Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

DINI MBILI KINZANI

Dini mbili kinzani zilianza mara tu baada ya anguko la dhambi. Dini moja ikiwakilisha mpango wa Mungu wa kuwaokoa wanadamu na dini ya pili ikiwakilisha dini iliyoundwa kimkakati kupinga, kudhoofisha na kuhujumu mpango wa kuwaokoa wanadamu. Wazo muhimu kulifahamu ni kuwa Mungu ameamuru tuokolewe na mkakati wowote wa kuzuia jambo hili haitafanikiwa. (Zaburi 71:3) “Uwe kwangu mwamba wa makazi yangu, Nitakakokwenda sikuzote. Umeamuru niokolewe, Ndiwe genge langu na ngome yangu.” (Yohana 10:28-29) “Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu. Baba yangu aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote; wala hakuna mtu awezaye kuwapokonya katika mkono wa Baba yangu.” (Waebrania 6:17-19) “Katika neno hilo Mungu, akitaka kuwaonyesha zaidi sana warithio ile ahadi, jinsi mashauri yake yasivyoweza kubadilika, alitia kiapo katikati; ili kwa vitu viwili visivyoweza kubadilika, ambavyo katika hivyo Mungu hawezi kusema uongo, tupate faraja iliyo imara, sisi tuliokimbilia kuyashika matumaini yale yawekwayo mbele yetu; tuliyo nayo kama nanga ya roho, yenye salama, yenye nguvu, yaingiayo hata mle mlimo ndani ya pazia.”

Mungu hakukurupuka katika kuweka mpango wa uumbaji wala haikutokea kama ajali kwamba mwanadamu awe mrithi wa ufalme wake. (Luka 12:32) “Msiogope, enyi kundi dogo; kwa kuwa Baba yenu ameona vema kuwapa ule ufalme.” Pamoja na udogo wetu na kutofaa kwetu ilimpendeza Mungu kutuchagua kuwa warithi wa ufalme wake tangu milele. (Warumi 8:29-30) “Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza.”

Ili tustahili kuwa warithi tulitakiwa tukidhi vigezo vya kuwa wana wa Mungu. kwanza ilipaswa tuumbwe kwa mfano na sura ya Mungu na ndivyo ilivyokuwa. (Mwanzo 1:26) “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.” Kuna mfanano ambao Mungu aliuweka kati yake na sisi ambao haupo kwa viumbe wengine wowote.

Adam and Eve had received endowments not unworthy of their high destiny. Graceful and symmetrical in form, regular and beautiful in feature, their countenances glowing with the tint of health and the light of joy and hope, they bore in outward resemblance the likeness of their Maker. Nor was this likeness manifest in the physical nature only. Every faculty of mind and soul reflected the Creator's glory. Endowed with high mental and spiritual gifts, Adam and Eve were made but "little lower than the angels" (Hebrews 2:7), that they might not only discern the wonders of the visible universe, but comprehend moral responsibilities and obligations.  {Ed 20.2} 

Kwa kadri walivyokuwa wakiendelea kuishi maisha matakatifu yasiyo na dhambi walizidi kudumisha sura na mfano wa Mungu na kudumisha nafasi yao kama wana wa Mungu. Baada ya wanadamu kushindwa kuishi maisha matakatifu yasiyo na dhambi kwa anguko la pale Edeni, walipoteza kwa kiwango kikubwa sura na mfano wa Mungu na kupoteza sifa ya kuwa wana wa Mungu. Mara tu baada ya anguko mpango ulioandaliwa tangu wakati wa kuwekwa misingi ya ulimwengu wa kuturejeshea hadhi ya kuwa wana wa Mungu ukaanza kufanya kazi. (Yohana 1:12-14) “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu. Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.”

Yesu alifanyika Mwana wa Mungu ili kuturejeshea sisi hadhi ya kuwa wana wa Mungu na kutustahilisha kuwa warithi wa ufalme. Hadhi hiyo tuliipoteza wazazi wetu wa kwanza walipoanguka dhambini. Warumi 8:15-17) “Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba. Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu; na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye.”

Mwanadamu aliyetenda dhambi anafananishwa na aliye uchi. (Ufunuo 3:17) “Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.” Yesu ana mpango wa kutufunika uchi wetu ili kutuepusha na aibu. (Ufunuo 3:18) “Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.” (2 Wakorintho 5:3) “Ikiwa tukiisha kuvikwa hatutaonekana tu uchi.”

Ilimlazimu Mungu kuchinja mnyama pale Edeni ili ipatikane ngozi ya kumtengenezea mwanadamu vazi la kumsetiri. (Mwanzo 3:21) “Bwana Mungu akawafanyia Adamu na mkewe mavazi ya ngozi, akawavika.” Mnyama aliyechinjwa Edeni alimwakilisha Kristo aliyechinjwa tangu milele ili atununulie wokovu wetu. Wokovu ulionunuliwa kwa ajili yetu ndiyo sababu kuu ya kumfanyia ibada.  (Ufunuo 5:9-10) “Nao waimba wimbo mpya wakisema, Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa, ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi.”

