Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

NDEMBELA YAVAMIWAShule ya Sekondari Ndembela iliyopo wilaya ya Rungwe na mkoa wa Mbeya, inayomilikiwa na Kanisa la Waadventista Wasabato, iliingia katika migogoro na Halmashauri ya Rungwe ikidaiwa kumiliki shule iliyokuwa ya wananchi isivyo halali. Madai haya si ya kweli kama nitakavyotoa maelezo hapa chini. Shule ya Sekondari ya Ndembela hapo mwanzo ilianza kama shule ya msingi huku ikimilikiwa na Wananchi chini ya usimamizi wa mamlaka ya Halmashauri inayoitwa RUDET (Rungwe Development Trust).

Baadaye wenye shule chini ya wakala wao wakaliomba Kanisa la Waadventista Wasabato kuiendesha shule ya Ndembela kutokana na changamoto za uendeshaji zilizokuwa zinaikabili shule wakati huo. Kanisa lilikubali ombi hilo la kuiendesha shule, lakini mambo yaliendelea kutoenda vizuri kwa upande wa wamiliki wa shule yaani Halmashauri ya Rungwe (iliyokuwa inawasimamia wananchi) na ndipo uamuzi wa viongozi wa vijiji vinavyomiliki shule hiyo ulipoamua kuliomba kanisa kuwa mmiliki wa shule ili kujaribu kuinusuru shule hiyo.(Nyaraka za makubaliano zipo)

Kanisa baada ya kupitia hatua za kisheria lililikubali ombi hilo na lilimilikishwa shule hiyo na Wizara ya Elimu na kuanzia wakati huo shule ikawa mali ya kanisa la Waadventista wa Sabato. Mchakato huo wa kuzimilikisha shule zilizokuwa zinaendeshwa na wananchi, ulitumika pia katika kuzimilikisha shule zingine tatu zilizokuwa zinaendeshwa na wananchi wa wilaya ya Rungwe, kwa madhehebu za kikristo kama ifuatavyo. Shule ya Kipoke ilimilikishwa kwa kanisa la Baptist, shule ya Lutengano ilimilikishwa kwa Kanisa la Moroviani na shule ya Mwakaleli ikamilikishwa kwa kanisa la Lutherani.

Kanisa la Waadventista Wasabato baada ya kumilikishwa shule hiyo, lilifanya juhudi kubwa ya kuiendeleza hadi leo imefikia kuwa na kidato cha tano na sita, kuongeza idadi ya majengo, miundo mbinu mbali mbali na uwekezaji mkubwa sana pamoja na kusajili idadi kubwa sana ya wanafunzi. Mmiliki alianzisha shule ya awali na ya msingi ambayo baadaye ilikuja kufungiwa kutokana na mambo yanayohusiana na mgogoro huu huu. Mafanikio ya shule ya Ndembela kwa malezi bora ya watoto na taaluma chini ya usimamizi wa kanisa la Waadventista Wasabato ni wa kupigiwa mfano. Mfano mdogo katika matokeo ya kidato cha nne mwaka 2012 shule imeshika nafasi ya kwanza kiwilaya kwa upande wa taaluma.

Madai ya kutaka shule irudishwe kwa wanainchi yalianza wakati shule ilipokuwa inapiga hatua kubwa za maendeleo na wakati kila kata ilipotakiwa ijenge shule ya sekondari ya wananchi. Baadhi ya wanakijiji kwa kushawishiwa walianza harakati za kudai  shule ya Ndembela irudi mikononi mwao. Kanisa halikuona sababu ya kukubali kuirudisha shule mikononi mwa wananchi kupitia Halamshauri ya Rungwe kwa kuwa ilikuwa kinyume cha makubaliano ya awali. Baada ya kutoridhika na uamuzi wa Kanisa, Halmashauri ya Rungwe ilipeleka mashtaka mahakamani ambako baada ya muda mrefu wa kusikilizwa, Mahakama Kuu ya kanda ya Mbeya iliyatupilia mbali madai na malalamiko hayo na kulitangaza Kanisa la Waadventista Wasabato kuwa ni wamiliki halali wa shule ya Sekondari Ndembela.

