Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

WOKOVU KATIKA UTATU

WOKOVU KATIKA UTATU:

Imekuwepo dhana ya kupinga UTATU inayoendelezwa na wale wanaodhamiria kuitia doa sababu ya UKRISTO kukubaliana na dhana hiyo. Wapingao UTATU wana nia ya kuwaaminisha watu kuwa fundisho limekosewa na makanisa yaliyopokea fundisho hayakuwa makini na kwamba yaliingizwa kwenye mtego. Hii si mara ya kwanza kwa jitihada kama hizi za kulishambulia kanisa kwa mafundisho yake. Kanisa la Waadventista wa Sabato limekuwa likipokea lawama kadha wa kadha kuhusiana na mafundisho yake linayoyaamini. Katika siku za hivi karibuni lawama hizo zimeelekezwa katika fundisho la UTATU.
Kanisa la Waadventista wa Sabato linayo mafundisho makuu 6.
1. Fundisho kuhusu Mungu
2. Fundisho kuhusu mwanadamu
3. Fundisho kuhusu wokovu.
4. Fundisho kuhusu Kanisa.
5. Fundisho kuhusu mwenendo wa Mkristo.
6. Fundisho kuhusu matukio ya siku za mwisho

Mafundisho haya ni matokeo ya utafiti wa kina na wa muda mrefu uliofanywa na watu makini na kuthibitishwa na mkutano mkuu wa kanisa wenye wajumbe kutoka pande zote za dunia. Hakukuwa na kukurupuka kama wanavyotaka kutuaminisha wale wanaokanusha mafundisho hayo.
Fundisho kuhusu Mungu ndilo linalobeba mafundisho mengine yote matano. Kushindwa kulielewa fundisho hili hujenga msingi wa kutoyaelewa mafundisho mengine yaliyobaki. Kwa sehemu kubwa fundisho kuhusu Mungu linabeba fundisho kuhusu wokovu wa mwanadamu. Fundisho kuhusu wokovu linategemea uelewa wa mtu juu ya fundisho kuhusu Mungu.

Fundisho kuhusu Mungu linasema yupo Mungu aliyeumba mbingu na nchi na vyote viijazavyo kwa uwezo wake mwenyewe. Taarifa juu ya Mungu huyo na uwezo wake wa kuumba na kuokoa zinapatikana katika Neno lake lililoandikwa lijulikanalo kama Maandiko Matakatifu. Kupitia Maandiko tunajulishwa kuwa Mungu ni mmoja na hakuna Mungu mwingine aliye kama yeye (Isaya 46:9; Kumb. 6:9).
Lakini katika namna ya kushangaza mara nyingi linapokuja swala la kuumba au kumuokoa mwanadamu Mungu huyu mmoja hujitambulisha katika nafsi zaidi ya moja.

Katika kuumba mwanadamu kauli ya kuzindua uumbaji ilikuja katika uwingi. "Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi." (Mwanzo 1:26)
Kauli hii ya uwingi inaashiria uwepo wa Mungu mmoja mwenye nafsi zaidi ya moja. Na uelewa huu unatiliwa mkazo zaidi wakati Mungu alipokuja kuwaokoa wajenzi wa mnara wa Babeli. Kauli iliyotumika kuanzisha mradi wa kusitisha uasi uliokuwa unaendelea ilikuwa katika uwingi kuashiria kuwa kulikuwa na zaidi ya nafsi moja katika huyo Mungu mmoja. "Bwana akasema, Tazama, watu hawa ni taifa moja, na lugha yao ni moja; na haya ndiyo wanayoanza kuyafanya, wala sasa hawatazuiliwa neno wanalokusudia kulifanya. Haya, na tushuke huko, tuwachafulie usemi wao ili wasisikilizane maneno wao kwa wao." (Mwanzo 11:6-7)

Kwa kusoma Maandiko imekuwa dhahiri kuwa zipo nafsi tatu za Uungu. Yesu alizitaja nafsi hizo alipokuwa anaelekeza utaratibu wa kufuata wakati mtu atakapohitaji kubatizwa. Aliagiza majina matatu yatumike kuwakilisha nafsi tatu za Uungu. "Go ye therefore, and teach all nations, baptizing them in the name of the Father, and of the Son, and of the Holy Ghost." "Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu." (Mathayo 28:19).

Hapa mtu aweza kujiuliza kwa nini majina yawe matatu na yasiwe mawili au moja? Mungu alikusudia kuitilia uzito dhana ya utatu au nafsi tatu za Uungu zinazounda Mungu mmoja. Hapa Mungu anaonekana katika harakati za kufanikisha wokovu wa mwanadamu akiwa katika utendaji wa nafsi tatu. Kwa hiyo Mungu ni mmoja ambaye katika shughuli ya kumuumba na kumkomboa mwanadamu huonekana na kutenda kazi katika nafsi tatu za Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu.

Majina ya nafsi tatu za Uungu yapo kimkakati zaidi na wala hayaashirii kuzidiana kwa uwezo wala hadhi. Nafsi ya Mwana ambaye ndiye Yesu haina hadhi ndogo kuliko nafsi ya Baba kama inavyodhaniwa na baadhi ya watu. Yesu mwenyewe alithibitisha hilo. "I and my Father are one. Mimi na Baba tu umoja." (Yohana 10:30). Kauli hiyo inatuelekeza kuwa nafsi ya Baba na nafsi ya Mwana hawazidiani. Alivyo huyu ndivyo alivyo huyu. Wote wana sifa za Uungu. Yesu alikuwa Mungu kabla hajafanyika mwanadamu (Wafilipi 2:5-8) na aliendelea kuwa Mungu hata alipofanyika kuwa mwanadamu (Mathayo 1:23; Wakolosai 2:9; Tito 2:10; Tito 2:13).

