Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

RATIBA YA MWISHO WA DUNIA


UNABII UNAOHUSU RATIBA YA MWISHO WA DUNIA

UTANGULIZI

Mwisho wa dunia ni usemi ambao siyo mgeni miongoni mwa wakazi wa dunia hii. Hata wale ambao hawana dini au wasioamini kama MUNGU yupo kwa nini husema mambo haya yanayotokea yanaashiria mwisho wa ulimwengu Sababu kubwa ni kwamba mabadiliko makubwa na ya haraka sana yanayotokea ulimwenguni. Hata mtu aliye na umri wa miaka ishirini anapitia uzoefu wa kasi ya mabadiliko kama nguo iliyozeeka na inayotatuka. Na hata wengine hudiriki kusema dunia hii ni tambara bovu Biblia inathibitisha usemi huo katika kitabu cha Isaya 24: 19, 20. Dunia kuvunjika inavunjika sana, na dunia kupasuka imepasuka sana, dunia kutikisika imetikisika sana dunia inalewa lewa kama mlevi nayo inawaya waya kama machela, mzigo wa dhambi zake utailemea nayo itaanguka wala haitainuka tena.

Katika kitini hiki tutaona kwa undani kadri itakavyowezekana mpangilio wa matukio kutoka katika vyanzo vya kuaminika ambavyo ni Biblia na Roho ya Unabii.

MATUMAINI YA MWANADAMU
Kila mtu ana mwelekeo wa kupata kitu fulani kwa jambo analolifanya. Mkulima anatumaini kuvuna wakati wa mavuno. Mfanyakazi anatumaini kulipwa mshahara mwisho wa siku, au mwisho wa juma au mwisho wa mwezi. Mfanya biashara hali kadhalika ana matumaini ya kupata faida baada ya kuuza bidhaa zake. Na watu wote hawa huchunguza na kuulizia, ni wakati upi ambao tarajio lao litatimia. Danieli 12:8 nami nikasikia, lakini sikuelewa ndipo nikasema ee Bwana wangu mwisho wa mambo haya utakuwaje?

Je wakristo wa madhehebu yote na watu wa dini zingine zote wasingependa kuelewa hatima ya kuabudu kwao itakuwa ni ipi? Na ni lini? Haitakuwa na maana kama tunaabudu bila lengo itakuwa ni kupoteza muda wetu bure afadhali tungefanya mambo mengine ambayo labda kwa muda mfupi wa kuishi katika dunia hii tungepata ndo ndo za afadhali ya maisha.

I Wakorinto 15:14-19, Tena kama kristo hakufufuka, basi kuhubiri kwetu ni bure, na imani yenu ni bure. Naam na sisi tumeonekana kuwa mashahidi wa uongo wa Mungu, kwa maana tulimshuhudia Mungu ya kuwa alimfufua Kristo, ambaye hakumfufua, ikiwa wafu hawafufuliwi. Maana kama wafu hawafufuliwi, kristo naye hakufufuka. Na kama Kristo hakufufuka imani yenu ni bure; mngalimo katika dhambi zenu. Na hapo wao nao waliolala katika kristo wamepotea. Kama katika maisha haya tumemtumaini kristo, sisi tu maskini kuliko watu wote.

SIKU MUNGU ALIPOTOA RATIBA YA MWISHO WA DUNIA

Adamu na Hawa wazazi wetu wa kwanza baada ya kuanguka dhambini waliahidiwa ukombozi (Mwanzo 3:15) lakini Adamu na Hawa hawakuelewa ni lini ukombozi kamili utapatikana. Henoko aliyetembea na Mungu miaka mia tatu alimwona Yesu akija mawinguni. Lakini hakuelewa itakuwa lini. Si hao tu lakini wazee wote wa imani pamoja na manabii waliona kwa mbali mwisho wa dunia lakini hawakuelewa itakuwaje. (Waebrania 11.13; Daniel 12:8). Baada ya miaka elfu tatu na mia nne hivi tangu dunia iumbwe, Bwana Mungu alitoa ratiba ya mwisho wa dunia. Tunao unabii wa aina mbili. Unabii wa muda mrefu na Unabii wa Nyakati na majira. Unabii wa muda mrefu ni ule ulioanzia mwaka 457-BC ukaishia 1844 AD.

Unabii wa nyakati na majira ndio makusudi yetu ya kujifunza katika kitini hiki. Unabii huu ulianza mwaka 606 BC. Wakati Mfalme Nebukadneza alipoota ndoto ya sanamu kubwa iliyofanana na mwanadamu ambayo ilikuwa na sehemu tano zenye madini tofauti.

Sanamu hii ilikuwa ni kichwa cha Dhahabu, kifua cha fedha, kiuno cha Shaba, miguu ya chuma, nyayo za mchanganyiko wa chuma na udogo. Na katika muhtasari wa ndoto hiyo Daniel alisema hii ni ratiba ya mwisho wa dunia. Lakini yuko Mungu Mbinguni afunuaye siri, naye, amemjulisha Mfalme Nebukadneza mambo yatakayokuwa siku za mwisho. basi Mungu aliye mkuu amemjulisha Mfalme mambo yatakayokuwa baadaye; na ndoto hii ni ya hakika, na tafsiri yake ni thabiti. Daniel 2:28, 45 Sehemu ya 2. Hivyo ndiyo kusema tangu mwaka 606 BC ratiba iko wazi hadi mwisho wa dunia.

Katika Kitabu cha GC. ukurasa 594 Nabii anasema, hivyo unabii wa mambo ya mbele umefunuliwa mbele yetu wazi kama ilivyofunuliwa kwa Mitume kwa maneno ya Kristo. Matukio yanayoambatana na kufungwa mlango wa rehema na kazi ya matayarisho kwa ajili ya wakati wa taabu, yameelezwa wazi. Lakini watu wengi hawana ufahamu zaidi juu ya kweli hizi muhimu kana kwamba hawakufunuliwa. Shetani anachunga kunyanganya kila mvuto ambao utawafanya kuwa na hekima katika wokovu, wakati wa taabu utawakuta hawajajiandaa. Hata wasafiri wa dunia hii wanaposafiri wanatazama saa zao au jua kuelewa ni wakati gani basi lao au gari moshi litaondoka, ili kasi yao ya matayarisho ilingane na wakati uliobaki. Sisi pia ni wasafiri wa kwenda mbinguni hebu tutazame saa yetu ambayo ni unabii, kama ifuatavyo:

Daniel 2.

606 BC 538 BC Kichwa cha Dhahabu Utawala wa Babeli
538 BC 331 BC Kifua cha fedha Utawala wa Umedi na Uajemi.
331 BC 168 BC Tumbo la Shaba Utawala wa Wayunani.
168 BC 476 AD Miguu ya Chuma Utawala wa Rumi ya kipagani.
476 AD Hadi mwisho wa dunia Nyayo za Chuma na Udongo
mnyama wa kutisha nusu Chuma na nusu Udongo
Falme zilizogawanyika.

HABARI KAMILI KUHUSU RATIBA YA MWISHO WA DUNIA

Mungu hakupenda watu wake wawe gizani. Amefanya kila njia kuwafahamisha ili wasiangamie. Hivyo ili wewe na mimi tusiangamie kwa kukosa maarifa. (Hosea 4:6) Mwenyezi Mungu aliendelea kuwafahamisha watu wake, katika Daniel sura ya Saba. Katika sura hii Daniel mwenyewe aliona ndoto wakati wa usiku. Daniel aliona wanyama wanne.

Bwana Mungu hakupenda watu wake wawe gizani. Amefanya kila njia kuwafahamisha watu wake wasiangamie. Kwa hiyo ili wewe na mimi tusiangamie tusome neno la Mungu kwa makini.