Hata baada ya maamuzi haya ya mahakama, Halmashauri ya wilaya ya Rungwe na Mkuu wa wilaya ya Rungwe waliendelea kushikilia kuwa shule hiyo ni lazima irudi kwa wananchi na Jumapili tarehe 16 Juni 2013 walitimiza azma hiyo kwa kuvamia shule hiyo, kuchukua vifaa vyote vya jengo la utawala lenye ofisi ya mkuu wa shule, makamu wa mkuu wa shule, ofisi za makarani, ofisi ya uhasibu, na ofisi ya taaluma na kupakia mali zote zilizokuwemo kwenye malori matatu ya halmashauri na kwenda nazo kusikojulikana huku wakifunga kwa makufuli yao lango la kuingilia kwenye jengo la utawala na jengo la maktaba.

Kana kwamba hiyo haitoshi siku ya Jumatatu tarehe 24/06/2013 wakitumia gari la matangazo walipita katika mitaa inayozungukia shule ya Ndembela wakiwaonya wafanyakazi na wanafunzi waliopo ndani ya maeneo ya shule ya Ndembela kuondoka ndani ya siku saba kuanzia siku ya tangazo na wote watakaokaidi agizo hillo watakuwa wanajihatarisha wenyewe kwa kuwa wananchi wataingia shuleni hapo ili kuichukua shule hiyo kwa nguvu. Uvamizi wote, na hatua hizo za matangazo hazina kibali cha mahakama, jambo linaloacha maswali mengi kama kweli maamuzi haya yanafanywa na serikali yetu tukufu ambayo huzingatia kuendesha shughuli zake kwa utawala wa kisheria.

Madai mapya yaliyoibuliwa sasa na viongozi wa wilaya ya Rungwe, pengine kwa kutambua kuwa uwezekano wa kufanikiwa katika kudai umiliki wa shule kwa njia za mahakama ni mdogo, yamejikita katika kudai ardhi wakiwahimiza wananchi kuiondoa shule kwenye ardhi yao. Hata katika hilo la ardhi, shule ina uhalali wa kumiliki ardhi ilikojengwa shule kwa kuwa wanayo hati inayowaruhusu kuendelea kuwepo kwenye ardhi hiyo hadi 2023. (Hati zipo). Hata hivyo, kwa sheria za Tanzania hakuna shule inayoweza kusajiliwa bila kuthibitisha kuwa na umiliki wa ardhi. Kanisa la Waadventista Wasabato lilimilikishwa shule ya Ndembela kwa kuwa liliweza kuthibitisha uhalali wa kumiliki ardhi. (Hati ya umiliki wa shule ipo)

Tunaiomba jumuiaya ya wapenda amani watambue kwamba kinachofanyika dhidi ya wamiliki halali wa shule ya Ndembela – kanisa la Waadventista Wasabato ni uonevu wa wazi, na ukiukwaji wa haki za kiraia. Tunawaomba watusaidie kuijulisha jamii na serikali yetu tukufu kuwa wamiliki wa shule ya Ndembela wana haki ya kutiwa moyo kwa maendeleo ya kielimu waliyochangia kwa wilaya ya Rungwe na Tanzania kwa ujumla, na kwamba kwa kuwa mahakama inawatambua kuwa ni wamiliki halali hivyo wana uhalali wa kuendelea kukaa na kuendesha shughuli za elimu kwenye shule ya Ndembela. Jitihada zetu za kuuona uongozi wa Wilaya na Mkoa ili kutatua mgogoro huu kwa njia za kistaarabu mara zote zimegonga mwamba.

Wamiliki wa shule ya Ndembela hawana ugomvi na Halmashauri ya Rungwe na wananchi wake wala hawana nia ya kuwadhulumu ama kuwa na ugomvi nao. Tumeishi nao vizuri kwa muda mrefu na hatuoni kwa nini haya yatokee wakati huu. Tunakaribisha mazungumzo yoyote yenye nia ya kuona pande zote za mgogoro zinanufaika kwa maridhiano yasiyo ya kushurutishwa. Lakini hatuoni uhalali wa kumlazimisha mmiliki anayetambuliwa kisheria kuondoka kwenye shule ya Ndembela bila kuzingatia ni nini itakuwa hatima ya mali yake aliyowekeza na hasa maagizo hayo yanapotolewa na vyombo ambavyo kikatiba havikupewa mamlaka na bila kuzingatia sheria. Mungu ibariki Ndembela. Mungu ibariki Tanzania.