Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

WAAMUZI

MASWALI YA KUJADLI: WAAMUZI 4:1-24

 1. Unadhani Baraka alikuwa na sababu nzuri ya kusita kwenda kulikabili jeshi kubwa lenye zana nyingi na bora za kivita la Sisera hata kama ni Mungu amemwagiza kufanya hivyo? Kwa nini kuwepo kwa Debora mwamuzi na nabii mke kulileta faraja kwa Baraka vitani? Upo wakati mwanamke anayetambulika kuwa mnyonge au dhaifu katika jamii nyingi anaweza kuwa msaada kwa wanaume kutimiza majukumu yao waliyopewa na Mungu?
  2. Kwa nini katika kisa hiki Mungu alileta ushindi kwa msaada wa wanawake zaidi kuliko wanaume? Jambo hili lilitokea kwa bahati mbaya au kuna jambo Mungu anataka kutufundisha? Kwa nini Sisera pamoja na kuwa na jeshi kubwa na zana bora za kivita alishindwa vitani? Hii inatufundisha nini juu ya umuhimu wa kumtegemea Mungu?

 
MASWALI YA KUJADILI: WAAMUZI 5:1-31

 1. Kuimba nyimbo ni njia mojawapo ya kutambua na kushukuru jinsi Mungu alivyokutendea makuu siku zilizopita ulipokuwa ukikabiliwa na changamoto. Je unakuwa na mazoea ya kuimba nyimbo za sifa kwa furaha? Debora na Baraka wanakiri kuwa ushindi wao umechangiwa kujitoa mhanga kwa hiari kwa viongozi wao?
 2. Je unatambua mchango wa viongozi wako katika kufikia mafanikio yako binafsi na mafanikio ya kundi lako la kiroho? Je kungekuwa na mabadiliko gani kama tungedumisha kawaida ya kutambua mchango wa wale waliochangia mafanikio yetu? Kutia hamasa watu unaowaongoza katika kipindi cha kukata tamaa na woga kunasaidiaje kuamsha tumaini la ushindi?
 3. Kama kiongozi anaonesha woga kuna hatari gani kwa anaowaongoza? Je wanawake wana mchango wowote katika vita ya kiroho na kiuchumi? Je wanafaa kuwa viongozi na kuleta mabadiliko yoyote ya maana?

 
MASWALI YA KUJADILI: WAAMUZI 6:1-40

 1. Je mkakati wa kuidhoofisha Israeli kwa njaa ulifanikiwa? Kwa nini Israeli hawakujitetea wakati uvamizi huo ulipokuwa ukifanyika? Kwa nini Mungu hakuingilia kati kuwatetea Israeli wakati uonevu huu ulipokuwa unaendelea? Je Mungu anahitaji ushirika wa wanadamu ili kuleta ukombozi wa kifikra na kiroho?
 2. Kwa nini Gideon pekee ndiye aliyechukua muda kutafakari uonevu wanaotendewa? Je wengine walikuwa wameridhika? Kuna haja ya kujitoa mhanga kutetea jambo linalowahusu wengi wakati wahusika wenyewe hawaoneshi kukuunga mkono? Ilikuwa ni muhimu kwa Gidioni kutaka ishara kutoka kwa Mungu?
 3. Je kuharibu miungu ya kipagani kulikofanywa na Gidioni kulikuwa kwa halali na kwa muhimu? Je ilikuwa halali kwa watu kumtetea Baali aliyeshindwa kujitetea mwenyewe asibomolewe? Je panahitajika watu majasiri kama Gidioni leo hii?


MASWALI YA KUJADILI: WAAMUZI 7:1-25

 1. Kumwacha Mungu kunakaribisha matatizo mengi maishani kama ilivyotokea kwa Israeli. Unadhani matatizo unayoyapitia yametokana na kumwacha Mungu. Ufumbuzi wa matatizo huja pale mtu anapotathmini maendeleo yake na kubaini mapungufu. Je unaridhika na maendeleo yako?
 2. Unadhani kuna ahadi unazoweza kuzidai kwa Mungu ili kuondokana na mkwamo huo? Sifa za mtu afaaye kutumika na Mungu kuongoza mapambano ya kujikomboa kwenye utumwa wa dhambi na utumwa mwingine wowote ni kujiona kutotosha kama Gideoni. Je, unadhani sifa hiyo bado inahitajika leo?
 3. Faida ya kuwa na sifa hiyo ni nini? Uhakika wa ushindi katika vita ya kiroho hautokani na uwingi wa wapiganaji au uwingi wa silaha na ubora wake. Ni nini kilichosababisha ushindi wa jeshi la Gideoni? Kwa nini Mungu anakubali kuwapigania watu waliokuwa wamechagua kumuasi?
 4. Mungu anapata faida gani kwa kufanya hivyo? Unadhani vijana wana nafasi ye yote katika kuleta mabadiliko chanya kwenye jumuia za kidini na kwenye jamii zetu leo hii. Je wanaaminika?

