Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

FILIPO KAMBA GUNINI

Filipo Kamba Gunini (1880–1996)

Filipo Kamba Gunini alikuwa mchungaji, mmishionari na mwalimu kutoka Tanzania.

Maisha ya Awali

Filipo Kamba Gunini alizaliwa mwaka 1880 wilayani Bariadi. Baba yake, Gunini Kahena, na mama yake, Silya Idete, walikuwa wakulima wadogo. Katika ujana wake, alisafiri na vijana wengine kutafuta kazi kama vibarua wa kawaida. Huko Tanga alijiandikisha katika kambi ya wafanyakazi wa shamba la mkonge ambako alifanya kazi hadi Vita vya Kwanza vya Dunia vilipoanza. Wajerumani waliokuwa na shamba la mkonge waliliacha na kwenda sehemu ya kusini mwa Tanzania ya sasa. Filipo Kamba Gunini alisafiri na Wajerumani hadi Mto Rufiji na kisha kurudi Tanga baada ya kusikia kuhusu wamishonari kutoka Ulaya wanaoishi katika milima ya Pare, huko Suji. Aliamua kwenda milimani na akaajiriwa na wamishonari kama mpishi. Wamishonari walimpa kazi, naye akamkubali Yesu na kubatizwa mwaka wa 1919. Baada ya kufundishwa na wamishonari Waadventista Wajerumani kusoma na kuandika (elimu ya msingi), walimpeleka Nairobi kwa mafunzo ya ualimu, na mwisho wa mafunzo alipata cheti cha ualimu daraja la II.

Ndoa na Kazi

Filipo Kamba Gunini alimuoa Rebecca Mahushi mwaka wa 1922. Pamoja walizaa watoto wanane walioitwa Barnaba, Yunis, Rupho, Hulda, Mbaraka, Esther, Tumaini, na Emmanuel. Rebeka alikuwa mama wa nyumbani ambaye alimsaidia mume wake katika kutunza familia huku akitumia muda wake mwingi katika kufundisha, kusafiri, kuanzisha makanisa, na kutembelea washiriki wa kanisa.

Kutoka Suji, Kanisa lilituma wamisionari katika ardhi ya Wasukuma ili waanzishe kazi ya umishonari kwa kufungua shule. Waliotumwa ni pamoja na: Filipo Kamba Gunini, Petro Mulungwana, Isaya Fue, Philip Sekisago, na Daniel Mwenda. Shule ya Msingi Bupandagila ilipofunguliwa mwaka 1928, Filipo Kamba alikuwa miongoni mwa walimu wanane walioianzisha. Walimu wengine walikuwa Ezekiel Mauro, Yohana Malili, Maria Malongo, Mesipereth Rutoryo, Simon Sayi, Apolo Kwilabya, na Leah Mnyuku kutoka nchi ya Pare ambaye alifariki na kuzikwa Bupandagila.

Isaya Fue na Filipo Kamba Gunini walikwenda kumsimamia Habiya, kwa kuwa hapakuwa na wamishionari wa Kizungu waliokuwa tayari kwenda Habiya kama matokeo ya mmishonari Mjerumani, Richard Muzing, kuuawa na Wamasai mwaka wa 1915 katika vita vya ng'ombe. Kwa hiyo, kazi ilimtegemea Isaya Fue kutoka nchi ya Pare na Filipo Kamba Gunini.

Filipo Kamba alifanya kazi kama mwalimu huko Abiya, Bupandagila na Ikizu Alitawazwa mwaka 1948 pale Mwanyili na Mchungaji Herald Robinson na Ernest H. Kotz. Akiwa mchungaji, alihudumu Mwamanyili, Kibumayi-Tarime na Nyambitilwa-Bunda. Eneo lake lilikuwa Mwanza na Geita kama wilaya moja ya kanisa. Alistaafu mnamo 1960 na kwenda kuishi na watoto wake huko Malili -Nasa. Alikufa Septemba 7, 1996, akiwa na umri wa miaka 115.

Mchango kwa Kanisa

Filipo Kamba anakumbukwa kwa kujitolea kwake katika utumishi. Aliweza kutembelea makanisa na matawi yake yote kwa miguu na kwa baiskeli. Alihamasisha watu kuhudhuria mikutano ya makambi bila kujali umbali. Aliwashirikisha washiriki wapya waliobatizwa katika huduma, na kusababisha ukuaji wa haraka wa kanisa la Kirumba na Kasamwa .