Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

SIMULIZI ZENYE TAFAKURI

USIMTUPE MAMA YAKO

Kuna kijana mmoja daktari alikwenda kuposa. Binti aliyemposa akamuwekea masharti mazito. Akamwambia chagua mawili ama kunioa mimi au kukaa na mama yako, kwa sababu ukinioa mimi sitokubali mama yako aje hata harusini kwangu achilia mbali kuishi naye! Yule kijana alilemewa asijue la kufanya. Akawa anajihoji, “Mke namtaka, lakini mama yangu pia nampenda.” Baada ya kukosa majibu aliamua kuomba ushauri kwa mwalimu wake wa Chuo Kikuu.
Alimwambia moyo wangu unampenda mno binti niliyekwenda kumposa, lakini pia siwezi kuishi mbali na mama yangu. Nifanye nini?

Yule mwalimu mwenye hekima ambaye alikuwa anajua taabu alizopitia mama wa kijana yule, alimjibu kwa kumwambia; “Kabla sijakueleza uchague yupi kati ya wawili hao, rudi nyumbani, na leo usifanye chochote, ila kuosha mikono ya mama yako.” Yule kijana alifanya kama alivyoshauriwa na mwalimu wake. Alipofika nyumbani aliomba idhini kwa mama yake amruhusu kuiosha mikono yake, na yule mama kwa kuona kijana wake amesisitiza sana alimkubalia bila ya ajizi yoyote.

Yule kijana alipoanza kuosha mikono na viganja vya mama yake na kuona jinsi vilivyokakamaa kwa kazi za sulubu, alilia sana. Muda wote huu alikuwa hajawahi kuangalia viganja vya mama yake kwa karibu. Wakati huo ndipo alipofahamu kisa kilichofanya mama yule apate shida zote zile. Kumbe baba wa yule kijana alifariki dunia yeye akiwa bado mdogo, na kwa bahati mbaya alidhulumiwa mali walizochuma na baba wa yule kijana na watu waliojitambulisha kama ndugu wa karibu wa marehemu.

Yule mama aliamua kusamehe kila kitu kwa ajili ya mustakbali wa mwanawe. Alikubali kuwa mtumishi wa ndani, kufua nguo, kupiga deki na kila kazi ambayo alihisi ingelimletea chumo la halali bila ya kujali ugumu wa kazi yenyewe. Juhudi zake zilizaa matunda na kufanikiwa kumlea na kumsomesha mwanawe hadi Chuo Kikuu na sasa ni daktari ambaye ana mustakbali mzuri. Baada ya yule kijana kupata ufafanuzi huo wote alifanya haraka kumpigia simu mwalimu wake huku macho yakiendelea kububujikwa na machozi na kumwambia; “Siwezi kusubiri hadi kesho. Jibu nimeshalipata. Siwezi kumtupa mama yangu kwa ajili ya mtu asiyejua thamani ya mama yangu. Ahsante sana kwa kunionesha ufumbuzi wa uchaguzi uliokuwa unanikabili! Kamwe siwezi kumuuza mama yangu kwa ajili ya mtu niliyekutana naye katika hatua za mafanikio, na kumtelekeza mama yangu, aliyeyatumia maisha yake yote kwa ajili ya mafanikio yangu.

Katika hatua hii ya mafanikio umemfanyia nini mama yako kinachoonesha unatambua mchango wake maishani mwako? Usimtupe. Mfariji kwa kadri unavyoweza hata kama dunia inakutaka umkane.

MWANANGU:

1. Mwanangu, mwanamke anaweza kuwa mkeo, mwingine anaweza kuwa mama wa watoto wako, lakini ukipata mwanamke ambae atakuwa kama mama kwako, mama kwa wanao na mama kwa familia, tafadhali mwanangu usimuache huyo!

2. Mwanangu, usimfanye mwanamke wako kuwa ndio wa kupika na kufanya kazi zote za jikoni peke yake, tabia hiyo sio nzuri Kwani hata nyakati zetu, mashamba yetu yalijulikana kwa majina yetu wanaume lakini tulifanya kazi pamoja!

