Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

UCHAKACHUAJI WA NENO

UCHAKACHUAJI WA HATI MILIKI YA MUNGU

Hatimiliki ni waraka unaokutambulisha kisheri kuwa ndiwe mmiliki halali wa mali inayohusika. Mali hiyo yaweza kuwa kipande cha ardhi, nyumba n.k. Hatimiliki ni muhimu ili kukuepusha kuingia kwenye migogoro isiyo ya lazima. Mungu anatambua umuhimu wa kuwa na hatimiliki ndiyo maana katika kusimamisha utawala wake hapa duniani alitangaza mali zinazomhusu na mali zinazotuhusu sisi kama raia wa ufalme wake. Kuanzia amri ya kwanza hadi ya nne Mungu anatangaza umiliki wake katika ibada na amri ya tano hadi ya kumi anatangaza umiliki wa wanadamu wa mali alizowapa. Hata hivyo Mungu ndiye mmiliki halali wa mali zote. “Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, Dunia na wote wakaao ndani yake” (Zaburi 24:1)

Hati miliki ni waraka unaotakiwa kutunzwa sana hasa katika kizazi kisichoaminika kama hiki tunachoishi. Watu wengi wamelizwa kwa kuuziwa viwanja vilivyo kwenye maeneo ya wazi au hifadhi ya barabara. (Bomoa bomoa). Katika ulimwengu wa kiroho hatari hiyo ni kubwa zaidi. Hatimiliki ya mali za watu ipo hatarini kama ilivyo hatarini hatimiliki ya Mungu. Uzinzi, wizi, uongo, kutotii walio juu yako, mauaji na kutamani ni njia zinazotumika kunyanga hati miliki ya watu wengine. Mambo haya yataendelea kujidhihirisha kadri mwisho ule unavyokaribia.

Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari. Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi, wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema, wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu; wenye mfano wa utauwa, lakini wakikana nguvu zake; hao nao ujiepushe nao. (2Timotheo 3:1-5)

Mungu anayo mipango mikubwa miwili iliyomgharimu sana na ambayo ina umuhimu mkubwa kuliko kitu chochote, ambayo ni mpango wa uumbaji na mpango wa wokovu. Mipango hii imefafanuliwa na kuhifadhiwa vizuri ndani ya Maandiko Matakatifu. Mipango hii ina manufaa makubwa kwa mwanadamu na ndiyo maana tunatakiwa kuiheshimu sana. Mustakabali wetu unategemea jinsi tunavyoiheshimu mipango hii na ile hazina (Maandiko) ambako mipango hii imefafanuliwa na kuhifadhiwa. Lakini zipo njama za adui zetu kuhujumu mipango hii na kupotezea umuhimu hata wa ile hazina ambako mipango hii imehifadhiwa na kufafanuliwa. “Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki.” (2Timotheo 3:16). “Lihubiri neno, uwe tayari, wakati ukufaao na wakati usiokufaa, karipia, kemea, na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho. (2Timotheo 4:2)

Hii hailengi kutuletea hasara tu wanadamu bali kumuondolea Mungu uhalali wa kutumiliki na kumiliki ibada iliyo kiungo kati yake na sisi. Bila mpango wa uumbaji na ukombozi Mungu hana hatimiliki ya kupokea ibada na kuheshimiwa kutoka kwa wanadamu. “Umestahili wewe, Bwana wetu na Mungu wetu, kuupokea utukufu na heshima na uweza; kwa kuwa wewe ndiwe uliyeviumba vitu vyote, na kwa sababu ya mapenzi yako vilikuwako, navyo vikaumbwa.” (Ufunuo 4:11) “Nao waimba wimbo mpya wakisema, Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa.” (Ufunuo 5:9)

