Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

MASHAURI YA NDOA

MAWASILIANO KWENYE NDOA

Inatosha mwanamume kumpa mkewe fedha na kila kitu bila kuzungumza naye na kusikiliza hisia zake? Inatosha mwananke kumpa mapenzi ya kila aina mumewe wawapo chumbani bila kusema hisia zake kwake na kuwa tayari kufungua njia za kujadili mambo yanayowahusu? Hebu soma mfano huo hapo chini kwani kuna uvumbuzi wa ni kwa nini tunaweza kuwa na kila kitu kimapato au kisura na kimaumbile, lakini wapenzi wetu wakatuacha.


Johnson amerudi nyumbani kutoka kwenya shughuli zake na kama kawaida yake, salaam yake ya kwanza kwa mkewe ni kuuliza, “Mbona viatu vimewekwa njiani.” Huenda hiyo itabaki kuwa kauli pekee atakayobaki kuitafakari kwa muda mrefu ujao wa jioni ile. Baada ya hapo Johnson anaingia chumbani ambako hukaa sana hadi chakula kinapoiva. Mkewe anajaribu kumuuliza jinsi kazi zilivyokuwa kwa siku ile, lakini Johnson baada ya kujivuta sana anajibu kwa kifupi, “safi tu”.

Mkewe anajaribu tena kutafuta njia ya kuwasiliana na mumewe. Anajaribu kumsimulia jinsi gari moja la mchanga lilivyotaka kumuuwa utingo wake hapo mtaani mchana ule. Johnson anasikiliza habari hiyo bila kuonyesha hali yoyote ya mabadiliko na wala hajibu wala angalau kusema, “Hawa utingo nao ni hatari sana.” Haoni haja ya kufanya hivyo na hana sababu ya kujibu. Lakini bado anaamini na anadai kwamba huyo ni mkewe, tena wakati mwingine akisema ni mkewe mpendwa.

Wengi wetu ni kama Johnson au tuna waume kama Johnson. Tunaweza kuwa na kila kitu kwa upande wetu – yaani mali, umaarufu mkubwa, kazi nzuri, watoto wazuri na vinginevyo, lakini tukakosa hisia kwa wapenzi wetu. Tukakosa kuwa na uwezo wa kubaini haja ya kujali kuhusu hisia za tuwapendao au tunaodai kuwa tunawapenda. Kukosa uwezo wa kubaini hisia ni kushindwa kwetu kufungua njia na mawasiliano kwa wenzetu hao.

Mawasiliano katika ndoa ni nini? Inaweza ikaonekana kama vile swali hili ni rahisi kupatiwa jibu, lakini kwa kweli ni wanandoa wachache sana wanaoweza kutoa jibu sahihi la swali hili. Mawasiliano kwa wengi ni kuzungumza au kijibizana. Huenda hiyo ni kweli, lakini hata wanaogombana huzungumza na kujibizana pia. Mawasilino katika uhusiano kwa kifupi, lakini kwa ufasaha, yana maana ya wanandoa kuzungumza kila mmoja kwa uhuru na kwa uadilifu. Wanandoa au watu wengine wowote wanapowasiliana vizuri, huzungumza juu ya matatizo yao, furaha, huzuni na kile kinachoenda kwenye akili na kugusa mawazo ya kila mmoja. Mazungumzo ni yale yanayogusa hisia zao.

Huwa tunasema na kushauri kuhusu mawasiliano mazuri ndani ya ndoa. Huwa tunasisitiza sana kuhusu wapenzi kuwa makini wanapojaribu kusema au kuwasilisha hisia zao kwa wenzao. Lakini huenda ugumu uko kwenye kufahamu maana ya mawasiliano ndani ya ndoa, achilia mali mawasiliano mazuri. Lakini bila shaka kutokana na fasili hiyo fupi, tunaweza kuwa na picha angalau ndogo kuhusu maana ya mawasiliano katika ndoa. Mawasiliano mazuri yanajengwa na vitendo fulani ambavyo vikifanyika katika utaratibu fulani, ndoa hukomaa na kushika mizizi kwa kiwango cha juu sana cha uimara, na ambayo kama hayafanyiki, uwezekano ni kwa ndoa husika kuanguka.