3. Mwanangu, nikikwambia wewe ni kichwa cha familia, simaanishi kutuna kwa pochi lako, usiangalie kabisa pochi yako, angalia kama utaona tabasamu usoni kwa mke wako. Pesa sio kila kitu katika ndoa na haileti ukuu wa familia!

4. Mwanangu, ukitaka kuwa na maisha marefu na ukapunguza misongo ya mawazo, ongea na mkeo pangeni bajeti ya mahitaji yenu, kisha mwache mkeo awe na jukumu la kuratibu mahitaji ya kila siku ya familia kwa kumkabidhi fungu husika hata kama limetokana na michango yenu wawili. wanawake wanajua sana kupanga bajeti na hii haitakuwa rahisi kwa yeye kutumia hela hovyo wakati akijua kuwa nyumbani kuna mahitaji ya msingi, lakini hela zikiwa mikono mwako ataendelea kuomba hata kama utakuwa umeishiwa!

5. Mwanangu, Usithubutu kumpiga mkeo, maumivu ya kipigo hukaa ndani ya moyo wake kwa muda mrefu sana na huacha kidonda ambacho hukawia sana kupona. Ni hatari sana kuishi na mwanamke mwenye majeraha moyoni!

6. Mwanangu, sasa unaamua kuoa,kama bado utaendelea kuishi maisha kama ya ubachela na mke wako, sio muda mrefu utakuwa bachela tena. ukioa Badilika anza kuishi maisha ya mke na mume!

7. Mwanangu, zamani,tulikuwa na wake wengi na watoto wengi kwa sababu tulikuwa na mashamba makubwa na mavuno yalikuwa makubwa, lakini kwa sasa maisha yamebadilika, kwa hiyo mkumbatie mwanamke wako peke yake kwani hakuna ardhi tena na mahitaji ya watoto ni makubwa sana. Angalia ukubwa wa familia yako!

8. Mwanangu, chini ya mwembe ambao nilikuwa nikikutana na mama yako inaweza kuwa ni hoteli kubwa kwa nyakati zenu,lakini kumbuka, kitu pekee tulichoweza kufanya chini ya mwembe ilikuwa ni kukumbatiana pekee.nakushauri ukikutana na marafiki wa kike kikubwa unachoweza kufanya nao ni kupeana mikono na ikizidi ni kukumbatiana hadharani sio vinginevyo!

9. Mwanangu, usibadilike mara utakapoanza kupata mafanikio Zaidi, kuliko kuwahudumia hao viruka njia wa mtaani ambao hawajui mmetoka wapi na mkeo, nakushauri utumie na kufurahia mafanikio yako na mkeo ambae aliweza kusimama imara wakati wote wa mapito yenu magumu.

10. Mwanangu, kumbuka unapoanza kusema au kuona mke wako kabadilika, ujue kuwa kuna kitu ambacho ulikuwa ukikifanya umeacha kukifanya. Jitathmini na anza kufanya au kutimiza wajibu wako.

11. Mwanangu, usijaribu kumfananisha au kumlinganisha mke wako na mwanamke mwingine wa nje, kwani hata yeye anakuvumilia sana na hajakufafanisha na mwanaume mwingine yoyote huko nje na ndio maana aliamua kuwa na wewe.

12. Mwanangu, sasa hivi kuna hiki kitu kinaitwa haki za wanawake, sawa,kama mwanamke anasema ana haki sawa na wewe katika nyumba, basi gawanya mahitaji yote ya ndani kwenu katika sehemu mbili zilizo sawa,halafu timiza nusu yako na mwambie atimize nusu iliyobaki.

13. Mwanangu, nilimuoa mama yako akiwa bado kigoli (bikra) na nilikuwa naenda sana kwao kabla sijamuoa, lakini kutomkuta mkeo bikra kusikufanye umlaumu kuwa alikuwa muhuni, kumbuka wanawake wa enzi zetu na wasasa ni tofauti, ulimchagua mwenyewe na ukigoli wake hukuujua kabisa. Usiingize mambo ya kabla ya ndoa kwenye ndoa yenu.

