Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

EZEKIELI


MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 1:1-28

 1. Ezekieli anajaribu kumuelezea Mungu kwa lugha ya kibinadamu. Dhana ya kuvutia ni kwamba palikuwa na mfano wa kiti cha enzi ambapo juu ya kiti kile palionekana mfano wa mwanadamu. Unalipokeaje wazo la mwanadamu kuwepo kwenye kiti cha enzi? Je mwanadamu yule ni wewe au ni Yesu? (Ufunuo 3:21)
 2. Maono aliyoonyeshwa Ezekieli yalikuwa yanaashiria binadamu anayo nafasi katika Uungu.  Unadhani wanadamu wanakidhi vigezo vya kukalia kiti cha enzi cha Mungu? Mwana mpotevu alivikwa pete na baba yake kuashiria kuwa atakuwa mtawala. Je wanadamu watawatawala na viumbe wasioanguka dhambini? (Danieli 7:27)

MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 2:1-10

 1. Kwa nini ilikuwa lazima Roho wa Mungu awe ndani ya Ezekieli ili kuweza kusikia Mungu anasema nini? Je hali hiyo ni hivyo hivyo hata leo kwetu?
 2. Je ni mtihani mgumu kiasi gani kutumwa kupeleka ujumbe kwa watu wenye mioyo migumu na wenye nyuso zisizo na haya? Je kuna matumaini yoyote kwa ujumbe huo kupokelewa?
 3. Unadhani tumekuwa waaminifu kwa agizo hilo la Mungu kwa kujituma kupeleka ujumbe hata kwa wale wasioukubali? Je ili ujumbe ukubalike kuna haja ya kuupunguza makali? Kama ujumbe umekuwa haupokelewi ni nini kifanyike?
 4. Je kutumia Maandiko ndiyo njia pekee ambayo Mungu aliichagua kupeleka ujumbe wa Injili? Neno la Mungu lina nafasi gani leo katika kupeleka ujumbe?


EZEKIELI 3:1-27

NILICHOGUNDUA NA KUJIFUNZA:

 1. Kula gombo ni kuingiza uelewa na maarifa kwenye akili za binadamu kutokea kwenye chanzo kikuu cha maarifa yaani Mungu. Kula gombo ni kuielewa akili ya Mungu juu ya dhana inayoshughulikiwa ili kupata lugha rahisi ya kuieleza au kuifafanua kwa walengwa. Kula gombo ni kuelewa msimamo na mtazamo wa Mungu juu ya mada husika.
 2. Katika kula gombo Roho Mtakatifu na malaika hutoa msaada. Ipo tofauti katika kupeleka Neno la Mungu kwa watu wapya na kwa wazoefu. Kinachofanya wazoefu wasilipokee Neno si ugumu wa Neno lenyewe ila ni kujiona bora kuliko Neno. Kuna hatari katika kujiweka mbali na Neno na kuna hatari ya kulizoea Neno. Yote mawili huhafifisha mguso unaoweza kuleta ukombozi.
 3. Mungu humhesabia hatia mjumbe asiyefikisha ujumbe wa onyo kwa walengwa kwa uaminifu. Ile adha inauoibuka baada ya mjumbe kufikisha ujumbe wa maonyo ndiyo iwezayo kumletea uponyaji yule mwonywaji. Huruma ya kweli ni kupeleka ujumbe kama ulivyo hata kama unasababisha maumivu. Mkosaji hahitaji maneno laini.

 
MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 4:17

 1. Unabii unaohusisha mahesabu hutumia kanuni ya siku moja kumaanisha mwaka mmoja kutoka Ezekieli 4:6. Je unafahamu kwa kutumia kanuni hiyo muda wa kusafiri kwa watakatifu kwenda mbinguni umejulikana kuwa utakuwa siku saba? Unaweza kuikokotoa hesabu hiyo?
 2. Je unaionaje lishe aliyoagizwa kuitumia Ezekieli katika kipindi chake cha kutoa unabii inawafaa wakazi wa leo wa dunia? Kuna kitu gani muhimu katika lishe hiyo? (Ezekieli 4:9).
 3. Je nyama ichukizayo (najisi) na nyamafu bado ni kitu kisichostahili kuliwa na wacha Mungu hadi leo? (Ezekieli 4:14)


MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 5:1-17

 1. Upendo wa Mungu kwa Israeli unamlazimisha atume adhabu kali kwao kwa kuwa hawataki kuitikia upendo huo kwa utii kwake. Je ni kawaida kwa mtu unayempenda kumuonea wivu? Je, hakuna njia nyingine ya kuonyesha unampenda mtu asiyekupenda zaidi ya kumuadhibu? 
 2. Kila wakati Mungu alipoliadhibu taifa la Israeli aligharimika kulijenga upya na kulirejeshea hali yake ya awali. Kwa nini Mungu alifanya hivyo? Kama Mungu aliwachagua Israeli ili wawe taifa la mfano na ulimwengu wote ukamtambue Yeye kama Mungu mwenye upendo, kitendo cha Israeli kutoishi sawa na kusudi la Mungu kulileta hasara gani kwa Mungu, kwa Israeli, na mataifa yaliyowazunguka?
 3. Je kitendo cha Mungu kumruma Ezekieli kunyoa nywele kwa panga kilikuwa cha lazima ili kuwaonyesha kile Mungu atakachowafanya wasipotubu? Ili kuwasaidia jamaa zako wanaopotea ni lazima wakati fulani kuingia gharama inayofanana na hiyo ya kunyoa nywele?


MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 6:1-14:

 1. Mungu anachukizwa na ibada ya uongo. Unadhani ni kwa nini Mungu anachukizwa sana na ibada hiyo? Umetathmini kwa kina kiasi gani kujiridhisha kama ibada unayomfanyia Mungu inafanyika kwa misingi ya Maandiko? Kumuabudu Mungu katika Roho na Kweli ndiyo msingi wa ibada ya kweli? (Yohana 4:23-24). Nini tafsiri ya kumuabudu Mungu katika Roho na Kweli?
 2. Je Shetani anahusika kwa kiasi gani katika kuwafanya wanadamu wawe na ibada iayopingana na Maandiko? Shetani ananufaikaje katika mpango huo? Je wanaofanya ibada isiyokidhi matakwa ya Maandiko wanajua kuwa ibada yao ni bure na kwamba watakuja kuhukumiwa? (Marko 7:7-8).
 3. Pambano la Mwisho kati ya Kristo na Shetani litahusu ibada (Ufunuo sura ya 13). Je wakati huo upo jirani kiasi gani? Maandalizi ya Mungu na ya Shetani kuiendea siku hiyo yapoje na yamefikia hatua gani? Wewe binafsi umejiandaaje?

 
MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 7:1-27

 1. Mungu anatoa angalizo kuwa siku ya fujo inakuja. Unadhani alikusudia kuwatambia Israeli au ilikuwa wajitambue na kumrudia Mungu wake? Kwa nini Mungu anatumia lugha ya kusema siku hiyo mtajua kuwa mimi Bwana napiga? Je kuna wakati wa kubadilisha lugha ya kubembeleza kwa watu wanaopotea na kutumia lugha inayoonekana kama ya kibabe?
 2. Mungu anaposema siku hiyo sitaona huruma ni kuonyesha kuwa asili yake ni mwenye huruma? Je, ni kweli kuwa dawa ya kiburi ni jeuri? Kwa nini anunuaye na auzaye hawatakuwa na tofauti siku hiyo ya ghadhabu ya Mungu? Kwa nini ghadhabu ya Mungu huenda kwa wanadamu katika hali ya kumwagwa? Je ghadhabu iliyomwagwa ina uwezo wa kuchagua wa kuangamiza na wa kupona katika jamii husika?


MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 8:1-18

 1. Dhambi za viongozi wa kiroho zinachukuliwaje na Mungu zinapofananishwa na dhambi za waumini wao? Dhana ya kwamba Mungu hatuoni tunapotenda dhambi inatokana na nini? Ni kweli kuwa hatuoni? Au ni kwa sababu anakawia kutoa hukumu?
 2. Tamuzi alikuwa ni nani katika ibada za kipagani za Agano la Kale? Kwa nini ibada juu yake iliwavutia Israeli? Ushawishi wa ibada ya Tamuzi ingali inaonekana hadi leo katika nyumba za ibada.
 3. Kwa nini waabuduo wa Tamuzi walikuwa wanazielekeza nyuso zao upande wa Mashariki? Ibada ya Jumapili inahusianaje na ibada ya Tamuzi?

 
MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 9:1-11

1.Yule mmoja aliyeingia hekaluni ana kidau cha wino ni nani? Kwa nini Mungu anatafuta idadi ya watu waliao kwa maovu yanayofanyika kabla ya kutekeleza hukumu?

 1. Je, kusudi la Mungu ni kuwaangamiza au kuwaokoa watu wake? Watu wanaoomba na kuugua kwa ajili ya maovu yanayotendeka wana umuhimu gani makanisani mwetu? Je kile kikundi cha maombi kinafanya kazi gani kanisani kwenu? Je ungependa kuona wadhambi wakiangamizwa au wakipona?


MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 10:1-22

 1. Kazi ya Mungu ulimwenguni inakamilishwa kwa ushirikiano wa nguvu za Uungu na za kibinadamu - kila mmoja akiwa na nafasi ya kufanya. Unahisi kustahili au kupendelewa unapoifanya kazi ya Mungu?
 2. Mungu ni Mungu wa utaratibu kama ilivyo katika makanisa yote ya watakatifu (1 Wakorintho 14:33, 40) na hali hii inadhihirishwa na kile alichooneshwa Ezekiel ambapo pamoja na utofauti wa majukumu viungo vyote vilifanya kwa ushirikiano. Unaizungumziaje hali ya mivutano tunayoishuhudia kwenye kazi ya Mungu katika taasisi na baadhi ya makanisa? Je tofauti za karama zimekusudia kuleta umoja au uhasama?
 3. Kupaa juu kwa Makerubi kunaashiria ukuaji wa kazi ya Mungu ukiwezeshwa na Roho Mtakatifu. Je unaiona kasi ya ukuaji wa kazi katika maeneo uliyopo? Umehusika kikamilifu kuikuza kazi ya Mungu katika mwaka ulioisha?

 
MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 11:1-25

 1. Wakuu wa watu watungao uovu na kutoa mashauri mabaya wana faida gani kwa kundi la waumini? Unadhani viongozi wa aina hii wanapungukiwa nini hasa? Ilikuwaje wakapate nafasi hizo za uongozi?
 2. Mungu ameahidi kuwapa watu wake moyo wa nyama ili waenende kwa kuzitii Amri zake. Je Amri za Mungu zinapingana na mpango wa wokovu? Je hitaji la wale wanaojikuta wakianguka anguka kwenye dhambi ni moyo mpya wa nyama? Je moyo mpya wa nyama hufanya nini kisichowezekana na moyo mgumu? Unawezaje kujua kama una moyo wa nyama?

 
MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 12:1-28

 1. Mwenye macho ya kuona lakini hayaoni na mwenye masikio ya kusikia lakini hayasikii shida ya mtu huyo hasa ipo kwenye macho na masikio au ipo kwenye tafsiri ya akili ya jambo husika ambayo ameing'ang'ania na hataki kuiachia. Je huwa ni jambo jepesi kupokea nuru mpya inayokinzana na uelewa wako wa awali?
 2. Je kutofautiana na wengine katika uelewa wa jambo fulani kwaweza kukujengea uadui na watu hao? Unapopokea nuru mpya ya uelewa wa Maandiko wapaswa kufanya uamuzi wa kuifuata kwa siri au kwa wazi mchana kweupe?
 3. Kuna wakati unatamani kutoa ujumbe wa faraja lakini sauti inakuhimiza kutoa ujumbe wa onyo kulingana na hali ya uasi inayoshamiri. Je ikiwa baada ya ujumbe huo lawama zitazuka hiyo ni ishara kuwa ujumbe huo haukutoka kwa Mungu?
 4. Kwa nini mara nyingi ukuu wa Mungu hutambulika na wanadamu hasa pale anaposababisha kuwepo kwa maafa yanayowaacha wanadamu wote midomo wazi kama njaa, magonjwa, mafuriko, vita, na mabadiliko ya hali ya nchi, lakini huwa nadra kutambua ukuu wake wakati wa amani?
 5. Mungu afanye nini ili wanadamu wamtambue na kumheshimu hata katika wakati wa amani? Je kukawia kwa Mungu kutekeleza yale aliyosema atayatenda watu wasipotubu ndiko kunakochangia watu kutoyapa uzito maonyo yake? Kipi bora Mungu akawie kutimiza hukumu zake au asikawie? (2 Petro 3:9).


MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 13:1-23

 1. Wale wanaotabiri kwa kufuata maoni yao wenyewe wanafananishwa na wajinga. Unadhani walistahili kuonekana hivyo? Ni jambo gani linaweza kumsukuma mtu kutoa unabii ambao hakutumwa na Mungu?
 2. Je kuna uwezekano wa wanadamu kumtumia (kumdalalia) Mungu ili kujinufaisha wao wenyewe? Kwa nini manabii wa uongo huwatumainisha watu kuwa jambo fulani litatokea wakati uhakika wa kutokea kwa jambo lenyewe hakuungwi mkono na Maandiko?
 3. Kwa nini kutoa unabii wa uongo kunafananishwa na kupaka ukuta chokaa isiyokorogwa vema? Miujiza inayofanywa na makanisa yaliyoasi maagizo ya Mungu inaonekana kupendezesha makanisa hayo kama chokaa isiyokorogwa vema ipendezeshavyo kuta. Je kuna wakati ambao Mungu ataweka dhahiri mbinu hizo za udanganyifu? Je Shetani ana mpango wa kuitumia mbinu hiyo kwa nguvu katika Siku za usoni? (Ufunuo 13:13-14).
 4. Wanawake wawindao roho za watu kwa kuwavutia kwa mwonekano wao wanafananishwa na makanisa yanayotumia hila kuvutia watu ili hatimaye waangamie. Unadhani ni mbinu gani ambazo makanisa huzitumia kunasa Roho za watu?
 5. Je hali ya wanawake wajao kwenye nyumba za ibada inafanana na ya wanawake wanaotajwa kwenye Ezekieli 13:18-19? Je mavazi ya wanawake yana uwezekano wa kuziwinda Roho za watu? Je Mungu atawaadhibuje watu hao?


MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 14:1-23

 1. Kutwaa vinyago na kuvitia moyoni ni kuwa na dini inayotunza dhambi unayoipenda moyoni ambayo usingependa Mungu na wanadamu wajue na kujidhania kuwa upo salama (Mathayo 15:8). Je inawezekana kuiacha dhambi unayoipenda? (Warumi 7:15).
 2. Kuwa na hila moyoni kwaweza kuzuia maombi yako yasimfikie Mungu (Isaya 59:2). Kwa nini hata kushindwa kusamehe wengine kwaweza kuzuia maombi yako yasipokelewe na Mungu? (Marko 11:25-26).
 3. Mungu anapoukaza uso wake au anapounyosha mkono wake dhidi ya mtu ni namna nyingine ya kusema anaweka kando huruma yake dhidi ya mtu huyo. Unadhani Mungu huifurahia hali hiyo au ni hatua ambayo analazimika kuichukua bila kuifurahia?
 4. Je, mwanadamu aweza kuokolewa kwa matendo mema ya mtu mwingine? Je iliwezekanaje watoto wa Nuhu na wa Lutu wakaokolewa? Je ilitokana na matendo mema ya wazazi wao? Je matendo mema ya Yesu Kristo yaweza kuwaokoa wanadamu wenye dhambi? Kwa nini?


MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 15:1-8

 1. Mungu alimchagua mwanadamu kama alivyoichagua Israeli ili azae matunda na matunda yake yakapate kukaa (Ezekieli 17:8; Yohana 15:6). Ni nani anahusika kuhakikisha mti unazaa matunda? Huduma za kuunyweshea maji na kuupa virutubisho inafanywa na nani? Nani anasababisha usizae matunda? Ni Mungu ni Shetani au ni Mwanadamu mwenyewe?
 2. Kwa nini mwanadamu, taifa la Israeli na Yuda, (na hata Yesu mwenyewe) wamefananishwa na Mzabibu au shamba la Mzabibu? (Yohana 15:1; Isaya 5:7). Mzabibu una sifa gani ambayo miti mingine ya matunda haina?
 3. Je miti mingine ya matunda isipozaa matunda inaweza kufaa kwa jambo gani lingine ambalo huwezi kulipata kwa mzabibu usiozaa matunda? Je wanaoshindwa kuishi kulingana na wito wao ni wabaya kuliko wale ambao hawajaitwa?
 4. Ili mzabibu ukue na kuzaa matunda unahitaji egemeo la mti. Je egemeo letu la kiroho ni nani? Kuna uhusiano gani kati ya kuzaa matunda na kiwango chetu cha kumtegemea Roho Mtakatifu?


MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 16:1-63

 1. Dhambi za viongozi wa kiroho zinachukuliwaje na Mungu zinapofananishwa na dhambi za waumini wao? Dhana ya kwamba Mungu hatuoni tunapotenda dhambi inatokana na nini? Ni kweli kuwa hatuoni? Au ni kwa sababu anakawia kutoa hukumu?
 2. Tamuzi alikuwa ni nani katika ibada za kipagani za Agano la Kale? Kwa nini ibada juu yake iliwavutia Israeli? Ushawishi wa ibada ya Tamuzi ingali inaonekana hadi leo katika nyumba za ibada.
 3. Kwa nini waabuduo wa Tamuzi walikuwa wanazielekeza nyuso zao upande wa Mashariki? Ibada ya Jumapili inahusianaje na ibada ya Tamuzi?


MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 17:1-24

 1. Mungu hutumia mifano vielelezo katika kufafanua uasi unaotendwa na wanadamu dhidi yake. Kwa kufanya hivi huwa anakusudia kuleta ugumu katika ujumbe wake au anakusudia kurahisisha? Je tunapowasimulia watoto hadithi za paka na panya au sungura na fisi ni kuwapotosha au kuwasaidia? Je kila kisa unachokisimulia katika kufundisha ni lazima kiwe cha kweli?
 2. Mfalme wa Yuda alivunja agano au makubaliano na Babeli na kuunda ushirika na nchi ya Misri ili kupata usaidizi wa kuipiga vita Babeli kinyume cha maelekezo ya Mungu. Kwa nini jambo hili lilimkasirisha Mungu?
 3. Hutokea shida gani ikiwa Kiongozi wa kiroho au wa taifa ataongoza bila kuzingatia miongozo inayoratibu kazi zake? Je mwanadamu ana uwezo na haki ya kubadilisha maelekezo na maagizo ya Mungu?
 4. Kitawi kidogo chororo ambacho hatimaye Mungu atakipanda juu ya mlima mrefu ni Yesu Kristo - mtawala mwenye haki na mfalme wa amani atakayetawala dunia yetu na malimwengu yote (Dan.7:27). Je ungependa kuwa mshirika wa utawala huo? (Ufunuo 3:21).
 5. Mungu ana mpango wa kuuinua mti mfupi na mkavu kuchukua mahali pa miti mirefu na mibichi isiyozingatia maagizo yake. Unaona Mungu akifanya hivyo katika chaguzi za kanisani na huko duniani? Kuna hatari gani kuwa na kiongozi asiye na hofu ya Mungu?


MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 18:1-32

 1. Kula zabibu mbichi huleta ganzi kwenye meno ya mlaji. Msemo kuwa Baba wamekula zabibu mbichi na watoto wakatiwa ganzi ulilenga kuhalalisha dhana kuwa madhara ya maovu yao yataonekana zaidi kwa watoto lakini Mungu anasisitiza roho ile itendayo dhambi ndiyo itakayokufa. Je kwa mtazamo huo kuna uwezekano wa dhambi iliyotendwa na wazazi au maagano ya ukoo yakakuathiri wewe usiyeshiriki dhambi hiyo?
 2. Ikiwa aliyefanya dhambi ataghairi na kuacha njia zake mbaya Mungu anaahidi kumhesabia kama ambaye hajatenda dhambi. Je kanuni hii ina nafuu gani kwa mwenye dhambi? Kwa utaratibu huu Mungu anaonekana kupendezewa na adhabu ya mwenye dhambi au anatamani kumuona anaishi?
 3. Wakati Biblia ikituambia roho itendayo dhambi itakufa zipo dhana kuwa wenye dhambi hawafi ila huenda sehemu ya mateso na ikiwa ndugu zao watawaombea hupokelewa mbinguni. Ipi ni dhana sahihi? Kwa nini wazo kuwa mwanadamu akifa amekufa huwa halipokelewi na wanadamu hata kama aliyelisema ni Mungu? (Mwanzo 3:3-4)
 4. Kwa mujibu wa (Ezekieli 18:5) mtu mwenye haki ni yule atendaye yaliyo haki na halali. Kama hivyo ndivyo kwa nini (Warumi 1:17) inasema mwenye haki ataishi kwa imani? Je mtoto aliyeishi akiyashuhudia maovu yanayotendwa na wazazi wake lakini hakuyashiriki ana uwezekano wa kupona hukumu ya Mungu? Usemi kuwa mtoto wa nyoka ni nyoka una ukweli gani katika mazingira haya?
 5. Kama Mungu hafurahii kufa kwa mtu mwovu anafanya jitihada gani ili huyo mtu mwovu asifie dhambini? Je uwezo wa kughairi au kuacha kutenda dhambi hutoka kwa Mungu au hutoka kwa mwovu mwenyewe? (Matendo 5:31; Matendo11:18; 2 Wakorintho 7:10). Kuna tofauti ya kuendelea kufanya uovu huku ukiamini njia za Mungu si sawa na kuendelea kufanya uovu ukiamini njia za Mungu ni sawa?