Katika kitabu cha (Amosi 3:7) anasema Hakika Bwana Mungu hatafanya neno lolote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake. Na (Hosea 4:6) anasema watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe.lakini kwa wote wanaohitaji kupata maarifa Mungu anasema katika kitabu cha (Habakuki 2:2,3) Bwana akajibu akasema iandike njozi ukaifanye iwe wazi sana katika vibao ili asomaye apate kusoma kama maji. Maana njozi hii bado ni kwa wakati uliamriwa, inafanya haraka ili kufikia mwisho wake, wala haitasema uongo, ijapokawia, ingojee, kwa kuwa haina budi kuja, haitakawia.

Mungu aliendelea kuwafahamisha watu wake mambo yajayo katika sura ya Saba ya kitabu cha Danieli. Katika sura hii Danieli mwenyewe aliona katika ndoto ya usiku. Danieli aliona Wanyama wanne.

Ufuatao ni muhtasari wa ndoto ya Danieli 7.

Simba Utawala wa Babeli 606 BC hadi 538 BC
Dudu Utawala wa Umedi na Uajemi 538 BC hadi 331 BC
Chui Utawala wa Wayunani 331 BC hadi 168 BC
Mnyama wa kutisha Utawala wa Kirumi na tawala zilizogawanyika 168 BC-hadi Mwisho wa dunia.

Hapa tunaona Daniel sura ya 7 inafanana na Daniel sura 2 tofauti yake tu ni kwamba Daniel sura ya 2 ina sehemu 5 ambapo Daniel sura ya 7 ina wanyama wa nne Mnyama wa nne anawakalisha sehemu mbili za mwisho ndiyo maana anaonekana ni mnyama wa kutisha. Kwa sababu anawakalisha falme nyingi.

Kwa hiyo ukiunganisha sura ya 2 na sura ya 7 ya Daniel inakuwa kama ifuatavyo:-

606 BC hadi 538 BC Kichwa cha Dhahabu Simba Babeli
538 BC hadi 331 BC Kifua cha fedha Dubu uwamedi na uwajemi
331 BC hadi 168 BC Chui Tumbo la Shaba uyunani
168 BC hadi Mwisho wa Dunia Miguu ya Chuma na nyayo za chuma na udongo utawala wa Rumi ya kipagani na falme zilizogawanyika.

MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA

Daniel 7:17 Wanyama hawa wakubwa walio wanne ni wafalme watakaotokea duniani Kwa hiyo maana ya neno mnyama katika biblia ni utawala unaotawala dunia yote (dola au empire)
Daniel 7:19 kisha nalitaka kujua maana ya yule mnyama wa nne, aliyekuwa mbali na wenziwe wote, mwenye kutisha sana..
Daniel 7:24 Na habari za zile pembe kumi, katika Ufalme huo wataondoka wafalme kumi…..

Mnyama wa nne ndiye mnyama pekee ambaye ana pembe kumi; ambapo wengine hawana pembe hata moja. Pembe hizi kumi ni Falme kumi ambazo zilitawala kwa wakati mmoja kila moja kisehemu cha dunia Daniel 7:24. Na habari za zile pembe kumi katika ufalme huo wataondoka wafalme kumi.. Falme saba kati ya hizo kumi zipo hadi leo nazo ni Uingereza, Ufaransa, Hispania, Ujerumani, Ureno, Uswissi na Italia ambapo karibu zote zimo katika shirika la NATO. Falme hizi zitaungana na Amerika kuwatesa watu wa Mungu. GC 579. Falme tatu kati ya zile kumi haziendelei kuwepo kwa sasa, zilitekwa na utawala wa Upapa. Majina yao kabla hazijatekwa yalikuwa ni Ostrogoths, Vandals na Heruli.

Mnyama wa nne wa Daniel 7 ana sehemu zifuatazo:-
Rumi ya kipagani Miguu ya Chuma 168 BC – 476 AD Daniel 2:40
Falme zilizogawanyika nyayo za chuma na udongo 476 AD 538 AD Daniel 2:41; 7:24
iii) Utawala wa Kipapa Nyayo za Chuma na Udongo:-
538 AD 1798 AD Daniel 7:24 Ufunuo 13:11-16.
iv) Falme zilizogawanyika-nyayo za chuma na udongo 1798 AD Amri
ya Jumapili Ufunuo 13:11-16

Falme hizi kumi zilitawala kuanzia mwaka 476 AD 538 AD wakati ambapo alitokea Mfalme Constantino wa Rumi akiwa mpagani akiabudu jua siku ya Jumapili akaamini kuwa Mkristo. Wakristo wote wa wakati huo walikuwa wakiabudu siku ya Sabato (Jumamosi) Hivyo mara tu baada ya mfalme Constantino kuamini kuwa mkristo waumini na viongozi wa Kikristo walimheshimu Constantino kuliko kumheshimu Yesu kwa kwenda kumbatiza Constantino kwa maji ya kunyunyizia kichwani na hivyo huo ulikuwa ubatizo wa kwanza wa kunyunyizia maji kichwani. Kumbuka kuwa Yesu alitoa kielelezo kwa kubatizwa kwa kuzamishwa katika maji mengi kule katika mto wa Yordani ili asije mtu mwingine akaleta ubatizo tofauti. Ndipo alipoona kuwa ameheshimiwa, Mfalme Constantino alitoa pendekezo ya kwamba, `alikuwa anaabudu jua siku ya Jumapili (Sun-day) na warumi wengi. Hivyo aliliomba kanisa la Kikristo libadili siku ya kuabudu, badala ya Sabato (Jumamosi) iwe Jumapili; bila kuelewa ya kwamba anatimiza unabii wa Danieli 7:25. . Naye ataazimu kubadili majira na sheria na Isaya 34:4-6; 19-20 Dunia inaomboleza inazimia, ulimwengu unadhoofika unazimia;.. kwa maana wameziasi sheria, wameibadili amri, wamelivunja agano la milele Kutoka 31:16 Kwa ajili ya hayo wana wa Israeli wataishika Sabato, kuiangalia sana hiyo Sabato katika vizazi vyao vyote ni agano la milele.


Wakristo wengine walikataa kuibadili amri ya nne katika amri kumi za Mungu. Hivyo Mfalme Constantino aliingilia kati kulitawala kanisa ili kuwaadhibu wapinzani. Watu zaid ya millioni hamsini waliuawa na utawala huo kati ya mwaka 538 AD -1798 AD. Mfalme Constantino alidai ya kwamba wapumzike siku ya Jumapili lakini huku wakimwamini Yesu badala ya kuliamini jua, huku akidai ya kwamba ili Warumi wote wawe wakristo. Na hivyo kanisa la Kikristo likabadilika jina na kuitwa kanisa Katoliki la Kirumi (Roman Catholic Church).

Neno Katoliki maana yake wote Na hivyo jina Kanisa Katoliki la Kirumi maana yake Kanisa la Warumi wote. Sasa ,leo mimi nashangaa kuona watu wengi ulimwenguni wanajiunga na kanisa la Warumi wote japokuwa wao sio Warumi. Hata mimi nilikuwamo humo lakini baada ya kugundua nilitafuta kanisa la Mungu sio la Warumi. Kwa vile Constantino sasa alikuwa na Kofia mbili akitawala Serikali na Kanisa; jina la utawala (Tittle) likabadilika badala ya kuitwa mfalme akaiitwa Papa. Na hivyo wengine waliofuata baada yake yeye walirithi jina hilo hadi mwaka 1798 wakati jeshi la Wafaransa chini ya jenerali Berthier liliingia Roma kumchukua mateka aliyekuwa Papa wakati huo Papa Pius VI na akafa uhamishoni Ufaransa katika mwaka 1799 Agosti Time Running Out Uk. 76.

