UCHAMBUZI WA KITABU CHA WARUMI
WARUMI SURA YA SITA
Kitabu cha Warumi sura ya sita kinajadili maisha ya mtu aliyehesabiwa haki kwa imani. Maisha ya mtu aliyehesabiwa haki ni maisha ya kuukulia wokovu. (1 Petro 2:2) “Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu.” Aliyehesabiwa haki amezaliwa upya na hivyo matarajio ni kumuona akikua hadi kufikia kimo chake Kristo. (Waefeso 4:12-13) “Kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo.”
Maisha ya kuukulia wokovu hayatarajiwi yawe ya kutumikia dhambi. (Warumi 6:6-7) “Mkijua neno hili, ya kuwa utu wetu wa kale ulisulibishwa pamoja naye, ili mwili wa dhambi ubatilike, tusitumikie dhambi tena; kwa kuwa yeye aliyekufa amehesabiwa haki mbali na dhambi.” Mwili wa dhambi uliobeba vinasaba na utegemezi wa dhambi ulisulubishwa msalabani wakati ule Yesu alipokuwa akiusulubisha mwili wake uliobeba dhambi za wanadamu. Kutokana na kitendo hicho kilichotokea msalabani mwili wa dhambi ulibatilika. Mwili wa dhambi kubatilika maana yake ni kawa batili na kuwa batili maana yake kutokuwepo tena.
Mwili huu tulionao baada ya kumwamini Yesu si ule wa dhambi uliofikia ukomo wake pale msalabani bali ni mwili mpya ule Kristo aliofufuka nao alipotoka kaburini. (Warumi 7:4) “Kadhalika, ndugu zangu, ninyi pia mmeifia torati, kwa njia ya mwili wa Kristo, mpate kuwa mali ya mwingine, yeye aliyefufuka katika wafu, kusudi tumzalie Mungu matunda.” Mwili huu hauna mgogoro tena na torati kwa kuwa mwili uliokuwa na mgogoro na torati ulikufa. (Warumi 7:1) “Ndugu zangu, hamjui (maana nasema na hao waijuao sheria) ya kuwa torati humtawala mtu wakati anapokuwa yu hai?”
Kitendo cha Yesu kufa alikuwa anaifia dhambi yaani alikuwa anakufa kwa kuwa mwili ulishindwa kutii matakwa na maagizo ya torati. (Warumi 6:23) “Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.” Aliyelipa madai ya sheria kwa kutumikia kifo hawezi tena kuwa mtumwa wa dhambi bali anahesabiwa kuwa mfu kwa dhambi. (Warumi 6:8-11) “Lakini tukiwa tulikufa pamoja na Kristo, twaamini ya kuwa tutaishi pamoja naye; tukijua ya kuwa Kristo akiisha kufufuka katika wafu hafi tena, wala mauti haimtawali tena. Maana kwa kule kufa kwake, aliifia dhambi mara moja tu; lakini kwa kule kuishi kwake, amwishia Mungu. Vivyo hivyo ninyi nanyi jihesabuni kuwa wafu kwa dhambi na walio hai kwa Mungu katika Kristo Yesu.”
Tulioifia dhambi katika mauti ya Kristo tunatakiwa tujihesabu kuwa wafu kwa dhambi na walio hai kwa Mungu. Hatuna mahusiano yoyote ya kimantiki na kisheria kati yetu na dhambi kwa kuwa dhambi ilitimiziwa haki yake kupitia kifo cha Kristo. Wazo la msingi la kushikilia wakati wote ni kuwa tulikufa pamoja na Kristo na hivyo dhambi au torati haitudai tena. (2 Wakorintho 5:14) “Maana, upendo wa Kristo watubidisha; maana tumehukumu hivi, ya kwamba mmoja alikufa kwa ajili ya wote, basi walikufa wote.”
Na kama hatudaiwi na dhambi mahusiano yetu na dhambi yanapaswa kuwaje? Sisi tulioifia dhambi sasa tunaishi katika neem ana neema inatufundisha kukataa kila aina ya ubaya. (Tito 2:11-12) “Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa.” (Warumi 6:1-2) “Tuseme nini basi? Tudumu katika dhambi ili neema izidi kuwa nyingi? Hasha! Sisi tulioifia dhambi tutaishije tena katika dhambi?” Neema si kibali cha kutenda dhambi lakini huanzisha mchakato wa maisha yasiyo ya dhambi.
Injili inapomfikia mtu humwingiza katika mfumo wa kuhesabiwa haki kwa imani na kumleta kwenye hatua ya wongofu ambao humpitisha kwenye uzoefu wa kutoshiriki matendo ya giza ambayo hitimisho lake ni kumfikisha kwenye hatua ya kutotenda dhambi tena. Huu huitwa pia mchakato wa kuwakamilisha watakatifu. Mungu kwa kuwa ana uhakika wa mtu aliyeuanza mchakato huo kumaliza akiwa mshindi humtunuku mtu huyo hadhi ya kuitwa mtakatifu. (Wafilipi 1:6) “Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu.” (Wakolosai 3:12-13) “Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi.”
