Ujana ni kipindi cha mpito kutoka utotoni kuelekea utu uzima. Hiki ndicho kipindi cha kuanza kujitambua, kujitathmini, kuweka malengo na kuweka mipango ya kufikia malengo hayo. Katika kipindi hiki kijana aliye timamu hujihoji ametoka wapi anaelekea wapi na afanye nini ili afike kule alikodhamiria kufika akiwachukua baadhi ya watu kama kipimo na hamasa ya kule anakotaka kufika. Mungu anamtarajia kijana kuweka ndoto zake za maisha na mpango mkakati wa kuzifikia ndoto au maono hayo katika umri huu. (Mhubiri 11:9) “Wewe kijana, uufurahie ujana wako, na moyo wako ukuchangamshe siku za ujana wako, ukaziendee njia za moyo wako, na katika maono ya macho yako, lakini ujue wewe ya kwamba kwa ajili ya hayo yote Mungu atakuleta hukumuni.”
Kuchagua ungependa kuwa nani?
Ujana ni wakati wa kuchagua ungependa kuwa nani maishani. Kwa sehemu kubwa umakini katika kufanya uchaguzi huo utategemea makuzi aliyopitia na namna yalivyomjenga kujiamini. Kwa kawaida kama alipata malezi ya kudekezwa au ya vitisho na maamrisho yasiyompa uhuru wa kufanya maamuzi na kujieleza atakuwa na kiwango kikubwa cha kutojiamini na uwezo mdogo wa kujua anataka kuwa nani na kuwa wapi baada ya muda gani. Lakini hata kama kijana alipitia makuzi mabaya yaliyoshusha uwezo wake wa kujiamini anapaswa kutambua kuwa Mungu ameahidi kumpigania na kumuokoa katika hatari zote. (Isaya 41:10) “Usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu.”
Hukumu uzeeni
Ujana ni wakati wa kupanda na uzeeni ni wakati wa mavuno. Ni wakati wa kuchagua welekeo wa Maisha baada ya kujiridhisha. Watu wa kukusaidia kufanya maamuzi katika hatua hii ni wengi; wengine wana ushauri mwema na wengine wana ushauri mbaya. Hukumu inayotajwa kumjia kijana endapo hataufurahia ujana wake na kujiwekea malengo ya kusaidia kutimiza ndoto zake itatokea hapa hapa duniani na hasa katika umri wa utu uzima au uzeeni. Umri wa uzee ni umri wa majuto kwa wengi kwa kuwa nguvu za kutekelezea mipango waliyojiwekea au waliyochelewa kujiwekea zimepungua. Wanaochekelea uzeeni ni wale ambao walifanikiwa kuutendea haki ujana wao. Katika wakati huo mtu hugundua amepoteza fursa muhimu ya kufikia ndoto zake akiwa amechelewa. (Mhubiri 12:1) “Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo.”
Yesu aahidi kuwasaidia vijana
Mungu ameweka ndani ya vijana nguvu ifananayo na moto unaowaka katika kuziona changamoto kuwa fursa ya kuleta mageuzi. Ujana hutafuta majawabu ya matatizo yanayoonekana kuwa kikwazo cha familia au jamii husika. Faida ya ujana ni kuwa sehemu kubwa ya yale unayoyapanga una uwezo wa kuyatekeleza kwa kuwa nguvu na wakati wa kuyatekeleza vipo tele kuliko kwa wale waliovuka kipindi hicho. (Joshua 1:6-7) “Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa. Uwe hodari tu na ushujaa mwingi, uangalie kutenda sawasawa na sheria yote aliyokuamuru Musa mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kuume, au wa kushoto, upate kufanikiwa sana kila uendako.”
Ujana na ari ya ukombozi
Ujana ni kipindi cha kutathmini waliokutangulia (wazazi au viongozi wajo) walikwama wapi hata kukusababisha unapata ugumu wa kujinasua. Kupitia katika tathmini hiyo unafikia hitimisho la njia ya kujinasua kwenye mkwamo huo. (1 Samweli 17:26) “Daudi akaongea na watu waliosimama karibu, akisema, Je! Atafanyiwaje yeye atakayemwua Mfilisti huyo, na kuwaondolea Israeli aibu hii? Maana Mfilisti huyu asiyetahiriwa ni nani hata awatukane majeshi ya Mungu aliye hai?” (1 Samweli 17:45) “Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la BWANA wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana.” (2 Wafalme 5:3) “Akamwambia bibi yake, Laiti bwana wangu angekuwa pamoja na yule nabii aliyeko Samaria! Maana angemponya ukoma wake.”
