Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

WALEA PWEKE MAJASIRI

 

YESU MLEZI WA WALEA PWEKE

Idadi ya wazazi (hasa wa kike) wanaolazimika kulea watoto wao au wa wenzao wakiwa peke yao inazidi kuongezeka katika jamii nyingi. Hali hiyo imetokana na mzazi mmoja kumtelekeza mtoto aliyemzaa na mzazi mwenzake kwa kuwa hakuwa amejipanga kuoa au kuolewa, au kutokana na kubadilisha mawazo ya kuoa au kuolewa. Ulea pweke mwingine hutokea baada ya wazazi kuachana au mzazi mmojawapo kutorudi nyumbani baada ya kuwa amesafiri, amefungwa, amefariki, au kutofahamika kutokana na kubakwa au kutojulikana alipo. Tamari ni mfano wa mlea pweke aliyetelekezwa baada ya kubakwa. (2 Samweli 13:15) "Kisha Amnoni akamchukia machukio makuu sana; kwa kuwa machukio aliyomchukia yakawa makuu kuliko yale mapenzi aliyokuwa amempenda kwanza. Amnoni akamwambia, Ondoka, nenda zako."

Jihadhari na wanaume waharibifu

Ni kawaida kwa wanaume waharibifu wasio na lengo la kuoa kuwachukia wanawake waliowapa ujauzito. Ikiwa umemzalisha binti ingekuwa busara zaidi kama ungemuoa ili kupunguza idadi ya watoto wanaolelewa na mzazi mmoja. (Kutoka 22:16-17) "Mtu akimshawishi mwanamwali, aliyeposwa na mume, na kulala naye, lazima atatoa mahari kwa ajili yake ili awe mkewe. Ikiwa baba yake huyo mwanamwali akataa kabisa kumpa, atalipa fedha kama hesabu ya mahari ya mwanamwali ilivyo."

Wanauguza machungu

Maumivu wanayoachiwa walea pweke waliotelekezwa na watoto wanaolelewa na mzazi mmoja ni mazito sana kiasi kwamba wengine hudiriki kutowaambia watoto wao baba zao walipo hata kusingizia kuwa walikufa. Wanahangaika peke yao kuuguza na kusomesha watoto wakati mzazi wa mtoto akiendelea na maisha yake.

Mungu anakuona 

Hata hivyo ikiwa uliingilia ndoa ya mtu ukazalishwa na baadaye ukatelekezwa jipe moyo Mungu anakuona. Kama alivyomuonea huruma Hajiri nawe atakuhurumia na kukusaidia kukabili machungi yanayokusibu. (Mwanzo 16:6-11) "Naye Abramu akamwambia Sarai, Tazama, mjakazi wako yu mkononi mwako, mtendee lililo jema machoni pako. Sarai akamtesa, naye akakimbia kutoka mbele yake. Malaika wa BWANA akamwona kwenye chemchemi ya maji katika jangwa, chemchemi iliyoko katika njia ya kuendea Shuri. Akamwambia, Hajiri, wewe mjakazi wa Sarai, unatoka wapi, nawe unakwenda wapi? Akanena, Nakimbia mimi kutoka mbele ya bibi yangu Sarai. Malaika wa BWANA akamwambia, Rudi kwa bibi yako, ukanyenyekee chini ya mikono yake. Malaika wa BWANA akamwambia, Hakika nitauzidisha uzao wako, wala hautahesabika kwa jinsi utakavyokuwa mwingi. Malaika wa BWANA akamwambia, Tazama! Wewe una mimba, utazaa mwana wa kiume, nawe utamwita jina lake Ishmaeli, maana BWANA amesikia kilio cha mateso yako."

Mjulishe mwanao alipo baba yake

Na wala usiache kumjulisha mwanao baba yake ni nani na yupo wapi na kumtembelea anapoumwa na kushiriki mazishi yake siku atakayofariki hata kama alikuwa hahudumii mtoto. (Mwanzo 25:9) "Isaka na Ishmaeli wanawe wakamzika katika pango ya Makpela, katika shamba la Efroni bin Sohari Mhiti, lielekealo Mamre.”

Mimba zisizotarajiwa

Wengine mimba zisizotarajiwa walizozipata zilisababisha wapate matatizo wakati wa kujifungua, wafukuzwe shule ama wafukuzwe nyumbani na kutengea na jamii. Idara ya Huduma za familia iwatambue wazazi hawa na kuwahudumia majumbani na hasa kwenye mikutano ya kanisani na kwenye makambi. 

Wazee walioachiwa wajukuu

Walea pweke wengine ni wazee walioachiwa wajukuu na watoto wao waliokufa au waliokimbilia mjini kutafuta maisha. Hawa wana changamoto za kukosa mahitaji muhimu na malezi bora kwa vile ambavyo mababu na mabibi wengi hawana ukali unaotakiwa katika kuthibiti tabia za watoto. Wazee hawa wasiposaiduwa wanaweza kuzalisha watoto vibaka na malaya mtaani.

Kujibebesha najukumu ya baba

Walea pweke huitwa mashujaa kwa kuwa hujibebesha majukumu yote ya baba na mama wa mtoto. Inafahamika kuwa mchango aupatao mtoto kutoka kwa baba ni tofauti na ule aupatao kwa mama. 