14. Mwanangu, sikuwapeleka dada zako shule kwa kuwa nilikuwa mjinga kama wazee wengi wa hapa kijiji wasemavyo, tafadhari usifanye ujinga huu, kwani kiwango cha mafanikio ya wanawake sasa kimefanya wanaume waonekane ni watu wa kawaida sana na sio muhimu kama enzi zetu. Ukijaliwa watoto wape elimu.

15. Mwanangu, zamani enzi za ujana wetu, wanawake walikuwa na urembo wa asili, ingawa siwezi kukudanganya, wengine waliongeza urembo kwa kujichora hina na hata kutoboa pua na masikio lakini usisahau hawakuonyesha maumbile yao nyeti hadharani kama sasa. Hakikisha mkeo analijua hili!

16. Mwanangu, mama yako na mimi hatuna hisa katika kila kitu kinachoendelea kwenye maisha yenu, jaribuni kutatua changamoto zenu wenyewe bila kila mara kuja kwetu kuomba usuluhishi. Ndoa ni pamoja na ukomavu wa kutatua changamoto zenu bila kuziuza kama gazeti kwa kila mtu.

17. Mwanangu,nilimnunulia mama yako kifaa cha kupikia vitumbua ili aanzishe mradi wa kuuza vitumbua, pia nilimsaidia kununua cherehani yake ya kwanza, tafadhari msaidie mke wako kutimiza ndoto zake kulingana na uwezo wako kama ambavyo unahangaika kutimiza ndoto zako.

18. Mwanangu, usiache kutusaidia mimi na mama yako, utu uzima una changamoto nyingi sana na Mungu akikujalia utaziona muda ukifika. Pamoja na kutimiza majukumu yako kama baba wa familia kumbuka pia bado tunaishi na wewe ni mtoto wetu.

19. Mwanangu, kila upatapo muda wa kusali, Sali na familia yako, kuna kesho ambayo huijui, ongea na MUNGU wako ambae anajua kila kitu kila siku!

20.NAKUTAKIA MAISHA MEMA YA NDOA MWANANGU….NAKUPENDA!

 

NIKAONA MAITI ZAO KANDO YA BARABARA:

Ilikuwa ni mwaka 1979, nikiwa nasafiri kutoka Dar es salaam kwenda Arusha. Sijui ilikuwaje, lakini ilitokea. Tuliondoka Dar es salaam saa 12:30 jioni. Wakati ule mabasi yalikuwa yakisafiri jioni na usiku, siyo kama siku hizi. Nilikuwa nakwenda Arusha kwenye usaili kwa ajili ya ajira, nikiwa ndo kwanza nimemaliza kidato cha nne. Niliajiriwa moja kwa moja serikalini, kwani siku zile ajira zilikuwa ni za kumwaga. Hata hivyo, sikulizishwa na kazi niliyokuwa nafanya, hivyo niliomba kazi kwenye kampuni moja kule Arusha na niliitwa kwa usaili.

Tulifika mji unaoitwa Korogwe, ambao wakati ule ulikuwa ndiyo mji maarufu kwa hoteli zake katika barabara yote ya Segera hadi Moshi na Arusha. Tulipofika Korogwe, basi lilisimama kwa ajili ya abiria kupata chakula. Niliingia kwenye hoteli moja ambayo nakumbuka hadi leo kwamba, ilikuwa ikiitwa Bamboo. Niliagiza chakula na kula haraka kutokana na muda mfupi wa kula uliotolewa na wenye basi la TTBS ambalo ndilo nililosafiri nalo.

Wakati wa kulipa ndipo niliposhangaa na kuogopa. Niliingiza mkono mifukoni na kukuta kwamba, sikuwa na hela. Nilianza kubabaika na mwenye hoteli alisema hawezi kukubali ujinga huo. “Abiria wengine wahuni bwana, anakula na kujifanya kaibiwa, ukikubaliana nao kla siku hasara tu.” Mwenye hoteli alisema kwa kudhamilia hasa.
Kulizuka zogo kubwa, huku mwenye hotel akisema ni lazima anipeleke polisi. Ni kweli, alimtuma mmoja wa watumishi wake kwenda kituo cha polisi ili nishughulikiwe.