Biblia inasema Nikaona kimoja cha vichwa vyake kama kwamba kimetiwa jeraha la mauti, na pigo lake la mauti likapona Ufunuo 13:3 Jeraha lilipona mwaka 1929 wakati Mussolini aliposaini mkataba na

v) Upapa katika kivuli cha Uprotestanti na Marekani:-
Nyayo za chuma na udongo Amri ya Jumapili kuja kwa Yesu mara ya pili au mwisho wa dunia Ufunuo 17:18.

Upapa ulitawala kuanzia wakati wa Mfalme Constantino ambayo ilikuwa 538 AD hadi 1798 AD wakati Papa Pius VI Alitekwa na majeshi ya kifaransa na kuuawa kule Ufaransa. Katika muda huo wote watu waliokuwa wakijitokeza kutunza Sabato ambayo ni amri ya nne katika amri kumi za Mungu walikuwa wakiuawa katika zile nchi zote zilizokuwa? nyakati hizo ambazo tumeziona hapo juu. Hata Papa John Paulo wa II
, amekiri wazi katika vyombo vya habari ya kwamba kwa `kweli kanisa Katoliki liliua watu hapo zamani.`

Hivyo kuanzia 1798 hadi leo ni utawala wa mgawanyiko na kisha wakati wowote kuanzia sasa Jumapili itaingizwa tena kama ilivyokuwa wakati wa Constantino lakini sasa wahusika watakuwa wengine kama itakavyojieleza hapo chini.

Ufuatao sasa ni muhtasari wa matukio kuanzia mwanzo hadi mwisho wa ratiba ya mwisho wa dunia:-
606 BC hadi 538 BC Kichwa cha Dhahabu simba Babeli – ufalme wa kwanza
Ufunuo 17:9-11; Daniel 7:4
538BC hadi 331 BC Kifua cha fedha – Dubu Wamedi na Uajemi Ufalme wa pili ufunuo 17: 9-11; Danieli 7: 5
331 BC hadi 168 BC Kiuno cha shaba- chui- Wayunani- ufalme wa tatu ufunuo 17:9-11; Daniel 7:6.
168 BC hadi 476 AD Miguu ya chuma – mnyama wa kutisha Rumi ya kipagani
ufalme wa nne- Daniel 7:7; Ufunuo 17:9-11.
476 AD hadi 538 AD Nyayo za chuma na udongo mnyama wa kutisha falme
zilizogawanyikaufalme wa tano Daniel 7:24;Ufunuo 17:9-11
538 AD hadi 1798 AD Nyayo za chuma na udongo Mnyama wa kutisha Upapa
ufalme wa sita Daniel 7:24;Ufunuo 13:1-10;Ufunuo 17:9-11
na mwingine ataondoka baada ya hao— Ufalme wa sita.
1798 AD hadi Amri Amri ya JumapiliMnyama wa kutishafalme zilizogawanyika Ufalme wa saba- Daniel 7: 24.
Amri ya Jumapili hadi Mwisho wa Dunia Nyayo za chuma na udongo Mnyama wa kutisha Upapa katika kivuli cha uprotestant na Marekani Daniel 7:7; Ufunuo 17:9-11 ufalme wa nane na wa mwisho ufunuo 13:11-16.

Kwa wakati huu tulio nao tunangoja tu utawala wa nane ili Yesu aje. Ili kufahamu utawala wa nane wa ufunuo 17:11 utaingiaje, inafaa kwanza kuelewa habari za wanyama wawili wa ufunuo 13. Hapa ndipo miongoni mwa watu wengi wanapokosea kuelewa unabii. Kukosa kuelewa unabii kwa usahihi ni hatari ya kupotea. Nabii anasema, Nalisikia mmoja akisema: tulijua kuwa Hukumu za Mungu zitakuja juu ya nchi, lakini hatukujua kwamba zingekuja mapema hivi; wengine, kwa sauti za maumivu makali, wakasema. Mlijua! Mbona basi hamkutuambia? Sisi hatukujua. Kila upande nikasikia maneno ya laumu yakisemwa 9T 28.

Wengi hata miongoni mwa Waadventista Wasabato hawaelewi jinsi Amri ya Jumapili itakavyoingizwa. Wengi wanachanganya mafungu ya Ufunuo 13. Ufunuo 13:1-10 ni utawala wa upapa ambao ulianzia mwaka 538 AD 1798 AD kama tulivyoona huko nyuma. Lakini Ufunuo 13:11-16 ni Utawala utakaoweka amri ya Jumapili ambapo hapo nyuma tumesema ni utawala wa nane ambao utakuwa ni Taifa la Marekani na wala sio Papa kama wengi wanavyodhani. Watu wengi wanadhani kwamba Papa atatangaza amri ya Jumapili lakini siyo kweli: Wala hatakuwa kiongozi wa dunia yote kama watu wanavyodhani. Na Hivyo watu wengi wanakashifu Wakatoliki badala ya kuwavuta kwa Yesu. Wakati wa mahubiri yetu, tusiingize uadui usio wa lazima katika mawazo yao, kwa kufikiri kuwa papa atatangaza amri ya Jumapili. Hii haina maana kwamba Upapa hauna hatia katika kuibadili Sabato ya Biblia na kuipeleka Jumapili, la hasha! Bali ninachoongelea hapa ni yule atakayetangaza Amri ya Jumapili katika siku zetu hizi kulingana na Neno la Mungu sio papa katika Ufunuo 13:14 Naye awakosesha wale wakaao juu ya nchi, kwa ishara zile alizopewa kuzifanya mbele ya huyo Mnyama. Kumfanyia sanamu yule mnyama, aliyekuwa na jeraha la upanga naye akaishi.

Na hata Hivyo washiriki wengi Wakatoliki wanaabudu Jumapili bila kuelewa maana hawajaelezwa. Hivyo tunatakiwa kuwaeleza kwa moyo wa upendo katika mahubiri yetu, tusiwaeleze kwa chuki na jazba juu ya wajibu wao kuitii Sabato ya kweli ya Mungu. Ndipo wakikataa wanaingia katika hatia. Lakini wengi walio katika kanisa la Katoliki ni watu wa Mungu na wako tayari kusikia sauti ya mchungaji mwema Yesu Kristo ambaye ndiye Bwana wa Sabato nao watatoka na kuitunza Sabato ya kweli. wako tayari kumtii Mungu kuliko mwanadamu. Yesu mwenyewe anasema (Yohana 10:16) Na kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta na sauti yangu wataisikia; kisha kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja Neno la Mungu linasema:- kuna wakristo wengi Wakatoliki wanaoishi vizuri zaidi kulingana na nuru yote waliyo nayo kuliko wengi wanaodai kuamini ukweli wa leo na Mungu atawapima na kuwahakikisha kama anavyotupima na kutuhakikisha sisi Manuscript 14,1887.

Mungu anao watoto wengi wao wapo katika makanisa ya Kiprotestanti na sehemu kubwa wapo katika makanisa ya Katoliki ambao wanatii nuru yote waliyo nayo na kutenda vizuri kile wanachokielewa kuwa ni kweli, kuliko sehemu kubwa ya Waadventista Wasabato ambao hawaishi kulingana na nuru waliyo nayo II SM 386. Pia neno la Mungu linaendelea kusema kuwa: kuna hatari kwamba wachungaji wetu watasema mengi dhidi ya Wakatoliki na kuwashambulia dhidi yao wenyewe na kuleta chuki kubwa ya kanisa hilo. Evangelism Uk. 574. Lakini watu wote wanaoitunza Jumapili bila kuelewa, leo wanaposoma habari hii njema ya wokovu juu ya wajibu wa kuitunza Sabato ya Biblia ambayo ndiyo sauti ya Mungu kwa wanadamu wote, basi, Usifanye moyo kuwa mgumu bali moja, tii sauti ya Roho Mtakatifu na kuitunza Sabato ya kweli ambayo ni Jumamosi. La sivyo sasa utakuwa na hatia maana sasa umeelezwa.

