UCHAMBUZI WA KITABU CHA WARUMI:
SURA YA TANO
Sura ya tano ya kitabu cha Warumi inaelezea matokeo ya kuhesabiwa haki kwa imani. Moja ya changamoto kubwa inayoletwa na utaratibu wa kujihesabia haki kwa matendo ni kukosekana kwa utulivu na amani moyoni kunakosababishwa na kukosekana kwa uhakika wa kuokolewa kwenyewe. (Waebrania 4:1-3) “Basi, ikiwa ikaliko ahadi ya kuingia katika raha yake, na tuogope, mmoja wenu asije akaonekana ameikosa. Maana ni kweli, sisi nasi tumehubiriwa habari njema vile vile kama hao. Lakini neno lile lililosikiwa halikuwafaa hao, kwa sababu halikuchanganyika na imani ndani yao waliosikia. Maana sisi tulioamini tunaingia katika raha ile; kama vile alivyosema, Kama nilivyoapa kwa hasira yangu, Hawataingia rahani mwangu.”
Wanaohesabiwa haki kwa imani wanaingia rahani kwa sababu wameacha kuzitegemea kazi zao wenyewe. (Mathayo 11:28-30) “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.” Wanajua kuwa wokovu wao hautegemei juhudi zao binafsi bali uwezo wa Mungu aliyeapa kuwasaidia katika hatua zote. (Yohana 10:29) “Baba yangu aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote; wala hakuna mtu awezaye kuwapokonya katika mkono wa Baba yangu.”
Waliohesabiwa haki kwa imani hawahofii hukumu ya Mungu kama wale wanaohesabiwa haki kwa matendo yao. Hii ni kutokana na kuwa Kristo alishapokea hukumu hiyo kwa niaba yao. (Isaya 53:4-5) “Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.” Yeye ndiyo amani yetu.
Yesu anakuwa amani yetu sote bila kujali kama tuna upendeleo maalumu kwa Mungu au la. Kama tu Waisraeli au watu wa Mataifa au wapagani. (Waefeso 2:12-15) “Kwamba zamani zile mlikuwa hamna Kristo, mmefarakana na jamii ya Israeli, wageni wasio wa maagano ya ahadi ile. Mlikuwa hamna tumaini, hamna Mungu duniani. Lakini sasa, katika Kristo Yesu, ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu kwa damu yake Kristo. Kwa maana yeye ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja; akakibomoa kiambaza cha kati kilichotutenga. Naye akiisha kuuondoa ule uadui kwa mwili wake; ndiyo sheria ya amri zilizo katika maagizo; ili afanye hao wawili kuwa mtu mpya mmoja ndani ya nafsi yake; akafanya amani.”
Waliohesabiwa haki kwa imani katika Kristo Yesu mambo ya hukumu ya siku ya mwisho siyo shida zao. (Warumi 8:1) “Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu.” Kristo ametutoa kwenye hofu ya mauti iliyokuwa sehemu ya maisha yetu kabla hatujahesabiwa haki kwa imani. (Waebrania 2:14-15) “Basi, kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo, ili kwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani, Ibilisi, awaache huru wale ambao kwamba maisha yao yote kwa hofu ya mauti walikuwa katika hali ya utumwa.”
Huwezi kuwa na hofu na hukumu ijayo ikiwa unafahamu fika upendo na gharama aliyoingia kwa ajili yako yule hakimu aliyepangiwa kuisikiliza na kuitolea maamuzi hukumu yako. (Warumi 8:33-34) “Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea.”
Amani siyo matokeo pekee ya wale waliohesabiwa haki kwa imani. Waliohesabiwa haki kwa imani huishi kwa matumaini huku wakifurahia maisha licha ya kuwa wanapitia dhiki na machungu huku wakijazwa na upendo na Roho Mtakatifu. (Warumi 5:1-5) “Ambaye kwa yeye tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo mnasimama ndani yake; na kufurahi katika tumaini la utukufu wa Mungu. Wala si hivyo tu, ila na mfurahi katika dhiki pia; mkijua ya kuwa dhiki, kazi yake ni kuleta saburi; na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo; na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini; na tumaini halitahayarishi; kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi.”