Tuwaamini vijana
Vijana wakiamua wanaweza kubadilisha mambo yanayoonekana na wazee kama yaliyoshindikana. Wazazi na kanisa watanufaika sana ikiwa watawaamini vijana na kuwaachia majukumu nyumbani na kanisani. Vijana wasipotumika kanisani watatumika na Shetani. Wale vijana wanapopewa nafasi na wazazi au na kanisa waitumie nafasi hiyo kuwadhihirishia wanaowatilia mashaka kuwa wanaweza. (1 Timotheo 4:12) “Mtu awaye yote asiudharau ujana wako, bali uwe kielelezo kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi.” (Yoshua 1:9) “Je! Si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako.”
Yesu awavusha vijana katika majaribu ya dhambi
Yesu anatamani kuwapa vijana wa leo ushindi kama alivyowapa Danieli, Yusufu, na Musa ambao hawakupenda kujifurahisha na anasa za dunia bali walichagua kumfurahisha Mungu wao. Waebrania 11:23-26) “Kwa imani Musa alipokuwa mtu mzima, akakataa kuitwa mwana wa binti Farao; akaona ni afadhali kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo; akihesabu ya kuwa kushutumiwa kwake Kristo ni utajiri mkuu kuliko hazina za Misri; kwa kuwa aliyatazamia hayo malipo.” (Mwanzo 39:11-12) “Ikawa, siku moja, akaingia nyumbani atende kazi yake, wala hapakuwa na mtu katika watu wa nyumbani humo ndani; huyo mwanamke akamshika nguo zake, akisema, Lala nami. Yusufu akaiacha nguo yake mkononi mwake, akakimbia, akatoka nje.”
Vijana wanaweza kuinuka tena baada ya anguko
Kijana aliyejikuta amenasa kwenye madanganyiko ya dunia na makundi mabaya anayo nafasi ya kujirudi na kuanza upya maisha yanayomtukuza Mungu. Wazazi wasiwakatie tamaa vijana wao waliofeli shule au waliokatiza masomo kwa ujauzito au waliozalia nyumbani. Wawasaidie kuinuka tena. (Waamuzi 11:1-5) “Basi huyo Yeftha, Mgileadi, alikuwa mtu shujaa sana, naye alikuwa ni mwana wa mwanamke kahaba; Gileadi akamzaa Yeftha. Mkewe huyo Gileadi akamzalia wana; na hao wana wa mkewe hapo walipokuwa wamekua wakubwa wakamtoa Yeftha, na kumwambia, Wewe hutarithi katika nyumba ya babaetu; kwa sababu wewe u mwana wa mwanamke mwingine. Ndipo Yeftha akawakimbia hao nduguze, akakaa katika nchi ya Tobu; na watu mabaradhuli walikwenda na kutangamana na Yeftha, wakatoka kwenda pamoja naye. Ikawa baadaye, wana wa Amoni wakapigana na Israeli. Ikatukia, hapo wana wa Amoni walipopigana na Israeli, wazee wa Gileadi wakaenda kumtwaa huyo Yeftha katika ile nchi ya Tobu.”