Yesu alichinjwa lini? Je alichinjwa siku ile mwanadamu alipotenda dhambi au siku aliyokufa msalabani? Yesu alichinjwa siku ile ilipoamuliwa kuwa angekuja kuwakomboa wanadamu. (Ufunuo wa Yohana 13:8) “Na watu wote wakaao juu ya nchi watamsujudu, kila ambaye jina lake halikuandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo, aliyechinjwa tangu kuwekwa misingi ya dunia.” Tangu alipoanza kuwepo Yesu amekuwa katika ufahamu kuwa siku moja atakufa kifo cha aibu kwa ajili ya wanadamu. Ndiyo maana Biblia inasema alichinjwa tanu kuwekwa kwa msingi wa dunia.

Kupitia kujitoa huko kwa Yesu Kristo Mungu alianzisha ibada ya kafara ili kuwakumbusha wanadamu umuhimu wa kutegemea kafara ya Kristo kwa wokovu wao. (Mwanzo 4:3-7) “Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa Bwana. Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. Bwana akamtakabali Habili na sadaka yake; bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana. Bwana akamwambia Kaini, Kwa nini una ghadhabu? Na kwa nini uso wako umekunjamana? Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde.” Mema aliyotakiwa Kaini ayatende ili kujipatia kibali kwa Bwana ni ya kutegemea kafara ya Kristo kwa wokovu wake na wala si kuanzisha mpango mwingine wa kujiokoa usiotegemea mpango ule uliowekwa na Mungu.

Ukimkataa Yesu maishani mwako haijalishi unafanya sadaka za kujitoa za namna gani au utende matendo mema ya namna gani mambo hayo hayawezi kununua wokovu wako. (1 Wakorintho 13:3) “Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu.” Msukumo wa chochote unachofanya kwenye ibada ni lazima utokane na upendo wa kweli wa Agape usio na misukumo ya ubinafsi ndani yake. Lazima iwe ibada iliyojengwa juu ya imani itendayo kazi kwa upendo. (Wagalatia 5:6) “Maana katika Kristo Yesu kutahiriwa hakufai neno, wala kutokutahiriwa, bali imani itendayo kazi kwa upendo.”

Kosa hilo hilo la kumwabudu Mungu kwa kutegemea ubunifu wa kibinadamu lilirudiwa na wajenzi wa Babeli. (Mwanzo 11:4) “Wakasema, Haya, na tujijengee mji, na mnara, na kilele chake kifike mbinguni, tujifanyie jina; ili tusipate kutawanyika usoni pa nchi yote.” Moja ya sababu za kujenga mnara ule ni kupinga mpango wa Mungu wa kutawanyika ulimwenguni. Ujenzi wa Babeli ulilenga kuhujumu mpango wa Mungu wa kuwaokoa wanadamu. Ulikuwa unakwenda kinyume na mpango wa Mungu.

Mungu aliwaagiza waliotoka kwenye Safina kutawanyika kama Yesu alivyowaagiza wanafunzi wake. (Mathayo 28:19-20) “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.” Watu wale wa wakati wa gharika hawakuwa na imani na kauli hivyo wakakataa kutawanyika hadi Mungu alipowatawanya kwa nguvu.

Wakati leo tukiitikia agizo la Yesu kwa kusema, “Nitakwenda” wao walisema “Hatuendi.” Lakini kwa kutawanyika huko Mungu alifanikiwa kukomesha uasi uliokuwa unaandaliwa dhidi ya yake. Kwa kujenga mnara wa Babeli walikuwa wanaunda mpango wa kibinadamu wa kujiokoa na adhabu ya gharika badala ya kutegemea mpango wa wokovu unaosimamiwa na Mungu mwenyewe kupitia ukombozi ulio ndani ya Kristo Yesu. Walitaka kuonyesha kuwa wanaweza kujiokoa wenyewe na wala hawahitaji msaada wa Mungu na pia walitaka kujifanyia jina kuwa na wao wana jambo la kuchangia katika wokovu wao. Mungu akiruhusu kuwepo kwa wokovu unaomfanya mwanadamu ajihisi kuwa amechangia kitu utakuwa mwendelezo wa uasi.  