Hapo hotelini kulikuwa na bwana mmoja aliyekuwa amekaa pembeni na mkewe na mtoto wao wakila. Yule bwana alipoona vile, alimtuma mhudumu mmoja aniiite. Niliondoka pale kaunta nilipokuwa nabembeleza na kuja kwa yule bwana. Alikuwa ni kijana mtu mzima kidogo, mwenye miaka kama 50 hivi. Nilimsalimia na aliniitikia. Nilimsalimia mkewe pia. Yule mtu aliniuliza kisa cha vurugu ile na nilimsimulia. Aliniuliza sasa huko Arusha ningeishi vipi wakati wa usaili kama nilikuwa nimeibiwa fedha zote, na ningerudi vipi Dar es salaam. Nilimwambia nilikuwa napanga kuangalia namna ya kurudi Dar es salaam, kama huko polisi ningeaminika.

Kama mzaha, bwana yule aliniambia angenipa fedha za kutumia huko Arusha na nikirudi Dar es salaam, nimrudishie fedha zake. Nakumbuka alinipa shilingi 90 kwa ahadi kwamba nikirudi Dar es salaam, nimpelekee pesa zake ofisini kwake. Alinielekeza ofisini kwake, mtaa wa Nkurumah na kuniambia kwamba, ameamua kunisaidia kwa sababu, kila binadamu anahitaji msaada wa mwingine na maisha haya ni mzunguko.
Nilishukuru na kuondoka kukimbilia basini. Basi lilikuwa linanisubiri mimi tu. Nilipanda ndani ya basi na abiria wengine walinipa pole. Tuliondoka Korogwe, lakini haikuchukuwa muda kabla basi letu halijapata tatizo la pancha ya gurudumu moja la mbele. Ilibidi tuegeshe pembeni ili litengenezwe. Baada ya matengenezo, tuliondoka kuendelea na safari yetu.

Karibu na mji wa Same kwenye saa saba usiku, basi letu lilisimama ghafla. Abiria walisimama ndani ya basi na kulizuka aina ya kusukumana. Huko nje kulikuwa na ajali. Abiria tulishuka haraka na wengine huko chini walishaanza kupiga mayowe, hasa wanawake. Niliposhuka niliona gari ndogo nyeusi ikiwa imebondeka sana na hapo kando kulikuwa na maiti wawili. Nilijua ni maiti kwa sababu, walikuwa wamefunikwa gubigubi. Halafu kulikuwa na katoto kalikokuwa kanalia sana, kakiwa kamefugwa kanga kichwani. “Tumwahishe huyu mtoto hapo Same hospitalini, ameumia, ingawa siyo sana”. Nilikatazama kale katoto ka kiume kenye umri wa miaka kama mitatu. Kalikuwa kameumia kwenye paji la uso, lakini kalikuwa hai. Bila shaka, wale walikuwa ni wazazi wake, kalikuwa yatima tayari. Machozi yalinitoka.

Baada ya kutoa msaada na askari wa usalama barabarani kuchukua maiti wale, tulipanda basini kuanza safari yetu. Kale katoto kalichukuliwa na jamaa fulani waliokuwa na Landrover ya serikali kukimbizwa hospitalini. Ndani ya basi mazungumzo yalikuwa ni kuhusu ajali ile tu, hadi tunafika Arusha. Tulichelewa sana kufika Arusha kwani tulifika kwenye saa tano asubuhi, badala ya saa mbili.

Nililala kwenye hoteli rahisi na kufanya usaili kesho yake. Ni hiyo kesho, baada ya usaili, niliponunua gazeti ndipo nilipata mshtuko mkubwa ajabu. Kumbe wale watu wawili waliokufa kwenye ajali ile ya Same walikuwa ni Yule bwana aliyenisaidia hela na mkewe. Yule mtoto wao ndiye aliyeokoka. Niligundua hilo baada ya kusoma jina lake na jina la Kampuni aliponiambia nimpelekee fedha zake nikirudi Dar, pamoja na picha yake, mke na mtoto. Nililia sana kama mtoto.

