FUNDISHO KUHUSU MUNGU
Wazo la kuwepo kwa Mungu linaafikiwa na karibu wanadamu wote. Kila binadamu aliye kamili, anatambua kuwepo kwa aliye juu yake anayehusika na si kuwepo kwake tu bali na hatima ya maisha yake. Licha ya kuwepo kwa tofauti ya namna huyo Mungu anavyotambuliwa na anavyodhaniwa kuwa, bado binadamu wa kawaida ana sifa ya kutambua kuwapo kwa Mungu. Ingawa hakuna mwanadamu aliyewahi kumuona Mungu, Maandiko Matakatifu yanatuthibitishia kuwa Mungu yupo. Waebrania 11:6 “Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.” Biblia inamtambulisha Mungu ambaye wengine humuabudu kwa kupapasa papasa bila kumjua vizuri.
Paulo Mtume alipoenda Ugiriki aliwakuta watu wakimuabudu Mungu wasiyemjua. Matendo 17:23 “Kwa sababu nilipokuwa nikipita huko na huko na kuyaona mambo ya ibada yenu, naliona madhabahu iliyoandikwa maneno haya, KWA MUNGU ASIYEJULIKANA. Basi mimi nawahubirini habari zake yeye ambaye ninyi mnamwabudu bila kumjua. Wanadamu wamekuwa katika hali hii ya kumtafuta Mungu na hivyo kuzua dhana nyingi kuhusiana na Mungu na nyingi kati ya hizo zikiwa dhana potofu. Ukweli usio na shaka kuhusu Mungu ni kuwa yeye ndiye aliyeumba dunia na vyote viijazavyo. Matendo ya Mitume 17:24-28 “Mungu aliyeufanya ulimwengu na vitu vyote vilivyomo, yeye, kwa kuwa ni Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika hekalu zilizojengwa kwa mikono; wala hatumikiwi kwa mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji kitu cho chote; kwa maana ndiye anayewapa wote uzima na pumzi na vitu vyote. Naye alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika mmoja, wakae juu ya uso wa nchi yote, akiisha kuwawekea nyakati alizoziamuru tangu zamani, na mipaka ya makazi yao; ili wamtafute Mungu, ingawa ni kwa kupapasa-papasa, wakamwone, ijapokuwa hawi mbali na kila mmoja wetu. Kwa maana ndani yake yeye tunaishi, tunakwenda, na kuwa na uhai wetu. . .”
Biblia inatutambulisha Mungu aliye muumbaji, mvumilivu na mwenye huruma anayefanya jitihada za kujihatarisha mwenyewe ili kuturejesha katika mahusiano yaliharibiwa na kuwepo kwa dhambi. Katika kutengeneza daraja kati yake na sisi aliwatuma manabii kutuletea habari ya tumaini la wokovu litakalokamilishwa baada ya muda mrefu kupitia kwa Yesu Kristo ambaye katika mpango huo anatambulika kama mwana. Manabii hawa baadaye waliagizwa kuandika waliyotumwa na kupelekea kuwapo kwa kitabu kimoja kikubwa chenye mkusanyiko wa vitabu 66 kutoka kwa waandishi wasiopungua 40 walioandika katika kipindi cha miaka 1500. Mengi ambayo hayakufahamika huko nyuma kuhusu Mungu yanafunuliwa katika kitabu hiki.
Biblia inatuhakikishia kuwa kuna Mungu mmoja ambaye katika utendaji wa kazi zake kwa wanadamu huonekana katika nafsi tatu. Kumbukumbu la Torati 6:4 Sikiza, Ee Israeli; Bwana, Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja. Tena Paulo anaitilia mkazo dhana hiyo. Waefeso 4:6 Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote. Wazo hili la kuwepo kwa nafsi tatu za Uungu limesumbua baadhi ya akili za watu kwa kuhofia kuwa ni jambo linaloweza kupelekea hali kulidhalilisha, kulifanyia dhihaka na kukufuru jina la Mungu. Pamoja na uwezekano wa kuwepo hatari hiyo, wazo hili si wazo lililozalishwa na mwanadamu. Mungu mwenyewe hujitambulisha mara nyingi katika uwingi (kuashiria kuwepo kwa nafsi zaidi ya moja) na si katika umoja kama inavyoonekana katika mafungu yafuatayo. Mwanzo 1:26 “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.” Mwanzo 11:6-7 “Bwana akasema, Tazama, watu hawa ni taifa moja, na lugha yao ni moja; na haya ndiyo wanayoanza kuyafanya, wala sasa hawatazuiliwa neno wanalokusudia kulifanya. Haya, na tushuke huko, tuwachafulie usemi wao ili wasisikilizane maneno wao kwa wao.”