Tukio la Kaini na wajenzi wa mnara wa Babeli likaibua dini na ibada mpya duniani kati ya jamii ya wanadamu. Dini na ibada isiyotegemea maelekezo na maagizo ya Mungu wala kutegemea msaada wa Mungu katika kutekeleza maagizo hayo. (Yeremia 17:5) “Bwana asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha Bwana.” Hii ndiyo dini rahisi ambayo watu wa mataifa waliichagua na ambayo Waisraeli walitamani kuwa nayo pia. (Isaya 4:1) “Na siku hiyo wanawake saba watamshika mtu mume mmoja wakisema, Tutakula chakula chetu, na kuvaa nguo zetu wenyewe, lakini tuitwe tu kwa jina lako; utuondolee aibu yetu.” Waisraeli walikuwa tayari watambulike kwa jina la Mungu wa mbinguni lakini wakiishi bila kutegemea neno lake (chakula) wala tabia yake (mavazi).

Yesu alipokuja duniani alikuta dini hiyo Ikiwa imeshamiri na aliikemea vikali. (Marko 7:6-8) “Akawaambia, Isaya alitabiri vema juu yenu ninyi wanafiki, kama ilivyoandikwa, Watu hawa huniheshimu kwa midomo Ila mioyo yao iko mbali nami; Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu, Ninyi mwaiacha amri ya Mungu, na kuyashika mapokeo ya wanadamu.” Ibada ya kweli lazima itokane na Mungu ikiendeshwa kwa misingi ya Biblia na kuongozwa na mioyo iliyoguswa na Roho Mtakatifu na siyo mihemko ya kimwili. (Yohana 4:24) “Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”

Ibada katika siku za mwisho itapuuzia kanuni hizo muhimu za ibada. Haitaongozwa na kweli yaani maagizo ya Biblia wala maongozi ya Roho Mtakatifu. Itaongozwa na mapokeo yasiyokubaliana na Maandiko na misisimko ya mwili kupia kinachoitwa miujiza na uombaji wa kupayuka. (Mathayo 6:7) “Nanyi mkiwa katika kusali, msipayuke-payuke, kama watu wa mataifa; maana wao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu ya maneno yao kuwa mengi.” Licha ya huduma za ibada zisizozingatia maelekezo ya Biblia kutakuwepo pia vivutio vya miujiza ambayo pia haizingatii viezo vya Biblia.

Shetani ataingilia kati ibada zisizozingatia maelekezo ili kujitwalia utukufu kwa yale yanayotendeka hapo. (Ufunuo 13:12-17) “Naye atumia uwezo wote wa mnyama yule wa kwanza mbele yake. Naye aifanya dunia na wote wakaao ndani yake wamsujudie mnyama wa kwanza, ambaye jeraha lake la mauti lilipona. Naye afanya ishara kubwa, hata kufanya moto kushuka kutoka mbinguni uje juu ya nchi mbele ya wanadamu. Naye awakosesha wale wakaao juu ya nchi, kwa ishara zile alizopewa kuzifanya mbele ya huyo mnyama, akiwaambia wakaao juu ya nchi kumfanyia sanamu yule mnyama, aliyekuwa na jeraha la upanga naye akaishi. Akapewa kutia pumzi katika ile sanamu ya mnyama, hata ile sanamu ya mnyama inene, na kuwafanya hao wote wasioisujudu sanamu ya mnyama wauawe. Naye awafanya wote, wadogo kwa wakubwa, na matajiri kwa maskini, na walio huru kwa watumwa, watiwe chapa katika mkono wao wa kuume, au katika vipaji vya nyuso zao; tena kwamba mtu awaye yote asiweze kununua wala kuuza, isipokuwa ana chapa ile, yaani, jina la mnyama yule, au hesabu ya jina lake.”

Shetani ni adui mkuu wa mpango wa Mungu. Yeye hapendi kuona watu wakiokolewa. Anapingana na kundi lolote lenye mwelekeo wa kuwasaidia watu kuokolewa. (Ufunuo 12:17) “Joka akamkasirikia yule mwanamke, akaenda zake afanye vita juu ya wazao wake waliosalia, wazishikao amri za Mungu, na kuwa na ushuhuda wa Yesu; naye akasimama juu ya mchanga wa bahari.” Shetani amejiundia kundi la watu wanaojitanabaisha kuwa ni wale watakatifu waliotabiriwa kuhubiri injili katika siku za mwisho. (Mathayo 24:14) “Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja.”

Kundi la watakatifu wenye kuitangaza injili ya kweli duniani katika siku za mwisho linatambulishwa kwa sifa maalum. (Ufunuo 14:12) “Hapa ndipo penye subira ya watakatifu, hao wazishikao amri za Mungu, na imani ya Yesu.” Kundi hili litakuwa likihubiri kuwa wokovu umepatikana kutokana na kile Yesu alichofanya kwa niaba ya wanadamu wote pale msalabani. (Waefeso 2:5) “Hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu; alituhuisha pamoja na Kristo; yaani, tumeokolewa kwa neema.” (Waefeso 2:8-9) “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu.”