Tumaini la utukufu linalotajwa hapa na Paulo limetajwa mahali pengine kama siri. (Waefeso 3:8-11) “Mimi, niliye mdogo kuliko yeye aliye mdogo wa watakatifu wote, nalipewa neema hii ya kuwahubiri Mataifa utajiri wake Kristo usiopimika; na kuwaangaza watu wote wajue habari za madaraka ya siri hiyo, ambayo tangu zamani zote ilisitirika katika Mungu aliyeviumba vitu vyote; ili sasa, kwa njia ya kanisa, hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi ijulikane na falme na mamlaka katika ulimwengu wa roho; kwa kadiri ya kusudi la milele alilolikusudia katika Kristo Yesu Bwana wetu.”
Waliohesabiwa haki kwa imani wamefunuliwa siri hii kubwa kwamba hali yao ya baada ya dhambi kukoma itakuwa bora mara nyingi zaidi kuliko hali waliyonayo sasa na bora zaidi hata ya ile hali waliyokuwa nayo Adamu na Eva kabla hawajaanguka dhambini. (Warumi 8:16-18) “Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu; na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye. Kwa maana nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu.”
Wokovu una hatua tatu muhimu. Hatua ya kwanza inatambulika kama kuhesabiwa haki yaani kutangazwa kuwa huna hatia na huna hukumu kutokana na kile Yesu alichofanya kwa niaba yako kwa kufa pale msalabani. Hatua hii inafanyika mara moja na kukamilika. Hatua ya pili inatambulika kama utakaso. Hii ni hatua ambayo aliyehesabiwa haki hupitia mchakato wa mabadiliko ya tabia yanayoletwa na Roho Mtakatifu. Hatua hii ni endelevu hadi Yesu atakapoonekana mawinguni au mtu atakapokoma kuishi. Hatua ya tatu inatambulika kama kutukuzwa au utukufu. Hii ni hatua inayoanza mara mtu anapohesabiwa haki na kuendelea kukua hadi kufikia hitimisho Yesu anaporudi tena.
Hatua hizi tatu za wokovu zimefafanuliwa na fungu lifuatalo. (2 Wakorintho 1:9-10) “Naam, sisi wenyewe tulikuwa na hukumu ya mauti katika nafsi zetu ili tusijitumainie nafsi zetu, bali tumtumaini Mungu, awafufuaye wafu, aliyetuokoa sisi katika mauti kuu namna ile; tena atatuokoa; ambaye tumemtumaini kwamba atazidi kutuokoa.” Maandiko yanamfunua Mungu aliyetuokoa (wakati uliopita mtimilifu), Mungu atakayetuokoa (wakati ujao), na Mungu anayezidi kutuokoa (wakati wa sasa na endelevu).
Kazi ya kutubadilisha tabia itakapokamilishwa tutakuwa tumekidhi vigezo vyote vya kuingia katika utukufu aliotuandalia tangu kuwekwa kwa misingi ya dunia. (1 Petro 5:10) “Na Mungu wa neema yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele katika Kristo, mkiisha kuteswa kwa muda kidogo, yeye mwenyewe atawatengeneza, na kuwathibitisha, na kuwatia nguvu.”
Ingawa wale waliohesabiwa haki hawaonekani katika hali ile watakayokuwa nayo watakapotukuzwa bado maisha yao yanatangaza utofauti wao na wengine kwamtindo wao wa maisha na mwonekano. (Waebrania 2:6-8) “Mwanadamu ni nini hata umkumbuke, Ama mwana wa binadamu, hata umwangalie? Umemfanya mdogo punde kuliko malaika, Umemvika taji ya utukufu na heshima, Umemtawaza juu ya kazi za mikono yako; Umeweka vitu vyote chini ya nyayo zake. Kwa maana katika kuweka vitu vyote chini yake hakusaza kitu kisichowekwa chini yake. Lakini sasa bado hatujaona vitu vyote kutiwa chini yake.”