Mungu anatutambua kama watakatifu wapendwao ingawa tumepungukiwa moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole na kuvumiliana. Na kwa hiyo ndani ya mchakato wa kuukulia wokovu kuna kuimarishwa kutoka hatua moja kwenda hatua nyingine. (Luka 22:31-32) “Akasema, Simoni, Simoni, tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano; lakini nimekuombea wewe ili imani yako isitindike; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako.” Hivyo aliyefikia kiwango fulani cha ukuaji wa kiroho anao wajibu wa kumuimarisha mwenzake anayechechemea.
Paulo anaainisha mchakato nzima wa kuukulia wokovu huzinduliwa kwa tukio gani. Tukio linalozindua mchakato wa kuukulia wokovu lina uhusiano na kifo na ufufuo wa Kristo. Kama Kristo alivyokufa na kufufuka siku ya tatu hivyo hivyo waliokufa pamoja na Kristo wanapaswa kuonyesha kielelezo cha kufa na kufufuka kwa Kristo. Kitendo kilichoidhinishwa kuwakilisha kifo na ufufuo wa Kristo ubatizo wa kuzamishwa kwenye maji mengi. (Warumi 6:3-5) “Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake? Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima. Kwa maana kama mlivyounganika naye katika mfano wa mauti yake, kadhalika mtaunganika kwa mfano wa kufufuka kwake.”
Kwenye ubatizo wa maji mengi tunaunganika na Kristo katika mfano wa mauti yake na tunaunganika na Kristo katika mfano wa kufufuka kwake pia. Ikiwa ubatizo hautoi kielelezo cha mtu aliyekufa akazikwa na wala hautoi kielelezo cha mtu aliyefufuka ubatizo huo umepoteza sifa muhimu na unamfanya anayebatizwa asinufaike na kifo cha Yesu pale msalabani kama ambavyo ilikuwa imekusudiwa. Mtu aliyebatizwa kwa ubatizo mwingine kando ya ule wa kuzamishwa majini anahesabiwa sawa na yule ambaye hajabatizwa kabisa. Kama Yesu atamruhusu mtu huyo kwenda mbinguni shetani atapinga jambo hilo akidai mtu huyo ni wake kwa kuwa hakutekeleza matakwa yanayotakiwa kwenye ubatizo. (Marko 16:16) “Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.”
Kitendo cha kushiriki ubatizo unaowakilisha kifo na ufufuo wa Kristo kinampa uhalali mhusika kuwa mnufaikaji wa ukombozi uliokamilika katika Kristo Yesu. (Yohana 5:24) “Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani.” Sababu ya mtu huyo kutoka mautini ni kule kushiriki tendo linalowakilisha kifo na ufufuo wa Kristo.
Wazo la kuleta ubatizo mwingine usioakisi kifo na ufufuo wa Kristo lilifanywa kimkakati ili kuhujumu ubatizo unaoakisi dhana ya kifo na ufufuo wa Kristo. Lengo limekuwa kuwakosesha watu na kupunguza idadi ya wanufaikaji wa ukombozi uliokamilishwa na Kristo. Biblia inasisitiza umuhimu wa kuwa na ubatizo mmoja kama ule uliofanywa na Yesu. (Mathayo 3:13-16) “Wakati huo Yesu akaja kutoka Galilaya mpaka Yordani kwa Yohana ili abatizwe. Lakini Yohana alitaka kumzuia, akisema, Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu? Yesu akajibu akamwambia, Kubali hivi sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote. Basi akamkubali. Naye Yesu alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake.”
(Warumi 6:12-14) “Basi, dhambi isitawale ndani ya miili yenu ipatikanayo na mauti, hata mkazitii tamaa zake; wala msiendelee kuvitoa viungo vyenu kuwa silaha za dhuluma kwa dhambi; bali jitoeni wenyewe kwa Mungu kama walio hai baada ya kufa, na viungo vyenu kwa Mungu kuwa silaha za haki. Kwa maana dhambi haitawatawala ninyi, kwa sababu hamwi chini ya sheria, bali chini ya neema.”
Paulo anatambua kuwa bado tuna mwili unaopatikana na mauti ingawa kimsingi ulisulibishwa pale msalabani. Mwili huu tutaendelea kuwa nao hadi tutakapopokea mwili mwingine wa utukufu. (Wafilipi 3:20-21) “Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu Kristo; atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote viwe chini yake.”