Vijana watiwe moyo
Katika familia, ukoo, au kanisani panahitajika watu wanaoweza kuwatia moyo vijana wasiokubalika kwenye jamii, kanisani, au nyumbani kutokana na kuteleza kwenye mwendo wa Maisha yaliyopita, ili wainuke na kuanza kujitafuta tena. (Matendo 9:26-27) “Na Sauli alipofika Yerusalemu, alijaribu kujiunga na wanafunzi, nao walikuwa wakimwogopa wote, wasisadiki ya kuwa yeye ni mwanafunzi. Lakini Barnaba akamtwaa, akampeleka kwa mitume, akawaeleza jinsi alivyomwona Bwana njiani, na ya kwamba alisema naye, na jinsi alivyohubiri kwa ushujaa katika Dameski kwa jina la Yesu.” (Matendo 15:37-39) “Barnaba akaazimu kumchukua Yohana aliyeitwa Marko pamoja nao. Bali Paulo hakuona vema kumchukua huyo aliyewaacha huko Pamfilia, asiende nao kazini. Basi palitokea mashindano baina yao hata wakatengana. Barnaba akamchukua Marko akatweka kwenda Kipro.” (2 Timotheo 4:11) “Luka peke yake yupo hapa pamoja nami. Umtwae Marko, umlete pamoja nawe, maana anifaa kwa utumishi.”
Vijana wavumiliwe kwa mitazamo yao
Katika umri wa ujana hasa wakati wanapopitia mabadiliko ya kibaolojia ni rahisi kwa vijana kufanya maamuzi yawezayo kuwaletea majuto huko mbeleni. Hii inatokana na ukweli kuwa katika umri huo kijana huwa na uthubutu wa kutaka kujaribu mambo aliyokuwa anaamini hapo mwanzo kuwa hayawezi. (Luka 15:13-16) “Hata baada ya siku si nyingi, yule mdogo akakusanya vyote, akasafiri kwenda nchi ya mbali; akatapanya mali zake huko kwa maisha ya uasherati. Alipokuwa amekwisha tumia vyote, njaa kuu iliingia nchi ile, yeye naye akaanza kuhitaji. Akaenda akashikamana na mwenyeji mmoja wa nchi ile; naye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe. Akawa akitamani kujishibisha kwa maganda waliyokula nguruwe, wala hapana mtu aliyempa kitu.
Vijana wasifokewe kama watoto
Vijana wa rika hili huwa hawapendi kufokewa au kuamrishwa bila kuelezwa sababu ya hatua inayochukuliwa ila wanapendelea kupewa maelekezo yanayotambua kuwa wao wamekua na wana uwezo wa kuchambua mambo na kwamba wanayo haki pia ya kushirikishwa. (1 Samweli 2:22-24) “Basi Eli alikuwa mzee sana; naye alisikia habari za mambo yote ambayo wanawe waliwatenda Waisraeli; na jinsi walivyolala na wanawake waliokuwa wakitumika mlangoni pa hema ya kukutania. Akawaambia, Mbona mnatenda mambo kama hayo? Maana nasikia habari za matendo yenu mabaya kwa watu hawa wote. Sivyo hivyo, wanangu, kwa maana habari hii ninayoisikia si habari njema; mnawakosesha watu wa Bwana.”
Vijana wanahitaji kuelekezwa siyo kuburuzwa
Vijana wanahitaji kuelekezwa na siyo kuburuzwa. Wanahitaji kushirikishwa katika maamuzi. Wanataka kujua kwa nini wanafanya kile walichoagizwa kufanya na kwa nini kisifanyike katika namna nyingine iliyo tofauti na yenye tija zaidi. Wazazi na viongozi wa vijana wafanye vikao vya mara kwa mara kufafanua maamuzi yaliyofanyika na mara nyingine kuwashirikisha kutoa maoni kabla ya kufanyika kwa maamuzi. (Luka 15:28-32) “Akakasirika, akakataa kuingia ndani. Basi babaye alitoka nje, akamsihi. Akamjibu baba yake, akasema, Tazama, mimi nimekutumikia miaka mingapi hii, wala sijakosa amri yako wakati wo wote, lakini hujanipa mimi mwana-mbuzi, nifanye furaha na rafiki zangu; lakini, alipokuja huyu mwana wako aliyekula vitu vyako pamoja na makahaba, umemchinjia yeye ndama aliyenona. Akamwambia, Mwanangu, wewe u pamoja nami sikuzote, na vyote nilivyo navyo ni vyako. Tena, kufanya furaha na shangwe ilipasa, kwa kuwa huyu ndugu yako alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana.”
