YESU MLEZI WA WAGANE NA WAJANE
Wajane, wagane, na yatima ni makundi mengine yanayojisikia kutengwa na jamii, kutengwa na kanisa, na kutengwa na familia zao, na ambayo kanisa ni lazima lifanye jitihada ya kuyafikia na kuyahudumia. Wajane ni wanawake waliofiwa na waume zao wakati wagane ni wanaume waliofiwa na wake zao. Mungu anaagiza kuwahudumia wajane. (Yakobo 1:27) “Dini iliyo safi, isiyo na taka mbele za Mungu Baba ni hii, Kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao, na kujilinda na dunia pasipo mawaa.”
Kwa bahati mbaya katika nyakati za kanisa la awali kuwahudumia wajane kulisahauliwa kabisa. “Hata siku zile wanafunzi walipokuwa wakiongezeka hesabu yao, palikuwa na manung'uniko ya Wayahudi wa Kiyunani juu ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahauliwa katika huduma ya kila siku.” (Matendo 6:1). Hali hiyo haina tofauti sana na hali ilivyo leo. Kilio cha wajane kusahauliwa hata leo kipo. Wanasahauliwa kutembelewa, kuombewa, kutambuliwa na wanasahauliwa hata kupewa mkufunzi wao katika vipindi vya familia makanisani na kwenye makambi.
Wajane wasio wazee waolewe
Makanisa yaainishe idadi na orodha ya wajane walionao wakiwapanga wale wenye uwezekano wa kuolewa tena na wale ambao umri umepita, na kuwahimiza wale wafaao kuoa na kuolewa kufanya hivyo. Wajane wasiruhusu Maisha ya kuwa na wapenzi wanaowahudumia kisirisiri huku wakiwa na mahusiano ya kingono. (1 Timotheo 5:14-15) “Basi napenda wajane, ambao si wazee, waolewe, wazae watoto, wawe na madaraka ya nyumbani; ili wasimpe adui nafasi ya kulaumu. Kwa maana wengine wamekwisha kugeuka na kumfuata Shetani.”
Wajane watu wazima
Wajane watu wazima waendelee na maisha ya ujane na kuachana na wazo la kuolewa na kushughulikia zaidi malezi ya watoto na kuwasaidia wajane vijana. (1 Timotheo 5:9-10) “Mjane asiandikwe isipokuwa umri wake amepata miaka sitini; naye amekuwa mke wa mume mmoja; naye ameshuhudiwa kwa matendo mema; ikiwa amelea watoto, ikiwa amekaribisha wageni, ikiwa amewaosha watakatifu miguu, ikiwa amewasaidia wateswao, ikiwa amefuata kwa bidii kila tendo jema.”
Wajane wasio waaminifu
Baadhi ya wajane uaminifu wao umekuwa ukitiliwa shaka. Nyendo zao na wanaume wa watu au wavulana zimekuwa hazimtukuzi Mungu. Kutokana na hali yao hiyo wamewatia doa wajane wengine walio waaminifu waonekane pia kuwa wasioaminika na hata kufanya baadhi ya wanawake wawanyanyapae. (1 Timotheo 5:11-13) “Bali wajane walio vijana ukatae kuwaandika hao, maana, wakizidiwa na tamaa kinyume cha Kristo, wataka kuolewa; nao wana hukumu kwa kuwa wameiacha imani yao ya kwanza. Tena, pamoja na hayo, hujifunza kuwa wavivu, wakizunguka-zunguka nyumba kwa nyumba; wala si wavivu tu, lakini ni wachongezi na wadadisi, wakinena maneno yasiyowapasa.
Biblia inawataja wajane kama walioonesha kiwango cha juu cha imani na waliowategemeza watumishi wa Mungu. “Wala Eliya hakutumwa kwa mmojawapo, ila kwa mjane mmoja wa Sarepta katika nchi ya Sidoni.” (Luka 4:26). Hii inatupa picha kuwa licha ya kuondokewa na wenzi wao, wajane na wagane wanayo kazi ambayo Mungu angetaka waifanye. Wanatakiwa kujikita katika kufanya kazi zao za mikono kwa umakini na juhudi nyingi. Wengine katika kundi hili ni walioachika. Makanisa yenye uwezo yawatafute washauri nasaha watakaosaidiana na wakuu wa huduma za familia katika kuwashauri walioachika maana mara nyingi huwa katika hali ya msongo. Wasiposaidiwa vya kutosha hawa hufikia mahali hawataki tena kuoa wala kuolewa. Watoto wanaolelewa na wazazi wa aina hii wanakosa huduma muhimu ya baba. Hivyo walioachika wenye uwezo wa kuolewa wasikate tamaa wanaweza kuolewa tena.