Kundi hili linakuwa vinara katika kutambua nafasi ya imani kwenye mchakato wa wokovu. Ili mtu aokolewe ni lazima awe na imani kwa Mungu. hata hivyo imani hiyo ni lazima ijengwe juu ya Neno la Mungu. (Warumi 10:17) “Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.” Imani isiyojengwa juu ya Neno la Mungu ni imani hatarishi maana hata Shetani ana imani kama hiyo. (Yakobo 2:19) “Wewe waamini ya kuwa Mungu ni mmoja; watenda vema. Mashetani nao waamini na kutetemeka.”

Kuamini kwa moyo humfanya mtu kupata haki ambayo haiwezi kupatikana kwa njia nyingine yeyote. (Warumi 10:10) “Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.” Kutokana na madhara yaliyoletwa na dhambi mwanadamu alipoteza uwezo wa kuwa mwenye haki mbele za Mungu. (Ayubu 25:4) Basi mtu awezaje kuwa na haki mbele ya Mungu? Au awezaje kuwa safi aliyezaliwa na mwanamke? Mpango wa wokovu ulitatua mgogoro huo kwa kumuibua mwanadamu mmoja aliyekidhi vigezo vinavyompasa mwenye haki ambavyo havikuwahi kufikiwa na mwanadamu mwingine yeyote kabla yake. Mwenye haki huyo aliyekidhi vigezo hivyo ni Yesu ambaye Wayahudi walimuua wakimhesabu kuwa mwenye hatia. (Matendo 3:14-15) “Bali ninyi mlimkana yule Mtakatifu, yule Mwenye haki, mkataka mpewe mwuaji; mkamwua yule Mkuu wa uzima, ambaye Mungu amemfufua katika wafu; na sisi tu mashahidi wake.”

Kifo cha Yesu msalabani kilikuwa kinalipa adhabu iliyokuwa inawastahili wanadamu wote waliotenda dhambi. Kifo chake kikawa ndiyo uzima wao. (Isaya 53:4-5) “Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.” Mtu anapomuamini Yesu anaondolewa kutoka kwenye adhabu ya mauti na kuhesabiwa kuwa mwenye haki anayestahili uzima wa milele. (Warumi 8:1) “Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu.” Yohana 5:24 Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani.

Imani kuwa kifo cha Yesu kilituhesabia haki ya uzima wa milele si imani pekee anayopaswa kuwa nayo yeyote anayetaka kuokolewa. Pamoja na kuamini kifo cha Yesu kilivyotukomboa tunapaswa kuamini uwezo wa Roho Mtakatifu wa kutubadilisha tabia zetu zilizopinda. Imani hiyo yenye mchakato mrefu zaidi inahitaji ushirikiano usiokoma unaoruhusu mabadiliko hayo kutokea. Katika hatua hii utu wa zamani huvuliwa hatua kwa hatua na kuvaliwa utu mpya. (Waefeso 4:22-24) “Mvue kwa habari ya mwenendo wa kwanza utu wa zamani, unaoharibika kwa kuzifuata tamaa zenye kudanganya; na mfanywe wapya katika roho ya nia zenu; mkavae utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya Mungu katika haki na utakatifu wa kweli.” Mabadiliko haya huletwa na Roho Mtakatifu na hivyo mwenye kutakaswa hana nafasi ya kujiinua au kujitukuza wala kujidhania kuwa amekamilika. (Wafilipi 3:12-14) “Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake nimeshikwa na Kristo Yesu. Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele; Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele.”

Dini kinzani imebuni imani ambayo mwenye kupokea sifa ni yule anayeamini na kuhesabiwa haki na yule anayetakaswa. Hii ndiyo dini ya Mafarisayo. Waliamini kuwa kwa kutimiza matakwa ya kidini wanaununua wokovu. Waliutumainia mwili badala ya kumtumainia Yesu aliye mwanzilishi na mtimizaji wa imani yetu. (Wafilipi 3:4-6) Walakini mimi ningeweza kuutumainia mwili. Mtu ye yote akijiona kuwa anayo sababu ya kuutumainia mwili, mimi zaidi. Nalitahiriwa siku ya nane, ni mtu wa taifa la Israeli, wa kabila ya Benyamini, Mwebrania wa Waebrania, kwa habari ya kuishika torati, ni Farisayo, kwa habari ya juhudi, mwenye kuliudhi Kanisa, kwa habari ya haki ipatikanayo kwa sheria sikuwa na hatia.” (Waebrania 12:2) “Tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.”

Matendo yetu hata yale yaliyo mema kama yametendwa kwa lengo la kujihesabia haki huwa machukizo mbele ya Mungu. Na huwa machukizo zaidi yakitendwa ibadani. Matendo ya Kaini ya kujibunia sadaka kinyume cha maelekezo yalikuwa machukizo na kuifanya ibada yake isikubalike. (Mwanzo 4:4-5) “Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. Bwana akamtakabali Habili na sadaka yake; bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana.” Kitendo cha Mafarisayo kujisifu kwa mambo mema anayoyafanya na kumdharau Mtoza ushuru kulifanya ibada yake isikubalike. (Luka 18:13) “Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi. Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.”