Shikamana na wanaokuelewa na kukutia moyo
Kijana mwenye kiu ya mafanikio atashikamana na wenye kiu ya mafanikio na wenye mrengo unaofanana na wake ili kuinua hali yake ya elimu, ujuzi, au uchumi bila kujali ni wa rika lililo tofauti na lake au ataonekanaje na watu wa rika lake. Lutu alichagua kuandamana na Ibrahimu katika jitihada za kuitafuta kesho yake. Waswahili wanasema alikuwa anajitafuta. (Mwanzo 11:27,31) “Na hivi ndivyo vizazi vya Tera. Tera akamzaa Abramu, na Nahori, na Harani. Harani akamzaa Lutu. Tera akamtwaa Abramu mwanawe, na Lutu mwana wa Harani, mwana wa mwanawe, na Sarai mkwewe, mke wa Abramu mwanawe, wakatoka wote katika Uru wa Wakaldayo, waende nchi ya Kanaani, wakafika mpaka Harani wakakaa huko.” Amosi 3:3 Je! Watu wawili waweza kutembea pamoja, wasipokuwa wamepatana? (Matendo 15:36) “Baada ya siku kadha wa kadha Paulo akamwambia Barnaba, Haya! Mrejee sasa tukawaangalie hao ndugu katika kila mji tulipolihubiri neno la Bwana, wa hali gani. Barnaba akaazimu kumchukua Yohana aliyeitwa Marko pamoja nao. Basi palitokea mashindano baina yao hata wakatengana. Barnaba akamchukua Marko akatweka kwenda Kipro.”
Nenda katafute maisha
Ikiwa umeshindwa kuinuka na kupata suluhisho la mipango yako ya maisha hapo ulipo nenda mahali pengine ukatafute maisha. Wakati fulani bahati yako ipo mbali na hapo mahali ulipo au hapo ulipozaliwa na kukulia. Uamuzi wa kijana Lutu wa kwenda kuishi na baba yake mkubwa Ibrahimu ingawa ulikuwa kama wa kujitoa mhanga hatimaye ulimlipa. Lutu alitoka kwenye daraja la wat0u wa kawaida na kuingia kwenye daraja la watu wa uchumi wa juu. (Mwanzo 13:5-6) “Na Lutu aliyesafiri pamoja na Abramu, yeye naye alikuwa na makundi ya ng’ombe na kondoo, na hema. Na ile nchi haikuwatosha, ili wakae pamoja; maana mali zao zilikuwa nyingi, hata wasiweze kukaa pamoja.” (Mwanzo 32:9-10) “Yakobo akasema, Ee Mungu wa baba yangu Ibrahimu, na Mungu wa baba yangu Isaka, Bwana, uliyeniambia, Rudi uende mpaka nchi yako, na kwa jamaa zako, nami nitakutendea mema; mimi sistahili hata kidogo hizo rehema zote na kweli yote uliyomfanyia mtumwa wako; maana nalivuka mto huo wa Yordani na fimbo yangu tu, na sasa nimekuwa matuo mawili.”
Yesu na mpango wa kutajirisha vijana
Mafanikio makubwa ya kiuchumi hutegemea ni kwa kiwango gani mhusika anazifahamu kanuni za uwakili na kuziishi. Mafundisho ya uwakili wa Kikristo yanatujulisha kuwa mafanikio ya kiuchumi yanategemea jinsi asivyonyanyapaa kufanya kazi zilizopo, jinsi anavyotumia kwa uaminifu muda wa kazi, jinsi anavyojiongezea ujuzi na maarifa ili kurahisisha na kuboresha uzalishaji wa huduma au bidhaa anayozalisha, jinsi anavyoweka juhudi ya kutosha kwenye uzalishaji wale, na jinsi anavyochunga nidhamu ya matumizi kwenye mapato yake. (Wafilipi 4:19) “Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu.” (2 Wakorintho 9:8) “Na Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema.”
