Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

KUANDAA NA KUTOA MAHUBIRI

UANDAAJI NA UTOAJI WA MAHUBIRI

Kuhubiri ni kufanyaje?

Kuhubiri ni kutangaza habari njema za ufalme

Kumbukumbu la Torati 4:13 Akawahubiri agano lake, alilowaamuru kulitenda, yaani, zile amri kumi; akaziandika juu ya mbao mbili za mawe.

Zaburi 145:4-7  Kizazi kwa kizazi kitayasifu matendo yako, Kitayatangaza matendo yako makuu. Nitaifikiri fahari ya utukufu wa adhama yako, Na matendo yako yote ya ajabu. Watu watayataja matendo yako ya kutisha, Nami nitausimulia ukuu wako.Watalihubiri kumbukumbu la wema wako mkuu. Wataiimba haki yako.

Mathayo 24:14 Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja.

Kwa nini tunahubiri?

Tunahubiri ili kufikisha ukweli kwa watu wapate kuokolewa.

Matendo 14:15 “Wakisema, Akina bwana, mbona mnafanya haya? Sisi nasi tu wanadamu hali moja na ninyi; twawahubiri habari njema, ili mgeuke na kuyaacha mambo haya ya ubatili na kumwelekea Mungu aliye hai, aliyeumba mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo.”

Ni nani wanaotakiwa kuhubiri?

Mungu ameweka jukumu hilo kwa kila mfuasi wa Kristo, bila kujali umri au jinsia.

Marko 16:15 Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.

Je kuna watu maalumu walioitwa kwa jukumu la kuhubiri?

Ndiyo wapo watu maalum walioitwa kuwa wahubiri wakuu kwa kuwa kuna vitu maalumu Mungu amewekeza kwao.

Warumi 1:1 Paulo, mtumwa wa Kristo Yesu, aliyeitwa kuwa mtume, na kutengwa aihubiri Injili ya Mungu;

Nitajijuaje kama nina wito wa kuwa mhubiri?

Kama Mungu amekuita kuwa mhubiri mkuu watu watakuambia na wewe mwenyewe utakuwa na moto unaokusuma ndani yako

1 Wakorintho 9:16 Maana, ijapokuwa naihubiri Injili, sina la kujisifia; maana nimewekewa sharti; tena ole wangu nisipoihubiri Injili!

Nehemia 6:3 Na mimi nikatuma wajumbe kwao, nikasema, Hii ni kazi kubwa ninayoifanya mimi, hata nisiweze kushuka; mbona kazi ikome, hapo ninapoiacha, niwashukie?

Nawezaje kujua namna bora ya kuhubiri?

Kuhubiri ni uwezo utolewao na Roho Mtakatifu.

Luka 4:18-19 Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.

Marko 5:20 Akaenda zake, akaanza kuhubiri katika Dekapoli, ni mambo gani makuu Yesu aliyomtendea; watu wote wakastaajabu.

Nini sifa muhimu za mhubiri mwenye mafanikio?

Mhubiri mwenye mafanikio ni lazima awe mtu wa maombi, msomaji wa Maandiko na anayeyaishi anayohubiri.

Matendo ya Mitume 18:24 Basi Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mzalia wa Iskanderia, mtu wa elimu, akafika Efeso; naye alikuwa hodari katika maandiko.

Warumi 2:21-23 basi wewe umfundishaye mwingine, je! Hujifundishi mwenyewe? Wewe uhubiriye kwamba mtu asiibe, waiba mwenyewe? Wewe usemaye kwamba mtu asizini, wazini mwenyewe? Wewe uchukiaye sanamu, wateka mahekalu? Wewe ujisifuye katika torati, wamvunjia Mungu heshima kwa kuiasi torati?

Je mhubiri anahitaji kujifunza kwa wenzake njia bora zaidi ya kuwasilisha hubiri na uboreshaji wa kile anachowasilisha?

Kwa kuwa kuhubiri ni sanaa na sayansi inayozingatia vigezo kadha wa kadha ni fani inayofundishika.

Matendo ya Mitume 4:2 “Wakifadhaika sana kwa sababu wanawafundisha watu na kuhubiri katika Yesu ufufuo wa wafu.”

“Basi Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mzalia wa Iskanderia, mtu wa elimu, akafika Efeso; naye alikuwa hodari katika maandiko. Mtu huyo alikuwa amefundishwa njia ya Bwana; na kwa kuwa roho yake ilikuwa ikimwaka, alianza kunena na kufundisha kwa usahihi habari za Yesu; naye alijua ubatizo wa Yohana tu. Akaanza kunena kwa ujasiri katika sinagogi; hata Prisila na Akila walipomsikia wakamchukua kwao, wakamweleza njia ya Bwana kwa usahihi zaidi.” Matendo 18:24-26

Nini nini faida za kujifunza kuhubiri?

