Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

RAFIKI WA MFALME

MFALME APOTEZA MARAFIKI

Tabia moja ya mfalme huyu ni ukarimu. Hawezi kuwa na jambo zuri asishiriki na wengine. Ni kama waafrika tulivyokuwa zamani. Unapofikiria wazo la Mungu hapo hapo fikiria wazo la upendo na umoja. Katika namna tusiyoweza kuielezea sana uungu umefungamana katika ushirika mtakatifu unaoitwa utatu mtakatifu. Wazo hili halieleweki kirahisi na akili zetu zilizoathiriwa na dhambi. Hata hivyo ni ukweli unaoukuta katika vitabu vitakatifu vinavyoheshimiwa sana. Katika Quran Tukufu Surat Ibrahim aya ya 5 inasomeka 5. “Na tulimtuma Musa pamoja na miujiza yetu, tukamwambia: Watoe watu wako kwenye giza uwapeleke kwenye mwangaza. Na uwakumbushe siku za Mwenyezi Mungu. Hakika katika hayo zipo ishara kwa kila mwenye kusubiri akashukuru.” Lugha hii ya kuweka uwingi kila Jina la Mwenyezi Mungu linapotajwa inapatikana pia ndani ya Maandiko Matakatifu: Mwanzo 1:26 Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi. Kwa imani tunatambua kwamba kuna Mungu mmoja mwenye nafsi tatu za uungu. Hawa si miungu watatu bali ni mmoja. Kama ulionavyo yai kuwa ni moja lakini limejengwa na kiini, ute na ganda. Si mayai matatu kwa sababu ya mgawanyiko huo lakini ni yai moja lenye mkusanyiko wa mada tatu. Mungu akusaidie kulielewa vema fundisho hili muhimu.

Mfalme apoteza rafiki wa kwanza:

Viumbe wa kwanza ambao Mungu alifikiri kuwashirikisha upendo na ukarimu wake wa ajabu ni malaika. Hawa aliwaumba akiwapatia uwezo mkubwa kuliko wanadamu na viumbe wengine. Malaika mmoja aliyependelewa kuliko wengine wote aliitwa Lusifa. Nabii Ezekiel anamuelezea malaika huyu kwa lugha hii. Ezekieli 28:14-15, 17 Wewe ulikuwa kerubi mwenye kutiwa mafuta afunikaye; nami nalikuweka hata ukawa juu ya mlima mtakatifu wa Mungu, umetembea huko na huko kati ya mawe ya moto. Ulikuwa mkamilifu katika njia zako tangu siku ile ulipoumbwa, hata uovu ulipoonekana ndani yako. 17. Moyo wako uliinuka kwa sababu ya uzuri wako; umeiharibu hekima yako kwa sababu ya mwangaza wako; nimekutupa chini, nimekulaza mbele ya wafalme, wapate kukutazama. Moja ya sababu ya mabadiliko haya ya tabia ya Lusifa ni wivu. Malaika huyu ambaye baadaye aliitwa Shetani alimwonea wivu Yesu, na pia alichukizwa na taarifa kuwa Mungu amewaumba viumbe wengine kwa mfano na sura yake ambao pia amepanga wawe marafiki zake wa karibu. Baada ya malalamiko yake yaliyochukua muda mrefu kuonekana hayana mashiko, kikao kilipitisha kwa kauli moja atimuliwe mbinguni. Luka 10:18 Akawaambia, Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme. Ufunuo wa Yohana 12:4 Na mkia wake wakokota theluthi ya nyota za mbinguni, na kuziangusha katika nchi. Na yule joka akasimama mbele ya yule mwanamke aliye tayari kuzaa, ili azaapo, amle mtoto wake. Ufunuo wa Yohana 12:12 Kwa hiyo shangilieni, enyi mbingu, nanyi mkaao humo. Ole wa nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu.

Mfalme apoteza rafiki wa pili:

Baada ya kuwaumba malaika Mungu aliwaumba wanadamu wawili – mwanaume na mwanamke. Hawa wakawekwa kwenye bustani ya Edeni ili wauendeleze upendo wa Mungu kwa kuilima ardhi na kuitunza. Walipewa uhuru kamili wa kufanya chochote katika vitu vilivyowekwa chini yao isipokuwa jambo moja. Hawakuruhusiwa kula matunda ya mti ulio katikati ya bustani. Matunda ya mti huu hayakuwa na sumu, bali yaliwekwa kama kipimo cha utii wao kwa Mungu. Walitahadharishwa kutotengana wakati wote na kujihadhari na udanganyifu wa malaika aliyeasi na kufukuzwa mbinguni. Licha ya tahadhari zote hizo, Shetani alipoingia bustani ya Edeni alifanikiwa kumdanganya Hawa/Eva naye akamshawishi mumwe kushirikiana kula tunda hilo na hivyo dhambi ikawafikia wanadamu wote. Warumi 5:12 Kwa hiyo, kama kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi.