Biblia inatambua kuwepo kwa Yesu tangu milele akiwa kama Mungu. Yohana 1:1,13 “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.” Wafilipi 2:5-7 “Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu.”
Biblia pia inatambua kuwepo kwa Roho Mtakatifu kama nafsi yenye utashi na ufahamu. Yohana 14:26 “Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.” Warumi 8:26 “Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.” Mathayo 12:31-32 “Kwa sababu hiyo nawaambia, Kila dhambi na kila neno la kufuru watasamehewa wanadamu, ila kwa kumkufuru Roho hawatasamehewa. Kwa sababu hiyo nawaambia, Kila dhambi na kila neno la kufuru watasamehewa wanadamu, ila kwa kumkufuru Roho hawatasamehewa.”
Katika kumkomboa mwanadamu nafsi hizi za uungu zimeshirikiana kikamilifu bila kuhitilafiana. Nafsi ya Baba (ambayo katika mpango wa wokovu ilipewa jukumu la kuwa Baba wa hiari wa nafsi nyingine) ndiyo iliyoruhusu Yesu aje awafie wanadamu. Yohana 3:16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.” Maandiko yanatuambia Yesu alipokamilisha kazi ya kumkomboa mwanadamu msalabani alikabidhi roho yake kwa baba. Luka 23:46 Yesu akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu. Lakini alipofufuka pia alirejea kwa baba yake kutoa taarifa ya ukombozi wa wanadamu. Yohana 20:17 “Yesu akamwambia. Usinishike; kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini enenda kwa ndugu zangu ukawaambie, Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu.”
Lakini Yesu (Mwana) hakushirikiana na Baba pekee bali alishirikiana na Roho Mtakatifu pia. Mathayo 1:18 “Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu.” Ilikuwa ni lazima Neno (jina lake la asili) afanyike Mwana (jina la kimkakati) na aitwe Yesu kumaanisha ndiye atakayewakomboa wanadamu kutoka dhambini. Mathayo 1:21 “Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao.” Kwa kufanyika mwanadamu Yesu alijipatia sifa (kigezo) muhimu iliyohitajika ili kuchukua nafasi ya Adamu wa kwanza aliyeshindwa mtihani wa dhambi na kuwatumbukiza wanadamu wote dhambini. Waebrania 2:16-17 “Maana ni hakika, hatwai asili ya malaika, ila atwaa asili ya mzao wa Ibrahimu. Hivyo ilimpasa kufananishwa na ndugu zake katika mambo yote, apate kuwa kuhani mkuu mwenye rehema, mwaminifu katika mambo ya Mungu, ili afanye suluhu kwa dhambi za watu wake.”
Yesu alifanyika Mwana ili sisi tuliogeuka na kuwa uzao wa nyoka tuwe wana wa Mungu kwa mfano wa Yesu Kristo. Athari moja tuliyonayo wanadamu wote iliyotokana na dhambi ni kupoteza asili yetu ya kutenda mema na kupandikiziwa asili nyingine isiyo na uwezo wa kuzalisha mema. Warumi 7:18 “Kwa maana najua ya kuwa ndani yangu, yaani, ndani ya mwili wangu, halikai neno jema; kwa kuwa kutaka nataka, bali kutenda lililo jema sipati.” Mathayo 12:34 “Enyi wazao wa nyoka, mwawezaje kunena mema, mkiwa wabaya? Maana, kinywa cha mtu huyanena yaujazayo moyo wake.” Yeremia 13:23 “Je! Mkushi aweza kuibadili ngozi yake, au chui madoa-doa yake? Kama aweza, ndipo na ninyi mwaweza kutenda mema, ninyi mliozoea kutenda mabaya.” Hiyo ni asili anayoipokea mtu bila hiari na asili hiyo huanza mara tu mimba inapotungwa! Zaburi 51:5 “Tazama, mimi naliumbwa katika hali ya uovu; Mama yangu alinichukua mimba hatiani.”