Nilishindwa kujua ni kwa nini ilikuwa afe. Nilijiuliza ni nani sasa ambaye angemlea mtoto yule? Yalikuwa ni maswali yasiyo na majibu nap engine ya kijinga pia. Nilijua kwamba, nilikuwa na deni, deni la shilingi tisini zilikuwa ni sawa na shilingi laki moja za sasa. Kwa mara ya kwanza sasa nilijiuliza ni kwa nini marehemu Yule aliniamini na kuamua kunipa fedha zile. Sikupata jibu. Nilikata kipande kile cha gazeti la kiingereza kilichokuwa na habari ile. Nilichukua kipande hicho na kukiweka kwenye diary yangu. Deni, ningelipa vipi deni la watu? Nilijikuta nkipiga magoti na kuomba. Niliomba Mungu anipe uwezo wa kuja kulilipa deni la mtu yule mwema. “Kwa njia yoyote Mungu naomba uje uniwezeshe kulilipa kwa sura na namna ujuavyo wewe. Nataka kulilipa ili nami niwe nimemfanyia jambo marehemu.” Niliomba. Nilirejea Dar es salaam siku hiyohiyo.

Kwa sababu ya mambo mengi na hasa baada ya matokeo ya usaili ule kuwa mabaya kwangu, nilijikuta nimekuwa na mambo mengi na kusahau haraka sana kuhusu mtu yule aliyenisaidia. Nilifanikiwa hata hivyo kupata nafasi ya kwenda kusoma Chuo cha Saruji na baadaye chuo cha Ufundi na hatimaye nilibahatika kwenda Uingereza. Mwaka 1991, nilianza shughuli zangu.

Ilikuwa ni mwaka 1995, nikiwa ofisini kwangu pale jengo la Nasaco, ambalo liliungua mwaka 1996. Nikiwa nafanya kazi zangu niliambiwa na seketari wangu kwamba kulikuwa na kijana aliyekuwa anatalkka kuniona. Nilimuuliza ni kijana gani, akasema hamjui. Nilimwambia amruhusu aingie. Kijana huyo aliingia ofisini. Alikuwa kijana mdogo wa miaka 17 au 18 hivi, mweupe mrefu kidogo. Alikuwa amevaa bora liende, yaani hovyohovyo huku afya yake ikiwa hairidhishi sana.
Nilimkaribisha ili mradi basi tu, kwani niliona atanipotezea bure muda wangu. Ni lazima niwe mkweli kwamba, sikuwa mtu mwenye huruma sana na nilikuwa naamini sana katika watu wenye pesa au majina. Nilimuuliza, “nikusaidie nini kijana na ukifanya haraka nitashukuru maana nina kikao baada ya muda mfupi.” Nilisema na sikuwa na kikao chochote, lakini nilitaka tu aondoke haraka.

“Samahani mzee, nilikuwa na shida. Nina..nimefukuzwa shule na sina tena mtu wa kunisaidia kwa sababu…Nime…nko kidato cha pili na hivyo natafuta tu kama atatokea mtu…” Nilimkatisha, “sikiliza kijana. Kama huna jambo lingine la kusema, ni bora ukaniacha nifanye kazi. Hivi unafikiri kama nikiamua kumsaidia kila mtu aliyefukuzwa shule, si nitarudi kwetu kwa mguu! Nenda Wizara ya Elimu waambie…Kwanza wazazi wako wanafanya kitu gani, kwa nini washindwe…Kwa nini walikupeleka shule ya kulipia kama hawana uwezio, wanataka sifa?”
“Hapana wazazi wangu walikufa na ninasoma shule ya serikali. Nimekosa mahitaji ya msingi na nauli ya kwendea shuleni. Nasoma shule ya Kwiro, Morogoro. Shangazi ndiye anayenisomesha, naye ana kansa hivi sasa hata kazi hafanyi…” Alianza kulia.