JINSI AMRI YA JUMAPILI ITAKAVYOINGIZWA

Amri ya Jumapili itaingizwa kwa hatua mbili. Hatua ya kwanza inaitwa amri ya Jumapili ya kitaifa (National Sunday law). Hatua ya pili itakuwa ni amri ya Jumapili ya kimataifa (International Sunday Law).

AMRI YA JUMAPILI YA KITAIFA (NATIONAL SUNDAY LAW)

Ufunuo 13:11 sehemu ya mwisho inasema akanena kama joka! Katika zile zama za giza ambazo ni kuanzia mwaka 538 AD hadi 1798 AD mhusika mkuu wa tukio au wa drama ya kuibadili Sabato ya kweli ambayo ni Jumamosi na kuipeleka Jumapili ulikuwa ni utawala wa upapa ufunuo 13:1-10. Lakini mbele yetu mhusika mkuu katika kutimiza unabii wa kutangaza amri ya Jumapili atakuwa ni Marekani na Uprotestanti wa Marekani ufunuo 13:11-16. Amri ya Jumapili haitatangazwa na Papa kama watu wengi wanavyofikiri. Narudia kusema jambo hili ili likae vizuri na kueleweka na watu wa Mungu. Tatizo si kwamba kuelewa kuwa kutakuwa na amri ya Jumapili lakini tatizo ni jinsi gani amri ya Jumapili itakavyo ingizwa. Wazazi wetu Adamu na Hawa walielewa kuwa tunda la kujua mema na mabaya walikatazwa na Mungu kuwa wasile; lakini hawakuelewa jaribu litakavyoingia.

Ili kuelewa mambo yatakavyokuwa kuhusu kuingizwa kwa amri ya Jumapili katika siku zetu hizi za mwisho, tunatakiwa kujifunza kwa uangalifu kitabu cha ufunuo sura 13. MR Vol. I ukurasa 91-92. Inasema Hebu watu wote wasome kitabu cha ufunuo sura 13 kuwa inahusika na kila mwanadamu wakubwa na wadogo..

Wakati vitabu vya Daniel na Ufunuo vitakapoeleweka vizuri, waumini watakuwa na uzoefu tofauti kabisa wa dini TM 114.
Wale wanaokula mwili na kunywa damu ya Mwana wa Mungu wataleta kutoka katika vitabu vya Daniel na Ufunuo ukweli ule ambao umevuviwa na Roho Mtakatifu. Wataaanza kuwa na nguvu ya utendaji ambayo haiwezi kuzimwa TM 116

Kuna hitaji kubwa la kujifunza kwa undani Neno la Mungu hasa vikitiliwa umuhimu wa pekee kwa Vitabu vya Danieli na Ufunuo kuliko wakati wowote wa historia ya kazi yetu. Tunaweza kusema mambo fulani machache yanayohusu nguvu ya Kirumi na upapa, lakini tunahitaji kutilia maanani zaidi kuona manabii na mitume walichokiandika chini ya uvuvio wa Roho wa Mungu CW 45,461896.

Mnyama aliye mfano wa chui wa Ufunuo 13:1-10 anawakilisha utawala wa upapa ulioanza mwaka 538 AD hadi 1798 AD Gc 439 katika kitabu cha GC uk. 578-9 inasema, Ufunuo 13:11-16 utatimizwa kwa kuwekwa amri ya Jumapili kwa upande wa Marekani. Pia katika kitabu cha IT 223 inasema Mnyama aliye mfano wa Mwana Kondoo mwenye pembe mbili ataweka jaribu la amri ya Jumapili. Mnyama mwenye pembe mbili aliye mfano wa Mwana Kondoo ndiye Marekani, atakayeweka amri ya Jumapili na siyo papa kama baadhi ya Waadventista wanavyofikiri. Warumi wenyewe wanasema kwamba; kutunza Jumapili kwa Waprotestanti ni kuheshimu mamlaka ya Kanisa la Kirumi (Mgs segue, plan talk about the protestantisim of today uk. 213).

KAZI YA WAKATOLIKI NA WAPROTESTANTI:

Pia tumechukua msimamo kwamba kabla ya kufungwa kwa rehema, hatua zingekuchukuliwa kuunganika kuhusu swali la kutunza Jumapili, ya kwamba wakati Waprotestanti watakapolazimisha kutunza siku ya kwanza ya Juma, Wakatoliki watatumia mvuto wao kwa kuendeleza jambo hilo. Na hivyo bonde lile ambalo limeendelea kuwepo kati yao kwa miaka mingi litaunganishwa na watakutana juu yake kushikana mikono na kukaribishana kwa moyo . E.G. White Article Vol. 2 P. 273

Ukisoma katika kitabu cha Wakati Unakwisha uk 75,76 kinasema Je ndiyo kusema makanisa yote ya Kikristo yatarudi na kuunganika na kanisa ambalo ni mama? Hapana, wako wengine ingawa wanapendelea Muungano huo, hawataweza kwenda mbali kiasi cha kumkiri papa kama wakatoliki wanavyomkiri. Watu kama hao hawataunganika na makanisa yasiyo kuwa ya Katoliki, bali yanayotumika badala ya Katoliki, kama muungano wa makanisa ya Ulimwengu. Makundi mawili haya, yaani Romani Katoliki na Katoliki iliyotengenezwa ( yaani uprotestanti wa jumapili) yataendelea sambamba yakifanana katika mafundisho na hali zao na makusudi yao, hata itakuwa vigumu kuyapambanua moja litakuwa nakala ya jingine mpaka kundi dogo linalopenda mafundisho ya Biblia likiangalia kundi hili kubwa mno ambalo limeenea na kujulikana sana, ghafla litatambua wazi mnyama na sanam yake.

Biblia na Roho ya unabii ambavyo ndivyo vyanzo vya wanadamu vya kuaminika vinasema serikali ya Marekani na Waprotestanti wa Marekani watatangaza amri ya Jumapili katika nchi yao. GC.580 nabii anasema Ni ajabu katika werevu na udanganyifu wa ujanja uliomo ndani ya kanisa Katoliki. Linaweza kuona na kuelewa kitakachokuwa, kinangojea tu muda wake unaofaa, likiona kwamba makanisa ya Kiprotestanti ya Marekani watatoa heshima kwa kanisa la Katoliki katika kuikubali kwao Sabato ya uongo ya Jumapili na kwamba wanajiandaa kuilazimisha kwa njia ileile ambayo kanisa la Katoliki ilifanya katika siku zilizo pita.

