KWA NINI NENO ALIFANYIKA MWILI
Kulikuwapo na nafsi iliyoitwa Neno iliyokuwapo tangu mwanzo kabla kitu chochote hakijaumbwa. Nafsi hiyo ilikuwa na sifa zote za Mungu na ilihusika kwa kiwango kikubwa katika uumbaji. Biblia inasema, “vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika” (Yohana 1:3). Hata hivyo hiyo haimaanishi kuwa nafsi hiyo ilifanya uumbaji huo bila kushirikisha nafsi zingine. Nafsi ya Baba ilihusika (Waebrania 1:1-2). Na nafsi ya Roho Mtakatifu pia ilihusika (Mwanzo 1:1).
Nafsi ya Neno ikishirikiana na nafsi ya Baba na Roho Mtakatifu iliazimia kuumba mwanadamu kwa namna ambayo itakidhi lengo fulani lililokusudiwa kwa huyo mwanadamu. Nafsi hizo tatu katika mipango iliyowekwa kabla ya ulimwengu kuumbwa zilikusudia kumfanya mwanadamu mtawala wa dunia kwa majaribio ili akishinda awe mtawala mwenza Pamoja na Mungu katika ulimwengu usio na dhambi.
Huyo Neno ambaye amekuwepo tangu zamani Pamoja na Baba na Roho Mtakatifu wakamuumba mwanadamu yaani mwanaume na mwanamke kwa sura yao na kuwavika uwezo wa kutawala na kujitawala (Mwanzo 1:26-27;). Wanadamu hawa walitakiwa kuchagua kuchukia yale Mungu asiyoyapenda na kuyapenda yale Mungu ayapendayo kwa hiyari bila kushurutishwa. Kwa bahati mbaya walishindwa kufanya hivyo baada ya kushawishiwa vibaya na Shetani. Wakamwasi Mungu na kuanguka dhambini.
Palihitajika namna ya kumrejesha mwanadamu katika kusudi la awali la kuumbwa kwake. Palihitajika ukombozi utakaomrejesha mwanadamu katika hali aliyokuwa nayo kabla ya dhambi ili lile kusudi la kumfanya mtawala likamilike. Ilikuwa lazima urejeshwaji huo uwe kwa hiyari na katika namna ambayo mwanadamu atatambua kwa kina zaidi kuhusu upendo wa Mungu ulivyo kwa wanadamu (Waefeso 3:18).
Hatua ya kwanza ya kumkomboa mwanadamu iliyohitajika sana ni kumpata atakayechukua nafasi ya Adamu ambaye aliitelekeza jamii ya wanadamu na urithi wao kwa Shetani na badala ya kuwa wana wa Mungu wakawa wana wa majoka (Mathayo 23:33; Mathayo 12:34). Adamu mwenyewe asingeweza kurejesha himaya aliyoipoteza bila msaada wa Mungu kwa kuwa alikuwa amepoteza uwezo wa kujipigania. Mungu akitambua ukweli huo aliahidi kuingilia kati tatizo hilo kwa kumtuma mkombozi atakayezaliwa katika jamii ya wanadamu mwenye uwezo wa kumshinda Shetani (Mwanzo 3:15).
Mzao aliyeahidiwa alikuwa awe na asili ya mwanadamu na asili ya Uungu. Ilikuwa muhimu awe na asili ya mwanadamu ili ajaribiwe katika mambo yote Adamu aliyojaribiwa bila kutenda dhambi (Waebrania 4:15). Kwa kuwa dhambi iliingia kwa njia ya mmoja asiye mtii na hivyo ikasambaa kwa wanadamu wote, mmoja mwingine aliye mtii alikuwa na uwezo wa kuiondosha na kuwafanya wanadamu wote wahesabiwe kuwa wenye haki (Warumi 5:17-19).
Mzao aliyeahidiwa alitakiwa pia kuwa na asili ya Uungu kwa kuwa alitakiwa kuwakilisha tabia ya Mungu ya upendo ambayo Shetani alikuwa ameitia doa kwa kumwakilisha kama Mungu aliye mkatili na asiye na huruma. Hivyo palihitajika mmoja kati ya nafsi tatu za Uungu ashuke aje auwakilishe Uungu katika jamii ya wanadamu. Palihitajika nafsi moja ya Uungu ifanyike mwanadamu. Mwanadamu wa aina yake ambaye ndani yake kuna Uungu ulioshikamanishwa na ubinadamu.