Mungu anajivunia uumbaji na ukombozi na hiki ndicho kinachomtofautisha na miungu mingine. Mtawaambia hivi, Miungu hiyo isiyofanya mbingu na nchi, hiyo itaangamia katika nchi, nayo itatoweka chini ya mbingu. (Yeremia 10:11) Maana miungu yote ya watu si kitu, Lakini Bwana ndiye aliyezifanya mbingu. (Zaburi 96:5) Ulikuwa wapi nilipoiweka misingi ya nchi? Haya! Sema, kama ukiwa na ufahamu. Ni nani aliyeamrisha vipimo vyake, kama ukijua? Au ni nani aliyenyosha kamba juu yake? Misingi yake ilikazwa juu ya kitu gani? Au ni nani aliyeliweka jiwe lake la pembeni, (Ayubu 38:4-6)

Mungu haabudiwi na kuheshimiwa kwa uwezo wake wa kuumba tu bali na kwa uwezo wake wa kuokoa. “Wako wapi miungu ya Hamathi na ya Arpadi? Wako wapi miungu ya Sefarvaimu? Je! Wameiokoa Samaria na mkono wangu?” (Isaya 36:19) Mungu katika Yesu Kristo alijitoa kutuokoa hata kabla ya kuwekwa misingi ya dunia. “Na watu wote wakaao juu ya nchi watamsujudu, kila ambaye jina lake halikuandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo, aliyechinjwa tangu kuwekwa misingi ya dunia.” (Ufunuo 13:8). Yesu alikamilisha wokovu huo pale msalabani alipojitoa kwa ajili yetu sote miaka 2,000 iliyopita. “Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.” (Isaya 53:5).

Gharama ya wokovu wetu ilikuwa ya kiwango cha juu kuliko fidia yoyote iliyowahi kutolewa kwa ajili ya makosa yaliyotendwa na wanadamu. “Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo.” (1 Petro 1:18-19). Alilipa adhabu ya makosa, dhambi, na uovu wetu kwa kuyatoa maisha yake yawe fidia. “Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.” (Marko 10:45)

Pamoja na kuwa Mungu anatupenda kiasi cha kutuokoa hivyo kwa gharama kubwa, anataka tuupokee wokovu huo kwa hiari bila kulazimishwa, kwa kuwa utii wa kweli ni ule unaotolewa kw upendo. Ili wokovu huo uwe wa hiari kila mmoja anatakiwa kupokea alama inayotambulisha kuwa ameokolewa. Alama hiyo ni ile inayotambulisha kuwa tunamilikiwa na Mungu kwa kuwa alituumba na kutukomboa. Alama hiyo hutambulisha kuwa tumepumzika kutoka kazi za dhambi kama Yesu mwenyewe alivyopumzika kutoka kazi ya kutuokoa. “Basi, imesalia raha ya sabato kwa watu wa Mungu. wa maana yeye aliyeingia katika raha yake amestarehe mwenyewe katika kazi yake, kama vile Mungu alivyostarehe katika kazi zake.” (Waebrania 4:9-10)

Amri Kumi ndicho kiini cha Agano la Mungu na wanadamu. “Akawahubiri agano lake, alilowaamuru kulitenda, yaani, zile amri kumi; akaziandika juu ya mbao mbili.” (Kumbukumbu 4:13). Kuanzia amri ya kwanza hadi ya nne inayotambulisha umiliki wa Mungu kwa wanadamu na sababu zake, Mungu aliitaja Sabato kuwa kiini cha umiliki huo. “Tena naliwapa sabato zangu, ziwe ishara kati ya mimi na wao, wapate kujua ya kuwa mimi, Bwana, ndimi niwatakasaye.” (Ezekieli 20:12). Amri ya Sabato ndiyo inayomtambulisha Mungu aliyetoa amri kumi. Kama Amri Kumi ni hati miliki kama tusemavyo, basi amri ya nne ndiyo inayoipa hati hiyo uhalali kwa kuwa ina muhuri unaotambulisha Jina la Mmiliki – (Bwana/Jehovah), Eneo analotawala – (Mbingu na nchi na bahari), na Cheo chake – (Muumbaji).   