Kanisa mahalia liwe na siku ya familia ambapo chakula kitaandaliwa kwa wote na zawadi kutolewa kwa makundi hayo maalumu na makundi mengine kanisani. Kanisa litambue familia zinazofanya vizuri kwa uinjilisti, na zifanye kila liwezekanalo kuwashirikisha katika huduma za kanisani kama kuongoza shule ya sabato na kadhalika. Kila familia iwekewe malengo ya kuongoa na utaratibu wa kutoa taarifa ya uinjilisti nyumbani. Familia zipange ziara za kutembelea maeneo mbalimbali yenye mandhari nzuri ili kubarizi na kujiburudisha. Kila mgeni aliye kwenye familia za Kiadventista afanyiwe kazi na kualikwa kanisani mara kwa mara. Hivyo ndivyo familia za kikristo zitakuwa vituo vya wokovu, mbingu ndogo, na kiwanda cha kutengenezea jamii iliyo bora.
Changamoto ya kuondokewa na mwenzi wa Maisha Miongoni mwa hasara kubwa ziwapatazo wanadamu ni kuondokewa na mtu wa karibu. Mke au mume ni mtu wa karibu ambaye kuondoka kwake kwa njia ya kifo huacha machungu na pengo lisilozibika. Jambo muhimu ambalo mjane au mgane hutakiwa kulifanya ni kukabili hali hiyo kwa ujasiri na mafanikio. Maumivu ya kufiwa humfanya mtu asiwe tayari kuipokea taarifa hiyo. Kukataa kupokea ukweli wa kufiwa ni hatua ya muda ya binadamu kujipanga katika kuikabili hali hiyo. Taratibu mtu hutoka katika hatua hiyo ya kutokubali kama amefiwa hadi kufikiwa hatua ya kukubali kabisa kuwa mtu wake wa muhimu ameondoka na Maisha ni lazima yaendelee.
Jitihada kubwa inatakiwa kuchukuliwa kuhakikisha aliyefiwa anakubali kuwa kifo kimetokea. Sababu za kwa nini Mungu aliruhusu kifo kitokee zaweza kuwa dhahiri au zenye utata lakini yote kwa yote ni muhimu kuamini kuwa Mungu alikuwa na sababu nzuri za kuruhusu kifo kitokee. (Warumi 8:28) “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.”
Changamoto kutoka kwa ndugu wa karibu
Pamoja na machungu ya kuondokewa na mwenzi wa maisha, mgane na mjane hukutana na machungu mengine yanayosababishwa na ndugu wa karibu au marehemu. Ndugu wa marehemu kutokana na uchungu wa kuondokewa na ndugu yao hupenda kuhusisha chanzo cha kifo na hila iliyofanywa na mjane au mgane aliyebaki. Wengine huenda mbali hata kumnyima mjane au mgane fursa ya kumzika mwenzi wake, na kumyima haki ya kulea watoto wake na haki ya kumiliki mali aliyochuma na marehemu. Katika hali hiyo wajane na wageni huachwa katika umaskini wa ghafla na upweke ambapo hata ndugu wa marehemu waliokuwa na mazoea ya kuwatembelea nyumbani kwao wakati wa uhai wa marehemu hukoma kufanya hivyo. Biblia inaagiza na kuonya juu ya tabia ya kutesa wajane. (Kutoka 22:22) “Usimtese mjane ye yote aliyefiwa na mumewe, wala mtoto yatima.”
Changamoto za malezi na mahitaji ya watoto
Watoto hupitia wakati mgumu wa mahitaji ambapo uwezo wa kuwahudumia hupungua na hata wengine kulazimika kukatiza masomo yao kwa kukosa ada ya shule na mahitaji mengine ya masomo. Hali kama hii ilimtokea mjane wa mtumishi mmoja wa Mungu. Marehemu mumewe, pengine kutokana na kujaribu kukidhi mahitaji ya maisha yaliyozidi kipato chao walilazimika kuazima fedha ambayo waliingiana mkataba kuwa isiporudishwa kwa wakati waliowekeana Watoto wa mtu yule wangeuzwa ili kurejesha fedha iliyokopwa. (2 Wafalme 4-7) “Basi, mwanamke mmoja miongoni mwa wake za wana wa manabii alimlilia Elisha, akasema, Mtumishi wako mume wangu amekufa; nawe unajua ya kuwa mtumishi wako alikuwa mcha Bwana; na aliyemwia amekuja ili ajitwalie wana wangu wawili kuwa watumwa. Elisha akamwambia, Nikufanyie nini? Niambie; una kitu gani nyumbani? Akasema, Mimi mjakazi wako sina kitu nyumbani, ila chupa ya mafuta. Akasema, Nenda, ukatake vyombo huko nje kwa jirani zako wote, vyombo vitupu; wala usitake vichache. Kisha uingie ndani, ukajifungie mlango wewe na wanao, ukavimiminie mafuta vyombo vile vyote; navyo vilivyojaa ukavitenge. Basi akamwacha, akajifungia mlango yeye na wanawe; hao wakamletea vile vyombo, na yeye akamimina. Ikawa, vilipokwisha kujaa vile vyombo, akamwambia mwanawe, Niletee tena chombo. Akamwambia, Hakuna tena chombo. Mafuta yakakoma. Ndipo akaja akamwambia yule mtu wa Mungu. Naye akasema, Enenda ukayauze mafuta haya, uilipe deni yako; nayo yaliyosalia uyatumie wewe na watoto wako.”