Mtu aliyepitia mafunzo ya kuhubiri ana uelewa mpana zaidi wa fani hiyo na matarajio ni kuwa atafanya vizuri zaidi katika jukumu la kuongoa roho

“Kazi ya kuongoa roho na kuzileta kwa Kristo inahitaji matayarisho yenye uangalifu. Mtu hawezi kuingia katika utumishi wa Bwana bila mafunzo yanayohitajika, na kutarajia mafanikio ya juu.” – Gospel Workers, p. 92. (1915). {Evangelism p. 128.1}

“Bwana anakualika kufanya maboresho ya makusudi katika namna yako ya kuwasilisha ukweli. Huhitaji kuwa mtu wa misisimko. Lihubiri Neno, kama Kristo, Mwana wa Mungu, alivyolihubiri Neno.” {Evangelism p. 184.1}

KANUNI ZA UANDAAJI NA UTOAJI WA MAHUBIRI

Kuhubiri ni sanaa na sayansi yenye kanuni zake na hivyo ni muhimu kuzijua kanuni hizo. Katika Sanaa na Sayansi ya kuhubiri tunajifunza;

 1. Kusudi la Hubiri
 2. Vyanzo vya Mahubiri
 3. Aina za Mahubiri
 4. Muundo wa Hubiri
 5. Uwasilishaji wa Hubiri

Nini lengo la hubiri?

Hubiri ni lazima liwe na lengo ambalo mhubiri angependa kulifikia

Wakolosai 1:27-28 Ambao Mungu alipenda kuwajulisha jinsi ulivyo utajiri wa utukufu wa siri hii katika Mataifa, nao ni Kristo ndani yenu, tumaini la utukufu, ambaye sisi tunamhubiri habari zake tukimwonya kila mtu, na kumfundisha kila mtu katika hekima yote, tupate kumleta kila mtu mtimilifu katika Kristo.

Matendo 14:15 “Wakisema, Akina bwana, mbona mnafanya haya? Sisi nasi tu wanadamu hali moja na ninyi; twawahubiri habari njema, ili mgeuke na kuyaacha mambo haya ya ubatili na kumwelekea Mungu aliye hai, aliyeumba mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo.”

Hubiri unalipataje?

Hubiri hupatikana kwa kurudia hubiri ulilolisikia, au alilolisoma mahali. Lakini njia bora ya kupata hubiri ni kwa kuangalia hali isiyoridhisha iliyopo katika jamii inayohitaji usahihishwaji kwa njia ya maonyo ama maelekezo.

Matendo 13:32 Na sisi tunawahubiri habari njema ya ahadi ile waliyopewa mababu.

Matendo 17:23 “Kwa sababu nilipokuwa nikipita huko na huko na kuyaona mambo ya ibada yenu, naliona madhabahu iliyoandikwa maneno haya, KWA MUNGU ASIYEJULIKANA. Basi mimi nawahubirini habari zake yeye ambaye ninyi mnamwabudu bila kumjua.”

Kuna aina ngapi kuu za mahubiri?

Kuna aina kuu mbili za mahubiri (a) Mahubiri ya Ufafanuzi wa aya (2) Mahubiri yaliyojengwa kwenye mada, (3) Mahubiri ya fungu moja

Mahubiri ya Ufafanuzi yakoje?

Ni mahubiri yanayojikita katika ufafanuzi wa aya iliyochaguliwa ikiangalia mtunzi, wakati, mahali, sababu za kuandikwa kwake, lugha iliyotumika, wahusika, kusudi na ujumbe wa aya husika.

Luka 4:16-22 Akaenda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake, akasimama ili asome. Akapewa chuo cha nabii Isaya, akakifungua chuo, akatafuta mahali palipoandikwa, Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa. Akakifunga chuo, akamrudishia mtumishi, akaketi; na watu wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho. Akaanza kuwaambia, Leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu. Wakamshuhudia wote, wakiyastaajabia maneno ya neema yaliyotoka kinywani mwake, wakasema, Huyu siye mwana wa Yusufu?

Mahubiri ya Mada yakoje?

Ni mahubiri yanayojikita kwenye mada moja iliyoteuliwa ikitumia mafungu kutoka sehemu mbalimbali za Biblia.