“Ikumbuke siku ya Sabato uitakase. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; lakini siku ya saba ni Sabato ya Bwana, Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya malango yako. Maana, kwa siku sita Bwana alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba; kwa hiyo Bwana akaibarikia siku ya Sabato akaitakasa.” (Kutoka 20:8-11)

Wana wa Israeli walipewa Amri kama matokeo ya kukombolewa. “Mimi ni Bwana, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa.” (kutoka 20:2). Leo wanadamu wote wamepewa amri kama matokeo ya kukombolewa pia. “Mkinipenda, mtazishika amri zangu.” (Yohana 14:15). Na wala amri hizo si nzito kama wengine wafikirivyo. “Kwa maana huku ndiko kumpenda Mungu, kwamba tuzishike amri zake; wala amri zake si nzito.” (1 Yohana 5:3) Kusudi la kupewa amri baada ya kukombolewa ni kutambulisha umiliki na asili ya uwezo ule ubadilishao. “Zitakaseni sabato zangu; zitakuwa ishara kati ya mimi na ninyi, mpate kujua ya kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.” (Ezekieli 20:20). Usipokuwa na sabato umepoteza umiliki wa Mungu.

Je kuna uwezekano wa mwingine kuchukua umiliki wa huyo aliyepoteza umiliki wa Mungu hata kama hana sifa ya kuwa mmiliki wa wanadamu ambayo kama tulivyosema mwanzo ni sifa inayomhusu Mungu pekee kwa kuwa ndiye mwenye uwezo wa kuumba na kukomboa? Jibu ni ndiyo. Kama tulivyo na watoaji wa hati miliki bandia wanaweza pia kuwepo watoa hati miliki bandia wa kiroho ikiwa uangalifu hautatumika. “Mtu awaye yote asiwadanganye kwa njia yo yote; maana haiji, usipokuja kwanza ule ukengeufu; akafunuliwa yule mtu wa kuasi, mwana wa uharibifu; yule mpingamizi, ajiinuaye nafsi yake juu ya kila kiitwacho Mungu ama kuabudiwa; hata yeye mwenyewe kuketi katika hekalu la Mungu, akijionyesha nafsi yake kana kwamba yeye ndiye Mungu.” (2 Wathesalonike 2:3-4)

Udanganyifu huu wa kutisha wenye lengo la kumuondolea Mungu hati miliki ya wanadamu ilianza kule mbinguni wakati malaika aliyependelewa sana alipofanyaa jaribio hili la kumuondolea Mungu umiliki wa malaikaa na wandamu. Alishindwa akatupw duniani. Yesu anasema hivi kumhusu malaika huyu. “Akawaambia, Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme.” (Luka 10:18). Pamoja na kutupwa hivyo hakukoma katika hila zake za udanganyifu. “Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye. Kwa hiyo shangilieni, enyi mbingu, nanyi mkaao humo. Ole wa nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu.” (Ufunuo 12:9, 12)

Ujio wa shetani duniani ulikuwa na lengo la kuiondosha kama si sheria yote basi angalo ile inayotambulisha umiliki wa Mungu kwa wanadamu – sheria ya Sabato itoke kwenye amri kumi. Mungu hawezi kuwaacha marafiki zake wanadamu anaowapenda bila kuwajulisha hatari inayowanyemelea kama asemavyo nabii Amosi. “Hakika Bwana MUNGU hatafanya neno lo lote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake.” (Amosi 3:7) Alitoa hadhari katika kitabu cha Danieli iliyokuja timizwa miaka kadhaa mbele baada ya Yesu kupaa mbinguni. “Naye atanena maneno kinyume chake Aliye juu, naye atawadhoofisha watakatifu wake Aliye juu; naye ataazimu kubadili majira na sheria; nao watatiwa mikononi mwake kwa wakati, na nyakati mbili, na nusu wakati.” (Danieli 7:25)