Mshirikishe Yesu
Kijana aliyedhamiria kufanikiwa katika maisha hatamsahau Mungu katika mapato yake. (Mithali 3:9) “Mheshimu Bwana kwa mali yako, Na kwa malimbuko ya mazao yako yote.” Yakobo akiwa njiani kumkimbia ndugu yake Esau aliweka nadhiri ya kumtolea Mungu sehemu ya kumi ya pato lake ikiwa Mungu kwa upande wake atafanikisha mambo yake. (Mwanzo 28:20-22) “Yakobo akaweka nadhiri akisema, Mungu akiwa pamoja nami, akinilinda katika njia niiendeayo, na kunipa chakula nile, na nguo nivae; nami nikirudi kwa amani nyumbani kwa baba yangu, ndipo BWANA atakuwa Mungu wangu. Na jiwe hili nililolisimamisha kama nguzo litakuwa nyumba ya Mungu; na katika kila utakalonipa hakika nitakutolea wewe sehemu ya kumi."
Usilalamikie umaskini
Hakuna sababu ya kijana kulalamikia umaskini alionao kama kikwazo cha mafanikio. Anachotakiwa kijana ili kujikwamua kwenye umaskini ni kutumia nguvu zake kama mtaji. (Kumb. 8:18) “Bali utamkumbuka Bwana, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo.” Shughuli ambazo mtaji wake ni nguvu ni kama kulima, kufyeka, kufyatua tofali za udongo, kufua, kupika, kukata mkaa, na kadhalika. Kinachohitajika kwa kijana ni kutoona aibu maana ni kazi za mpito ambazo my huzifanya akisubiri alizozisomea au anazozipenda. (Mithali 14:23) “Katika kila kazi mna faida; Bali maneno ya midomo huleta hasara tu.” (Mithali 28:19) “Alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele; Bali afuataye mambo ya upuzi atapata umaskini wa kumtosha.”
Elimu mtaji wa kukupeleka kwenye mafanikio
Kazi inapofanywa kwa ujuzi na maarifa zaidi badala ya kutegemea nguvu peke yake, malipo yake huzidi kuwa mazuri na uzalishaji wake kuwa wenye ufanisi na tija zaidi. Elimu inamfanya mtu kuwa Hodari kwa maneno na matendo na kumuongezea ari ya kuitumikia jamii yake. (Matendo 7:22-23) “Musa akafundishwa hekima yote ya Wamisri, akawa hodari wa maneno na matendo. Umri wake ulipopata kama miaka arobaini akaazimu moyoni mwake kwenda kuwatazama ndugu zake Waisraeli.” Biblia inahimiza kuitafuta elimu, uiuzi, maarifa, au teknolojia kama kitu muhimu kinachofananishwa na uzima wa mtu. (Mithali 4:13) “Mkamate sana elimu, usimwache aende zake; Mshike, maana yeye ni uzima wako.” Elimu ni nyenzo muhimu ambayo kijana hapaswi kuikosa. Familia ifanye kadri inavyowezekana kuwekeza kwenye elimu kwa mapato yake yote. (Methali 4:7) “Bora hekima, basi jipatie hekima; Naam, kwa mapato yako yote jipatie ufahamu.”
Yesu chimbuko la hekima
Yesu ni chimbuko la hekima na akili. (Warumi 16:27) “Ndiye Mungu mwenye hekima peke yake. Utukufu una yeye kwa Yesu Kristo, milele na milele. Amina.” Wale waliomweka Yesu mbele katika mipango ya maisha yao wana nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika masomo yao kama Danieli na wenzake. (Danieli 1:19-20) “Naye mfalme akazungumza nao; na miongoni mwao wote hawakuonekana waliokuwa kama Danieli, na Hanania, na Mishaeli, na Azaria; kwa hiyo wakasimama mbele ya mfalme. Na katika kila jambo la hekima na ufahamu alilowauliza mfalme, akawaona kuwa walifaa mara kumi zaidi ya waganga na wachawi waliokuwa katika ufalme wake.”
