Marecha , Ezekiel Kibwana (1882–1982)
Ezekiel Kibwana Marecha alikuwa mwalimu wa kwanza wa Waadventista Wasabato nchini Tanzania. Alikuwa mwinjilisti wa mstari wa mbele na mzee aliyewekwa wakfu wa Kanisa la Waadventista Wasabato.
Miaka ya Awali, Elimu, na Uongofu
Alizaliwa mwaka 1882 katika Kijiji cha Kihurio, Wilaya ya Same, Mkoa wa Kilimanjaro, Tanzania. Ezekiel Kibwana Marecha alikuwa mtoto wa kwanza kati ya watoto wawili wa familia ya Marecha Wandeya na Migayo Manentho. Dada yake alikuwa Kigenda Kibwana. Baba yake alitoka Tewe, kijiji jirani na Milima ya Usambara, huku mama yake akitokea Kijiji cha Mamba kwenye Milima ya Upare. Kibwana alilelewa na mama yake kama mzazi mmoja kutokana na kifo cha baba yake wakati Kibwana alipokuwa bado mtoto mdogo.
Frida Brietly na Chris Wunderlich, wamishionari kutoka Ujerumani mwaka 1904, walianzisha shule ya kwanza ya Waadventista huko Lukuta huko Kihurio, nyumbani kwa Ezekiel Kibwana. Mnamo 1905 Ernst Kortz alianzisha kituo cha misheni cha Waadventista na jengo la kanisa. Katika mwaka huo huo, Kibwana alianza miaka minne ya elimu rasmi huko Lukuta huku akichukua kozi za kujifunza Biblia na Ernst Kortz. Mnamo 1909, Kibwana alibatizwa na Ernst Kortz na, katika mwaka huo huo, kozi yake ya miaka minne ilimstahilisha kwa taaluma ya ualimu.
Ndoa na Familia
Mnamo 1910, Ezekiel Kibwana alimuoa Ruth Kime. Walijaliwa watoto wanne. Wana watatu waliitwa Uzia Ezekieli, Dani Ezekieli, na Elirehema Ezekieli. Binti mmoja aliitwa Suzan Ezekieli. Mnamo 1936, Kibwana alimuoa Mfele Shangari kama mke wa pili. Hilo lilipingana na kanuni za kanisa na kumfanya atengwe na ushirika wa kanisa. Mke wake wa pili alizaa watoto saba: wana wawili, Daudi Ezekiel na Gadi Ezekiel, na binti watano, Mangereza Ezekiel, Tabu Ezekiel, Dina Ezekiel, Miriam Ezekiel, na Hellen Ezekiel. Mnamo 1950, Kibwana alimtaliki mke wake wa kwanza; na hivyo kuleta suluhisho na kanisa lake la Kihurio juu ya tatizo la mitara na akaanza tena kazi yake kama mzee wa kanisa.
Ajira na Uchungaji
Kibwana aliajiriwa kwa mara ya kwanza kama mwalimu kuanzia 1909 hadi 1912 katika Shule ya Lukuta. Mnamo 1913, alihamishiwa Kijiji cha Bwiko ili kutoa huduma za kanisa na majukumu ya kufundisha huko. Wakati wa Vita vya Kwanza vya Ulimwengu, wamishonari Wajerumani walikamatwa na kuwa wafungwa wa vita mwaka wa 1916. Ezekiel Kibwana alikuwa miongoni mwa wanaume wanne Waafrika wenye uwezo waliowekwa rasmi kuchukua madaraka ya uongozi yaliyoachwa na Wajerumani waliokamatwa. Kibwana alipewa jukumu la kusimamia kazi hiyo Kihurio pamoja na kuwasimamia wazee watatu wa kanisa waliowekwa wakfu, Petro Sebughe katika Kituo cha Suji, Daniel Teendwa katika Kituo cha Mamba, na Abraham Msangi katika Kituo cha Vunta. Walimu walikuwa miongoni mwa wamishonari waliokamatwa. Kibwana aliteuliwa kuwa msimamizi wa shule, akisimamia uendeshaji wa shule kumi na tano za Waadventista wa Pare hadi 1921. Shule moja tu kati ya shule kumi na sita za awali ilifungwa wakati wa vita .
Mmishonari Spencer George Maxwell alisema kwamba Kibwana alikuwa Mkristo ambaye misheni yoyote inaweza kujivunia na ambaye mmishonari yeyote angeweza kufurahi kuwa pamoja naye akiwa mshirika. Alizungumza Kipare, Kiswahili, Kijerumani, na Kiingereza. Alisimamia kazi yote ya Tanganyika, ambayo awali ilikuwa na vituo kumi na saba vya misheni. Alifanya mikutano ya uamsho makanisani, akawapanga washiriki kufanya kazi kwa ufanisi, na kuungwa mkono na makanisa. Pia aliyaweka makazi ya Wazungu katika hali ya salama wakati wamishionari hao walipokuwa hawapo.
Wakati wamisionari walipokuwa hawapo, Kibwana aliweza kushughulikia majukumu ya kanisa ndani ya kanisa la Waadventista huko Pare, kuendesha ndoa na mazishi, na kutoa ushauri kwa makanisa. Mnamo 1921, alitumwa kutoka kwa makanisa ya Wapare hadi Usukuma kubatiza waumini wapya 120. Spencer George Maxwell, ambaye alifika Kihurio mwaka wa 1921, alikiri kwamba Kibwana alikuwa kiongozi wa eneo hilo aliyejitolea sana. Aliipanga kazi pamoja katika nyakati ambazo hazikuwa na viongozi wazungu. Hivyo alistahili kutengwa kwa ajili ya kuwekwa wakfu. Mwaka 1924, Kibwana na mkewe walitembelea Misheni ya Ntuzu na akatumwa kufundisha Ikizu mkoani Mara ambako alikua mwalimu mkuu. Mnamo 1950, alipewa jukumu na mkuu wa wilaya ya Same kuandika historia ya kabila la Wapare kwa mshahara wa shilingi 100 na alikamilisha kazi hiyo katika kipindi cha miezi mitatu.
Kustaafu na Umauti
Mnamo 1927, Kibwana alirudi Kihurio na kuishi mahali paitwapo Nazareti karibu na kanisa la sasa la Kihurio Mission. Hata hivyo, baadaye alihamia eneo la Kankokoro. Kuanzia 1930 hadi 1950, Kibwana aliajiriwa kama karani wa mahakama ya serikali kwa vijiji vya Mamba, Kirangare na Gonja. Kati ya 1958 na 1962, alifanya kazi kama mwenyekiti wa Jumuiya ya Wakulima wa Kihurio. Kibwana aliendelea kumtumikia Mungu maisha yake yote hadi alipofariki Machi 16, 1982 na kuzikwa katika Kijiji cha Kihurio eneo la Uzambara.
Urithi
Kibwana atakumbukwa kama mwalimu wa kwanza wa Waadventista Wasabato nchini Tanzania. Pia alithaminiwa kwa kutunza kazi za Kanisa la Waadventista, makanisa na shule, nchini Tanzania wakati wa Vita vya Kwanza vya Kidunia bila wamishionari. Alikuwa mtu wa kwanza kuandika historia ya Wapare. Alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kabisa kutoka Pare kutumwa kuwa mmishionari wa eneo la Usukuma na Mara akiwa mzee wa kanisa. Maisha yake ya ajabu yalijulikana zaidi wakati Kibwana alipofariki akiwa na umri wa miaka mia moja.