Dini inayomruhusu mwanadamu kujiwekea nyongeza zilizo kinyume na maelekezo ya awali na ambayo hutegemea jitihada zake katika kufikia viwango vinavyomtambua kama mwenye haki ni dini inayopendwa na vizazi vyote vya wanadamu wa nyakati zote. Dini hizo kwa wakati zaweza kuonekana zimetofautiana lakini zimejengwa kwenye msingi mmoja wa kujihesabia haki na kutotegemea neema ya Mungu. dini hii inakwenda kinyume cha mpango na inauhujumu mpano wa wokovu. Wakati mpango wa wokovu ukielekeza ubatizo wa kuzamishwa majini ili kuonesha kuwa mtu amekiri kuwa kifo cha Yesu kinawakilisha kifo chake utapokelewa kama ishara ya nje ya mtu huyo kukubali mauti ya Kristo iwe badala yake, dini kinzani inabatilisha na kuagiza kuwa ubatizo wowote hata wa maji machache yasiyozamisha mwili wote yanatosha. (Warumi 6:3-4) “Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake? Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima.”

Kuzikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo hufanyika pale mtu anapozamishwa kwenye maji mengi. Wakristo wa awali ambao msingi wa dini yao haukuwa kujihesabia haki na kutaka kumsahihisha Mungu walizingatia agizo hili. (Yohana 3:23) “Yohana naye alikuwa akibatiza huko Ainoni, karibu na Salimu, kwa sababu huko kulikuwa na maji tele; na watu wakamwendea, wakabatizwa.” Wakati huo hapakuwa na ubatizo wa kunyunyizwa kichwani. Kama maji yaliyokuwepo hayakuwa ya kutosha kuzamisha mwili wote ubatizo huo haukuweza kufanyika. Kitendo cha kuruhusu ubatizo wa maji kidogo uliofanywa na Wakristo wa zama za giza la kiroho ulihujumu mpango wa wokovu kwa kiwango kikubwa. Hii ndiyo dini kinzani inayotembea sambamba na dini ya kweli katika zama zote za wanadamu.

Kuruhusu ubatizo wa maji kidogo kulifungulia ubatizo wa watoto wachanga ambao haukuwepo kwenye maelekezo yaliyotolewa awali. (Mathayo 28:19-20) “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.” Yesu aliagiza kila anayebatizwa ni lazima afundishwe kwanza. Na baada ya kufundishwa aamini alichofundishwa. (Marko 16:16) “Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.” Watoto wadogo wanaobatizwa wakiwa wachanga hawapati fursa ya kujifunza na kuamini na hivyo wanaingizwa kwenye agano la ubatizo bila ridhaa yao.

Kutokana hujuma hiyo idadi fulani ya wanaotambulika leo kuwa ni Wakristo ni Wakristo hewa maana walijiunga na Ukristo bila ridhaa yao na bila kujua chochote kuhusu Ukristo. Hawa wanaweza kutambulika hapa duniani kama Wakristo lakini hawatambuliki hivyo mbinguni. (Luka 10:20) “Lakini, msifurahi kwa vile pepo wanavyowatii; bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni.” Ili jina liwe limeandikwa mbinguni ni lazima mwenye jina awe ameafikiana na mpango wa wokovu. Mpango wa wokovu ulihitaji watu wawe wanabatizwa kwenye maji mengi baada ya kujifunza na kuamini.

Wanaoandikwa majina yao katika kitabu cha uzima mbinuni ni wale wanaohubiri injili isiyoruhusu vitendo vya kujihesabia haki ambavyo havikuwepo kwenye maelekezo ya awali na ambavyo vinahujumu mpango wa wokovu. (Wafilipi 4:3) “Naam, nataka na wewe pia, mjoli wa kweli, uwasaidie wanawake hao; kwa maana waliishindania Injili pamoja nami, na Klementi naye, na wale wengine waliotenda kazi pamoja nami, ambao majina yao yamo katika kitabu cha uzima.” Kundi la dini kinzani lenye malengo ya kuhujumu mpango wa wokovu majina yao hayawezi kuwamo kwenye kitabu cha uzima kwa kuwa dhamira yao ni kinyume cha mpango wa wokovu. (Ufunuo 17:8) “Yule mnyama uliyemwona alikuwako, naye hayuko, naye yu tayari kupanda kutoka kuzimu na kwenda kwenye uharibifu. Na hao wakaao juu ya nchi, wasioandikwa majina yao katika kitabu cha uzima tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu, watastaajabu wamwonapo yule mnyama, ya kwamba alikuwako, naye hayuko, naye atakuwako.”