 
MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 19:1-14

 1. Kushindwa kutumika vyema kwa watumishi wa Mungu na vitendea kazi vya injili kumefananishwa na simba aliyefundishwa kuwinda hatimaye akaishia kunaswa kwenye kulabu ili sauti yake isisikike tena. Unaonaje matumizi ya vyombo vyetu katika kupeleka injili? Ni maeneo gani tunapaswa kuyaboresha ili yaendelee kufanya jukumu lililokusudiwa?
 2. Je kuna jambo lingine linalopaswa kupewa kipaumbele katika kanisa zaidi ya uinjilisti? Je ujenzi wa makanisa yenye hadhi na yanayotosheleza ni sehemu ya uinjilisti au utume?


MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 20:1-49

 1. Mungu aliwaleta Waisraeli jangwani na kuwapa Amri ambazo alikusudia ziwe kwa ajili ya wanadamu wote. Kwa nini leo baadhi ya watu wanazieleza kama zilihusu Wayahudi pekee? Sabato ilikusudiwe iwe ishara au kitambulisho cha watu wa Mungu. Kwa nini Wakristo wa leo wanaonekana kutoitaka Sabato iliyowekwa na Mungu na kukumbatia Sabato iliyowekwa na wanadamu?
 2. Mungu alimaanisha nini aliposema aliwapa Waisraeli amri zisizo njema na hukumu ambazo hawakuweza kuishi kwazo? Je hapa alikuwa anazungumzia Torati? Kwa nini Mungu aliwapa amri ambazo alijua kuwa si njema?

 
MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 21:1-32

 1. Ujumbe wa Ezekiel 21 unatolewa wakati taifa la Yuda likinyemelewa na maangamizo ya upanga kutoka Babeli huku wakiwa wameyapuuza maonyo yote kutoka kwa Mungu. Unauona ulimwengu wetu ukiwa unaelekea katika hali kama hiyo hiyo? Ni kweli kuwa katika zahama hiyo wenye haki na wasio na haki watakuwa katika mateso makuu? Mungu ameahidi kufanya nini kwa watu wake? (Danieli 12:1-3).
 2. Mungu humwinua amtakaye na kumshusha aliyempandisha juu. Kwa nini mwanadamu akiinuliwa ana kawaida ya kumwacha Mungu?


MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 22:1-31

 1. Mungu 'huipiga kofi' faida iliyopatikana kwa njia isiyo ya haki. Taarifa hizi zina nafuu yoyote kwa mtu aliyedhulumiwa haki yake? Kwa nini Mungu anaruhusu dhuluma katika jamii kutokea? Je uzingatiaji wa sheria za Mungu na zile za kijamii una nafasi gani katika kuzuia au kupunguza dhuluma hizi? Unadhani Sheria hizo zilizingatiwa katika nyakati hizi za Ezekieli kule Yerusalemu?
 2. Mchakato wa kuyeyusha fedha, shaba, chuma, risasi na bati huzalisha madini iliyo bora ifaayo kwa matumizi. Unadhani kuangamizwa kwa waovu huleta matokeo yaliyo bora zaidi?
 3. Kuwafundisha watu kupambanua kati ya vitu vichafu na vilivyo safi ni wajibu wa viongozi wa kiroho. Unadhani viongozi wote wa kiroho wanautekeleza wajibu huo kwa viwango sawa? Unazungumziaje wale wanaoruhusu unywaji wa pombe na ulaji wa wanyama walioorodheshwa kwenye Biblia kama najisi?
 4. Mungu anatafuta mtu atakayetengeneza mahusiano ya wanadamu na Mungu na mahusiano baina yao wenyewe na atakayesimamia haki katika jamii ya waumini na katikati ya wanadamu. Je mtu huyo ni wewe? Yona alipotumwa Ninawi alikataa je na wewe utakataa? Je kusimamia haki katika mazingira ya uovu uliokithiri kunahatarisha maisha?

 
MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 23:1-49

 1. Maneno kama "walilala naye, wakayabana matiti ya ubikira wake wakamwaga uzinzi wao juu yake" yanaonekana kuwa na lugha kali isiyo na staha. Unadhani ni kwa nini Mungu analazimika kutumia lugha hiyo? Je alikuwa amekasirika? Kwa nini ibada ya uongo ni jambo la kuchukiza kiasi hicho kwa Mungu?
 2. Kuchukuliana na taratibu za kidunia na kuziingiza kanisa huanza taratibu lakini zikikomaa huwa vigumu kuziondoa. Ni kawaida gani zilizoingizwa kwa mtindo huo ambazo zimekuwa vigumu kuziondoa? Je wakati upagani ukiingia kanisani hawakuwapo watu walioona hatari hiyo na kutoa angalizo? Je ikiwa umetoa angalizo na wenzako wamepuuza ufanye nini?
 3. Mungu ana mpango wa kukomesha uzinzi na uasherati wa kiroho. Je ungependa afanye hivyo kwako sasa? Je unadhani ana mpango wa kukomesha uasherati na uzinzi wa kimwili pia? Uasherati na uzinzi wa kimwili una mchango gani katika kuvuruga ndoa?


MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 24:1-27

 1. Je ungejulishwa siku mwizi atakuja kuvunja na kufanya unyang'anyi nyumbani kwako ungechukua hatua gani? Je ungezifanyia kazi taarifa hizo ama ungezipuuza? Kutokuwa na hofu wakati changamoto ya maisha zinapokukabili ni ishara ya ujasiri au ujeuri? Kwa nini Israeli hawakupokea maonyo hadi Mungu akalazimika kuruhusu mke wa Nabii Ezekieli afariki kama njia ya kuwaonyesha Waisraeli kile kitakachotokea kwa hekalu lao litakaloshambuliwa na wavamizi wa Babeli katika Siku za karibuni?

 
MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 25:1-17

 1. Wakuu wa watu watungao uovu na kutoa mashauri mabaya wana faida gani kwa kundi la waumini? Unadhani viongozi wa aina hii wanapungukiwa nini hasa? Ilikuwaje wakapate nafasi hizo za uongozi?
 2. Mungu ameahidi kuwapa watu wake moyo wa nyama ili waenende kwa kuzitii Amri zake. Je Amri za Mungu zinapingana na mpango wa wokovu? Je hitaji la wale wanaojikuta wakianguka anguka kwenye dhambi ni moyo mpya wa nyama? Je moyo mpya wa nyama hufanya nini kisichowezekana na moyo mgumu? Unawezaje kujua kama una moyo wa nyama?

 
MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 26:1-21

 1. Kosa la Tiro ni nini? Je kuingilia ugomvi usiokuhusu kwaweza kukuletea majuto? Wakati mtu na mkewe wanapogombana wajibu wako ni nini ili usionekane unaingilia ugomvi usiokuhusu?
 2. Mungu anapolalamika juu ya kanisa lake la Laodikia kuwa ni maskini, kipofu, lenye mashaka na uchi anakusudia kulidhalilisha mbele za watu na kuliacha au ana mpango wa kuliimarisha ili asiliache? Wale wanaolisema vibaya kanisa la Mungu na kulizulia mambo ya uongo wataachwa salama? Wanapaswa kujifunza nini kwa uzoefu wa Tiro?


MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 27:1-36

 1. Tiro ilikuwa na uwingi wa utajiri, maarifa, mbinu na ilikuwa bora sana kwa mwonekano na akili kuliko jirani zake. Kwa lugha ya leo tungesema Tiro ilikamilika katika idara zote. Unadhani Tiro ilipungukiwa na nini? Leo Tiro ingefananishwa na nchi gani kwa mafanikio ya kijeshi, kiuchumi, na kidiplomasia? Unadhani Marekani yaweza kukutwa na zahama zilizotabiriwa kwa Tiro?
 2. Je Mungu ana mchango wowote katika mafanikio ya Tiro? Jambo gani lililo machukizo kwa Mungu na ambalo watu wengi waliofanikiwa hulifanya? Je ni sahihi kumuomba Mungu asinifanikishe nisije nikajivuna kama Tiro? Je uhusiano wa kimataifa na kikanda ni wa muhimu kiasi gani katika kufanikisha biashara na kukuza uchumi wa nchi na wa mtu binafsi?
 3. Je ni kweli kuwa wewe unauhitaji ulimwengu kuliko ulimwengu unavyokuhitaji wewe hasa linapokuja swala la soko za bidhaa na huduma zako? Kama kuna mkulima wa nyanya aliyekosa soko la nyanya zake hata kulazimika kuzimwaga au kuziuza kwa hasara unamshauri nini kuhusiana na uzoefu wa Taifa la Tiro?
 4. Unaitumiaje mali uliyonayo kutegemeza kazi ya Mungu? Je mali iliyotumika kuimarisha utawala wa Shetani duniani itadumu? Kwa nini utawala wa Tiro unafananishwa na utawala wa Shetani?

 
MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 28:1-26

 1. Utajiri huleta majivuno. Lakini huwaje hata binadamu ajione kuwa yupo sawa na Mungu? Je kupenda kuabudiwa ndicho chanzo cha mtu kutamani kuitwa Mungu?
 2. Ni utawala gani wa kidini unaodai kutambuliwa kama Mungu kwa mujibu wa (2 Wathesalonike 2:3-4)? Je kubadilisha taratibu za ibada ni jitihada za kutaka kuchukua nafasi ya Mungu?
 3. Ezekieli 28 kuanzia fungu la 12 hadi 19 linamzungumzia Shetani kwa kivuli cha mfalme wa Tiro. Unadhani mfalme wa Tiro amevaa uhalisia wa Shetani kwa matendo yake? Je unajisikiaje ukitambulishwa kama Shetani au Mnyama, au Mwanamke Kahaba? (Mathayo 16:23; Ufunuo 13:4; Ufunuo 17:5).
 4. Chanzo cha anguko la Shetani ni kujivunia uzuri na hekima au akili. Je ni vibaya kuwa na hekima na uzuri? Je mwenye hekima kama Sulemani alishindwaje kuona hatari ilipokuwa inamnyemelea? Nini kinahitajika ili vipawa, hekima, na uzuri visikuletee maangamizo? Kama Shetani aliumbwa mkamilifu uovu na mapungufu yake mengine vilitoka wapi? Kwa nini ukamilifu wake ulishindwa kuzuia dhambi isitokee?

 
MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 29:1-21

 1. Wakati taifa la Tiro lililotegemea ustawi wake wa kiuchumi likiadhibiwa na Mungu kwa sababu ya kuidhihaki Yuda iliyokuwa imepokea maonyo kwa Bwana, Misri inaendeleza dhana ile ile ya kujiona mbabe anayeweza kuwalinda wale waliokataliwa na Mungu akitumainia mto Nile. Ni nini unachokitegemea zaidi maishani mwako ambacho siku kikiondoka na maisha yako yatakuwa yamefika mwisho?
 2. Je ni sahihi kumtegemeza aliyekataliwa na Mungu? Misri iliyookoa maisha ya mtoto Yesu alipokuwa anatafutwa na Herode iliwezaje kutofautiana na Mungu kwa kuisaidia Yuda?
 3. Misri ilipataje jeuri ya kujivunia mto Nile ambao chanzo chake ni mvua zinazonyesha katika ukanda wa maziwa makuu ya Afrika Mashariki? Una sababu gani ya kujivunia mafanikio uliyoyapata kwa msaada wa Mungu hata ukadharau wengine na kumdharau aliyekuwezesha?


MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 30:1-26

 1. Mungu anapolipiza kisasi ni nani atasimama? Uvumilivu wa Mungu usipotumika vizuri huleta maangamizo hata kwa wasio na hatia. Zamani hizo nchi zisizozingatia maagizo ya Mungu na haki za wanadamu Mungu alikuwa anaamuru zishambuliwe kijeshi. Je kuwekewa vikwazo vya kiuchumi ni njia anayoitumia kwa nchi hizo leo? Je vikwazo vya kiuchumi ni njia sahihi ya kushughulikia watawala wanaokandamiza raia wao?
 2. Je ubabe katika kutatua migogoro ya kijamii ni njia sahihi? Unadhani Misri kwa jinsi ilivyokuwa imejizatiti ilikuwa na shaka kuwa siku moja ingeweza kushambuliwa na mataifa ya kigeni?Je anguko la kiroho huja katika wakati usiodhania au dalili zake huanza kuonekana mapema? Siyo kila mshikamano una lengo jema kwani ipo mishikamano inayoimarisha uovu na ukandamizaji. Unadhani Ethiopia na miji mingine ya Afrika ilikuwa na sababu ya kufanya mashirikiano na Misri ili kwenda kinyume na tamko la Mungu kupitia nabii Isaya?
 3. Je mtu unayempenda unaweza kukataa kumuunga mkono katika mambo yanayopingana na maagizo ya Mungu? Je kutounga mkono udhalimu unaofanywa na rafiki yako kwaweza kukuletea matatizo? Kwa nini ukiunga mkono udhalimu unaofaanywa na rafiki yako Mungu hukuhukumu? Je, kuna wakati unaweza kumuunga mkono mtu au taasisi kutokana na maslahi unayopata kwa kufanya hivyo hata kama haukubaliani na anayofanya? Kwa nini watu wa aina hiyo wanaoitwa chawa wameongezeka sana nyakati hizi?


MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 31:2-18

 1. Ukiwa umependelewa ukawa na madaraka makubwa, elimu nzuri, kazi nzuri, mume, mke, na watoto wazuri, na uchumi nzuri je kuna uwezekano wa kubaki mpole na mnyenyekevu kwa Mungu na kwa watu wote? Kwa nini Mungu pamoja na kuwa na madaraka makubwa na kumiliki kila kitu hana tabia ya kiburi kujiona na kujikweza au hata kudharau wasiokuwa nacho?
 2. Je ni rahisi kutambua kuwa mafanikio yetu yanatokana na Mungu? Je wanaojishughulisha hufanikiwa zaidi kuliko wasiojishughulisha? Kwa yako wanaojishughulisha wasiwe na sababu ya kujivunia mafanikio yao kwa kuwatambishia wale wasiojishughulisha?
 3. Mungu anapomuinua kiuchumi mtu mmoja katika familia, ukoo, au jamii anakusudia mafanikio hayo yawafikia wote au yawe yake peke yake? Kama ndugu zake wakimbagua kwa kuwa amefanikiwa afanyeje?
 4. Misri ndiyo nchi pekee iliyotajwa kwenye Amri Kumi za Mungu na ni nchi iliyokuwa imestaarabika tangu zamani kwa mujibu wa wana historia na Maandiko Matakatifu. Unadhani hapo ilipo leo ndipo mahali Misri ingepaswa kuwa kama ingefuata maelekezo ya Mungu? Unadhani kuna sababu gani iliyomfanya Mungu aipendelee Misri hivyo? 
 5. Je Tanzania iliyotumika kukomboa nchi nyingi zilizo kusini mwa Afrika ilitumiwa na Mungu? Mungu ana mpango gani kwa ajili ya Tanzania?