Usibague kazi
Kwa upande wa afya ya mwili na akili ya kijana wako hakikisha anapata lishe bora na ya kutosha. Usiruhusu Watoto wako kutokula vizuri wakiwa hapo nyumbani au wakiwa shuleni ili miili ijengeke kikamilifu. Mzoeshe kula, kushiba, na hata kusaza ili kumuongezea ari ya kujitafutia atakapoanza kujitegemea. Weka utaratibu ili ulaji uendane na kukifanyia kazi hicho chakula. (Mithali 31:15) “Tena huamka, kabla haujaisha usiku; Huwapa watu wa nyumbani mwake chakula; Na wajakazi wake sehemu zao.” Ili kupata mchango wa kila mtoto katika utendaji kazi hapo nyumbani ni wajibu wa wazazi kumpangia kila mtu jukumu lake na muda anaotakiwa kukamilisha kazi hiyo. (Mithali 31:27) “Huangalia sana njia za watu wa nyumbani mwake; Wala hali chakula cha uvivu.”
Washirikishe walezi wengine kwenye malezi ya wanao
Mhimize na kumruhusu mwanao kujiunga na vyama vinavyolea kiroho kanisani, mashuleni na vyuoni ili vimsaidie kuwa na maadili. Shirikiana na waalimu wa shule yake wanapokuwa taarifa za utovu wa nidhamu wa mtoto wako badala ya kumtetea. Ipo haja ya wazazi na viongozi wa kanisa kuwa na vikao vya mara kwa mara na vijana ili kusikiliza maoni na malalamiko yao. Utovu wa maadili ukijadiliwa kwa uwazi na bila vitisho hatimaye tishio la ushoga, usagaji na mimba zisizotarajiwa na tabia zingine zisizofaa vitathibitiwa. Paulo alifanikiwa kumbadilisha Onesmo ambaye hapo awali alikuwa na mwenendo mbaya bada ya kukaa naye kwa muda. Shule za kikanisa na idara zinazolea Watoto kanisani zinafanya jukumu hilo pia, (Filemoni 1:10-11) “Nakusihi kwa ajili ya mtoto wangu niliyemzaa katika vifungo vyangu, yaani, Onesimo; ambaye zamani alikuwa hakufai, bali sasa akufaa sana, wewe na mimi pia.”
Msidanganywe na mitandao ya kijamii
Zinaa huharibu mahusiano ya vijana wenyewe na mahusiano baina ya vijana na wazazi, na waalimu wao na pia huvuruga matarajio ya siku za usoni. (1 Wakorintho 6:18) “Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe.” Vijana wanapojiingiza mapema kwenye mahusiano ya kingono wanajiweka katika hatari ya kujipatia maradhi ya kuambukiza na mimba zisizotarajiwa. (Wimbo Ulio Bora 3:5) “Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, Kwa paa na kwa ayala wa porini, Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, Hata yatakapoona vema yenyewe.”
Msijiingize majaribuni
Wakati mwingine mambo yanayoweza kukushawishi kuingia kwenye mazoea ya ngono za ujanani ni mazungumzo mabaya au picha mbaya za uchi. (1 Wakorintho 15:33) “Msidanganyike; Mazungumzo mabaya huharibu tabia njema.” (Ayubu 31:1) “Nilifanya agano na macho yangu; Basi nawezaje kumwangalia msichana” Msichana anayetajwa hapa (ambaye haifai wavulana kumwangalia) ni yule aliye kwenye mazingira ya kumtamanisha mtu kingono. Awe ni yule apitaye barabarani, aliye kwenye picha za mnato au aliye kwenye video, weka agano la kutowaangalia wanawake hao. Kumbuka kuwa tendo la ngono daima huanzia kwenye mawazo. (Mathayo 5:28) “Lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake.”
Jitenge na makundi mabaya
Mbinu nyingine ya kujizuia na majaribu ni kujitenga na makundi mabaya. Marafiki wabaya ambao vijana hukutana nao wakiwa shuleni na vyuoni ndiyo kimekuwa chanzo kikubwa cha wao kuharibikiwa maadili. Makundi rika hayo huweza kuwafundisha umalaya, ulevi wa pombe, wizi na ujambazi hata ulawiti na matumizi ya madawa ya kulevya. Biblia inashauri kuachana na makundi hayo. (Marko 9:43) “Na mkono wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima u kigutu, kuliko kuwa na mikono miwili, na kwenda zako jehanum, kwenye moto usiozimika.” Mkono unaoelekezwa kukatwa hapa ni hayo makundi maovu.