Huruma fulani ilinijia na nilijiambia, kama ni nauli tu na matumizi ni kwa nini nisiwe mwema, angalau kwa mara moja tu. “Baba na mama wamekufa lini?” Niliuliza nikijua kwamba watakuwa wamekufa kwa ukimwi, maana kipindi kile ndipo fasheni ya ukimwi ilipoanza, ambapo kila anayekufa alihesabiwa kwamba kafa kwa ukimwi. “Walikufa kwa ajali nilipokuwa mdogo sana, nilipokuwa na miaka mitatu. Ndiyo shangazi yangu alinichukua na kunilea hadi sasa anakufa kwa kansa.” Yule kijana alilia zaidi. Naomba niwaambie wasomaji kwamba, kuna nguvu fulani na sasa naamini kwamba, ziko nguvu nyingi ambazo huwa zinaongoza maisha yetu bila sisi kujua.

Kitu Fulani kilinipiga akilini paa! Nilijikuta namuuliza yule kijana. “Kwa nini umeamua kuja kwangu, ni nani alikuelekeza hapa na wazazi wako walikufa mwaka gani na wapi?” Yule kijana alisema “nimeona nijaribu tu kwa mtu yeyote ambaye anaweza kunisaidia, ndiyo nimejikuta nikiingia hapa, sijui…sikutumwa na mtu. Wazazi wangu walikufa mwaka 1979 huko Same na mimi wanasema nilikuwa kwenye ajali, nikaokoka. Niliumia tu hapa,” alishika kwenye kovu juu ya paji lake la uso.
Nilihisi kitu fulani kikipanda tumboni na kuja kifuani, halafu niliona kama vile nimebanwa na kushindwa kupumua. “Baba yako alikuwa anaitwa nani?” “Alikuwa anaitwa Siame…Cosmas Siame…” Niliinuka ghafla hadi yule kijana alishtuka. Nilikwenda kwenye kabati langu mle ofisini na kuchakura kwenye droo moja na kutoka na diary. Mikono ikitetemeka, nilitoa kipande cha gazeti kutoka ndani ya diary hiyo, nilichokuwa nimekihifadhi.

“Ndiyo, alikuwa anaitwa Cosmas Siame. Huyu ni mtoto wake, ni yule mtoto aliyenusurika.” Nilinong’ona. Nilijikuta nikipiga magoti na kusali. “Mungu wewe ni mweza na hakuna kinachokushinda. Nimeamini baba kwamba, kila jema tunalofanya ni akiba yetu ya kesho na kesho hiyo huanzia hapa duniani.” Halafu nilinyamaza na kulia sana. Nililia kwa furaha na ugunduzi wa nguvu zinazomgusa binadamu kwa analofanya.
Nilisimama nikiwa nimesawajika kabisa. Nilijihisi kuwa mtu mwingne kabisa. Nilimfuata yule kijana na kumkumbatia huku bado nikiwa ninalia. “Mimi ni baba yako mdogo, ndiye nitakayekulea sasa. Ni zamu yangu sasa kukulea hadi mwisho.” Naye alilia bila kujua sababu na alikuwa amechanganyikiwa kabisa. Nilirudi kwenye kiti na kumsimulia kilichotokea miaka 17 iliyopita.

Tuliondoka hapo na kwenda kumwona shangazi yake Ubungo, eneo la Maziwa ambako alikuwa amepanga chumba. Kutokana na hali yake nilimhamishia kwangu, baada ya kumsimulia kilichotokea. Huyu dada yake Cosmas alifurahi hadi akashindwa kuzungumza kwa saa nzima. Hata hivyo alifariki mwaka mmoja baadaye, lakini akiwa ameridhika sana.

Kijana Siame alisoma na kumaliza Chuo Kikuu na kwenda Australia kufanya kazi. Ukweli ni kwamba, ni mwanangu kabisa sasa. Naamini huko waliko Mbinguni wazazi wake wanafurahia kile walichokipanda miaka mingi sana nyuma. Lakini nami najiuliza bado, ilikuwaje Cosmas akanipa msaada ule? Halafu najiuliza, ni kitu gani kilimvuta mwanaye Siame hadi ofisini kwangu akizipita ofisi nyingine zote? Nataka nikuambie, usiwe mbishi sana bila sababu, kuna nguvu za ziada zinazoongoza matokeo maishani mwetu.

***************************