Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

WARUMI 3

UCHAMBUZI WA KITABU CHA WARUMI:

SURA YA TATU:

Sura ya tatu ya kitabu cha Warumi inazungumzia namna mwanadamu anavyohesabiwa haki. Paulo anaendeleza madai yake kuwa wanadamu wote baada ya anguko la dhambi walipoteza uwezo wa kuwa wenye haki mbele ya Mungu na kwamba hali hiyo inawahusu Wayahudi na jamii ya watu wasio Wayahudi ambayo hapa inawakilishwa na Wayunani. (Warumi 3:9-10) “Ni nini basi? Tu bora kuliko wengine? La! Hata kidogo. Kwa maana tumekwisha kuwashitaki Wayahudi na Wayunani ya kwamba pia wamekuwa chini ya dhambi; kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Hakuna mwenye haki hata mmoja.”

Katika nyakati hizo Wayahudi walitambulika kama watu wenye upendeleo maalum kwa kuwa walikuwa wamepewa mausia ya Mungu tofauti na watu wa mataifa mengine. Paulo anakiri hilo kwa sehemu lakini bado anadai upendeleo huo hauwapi Wayahudi ya kuwa wenye haki mbele za Mungu kuliko watu wa jamii nyingine. (Warumi 3:1-2) “Basi Myahudi ana ziada gani? Na kutahiriwa kwafaa nini? Kwafaa sana kwa kila njia. Kwanza kwa kuwa wamekabidhiwa mausia ya Mungu.”

Kwa upande mwingine Wayunani walitambulika kama jamii ya watu iliyoendelea duniani iliyokuwa inaongoza kwa uwezo wa tafakuri na hekima na ambao waliyachukulia masuala ya wokovu kwa uzito mwepesi. (1 Wakorintho 1:22-23) “Kwa sababu Wayahudi wanataka ishara, na Wayunani wanatafuta hekima. bali sisi tunamhubiri Kristo, aliyesulibiwa; kwa Wayahudi ni kikwazo, na kwa Wayunani ni upuzi.”

Halikuwa wazo rahisi kulikubali kwamba Wayahudi hawana la kuwazidi wasio Wayahudi kama ambavyo si rahisi kushawishi watu leo kuwa Wakristo hawana la kuwazidi watu wa dini zingine linapokuja swala la kuwa mwenye haki mbele za Mungu kwa sababu katika kila jamii wapo wale wanaoonekana kuwa mbele kuliko wengine. Lakini kauli kuwa wanadamu wote huhesabiwa kutokuwa wenye haki mbele za Mungu inatokana na ukweli kuwa wote wamekuwa chini ya dhambi.

Kuwa chini ya dhambi maana ya kujua kutenda mema na bado usiweze kutenda mema. (Yakobo 4:17) “Basi yeye ajuaye kutenda mema, wala hayatendi, kwake huyo ni dhambi.” Hali ya mwanadamu aliyeanguka dhambini ni ya namna hiyo. (Warumi 7:19) “Kwa maana lile jema nilipendalo, silitendi; bali lile baya nisilolipenda ndilo nilitendalo.” Mtu wa aina hii yupo chini ya dhambi kwa kuwa anatawaliwa na dhambi au sheria ya dhambi inayotawala ndani yake. (Warumi 7:20) “Basi kama lile nisilolipenda ndilo nilitendalo, si mimi nafsi yangu nilitendaye, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu.”

Mtu wa aina hii nia yake imeharibika katika kiwango kisichorekebika. (Yeremia 13:23) “Je! Mkushi aweza kuibadili ngozi yake, au chui madoa-doa yake? Kama aweza, ndipo na ninyi mwaweza kutenda mema, ninyi mliozoea kutenda mabaya.” Kila tendo na neno huchipuka kutoka kwenye wazo au nia ya mtu. (Yakobo 1:14-15) “Lakini kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa. Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti.” Kwa bahati mbaya nia ya mwanadamu tangu anguko la dhambi imetengeneza uadui na kanuni zinazoweza kumfanya mwanadamu kuwa mwenye haki. Kanuni zinazoweza kumfanya mwanadamu kuwa mwenye haki ni sheria au Amri za Mungu. Mtu aishiye kulingana na sheria za Mungu huwa mwenye haki na mkamilifu kama Mungu alivyo. (Warumi 2:13) “Kwa sababu sio wale waisikiao sheria walio wenye haki mbele za Mungu, bali ni wale waitendao sheria watakaohesabiwa haki.”