Malezi ya mzazi mmoja hayatoshi

Na mara nyingi mtoto akosaye mchango wa malezi wa mmojawapo wa hao wazazi katika malezi mtoto huyo huathirika kitabia. Lakini wapo walea pweke waliofanya vizuri kwa malezi ya watoto wao. Mama Ben Carson ni mlea pweke aliyeweka juhudi ya kutosha katika kumtia moyo mwanae kufanya vizuri kimasomo. Leo hii Ben Carson ni mmoja wa madaktari bingwa wa upasuaji wa kichwa anayeheshimika sana duniani.

Mariamu alikuwa single parent

Mariamu mama yake Yesu ni mlea pweke mŵngine jasiri aliyemlea mwanae kwa uvumilivu mwingi. Alipoambiwa atazaa mtoto asiye na baba wa kibinadamu alipokea agizo hilo kwa imani. (Luka 1:30-38) “Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho. Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu. Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu. Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake.”

Changamoto za kulea peke yako

Alipokuwa wa makamo Yesu alitafutwa kwa siku tatu akakutwa akifundisha kwenye Sinagogi. Majibu yake yalimpa wakati mgumu mama yake Mariamu pengine na hata Yusufu. (Luka 2:48-51) “Na walipomwona walishangaa, na mama yake akamwambia, Mwanangu, mbona umetutenda hivi? Tazama, baba yako na mimi tulikuwa tukikutafuta kwa huzuni. Akawaambia, Kwani kunitafuta? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu? Nao hawakuelewa na neno hilo alilowaambia. Akashuka pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii; na mamaye aliyaweka hayo yote moyoni mwake.”

Kuoza mtoto

Wakati mwingine changamoto kwa walea pweke ni pale mtoto anapohitimu masomo au anapooa na kuolewa. Kukaa meza moja na mzazi mwenzako wakati mkewe au mumewe amekaa meza nyingine huleta mivutano inayoweza kuzua migogoro kwenye ndoa kama busara isipotumika.

Kujikimu kimaisha

Changamoto nyingine waipatayo walea pweke ni namna ya kujikimu kimaisha. Changamoto hii huwatokea pia wajane walioachiwa watoto na marehemu. (2 Wafalme 4:1) "Basi, mwanamke mmoja miongoni mwa wake za wana wa manabii alimlilia Elisha, akasema, Mtumishi wako mume wangu amekufa; nawe unajua ya kuwa mtumishi wako alikuwa mcha BWANA; na aliyemwia amekuja ili ajitwalie wana wangu wawili kuwa watumwa.” Mlea pweke katika mazingira haya asipokuwa jasiri vya kutosha anaweza kujikuta akijitumbukiza kwenye tabia mbaya ya kuomba omba au kujiuza ilia pate helaya kujikimu.

Matatizo ya kisaikolojia

Walea pweke wanasumbuliwa na matatizo ya kisaikolojia. Wanamini kutoolewa tena ni namna sahihi ya kukwepa kukutana na tabia za kikatili za wanaume. Maumivu waliyoyapitia ya kutelekezwa, kutendwa vibaya, kuachika au kufiwa yamewaachia majeraha yasiyopona. Lakini kwa kadri wanavyoshindwa kusamehe na kusahau yaliyopita ndivyo wanavyoshindwa kusonga mbele katika hatua nyingine ya Maisha. 

Wanaume wote hawafanani

Upo ukweli kuwa wanaume wana tabia nyingi wanazofanana zikiwepo za ukatili lakini si wote. Kuna uwezekano wa mlea pweke kuolewa tena na mwanaume asiye katili aliye tayari kulea watoto wa mwanaume mwingine na atakayempenda kwa dhati. Mlea pweke hasa kama umri unamruhusu asijikatie tamaa bali ajiweke kwenye soko la kuolewa. Kosa moja linaloweza kufanywa na mlea pweke ni la kuendelea kuongeza watoto wenye baba wasio na mpango wa kuoa. Kwa kadri idadi ya watoto inavyokuwa kubwa ndivyo inavyopunguza uwezekano wa yeye kuoa au kuolewa.

Haki sawa

Katika nyakati hizi tunazoishi kumeibuka vuguvugu la wanawake wanaodai haki sawa kwa mtazamo wa kidunia ambao waechagua kuwa walea pweke ili kuepuka adha za wanaume wa kwenye ndoa. Hawa wanawahimiza wanawake wasomi au wanaojimudu kiuchumi kutoolewa kabisa bali kutafuta Maisha yao wenyewe yasiyo ya kutawaliwa na mume. Kanisa lisikubali kuingizwa kwenye mtego huu. Dunia ikijaa familia za walea pweke madhara yake kwa jamii yatakuwa yasiyobebeka. Maisha ya kulea pweke hutokea katika mazingira ya ajali za Maisha na si kwa kujitakia. Upweke anaoupata mtoto kwa kukosa mzazi mmoja humfanya ajisikie mnyonge na kuathiri makuzi yake na hali huwa mbaya zaidi kwake anapotambua mzazi wake yupo mahali Fulani lakini kutokana na maamuzi ya mama au baba amezuia asiwasiliane naye.

Ongezeko la Walea pweke

Ukizingatia manyanyaso ya wanaume kwenye ndoa na ongezeko la idadi ya wanawake na hasa wenye uwezo wa kiuchumi hali hii inaweza kuongezeka katika siku zijazo. Kanisa na wazazi na idara ya familia wana wajibu wa kulitupia jicho jambo hili na kulitafutia ufumbuzi. Kanisa liwasaidie walea pweke kukamilisha mchakato wa machungu yaliyowakuta wakati wa kuachana au kufiwa na wenzi wao wa Maisha hadi waikubali hali hiyo na kuendelea na Maisha.