Mazingira hatarishi kwa wasichana
Yapo mazingira yasiyo salama kwa vijana kuyaendea. Mazingira ambayo wavulana wanaishi peke yao si mazingira ya msichana kuyaendea. (2 Samweli 13:10-14) “Amnoni akamwambia Tamari, Kilete chakula chumbani, nipate kula mkononi mwako. Basi Tamari akaitwaa mikate aliyoifanyiza, akamletea Amnoni nduguye mle chumbani. Naye alipokwisha kuileta karibu naye, ili ale, Amnoni akamkamata, akamwambia, Njoo ulale nami, ndugu yangu. Naye akamjibu, La, sivyo, ndugu yangu, usinitenze nguvu; kwani haifai kutendeka hivi katika Israeli; usitende upumbavu huu. Nami nichukue wapi aibu yangu? Wewe nawe utakuwa kama mmoja wa wapumbavu wa Israeli. Basi, sasa, nakusihi, useme na mfalme; kwa maana hatakukataza kunioa. Walakini yeye hakukubali kusikiliza sauti yake; naye akiwa na nguvu kuliko yeye, akamtenza nguvu, akalala naye.”
Mazingira hatarishi kwa wavulana
Mvulana au msichana asiruhusu sehemu zake za siri kushikwashikwa na mtu wa jinsia nyingine. Wengi wamejikuta wakianguka kwenye uzinzi au kubakwa kupitia njia hiyo. Tahadhari hiyo inahusu watu wote kuanzia kaka na dada yako, mama na baba yako, ndugu zako wa karibu na watu wazima wote isipokuwa wataalam wa afya wakati wa kukuhudumia hospitali. (Mithali 7:7-13, 21-22) “Nikaona katikati ya wajinga, Nikamtambua miongoni mwa vijana, Kijana mmoja asiyekuwa na akili, Akipita njiani karibu na pembe yake, Akiishika njia iendayo nyumbani kwake, Wakati wa magharibi, wakati wa jioni, Usiku wa manane, gizani. Na tazama, mwanamke akamkuta, Ana mavazi ya kikahaba, mwerevu wa moyo; Ana kelele, na ukaidi; Miguu yake haikai nyumbani mwake. Mara yu katika njia kuu, mara viwanjani, Naye huotea kwenye pembe za kila njia. Basi akamshika, akambusu, Akamwambia kwa uso usio na haya. Kwa maneno yake mengi na ulaini akamshawishi, Kwa ubembelezi wa midomo yake akamshinda. Huyo akafuatana naye mara hiyo, Kama vile ng'ombe aendavyo machinjoni; Au mpumbavu kuadhibiwa katika pingu.”
Usiwe na mwenendo unaotiliwa mashaka
Usiwe na mazoea ya karibu sana na watu wa jinsia nyingine yanayotiliwa shaka na watu. Waalimu wa kway ana viongozi wa idara za Watoto na vijana wawe na tahadhari katika mahusiano yao na wale wanaowaongoza. Wamama na wababa wa kanisa wanaoombwa misaada na vijana na Watoto wametuhumiwa pia kuwa na tabia ya kuwarubuni Watoto na vijana katika maeneo mengine. Kanisa husika lichukue hatua za kutatua hali hiyo ili kuwanusuru watoto wetu na kuinusuru kazi ya Mungu. (2 Wakorintho 6:3) “Tusiwe kwazo la namna yo yote katika jambo lo lote, ili utumishi wetu usilaumiwe.”
Jiwekee ratiba ya matukio
Kijana asisubiri muda umuamulie cha kufanya. Anayo nafasi ya kupanga nini kitokee lini ili kujijengea nidhamu katika utekelezaji wa mipango yake na kujiwekea vipaumbele katika kila hatua anayopitia. Atapanga lini atamaliza masomo, lini ataanza kazi, na lini ataoa au kuolewa na lini ataanza kuzaa watoto. Kwa kuiweka mipango hii mikononi mwa Mungu kuna uwezekano wa mambo kutokea kama yalivyopangwa. (Mithali 16:3) “Mkabidhi Bwana kazi zako, Na mawazo yako yatathibitika.” (Mithali 3:5) “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe.”