Wayahudi licha ya kujinadi kuwa wamekuwa washikaji wa sheria lakini kimsingi walikuwa ni wasikiaji wa sheria na kamwe hawakuwa watendaji wa sheria. Paulo anatoa sababu kwa nini walishindwa kukidhi matakwa ya sheria. (Warumi 8:6-7) “Kwa kuwa nia ya mwili ni mauti; bali nia ya roho ni uzima na amani. Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii.”

Ilikuwa ni muhimu mwanadamu awe mwenye haki ili kumwepusha na utumwa wa dhambi na adhabu ya kifo. Njia ya kumfanya mwanadamu mdhambi kuwa mwenye haki ilitakiwa isitokane na matendo yake bali itokane na Imani yake kwa yule mwenye haki mmoja aliyekidhi vigezo. Kwa sababu ya kutanguliza dharau na kujiinua Wayahudi walishindwa kumtambua na kumwamini Yesu aliyetumwa na Mungu wakishikilia kuwa matendo yao yangetosha kuwaokoa. (Matendo 3:14-15) “Bali ninyi mlimkana yule Mtakatifu, yule Mwenye haki, mkataka mpewe mwuaji; mkamwua yule Mkuu wa uzima, ambaye Mungu amemfufua katika wafu; na sisi tu mashahidi wake.”

Paulo anasema njia ya kuthibitisha kama mwanadamu ana haki mbele ya Mungu ni pale atakapoibuka mshindi kwenye hukumu ya Mungu. (Warumi 3:4) “Hasha! Mungu aonekane kuwa amini na kila mtu mwongo; kama ilivyoandikwa, Ili ujulike kuwa una haki katika maneno yako, Ukashinde uingiapo katika hukumu.” Sheria hazipo ili kumwezesha mwanadamu kuhesabiwa haki. Sheria zipo kwa ajili ya kupima uadilifu wa mtu. (Mhubiri 12:13) “Hii ndiyo jumla ya maneno; yote yamekwisha sikiwa; Mche Mungu, nawe uzishike amri zake, Maana kwa jumla ndiyo impasayo mtu. Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au likiwa baya.”

Mwanadamu mwenye mwili wa dhambi ambaye nia yake ni kinyume cha sheria asimamapo mbele ya sheria hujiona alivyopungua. Na hili ndilo lilikuwa kusudi kuu la Mungu kuileta sheria kwa mwanadamu mwenye asili ya dhambi. Lengo lilikuwa kumfanya mwanadamu afumbwe mdomo katika jitihada zake za kutafuta haki kupitia matendo ya sheria. (Warumi 3:19) “Basi twajua ya kuwa mambo yote inenayo torati huyanena kwa hao walio chini ya torati, ili kila kinywa kifumbwe, na ulimwengu wote uwe chini ya hukumu ya Mungu.” Sheria ilitolewa ili kumsaidia mwanadamu aone jinsi jambo hilo la kujitafutia haki kupitia matendo ya sheria lilivyo gumu na lisivyowezekana.

Janga la dhambi lilionekana kumletea mwanadamu upungufu wa nguvu za kiroho mara tu lilipoingia katika jamii ya wanadamu. Lilileta upofu wa kiroho uliomfanya mdhambi apate wakati mgumu katika kutambua na kukubali makosa yake. (Mwanzo 3:9-12) “Bwana Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi? Akasema, Nalisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha. Akasema, Ni nani aliyekuambia ya kuwa u uchi? Je! Umekula wewe matunda ya mti niliyokuagiza usiyale? Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala.”

Adamu aliweza kutambua na kukubali kuwa yupo uchi jambo ambalo nalo liliwezekana kwa neema ya Mungu kwa sababu mwanadamu mwenye asili ya dhambi hata anapokuwa uchi hupata wakati mgumu kulitambua na kulikubali jambo hilo. (Ufunuo 3:17) “Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.”