Baba (nafsi ya Baba) aliwashawahi kukiri kuwa Yesu anayetambulika kama Mwana kwa sababu za kimkakati alikuwa Mungu (Waebrania 1:8).
Kimsingi Maandiko Matakatifu yanampa Yesu hadhi kubwa inapokuja majukumu ya kuumba na kumkomboa mwanadamu (Yohana 1:1-3; Wakolosai 1:16; Waebrania 2:9-10; Wafilipi 2:9-11; Mathayo 18:28; Yohana 3:35).

Yesu mwenyewe wakati akitambulishwa kwa wanadamu alitambulishwa kama Mwana wa Mungu (Luka 3:21-22) na alitambulishwa pia kama Baba wa milele (Isaya 9:6). Hii ni kwa sababu majukumu mengi ya Baba katika kipindi cha mchakato wa ukombozi na baada ya ukombozi kukamilika yatawekwa kwa Mwana (Yohana 5:22; Waebrania 1:6).

Majina ya Baba na Mwana ni ya kimkakati. Si lazima yawe ya kudumu. Tunamuona Yesu akiitwa majina mengi ya kimkakati kama Mwanakondoo wa Mungu, Mwana wa Mungu, Mwana wa Daudi nk. Haya yanalenga kutimiza kusudi fulani kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu.

Hali kadhalika Roho Mtakatifu ameonekana akitambulishwa kama Upepo (Matendo 2:3-4), Mafuta (Luka 4:18), au Hua (Mathayo 3:16) nk.
Jukumu la Roho Mtakatifu katika ukombozi wa mwanadamu linafuatia lile la Baba na la Mwana. Baba katika ukombozi wa mwanadamu ndiye anayekabidhi ufalme kwa Yesu (kama mwakilishi wa wanadamu) na kwa wanadamu walioshinda kwa kazi ya ukombozi na nafsi zote tatu za Uungu (Mathayo 20:23; Luka 12:32; Danieli 7:13-14, 27).

Jukumu jingine la Baba ni kutoa matamko ya kuanza kwa hatua fulani katika mchakato wa kumkomboa mwanadamu. Tangazo la ujio wa Yesu (Mathayo 17:5). Baba amehusika pia kutoa kibali cha Neno kufanyika mwili kwa kusudi la kuwakomboa wanadamu (Yohana 3:16).
Mungu alupompoteza mwanadamu baada ya kuanguka dhambini lilikuwa jambo zito lililohitaji kutafutiwa ufumbuzi. Ufumbuzi pekee ulikuwa ni mmoja miongoni mwa nafsi tatu za Uungu afanyike mwanadamu kwa hiyari yake mwenyewe na kwenda kuishi maisha ya ushindi dhidi ya dhambi na hatimaye kulipa adhabu ya dhambi kwa kifo cha msalabani.

Yesu akatolewa kwenda kuifanya kazi hiyo jambo lililoleta uchungu mkubwa kwa nafsi zote tatu. Yesu akatwaa nafasi ya Adamu aliyeshindwa. Akapitia majaribu yote Adamu aliyopitia na kushinda (1 Petro 2:21-24). Yeye alibeba adhabu yetu na kutulipia hukumu ya kifo (Warumi 8:1; Yohana 5:24). Ushindi wake ndiyo ukawa ushindi wetu (Warumi 5:12-18). Hakuitwa Mwana wa Mungu kwa sababu alizaliwa na Mungu. Aliitwa Mwana wa Mungu maana yeye ndiye mzaliwa wa kwanza katika kizazi cha Wanadamu aliyeshinda dhambi. Tukimwamini uahindi wake unahesabiwa kwetu.

Roho Mtakatifu ndiye aliyefanya iwezekane Yesu mwenye asili ya Uungu atungwe mimba katika tumbo la mwanamke bikira (Mathayo 1:18-20).
Roho Mtakatifu ndiye mwenye jukumu la kubadilisha tabia za wanadamu ili zifanane na tabia za wakazi wa mbinguni. Yeye hufanikisha hilo kwa kubadilisha asili yetu ya dhambi (Wagalatia 5:17-18). Mchakato huo huanzia pale mtu anaposikia hatia moyoni mwake na kutamani kurejea kwa Mungu (Matendo 2:37-38). Mabadiliko hayo ni ya kudumu katika siku zote za uhai za aliyeamini na kwa kadri mtu anavyoendelea kutakasika ndivyo anavyojiona asivyofaa (Wafilipi 3:12-14).

Yesu akiitukuza kazi ifanywayo na Roho Mtakatifu aliionesha kuwa na ya muhimu ambayo haipaswi kubezwa (Mathayo 12:32).
Roho Mtakatifu ana hadhi ya Uungu iliyo sawa na ya Baba na Mwana. Yeye huchunguza mawazo yote ya Mungu na kujua siri zote za Mungu (1 Kor. 2:10)