwanza ya kuwasaidia wagombanao na viongozi wao wa kiroho ni kutuliza hasira yao ili wapate kurudiwa na fahamu zao na kutoka katika mtego wa Ibilisi. Je ni sahihi katika kutuliza hasira zao kuwaambia wanaongozwa na Ibilisi? Je ni muhimu wakajua kwamba wanaongozwa na Ibilisi?
- Kipawa cha kufundisha kwa watumishi wa Mungu kina mchango gani kwa ukuaji wa kanisa na ukomavu wa waumini? Ni wakati gani mtu huandikwa kuwa askari mwema wa Kristo Yesu?Je, Mungu ameahidi kutupa akili katika mambo yote atuambiayo katika Maandiko? Je, kuna ushahidi wowote kuwa neno la Mungu halifungwi?
- Kwa nini mashindano ya maneno hayana faida? Unafanya nini ili kuthibitisha umekubaliwa na Mungu? Bwana anatumia vigezo gani kuwajua walio wake? Utayatambuaje maswali ya upumbavu yasiyo na elimu yanayoweza kuzaa magonvi ili uyakatae mapema kabla hamjaenda mbali? Je, mtu mwenye hasira ana tatizo la kuondokewa na fahamu? Kwa nini haishauriwi kushindana na mtu mwenye hasira? Kwa nini kuonya kwa upole ni bora kuliko kuonya kwa ukali?
MASWALI YA KUJADILI: 2TIMOTHEO 3:1-17
- Nyakati za hatari za siku za mwisho hazitokani na vita bali zitatokana na kukithiri kwa tabia za ubinafsi. Kwa nini unadhani tabia zina mchango mkubwa katika kuzifanya siku za mwisho kuwa za hatari? Kwa nini nyakati za hatari zinatokea siku za mwisho? Kuna kosa gani kujipenda mwenyewe?
- Kwa nini wanawake wajinga wenye mizigo ya dhambi wamekuwa wahanga wa mafundisho ya uongo yanayoahidi uponyaji wa kimwili? Inawezekanaje watu wawe wakijifunza siku zote lakini wasiweze kabisa kuufikia ujuzi wa kweli?
- Kwa nini wanaopingana na ukweli hawataendelea sana? Kwa nini wanaitwa ni watu walioharibika akili zao na kukataliwa kwa mambo ya imani? Kwa nini wote wapendao kuishi maisha ya utawa katika Kristo wataudhiwa? Ahadi ya Mungu ya kuwa atawalinda watu wake iko wapi?
- Kwa nini wadanganyaji wana kawaida ya kudanganya wenzao na kujidanganya wenyewe? Je! Wanapojidanganya huwa wanajua kuwa wanajidanganya? Ili mtu wa Mungu akamilike anatakiwa atende kila tendo jema. Jambo hilo linawezekanaje kwa kuzingatia hoja ya Yeremia na Paulo? (Yeremia 13:23; Warumi 7:18)
- Je inatosha kufundisha, kuonya, na kuongoza watu kwa kutumia Maandiko peke yake bila kutumia Roho ya Unabii? Utajuaje kama vitabu vilivyo ndani ya Biblia vina pumzi ya Mungu?
MASWALI YA KUJADILI: 2TIMOTHEO 4:1-22
- Kuhubiri Neno ni lazima kuandamane na kukaripia, kukemea, na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho. Kwa nini uvumilivu unahitajika katika kazi hiyo? Je ni lazima kila mhubiri awe na vipengere vyote hivyo kwa viwango vinavyofanana?
- Unafanyaje ikiwa uliopewa kuwaongoza ni watu walioyakataa mafundisho ya uzima na wanaojiepusha wasisikie yaliyo kweli? Mtu anayechagua mtu wa kumhubiria anaonesha dalili ya kuwa mzima au bado hajapona?
- Dalili za kutambua kuwa umevipiga vita vilivyo vizuri na imani umeilinda ni nini? Je mtu aliyewahi kukutendea ubaya ukiwa kwenye kazi ya Mungu unatakiwa umuombee mabaya? Kwa nini Paulo alifanya hivyo? Unajifunza nini kwa Paulo ambaye hapo mwanzo alimkataa Marko lakini baada ya kusaidiwa na Barnaba akamwona anafaa kwenda naye kazini? Je maswali ya kizushi yanastahili kupewa nafasi ya kujadiliwa?