Changamoto za madeni
Hapa tunajifunza mambo kadhaa. Kwa kadri inavyowezekana tujiepushe na madeni yasiyo ya lazima au yenye masharti magumu. Laiti yule mume angejua kuwa Watoto wake wangeuzwa ili kulipia deni huenda asingekopa au asingekuwa tayari kuingia deni la masharti magumu kama lile. Na kama ni lazima kukopa basi ulipaji wake ufanyike mapema iwezekanavyo kuepuka kuliacha deni hilo kwa mjane au mgane.
Changamoto za kutokuwa na makazi na vyanzo vya kuaminika vya mapato
Namna nyingine ya kuhakikisha wanao na mke au mume wako hawaingii katika uhitaji mkubwa baada ya kuondoka kwako ni kuwaachia makazi ya uhakika na miradi au uwekezaji utakaoendelea kuwapatia mahitaji. Kila inapowezekana wekeza mapema wakati ukiwa hai maana hujui ni wakati gani uhai wako utakoma. (Mithali 24:27) “Tengeneza kazi yako huko nje, Jifanyizie kazi yako tayari shambani, Ukiisha, jenga nyumba yako.” Kila mume na mke ana wajibu wa kuitunza familia yake kwa kuipatia mahitaji ya lazima sasa na baada ya kufa kwake. (1 Timotheo 5:8) “Lakini mtu ye yote asiyewatunza walio wake, yaani, wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana Imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini.”
Changamoto za umiliki wa mali
Namna nyingine ya kuhakikisha usalama wa familia yako ni kuondoa uwezekano wa ndugu wa familia yako kujimilikisha mali zako baada ya kufa kwako kinyume cha ridhaa yako. Hiyo inawezekana kwa kuwajulisha mapema ndugu zako uhalali wa Watoto au mwenzi wako kumiliki mali ikiwa utatangulia kufa. Mali zako unazotaka ziendelee kumilikiwa na familia yako ziweke chini ya umiliki wa mwenzi wako na Watoto wako. Pale ambapo kuna hatari ya ndugu zako kujimilikisha mali za familia yako inashauriwa kuandika wosia. Wosia unaainisha mgawanyo wa mali ya familia pale utakapokufa. Baadhi ya watu waliopuuzia kuandika wosia, mali zao zilitapanywa na ndugu waliojimilikisha huku wakiwasahau wanufaikaji ambao ni wana familia.
Changamoto za kutoona fursa
Jambo jingine tunalojifunza katika kisa hiki ni kutumia fursa ili kujiongezea kipato kwa kuendesha miradi mbalimbali kulingana na mahitaji ya jamii inayokuzunguka. Mjane katika kisa hiki alitumia kile alichonacho kuzalisha mali alizotumia kuuza na kulipa deni. Alianza kwa kusita na kusema sina kitu isipokuwa chupa. Hakujua kuwa ile chupa ilikuwa fursa. Bidii ya kuazima vyombo na kuvijaza mafuta waliyoifanya wangeweza kuitumia kujipatia kipato kwa kubuni miradi ya mitaji midogo midogo hata kabla ya kupewa ushauri huo na nabii. Kuna wakati watu huweza kuingia kwenye uhitaji wakati wangeweza kuibadilisha hali hiyo kwa kushauriana na watu wengine juu ya namna ya kujinasua kwenye shida waliyonayo.
Changamoto za kukosa ushauri
Wakati mwingine kile wajane na wagane wanachohitaji ni ushauri wa namna ya kujinasua kwenye uhitaji na wala si fedha wala mali. Wajane waunde vikundi vya kushauriana juu ya ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili. Miongoni mwa mada za kujadili ni zile zinazohusu namna ya kuinua uchumi wao na namna ya kukidhi mahitaji na malezi ya Watoto wao. Wataalam na watu waliofanikiwa katika maeneo hayo waalikwe ili kutoa mad ana uzoefu wao.