Lakini kupitia Maisha, mauti, na ufufuo wa kristo hali hiyo ya asili inapata nafasi ya kubadilishwa pale mwanadamu kwa ridhaa yake mwenyewe anapomkubali Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yake. Warumi 8:29 “Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi.” Wakolosai 1:15 “Naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote.” Mungu alitambua tangu mwanzo kuwepo kwa wanadamu watakaotamani kufanyika watoto wa Mungu kwa asili ya Adamu wa pili yaani Yesu huku wakiikana asili yao ya awali waliyoirithi kwa Adamu wa kwanza. Mungu aliwachagua watu hao si kinyume cha hiari yao lakini kama itikio la uhuru wao wa kuchagua.
Yesu ingawa anashiriki pambano kuu mahali pa Adamu na kutambulika kama Adamu wa pili (au wa mwisho), bado anakuwa mzaliwa wa kwanza wa jamii ya wanadamu aliyeishinda ile asili ya mwanadamu ya kutenda dhambi. 1 Wakorintho 15:45 “Ndivyo ilivyoandikwa, Mtu wa kwanza, Adamu, akawa nafsi iliyo hai; Adamu wa mwisho ni roho yenye kuhuisha.” Wanadamu hufanyika watoto wa Mungu si kwa kumwamini Yesu pekee bali hukamilika kuwa watoto wa Mungu kwa wanapoongozwa na Roho Mtakatifu. Warumi 8:14,17 “Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu, na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye.”
Wanadamu walioanguka dhambini wanapompokea Yesu kama Bwana na Mwokozi wao hujipatia daraja ya juu sawa na ile waliyokuwa nayo kabla hawajaanguka dhambini na hata kuzidi. Wale wamwaminio Yesu hurithishwa asili hiyo hiyo ya kushinda dhambi na kufanyika sehemu ya kundi kubwa la wazaliwa wa kwanza. Mkutano wa wakombolewa kule mbinguni utajumuisha wanadamu wenye sifa hii ya uzaliwa wa kwanza. Waebrania 12:23 “Bali ninyi mmeufikilia mlima Sayuni, na mji wa Mungu aliye hai, Yerusalemu wa mbinguni, na majeshi ya malaika elfu nyingi; mkutano mkuu na kanisa la wazaliwa wa kwanza walioandikwa mbinguni, na Mungu mwamuzi wa watu wote, na roho za watu wenye haki waliokamilika.”
Miongoni mwa haki za msingi za wazaliwa wa kwanza ni kurithishwa utawala. Walawi walikuwa sehemu ya utawala wa Taifa la Israeli, utawala uliojumuisha Makuhani, Manabii, na Wafalme. Mungu aliwahesabia Walawi kama wazaliwa wa kwanza ili kuwapatia uhalali wa kuwa watawala. Hesabu 8:18 “Nami nimewatwaa Walawi badala ya wazaliwa wa kwanza wote walio katika wana wa Israeli.” Hali kadhalika Mungu anawafanya wanaomgeukia Kristo na kumwamini kuwa wazaliwa wa kwanza ili kuwahalalishia haki ya kuwa watawala.
Makuhani katika Agano Jipya wanabeba hadhi ya watawala. 1 Petro 2:9 “Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu.” Kazi yao kuu ni kutangaza fadhila zake yeye aliyewatoa gizani. Na hata baada ya dhambi, waliokombolewa wataendelea na huduma hiyo ya kikuhani itakayokwenda sambamba na utawala. Ufunuo wa Yohana 5:10 “Ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi.” Waliokombolewa watakuwa na eneo pana zaidi la kutawala kuliko lile walilokuwa nalo kabla ya dhambi. Danieli 7:27 “Na ufalme, na mamlaka, na ukuu wa ufalme, chini ya mbingu zote, watapewa watu wa watakatifu wake Aliye juu; ufalme wake ni ufalme wa milele, na wote wenye mamlaka watamtumikia na kumtii.” Kitakachowastahilisha kuwa washirika wa utawala huu ni haki ya uzaliwa wa kwanza waliyoirithi kwa kumwamini Yesu. Zaburi 89:27 “Nami nitamjalia kuwa mzaliwa wangu wa kwanza, Kuwa juu sana kuliko wafalme wa dunia.”