Mfano: Kulijua Neno la Mungu

Kichwa cha Somo: Faida za Kulijua Neno la Mungu

I. Kulijua Neno la Mungu humfanya mtu kuwa na hekima ya wokovu (2Tim. 3:15)

II. Kulijua Neno la Mungu humwepusha mtu kutenda dhambi. (Zaburi 119:11)

III. Kulijua Neno la Mungu hutupatia ukuaji wa kiroho (I Pet. 2:2)

IV. Kulijua Neno la Mungu husababisha maisha ya ushindi (Joshua. 2:7-8)

Hubiri la Fungu Moja Likoje?

Ni hubiri lililojengwa juu ya fungu moja ambalo hufanyiwa uchambuzi na ufafanuzi wa kina ili kupata maana zaidi.

Mfano: Mungu Wetu Yukoje? (Isaya 40:28)

 1. Kamwe Hakati tamaa
 2. Hachoki wala Hazimii
 3. Akili Zake Hazina Ukomo

Zoezi:

 • Andaa hubiri la fungu moja kutoka Isaya 1:18 ukionesha kichwa cha somo, na mgawanyiko wa ufafanuzi wako.
 • Andaa mahubiri ya ufafanuzi wa aya kwa kutumia mafungu yafuatayo ukichagua kichwa cha somo, wazo kuu, na mgawanyo wa mada ndogondogo, Kutoka kitabu cha Waebrania sura ya 11

“Abel – Kafara ya Imani” (Mwa. 4:1-5; Waeb. 11:4)

“Enoki – Mwendo wa Imani” (Mwa. 5:21-24; Waeb . 11:5-6)

“Abraham – Utii wa Imani” (Mwa. 12-18; Waeb. 11:8-10)

“Isaac – Njozi ya Imani” (Mwa. 26, 27; Waeb. 11:20)

“Jacob – Utambuzi wa Imani” (Mwa. 27-35; Waeb 11:21)

“Joseph – Uhakika wa Imani” (Mwa. 37-50; Waeb. 11:22)

MUUNDO WA HUBIRI

Hubiri limegawanyika katika sehemu kuu tano:

 1. Kichwa cha somo
 2. Kusudi la somo
 3. Utangulizi
 4. Hubiri
 5. Hitimisho na wito

Kichwa cha somo kinapatikanaje na kina umuhimu gani?

Kichwa cha somo kinatoa mwaliko kwa wasikilizaji juu ya kile kinachokwenda kuzungumziwa. Kinasaidia kuvuta usikivu na kinaelezea wazo kuu la hubiri. Kichwa cha somo kinachofumba ni bora zaidi kuliko kilicho wazi. Ni muhimu kutambulisha kichwa cha somo kabla ya hubiri ili kukusaidia kutohama kwenye wazo kuu la hubiri

Zoezi: Tafuta kichwa cha somo cha Yohana 3:16, Waebrania 4:9, na Ufunuo 12:17

Kusudi la somo linapatikanaje na lina umuhimu gani?

Kusudi la somo (ambalo kwa kawaida hulitangazi kwa wahubiriwa) huonesha kile mhubiri anachokusudia kufanikisha katika hubiri lake. Kusudi linawakilisha hitaji la watu anaowahubiria kwa wakati husika.

Utangulizi ni nini na una umuhimu gani?

Utangulizi ni maelezo ya mwanzo mhubiri anapojiandaa kuhubiri ambayo huwaandaa wasikilizaji kupokea ujumbe aliouandaa. Hapa mhubiri atasalimia, atajitambulisha, atatambulisha somo na kuleta kisa kinachobeba wazo kuu na kusudi la somo lake. Kisa cha maisha ni bora zaidi na badala ya kisa pia anaweza kuleta dondoo au kufanya kielelezo fulani. Utangulizi unamfanya msikilizaji kutulia na kutamani kuendelea kuwepo ili kujua hitimisho la hubiri. Visa viwe na uhalisia na vile vya wanyama wanaopewa uwezo wa kibinadamu viepukwe kadri iwezekanavyo.

Mwili wa hubiri ni nini na una umuhimu gani?

Hapa ndipo penye hubiri lenyewe likiwa limegawanyika katika mada ndogo ndogo ili kuthibitisha wazo kuu la hubiri. Ushahidi wa Maandiko na wasemaji wengine unahitajika hapa ili kushawishi kuwepo kwa tatizo linalohitaji ufumbuzi wa haraka. Mada ndogo ndogo ziwe kati ya tatu na tano ili hubiri lisiwe refu la kuchosha. Mada ndogo ndogo ziwe katika mtiririko wenye uwiano.