GC 578-579 inasema Nalionyeshwa kwamba Marekani ndiyo mamlaka inayowakilishwa na mnyama mwenye pembe mbili mfano wa Mwana Kondoo, na kwamba unabii huu utatimizwa wakati Marekani itakapolazimisha amri ya Jumapili ambayo Rumi inadai kuwa ni alama ya ukuu wake Hapa tunaona kuwa papa hatoi sauti yake kutangaza amri ya Jumapili. Marekani haitakuwa peke yake GC 579 inasema; Lakini katika kutoa heshima hii kwa upapa Marekani haitakuwa peke yake. Mvuto wa Rumi katika nchi zile ambazo kwanza zilitambua utawala wake bado upo Na hizi nchi ni zile pembe kumi ambazo siku hizi tunaita washirika wa Marekani au Marekani na washirika wake. Kushurutishwa kwa kuishika Jumapili katika nchi ya Amerika kutakuwa ni shurutisho la kuabudu mnyama na sanamu yake. GC 449. Athari yake ni kwamba itakapotangazwa amri ya Jumapili kule Marekani rehema itakuwa imefungwa kwa Wasabato katika ulimwengu wote. Tutaona zaidi kwa kadiri tunavyoendelea kujifunza katika kiti hiki. Unaweza kuielezea kwa mtazamo wa makundi mawili ndani ya Kanisa ili msomaji asielewe kuwa wasabato watakataliwa!

CHANZO CHA KUANZISHA AMRI YA JUMAPILI MAREKANI

Viongozi wa kanisa na serikali wataungana kutoa rushwa, kushawishi au kulazimisha madaraja yote ya watu kuheshimu Jumapili. Kukosekana kwa mamlaka ya Mbinguni kutafuatiwa na vitendo vya ukandamizaji, uhujumu wa kisiasa, kuharibu upendo wa haki na kujali ukweli, na hata katika Amerika iliyo huru, watawala na wanasheria, ili kutafuta kupendwa na umma, watajirahisisha kwa madai ya kulazimisha amri ya Jumapili GC 592.

Kwa kutafuta umaarufu na kupendwa na watu, Wanasheria wa Marekani watakubali na kupitisha madai ya amri ya Jumapili ST451
Kuna wengi hata wale waliojiingiza katika mpango huo wa kuilazimisha amri ya Jumapili ambao wamepofushwa kuhusu matokeo yatakayofuata katika kufanya hivyo Hawaoni kwamba watapambana moja kwa moja dhidi ya uhuru wa dini. Wako wengi ambao hawafahamu madai ya Sabato ya Biblia na msingi potofu ambao fundisho la Jumapili linasimama ST 711

Wanafanya katika upofu, Hawaoni kwamba kama Serikali ya Kiprotestanti inaacha kanuni iliyo wafanya wawe huru. Taifa lenye uhuru na kujitegemea na kwa njia ya marekebisho ya sheria italeta kanuni itakayopendekeza uongo na madanganyifu ya upapa wanaingia katika masikitiko ya Rumi ya miaka ya giza RH Extra 12-11-1888 P.4
Wakati unakuja amri ya Mungu kwa namna ya pekee itakapopigwa marufuku katika nchi yetu (Marekani) watawala wa taifa letu (Marekani) kwa njia ya wanasheria itakapowekwa sheria ya kuzuia/kufunga dhamira za watu kuhusiana na uhuru wao wa dini. Kwa kulazimisha kuabudu Jumapili na kuleta nguvu ya kukandamiza dhidi ya wale wanaoitunza Sabato ya kweli ya Biblia; amri ya Mungu kwa nia na makusudi yote itapigwa marufuku katika nchi yote. Itapigwa marufuku katika nchi yetu (Marekani) na uasi wa kitaifa utafuatiwa na uangamivu. RH 12-18-1888 P.785 9-7BC 977.

AMRI YA JUMAPILI KIMATAIFA (INTERNATIONAL SUNDAY LAW)

Baada ya Marekani kutangaza amri ya Jumapili kwa nchi yake nchi zingine zitafuata mfano wa Marekani. Mataifa mengine yatafuata mfano wa nchi ya Amerika. Ijapokuwa inaongoza hata hivyo shida itawapata watu wetu katika sehemu zote za ulimwengu. 6T 395.

Hapa tunaona kwamba amri ya Jumapili ya kitaifa na kimataifa itakuwa kama jinsi ambavyo vyama vingi vilivyoingia katika nchi za ulimwengu ambapo chanzo chake ni Serikali ya Marekani. Nchi zingine ulimwenguni zilifuata mfano wa Marekani na wala hazikulazimishwa bali ni kwa hiari zilikaribisha mpango wa vyama vingi katika nchi zao ndivyo itakavyokuwa kwa amri ya Jumapili; ambapo pia chanzo chake kitaanzia Marekani kama tulivyojifunza na hatimaye ndipo zingine zitafuata mfano wa marekani.

Kama ilivyokuwa katika demokrasi ya vyama vingi kuna baadhi ya nchi zingine hazikupokea mfumo wa vyama vingi kama vile Uganda, Cuba, na nchi zingine za kiarabu; Pia hata wakati wa kuwekwa kwa amri ya Jumapili viongozi wa nchi fulani hazitakubali kufuata mfano wa Marekani kama nabii anavyosema GC 610-611 Lakini kwa kadri Yesu atakavyokuwa anaendelea kama mpatanishi katika chumba cha patakatifu pa patakatifu huko mbinguni kushikilia kwa mvuto wa Roho Mtakatifu kutasikiwa kwa watawala na watu.

Hali hii kwa kiasi fulani itaendelea kutawala sheria za nchi. Isingekuwa sheria hizo hali ya ulimwengu ingekuwa mbaya sana kuliko ilivyo sasa wakati wengi wa viongozi wetu wakiwa mawakala hai wa shetani Mungu pia anao mawakala wake miongoni mwa viongozi wa taifa. Adui anakwenda kwa watumishi wake kupendekeza hatua itakayopunguza sana kasi ya kazi ya Mungu; lakini Viongozi wa nchi waliomwogopa Bwana walivutwa na malaika watakatifu kupinga mapendekezo ya kuiweka Jumapili kwa maswali yasiyojibika. Hivyo watu wachache watashikilia kwa muda uovu uliokuwa ukija kwa nguvu. Upinzani wa adui wa ukweli utazuiwa ili ujumbe wa malaika wa tatu ufanye kazi yake. Wakati onyo la mwisho litakapotolewa utachukua usikivu wa watu hawa viongozi ambao Bwana anafanya kazi kupitia kwao na baadhi yao wataukubali ujumbe na watasimama na watu wa Mungu wakati wa taabu.

KUFUNGWA KWA MLANGO WA REHEMA

Kufungwa kwa mlango wa rehema ni jambo nyeti kuliko sehemu yoyote katika unabii na katika historia Somo hili linatakiwa kufundishwa mbele za watu kwa maumivu makali; Ukweli halisi unatakiwa ufundishwe si mbele za ulimwengu tu bali katika makanisa yetu pia; kwamba siku ya Bwana itafika ghafla bila kutazamia Onyo la kuogofya la unabii limehubiriwa kwa kila mtu. Hebu asije mtu akafikiri kuwa yuko salama kutoka katika hatari ya kughafilishwa. Hebu tafsiri ya mtu yoyote ya unabii isiwachukulie nafasi ya kuwa na ufahamu wa matukio yanayoonyesha kwamba tukio hili kubwa la mwisho wa dunia liko karibu. FE 336.

Katika kitabu cha 1Wathesalonike 5:1-5 anatukumbusha ya kwamba inabidi tusivamiwe ghafla kama mwivi. Hapa anaelezea kufungwa kwa mlango wa rehema. Yesu alijitahidi sana kutueleza jinsi mambo yatakavyokuwa na hasa kuhusiana na kufungwa kwa mlango wa rehema. Mathayo 24:1-3 Yesu aliwaambia wanafunzi wake kwamba Yerusalem itaharibiwa halitasalia jiwe juu ya jiwe. Hivyo wanafunzi wake walidhani kwamba mwisho wa dunia na kuharibiwa kwa Yerusalemu na hekalu lake itakuwa siku moja. Wakamuuliza maswali yanayohusu mambo yote mawili. Mathayo 24:3. Na Yesu aliwajibu jibu moja kwa maswali hayo mawili ingawa matukio hayo yatatokea kwa wakati tofauti na mtazamo tofauti.