Changamoto ya kukosa mshikamano na watoto
Wajane na wagane wawe na mshikamano na Watoto wao wakiweka wazi mbele yao changamoto zinazowakabili ili kushauriana nao juu ya njia zinazopendekezwa za kukabiliana nazo. Watoto wasichukuliwe kama wasioweza chochote. Wapewe majukumu kulingana na uwezo wao ili kuhakikisha wanashiriki katika mikakati ya kujinasua kiuchumi. Watoto wawe na miradi wanayoisimamia na tathmini ifanyike mara kwa mara ili kuwatia moyo na kuiboresha pale inapokuwa lazima. Bila jitihada kama hizi Watoto wa mjane au mgane wanaweza kuwa mzigo kwake na kwa jamii kwa kutafuta njia za mkato zisizo halali za kujipatia mahitaji yao.
Changamoto za kutokuwa na mahusiano na jirani
Mjane au mgane lazima awe na mahusiano mazuri na majirani, waumini wenzake na viongozi wake wa kiroho. Ajihusishe kwenye matukio ya furaha na huzuni yawapatayo majirani zake ili siku akifikwa na magumu awe na watu wanaoweza kumsaidia. Mjane huyu aliishi vizuri na majirani zake maana walikuwa tayari kumwazimisha vyombo vyao. Jenga mtandao mpana na watu wa aina mbalimbali unaoweza kuwategemea kama ndugu. Watu wanaoweza kukuombea kwa Mungu siku utakapopatwa na magumu. (Matendo 9:36-41) “Na mwanafunzi mmoja alikuwako Yafa, jina lake Tabitha, tafsiri yake ni Dorkasi (yaani paa); mwanamke huyu alikuwa amejaa matendo mema na sadaka alizozitoa. Ikawa siku zile akaugua, akafa; hata walipokwisha kumwosha, wakamweka orofani. Na kwa kuwa mji wa Lida ulikuwa karibu na Yafa, nao wanafunzi wamesikia ya kwamba Petro yuko huko, wakatuma watu wawili kwake, kumsihi na kusema, Usikawie kuja kwetu. Petro akaondoka akafuatana nao. Alipofika, wakampeleka juu orofani wajane wote wakasimama karibu naye, wakilia na kumwonyesha zile kanzu na nguo alizozishona Dorkasi wakati ule alipokuwa pamoja nao. Petro akawatoa nje wote, akapiga magoti, akaomba, kisha akaelekea yule maiti, akanena, Tabitha, ondoka. Naye akafumbua macho yake, na alipomwona Petro akajiinua, akaketi. Akampa mkono, akamwinua; hata akiisha kuwaita wale watakatifu na wajane akamweka mbele yao, hali yu hai.”
Changamoto za upweke
Njia mojawapo ya kujisahaulisha machungu ya kuondokewa na mwenzi wako wa maisha ni kufanya shughuli za kuisaidia jamii na wenye mahitaji. Baadhi ya vyanzo vinamtambulisha Tabitha kama mjane Tajiri. Ukweli kuwa alipofufuliwa alikabidhiwa kwa wajane unaonesha alikuwa na mahusiano mazuri na wajane. Kuna uwezekano kuwa ama aliwasaidia wajane au alishirikiana na wajane kuhudumia wenye mahitaji. Wajane wanaweza kujiundia vikundi vya kusaidia yatima au wahitaji kutokana na vipato vyao au miradi yao.
Changamoto ya kukosa mahusiano na waumini
Mjane au mgane anapaswa kuimarisha mahusiano na waumini wenzake na viongozi wake wa kiroho. Atumie muda wa kutosha kwa shughuli za kiroho akijiweka karibu Zaidi na Mungu. Biblia inamtaja mjane wa miaka 84 aliyedumu hekaluni akiomba. Mwanamke huyu muombaji alibahatika kuonana na mtoto Yesu aliyeletwa hekaluni ili abarikiwe. Moyo wake ulifarijika kupata fursa ya kumuona Masihi aliyekuwa anatazamiwa na taifa zima la Israeli. (Luka 2:37) “Palikuwa na nabii mke, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila ya Asheri, na umri wake ulikuwa miaka mingi, alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya uanawali wake. Naye ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na mchana kwa kufunga na kuomba. Huyu alitokea saa ile ile akamshukuru Mungu, na wote waliokuwa wakiutarajia ukombozi katika Yerusalemu akawatolea habari zake.”