Hitimisho na Wito ni nini na ina umuhimu gani?

Hitimisho ni hatua ya kumaliza hubiri ambayo hutoa muhtasari wa kilichozungumzwa na kumwaandaa msikilizaji kufanya maamuzi. Kisa cha kutolea wito kitahitajika na wito unaweza kuwa wa kuinua mkono, kuwainua, au kuwaita mbele wale wanaotaka kufanya maamuzi.

UWASILISHAJI WA MAHUBIRI

Uwasilishaji wa mahubiri hufanikiwa mambo kadhaa yanapozingatiwa. Mambo hayo ni; Mwonekano

 1. Matumizi ya wakati
 2. Matumizi ya mwili
 3. Kiwango cha usikivu
 4. Matumizi ya sauti.

Mwonekano

Mwonekano ni wa muhimu kwa mhubiri maana unabeba ujumbe unaochangia kukubaliwa na wasikilizaji ama kukataliwa hata kabla hajaanza kuhubiri. Mhubiri aliye makini atajali vile anavyotokea kwa watu.

“Mtumishi ni lazima akumbuke kwamba hisia za kuridhishwa ama za kutoridhishwazinaendelea kwa wasikilizaji wake kutokana na mwonekano wake mimbarani, tabia yake, namna yake ya kuongea, na nguo zake. Ni lazima akuze tabia njema na kuboresha mwenendo, na ajichukulie mwenyewe heshima tulivu ili kuufikia wito wake mkuu. Udhati na mamlaka fulani ya Kimungu vilivyochanganyika na unyenyekevu , ni lazima viwe sehemu ya tabia yake.” {GW 172.1}

Mwonekano wenye matumaini

Mwonekano uwe wa mtu anayejiamini na aliyejaa matumaini. Mwonekano huo utajidhihirisha kupitia unavyotembea, unavyosimama, unavyoangalia watu na unavyoongea. Mwonekano wa huzuni unahafifisha ujumbe. Mwombe Mungu akusaidie kuishinda hali yoyote inayoharibu mwonekano wako.

Mwonekano nadhifu

Mwonekano nadhifu unahusu usafi wa mwili na mavazi ya nje na ndani, utunzaji wa nywele, kucha, mdomo, macho, na masikio, utayarishwaji, uchaguzi na mpangilio wa mavazi. Uwe na kitambaa cha kufutia jasho, tongotongo za macho, na povu la kingo za midomo. Meno yasuguliwe kuondoa mabaki ya chakula yanayoweza kukupa mwonekano usiovutia na kusababisha harufu mbaya mdomoni. Nguo zisiwe na makunyanzi, zinazooana vizuri, zenye adabu na zinazokubalika katika jamii. Zisiwe na maandishi au picha zinazoleta maswali kwa watazamaji. Hakikisha zipu yako imefunga vizuri na suruali yako ina uwezo wa kubaki kiunoni endapo mkanda utakatika ghafla.

Epuka mazoea yanayoudhi.

Mazoea yanayoudhi ni pamoja na kujipangusia jasho mikononi, kuchokonoa pua na masikio kwa vidole, kupandisha makamasi, kukata kucha kwa meno, kushika na kuifunua Biblia bila kuonesha staha, kuomba muda mrefu, kulazimisha watu kutamka au kufanya vitendo fulani fulani, kujigamba na kudharau watu au matusi. Usipendelee kuweka mikono mfukoni maana kwa wengine hiyo ni dalili ya dharau.

Matumizi ya wakati

Muda uliopangwa kuanza hubiri ukifika anza kuhubiri. Usipoteze muda kusubiri watu waongezeke au kuomba msamaha kwa kuchelewa. Hubiri liwe la nusu saa, dk 45 na kama ni lazima saa moja. Usikivu wa watu huanza kupungua baada ya nusu saa. Si lazima hubiri uliloliandaa liishe. Kipimo kizuri cha kumaliza hubiri ni pale unapoona umejenga hoja zako vya kutosha kuweza kuwatolea watu mwito. Watu waliochoka kukusikiliza wanaonekana. Usisubiri watu wakafikia mahali pa kukuchoka kwa sababu wito wako hautafanikiwa.