Unabii wa Mathayo 24 unaweza kugawanywa katika sehemu mbili ili upate kueleweka vizuri kama ifuatavyo:-
Mathayo 24: 4-14 ni unabii unaoelezea magonjwa, vita, matetemeko n.k. huu unaitwa unabii unaoweza kueleweka na kila mtu hata walevi wanaelewa matukio hayo ni ya mwisho wa dunia. Kwa hiyo sehemu hii inaitwa unabii unaoeleweka na kila mtu. (Common Prophecy). Lakini Mathayo 24:15-22 ni unabii ambao unaohusiana na chukizo la uharibifu ambalo tutalifuatilia maana yake baadaye. Huu unabii ni kwa ndugu ambao Paulo amewaandikia katika 1Wathasalonike 5:1-5 ni unabii wa pekee kwa watu wa pekee (Unique prophecy for unique people).

MAANA NA NAMNA YA KUFUNGWA KWA MLANGO WA REHEMA

Kwanza tunatakiwa kuelewa ni nini maana ya kufungwa kwa mlango wa rehema. Yesu alituelekeza namna ya mlango wa rehema ulivyofungwa wakati wa Nuhu. Mathayo 24:36-41.

Baada ya kuhubiri kwa muda wa miaka 120 Nuhu hakupata mwongofu hata mmoja isipokuwa yeye na watu wa nyumbani mwake watu wanane tu. Wengine wakihubiri wiki tatu wakakosa mtu wanakata tamaa. Lakini Nuhu alihubiri miaka 120 alipotoa wito wa mwisho akajikuta yeye na jamaa yake tu. Lakini kazi yake ilikubalika Mbinguni. Kitu cha maana kazi yako ikubalike Mbinguni na siyo machoni pako mwenyewe. Luka 10:20.

Wakati wa Nuhu mvua ilikuwa hainyeshi walikuwa wakiotesha mazao yao kwa umande. Na Hivyo ilikuwa vigumu kwa watu wa wakati ule kuamini kwamba mvua itanyesha kwa hiyo waliomba dalili ya mvua; Nuhu aliwaambia dalili ya mvua ni mawingu. Watu wa wakati wa Yesu walimwuliza Yesu dalili. Hivyo watu walingojea mawingu ndipo wangeingia ndani ya safina. Na kuna wengine wanangojea siku zetu hizi amri ya Jumapili ndipo waanze kazi hapo wanakosea. Soma kitabu cha kutayarisha njia No.2 Uk.66.

Kabla ya mawingu Nuhu aliambiwa na mwenyezi Mungu na jamaa yake waingie ndani ya safina hivyo, ilikuwa ni ghafla. Mwanzo 7:1 Hata jamaa yake ilishangaa ujumbe huu wa ghafla kuingia ndani ya safina lakini waliingia ndani ya safina kwa imani wala si kwa kuona mawingu. Waebrania 11:7. Mara tu baada ya Nuhu na jamaa yake kuingia ndani ya safina Malaika alitoka mbinguni na kufunga mlango kisha akaenda na ufunguo. Hii ilikuwa ni ishara ya kwamba Nuhu na ndugu zake walifungiwa ndani ya safina tayari kwa kuokolewa na watu wote waliobaki walifungiwa nje ya safina tayari kwa kupotea au kuangamia kwa maji.

Nuhu aliingia ndani ya safina siku saba kabla ya gharika. Hii ina maana kwamba mlango wa rehema ulifungwa siku saba kabla ya gharika lakini bila wakazi wa ulimwengu kujua na wala Nuhu mwenyewe.
Yesu alisema kwamba kama ilivyokuwa wakati wa Nuhu ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Siku ya saba mawingu yalionekana lakini hawakuweza kuingia ndani ya safina maana mlango ulifungwa siku zilizopita. Baada ya kuwekwa amri ya Jumapili ya kitaifa maungamo yetu hayatakuwa na maana tutakuwa tumechelewa. Maandalizi ni ya wakati huu.

JE KWETU SISI MLANGO WA REHEMA UTAKUWAJE?

Mathayo 24:15 Anaelezea chukizo la uharibifu. Watu wengi pia mafungu haya wanayachanganya wengine wanasema mafungu hayo yanahusu wakati wa Yerusalemu ilipoharibiwa. Lakini hebu tuone ukweli ni upi? Chukizo la uharibifu Dr. Luka amesema kwa lugha rahisi zaidi. Luka 21:20 Anasema Mji wa Yerusalemu utakapozungukwa na majeshi katika kitabu cha Great Controversy au Pambano Kuu sura ya kwanza inaeleza jinsi mji wa Yerusalemu ulivyoharibiwa. Kwanza mji wa Yerusalemu ulizungukwa na majeshi ya Kirumi chini ya jemedari Sestus.

Katika mafungu hayo tuliyokwisha yasoma Yesu aliwaonya mtakapoona majeshi yameuzunguka mji wa Yerusalemu wakristo waukimbie mji waliotii walipona lakini wengine hawakutii maagizo hayo mahususi ya Mwokozi wetu walisema mji wa Yerusalemu hautaharibiwa. Majeshi ya Sestus yaliitwa nyumbani hivyo yakaenda na ndipo ulikuwa ni wakati wa Wakristo kuukimbia mji. Wengine walikimbia lakini wengine waliona kama majeshi ya Kirumi yameshindwa kwamba Yerusalemu ni mji mtakatifu wa Mungu. Kumbe mlango wa rehema wa Yerusalemu ulikuwa umefungwa.

Hatimaye majeshi ya Kirumi chini ya Jemadari Tito yalirudi na kuuzunguka mji wa Yerusalemu. Jemedari Tito alitoa mwongozo kwa Jeshi la Kirumi kwamba wauzunguke mji wa Yerusalemu lakini wasiushambulie ili wafe kwa njaa baada ya akiba ya chakula kwisha kilichokuwa ndani ya mji wa Yerusalemu. Kweli baada ya chakula kwisha, wakazi wa mji wa Yerusalemu walikuwa wakitoka nje saa za usiku ili kuiba chakula na askari wa Kirumi waliwashika na kuwassulubisha.

Ukuta wa mji wa Yerusalemu ulizungukwa na misalaba iliyosulubishwa miili ya wana wa Israel. Walitimiza maneno yao wenyewe walipomsulubisha Yesu wakisema Damu yake itakuwa juu yetu na juu ya watoto wetu. Misalaba hiyo haikuishia ukutani bali ilipangwa huku na huku katika barabara iliyopitia katika bonde la Yehoshafati hadi mlima wa Kalvari. Kwa sababu walisema Damu yake itakuwa juu yetu na juu ya watoto wetu Maiti zilipozidi kunuka mwanajeshi mmoja aliasi amri ya Jemedari wake akatupa kiginga cha moto katika hekalu na wote waliojificha humo waliungua na damu yao ilibubujika kama maji. Mji wa Yerusalemu ukaharibiwa na hekalu halikusalia jiwe juu ya jiwe kama Yesu alivyotabiri.

CHUKIZO LA UHARIBIFU LA KISASA

Wengi wanafikiri kuwa Papa kuhamia Yerusalemu itakuwa ni chukizo la uhabirifu lakini siyo kweli. Yerusalemu leo siyo mji mtakatifu bali tunautegemea mji wa Yerusalemu mpya kutoka Mbinguni Ufunuo 21:10-20. Leo mji wa Yerusalemu ni kanisa la Mungu. Kanisa la Mungu lina majina mengi. Sayuni pia ni kanisa la Mungu n.k.