 
MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 32:1-32

 1. Wasiotahiriwa ni watu wasioyatoa maisha yao kwa Mwokozi ili waokolewe (Wafilipi 3:3). Kwa nini maisha ya watu hao yanaishia vibaya kwa vifo vya kutisha? Kwa nini Wayahudi waliokubali agizo la tohara hawaonekani kuathirika na maangamizo yanayotajwa kwenye sura hii ingawa wenyewe pia siyo wakamilifu?
 2. Je maangamizo ya wenye dhambi hutokana na ukaidi wa wenye dhambi wenyewe au huweza kutokana na kukaa kimya kwa waliotumwa kupeleka maonyo? Unadhani ulimwengu na watu unaofahamiana nao wakiangamia leo itakuwa imetokana na ukaidi wao au itatokana na wewe kushindwa kutoa maonyo?
 3. Ikiwa Mungu alitabiri tangu zamani kuwa Wayahudi wangeenda utumwani kwa nini anatumia muda mwingi kuwaonya ili wasiende utumwani? Je kuna uwezekano wa kubadilisha kilichotabiriwa kwenye unabii?

 
MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 33:1-33

 1. Hakika nabii alikuwako katika Israeli kwa jina la Ezekieli naye kwa uaminifu alitoa maonyo bila kukoma ili Israeli wasiangamie lakini wakaangamia. Unadhani tatizo lilikuwa katika kufikisha ujumbe au katika kupokea ujumbe? Kauli kuwa Nabii haheshiliki nyumbani kwake ina ukweli gani ukizingatia kile Yesu alichofanyiwa na watu wa Nazareti na taifa lake la Israeli ? (Marko 6:4; Luka 4:16-30) Je pengine walihitaji Nabii kutoka taifa jingine kama Ninawi ilivyohitaji Nabii kutoka Yuda? 
 2. Kwa nini Yesu alisema wasipowasikia Musa na manabii hawatashawishwa hata mtu akifufuka kwa wafu? (Luka 16:31). Je, alimaanisha upokeaji wa ujumbe hautegemei aina ya mjumbe aliyetumwa? Ujumbe uliotolewa na mwanamke kanisani unapokelewa kwa umuhimu sawa kama uliotolewa na mwanaume? Je ni kanisa gani limepokea ujumbe wa Mungu kupitia mwanamke na ujumbe huo ndiyo unaoendelea kuliongoza kanisa hilo hadi sasa? Je unadhani kanisa hilo linashambuliwa kwa madai kuwa linaongozwa na mwanamke? Je, walio kwenye kanisa hilo wanajisikia vizuri kuongozwa na mwanamke?
 3. Kama kumuonya mwenye makosa kunaweza kuhatarisha mahusiano yenu na kuacha kumuonya kunaweza kuhatarisha maisha yako ni lipi jema kufanya kati ya hayo? Ikiwa umetumwa kumuonya mtu nawe unajihisi una makosa hayo hayo unapaswa kufanyaje? Je akipuuza maonyo yako kwa kudai kuwa hata wewe si mkamilifu umetimiza wajibu wako? Kwa nini mtu mbaya akigeuka na kuacha njia zake Mungu hugairi mabaya aliyopanga kwa ajili yake na mwenye haki akigeuka na kufanya yasiyo haki hugairi mema aliyopanga kwa ajili yake? Je Mungu ni kigeugeu? 
 4. Je kuna uwezekano kwa mtu aliyeokoka kutenda dhambi tena? Kama uwezekano huo upo kwa nini anaitwa aliyeokoka? Unazungumziaje wale wanaopelekewa maonyo na kujitetea kuwa Roho hajawafunulia hilo unalowaonya. Je ni kweli hawajafunuliwa au utetezi huo ni wa uongo? Kwa nini Mungu amhukumu mtu ambaye hakusikia kuonywa katika maonyo yaliyotumwa? Je ni halali kumhukumu asiyesikia hatia kwa kosa unalomuonya? Je hiyo haipo sawa na kumwadhibu mtoto kwa sababu ya kukaa uchi?

 
MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 34:1-31

 1. Wachungaji wanakumbushwa kuwa wajibu wao ni kuwalisha kondoo, kuwarudisha waliofukuzwa na kuwatafuta waliopotea na wala siyo kuwatawala kwa nguvu na ukali. Unadhani ushauri huo unazingatiwa? Anaposema wachungaji wasiwachinje kondoo walionona anamaanisha nini?
 2. Kuna utapeli mwingi wa kiroho unaoendelea kiasi wale wenye kiu ya kutafuta wokovu wa kweli wanajikuta wakitanga tanga kutoka dhehebu moja kwenda lingine. Nani wa kulaumiwa hapa kati ya wachungaji waongo na wale kondoo wanaodanganywa?
 3. Njia sahihi ya kuwakinga waumini wasitange tange wasihadaiwe na wachungaji mbwa mwitu waliojivika mavazi ya kondoo ni kuwapa mafundisho ya kweli ya kutosha, kuwa karibu nao katika changamoto zao za maisha au kuwatendea miujiza au vyote?
 4. Mungu anaahidi kuwatafuta kondoo wake waliopotezwa na kuwaleta kwenye zizi moja (Ezekieli 34:11; Yohana 10:16). Hilo zizi moja ni lipi?
 5. Biblia inaposema mavuno ni mengi ila watendakazi ni wachache ina maana gani wakati leo tunashuhudia idadi ya watumishi wa kiroho ikiongezeka kila uchao wakijiita manabii, mitume, bishop, wainjilisti n.k.? Je Mungu anazungumzia uwingi au ubora?

 
MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 35:1-15

 1. Uadui usiokoma Mungu anauchukia. Nini kinafanya watu wawe na uadui usiokoma? Je roho ya kulipiza kisasi ndiyo inayofanya watu kuwa na uadui usiokoma? Nifanyeje ikiwa nashindwa kusamehe kosa nililokosewa? Je kupatanisha watu kwaweza kupunguza visa hivi vya uadui usiokoma? (Warumi 12:19; Mathayo 6:15; Mathayo 5:9).
 2. Je Ukristo una nafasi gani katika kuondoa chuki zinazotokana na tofauti za utaifa, makabila, na jinsia? Kama bado namchukia mtu kwa sababu ya kabila lake hiyo inaashiria kwamba sijaongoka? Je unachukuliaje pale mtu anapoona ni heri binti yake aolewe na mpagani wa kabila lake kuliko na Mkristo wa kabila jingine? Nini kimesaidia Tanzania kutokuwa na uhasama mkubwa wa makabila kama nchi kadhaa za jirani?


MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 36:1-38

 1. Mungu anaonekana kutokuwa na ugomvi na viumbe vyake vya asili alivyoviangamiza kwa ajili ya uovu wa Israeli. Je, mara zote Mungu anaporuhusu majanga na maafa hali hiyo inatokana na uasi wa wanadamu wanaoikaa ardhi husika? Je Mungu kwa kuongea na milima na mifereji iliyoharibiwa anaonyesha kiwango chake cha kujali viumbe na maumbile yake ya asili? Ni vipi anavyovijali zaidi kati ya viumbe vyake vya asili na wanadamu?
 2. Je, ni sahihi kuulinganisha uovu wa wanadamu mbele za Mungu na uchafu wa mwanamke siku za kutengwa kwake? Wanadamu wanalitiaje unajisi jina la Mungu? Kwa nini mwanadamu hawezi kulisafisha jina la Bwana lililotiwa unajisi? Mungu anaondoaje moyo wa jiwe ulio ndani ya mwanadamu na kuweka moyo wa nyama?


MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 37:1-28

 1. Kwamba mifupa mikavu sana yaweza kuishi hakika hilo ni Mungu peke yake anayejua. Je Mungu anao uwezo wa kugeuza maisha yako yanayoonekana kufanana na mifupa mikavu sana? Kama maisha yaliyopoteza thamani yanaweza kurejea unafanya nini kuwasaidia wenye changamoto hizo?
 2. Jinsi Roho Mtakatifu anavyobadilisha maisha ya watu ni muujiza mkubwa. Je unamfahamu aliyekuwa mtumwa wa dhambi ambaye sasa amefunguliwa na Mungu? Kwa nini Ezekieli alipoulizwa mifupa yaweza kuishi hakujibu haiwezi bali lisema yeye Mungu anajua?
 3. Kutoa unabii kunahusika kutoa habari njema kwa waliokata tamaa. Je, ni mara ngapi umewatolea watu unabii wa matumaini? Je, Mungu anapofanya agano la milele na watu wake anafanya hivyo kwa kuvutiwa na utii wao au kwa kuzingatia uaminifu wake?

 
MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 38:1-23

 1. Jitihada za kuhujumu mpango wa wokovu zinaonekana kupitia hila za Shetani ambazo hapa zinawakilishwa na ushirika wa Gogu. Mara ngapi umekutana na hali ya kukatishwa tamaa baada ya Mungu kukutendea muujiza fulani wa kushinda dhambi wakitaka ionekane ulikosea kuchukua uamuzi wa kuacha dhambi?
 2. Je wachanga wa imani wanapaswa kulindwa na mashambulizi kutoka kwa mawakala wa Shetani waliowatumikia mwanzo kwa kiasi gani? Je kwa kuwa mtu amebatizwa hiyo ni sababu tosha ya kujiridhisha kuwa hawezi kuanguka dhambini?
 3. Je uasi wa Shetani na nia yake ovu ya kutaka kupambana na Mungu inaweza kuwa imesaidia wema wa Mungu kuonekana dhahiri zaidi na hivyo kumpatia utukufu? Je unadhani ni rahisi kshindana na Mungu na wale walio upande wake?


MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 39:1-29

 1. Kuna nini katika Jina la Mungu ambalo linafanya Mungu atumie nguvu kubwa kulipigania? (Ezekieli 39:7; Matendo 4:12). Kwa muda mrefu dunia kupitia tawala zake mbalimbali zimekuwa na kigugumizi katika kumtambua Mungu wa Biblia kuwa ndiye mkuu wa viumbe vyote na mwenye mamlaka. Unadhani kigugumizi hiki kinatokana na Mungu kushindwa kujitambulisha vyema kwao au ni kutokana na upinzani unaochochewa na Shetani? Je kuwaadhibu wasiomtambua kumesaidia lolote kuwatambulisha kuwa yeye ndiye mkuu? Je kuna gharama inayoandamana na kujenga jina zuri katika jamii? Kwa nini mtunga Zaburi anatushauri kuchagua jina jema kuliko mali? (Methali 22:1).
 2. Mungu anaahidi kuwahurumia nyumba yote ya Israeli kwa kuwa aliwaadhibu kwa sababu ya makosa yao na si kwa kuwa alikuwa hawapendi. Je kuna wakati umewahi kudhania Mungu hakupendi kwa kuwa aliruhusu ukutwe na mambo magumu? Unawezaje kuutambua upendo wa Mungu unapokuwa kwenye dhiki? Mungu anaahidi kutowaficha tena uso wake watu aliowakomboa maana amemwaga roho yake juu yao. Je ahadi hiyo ni ya hakika kiasi gani? Kwa nini kumwaga roho kuwe hakikisho la Mungu la kutowaadhibu tena aliowakomboa? Je ni kwa nini Ezekieli 39:29 inaonekana kutoa ujumbe tofauti na Isaya 59:1-2? Je wenye dhambi wana tumaini la kupona ikiwa Mungu atauwa akijificha uso wake wasimuone?
 3. Je utumwa wa wana wa Israeli ulikuwa na faida yoyote kwao, kwa mataifa yaliyowatawala, na kwa Mungu? Je, Mungu aliutumia utumwa wa Waisraeli kama darasa la kufundishia ubaya wa dhambi na mpango wa wokovu? Kwa nini kuoondoa dhambi kumegharimu maisha ya watu na hata watoto ambao hawakuwa na hatia? Je Mungu hakuwa na namna nyingine iliyo bora zaidi ya kuikabili dhambi na Shetani ila kwa njia ya kuwaadhibu wanaoikumbatia? Kama Shetani amemuingiza Mungu gharama kubwa ya kumfanya asieleweke na viumbe wake unadhani ni adhabu gani hasa ingemstahili Shetani kwa ubaya aliomtendea Mungu? Je kuchomwa moto kunatosha?


MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 40:1-40

 1. Katika kuturejeshea utukufu uliopotea kwa sababu ya dhambi Mungu anahusisha wokovu huo na huduma za hekalu la hapa duniani na huduma za hekalu lililopo mbinguni. Huduma ya hekalu imefanikishaje mpango wa wokovu? Je, huduma ya hekalu iliyoandamana na uchinjaji wanyama wasio na hatia ilikuwa na ulazima wowote? Umakini wa vipimo katika ujenzi wa hekalu ulilenga kutufundisha nini? Je, ujenzi wa nyumba zetu za ibada unapaswa kufuata vipimo hivyo?
 2. Yule ambaye kuonekana kwake kulikuwa kama shaba ni nani? Je ana uhusiano wowote na yule anayeelezwa kwenye Ufunuo 1:12-16? Kwa nini Yeye ndiye anayefanya shughuli zote za upimaji na Ezekieli anabakia kuwa kama mtazamaji? Katika kutafuta suluhisho la dhambi ni nani kati ya Mungu na mwanadamu anayeshughulika zaidi? Kati ya mgonjwa aliyelazwa na wahudumu wa hospitali ni nani zaidi anayeshughulika na ugonjwa? Kuna namna ambayo mgonjwa anaweza kuchelewesha uponyaji kwa kuingilia au kutozingatia taratibu za matibabu alizopewa?
 3. Je kuna umuhimu wowote leo kujifunza huduma za hekalu la hapa duniani kama njia ya kutambua kile kinachoendelea kwenye hekalu la mbinguni na kama sehemu ya maandalizi ya wokovu wetu? Yesu anafanya nini sasa katika hekalu la mbinguni? (Waebrania 9:11-15). Unadhani kwenye hekalu la mbinguni ndiko inakofanyika hukumu ya wanadamu? (Danieli 7:9-14)