Lakini kuonyesha kuwa dhambi huleta upungufu wa nguvu za kiroho Adamu alishindwa kulitambua na kulikubali kosa lake na alishindwa pia hata kuomba msamaha. Adamu alidai kosa lake lilisababishwa na mkewe na kama Mungu asingemletea mke huyo asingefanya kosa hilo. Hizi hazikuwa sababu za kweli zilizomsukuma Adamu kutenda kosa alilotenda. Adamu alisukumwa na tamaa huku akitilia shaka Neno la Mungu na upendo wake.

Mungu alituma sheria ili uwe uthibitisho wa makosa. Kuthibitisha kosa kulikuwa kwa muhimu ili kuruhusu kuwepo kwa adhabu ya haki au kuwepo kwa ungamo na toba kama sehemu ya matayarisho ya mtu kusamehewa. Kwa vipimo vya sheria ya Mungu hakuna mwanadamu aliye mwema au mwadilifu. Uadilifu na wema hupimwa na sheria. (Warumi 3:11-12) “Hakuna afahamuye; Hakuna amtafutaye Mungu. Wote wamepotoka, wameoza wote pia; Hakuna mtenda mema, la! Hata mmoja.”

Biblia inaposema hakuna mtenda mema inamaanisha hakuna asiye na dhambi. (Mhubiri 7:20) “Bila shaka hakuna mwanadamu mwenye haki hapa duniani, ambaye afanya mema, asifanye dhambi.” Mwanadamu aliyewahi kuishi hapa duniani aliyesifiwa kuwa ni mtenda mema ni mmoja tu yaani Yesu Kristo. (Marko 10:17-18) “Hata alipokuwa akitoka kwenda njiani, mtu mmoja akaja mbio, akampigia magoti, akamwuliza, Mwalimu mwema, nifanye nini nipate kuurithi uzima wa milele? Yesu akamwambia, Kwa nini kuniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu.”

Mungu pia ni mwema kwa sababu hatendi dhambi. (Zaburi 34:8) “Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema; Heri mtu yule anayemtumaini.” Lakini Yesu naye ingawa hakutaka kukiri kuwa ni mwema kiuhalisia alikuwa mwema maana hakuwa amefanya dhambi. (1 Petro 2:22) “Yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana kinywani mwake.” Yesu hakukubali kuitwa mwema si kwa sababu hastahili sifa hiyo bali ni kwa sababu wema hawana tabia ya kujisifu. Aliye mwema ana kawaida ya kujilinganisha na Mungu na kamwe hajilinganishi na wanadamu wenzake. (Luka 18:11) “Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang'anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru.”

Mtu anayejitambua kuwa ni mwenye dhambi ni yule amtafutaye Mungu. Hutamani kujua Mungu alivyo ili ikiwezekana afanikiwe kuwa kama alivyo. Kwa kadri mtu anavyomsogelea Mungu na kwa kadri anavyozidi kumfahamu husikia badiliko la amani moyoni mwake. Hutambua jitahada za kutaka kufanana na Mungu zinawezekana kwa njia ya Kristo peke yake. (Warumi 3:21-24) “Lakini sasa, haki ya Mungu imedhihirika pasipo sheria; inashuhudiwa na torati na manabii; ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Yesu Kristo kwa wote waaminio. Maana hakuna tofauti; kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu. wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu.”

Haki ya Mungu inapatikanaje bila sheria? Haki ya Mungu inapatikana kwa njia ya imani. Hapakuhitajika wanadamu wote watende dhambi ili dhambi iwafikie wanadamu wote. Palihitajika mtu mmoja atenda dhambi ili dhambi hiyo iwafikie wanadamu wote, na palihitajika mtu mmoja aliye mkamilifu atende tendo moja la haki ili haki hiyo iwafikie wanadamu wote. Mtu huyo mmoja mkamilifu aliyetumwa na Mungu ni Yesu Kristo. Lakini kwa sababu ya kiburi chao Wayahudi hawakumkubali. (Matendo 3:14-15) “Bali ninyi mlimkana yule Mtakatifu, yule Mwenye haki, mkataka mpewe mwuaji; mkamwua yule Mkuu wa uzima, ambaye Mungu amemfufua katika wafu; na sisi tu mashahidi wake.”