“Wahubiri wengi wanapoteza muda wao na nguvu zao katika kutoa udhuru mrefu wanapoanza mahubiri. Wengine hutumia karibu nusu saa kuomba msamaha, na hivyo muda unapotea, na wanapofikia wakati wa kutoa somo lao na kujaribu kukazia ujumbe wa ukweli mioyoni mwa wasikilizaji wao, watu wamechoka na hawezi kuona nguvu yao.” {GW 168.2} 

 “Usikatishwe tamaa unapokuta watu wachache wapo kusikiliza mkutano. Hata kama unao wasikilizaji wawili watatu, nani ajuaye kama siyo hao ambao Roho wa Bwana aliokuwa amewakusudia? Mungu anaweza kukupatia ujumbe kwa ajili ya roho hiyo moja, na akishaongoka, akawa njia ya kuwafikia wengine. Yote yamefichwa kwako, matokeo ya kazi yako inaweza kuzidishwa mara elfu.”    {GW 167.2} 

Usiviangalie viti vitupu, na kuruhusu imani yako na ujasiri wako kuzama; bali fikiria kile Mungu anachofanya kuleta ukweli kwa ulimwengu. Kumbuka kwamba unashirikiana mawakala wa mbinguni – mawakala ambao kamwe hawashindwi. Ongea kwa dhati, kwa imani, na kwa mvuto kana kwamba kuna watu alfu moja waliohudhuria wanaosikiliza sauti yako. {GW 167.3}

Ikiwa umeanza hubiri muda ukiwa umeenda sana, patana nao muda wa kumaliza hubiri lako au waahidi kumaliza mapema. Usichelewe kuanza kwa maelezo mengi yasiyo na msaada kwa hubiri lako na usitumie mafungu mengi. Kwa kawaida mafungu matano, saba na ama kumi yanatosha kwa hubiri. Kumbuka hata fungu moja linatosha kuhubiria na kutoa wito. Jifanyie mazoezi ya kuhubiri kwa dakika tano ili umudu kufupisha hubiri pale inapokuwa lazima.

Hebu ujumbe wa wakati huu uwasilishwe, siyo kwa hubiri refu la kuchosha, lakini kwa mazungumzo mafupi, yanayokwenda moja kwa moja ujumbe. Mahubiri marefu huchosha nguvu za mhubiri na subira ya wasikilizaji wake. Kama mhubiri ni yule anayejali umuhimu wa hubiri lake, atahitaji kuwa mwangalifu asije akazichosha nguvu za mwili wake na kuwapatia watu kingi kuliko wanachoweza kukumbuka. {GW 167.5} 

Kiwango cha usikivu

Kukosa usikivu kutokana na hali ya eneo la mkutano.

 • Je, eneo la mkutano linaruhusu mzunguko mzuri wa hewa? Matendo ya Mitume 20:9 Kijana mmoja, jina lake Eutiko, alikuwa ameketi dirishani, akalemewa na usingizi sana; hata Paulo alipoendelea sana kuhubiri, akazidiwa na usingizi wake akaanguka toka orofa ya tatu; akainuliwa amekwisha kufa.

“Mara nyingi mhubiri amelazimika kuhubiri kwenye chumba kilichofurika, na chenye joto jingi. Wasikilizaji wanapatwa na usingizi na akili zao hupotea na inakuwa karibu haiwezekani kwao kushika ukweli unaotolewa.”  {GW 166.3} 

Kukosa usikivu kutokana na kuwepo kwa makelele

 • Je, kuna kelele zinazoingiliana na mahubiri? Eneo la mkutano lisiingiliane na kelele kutoka nje au kutoka ndani. Badilisha muda au eneo la mkutano kuepuka kelele hizo au inapobidi waone wahusika na kuwaomba wapunguze kelele. Hakikisha kelele za simu zinathibitiwa kwa kuzima au kuziweka kwenye ukimya wewe mwenyewe ukiwa mfano wa jambo hilo. Matendo ya Mitume 21:34 Wengine katika makutano wakapiga kelele wakisema hivi, na wengine hivi. Basi alipokuwa hawezi kupata hakika ya habari kwa sababu ya zile kelele, akatoa amri aletwe ndani ya ngome.
 • Je, kuna kiwango cha kutosha cha usikivu wa vyombo unavyotumia? Hakikisha vyombo unavyotumia havitoi kelele zinazoleta usumbufu kwa na kupoteza usikivu.

Kukosa usikivu kutokana na sauti kutowafikia watu

Hakikisha sauti yako inawafikia walio karibu na walio mbali. Waulize wasikilizaji waliokaa mbali kama wanakusikia na ikiwa hawakusikii rekebisha ukubwa wa sauti yako ama waambie wasogee mbele. Katika kipindi hiki cha mawasiliano ya habari mhubiri anatakiwa kutumia vyombo vinavyotuma sauti mbali katika hali nzuri ya usikivu.