Ubatizo hufanyika ili kuzika utu wa kale. Kwenye ubatizo utu wa le huachwa majini na utu mpya hufufuka na anayeibuka baada ya kubatizwa. Katika tukio hilo kuna badiliko lisilo la kawaida lililoahidiwa ambalo wale wanaobatizwa kwa maji machache na watoto wachanga hulikosa. (Matendo 8:36-39) “Wakawa wakiendelea njiani, wakafika mahali penye maji; yule towashi akasema, Tazama, maji haya; ni nini kinachonizuia nisibatizwe? Filipo akasema, Ukiamini kwa moyo wako wote, inawezekana. Akajibu, akanena, Naamini ya kwamba Yesu Kristo ndiye Mwana wa Mungu. Akaamuru lile gari lisimame; wakatelemka wote wawili majini, Filipo na yule towashi; naye akambatiza. Kisha, walipopanda kutoka majini, Roho wa Bwana akamnyakua Filipo, yule towashi asimwone tena; basi alikwenda zake akifurahi.”

Kuna ubatizo wa aina moja tu ambao ni ule Yesu aliobatizwa yaani ubatizo wa maji mengi. (Marko 1:9-11) “Ikawa siku zile, Yesu alikuja kutoka Nazareti ya Galilaya, akabatizwa na Yohana katika Yordani. Mara alipopanda kutoka majini, akaona mbingu zinapasuka, na Roho, kama hua, akishuka juu yake; na sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe.” Yesu hakustahili kubatizwa bali alifanya hivyo ili kutupatia kielelezo na kutimiza haki yote. (Mathayo 3:13-15) “Wakati huo Yesu akaja kutoka Galilaya mpaka Yordani kwa Yohana ili abatizwe. Lakini Yohana alitaka kumzuia, akisema, Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu? Yesu akajibu akamwambia, Kubali hivi sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote. Basi akamkubali.”

Kama Yesu asiye na dhambi alikubali kubatizwa kwenye maji mengi tena machafu ya mto Yordani, wewe uliye na dhambi unapata wapi ujasiri wa kukataa ubatizo wa kuzamishwa majini? Je, wewe u mkubwa kuliko Yesu? Dini kinzani iliyojikita katika kupinga maagizo ya Mungu ni ile ile iliyokuwepo kwa Kaini na wajenzi wa mnara wa Babeli. Dini hii hupenda kujiinua juu ya kila kiitwacho Mungu. (2 Wathesalonike 2:4) “Yule mpingamizi, ajiinuaye nafsi yake juu ya kila kiitwacho Mungu ama kuabudiwa; hata yeye mwenyewe kuketi katika hekalu la Mungu, akijionyesha nafsi yake kana kwamba yeye ndiye Mungu.” Ni dini inayomwinua Mwanadamu zaidi ya Mungu. ni dini iliyoasisiwa na yule aliyeanzisha uasi mbinguni. (Isaya 14:13-14) “Nawe ulisema moyoni mwako, Nitapanda mpaka mbinguni, Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu; Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano, Katika pande za mwisho za kaskazini. Nitapaa kupita vimo vya mawingu, Nitafanana na yeye Aliye juu.”

Mpango wa wokovu ulikusudia sheria au amri za Mungu ziwe kipimo cha tabia ya Mungu tabia ambayo Mungu alituumba nayo na ambayo Roho Mtakatifu anakusudia kuirejesha kwetu pale tunapomwamini Kristo. (Waefeso 2:10) “Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo.” Lakini tulishindwa kuchukuliana na sheria hizo kutokana na udhaifu wa mwili. (Warumi 8:7) “Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii.” (Warumi 7:14) “Kwa maana twajua ya kuwa torati asili yake ni ya rohoni; bali mimi ni mtu wa mwilini, nimeuzwa chini ya dhambi.” Yesu mwenyewe alilitatua tatizo hilo pale alipoifia sheria au torati. (Warumi 8:2-4) “Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti. Maana yale yasiyowezekana kwa sheria, kwa vile ilivyokuwa dhaifu kwa sababu ya mwili, Mungu, kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe katika mfano wa mwili ulio wa dhambi, na kwa sababu ya dhambi, aliihukumu dhambi katika mwili; ili maagizo ya torati yatimizwe ndani yetu sisi, tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali mambo ya roho.”