Katika siku ile mwili huu wa kuharibika utavaa kutokuharibika. (1 Wakorintho 15:51-53) “Angalieni, nawaambia ninyi siri; hatutalala sote, lakini sote tutabadilika, kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho; maana parapanda italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika.Maana sharti huu uharibikao uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa uvae kutokufa.” Huo ndiyo mwili utakaokomesha uzalishaji wa dhambi.
Katika mazingira ya sasa ya mwili huu wa kufa Paulo anashauri tusiruhusu dhambi kutawala kwenye miili yetu hata kuzitii tamaa zake. Dhambi haipati nafasi ya kutawala kwenye miili yetu kwa sababu ya kile kilichotokea msalabani. (Warumi 8:3-4) “Maana yale yasiyowezekana kwa sheria, kwa vile ilivyokuwa dhaifu kwa sababu ya mwili, Mungu, kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe katika mfano wa mwili ulio wa dhambi, na kwa sababu ya dhambi, aliihukumu dhambi katika mwili; ili maagizo ya torati yatimizwe ndani yetu sisi, tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali mambo ya roho.”
Yesu aliihukumu dhambi katika mwili wa dhambi na kujenga mazingira ambayo utiifu wa sheria uliwezeshwa. Hilo linafanyika kupitia utendaji wa Roho Mtakatifu. (Wagalatia 5:16-17) “Basi nasema, Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka.” Kupitia usaidizi wa Roho Mtakatifu yale yaliyokuwa hayawezekani hapo mwanzo sasa yanawezekana kwa sababu Roho anaitawala nia. (Warumi 12:2) “Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.”
Kinachofanywa na Roho Mtakatifu katika nia zetu ni kuitahiri mioyo ili ikubaliane na matakwa ya sheria. (Matendo 7:51) “Enyi wenye shingo gumu, msiotahiriwa mioyo wala masikio, siku zote mnampinga Roho Mtakatifu; kama baba zenu walivyofanya, na ninyi ni vivyo hivyo.” (Waebrania 10:16) “Hili ni agano nitakaloagana nao baada ya siku zile, anena Bwana, Nitatia sheria zangu mioyoni mwao, Na katika nia zao nitaziandika; ndipo anenapo.” Mwenye dhambi husumbuliwa na tamaa za mwili ambazo humsukuma kuyafanya mapenzi ya mwili na mapenzi ya nia. (Waefeso 2:3) “Ambao zamani, sisi sote nasi tulienenda kati yao, katika tamaa za miili yetu, tulipoyatimiza mapenzi ya mwili na ya nia, tukawa kwa tabia yetu watoto wa hasira kama na hao wengine.”
Roho Mtakatifu akishatawala nia mwanadamu hukoma kuwa mtumwa wa dhambi. (Yohana 8:34-36) “Yesu akawajibu, Amin, amin, nawaambia, Kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi. Wala mtumwa hakai nyumbani sikuzote; mwana hukaa sikuzote. Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli.” Dhambi zinazotendeka wakati huu hazitokani na utumwa bali hutokana na uzembe wa kutoruhusu Roho Mtakatifu ashike utawala wa mwili na nia.
Mtu anayeukulia wokovu hayupo huru kuishi anavyotaka. Bado yupo katika utumwa wa haki wa kutii matakwa ya Roho Mtakatifu. (Warumi 6:18) “Na mlipokwisha kuwekwa huru mbali na dhambi, mkawa watumwa wa haki.” Huu ni utumwa ambao anayeukulia wokovu hutoa mwili wake uthibitiwe na nguvu za Roho Mtakatifu. Zoezi hilo ni lenye maumivu maana linaunyima mwili matamanio yake. Yesu alipitia mchakato huu. (Waebrania 2:10) “Kwa kuwa ilimpasa yeye, ambaye kwa ajili yake na kwa njia yake vitu vyote vimekuwapo, akileta wana wengi waufikilie utukufu, kumkamilisha kiongozi mkuu wa wokovu wao kwa njia ya mateso.”
Atatakiwa aombe, afunge, ajinyime vyakula na vinywaji vinavyoweza kuharibu mwili wake ambao ni hekalu la Roho Mtakatifu. Anapaswa kutenga muda wa kujifunza Maandiko, muda wa wenda kushiriki maarifa ya wokovu aliyonayo na wengine, muda wa kushiriki ibada na kazi ya kutegemeza kanisa kwa matoleo na vipawa vyake. Tofauti na wakati mambo hayo yalipokuwa yanafanyika ili kutafuta kuhesabiwa haki kwa matendo na kununua wokovu; sasa matendo hayo yanafanyika kuitikia upendo wa Mungu unaofunuliwa kwa anayeukulia wokovu. Amri ambazo awali zilikuwa ngumu sasa zinakuwa nyepesi kwa msaada wa Roho Mtakatifu. (1 Yohana 5:3) “Kwa maana huku ndiko kumpenda Mungu, kwamba tuzishike amri zake; wala amri zake si nzito.”