Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

UKOMBOZI KATIKA UTATU

 UTATU ULIVYOSHIRIKIANA KURAHISISHA UKOMBOZI WETU:
  1. Mungu alifikia uamuzi wa kumuumba mwanadamu kwa kuwa kuna jambo kubwa alikusudia kulifanya kupitia huyo kiumbe kuliko alilowahi kufanya kwa kiumbe mwingine yeyote. Licha ya kuwa ni kiumbe duni na mdogo akilinganishwa na malaika (Waebrania 2:7) alimkusudia baada ya kupitia vipimo mbalimbali amtawaze na kumfanya mrithi wa ufalme wake. Mtunga Zaburi anaandika, "Nikiziangalia mbingu zako, kazi ya vidole vyako, Mwezi na nyota ulizoziratibisha; Mtu ni kitu gani hata umkumbuke, Na binadamu hata umwangalie?Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu; Umemvika taji ya utukufu na heshima; Umemtawaza juu ya kazi za mikono yako; Umevitia vitu vyote chini ya miguu yake." (Zaburi 8:3-6). Kimsingi Mtunga Zaburi anatudokeza kuwa mwanadamu aliumbwa akizidiwa tu na Mungu kwa hadhi!
  2. Mwanadamu aliumbwa akiwa na hadhi ya chini kuliko hadhi ya Mungu na kuliko hadhi ya malaika lakini bado kuna kitu cha thamani ambacho Mungu aliwekeza kwa kiumbe huyo. Hakuumbwa kama walivyoumbwa viumbe wengine. “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.” (Mwanzo 1:26). Kuna mfano na sura ya Mungu ndani yetu ambavyo havipo kwa viumbe wengine. Tunayo asili ya utawala ndani yetu. Asili hiyo ilikuwa ikomazwe kwa kushinda mtihani wa kujitawala waliopewa wazazi wetu pale Edeni. Walishindwa kujitawala. Mungu akaweka mpango utakaohakikisha kuwa lengo lake la awali la kuweka kila kitu chini ya nyayo zetu linatimia. Mpango huo ukamuhusisha Baba, ukamuhusisha Yesu, na ukamuhusisha Roho Mtakatifu. Kila nafsi ikishiriki kwa kina zaidi katika eneo moja kati ya yale maeneo matatu muhimu ya wokovu.
  3. Wokovu wetu ulilenga kurejesha maeneo matatu muhimu tuliyoyapoteza kupitia anguko la dhambi. Kupitia anguko la dhambi tulipoteza uzima au uwezo wa kuishi milele (Warumi 6:23). Tulipoteza uwezo wa kutenda mema yaani utakatifu (Yeremia 13:23). Na tulipoteza ufalme wenye utukufu na utajiri usiomithilika (Luka 4:6). Paulo anaielezea hali hiyo ya kurejesha mambo hayo matatu tuliyoyapoteza kupitia anguko la dhambi kama wokovu ulio katika wakati uliopita, uliopo na ujao. "Aliyetuokoa sisi katika mauti kuu namna ile; tena atatuokoa; ambaye tumemtumaini kwamba atazidi kutuokoa." (2Wakorintho 1:10).