Changamoto ya kutojiunga na vikundi vya kijamii
Mjane au mgane asiache kujihusisha na vyama vya wanaume na wanawake wenzake au vikundi vya uimbaji ili karama zake zikaendelee kutumika. Muda anaotumia kushirikiana na wenzake unapunguza upweke na muda wa kufikiria uchungu wa kuondokewa na mwenzi wake. Hiyo itamsaidia kurejea hatua kwa hatua kwenye Maisha ya kawaida na kujiona mtu muhimu na anayethaminiwa. Mjane asiridhike kushiriki shughuli za kiroho na wenzake bali ahakikishe anatumia mud ana mali zake katika kuitegemeza kazi ya Mungu.
Changamoto ya kutokuwa wakili mwaminifu
“Naye akaketi kulielekea sanduku la hazina, akatazama jinsi mkutano watiavyo mapesa katika sanduku. Matajiri wengi wakatia mengi. Akaja mwanamke mmoja, mjane, maskini, akatia senti mbili, kiasi cha nusu pesa. Akawaita wanafunzi wake, akawaambia, Amin, nawaambia, Huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina; maana hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndiyo riziki yake yote pia.” (Marko 12:41-44) Mjane huyu ingawa alikuwa maskini alijizoeza kumtolea Mungu mali zake kwa uaminifu. Hakujifariji kwamba kwa kuwa ni maskini basi asitoe sadaka ili kuitegemeza kazi ya Mungu. Alitoa chote alichonacho akiamini kuwa Mungu atamrudishia maradufu. (Luka 12:33) “Viuzeni mlivyo navyo, mtoe sadaka. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, akiba isiyopungua katika mbingu, mahali pasipokaribia mwivi, wala nondo haharibu.” Wajane wana asili ya utoaji kwa kupitia utoaji huo wameshuhudia uwezo wa Mungu ukiwaruzuku pale wanapopungukiwa.
Changamoto za kunyanyapaliwa
Wajane na wagane hukabiliwa na changamoto za upweke si tu kwa ajili ya kuondokewa na wenzi wao wa Maisha bali pia kutokana na ndugu na majirani zao kuwanyanyapaa. Kunyanyapaa huku hutokana na dhana potofu kuwa huenda walihusika na vifo vya wenzi wao kwa kuwaambukiza magonjwa au kuwadhuru kwa nia ya kutaka kurithi mali. Wakati mwingine hunyanyapaliwa kwa kuhofia kuwa kuzoeana nao kwaweza kusababishwa kuombwa misaada au kushawishiwa kuingizwa kwenye mahusiano ya ngono. Ka hali hiyo mjane aliyedhamiria kubaki katika ujane anapaswa kuwa mtu wa maombi. (1 Timotheo 5:5) “Basi yeye aliye mjane kweli kweli, ameachwa peke yake, huyo amemwekea Mungu tumaini lake, naye hudumu katika maombi na sala mchana na usiku.” Wajane na wagane wanaweza kuunda ushirika wa kuombeana na kuomba Pamoja ili kuimarishana na kutiana nguvu.
Changamoto ya kutoshirikiana na viongozi wa kiroho
Wajane na wageni wasiache kuwaona viongozi wa kiroho kwa ajili ya changamoto zinazohitaji ushauri na msaada wa mali. (2 Wafalme 4:1) “Basi, mwanamke mmoja miongoni mwa wake za wana wa manabii alimlilia Elisha, akasema, Mtumishi wako mume wangu amekufa; nawe unajua ya kuwa mtumishi wako alikuwa mcha Bwana; na aliyemwia amekuja ili ajitwalie wana wangu wawili kuwa watumwa.” Viongozi nao kwa upande wao wasiwasahau wajane kama walivyofanya viongozi wa kanisa la awali. (Yakobo 1:27) “Dini iliyo safi, isiyo na taka mbele za Mungu Baba ni hii, Kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao, na kujilinda na dunia pasipo mawaa.”
Changamoto ya kusahauliwa kwenye mipango ya kanisa
Viongozi wa kanisa wasirudie kosa la kuwasahau wajane kwenye huduma zinazopangwa kwa ajili ya washiriki wake. (Matendo ya Mitume 6:1) “Hata siku zile wanafunzi walipokuwa wakiongezeka hesabu yao, palikuwa na manung'uniko ya Wayahudi wa Kiyunani juu ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahauliwa katika huduma ya kila siku.” Wakati wa mafunzo ya familia wajane wapewe wakufunzi wao wanaojua changamoto zao na uzoefu wao watakaojadili nao mada zinazowahusu. Kuwachanganya wajane na wagane kwenye madarasa ya wanandoa ambako mambo ya unyumba yanachukua nafasi kubwa ya majadiliano ni kutowatendea haki. Tena wajane na yatima wangepaswa kuhudumiwa kama kundi maalumu sawa na wageni wengine wa kambi kwenye sikukuu za vibanda kama Maandiko yasemavyo. (Kumbukumbu la Torati 16:11) “Nawe utafurahi mbele ya Bwana, Mungu wako, wewe na mwana wako na binti yako, na mtumwa wako na mjakazi wako, na Mlawi aliye ndani ya malango yako, na mgeni, na yatima, na mjane aliyefiliwa na mumewe, walio katikati yako, katika mahali atakapochagua Bwana, Mungu wako, apakalishe jina lake.”