Ipo sheria moja katika amri kumi inayozungumzia majira nayo ni ile inayotambulisha ibada kwa Mungu inafanywa lini na inafanywaje na kwa nini. Ni sheria ya Sabato. Sheria hiyo inavyosomeka leo katika machapisho mbalimbali ni tofauti na ilivyokuwa inasomeka hapo awali ilipotolewa na Mungu mwenyewe. Hapa kumefanyika hila kubwa ya kubadilisha hati miliki hata hivyo waliofanya hivyo wanatambulika na si kutambulika tu wanapewa heshima kubwa duniani kana kwamba walichofanya kimeleta tija yoyote kwa wanadamu. Mungu anatahadharisha kuwa uchakachuaji huu wa sheria utaigharimu dunia. “Dunia inaomboleza, inazimia; ulimwengu unadhoofika, unazimia; watu wakuu wa dunia wanadhoofika. Tena dunia imetiwa unajisi kwa watu wanaoikaa; kwa maana wameziasi sheria, wameibadili amri, wamelivunja agano la milele. Ndiyo sababu laana imeila dunia hii, na hao wanaoikaa wameonekana kuwa na hatia, ndiyo sababu watu wanaoikaa dunia wameteketea, watu waliosalia wakawa wachache tu.” (Isaya 24:2-6).
 
Uchakachuaji wa sheria ya Mungu umemuondolea Mungu watu wanaomwabudu kama alivyoagiza ambaye yeye amewaita waabuduo wa kweli na sasa ameingia katika mchakato wa kuwatafuta watu hao. “Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu.” (Yohana 4:23). Kwa sasa watu wa Mungu wametapakaa katika milima na vilima, kama kondoo waliopoteza mchungaji, wakitafuta mahali pao pa kupumzikia “Watu wangu wamekuwa kondoo waliopotea, wachungaji wao wamewapoteza; wamewapotosha milimani; wamekwenda toka mlima hata kilima, wamesahau mahali pao pa kupumzika.” (Yeremia 50:6).

Mungu ana wathamini watu wake hao na anao mpango maalumu kwao ajili yao. “Na kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta; na sauti yangu wataisikia; kisha kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja.” (Yohana 10:16). Anafanya hivyo kwa sababu katika mazizi hayo wamefundishwa kufanya ibada haramu na bandia isiyokidhi viwango vinavyohitajika – ibada isiyo ya kiroho na isiyo ya kweli. Na kwa kuwa haikidhi vigezo Mungu anaiita ibada hiyo ni ya bure. “Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu.” (Mathayo 15:9). Ibada ili iwe ibada ni lazima itokane na maagizo ya Mungu. Hata ibada ya Kaini haikutambuliwa kuwa ibada halali kwa kuwa haikufanywa kulingana maagizo ya Mungu. Pamoja na kuwa Mungu anatumia uvumilivu mwingi akiwasubiri wale wafanyao ibada iliyo maagizo ya wanadamu, subira yake hiyo itafikia mwisho. Atatoa ujumbe wa mwisho kuwataka watu wake wajitenge na ibada hizo potofu ili kujiepusha na adhabu ya kutisha itakayotolewa kwa wote walioshiriki kuwapotosha wanadamu kumfanyia Mungu ibada bandia ya kumdhihaki. “Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni, ikisema, Tokeni kwake, enyi watu wangu, msishiriki dhambi zake, wala msipokee mapigo yake.” (Ufunuo 18:4)

Ibada ya kweli kama mwinjili Yohana asemavyo huandamana na mambo mawili makubwa; kuabudu katika roho na kuabudu katika kweli. Kuabudu katika roho ni utambuzi kuwa anayestahili kuabudiwa ni Mungu pekee na mwanadamu anashirikishwa katika tendo hilo kwa neema tu ipatikanayo kupitia Kristo, na ya kwamba sifa za Kristo pekee ndizo zimpatiazo uhali wa kukisogelea kiti cha neema kwa ujasiri. “Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.” (Waebrania 4:16).