Wale wanaohoji iliwezekanaje Mungu aliyeumba vyote ajishushe hata kufanyika mwanadamu na kuishi kama mwanadamu wa kawaida wanakosa kuelewa tabia halisi ya Mungu. 1 Yohana 4:8, 16 “Yeye asiyependa, hakumjua Mungu, kwa maana Mungu ni upendo. Nasi tumelifahamu pendo alilo nalo Mungu kwetu sisi, na kuliamini. Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake.” Tabia moja inayochomoza juu sana miongoni mwa tabia zake Mungu ni tabia ya upendo. Upendo ni tabia iliyojidhihirisha zaidi alipochagua kwa hiari yake kuchukua adhabu yetu ili sisi tupone. 1 Petro 2:24 Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa kupigwa kwake mliponywa.
Kama kitendo cha kujishusha kwake ili atuokoe kinachukuliwa kama sababu ya kumuondolea hadhi yake ya kuwa Mungu, huo ni ushahidi tosha kuwa tumekuwa watovu wa shukurani wa kiwango cha juu kwani hayo ya kudhalilika yalimpata kwa ajili yetu. Yesu alikufa kifo cha aibu cha kuangikwa msalabani kama mhalifu – adhabu iliyokuwa ya kikatili kuliko zote zilizowahi kubuniwa na dola la Kirumi. Lakini Yesu alistahimili aibu hiyo kwa ajili yako. Waebrania 12:2 tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu. 1 Petro 2:23 “Yeye alipotukanwa, hakurudisha matukano; alipoteswa, hakuogofya; bali alijikabidhi kwake yeye ahukumuye kwa haki.”
Kabla hujadhihaki kile Yesu alichofanyiwa tafakari kama alistahili hayo aliyotendewa? Biblia inatuambia hapakuwepo mwanadamu aliyekuwa mwema, mkamilifu na asiye na dhambi kama Yeye. 1 Petro 2:22 “Yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana kinywani mwake. Pamoja na kuishi kwenye mazingira ya kujaribiwa ambapo hakutakiwa atumie Uungu wake kuyashinda, bado aliweza kushinda dhambi.” Waebrania 4:15 “Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi. Yesu alipigwa na kuonewa kwa ajili yetu. Isaya 53:5 “Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.”
Katika kuwaokoa wanadamu nafsi moja ya Uungu iliruhusu nafsi ya Mwana ijiunge na jamii ya wanadamu ili kulipa adhabu iliyokuwa inawakabili na hivyo kuwafungulia kutoka kifungo cha mauti, wakati ile nafsi ya Roho Mtakatifu ilikuwa na jukumu la kuwafungulia wanadamu kutoka kifungo cha utumwa wa dhambi na kuwakamilisha kuwa watoto wa Mungu. Warumi 7:4 Kadhalika, ndugu zangu, ninyi pia mmeifia torati, kwa njia ya mwili wa Kristo, mpate kuwa mali ya mwingine, yeye aliyefufuka katika wafu, kusudi tumzalie Mungu matunda.
Roho Mtakatifu ndiye anayehusika na kuzalisha na kufufua kile kilichokufa. Warumi 8:11 Lakini, ikiwa Roho yake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu.” Mchakato huo kwa mwanadamu mdhambi aliyemgeukia Kristo unachukua maisha yake yote nao hukoma tu pale Kristo anapokuja na mwili mwingine usio wa dhambi.
Roho huihuisha mioyo yetu ya dhambi kwa kuishuhudia kuwa na hatia kama hatua muhimu ya kuelekea kupokea msamaha wa dhambi. Yohana 14:26 “Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.” Yohana 16:7 “Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu. Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu.”