Unapomwamini Yesu, Roho Mtakatifu huja na kukusaidia kuzitii sheria ambazo hapo awali zilikuwa ngumu kutokana na udhaifu wa mwili. (Warumi 7: 5-6) “Kwa maana tulipokuwa katika hali ya mwili, tamaa za dhambi, zilizokuwako kwa sababu ya torati, zilitenda kazi katika viungo vyetu hata mkaizalia mauti mazao. Bali sasa tumefunguliwa katika torati, tumeifia hali ile iliyotupinga, ili sisi tupate kutumika katika hali mpya ya roho, si katika hali ya zamani, ya andiko.” Mtu anapomwamini Yesu, mahusiano yake na sheria pia hubadilika. Badala ya kuiona sheria kuwa ni mbaya na ngumu huiona ni njema na nyepesi. (Warumi 7:12) “Basi torati ni takatifu, na ile amri ni takatifu, na ya haki, na njema.” (1 Yohana 5:3) “Kwa maana huku ndiko kumpenda Mungu, kwamba tuzishike amri zake; wala amri zake si nzito.”

Jipya halina mtazamo tofauti na ule wa Agano la Kale kuhusu sheria. Katika Agano Jipya, sheria zote za Mungu kama zilivyopokelewa Sinai huandikwa moyoni mwa muumini. (Waebrania 8:8-10) “Maana, awalaumupo, asema Angalia, siku zinakuja, asema Bwana, Nami nitawatimizia nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda agano jipya; Halitakuwa kama agano lile nililoagana na baba zao, Katika siku ile nilipowashika mikono yao niwatoe katika nchi ya Misri. Kwa sababu hawakudumu katika agano langu, Mimi nami sikuwajali asema Bwana. Maana hili ndilo agano nitakaloagana na nyumba ya Israeli Baada ya siku zile, asema Bwana; Nitawapa sheria zangu katika nia zao, Na katika mioyo yao nitaziandika; Nami nitakuwa Mungu kwao, Nao watakuwa watu wangu.”

Sheria hizo hazipo ili zitumike kama kigezo cha kutupatia wokovu au kutuhesabia haki. Sheria hizo zipo ili kututambulisha kuwa tumeokolewa na tumehesabiwa haki kwa neema ya Kristo. Sheria hutusaidia pia tusijikwae na kurejea kwenye maisha ya dhambi. Sheria inatusaidia kutambua dhambi ili tukimbilie kwa Mwokozi atupaye msamaha na uwezo wakuishinda. (Warumi 3:20) “Kwa sababu hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki mbele zake kwa matendo ya sheria; kwa maana kutambua dhambi huja kwa njia ya sheria.” (Yohana 15:5) “Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote.” (Wagalatia 3:24) “Hivyo torati imekuwa kiongozi kutuleta kwa Kristo, ili tuhesabiwe haki kwa imani.”

Katika hali hii ambapo sheria haituokoi bali inatusaidia kutambua dhambi na kutusogeza kwa Kristo, mtu asingetarajia kuona jitihada za kuziondoa au kuzibadilisha zikifanywa na wanaojitambulisha kama Wakristo. Historia imeandika kuwa katika kipindi cha giza la kiroho la Ukristo wa kale, viongozi waliondoa sheria ya pili inayokataza kuabudu sanamu na kubadili sheria ya nne inayoagiza kutunza Sabato. Mtu aweza kujiuliza badiliko hilo lililenga kuleta unafuu gani kwa Mkristo wakati ambapo sheria hiyo haiokoi? Jibu ni kuwa huu ulikuwa mwendelezo wa hujuma dhidi ya ukombozi, ufanywao na dini ile kinzani inayofanya shughuli zake kwa kujiinua, kujihesabia haki, kupimana ubavu na Mungu na kudhoofisha mpango wa wokovu.

Kama sheria haiokoi kama Neno la Mungu lisemavyo kulikuwa na haja gani ya kuifanyia mabadiliko? Je, mabadiliko hayo yalilenga kuleta unafuu gani kwa Mungu au kwa mwanadamu? Kwa nini mabadiliko yafanyike kwa amri ya pili na ya nne na siyo kwenye amri zingine? Mungu aliiweka sheria ili itumike kama kioo cha kujiangalizia ili kama mtu amechafuka aone haja ya kwenda kwa Kristo apate kuoshwa. (Yakobo 1:23-25) “Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo. Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo. Lakini aliyeitazama sheria kamilifu iliyo ya uhuru, na kukaa humo, asiwe msikiaji msahaulifu, bali mtendaji wa kazi, huyo atakuwa heri katika kutenda kwake.”

Mabadiliko hayo ya sheria yaliyofanywa na wanadamu bila kibali cha Mungu, yanamfanya mtu aliyevunja amri ya pili na ya nne asijione kuwa na hatia kwa sababu haimhukumu tena kwa uvunjifu huo. Sheria hiyo iliyobadilishwa inamfanya kuwa huru kuendelea kuvunja amri ya pili na ya nne huku ikiendelea kumtia hatiani kupitia amri zingine nane ambazo hazijabadilishwa. Hii ni hujuma kubwa dhidi ya wokovu. (Yakobo 2:11) “Kwa maana yeye aliyesema, Usizini, pia alisema, Usiue. Basi ijapokuwa hukuzini, lakini umeua, umekuwa mvunja sheria.”