Chaguo likamwangukia Neno. Neno akakubali kwa hiyari kujitoa nafsi yake iwe fidia ya wanadamu (Mathayo 20:28). Akakubali kufanyika mwili (Yohana 1:14). Kwa kukubali kufanyika mwili akawa amekubali kupoteza kwa muda utukufu aliokuwa nao tangu mwanzo wa kuumbwa kwa misingi ya dunia (Yohana 17:5). Akakubali kushuka duniani kama mwanadamu. Akawa mtii hadi mauti ya msalaba. Alikuja kutufundisha kunyenyekea (Wafilipi 2:5-8). Moja ya sifa kuu ya Uungu ni kujishusha.
Kuanzia wakati aliofanyika mwili, Neno akatambuliwa kama Mwana wa Mungu. Kwa sababu hiyo wengine huona ugumu katika kumtambua yule anayeitwa Mwana kama Mungu halisi. Wanahoji Mungu anawezaje kuwa mwanadamu wa kawaida anayeishi na kuchangamana na wenye dhambi? Wengine wakaenda mbali sana na kumwita rafiki wa wenye dhambi (Luka 7:34). Yeye alikuja kutimiza ahadi ya mkombozi aliyeahidiwa kwa Adamu na Hawa siku waliyoasi bustani ya Edeni.
Ujio wa Mwana wa Mungu au Mwana wa Adamu duniani ulichukua miaka 4,000 tangu wakati alipoahidiwa. Kila mzazi akajenga matarajio ya kuzaa mtoto huyo asiye wa kawaida. Isaka akabeba sifa za mzao aliyeahidiwa lakini hakuwa Yeye. Hata nabii aliposema fimbo ya ufalme haitaondoka katika Yuda ikadhaniwa Daudi angekuwa mzao aliyeahidiwa lakini haikuwa hivyo. Baadaye kabisa Yesu akaja kuzaliwa katika kabila la Yuda na ndiyo sababu wakati mwingine hutambuliwa kama Mwana wa Daudi. Yesu alipozaliwa.
Kuzaliwa kwake Yesu kunasimuliwa kwa kuonyeshwa kwanza uhalali wake wa kuwa Mwana wa Adamu, Mwana wa Ibrahimu, na Mwana wa Daudi ili kuthibitisha kuwa ndiye mzao aliyeahidiwa (Mathayo 1:1-16; Wagalatia 3:16). Isaka, Yakobo, na Daudi ingawa walikuwa wazao wa ibrahimu hawakutosha kukidhi sifa za mzao aliyeahidiwa. Nafsi ya Neno ambayo baadaye ilitambulishwa kama Mwana wa Mungu, Mwana wa Adamu, Mwana wa Ibrahimu, na Mwana wa Daudi akaja akaitwa Yesu wakati alipozaliwa (Mathayo 1:21).
Huyu ndiye Neno ambaye kuwepo kwake ni tangu milele (Mika 5:2; Yohana 1:1-3). Huyo amekuwepo tangu mwanzo lakini amefunuliwa mwisho wa zamani zetu kwa ajili ya ukombozi wetu (1 Petro 1:20). Kama Mwana wa Mungu au Mwana wa Adamu au Mwana wa Daudi umri wake unaanzia alipozaliwa lakini alianza kukaimu nafasi hiyo tangu mpango wa wokovu ulipowekwa mbinguni (Ufunuo 13:8). Jina la Mwana wa Mungu halikusudii kumpunguzia hadhi ya Uungu aliyokuwa nayo zamani. Jina hili na Jina la Yesu limebeba majukumu ya kimkakati anayolenga kuyafanya akiwa duniani kwa niaba yetu na kwa ajili yetu.
Zipo kauli ambazo Yesu amezitoa akiwawakilisha wanadamu ambazo katika nafsi ya Uungu asingezitoa (Mathayo 24:36). Na zipo kauli ambazo Yesu amezitoa akiwakilisha nafsi ya Uungu ambazo katika hali yake kama Mwana wa Mungu au Mwana wa Adamu asingezitoa (Mathayo 9:2). Wakati Yesu anaposema nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani hiyo anaisema kama Mwana wa Adamu akiwakilisha jamii ya wanadamu (Mathayo 28:18). Yesu kama nafsi ya Uungu alikuwa na mamlaka isiyotoka kwa Baba mamlaka ambayo haikuondolewa alipofanyika mwanadamu (Tito 2:13).