Roho Mtakatifu pia ndiye atuombeaye kwa kuugua. Warumi 8:26 Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Roho Mtakatifu si nguvu ya Mungu bali ni nafsi kamili ifanyayo maamuzi kwa kutumia uwezo wake Mwenyewe. 1 Wakorintho 12:11 “Lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye.” Roho Mtakatifu si pumzi, si upepo, si ndimi za moto bali ni nafsi ya Uungu yenye uwezo wa kuhisi. Waefeso 4:30 “Wala msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi.” Mtume Paulo anamtaja kama sehemu ya utatu anapohitimisha waraka wa pili kwa Wakorintho. 2 Wakorintho 13:14 “Neema ya Bwana Yesu Kristo, na pendo la Mungu, na ushirika wa Roho Mtakatifu ukae nanyi nyote.”
Mchakato wa kumbadilisha mwenye dhambi ili afanyike mtoto wa Mungu unasimamiwa na Roho Mtakatifu, nao huanza kwa Roho Mtakatifu kumshuhudia mwenye dhambi kuwa na hatia. Yohana 16:7-8 “Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu. Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu.” Kule kujitambua kwamba u mwenye dhambi na kutamani kupata msamaha ili uondokane na hatia, ni dalili tosha kuwa una Roho Mtakatifu. Mtu anaposhupaza shingo baada ya dhamira kumshuhudia kuwa ni mkosaji au mwenye dhambi anafanya kazi ya kumkufuru Roho Mtakatifu. Kwa kuwa Roho Mtakatifu ndiye anayehusika kutoa taarifa ya mwisho ya maendeleo ya mdhambi aliyemgeukia Mungu na kumwamini Yesu Kristo, kitendo hicho cha kumkufuru hufunga kabisa uwezekano wa mtu huyo kuokolewa. Luka 12:10 “Na kila mtu atakayenena neno juu ya Mwana wa Adamu atasamehewa, bali aliyemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa.” Marko 3:29 “Bali mtu atakayemkufuru Roho Mtakatifu hana msamaha hata milele; ila atakuwa ana dhambi ya milele.”
Ili ukombozi wa mwanadamu ukamilike ulihitaji uungu ujipange katika majukumu ya kumuokoa mwanadamu. Yesu akihitimisha kazi yake hapa duniani aliagiza wanaoongoka na kumwamini wabatizwe wakitumia majina matatu yanayounda utatu katika Mungu mmoja. Mathayo 28:19 “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu.” Kwa akili zetu za kibinadamu zilizoathiriwa na dhambi jambo hili laweza kuwa gumu kulielewa. Lakini haina sababu ya kutupelekea kutoiamini dhana hii. Uwezekano wa kuwepo Mungu mmoja mwenye nfsi tatu upo kama ulivyo uwezekano wa kuwepo yai moja lenye kiini, ute, na ganda. Haya si mayai matatu bali ni yai moja lenye sehemu tatu zilizoshikamana.
Yapo mengi magumu ya kujifunza kuhusu Mungu. Lakini Mungu kwa hekima yake ametufunulia kiasi kidogo kutuwezesha kushiriki kikamilifu katika mpango wa wokovu. Mengi yaliyofichwa sasa yatafunuliwa wakati muafaka Mungu mwenyewe atakapopenda kufanya hivyo. Kumbukumbu la Torati 29:29 “Mambo ya siri ni ya Bwana, Mungu wetu; lakini mambo yaliyofunuliwa ni yetu sisi na watoto wetu milele, ili tuyafanye maneno yote ya sheria hii.” Kwa sasa kilichofunuliwa kwetu ni kuwa tunaye Mungu mmoja ambaye amehusika katika mpango wa kumuokoa mwanadamu katika sura tatu za Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu. Mathayo 28:19 “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu.”
Usiwe miongoni mwa wale wanaokana kuwa hakuna Mungu. Zaburi 53:1 “Mpumbavu amesema moyoni, Hakuna Mungu; Wametenda uovu wa ufisadi na kuchukiza, Hakuna atendaye mema.”