Kazi ya kuwatafuta marafiki yaanza:

Mungu alitumia muda mrefu kumwelewesha na kumsihi shetani aachane na madai yake hayo lakini haikufua dafu na yeye aliendelea kwa kiburi kutetea msimamo wake. Karibu theluthi moja ya malaika wote walijiunga na madai ya Shetani na shetani alipofukuzwa nao wakafukuzwa 
pia. Baada ya kutoka mbinguni shetani alielekea kwenye sayari zingine zenye kukaliwa na viumbe wa Mungu lakini hakufanikiwa kupokelewa isipokuwa katika dunia yetu. Baada ya wanadamu kujiunga na shetani kuupinga utawala wa Mungu, mbingu zikaja na mkakati wa ukombozi. Waliazimia kuwa mwanadamu ni lazima atafutwe na kurejeshwa kwa gharama yoyote ile. Siku ile ile wal;iyoanguka dhambini Mungu alikuja bustanini kuwatafuta. Mwanzo 3:7-9 Wakafumbuliwa macho wote wawili wakajijua kuwa wa uchi, wakashona majani ya mtini, wakajifanyia nguo.Kisha wakasikia sauti ya Bwana Mungu, akitembea bustanini wakati wa jua kupunga; Adamu na mkewe wakajificha kati ya miti ya bustani, Bwana Mungu asiwaone.Bwana Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi? Mdhambi hawezi kumtafuta Mungu. Ni Mungu daima anayemtafuta mwanadamu. Ni kama maji kukuta yakipanda mlima. Mfalme tunayewaletea habari zake yeye mwenyewe huwatafuta kondoo. Usijidanganye kuwa kwa kufanya matendo mema utamfurahisha Mungu. Matendo yanayomfurahisha Mungu ni yale yaliyotendwa kwa upendo kwa msaada wa Mungu tu. Isaya 64:6 Kwa maana sisi sote tumekuwa kama mtu aliye mchafu, na matendo yetu yote ya haki yamekuwa kama nguo iliyotiwa unajisi; sisi sote twanyauka kama jani, na maovu yetu yatuondoa, kama upepo uondoavyo.
 
Kumsaidia aliyepotea asipotee zaidi

Mungu ameunda uadui kati yako na shetani. Si mara zote unapopokea ushauri wake kwa sababu kupitia uzoefu umegundua ushauri wake umejikita kwenye kupoteza. Mungu ameunda kitu fulani kwenye akili/moyo wako kinachoitwa dhamiri kinachokusaidia usipotee. Unapokaribia kutenda dhambi au unapokuwa umekwisha kutenda dhambi dhamiri hukupigia kelele nzito. Mshukuru Mungu kama bado unayo hali hiyo. Wengine kifaa hicho wamekichomoa na sasa wanapotenda yaliyo kinyume hujiona ni sawasawa tu. Hawa hawana udhuru. Yohana 8:9 Nao waliposikia, wakashitakiwa na dhamiri zao, wakatoka mmoja mmoja, wakianzia tangu wazee hata wa mwisho wao; akabaki Yesu peke yake, na yule mwanamke amesimama katikati. Kilichofanya Adamu na Hawa wajifiche na dhamira zao ziliwasuta.

Dhamira ni sauti ya Mungu

Dhamira ni sauti ya Mungu. Kila sauti ya Mungu inaposikika masikioni mwa mwanadamu huleta muwasho fulani unaomwonesha makosa yake. Hata sauti ya Mungu ikiwa katika maandishi ina uwezo ule ule. Waebrania 4:12 Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo. Ili kuifanya sauti hiyo iwe ya kudumu Mungu aliazimia kuweka matamko kumi yenye nguvu yanayoitwa Amri Kumi za Mungu. Amri hizi ziliandikwa kwenye mbao mbili za mawe ili kuonesha ni za kudumu. Zinampambanua mwanadamu aliye mdhambi na aliye mtakatifu. Warumi 7:7 Tusemeje, basi? Torati ni dhambi? Hasha! Walakini singalitambua dhambi ila kwa sheria; kwa kuwa singalijua kutamani, kama torati isingalisema, Usitamani.
Mambo ambayo marafiki wa mfalme waliyapoteza
  1. Uzima wa milele. Warumi 6:23 Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.
  2. Uwezo wa kutenda mema. Yeremia 13:23 Je! Mkushi aweza kuibadili ngozi yake, au chui madoa-doa yake? Kama aweza, ndipo na ninyi mwaweza kutenda mema, ninyi mliozoea kutenda mabaya.
  3. Urithi na hadhi. Mwanzo 3:24 Basi akamfukuza huyo mtu, akaweka Makerubi, upande wa mashariki wa bustani ya Edeni, na upanga wa moto uliogeuka huko na huko, kuilinda njia ya mti wa uzima.
Leo hii ukiisikia sauti yake usifanye moyo kuwa mgumu.