Katika mambo ambayo Mungu wa mbinguni hayupo tayari kushiriki na mwanadamu ni kujitwalia sifa zinazomstahili yeye. Jambo hili la mwanadamu kujitwalia nafasi ya Mungu hulitofautisha na dhambi ya kawaida kwa kuliita chukizo la uharibifu.  “Lakini mlionapo chukizo la uharibifu likisimama pasipolipasa, (asomaye na afahamu), ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani.” (Marko 13:14). Mfalme wa Kirumi aitwaye Herode wakati fulani alijaribu kujitwalia mahali pa Mungu na yaliyomkuta yalitosha kutambulisha kuwa Mungu hana ushirika na mwanadamu mwenye mwili katika kupokea sifa hiyo. “Basi siku moja iliyoazimiwa, Herode akajivika mavazi ya kifalme, akaketi katika kiti cha enzi, akatoa hotuba mbele yao. Watu wakapiga kelele, wakisema, Ni sauti ya Mungu, si sauti ya mwanadamu. Mara malaika wa Bwana akampiga, kwa sababu hakumpa Mungu utukufu; akaliwa na chango, akatokwa na roho.” (Matendo 12:21-23)

Kitendo cha wanadamu kujaribu kusimama mahali pa Mungu na kujitwalia heshima inayomstahili hutambuliwa na Maandiko kuwa ni kufuru. “Wakamsujudu yule joka kwa sababu alimpa huyo mnyama uwezo wake; nao wakamsujudu yule mnyama, wakisema, Ni nani afananaye na mnyama huyu? Tena ni nani awezaye kufanya vita naye? Naye akapewa kinywa cha kunena maneno makuu, ya makufuru. Akapewa uwezo wa kufanya kazi yake miezi arobaini na miwili. Akafunua kinywa chake amtukane Mungu, na kulitukana jina lake, na maskani yake, nao wakaao mbinguni. Tena akapewa kufanya vita na watakatifu na kuwashinda, akapewa uwezo juu ya kila kabila na jamaa na lugha na taifa. Na watu wote wakaao juu ya nchi watamsujudu, kila ambaye jina lake halikuandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo, aliyechinjwa tangu kuwekwa misingi ya dunia.” (Ufunuo 13:4-8) 
Utagundua kwamba mkakati wa kuwapotosha wanadamu ili wamfanyie ibada mwanadamu badala ya Mungu anayestahili umesukwa kwa umakini na si jambo jepesi kama wengine walichukuliavyo. Ni vita iliyoanza mbinguni na inayoendelea katika kipindi chote cha uhai wa dunia yetu; vita itakayoamua mustakabali wa maisha yako ya umilele.

Ili ibada isiwe ya kweli si lazima yote iwe ya uongo. Kunaweza kuwepo ukweli kwa kiwango kikubwa na upotoshaji kwa kiasi kidogo lakini madhara na matokeo yake yakawa sawa na aliyefanya ibada ya uwongo kwa asilimia mia moja. Ndiyo maana Mungu mara zote amekuwa mwangalifu kutoa maelekezo ya wazi juu ya namna anavyotaka aabudiwe na kuyahifadhi maelekezo hayo ndani ya Maandiko Matakatifu. Mungu ameagiza ibada ifanyike mara moja kila inapofika siku ya saba ya juma yaani Jumamosi. Hii haizuii ibada kufanyika siku nyingine ya juma ikiwa mtu atajisikia kufanya hivyo. “Wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia.” (Waebrania 10:25).

Lakini agizo hili la ibada ya siku ya saba ni la lazima kwa wanadamu wote. Ili kulipa uzito agizo hili la ibada ya siku ya saba (ibada ya mara moja kwa juma), Mungu aliitenga siku hiyo kwa kuitofautisha na zingine kwa kuijaza Baraka wakati alipokuwa anazindua ibada hiyo kwa wanadamu, katika juma la kwanza la uumbaji. “Basi mbingu na nchi zikamalizika, na jeshi lake lote. Na siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyoifanya; akastarehe siku ya saba, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoifanya. Mungu akaibarikia siku ya saba, akaitakasa kwa sababu katika siku hiyo Mungu alistarehe, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoiumba na kuifanya.” (Ufunuo 2:1-3).