Kukosa usikivu kutokana na lugha unayotumia

Usipendelee kutumia maneno magumu na hakikisha lugha unayoitumia inaeleweka vyema na wasikilizaji wako vinginevyo uwe na mkalimani. Siku hizi wenye ulemavu wa kusikia huja kwenye mikutano ya mahubiri hivyo ni muhimu pia kuwaandaa wakalimani watakaotafsiri hotuba yako katika lugha ya ishara wanayoielewa wenye ulemavu wa kusikia. Mwombe Mungu akujalie kipawa cha kufahamu lugha za watu maana ina mvuto wa pekee katika shughuli hii ya kuhubiria watu hasa katika maeneo ya ugenini. Matendo 2:11 Wakrete na Waarabu; tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu.

Kukosa usikivu kutokana na kutosikia kilichotamkwa

Hakikisha unatamka wazi wazi maneno yako bila kuyamung’unya. Watu wasipoyaelewa matamshi yako huchoka kusikiliza na hivyo kupoteza ujumbe ambao ungewafaa. Usifume midomo wakati wa kutamka maneno. Tamka maneno kwa kuumba midomo inavyotakiwa na kwa maneno mageni au ya lugha ya kigeni yafanyie mazoezi mapema jinsi yanavyotamkwa. 1 Wakorintho 14:8-9 Kwa maana baragumu ikitoa sauti isiyojulikana, ni nani atakayejifanya tayari kwa vita? Vivyo hivyo na ninyi, msipotoa kwa ulimi neno lililo dhahiri, neno lile linenwalo litajulikanaje? Maana mtakuwa mkinena hewani tu.

Kukosa usikivu kutokana na sauti kuwa moja isiyopanda isiyoshuka

Hakikisha sauti yako inashuka na kupanda. Kuhubiri kwa sauti moja kunachosha na kupoteza usikivu. Mwombe Roho Mtakatifu akujulishe mahali panapofaa kupandisha na pa kushusha sauti. Kuhubiri ni kuzungumza si kufoka au kugombeza tu muda wote.

Matumizi ya mwili

Ni vizuri mhubiri ahubiri akiwa amesimama na si akiwa amekaa isipokuwa pale inapokuwa lazima kufanya hivyo. Mhubiri ajue kulitawala jukwa kwa kutembea tembea kila baada ya muda fulani kuhakikisha kuwa watu wote anawaona. Asisimame mahali pamoja kama mlingoti wa umeme. Atumie viungo vyake wakati anapozungumza ili kuweka msisitizo. Mikono, vidole vya mikono, miguu, na kiwili wili chote kihusike katika kuwasilisha mada. Kusudi hapa ni kuleta uhalisia wa unachokisimulia ili watu wajihisi wapo kwenye eneo la tukio unaloliongelea. Hiyo itawafanya wakumbuke zaidi, waelewe zaidi na waguswe zaidi.

Uso wa mhubiri uwe mchangamfu uliojaa matumaini. Beba hisia zinazoendana na unachokisimulia. Huzunika, cheka, na unyesha mshangao, pale inapobidi. Macho yako yawaangalie unaowahubiria na wala usiangalie juu ya vichwa vyao au chini. Watu wanapenda kuona uso na macho ya mhubiri.

Usisimame kwa mguu mmoja au kwa kuegemea nguzo, ukuta au kwa kuegemea kibweta. Usiweke mikono nyuma au kushika kiuno au kuweka kichwa upande kila wakati. Hali hiyo kwa wengine huashiria kuwa mhubiri amekosa kujiamini. Pia si desturi nzuri kutupatupa mikono hewani kama kichaa au kugonga gonga meza au kuzungumza ukiwa chini ya meza, sakafuni, au mahali usipoweza kuonekana kirahisi.

Matumizi ya Sauti

Mhubiri anatakiwa kuilinda sauti yake ili iendelee kuwa kwenye ubora wakati wote kwa kuwa sauti ni nyenzo muhimu inayobeba ujumbe wake. Ili sauti ibaki katika ubora ni lazima utoke tumboni na kutokea mdomoni bila kuminywa kooni. njia nyingine za kudumisha ubora wa sauti ni kuepuka mavumbi kuingia mdomoni ama puani, kuepuka vinywaji vyenye sukari na kunywa maji ya kutosha