Matokeo yake dini kinzani imejizolea watu wanaojitambulisha kama Wakristo huku wakiishi kinyume na matakwa ya Ukristo kwa kutozingatia matakwa ya amri ya pili na ya nne kama Biblia inavyohimiza, kwa kuwa viongozi wa dini hizo wamewaaminisha kuwa wasihangaike na sheria maana haziokoi. Ukweli wa mambo ni kuwa pamoja na ukweli kuwa sheria haziokoi lakini zinasaidia kubaini makosa na wenye makosa. Katika dini hizo kinzani mtu anayeishi kinyume na mataka ya sheria nane ambazo hazikurekebishwa huonywa, hupewa adhabu na ikibidi hutengwa. Je kama sheria haina umuhimu tungewatambuaje, wezi, na wazinzi? Tungepataje ujasiri wa kukemea dhambi? (Warumi 7:8) “Lakini dhambi ilipata nafasi kwa ile amri, ikafanya ndani yangu kila namna ya kutamani. Kwa maana dhambi bila sheria imekufa.” Dhana kuwa sheria haiokoi inatumika vibaya ili kuficha hujuma iliyofanyika ya kuondoa amri ya pili na kubadilisha amri ya nne kulikofanywa na viongozi wa Kikristo wa zama za giza wasio waadilifu.

Darubini ya magonjwa haitoi dawa lakini inabainisha aina ya ugonjwa alionao mtu. Je kwa kuwa haitoi tib abasi iondolewe hospitalini? Ikiondolewa daktari atamsaidiaje mgojwa aliyefuata tiba kwake hali hajui aina ya wadudu waliosababisha ugonjwa wake na idadi yao mwilini? Kuondoa sheria kwa madai kuwa haiokoi ni sawa ma kuondoa darubini hospitalini kwa madai kuwa haitoi tiba. Sheria ina nafasi yake na Mwokozi ana nafasi yake pia. (Zaburi 119:155) “Wokovu u mbali na wasio haki, Kwa maana hawajifunzi amri zako.”

Kundi hilo la Wakristo waaminifu halitaishia katika kuwatangazia wanadamu kile kilichokamilika pale msalabani bali pia litatangaza awamu ya wokovu inayoendelea sasa na ile ijayo. (2 Wakorintho 1:9-11) "Naam, sisi wenyewe tulikuwa na hukumu ya mauti katika nafsi zetu ili tusijitumainie nafsi zetu, bali tumtumaini Mungu, awafufuaye wafu, aliyetuokoa sisi katika mauti kuu namna ile; tena atatuokoa; ambaye tumemtumaini kwamba atazidi kutuokoa; ninyi nanyi mkisaidiana nasi kwa ajili yetu katika kuomba, ili, kwa sababu ya ile karama tupewayo sisi kwa msaada wa watu wengi, watu wengi watoe shukrani kwa ajili yetu."

Kundi la Wakristo waaminifu linatangaza kazi ya ukarabati wa tabia inayofanywa na Roho Mtakatifu kwa lengo la kurejesha matendo mema yasiyochafuliwa na ubinafsi tuliyokuwa tumeumbiwa nayo na ambayo tuliyapoteza kutokana na anguko la dhambi. (Waefeso 2:10) “Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo.” Lakini dhambi ilipoingia tukapoteza matendo hayo na kuishi kulingana na mwenendo tuliourithi kutoka kwa Adamu. (1 Petro 1:18) "Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu." Mungu amejiridhisha kuwa kazi hiyo ya mabadiliko ya tabia iliyoanza mioyoni mwetu inayofanywa na Roho Mtakatifu itakamilika kwa mafanikio makubwa. (Wafilipi 1:6) "Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu."

Wakristo wa kweli wataendelea kupinga hila zifanywazo na kundi hili kinzani hadi mwisho wa wakati. Pamoja na mbinu zao chafu kuungwa mkono na mamlaka za kidunia, dini hii kinzani haitafaulu katika kuhafifisha na kuhujumu mpango wa Mungu wa ukombozi.  (Ufunuo wa Yohana 15:2) “Tena nikaona kitu kama mfano wa bahari ya kioo iliyochangamana na moto, na wale wenye kushinda, watokao kwa yule mnyama, na sanamu yake, na kwa hesabu ya jina lake, walikuwa wamesimama kando-kando ya hiyo bahari ya kioo, wenye vinubi vya Mungu.”

(Ufunuo wa Yohana 19:20) “Yule mnyama akakamatwa, na yule nabii wa uongo pamoja naye, yeye aliyezifanya hizo ishara mbele yake, ambazo kwa hizo aliwadanganya watu wale walioipokea ile chapa ya huyo mnyama, nao walioisujudia sanamu yake; hao wawili wakatupwa wangali hai katika lile ziwa la moto liwakalo kwa kiberiti.”