Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

FARIDA MUSSA MIKA

FARIDA MUSSA MIKA (FARIDA SALEHE MASHAMBO) 1972 - 2021

Wasifu wa Farida Mussa Mika:


Farida Salehe Mashambo ambaye baadaye alijulikana kama Farida Mussa Mika aliyezaliwa Lushoto Mkoani Tanga, Februari 22, 1972, ni mtoto wa kwanza wa familia ya kiislamu ya Salehe Mashambo na Mwanaisha Omari. Farida alihitimu elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Kitopeni mwaka 1990 ambapo alifaulu na kusoma elimu ya sekondari shule ya Shambalai zote mbili zikiwa Lushoto Mjini. Farida alifaulu kusoma kidato cha tano na sita Shule ya Sekondari Loleza mkoani Mbeya mchepuo wa sayansi (PCB) akikusudia kuwa daktari. Hata  hivyo  mwaka  1996 alihitimu stashahada ya Usimamizi wa Biashara - Uhasibu chuoni Tanzania Adventist College. Baadaye mwaka 2012 Farida alihitimu shahada ya kwanza ya Usimamizi wa Biashara toka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Mnamo mwaka 2020 Farida alianza masomo ya Shahada ya Uzamili ya Usimamizi wa Biashara katika Masoko na Ujasiriamali ambapo mauti ilimkuta akiwa muhula wa tatu akitaraji kuhitimu mwaka huu, 2021.

Maisha Yake Kiimani:

Farida alizaliwa na kulelewa katika familia ya kiislamu akiwa mahiri katika elimu ya Madrasa. Baada ya kumaliza kidato cha sita, kupitia huduma ya uinjilisti wa vitabu, Farida alikuwa wa kwanza katika familia yake kupokea imani ya Kiadventista na kubatizwa katika mahubiri ya hadhara yaliyoendeshwa na marehemu Mchungaji Joseph Onyango, Lushoto mjini, mwaka 1994, imani aliyodumu nayo kwa uaminifu hadi kifo chake.

Familia:

Farida Mashambo alifunga ndoa na Mchungaji Mussa Daniel Mika tarehe 22 Juni, 1997 kwenye kanisa la Waadventista wa Sabato Ukonga huduma iliyoendeshwa na marehemu Dr. John Azza Kisaka akisaidiana na Mchungaji Benard Mambwe. Katika ndoa yao walifanikiwa kupata watoto wawili wa kiume Daniel na Mika, na binti mmoja aitwaye Maryclaudia. Mume wake anamwelezea Farida kuwa alikuwa mama mcha Mungu, mcheshi, mkarimu na kipenzi cha mume na watoto wake katika miaka yote karibia 24 ya ndoa yake.

Maisha ya Utumishi:

Farida Mussa Mika aliajiriwa na Konferensi ya Mara mwaka 1996 kama mhasibu. Mwaka 1997 baada ya kufunga ndoa alihamia shule ya Sekondari ya Ndembela kama mhasibu. Hata hivyo mwaka 1998 familia yake ilipohamia Iringa, alifanya kazi katika kampuni binafsi ya Pilos Accountants and Auditor. Mwaka 1999 -2003 alirudi tena Mbeya akiajiriwa na South West Tanzania Field kama mhasibu. Mwaka 2003 alihamia Shule ya Msingi ya Kiadventista ya Kongowe hadi 2004 alipochaguliwa kuwa Kaimu Mhazini wa Taasisi ya Vyombo vya Habari vya Kanisa la Waadventista Tanzania (VOP/TAMC) na baadaye kuwa Mhazini wa VOP/TAMC mwaka 2005-2010.

Mwaka 2010 -2013 alikuwa Mhazini Mwenza wa Tanzania Union Mission. Kwa miezi sita mwaka 2013 alikuwa mhasibu Southern Tanzania Union Mission jijini Dar es salaam. Hata hivyo mwaka 2014 hadi 2018 Farida alikuwa Mhazini wa Nyumba ya Uchapishaji ya Ufunuo. Mwaka 2018 mwishoni alichaguliwa kuwa Meneja wa HHES ya Unioni ya Kusini mwa Tanzania, Mkurugenzi wa Seminari ya Wainjilisti wa Vitabu Unioni ya Kusini mwa Tanzania, na amekuwa pia Mwenyekiti wa Chama cha Wake wa Wachungaji Unioni ya kusini mwa Tanzania kazi ambazo amekuwa akizifanya hadi mauti ilipomkuta. Tarehe 14 Januari yapata saa nne usiku alimwaga mume wake kwa simu kisha akaomba na kulala akitaraji kuamka asubuhi yake. Lakini usiku ule alipata hali ya kushindwa kupumua na kulala usingizi wa mauti.

Marehemu ameacha Mume, Watoto wawili wa kiume, Daniel na Mika, na binti mmoja Maryclaudia.