Chukizo la uharibifu linatokea pale giza au watu wamataifa wanapotaka kuwaua watu wa Mungu kwa ajili ya ukweli. Chukizo la uharibifu la kisasa tunapata kutoka katika kitabu cha 5 T 464,465. kama vile Yerusalemu ilivyozungukwa na majeshi ya Kirumi, ilikuwa dalili kwa wakristo wa Yuda kuukimbia mji wa Yerusalemu, hivyo kufanya nguvu katika, nchi yetu katika kutangaza kuwalazimisha watu kuabudu Sabato ya upapa itakuwa ni onyo kwetu. Itakuwa ni wakati wa kuhama miji mikubwa kujiandaa kwenda kwenye miji midogo hatimaye kwenda vijijini kisha katika mapango na milimani.

Na katika kitabu cha 5T451 inasema kama vile majeshi ya Kirumi yalivyouzunguka mji wa Yerusalemu ilikuwa dalili ya wafuasi wa Yesu kuwa uharibifu wa mji wa Yerusalemu umefika ndivyo uasi wa kuwatesa wasabato itakuwa ni dalili kwetu kwamba kipimo cha uvumilivu wa Mungu umefika na kwamba kipimo cha uovu wa taifa letu kimejaa (Marekani) na kwamba malaika wa rehema karibu atahama na hatarudi tena.

Nabii anaposema nchi yetu ina maana nchi ya Marekani maana ndiko ilikuwa nchi yake alimozaliwa na uraia wake ulikokuwa. Hivyo hapa tumeona kutoka katika vyanzo vya kuaminika kwamba chukizo la uharibifu ni amri ya Jumapili ya kitaifa (National Sunday law) taifa la Marekani. Kwa sababu uovu wa kulitesa kanisa la Mungu utaizunguka kanisa kuwatesa na kuwaua watu wa Mungu.

JE MAMBO YATAKUWAJE

Amri ya Jumapili ya kitaifa itakapotangazwa Marekani kwa Wamerikani wenyewe yaani katika nchi yao mlango wa rehema utakuwa umefungwa kwa Waadventista Wasabato katika ulimwengu wote. Biblia inasema katika Ezekiel 9:6 waueni kabisa, Mzee na kijana na msichana na watoto wachanga, na wanawake—-tena anzeni katika patakatifu pangu. Basi wakaanza kwa wazee waliokuwa Mbele ya nyumba. Yeremia 25:29 anasema. Maana, angalieni ninaanza kutenda mabaya katika mji uitwao kwa jina langu, Je! Mtaachiliwa ninyi msiadhibiwe? Hamtaachiliwa uwapige wote wakaao katika dunia asema Bwana wa majeshi. 1Petro 4:17-19 anasema kwa maana wakati umefika wa Hukumu kuanza katika nyumba ya Mungu, na ikianza kwetu sisi mwisho wao wasioitii injili ya Mungu utakuwaje?

7ABC 979 (RH July 5, 1906 chini ya kichwa cha habari kinachosema Namba kubwa ya watu wanaupokea ukweli Wakati wa Hukumu za Mungu za uharibifu ni wakati wa rehema kwa wale ambao hawakupata nafasi ya kuelewa ukweli ni nini. Kwa uvumilivu Bwana atawaangalia. Moyo wake wa rehema umeguswa. Mkono wake bado umeinuliwa kwa ajili ya kuokoa, Wakati mlango umefungwa kwa wale ambao hawakuweza kuingia (wasabato) Namba kubwa ya watu wataruhusiwa kuingia ambao katika siku hizi za mwisho watausikia ukweli kwa mara ya kwanza.

Baada ya kutangaza amri ya Jumapili kitaifa wasabato ambao wataghafilishwa kama mwivi usiku wa manane watafanyaje?

35G134 Wale washiriki waliokutwa wakati wa taabu bila kujiandaa katika kukata kwao tamaa, waliungama dhambi mbele ya wote kwa maneno yenye uchungu mkali wakati waovu watawainukia juu ya shida zao. Maungamo yao yote yalikuwa hayana matumaini wakati Yesu akisimama na kuondoka katika chumba cha patakatifu pa patakatifu ndipo wakati wa taabu utaanza na kesi ya kila mtu itakuwa imekatwa.

Kuna aina mbili za wakati wa taabu nazo ni Wakati wa taabu ndogo na Wakati wa taabu ya Yakobo Wakati wa taabu ndogo ni Wakati wa amri ya Jumapili ambapo Wakati wa taabu ya Yakobo itakuwa ni wakati wa mapigo saba.

Ew 85, 86 Wakati wa taabu ulipoanza, wakati wa taabu unaotajwa hapa si ule wa kumwagwa kwa mapigo saba, bali muda mfupi kabla ya mapigo hayajamwagwa, wakati Kristo akiwa bado ndani ya hekalu. Wakati huo, wakati kazi ya wokovu inafungwa, taabu itaujia ulimwengu na mataifa yatakasirika, lakini yatazuiwa kidogo ili kazi ya malaika watatu isizuiliwe. Wakati huo mvua ya masika au kuburudishwa kwa kuwepo kwa Bwana kutakuja kutoa uwezo au nguvu kwa ajili kilio kikuu cha malaika watatu, na kuwaandaa watakatifu kusimama wakati wa mapigo saba ya mwisho. 7BC 989 Mlango wa rehema utakapofungwa itakuwa ghafla bila kutazamia.

MAMBO MAKUU MANNE YATATOKEA KWA KUFUATANA PAMOJA
Kuwekwa muhuri wa Mungu.
kutangaza amri ya Jumapili
kumwagwa kwa Roho mtakatifu
kuhubiri injili kwa sauti ya kilio kikuu cha usiku wa manane.

WASABATO WATAKUWA MAKUNDI MAWILI

Kundi la kwanza ni kundi dogo linalotii amri za Mungu, Sabato ikiwa mstari wa mbele wa mapambano.
Kundi la pili ni kubwa ambalo litakuwa limemwasi Mungu ingawa walikuwa wasabato.
Je vyanzo vya kuaminika vinasemaje kuhusu makundi hayo mawili? Je. wewe unajiandaa kuwa kundi lipi?
Kundi dogo

G.C. 592 na PK183 Vinasema; Wale ambao wanaheshimu Sabato ya Biblia watashutumiwa kama maadui wa sheria na ataratibu, wanasababisha uasi na uovu na kuita Hukumu za Mungu zije hapa duniani. Katika kujitetea kwao watu hawa wa Mungu watasemwa kwamba ni wabishi wenye kiburi na wapinzani wa mamlaka. Watashitakiwa kwamba hawafai Mbele ya serikali. Wachungaji ambao walikataa wajibu wa kutii sheria takatifu watasimama kwenye mimbara na kuwaambia washiriki kuwa wanapaswa kuitii mamlaka ya nchi kwa sababu imewekwa na Mungu. Walisahau fungu la matendo 5:29 Petro na mitume wakajibu, wakisema, Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu. Ikiwa mamlaka ya nchi inapingana na amri ya Mungu.

KUNDI KUBWA

Katika majumba ya mahakama watunza Sabato watawakilishwa vibaya. Na adui zao au washitaki wao na kushutumiwa. Maneno mazuri yatakayosemwa watakayobadilisha na kutia maneno mengine ambayo hawakusema mambo mabaya sana yatasemwa juu yao. kutakuja wakati ambapo kwa sababu ya kusimamia kweli ya Biblia tutafanywaa kama waasi au wahaini 6T394.