Changamoto ya kukosa walezi kanisani
Katika kanisa ni muhimu ifahamike wajane wanakuwa chini ya mwavuli wa idara gani kama ni mashemasi, idara ya wanawake au Huduma binafsi. Mwanzoni mwa mwaka wajane na wagane wapangiwe bajeti yao kwa ajili ya mikutano yao na shughuli za ujasiriamali na miradi mingine. Wazee wa kanisa na mashemasi waweke utaratibu unaotambulika wa kuwatembelea wajane na kuwatia nguvu. Katika ziara hizo wapokee kero na malalamiko ya wajane na wageni na kuyatendea kazi. Ikiwa mjane au mgane amedhulumiwa haki zake na ndugu wa marehemu au ananyanyaswa kingono viongozi hao waone namna ya kumsaidia. Ikiwa mjane ana Watoto watukutu wasiomsikiliza viongozi waone namna ya kuwasaidia Watoto hao pia. Viongozi wasisite kuwachukulia hatua waumini wanaodhulumu wajane na wagane. (Kumbukumbu la Torati 27:19) “Na alaaniwe apotoaye hukumu ya mgeni, na yatima, na mjane aliyefiliwa na mumewe. Na watu wote waseme, Amina.”
Changamoto ya kutotembelewa
Tahadhari kubwa ichukuliwe ili katika kutembelea wajane kusiibuke lawama au tuhuma za mjane kutotendewa inavyostahili na viongozi hao wa kiroho. (Mathayo 23:14) “Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnakula nyumba za wajane, na kwa unafiki mnasali sala ndefu; kwa hiyo mtapata hukumu iliyo kubwa zaidi. Viongozi wasijinufaishe kwa mali za wajane na wagane. Wasitumie hali yao ya uhitaji na upweke kujenga nao mahusiano yasiyofaa. Pale inapokuwa lazima kuwatembelea wajane na wagane, utembeleaji huo usiwe mzigo kwao wala usiwe na masharti na mzee wa kanisa au mzee asitembelee akiwa peke yake. Aambatane na watu wawili ili kuondoa hisia kuwa wana mahusiano yasiyofaa. (2 Wakorintho 6:3) “Tusiwe kwazo la namna yo yote katika jambo lo lote, ili utumishi wetu usilaumiwe.”
Changamoto ya kutovitumia vyombo vya kisheria kudai haki
Wajane na wagane wanapaswa kutoendelea kulia kwa ajili ya dhuluma na unyanyasaji wanaofanyiwa badala yake wachukue hatua ya kutafuta haki yao kwa bidii kupitia vyombo vya kutoa haki. (Luka 18:1-5) “Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa. Akasema, Palikuwa na kadhi katika mji fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu. Na katika mji huo palikuwa na mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendea-endea, akisema, Nipatie haki na adui wangu. Naye kwa muda alikataa; halafu akasema moyoni mwake, Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu, lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima.”
Changamoto ya kutoshirikisha mashirika ya msaada
Haki hudaiwa haitolewi kama zawadi. Wajane wengine kwa sababu ya kutojua sheria wamejikuta wakikosa haki zao. Kila inapowezekana wajane na wagane wawaone watu wa ustawi wa jamii au NGO zinazojishughulisha kuwasaidia wasio na uwezo au wanaoonewa katika jamii kupata haki zao. Mungu ana Habari njema kwa mashirika hayo yasiyo ya kiserikali yanayosimamia haki za yatima na watoto. (Isaya 1:17) “Jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane.” Na kwa mahakimu na wanaosimamia haki za watu wanatahadharishwa kutowaonea wajane na yatima. (Yeremia 22:3) “Bwana asema hivi, Fanyeni hukumu na haki, mkamtoe yeye aliyetekwa katika mikono ya mdhalimu; wala msiwatende mabaya mgeni, wala yatima, wala mjane, wala kuwadhulumu, wala msimwage damu ya mtu asiye na hatia katika mahali hapa.”
