Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

FARESI MUGANDA

Muganda , Fares Masokomya (1920–1974)

Fares Masokomya Muganda alikuwa mchungaji, mwinjilisti, na msimamizi wa kanisa kutoka Tanzania.

Maisha ya Awali

Tangu 1903 kazi ya Waadventista ilipoanza nchini Tanzania, kumekuwa na waanzilishi mashuhuri waliotoa mchango mkubwa katika kupanua kazi ya Mungu katika nchi hii na kwingineko. Mmoja wa hao alikuwa Mchungaji Fares Masokomya Muganda, ambaye alikuwa mhubiri mahiri na mchungaji na kiongozi wa Waadventista katika Tanganyika na Tanzania baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliotokea mwaka 1964. Alikua mchungaji mwaka 1951, akihudumu katika mitaa kama vile Ukerewe, Mibungo na Busegwe. Alikuwa mwenyekiti katika fildi ya Bwasi (1963-1964) na mkurugenzi wa idara katika fildi ya Misheni ya Tanganyika na Union Misheni nchini Tanzania (1969-1974).

Elimu na Familia

Fares Muganda alichukua kozi ya teolojia kati ya 1950-1951 katika Chuo cha Bugema, na alisoma shahada ya kwanza ya theolojia katika Chuo cha Solusi nchini Zimbabwe kuanzia 1965-1969. Alikuwa miongoni mwa watu na wachungaji wachache walioweza kuongea Kiingereza kizuri enzi hizo za Tanganyika.

Alikuwa na mke, Lois (aliyezaliwa Januari 10, 1925, huko Musoma), na watoto watano. Miongoni mwa watoto hao ni Baraka Muganda ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Vijana wa Konferensi Kuu kwa miaka 15. Lois alifariki mwaka 2017 na watoto waliobaki ni Baraka, Ruth, na John.

Fares aliteuliwa kuwa mkurugenzi wa uchapishaji wa kwanza Mtanzania katika fildi ya Misheni ya Tanganyika mwaka 1952 na jukumu lake lilikuwa kuandaa idara, ingawa Stefan Hoeschele katika kitabu chake anamtambulisha Paulo Kilonzo kama mkurugenzi wa kwanza. Wainjilisti wa vitabu kote kwenye fildi walikuwa na lengo la kueneza ujumbe wa habari njema kupitia vitabu kwa wale walioweza kusoma. Lengo lilikuwa ni kumshuhudia Yesu na kueleza yale yaliyokuwa katika vitabu hivyo, na hivyo kuandaa roho kwa ajili ya kampeni ya uinjilisti. Alipanga timu za kuwafikia watu mijini na sehemu za mbali katika milima na tambarare za Tanganyika. Wakati huo Watanganyika walikuwa takriban milioni tisa na jumla ya wainjilisti wa vitabu walikuwa 22. Kutokana na kazi hii, makanisa yalifunguliwa katika miji kama Dar es Salaam, Morogoro, Singida, na Mtwara.

Mwinjilisti wa Misheni ya Union ya Tanzania Mijini

Mchungaji Fares Muganda, baada ya kumaliza shahada yake ya teolojia katika Solusi, alirejea Tanzania. Huko alipewa kazi ya kuwa mwinjilisti wa Union na kufanya kazi hasa mijini. Mapema mwaka wa 1970 Kamati ya Union iliwapa A. Kiboko, S. Boi, na Baraka Muganda, chini ya uongozi wa Fares Muganda, kuhubiri katika miji ya Mbeya, Iringa, Tanga, Mwanza, Moshi, Arusha, na Bukoba.

Matokeo ya kampeni hizi za uinjilisti yalikuwa makubwa. Katika jiji la Mbeya watu 75 walibatizwa na Tanga walikuwa 50. Dk. Godwin Lekundayo, aliyekuwa mwenyekiti wa Union Konferensi ya Kaskazini mwa Tanzania, ni zao la mikutano ya injili ya Mchungaji Muganda katika miaka ya 1970. Mchungaji Muganda alikuwa miongoni mwa “kizazi cha kwanza cha uongozi wa Kiafrika zaidi ya ngazi ya mtaa na kwa hiyo aliwakilisha maendeleo ya Uadventista wa Tanzania baada ya uhuru kama kitambulisho cha kitaifa cha kanisa.”

Sababu za Kampeni za Uinjilisti Mijini

Kuanzishwa na kubadili mwelekeo wa mikakati ya uinjilisti kulichochewa na kupandishwa hadhi kutoka Fildi ya Misheni ya Tanganyika hadi kuwa Union Misheni ya Tanganyika katika miaka ya 1960 ambapo viongozi wa wakati huo walisisitiza kuhubiri injili mijini na kwenye majiji. Kwa kuwa kazi hiyo ilianzishwa Tanganyika, ilikuwa ni desturi kuanzisha makanisa nje ya miji na majiji. Labda walifuata tu sehemu ya kwanza ya mwongozo wa Ellen G. White kwamba “Ni mpango wa Mungu kwamba watu wetu wanapaswa kuwa nje ya miji, na kutoka kwenye vituo hivi vya nje waonye majiji, na kuinua ndani yake ukumbusho kwa ajili ya Mungu.” Inaonekana kwamba watangulizi wetu kimsingi waliishi katika maeneo ya mashambani na kusahau kurudi mijini.