 
MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 41:1-26

 1. Ujenzi wa hekalu la Agano la Kale ulizingatia vipimo maalum na kuwepo kwa samani maalum ndani yake. Je, miili yetu ambayo pia ni hekalu la Roho Mtakatifu inazingatia mambo hayo? Kwa muktadha wa hekalu unadhani ni kwa nini Biblia inasisitiza kulinda moyo wako? 6(Methali 4:23).
 2. Je katika Agano Jipya Mungu ameagiza ujenzi wowote wa nyumba za ibada unaofanana na ujenzi wa hekalu la Agano la Kale? Je hekalu la mfano wa lile la Agano la Kale linapatikana wapi na tunalifikiaje? (Waebrania 4:16).
 3. Huduma katika hekalu la mbinguni ilianza lini na kwa nini? Makuhani na Kuhani Mkuu katika hekalu hilo ni nani na wanatoka katika kabila gani? (Waebrania 7:14). Je kudhani kuwa wanawake hawawezi kuwa makuhani ni dhana inayotokana na kuyaelewa Maandiko au kutoyaelewa Maandiko? (1Petro 2:9).


MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 42:1-20

 1. Makuhani wa Agano la Kale walikuwa na mavazi rasmi ya kuvaa walipokuwa wanahudumu hekaluni. Wahudumu wa Agano Jipya wanayo mavazi maalum ya kuhudumia yaliyotengenezwa kwa ajili hiyo?
 2. Je kuna umuhimu wa kuwa nadhifu na kuvalia vizuri unapotoa huduma za kiroho leo?


MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 43:1-27

 1. Kuna ulinganifu kati ya utukufu wa Mungu wa Israeli unaotokea Mashariki na wingu la utukufu litakalotokea Mashariki likimleta Mkombozi wa ulimwengu kwa ujio wake wa pili. Upande wa Mashariki una umuhimu gani katika mpango wa wokovu?
 2. Kwa nini wanyama waliotolewa kafara walitakiwa wawe wakamilifu? Tunaitoaje miili yetu iwe dhabihu kama Maandiko yanavyotuagiza? (Warumi 12:1).


MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 44:1-31

 1. Kwa nini wageni wasiotahiriwa hawakuruhusiwa kuingia kwenye nyumba ya Bwana? Je amri hiyo bado ina nguvu hata leo? (Matendo 21:28) Kutahiriwa kulisimama badala ya nini leo? Je kuzishika amri za Mungu kunaweza kuwa badala ya kutahiriwa leo? (1 Wakorintho 7:19).
 2. Kwa nini lango la Mashariki la hekalu lilifungwa? Mkuu anayetajwa hapa anayeruhusiwa kuketi ndani yake na kula chakula ni nani? Huo utukufu unaotajwa kuujaza nyumba ya Bwana ni nini? Mungu anaposema katika machukizo yenu yote iwatoshe anamaanisha nini? Kwa nini makuhani hawakuruhusiwa kunywa mvinyo? Je makasisi wa leo wamepata wapi kibali cha kunywa mvinyo?
 3. Kwa nini makuhani hawakuruhusiwa kuoa wajane na mke aliyeachwa? Je, sheria hiyo ingali bado ina nguvu hata leo? Kwa nini wageni wasio Waisraeli hawakuruhusiwa kuingia hekaluni?Vyakula vya malimbuko vilikuwa vinatolewa ili viliwe na makuhani. Je, sheria hiyo bado ingali inazingatiwa leo? Sadaka ya malimbuko inapewa msisitizo unaostahili leo?


MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 45:1-25

 1. Makosa na ujinga vilikuwa na namna ya kupatanishwa kwa Mungu katika huduma za hekalu la Agano la Kale. Makosa na ujinga vina nafasi gani ya kupatanishwa kwenye huduma ya hekalu la mbinguni?
 2. Idadi kubwa ya wanyama iliuawa kama fidia ya wenye dhambi walioungama kipindi cha Agano la Kale. Kwa nini wanyama hao hawaendelei kuuawa sasa kwa huduma hiyo? Je ilikuwa ni halali kwa wanyama hao kuuawa kwa kosa ambalo hawakulitenda? Je ilikuwa halali kwa Yesu kufa kwa ajili ya dhambi ambazo hakuzitenda?


MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 46:1-24

 1. Kuwa na utaratibu katika ibada ni jambo linalosisitizwa katika somo la leo (1Wakorintho 14:33, 40). Unadhani utaratibu unazingatiwa katika ibada unayofanya kwenye nyumba ya ibada mahali unapoabudu? Je kuwaelekeza watu (kuwapanga namna ya kukaa) kwenye nyumba ya ibada ni kuingilia uhuru wao au ni jambo linalokubalika na Mungu. 
 2. Je ni sahihi kuwa na utaratibu maalumu wa namna ya kutoka kwenye ibada kwa kufuata maelekezo ya Shemasi wa zamu? Na wale wanaosali kwenye eneo la wazi wanapaswa kufanya hivyo? Unadhani kipi ni sahihi kufuata chombo cha kukusanyia sadaka mbele au kuruhusu chombo kizunguke na kuwafikia watu mahali walipoketi?


MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 47:1-23

 1. Tunapokutana na changamoto Mungu ndiye anayetuvusha kwenye changamoto hizo. Je kuna wakati umehisi kuzingirwa na maji usiyoweza kuyavuka? Je umekumbuka kumshikilia Mungu ili akuvushe au umetegemea akili zako? Je mafuriko ya maji huleta baraka zozote kwa viumbe wengine wa Mungu?
 2. Kwa nini kwenye maziwa na matope maji hayawezi kuleta uponyaji? Je Mungu alikusudia majani ya miti yawe dawa kwa viumbe wengine na wanadamu? Kwa nini wageni watakaozalia Watoto katika Israeli walistahili kupewa urithi sawa na Waisraeli?


MASWALI YA KUJADILI: EZEKIELI 48:1-35:

 1. Utabiri wa Ezekiel haukutimia ingawa kwa sababu ya kuasi kwa Waisraeli lakini utatimia wakati Mungu atakapotupatia urithi sisi pamoja na wao katika makao ya mbinguni. Unajisikiaje unapoona maonyo au mahubiri yako hayapokelewi na matokeo yake hayaonekani mara moja?
 2. Unajisikiaje kuwa miongoni mwa makabila 12 ya Israeli? Unadhani kabila utakalopangiwa utakuwa unafanana nalo? Je wanadamu wote kuwa kwenye makabila 12 inamaanisha kuna tabia 12 tu zinazotofautisha wanadamu?
 3. Kwa nini Mungu anawagawia wanadamu urithi? Je kabla ya hapo wanadamu hawakuwa na urithi wowote? Je urithi huu unatokana na kile Yesu alichoshinda msalabani? Kuwepo kwa urithi huu kunakuongezea hamasa kiasi gani katika kumtumikia Mungu na wanadamu wenzako?