Changamoto ya wasimamizi wa mirathi
Kwenye usimamizi wa mirathi baadhi ya ndugu wa marehemu na wasimamizi wa mirathi wamekuwa vikwazo katika upatikanaji wa mirathi hiyo. Hapa panahitaji ustahimilivu mwingi maana wengine wamechukua hadi miaka 20 kupata mirathi yao. Wajane na wagane wawe watu wasiokata tamaa katika kutafuta haki zao. Ustawi wao na wa Watoto wao unategemea mali hiyo. Wasimame kidete haki hiyo. Ikiwa wanaoletavikwazo ni waumini wa kanisa uongozi wa kanisa ujulishwe ili uone namna kuingilia kati jambo hilo. Mungu anawaonya wanaowanyanyasa wajane waache kufanya hivyo. (Kutoka 22:22) “Usimtese mjane ye yote aliyefiwa na mumewe, wala mtoto yatima.”
Changamoto ya kusimamia haki za watoto
Wajane na wagane wasisite kuwaona viongozi wa serikali au wa kijamii katika kusimamia haki za Watoto wao. Haki hizo zaweza kuwa haki za kupata elimu au matibabu kwa Watoto wao walioikosa huduma hizo kutokana nakutokuwa na uwezo wa kiuchumi. (2 Samweli 14:4-10) “Naye yule mwanamke wa Tekoa aliponena na mfalme, akaanguka kifulifuli chini, akamsujudia, akasema, Nisaidie, Ee mfalme. Mfalme akamwuliza, Una nini? Naye akajibu, Hakika ni mjane mimi, niliyefiwa na mume wangu. Nami mjakazi wako nalikuwa na wana wawili, na hao wawili wa kashindana uwandani, wala hapakuwa na mtu wa kuwaamua, lakini mmoja akampiga mwenzake, akamwua. Na tazama, jamaa yote wameniinukia mimi mjakazi wako, wakasema, Mtoe yule aliyempiga nduguye, ili tupate kumwua yeye kwa maisha ya nduguye aliyemwua, hata na kumfisha mrithi pia; ndivyo watakavyolizima kaa langu lililobaki, wasimwachie mume wangu jina wala masalio usoni pa nchi. Mfalme akamwambia huyo mwanamke, Nenda nyumbani kwako, nami nitakufanyia agizo. Ndipo huyo mwanamke wa Tekoa akamwambia mfalme, Na uwe juu yangu, Ee bwana wangu mfalme, na juu ya nyumba ya baba yangu uovu huu; wala kwa mfalme na kwa kiti chake cha enzi pasiwepo hatia. Mfalme akasema, Ye yote atakaye kuambia neno, mlete kwangu, naye hatakugusa tena.” Kanisa mahalia laweza pia kuwanunulia wajane na yatima kazi za bima ya afya ili kuwawezesha kutibiwa hata kama hawana fedha.
Changamoto ya kutoamini ahadi za Mungu
Mungu anawafikiria sana wajane kutokana na magumu wanayoyapitia. Mjane wa Sarepta alikuwa anakaribia kuishiwa akiba yake ya chakula hivyo akamtuma Eliya amtembelee ili kama atashinda mtihani wa Imani apewe chakula cha kumtosha kwa muda mrefu. Mjane huyu alishinda mtihani aliowekewa wa kumkarimu mtumishi wa Mungu. Mjane yule alitoa chakula alichonacho kwa mgeni kwa imani na chakula chake hakikupungua kwenye chombo alichohifadhia. (1Wafalme 17:11-16) “Alipokuwa akienda kuleta, akamwita akasema, Niletee, nakuomba, kipande cha mkate mkononi mwako. Naye akasema, Kama Bwana, Mungu wako, aishivyo, sina mkate, ila konzi ya unga katika pipa, na mafuta kidogo katika chupa; nami ninaokota kuni mbili ili niingie nijipikie nafsi yangu na mwanangu, tuule tukafe. Eliya akamwambia, Usiogope; enenda ukafanye kama ulivyosema; lakini unifanyie kwanza mkate mdogo ukaniletee; kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao. Kwa kuwa Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Lile pipa la unga halitapunguka, wala ile chupa ya mafuta haitaisha, hata siku ile Bwana atakapoleta mvua juu ya nchi. Basi akaenda, akafanya kama alivyosema Eliya; na yeye mwenyewe, na Eliya, na nyumba yake, wakala siku nyingi. Lile pipa la unga halikupunguka, wala ile chupa ya mafuta haikuisha, sawasawa na neno la Bwana alilolinena kwa kinywa cha Eliya.”
Mungu anajali shida zinazowakabili wajane na wagane siku kwa siku na anatamani wajue kuwa anazijua na anazishughulikia. (1 Petro 5:6-7) “Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake; huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.” Hajawahi kuwaacha wala hana mpango wa kuwaacha. (Waebrania 13:5) “Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa.”