Kuundwa kwa timu ya Muganda kuinjilisha miji kulifaa. Utume kwa miji ulichochewa pia na kampeni ya uinjilisti iliyofanyika jijini Dar es Salaam mwaka 1963 iliyojumuisha warsha ya wainjilisti na wachungaji iliyofanywa na mwezeshaji kutoka Konferensi Kuu, Mchungaji E. Cleveland. Wachungaji na wainjilisti kutoka Afrika Mashariki na Kati walikuwa wajumbe. Katika kampeni hiyo ya uinjilisti watu 300 walimpokea Yesu na kubatizwa.

Zana zilizotumika kwa huduma ya uinjilisti zilijumuisha filamu, vijizuu vya Sauti ya Unabii, na vijitabu maalum. Pia walitumia safu za picha ili kuvutia wasikilizaji wao watarajiwa walipokusanyika katika maeneo ya wazi ya umma. Mikutano ilifanywa katika mahema na kumbi katika majiji na miji. Mabasi na treni zilitumika kuhama kutoka eneo moja hadi jingine. Mikutano ilichukua wiki tatu hadi sita, ingawa baadhi iliendelea kwa miezi mitatu, kama vile ule wa Cleveland jijini Dar es Salaam.

Utawala na Muundo wa Kanisa wakati wa Muganda

Katika Fildi ya Misheni ya Tanganyika na baadaye kwenye Union Misheni ya Tanganyika wakati wa Fares Muganda, kazi hiyo iliongozwa na watu kutoka nje ya nchi katika ngazi ya Union. Kwa mfano, katika fildi ya Misheni ya Tanganyika kuanzia 1951 hadi 1955 mwenyekiti alikuwa FG Reid, na katibu/mweka hazina alikuwa H. Robson. Kuanzia 1956 hadi 1958, JD Harcombe alikuwa mwenyekiti na MW Curthbert alikuwa katibu/mweka hazina. Wakati wa kampeni za uinjilisti za majiji za Fares Muganda, uongozi wa union ulishikwa na Leonard Robinson kama mwenyekiti na H. Salzmann kama katibu/mweka hazina (1969-1975). Wafanyakazi wa kitaifa walikuwa na majukumu ya idara katika kipindi hiki kama Hoeschele anavyoshuhudia, "katika miaka ya 1970 idara nyingi za Union zilishikiliwa na raia."

Katika siku hizo Kanisa la Waadventista wa Sabato ndilo lilikuwa dhehebu pekee la Kikristo lililoshiriki kikamilifu katika uinjilisti wa hadhara katika miji. Makanisa kama vile Kanisa Katoliki la Roma na makanisa ya Kilutheri yalipata waumini kwa kutoa huduma za kijamii kama vile shule na hospitali na kwa kutoa mahitaji mengine muhimu katika jamii.

Fares Muganda alipata fursa ya kuwa mhubiri wa kimataifa kutoka Tanzania alipoenda kuhubiri katika mji mkuu wa Misri, Cairo, kati ya 1971 na 1972. Mwanawe John anashuhudia kwamba katika kampeni hiyo ya uinjilisti huko Cairo Waarabu watu wazima wapatao 22 walimkubali Yesu kuwa Mwokozi wao nao wakabatizwa.

Mchango

Fares Muganda atakumbukwa kwa mchango wake katika upanuzi wa makanisa nchini Tanzania hasa mijini. Alikuwa mwinjilisti na mchungaji ambaye alitumia vipawa vyake vya kiroho na utu wake kuvutia wengi kumpenda Kristo na kujiunga na kanisa lake. Kukua kwa makanisa katika miji kama Mwanza, Dar es Salaam, Tanga, Bukoba, Iringa, Mbeya, Arusha na Moshi ni ushahidi wa kazi kubwa ya Mchungaji Fares Muganda na matokeo yake katika ukuaji wa Kanisa la Waadventista wa Sabato Tanzania. Alikuwa mmoja wa waanzilishi katika historia ya kanisa letu la Tanzania. Mfano wake unatufundisha jinsi tunavyopaswa kuthubutu kuchukua hatua na kuwa wabunifu kwa ajili ya kazi ya Mungu na injili. Ellen G. White anapendekeza “Wacha watu wafaao, ambao hawajawahi kufunua roho yenye ubinafsi, na yenye kung’ang’ania izuiayo njia zinazopaswa kutumika katika miji mikubwa, wachaguliwe kuendeleza kazi hiyo, kwa sababu Mungu anawakubali kuwa wateule wake. . . . . Katika miji hii ukweli ni kama taa iwakayo . ”