Hii humaanisha ibada inayofanywa katika siku hiyo ina jambo la ziada lisilopatikana katika siku nyingine za juma na wala utakatifu ule uliowekwa na Mungu katika siku hiyo ya saba hauwezi kuhamishiwa kwenye siku nyingine ya juma. Ibada ya kila juma iliyoamriwa na Mungu inamtaka anayeabudu kutojihusisha na shughuli zingine za kawaida za maisha ila autumie muda wote wa masaa ishirini na nne tangu jua linazama Ijumaa hadi linapotua tena Jumamosi  kwa ajili ya kuimarisha uhusiano wake na Mungu. “Lakini siku ya saba ni Sabato ya Bwana, Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya malango yako.” (Kutoka 20:10)

Sifa hizi mbili muhimu za kuabudu katika roho na kweli hukosekana pale mtu abudupo pasi na kufuata malekezo ya namna ya kuabudu. Katika mambo ambayo Mungu hakumwachia mwanadamu ajiamulie ni lile linalohusu ibada. Anayejua anavyotaka kuabudiwa ni Yule mwenye kuabudiwa na si Yule mwenye kuabudu. Mwenye kuabudu anapokuwa mwamuzi wa namna ya kuabudu inamuondolea mwenye kuabudiwa sifa ya kuabudiwa.

Hata kama utaratibu wa kuabudu umepangiliwa vizuri kiasi gani lakini ikiwa umekiuka misingi ya kuabudu Mungu anasema, utaratibu huo haufai kwa ibada. “Mambo hayo yanaonekana kana kwamba yana hekima, katika namna ya ibada mliyojitungia wenyewe, na katika kunyenyekea, na katika kuutawala mwili kwa ukali; lakini hayafai kitu kwa kuzizuia tamaa za mwili.” (Wakolosai 2:23). Maandiko yanamtaja mwanzilishi wa ibada hizi za kujitungia kama mtoto wa kwanza wa kiume wa adamu aitwaye Kaini. Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. Bwana akamtakabali Habili na sadaka yake; bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana. Bwana akamwambia Kaini, Kwa nini una ghadhabu? Na kwa nini uso wako umekunjamana? Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde. Kaini akamwambia Habili nduguye, Twende uwandaniIkawa walipokuwapo uwandani,Kaini akamwinukia Habili nduguye,akamwua.” (Mwanzo 4:4-8)

Kaini aliamini kuwa ibada inaweza kufanywa kwa namna apendavyo mtu bila kufuata maelekezo yaliyotolewa jambo ambalo ni kosa kabisa. Jitihada ninazofanya hapa za kurekebishana katika namna tunavyomwabudu Mungu ni sawa na zile zilizochukuliwa na Abeli kwa kaka yake alipomwonya juu ya hatua anayofanya. Hatua hii haikusudii kuwaudhi watu au kuleta ushindani wa kidini japo tunajua ukweli unapodhihirishwa hayo ni mambo yasiyoepukika. Matokeo hayakuwa mazuri kwa muonyaji wakti ule Kaini alipoonywa juu ya ibada bandia aliyokuwa amejiundia maana Maandiko yanatuambia aliuawa. Maandiko hayo hayo yanatujulisha kuwa zitakuwepo jitihada za kurekebisha utaratibu usiofaa wa ibada katika siku za karibu na mwisho ambazo zitazua hali tete duniani. “Naye awakosesha wale wakaao juu ya nchi, kwa ishara zile alizopewa kuzifanya mbele ya huyo mnyama, akiwaambia wakaao juu ya nchi kumfanyia sanamu yule mnyama, aliyekuwa na jeraha la upanga naye akaishi. Akapewa kutia pumzi katika ile sanamu ya mnyama, hata ile sanamu ya mnyama inene, na kuwafanya hao wote wasioisujudu sanamu ya mnyama wauawe. Naye awafanya wote, wadogo kwa wakubwa, na matajiri kwa maskini, na walio huru kwa watumwa, watiwe chapa katika mkono wao wa kuume, au katika vipaji vya nyuso zao.” (Ufunuo 13:14-16)