Mama mmoja mjane wa mji wa Naini alikuwa amefiwa na mumewe na kubaki na kijana wake pekee wa kiume. Baadaye kijana huyu naye akafa, jambo hili lilileta uchungu mkubwa kwa mjane huyu na jamii ya watu waliomzunguka. Aliona giza tupu kwa Maisha yake ya usoni kiasi ambacho Yesu aliguswa. Siku ya msiba wa kijana huyu Yesu akafunga safari kuelekea mji huo ili akakutane na mjane yule na kumpa faraja. (Luka 7:11-17) “Baadaye kidogo alikwenda mpaka mji mmoja uitwao Naini, na wanafunzi wake walifuatana naye pamoja na mkutano mkubwa. Na alipolikaribia lango la mji, hapo palikuwa na maiti anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa mjini wengi walikuwa pamoja naye. Bwana alipomwona alimwonea huruma, akamwambia, Usilie. Akakaribia, akaligusa jeneza; wale waliokuwa wakilichukua wakasimama. Akasema, Kijana, nakuambia, Inuka. Yule maiti akainuka, akaketi, akaanza kusema. Akampa mama yake. Hofu ikawashika wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, Nabii mkuu ametokea kwetu; na, Mungu amewaangalia watu wake. Habari hii yake ikaenea katika Uyahudi wote, na katika nchi zote za kando kando.”
Hata leo Yesu anatamani kuja kufufua matumaini ya mjane au mgane fulani aliyekata tamaa. Kama alimfufua kijana aliyekufa hatashindwa kutatua changamoto za mjane au mgane. Yesu aweza kumpatia mjane na mgane mwenzi mwingine wa Maisha ikiwa umri wake unamruhusu kufanya hivyo. Katika kuoa au kuolewa kwao wajane na wagane wamshirikishe Mungu. (Mithali 19:14) “Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa babaye; Bali mke mwenye busara, mtu hupewa na Bwana.” Kwa kadri inavyowezekana wagane waoe wajane kwa kuwa wana uzoefu unaofanana. Tena inashauriwa wagane wasioe mabinti wadogo waliowazidi umri sana. Tofauti kubwa ya umri yaweza kuwa chanzo cha changamoto za kiafya au kukosa uaminifu wa ndoa.
Changamoto ya kuoa na kuolewa tena
Ni vibaya kujizuia kutoolewa wakati unahitaji mwenzi wa maisha. (1 Timotheo 5:14) Basi napenda wajane, ambao si wazee, waolewe, wazae watoto, wawe na madaraka ya nyumbani; ili wasimpe adui nafasi ya kulaumu.” Wajane na wagane wengine wamempa adui nafasi ya kulaumu. Wamekosa uaminifu na kuwa na tabia ya umalaya. Yesu ana ushauri kwa wagane. (1 Wakorintho 7:9) “Lakini ikiwa hawawezi kujizuia, na waoe; maana ni afadhali kuoa kuliko kuwaka tamaa.” Watoto wasijitwalie mamlaka ya kuwaamulia wazazi wao wasioe au wasiolewe. Wanaume huonekana kutostahimili kukaa peke yao kwa muda mrefu baada kufiwa na wake zao. Hii kwa sehemu kubwa inatokana na kushindwa kustahimili kuishi peke yao. Ikiwa itaonekana hali ya mgane inazorota ni afadhali kumshauri kuoa na kumsaidia katika katika uchakataji wa jambo hilo.
Mjane anapoolewa hulazimika kutoka kwa nyumba aliyojenga na marehemu mume wake. Jambo hilo kwa wengine huwa kikwazo cha kuolewa. Hali ni hiyo hiyo pia kwa wagane. Hulazimika kuhamia nyumba nyingine au Kwenda kupanga. Kwa wale wajane na wageni ambao umri umeenda sana wanashauriwa kutojishughulisha na kuoa au kuolewa. (1 Wakorintho 7:8) “Lakini nawaambia wale wasiooa bado, na wajane, Ni heri wakae kama mimi nilivyo.
Neno la mwisho ni hili wajane wanatakiwa kumtumaini Mungu. Mmungu anawajali na Mungu atawasaidia katika changamoto zao zote. (Yeremia 49:11) “Waache watoto wako wasio na baba, mimi nitawahifadhi hai, na wajane wako na wanitumaini mimi.” Yeye ni baba wa yatima wote na mtetezi wa wajane. (Zaburi 68:4-6) “Mwimbieni Mungu, lisifuni jina lake, Mtengenezeeni njia ya barabara, Apitaye majangwani kama mpanda farasi; Jina lake ni YAHU; shangilieni mbele zake. Baba wa yatima na mwamuzi wa wajane, Mungu katika kao lake takatifu. Mungu huwakalisha wapweke nyumbani; Huwatoa wafungwa wakae hali ya kufanikiwa; Bali wakaidi hukaa katika nchi kavu.”