Waliohesabiwa haki kwa imani wameyashinda manung’uniko kwa kuwa wanaamini kila kinachotokea kimekusudia jambo jema kwao. (Warumi 8:28) “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.” Wanaamini kuwa kukamilika kwa mchakato utakaohitishwa katika kuwatukuza ni jambo la hakika lisilo na shaka yoyote nak ama kuna kucheleweshwa kokote ni kwa nia njema inayothibitiwa na Mungu mwenyewe.
Mungu anachukulia hatua ya tatu ya wokovu ya kutukuzwa kama iliyokwisha kamilika kwa kuwa uwezo wa kuwakamilisha upo kwake na hakuna anayeweza kulizuia jambo hilo lisikamilike. (Warumi 8:30) “Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza.”
Kuhesabiwa haki na kutakaswa mara nyingi kunachukuliwa kama kitu kimoja. Hakuna uwezekano wa mchakato mmoja kuanza bila kukamilisha ule wa pili. (Waefeso 2:4-6) “Lakini Mungu, kwa kuwa ni mwingi wa rehema, kwa mapenzi yake makuu aliyotupenda; hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu; alituhuisha pamoja na Kristo; yaani, tumeokolewa kwa neema. Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu.” Waliohesabiwa haki kwa imani Mungu anawatambua kama wameshatukuzwa tayari kwa sababu mojawapo ya manufaa ya kufikia hatua ya kutukuzwa ni kuketi kwenye kiti cha enzi. (Ufunuo 3:21) “Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi.”
Wanaohesabiwa haki kwa imani wamekamilishwa na upendo wa Mungu. Upendo wa Mungu ukiwepo hufukuza hofu. (1 Yohana 4:18) “Katika pendo hamna hofu; lakini pendo lililo kamili huitupa nje hofu, kwa maana hofu ina adhabu; na mwenye hofu hakukamilishwa katika pendo.” Kuwapenda wengine na kumpenda Mungu ni kanuni ya aliyefikiwa na kujazwa na upendo wa Mungu. Upendo ule uliomsukuma Yesu kujitoa kwa ajili ya wengine ndiyo ambao Roho ameumimina kwenye mioyo ya watu wake. Upendo ule waKristo unawabidisha kufanya yote wanayoagizwa kufanya. (2 Wakorintho 5:14) “Maana, upendo wa Kristo watubidisha; maana tumehukumu hivi, ya kwamba mmoja alikufa kwa ajili ya wote, basi walikufa wote.”
Mungu wa Biblia ndiye Mungu pekee anayewatafuta waliopotea. Miungu ya kipagani haiwezi kutafuta wale wanaoitumainia ila wale wanaoitumainia ndiyo wenye jukumu la kuitafuta hiyo miungu. (Warumi 5:7-8) “Kwa kuwa ni shida mtu kufa kwa ajili ya mtu mwenye haki; lakini yawezekana mtu kuthubutu kufa kwa ajili ya mtu aliye mwema. Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi.”
Dhambi inatawala katika mauti. (1 Wakorintho 15:56-57) “Uchungu wa mauti ni dhambi, na nguvu za dhambi ni torati. Lakini Mungu na ashukuriwe atupaye kushinda kwa Bwana wetu Yesu Kristo.” Ushindi wetu hauji kwa kutumia nguvu zetu kama Waisraeli. Warumi 10:1-3) “Ndugu zangu, nitakayo sana moyoni mwangu, na dua yangu nimwombayo Mungu, ni kwa ajili yao, ili waokolewe. Kwa maana nawashuhudia kwamba wana juhudi kwa ajili ya Mungu, lakini si katika maarifa. Kwa maana, wakiwa hawaijui haki ya Mungu, na wakitaka kuithibitisha haki yao wenyewe, hawakujitia chini ya haki ya Mungu.”
Kupitia haki ipatikanayo na imani sasa tuneema inatawala hadi uzima wa milele. Ukiwa chini ya neema una uhakika wa uzima wa milele na hivyo unakuwa na amani daima. Mungu akusaidie kukua katika neema.