Ibada isiyofuata maelekezo yaliyotolewa inapaswa kurekebishwa na siyo kulazimishwa. Mungu anataka watu wamwabudu kwa uhuru na siyo kwa vitisho au kwa maelekezo yaliyopotoshwa. Ndiyo maana kabla ya hatua za juu dhidi ya waabuduo wasio halisi kuchukuliwa Mungu anatuma watu (malaika) kuionya dunia. “Akasema kwa sauti kuu, Mcheni Mungu, na kumtukuza, kwa maana saa ya hukumu yake imekuja. Msujudieni yeye aliyezifanya mbingu na nchi na bahari na chemchemi za maji.” (Ufunuo 14:7). Ibada isiyotoka kwa Mungu lazima itoke kwa adui wa Mungu na ni lazima imnufaishe huyo adui, na kwa mujibu wa Maandiko adui wa Mungu ni Shetani ambaye Yesu humwita Mungu wa dunia hii. “Ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu.” (2 Wakorintho 4:4).

Wengine wanaonufaika na ibada isiyotoka kwa Mungu ni wale wanaopokea sifa kutokana na ubunifu huo wa ibada, bila kujali ni wanadamu wa taifa gani. “Nami nitatamka hukumu zangu juu yao kwa habari ya uovu wao wote; kwa kuwa wameniacha mimi, wakaifukizia uvumba miungu mingine, wakaziabudu kazi za mikono yao wenyewe.” (Yeremia 1:16) “Wakafanya ndama siku zile, wakaleta dhabihu kwa sanamu ile, wakafurahia kazi za mikono yao.” (Matendo 7:41)

Wakati Yesu alipokuwa akiishi hapa duniani, uchakachuaji huu wa sheria ya ibada ulikuwa katika sura tofauti na ilivyo leo. Wakati ule watu walimwabudu Mungu siyo katika roho bali zaidi katika hali ya kimwili, ingawaje waliendelea kumwabudu Mungu katika kweli yaani kwa kuzingatia ni wakati gani ibada ifanyike na ifanyike kwa nani. “Bwana akanena, Kwa kuwa watu hawa hunikaribia na kuniheshimu kwa vinywa vyao, bali mioyo yao wamefarakana nami, na kicho chao walicho nacho kwangu ni maagizo ya wanadamu waliyofundishwa.” (Isaya 29:13). Watu wa wakati wa Yesu waliendeleza hali hiyo kiasi cha kumlazimisha Yesu mara kadhaa kutofautiana nao na kujaribu kutumia nguvu nyingi kujaribu kuleta mabadiliko katika namna ya kuabudu. 

Sheria ya ibada inayowaagiza wanadamu wote kumuabudu Mungu siku ya saba ya juma ambayo ni Jumamosi iliondolewa na viongozi wenyewe wa kanisa wa wakati huo unaoitwa na wanahistoria zama za giza. Haukuwa uvamizi kutoka nje uliofanya mabadiliko hayo. Kunatolewa sababu nyingi kwa nini mabadiliko hayo yalifanyika lakini hiyo bado haijakidhi kiu ya wale wanaotaka uthibitisho kama Mungu aliruhusu kweli mabadiliko hayo, kwa kuwa kutokana na mwelekeo wa Maandiko, Mungu haoneshi kukubaliana na mabadiliko hayo. Mungu amerejea mara nyingi kuthibitisha kuwa hana kigeugeu na habadilishi neon lililotoka kinywani mwake.  “Kwa kuwa mimi, Bwana, sina kigeugeu; ndio maana ninyi hamkuangamizwa, enyi wana wa Yakobo.” (Malaki 3:6) Na tena “Mimi sitalihalifu agano langu, Sitalibadili neno lililotoka midomoni mwangu.” (Zaburi 89:34)