Pengine mtu anaweza kuuliza, inakuwaje watu ambao tulikutana tukiwa hatujuani, tukavutiana kwa sababu mbalimbali hadi tukafikia uamuzi kwamba tunaweza kuishi pamoja, leo hii tushindwe kuzungumza kwa uhuru na uadilifu? Kwa nini wanandoa hushindwa kuwasiliana? Kuna sababu nyingi, lakini inayokusanya zote ni moja. Wengi hatujui umuhimu wa mawasiliano na pengine hatuoni kuwasiliana kama sehemu muhimu kwenye maisha yetu ya kindoa.Kuna wakati tunadhani kwamba kuwasiliana kunaweza kutuharibia uhusiano wetu badala ya kuujenga. Kwa hiyo, tunaamua kuzifukia hisia zetu, mawazo yetu na ushauri wetu vifuani mwetu.

Mtu amepatikana na tatizo, na anadhani akimwambia mwenzake atamvunja nguvu, atamtisha au atamfanya amlaumu au kumuona hana maana. Hivyo, anaamua kunyamaza. Tatizo lile linapokuja kufahamika baadaye, mwenzake hudhani alimficha kwa kutomjali, kutomwamini au kwa kutompenda. Badala ya kutatua tatizo, hali hiyo inakuwa imezua tatizo jipya. Lakini kuna ukweli ambao sisi kama binadamu, kila mmoja wetu ni lazima aukubali. Ukweli huu ni ule kwamba, ndani kabisa ya mioyo yetu huwa tunatamani kuzungumzia hisia zetu. Tungependa sana bila shaka kuonyesha undani wetu, yaani hisia zetu kwa wengine.

Si jambo la bahati nasibu kwamba wengi wetu tunajikuta tunataka au tuna rafiki wa karibu angalau mmoja (bila kujali kama umeoa au hujaoa) kwenye maisha yetu. Hii ni kwa sababu tunataka mahali pa kuonyesha nafsi zetu katika uhalisia wake, yaani mahali tunapoweza kusema tunavyohisi. Tungependa kuwa na mtu ambaye hatatudharau atakapotambua kuwa tuna mapungufu. Badala yake atashiriki nasi katika hisia hizo, ziwe mbaya au nzuri, za kutisha au kufurahisha, za aibu au za kuvutia.


Lakini tunakuwa na marafiki wa karibu si kwa sababu ya sisi kusikilizwa na kueleweka tu, bali pia ni kwa sababu tungependa kuwasikiliza wale ambao nao wanatusikiliza. Yaani kusikia hisia zao za ndani na ukweli unaoenda kwenye mawazo au hisia zao. Ukiangalia sana kutokana na ukweli huo, utaona kwamba, moja ya sababu ya kuoa au kuolewa ni kuwasiliana. Sasa kama kwenye ndoa kiwango cha mawasiliano ni cha hadhi ya chini sana kiasi hicho, hiyo ni sawa na kusema ndoa hiyo haipo kabisa.

Bila mawasiliano, ndoa inakuwa ni sawa na muungano wa watu wawili wanaoishi chini ya paa moja na siyo watu wawili wanopendana. Ni watu wanaokaa pamoja lakini si kwa umoja. Hebu tujiulize. Unawezaje kusema au kupima kwamba ndoa fulani haina mawasiliano? Suala hili linaonekana kama vile liko wazi sana, lakini kamwe siyo hivyo. Watu wengi kwenye ndoa wanakabiliwa na migogoro na kutoelewana kwingi, lakini kamwe hakuna ajuaye kati yao kwamba tatizo ni kukosa mawasiliano. Kukosa mawasilino kunaweza kuzaa hali ambayo ndiyo hasa chanzo cha tatizo ndani ya ndoa. Kukosa mawasiliano kwenyewe kuwe kumejificha au kuwe wazi, lakini kwa sababu hatujali kuwepo au kutokuwepo kwake kutafanya tushindwe kubaini tatizo.

Wakati mwingine ni kweli kwamba tatizo lililopo siyo kukosa mawasiliano, lakini kwa sababu hakuna mawasiliano, tatizo hilo huwa kubwa na pengine kuzaa matatizo mengine ambayo hatimaye huwa magumu kusuluhishwa. Matatizo ambayo yangesuluhishwa hufikia mahali yakaiangusha ndoa sababu yamekosa kusemwa na kutafutiwa ufumbuzi. Yatasemwa wapi na saa ngapi, wakati hakuna mawasiliano? Mjadala huu utaendelea….