Mtu anapomwamini Yesu yale Yesu aliyofanikiwa kuyafanya katika kutii sheria za Mungu huhesabiwa kwake. Husamehewa dhambi, makosa, na maovu yote kwa kuwa damu ya Yesu ina uwezo wa kutakasa dhambi. Machoni pa Mungu mtu huyo husimama akiwa hana hatia na mwenye haki. Tofauti ni kuwa haki anayosimama nayo mbele za Mungu si ile haki ipatikanayo kwa matendo ya sheria bali ni ile haki ipatikanayo kwa njia ya imani. Haki ya Kristo. (Wafilipi 3:9) “Tena nionekane katika yeye, nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani iliyo katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu, kwa imani.”

Katika mazingira haya kujisifu kunakuwa kumefungiwa nje. (Warumi 3:27) “Ku wapi, basi, kujisifu? Kumefungiwa nje. Kwa sheria ya namna gani? Kwa sheria ya matendo? La! Bali kwa sheria ya imani.” Wale wanaotafuta kuhesabiwa haki kwa matendo wanasukumwa kufanya hivyo ili kujipatia sifa. (Wagalatia 6:12-13) “Wote watakao kuonekana ni wazuri kwa mambo ya mwili, ndio wanaowashurutisha kutahiriwa; makusudi wasiudhiwe kwa ajili ya msalaba wa Kristo, hilo tu. Kwa maana hata wao wenyewe waliotahiriwa hawaishiki sheria; bali wanataka ninyi mtahiriwe, wapate kuona fahari katika miili yenu.”

Kujisifu kwa mtu aliyehesabiwa haki kwa imani ni jambo lisilowezekana kwa sababu anatambua kila jema alilonalo halitokani na yeye. (Waefeso 2:8-9) “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu.” Mtu aliyehesabiwa haki kwa imani anadumu katika kusifu wema wa Mungu uliompa fursa ya kutambuliwa kama mwenye haki. (Yeremia 9:24) “Bali ajisifuye na ajisifu kwa sababu hii, ya kwamba ananifahamu mimi, na kunijua, ya kuwa mimi ni Bwana, nitendaye wema, na hukumu, na haki, katika nchi; maana mimi napendezwa na mambo hayo, asema Bwana.”

Kuhesabiwa haki kwa imani ndiyo njia iletayo amani ya kweli moyoni. Njia ya kuhesabiwa haki kwa matendo inayopendelewa na wengi inakosesha amani kwa kuwa haikupi uhakika wa kukubaliwa kwa yale uyafanyayo kama njia ya kukupatanisha na Mungu. (Warumi 3:16-18) “Uharibifu na mashaka yamo njiani mwao. Wala njia ya amani hawakuijua. Kumcha Mungu hakupo machoni pao.” Wacha Mungu hawategemei utaratibu fulani uliowekwa na watu au jamii ili kumfikia Mungu au kupatanishwa naye. Wacha Mungu wanapata mwongozo wa moja kwa moja kutoka kwa Mungu. 

Dini ni mfumo unaopendekeza mambo ya kufanya ili mwenye dhambi amridhishe Mungu na kuhesabiwa kuwa mwenye haki tena. Injili haipendekezi mambo ya kufanya ili mdhambi apatanishwe na Mungu na kutambulika kama mwenye haki bali inatoa suluhisho ambalo mwenye dhambi anatakiwa kuliamini tu ili ahesabiwe haki. (Warumi 3:24-25) “Wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu; ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake, ili aonyeshe haki yake, kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa MUNGU dhambi zote zilzotangulia kufanywa.”

Wanadamu wenye dhambi hawapatanishwi na Mungu kupitia jitihada za matendo yao. Matendo yao hayawezi kuununua wokovu. Wokovu unanunuliwa kwa niaba yao na Mungu mwenyewe kupitia Yesu Kristo. Ingawa wenye dhambi wanahesabiwa haki bure haki hiyo haipatikani bure. Ni haki iliyonunuliwa kwa gharama kubwa. (Ufunuo 5:9-10) “Nao waimba wimbo mpya wakisema, Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa, ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi.”