Yesu mwenyewe alipokuwa hapa duniani aliabudu katika wakati na siku ile ile aliyokuwa ameagiza kwenye amri alizozitoa pale mlimani Sinai. “Akaenda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake, akasimama ili asome.” (Luka 4:16). Hakubadili siku. Hata wafuasi wake wa karibu walioandaa mazishi yake mara tu baada ya kufa kwake waliendelea kufuata kilichoandikwa kwenye amri kuhusiana na siku hii ya ibada. “Na siku ile ilikuwa siku ya Maandalio, na sabato ikaanza kuingia. Na wale wanawake waliokuja naye toka Galilaya walifuata, wakaliona kaburi, na jinsi mwili wake ulivyowekwa. Wakarudi, wakafanya tayari manukato na marhamu. Na siku ya sabato walistarehe kama ilivyoamriwa.” (Luka 23:54-56). Hawakubadili siku. Yesu mwenyewe kwa kuwepo kaburini kuanzia Ijumaa jioni (Sabato inapoanza) hadi Jumapili alipofufuka alidhirisha kuwa ilikuwa ni lazima apumzike baada ya kukamilisha kazi ya ukombozi kama alivyopumzika alipomaliza kazi ya uumbaji na kufufuka jumapili inayoitwa na Maandiko siku ya kwanza ya juma yaani siku ya kazi. Hakubadili siku.

Na Paulo mtume na mfuasi kinda kinda wa Bwana Yesu Kristo (anayedhaniwa kuwa na mafunuo mapana zaidi ya wanafunzi wengine), aliendelea kuabudu katika siku ile ile Bwana wake aliyoabudu. “Na Paulo, kama ilivyokuwa desturi yake, akaingia mle walimo, akahojiana nao kwa maneno ya maandiko sabato tatu.” (Matendo17:2). Hakubadili siku. Tena yeye ndiye aliyetufunulia kuwa sheria ni njema na kuna raha ya Sabato inayowahusu watu wote wa Mungu. “Basi torati ni takatifu, na ile amri ni takatifu, na ya haki, na njema.” (Warumi 7:12). “Basi, imesalia raha ya sabato kwa watu wa Mungu” (Waebrania 4:9). Tena katika mazungumzo yake Yesu hakuwahi kudokeza au kuashiria kwamba angeweza kuja kufanya badiliko lolote la siku ya kumuabudu katika siku za usoni. Jambo alilolikazia ni kuwa watu waendelee kuiheshimu siku hiyo hata baada ya yeye kuondoka. “Ombeni, ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi, wala siku ya sabato.” (Mathayo 24:20). Yesu angewezaje kuruhusu siku ya ibada ibadilishwe wakati kule mbinguni siku itakayotumika kwa ibada ni ile ile aliyoiagiza na ambayo yeye mwenyewe aliitunza alipokuwa hapa duniani? “Na itakuwa, mwezi mpya hata mwezi mpya, na sabato hata sabato, wanadamu wote watakuja kuabudu mbele zangu, asema Bwana.” (Isaya 66:23). Mabadiliko ya siku ya ibada hayakutoka kwa Mungu yalitoka kwa wanadaamu.

Ikiwa hawa wote hawakuhusika kubadili siku ya ibada iliyowekwa na Mungu iliyo hati miliki ya Mungu kwa watu wake ni nani basi alifanya badiliko hilo kubwa na kwa mamlaka ya nani? Endelea kufuatilia kisa hiki cha kusisimua katika toleo lijalo ili kufahamu UCHAKACHUAJI WA HATI MILIKI YA Mungu.