5T450 Shetani ataleta uadui dhidi ya wanyenyekevu wachache ambao katika dhamiri zao wanakataa kukubali mapokeo ya watu na utamaduni unaopendwa na wengi. Watu wenye vyeo na heshima watajiunga na wavunjaji wa sheria za Mungu na kutoa ushauri dhidi ya watu wa Mungu.


GC 608 Matajiri, wenye akili ya kuzaliwa, wenye elimu wataungana na kajazwa na dharau. Watawala watesaji, wachungaji na washiriki wa kanisa watafanya njama kinyume chao kwa sauti na kwa maandishi/kuandika kwa kiburi na vitisho na dharau, watatafuta kuangamiza imani yao.

GC 608 Watu wenye talanta na ambao ni wahubiri wazuri ambao kwanza walikuwa wanafurahia ukweli, walitoa nguvu na uwezo wao kudanganya na kupotosha roho za watu. Wanakuwa adui wakubwa wabaya kwa ndugu zao wa awali. Wakati watunza sabato wanapoletwa mbele ya mahakama kujibu juu ya imani yao, waasi hao wanakuwa mawakala wakubwa wa shetani kupotosha na kuwashitaki watu hawa wa Mungu kwa taarifa za uongo na uchochezi ili kuwafanya viongozi wawe kinyume cha watu hawa wa Mungu ST 450.

JE UTAFANYAJE?

Wakati wowote ule mlango wa rehema unaweza kufungwa, kwa sababu maandiko yanasema itakuwa ghafla bila kutazamia. Watakatifu hatimaye wataelewa siku na saa ya kuja kwa Yesu. Kwa sababu Mungu Mwenyewe atatangaza. Waovu watasikia kama ngurumo hawataelewa, lakini washindi watajua maana ya sauti itakayoeleza siku na saa ya kuja kwa Yesu.

Lakini kuhusu kufungwa kwa mlango wa rehema Neno la Mungu linasema:- CT419 GC490 kutangazwa kwa amri ya Jumapili itakuwa ni alama au dalili ya kufungwa kwa mlango wa rehema (Maalumu kwa wasabato) Shetani hataelewa kufungwa kwa mlango wa rehema GC 618. Taratibu za dini zitaendelea kufanywa na wale ambao ni waovu ambao hawakuwa na Roho wa Mungu GC615.


Wakazi wa dunia hii hawataelewa Wakati wa kufungwa kwa mlango wa rehema GC 615.

Itakuwa kinywa bila kujua kama mwivi ajavyo usiku wa manane GC 491 S.D. 355 1 Wathesalonike 5:3
Tabia haitabadilishwa baada ya mlango wa rehema kufungwa TM 235-6
Rehema imeendelea zaidi kuliko ilivyotazamiwa EW 58, 4T306.
Injili lazima itolewe kwa namna tofauti. CW 97
Ujumbe utatolewa tofauti kuliko hapo awali 6T19

Kuna watu wengi ambao wako kirahisi tu kama vile wamelala, wanasema kama unabii umetolewa kuilazimisha Jumapili, kwa kweli itatolewa, wakifika katika jawabu hilo, wanakaa kimya wakingojea tukio, wakijifariji wenyewe kwa wazo kwamba Mungu atawaokoa watu wake katika siku ya taabu. Lakini Mungu hatatuokoa kama hatutafanya bidii kufanya kazi ambayo ametupatia kufanya katika dunia yetu R.H. Extra 12-24 P.

HITIMISHO

Ikiwa wewe na mimi yanatuingia maneno haya tubadilike haraka kabla ya amri ya Jumapili haijatangazwa kule Marekani. Matukio yanayohusiana na kufungwa kwa mlango wa rehema maandiko yamefunua wazi GC 594. Naam tukijua wakati kwamba saa ya kuamka katika usingizi imekwisha kuwajia kwa maana sasa wokovu wetu u karibu nasi kuliko tulipoanza kuaminiusiku umeendelea sana, mchana umekaribia, basi na tuyavue matendo ya giza, na kuzivaa silaha, za nuru-kama ilivyohusika na mchana na tuenende kwa adabu; si kwa ulafi na ulevi, si kwa ufisadi na uasherati, si kwa ugomvi. Bali mvaeni Bwana Yesu kristo, wala msiangalie mwili, hata kuwasha tamaa zake Warumi 13;11-14.

Tukijua ya kwamba miaka kadhaa iliyopita dalili zifuatazo zilionekana Msimamo mkubwa ulichukuliwa na chama cha Republican katika kampeni yake ya hivi karibuni wa kushikilia mamlaka ya mwisho ya mahakama kuu katika mambo yote ambayo yatasaidia. Maamuzi kuhusika katika kushikilia. Maamuzi yote ya mahakama hiyo, inaonyesha ni jinsi gani mwelekeo wa chama hicho kinachokaribia kuingia katika madaraka kitakavyokuwa kuhusika na jambo hili la kuwa taifa la kikristo.

Pia ni wazi kwamba Papa, Askofu mkuu wa Ireland na wakatoliki wengine waliokubuhu wamejitangazia wenyewe kuwa upande wa chama cha Republican. Na kwamba katiba, kama inavyotafsiriwa sasa na mahakama kuu, inaaminiwa na wakatoliki kukubaliana na aina ya serikali ya Upapa.
Chama sasa karibu kitaingia katika madaraka kikiwa na nia ya kuwa na ya serikali ya upapa katika kukubaliana na serikali hiyo ..
Review and Herald Vol. 3 Jan 19, 1897 Page 432.

Tukijua kuwa Marekani imeanza kunena kama Joka; kwa sababu sasa hivi Marekani ndiyo taifa pekee lenye nguvu duniani; ni taifa pekee tajiri duniani; ni taifa pekee linaloongoza katika sayansi na teleknolojia katika ulimwengu. Marekani ni taifa pekee lenye mvuto mkubwa ulimwenguni; ndilo taifa pekee ambalo kiongozi wake anazunguka katika ulimwengu kupatanisha mataifa yanayopigana; ni taifa pekee lililopewa jina la polisi wa ulimwengu; ni taifa pekee likitoa kauli ulimwengu unatilia maanani; ni taifa pekee lenye mchango mkubwa katika umoja wa mataifa.

Marekani ni kiongozi wa shirika la NATO shirika ambalo likiamua kupiga nchi iliyo kinyume chake unapiga bila kujali umoja wa mataifa unakubali au la! Marekani nchi pekee ambayo katika Bilblia imeatajwa kwa jina kuwa na sehemu kubwa ya kutimiza unabii wa kumaliza historia ya dunia. 5 T 452 maandalio ya amri ya Jumapili sasa yanaendelea gizani. Viongozi wanaficha tatizo halisi, na wengi wanajiunga na mpango huo wa kuandaa amri ya Jumapili hawaoni kama ni jambo lililokusudiwa. Washiriki wake ni wakristo wazuri, itakoponena itafunua roho ya Joka—-

Mwenyezi Mungu atubariki kwa kadri tunavyoendelea kutafakari ujumbe huu mzito unaotufikilia katika miisho hii ya dunia. Na hebu tumwombe Mwenyezi Mungu kutubadilisha udhaifu wetu na kutuwezesha kusonga mbele kuinua bendera ya Mwokozi wetu Yesu Kristo kwa njia ya kupeleka injili ya milele kwa kila mtu haraka kwa kadiri Bwana wetu Yesu Kristo atakavyotuwezesha. Bwana awe nasi sote milele Amina.


Imetayarishwa na
Pr. Joackim Msembele
Sauti ya mtu aliaye nyikani,
Itengenezeni njia ya Bwana
Yanyosheni Mapito yake.
P.O. Box 99
MBEYA.