  4. Katika kufanikisha mpango wa kurejesha yote hayo kuliundwa mpango wa wokovu ambapo Yesu (wakati huo akiitwa Neno) alisimamia jukumu la kulipa adhabu ya dhambi kwa kubeba dhambi zetu wakati akiwa hana hatia yoyote jambo jambo lililomlazimu kubeba adhabu ya kifo iliyokuwa inatustahili. Yeye aliye mkamilifu akafanyika laana kwa kubeba dhambi zetu. "Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti." (Wagalatia 3:13). Na kama matokeo ya dhambi hizo alitengwa na uso wa Mungu kupitia mauti kuu ile ya msalabani (2 Wathesalonike 1:9; Mathayo 27:46). Yesu alichukua nafasi ya mwanadamu ili kuonyesha inavyowezekana mwanadamu kuishi Maisha yasiyo ya dhambi na kufanya yale mwanadamu yaliyompasa kufanya ili ae mwenye haki. Mpango huu uliundwa mapema kabla dhambi haijatokea na katika hatua za awali za kuweka mpango wa uumbaji. Yesu alitambua kuwa siku moja angekufa kwa ajili ya kumuokoa mwanadamu tangu mwanzo kabisa wa kuwekwa misingi ya dunia. Mpango huu wa wokovu uliwekwa mapema kabla ulimwengu haujaumbwa. “Naye amejulikana kweli tangu zamani, kabla haijawekwa misingi ya dunia; lakini alifunuliwa mwisho wa zamani kwa ajili yenu." (1 Petro 1:20).
  5. Roho Mtakatifu alikuwa aje baada ya Yesu kukamilisha kazi ya kuwanunulia wanadamu wokovu. Yeye huanza kazi yake kwa kushawishi wanadamu wamuamini Yesu ili waokolewe na wakisha kumuamini anawawezesha kujenga tabia njema iliyoharibiwa na dhambi ili kuwawezesha kuishi maisha ya ushuhuda hapa duniani kujizoeza tabia za mbinguni. "Basi nasema, Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka." (Wagalatia 5:16-17).
  6. Roho Mtakatifu ndiye anayeidhinisha ikiwa mtu amehitimu katika viwango vya tabia inayostahili mbinguni. Nafsi ya Baba na ya Mwana zina majukumu mengine katika kukamilisha wokovu wetu. Kwa sababu hii Yesu alitoa heshima kubwa kwa Roho Mtakatifu na kuwatahadharisha wanadamu wasimkufuru. "Naye mtu ye yote atakayenena neno juu ya Mwana wa Adamu atasamehewa, bali yeye atakayenena neno juu ya Roho Mtakatifu hatasamehewa katika ulimwengu wa sasa, wala katika ule ujao." (Mathayo 12:32).
  7. Kazi ya kubadili tabia ya asili ya mwanadamu itafanikiwa na kukamilika kwa kadri mtu anavyomruhusu Roho kuleta badiliko hilo. “Nami najitaabisha kwa neno lilo hilo, nikijitahidi kwa kadiri ya kutenda kazi kwake atendaye kazi ndani yangu kwa nguvu." (Wakolosai 1:29) Yeye atendaye kazi yake ndani yetu kwa nguvu ni Roho Mtakatifu. Kazi aifanyayo Roho ndani yetu ni ile ya kubadilisha nia yetu ili kuwezesha matendo mema kutokea. "Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu." (Wafilipi 1:6). Kazi hiyo ya kuleta mabadiliko chanya yanayoanzia kwenye ni ya mwanadamu isipoingiliwa kati na tamaa ya mwanadamu kutaka kuifanya mwenyewe kazi hiyo hatimaye itakamilika kwa ushindi mkuu.
  8. Baba katika kukamilisha mpango wa wokovu wa wanadamu alipewa mamlaka ya kutoa kibali na maagizo kwa nafsi ya Baba na Mwana pamoja na kutunuku urithi wa ufalme uliojaa utukufu na utajiri mwingi kwa washindi wa dhambi walioidhinishwa na Roho Mtakatifu. Wakati Yesu anakuja kuukomboa ulimwengu ni Baba aliyetoa kibali. “Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye?" (Warumi 8:32). Baba ndiye aliyetoa agizo wanadamu wamsikilize Yesu. "Naye Yesu alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake; na tazama, sauti kutoka mbinguni ikisema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye." (Mathayo 3:16-17)
  9. Baba pia ndiye aliyemtuma Roho Mtakatifu aje achukue nafasi ya Yesu alipokamilisha kazi ya kuwanunulia wokovu wanadamu. “Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia." (Yohana 14:26). Baba ndiye hufanya kazi za kutuma. Ikumbukwe Yesu alipokuja duniani akichukua asili ya mwanadamu kwa kusudi la kufanikisha ukombozi ni Baba ndiye alimtuma. "Alipokuwa katika kusema, tazama, wingu jeupe likawatia uvuli; na tazama, sauti ikatoka katika lile wingu, ikasema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye." (Mathayo 17:5).