Wokovu wa wanadamu haukununuliwa ili kuwafanya waendelee kuishi dhambini. Wokovu ulikuja na suluhisho la tabia sugu ya dhambi waliyoirithi wanadamu. Ulikuja ili kuibadilisha tabia hiyo. (1 Petro 1:18-19) “Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo.” Wokovu unatoa suluhisho la kudumu la kuondokana na mwenendo wetu usiofaa tuliourithi.

Mungu wa Wayahudi ndiye huyo huyo Mungu wa wapagani. Mungu wa Wakristo ndiye huyo huyo Mungu wa Waislamu. Mungu wa Waprotestanti ndiye huyo huyo Mungu wa Wakatoliki. Kinachowaunganisha wote ni hali yao ya dhambi na upatanisho uliofanywa na Mungu kwa jamii yote ya wanadamu. Wote wanatakiwa kuwa na kigezo kimoja cha kuwafanya wenye haki na kigezo hicho ni imani yao kwa Yesu aliyechaguliwa kuwa mpatanishi wa Mungu na wanadamu. (Warumi 3:29-30) “Au je! Mungu ni Mungu wa Wayahudi tu? Siye Mungu wa Mataifa pia? Naam, ni Mungu wa Mataifa pia; kama kwa kweli Mungu ni mmoja, atakayewahesabia haki wale waliotahiriwa katika imani, nao wale wasiotahiriwa atawahesabia haki kwa njia ya imani iyo hiyo.”

Mfumo huu wa kuhesabia haki wanadamu kwa njia ya imani haiondoi umuhimu wa sheria badala yake unaithibitisha sheria kuwa ina umuhimu na uhalali. (Warumi 3:31) “Basi, je! Twaibatilisha sheria kwa imani hiyo? Hasha! Kinyume cha hayo twaithibitisha sheria.” Wokovu unaturejeshea uwezo wa kutii sheria zake tuliokuwa tumeupoteza kupitia anguko la dhambi. (Warumi 8:3-4) “Maana yale yasiyowezekana kwa sheria, kwa vile ilivyokuwa dhaifu kwa sababu ya mwili, Mungu, kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe katika mfano wa mwili ulio wa dhambi, na kwa sababu ya dhambi, aliihukumu dhambi katika mwili; ili maagizo ya torati yatimizwe ndani yetu sisi, tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali mambo ya roho.”

Yesu ambaye wote wanaomwamini wanahesabiwa haki alifikia uhalali huo kwa kuwa yeye mwenyewe alitii kikamilifu matakwa ya sheria. (Yohana 15:10) “Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake.” Yesu hana uadui wowote na sheria au torati. Yeye ndiyo Daraja kati ya torati na neema. (Wagalatia 3:24) “Hivyo torati imekuwa kiongozi kutuleta kwa Kristo, ili tuhesabiwe haki kwa imani.” Waliohesabiwa haki kwa imani baada ya majaribio ya kutafuta kuhesabiwa haki kwa sheria kushindwa watakuwa wamesaidiwa kujua hali yao ya kuhesabiwa haki kwa matendo isivyo na matumaini na hivyo kubaki na uwezekano mmoja tu wa kuokolewa yaani kujisalimisha kwa Yesu.

Wapagani wasiopitia mchakato wa kujihesabia haki kwa matendo ya sheria uliokuwa unafuatwa na Wayahudi, walioshindwa kufikia viwango vya utakatifu na upatanisho na Mungu, kupitia makafara na ibada zao, watazipokea kwa shukrani taarifa za kuwepo suluhisho la hali yao hiyo. Kwao huu utachukuliwa kama upendeleo kutokana na jamii ya wanadamu kuwahesabu kama waliotengwa na Mungu. (Waefeso 2:11-12) “Kwa ajili ya hayo kumbukeni ya kwamba zamani ninyi, mlio watu wa Mataifa kwa jinsi ya mwili, mnaoitwa Wasiotahiriwa na wale wanaoitwa Waliotahiriwa, yaani, tohara ya mwilini iliyofanyika kwa mikono; kwamba zamani zile mlikuwa hamna Kristo, mmefarakana na jamii ya Israeli, wageni wasio wa maagano ya ahadi ile. Mlikuwa hamna tumaini, hamna Mungu duniani.”