  10. Yesu hakuja duniani kutukomboa mpaka idhini ilipotoka kwa Baba. Na hali kadhalika Roho Mtakatifu hakutoka mbinguni mpaka idhini ilipotoka kwa Baba. Hiyo haimaanishi kuwa Baba alijipa mamlaka hayo yeye mwenyewe ila walikubaliana kuwa lazima awepo kiongozi. Ile dhana ya kuwa yule anayetumika sana ndiye mdogo sana huenda ikatukosesha kuujua uhalisia wa ukuu wa mbinguni. “Basi, ye yote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni.” (Mathayo 18:4)
  11. Baba kama alivyo baba wa kibinadamu ndiye mwenye mamlaka ya kutoa urithi. Nafsi ya Baba inahusika kutoa urithi kwetu sisi tuliofanyika wazaliwa wa kwanza kwa kafara ya Yesu. "Msiogope, enyi kundi dogo; kwa kuwa Baba yenu ameona vema kuwapa ule ufalme." (Luka 12:32). Baba anaonekana akitoa ujira kwa washindi wa dhambi walioshinda kutokana na kazi iliyofanywa na Kristo pamoja na Roho Mtakatifu.  "Kisha Mfalme atawaambia wale walioko mkono wake wa kuume, Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu." (Mathayo 25:34). Hii ndiyo sababu kwenye sala ya Bwana Yesu anatukumbusha tumhimize Baba atupe ufalme. "Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje." (Mathayo 6:9). Nafsi ya Baba ndiyo inayoelekezewa maombi yote kwa kuwa kila tukiombacho kinatoka katika ule urithi tuliotunziwa mbinguni ambao Baba atatupa tutakaposhinda dhambi. (1 Petro 1:4). Urithi uliotunzwa mbinguni kwa ajili yetu siyo utajiri peke yake ni pamoja na utukufu mwingi na fahari. Sisi tutakaa mbinguni kwa miaka alfu moja tukiwahukumu waovu na kupewa elimu juu ya utawala wa Mungu. Huo ni wakati ambao wazaliwa wa kwanza wataketi kule mbinguni kama mkutano mkuu wakila na kunywa lishe ya kuwawezesha kukua na kufikia viwango vya ukuu wa mbinguni. (Waebrania 12:22-23).
  12. Baada ya miaka alfu moja ya kushiriki kupitisha hukumu za waovu na kurejeshewa afya kamili ya kimwili tuliyoipoteza tutarejea duniani ambako yatakuwa maskani ya kudumu ya Mungu na wanadamu.Nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao." (Ufunuo21:3)
  13. Tutakuwa tunaishi nyumbani mwake Mungu yaani ikulu. Nasi tutaketi kwenye kiti cha enzi kama watawala wenza wa Mungu kama Yesu alivyotuahidi. "Basi tangu sasa ninyi si wageni wala wapitaji, bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu." (Efeso2:19). Wanadamu waliokombolewa watapewa hadhi ya kifalme wakitawala na Mungu.Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi." (Ufunuo 3:21)
  14. Ufalme wetu utakuwa wa kutawala sayari za viumbe wa Mungu ambao hawajawahi anguka dhambini. "Na ufalme, na mamlaka, na ukuu wa ufalme, chini ya mbingu zote, watapewa watu wa watakatifu wake Aliye juu; ufalme wake ni ufalme wa milele, na wote wenye mamlaka watamtumikia na kumtii." USIKOSE FURSA HIYO ADIMU. (Danieli 7:27)