 
MASWALI YA KUJADILI: WAAMUZI 8:1-35   

 1. Je, lawama alizopewa Gideoni na watu wake alipotoka kushinda vita zilikuwa za halali? Wakati mwingine lawama wanazopewa viongozi ni kutokana na kuonewa wivu kwa mafanikio yao? Je, hekima inahitajika katika kuwatuliza watu wenye hasira hata kama madai yao si ya msingi?
 2. Kitendo cha Gideoni kukataa ofa ya kutawala Israeli na vizazi vyake na kutaka Mungu ndiye awe mtawala ni udhihirisho wa ukomavu wake wa kiroho? Nini kingetokea kama watawala wetu wangekuwa na roho ya kutambua kuwa Mungu ndiye mtawala na wao ni wasaidizi tu?


MASWALI YA KUJADILI: WAAMUZI 9:1-57    

 1. Uongozi wa kiroho hupatikana kwa kujifanyia kampeni kwa ndugu wad amu ili wakuchague? Je, mtu anayefanya hivyo anaonesha dalili za kufilisika kiroho? Je, kuna uwezekano wa mtu aliyechaguliwa kwa misingi ya undugu kuwa na upendeleo? Je, kuna wakati Madaraka huwa matamu kiasi cha kutoona umuhimu wa Maisha ya watu wengine?
 2. Mtu mwenye ukabila ana kawaida pia ya kuwa mkatili kwa ndugu zake? Kwa nini Abimeleki aliwaua nduguze sabini? Je, ni hatari kiasi gani kukemea uovu uliotendwa na mtawala? Je, nini kitatokea Ikiwa watu wote watajifanya hawajauona ubaya uliotendwa na mtawala wao na kukemea? Je, ndugu waweza kuuana kwa kugombea uongozi katika familia?
 3. Je, mwanamke anaweza kutegemewa kumshinda adui aliyeshindikana na wanaume? Abimeleki alishindwaje kutambua uwepo wa mwanamke aliyemporomoshea jiwe la kusagia na kumvunja fuvu la kichwa? Je, kwa mujibu wa tukio la kifo cha Abimeleki kila ovu linalotendwa lina malipo yake?


MASWALI YA KUJADILI: WAAMUZI 10:1-18   

 1. Kutambua chanzo cha matatizo yako ni chanzo cha kutambua tiba yake. Je, mwanadamu wa kawaida anaweza kujitambua kuwa ni mwenye dhambi asiposaidiwa na Mungu? (Matendo 5:31; 2 Wakorintho 7:10). Kwa nini Mungu hutaka tutubu kwanza ndipo atuokoe? Masharti ya Mungu ya kutuokoa na adui zetu ni nini?
 2. Je tunapochagua miungu mingine zaidi ya Mungu wa mbinguni huwa tunachagua pia ulinzi wa huyo Mungu mwingine? Je tunapopitia mapigo ya nguvu za giza ni udhihirisho kuwa kwa namna Fulani tumemuacha Mungu? Je, ni halali watu wa Mungu kuwa na mapepo au kuogopa kulogwa?


MASWALI YA KUJADILI: WAAMUZI 11:1-40

 1. Moja ya matatizo yanayotokana na kuwa na ndoa za mitala ni magomvi ya waliozaliwa kwenye familia moja. Unadhani Yeftha alistahili kufukuzwa na ndugu zake na kunyimwa urithi? Tabia mbaya za watoto wanaoitwa mitaani zinatokana na kukataliwa na familia zao au na tabia wanazojifunza mtaani? Nini kifanyike kupunguza wimbi la watoto wa mitaani? Je ni busara kuwatumia au kuwathamini watu waliokataliwa na jamii zao pale vipawa vyao vinapohitajika kuokoa familia, kanisa, au jamii?
 2. Je, inafaa kukubali kuwatumikia watu waliokukataa kwa dharau hapo mwanzo? Utafanyaje mtu akikutaka urudishe mali yake ambayo Mungu alikuagiza uitwae? Utajisikia hatia na kumrudishia? Ni muhimu kwa kiongozi wa kiroho kujua historia ya taasisi anayoiongoza na jinsi Mungu alivyoivusha katika nyakati ngumu huko nyuma. Unadhani Yeftha alipatia wapi uelewa huu? Hiyo inakuambia nini juu ya umuhimu wa viongozi leo kuijua historia ya kanisa na uwezo wa Mungu wanayemtumikia?
 3. Yeftha alitoa ahadi yake kwa kukurupuka lakini akawa mwaminifu kuitimiza. Hii inatufundisha nini kuhusu kutoa ahadi au nadhiri? Binti wa Yeftha alikuwa na tabia njema hata kuliko baba yake wakati alipokuwa mtoto ambaye aliungana na mabaradhuli. Hii inapingana na ukweli kuwa mtoto wa nyoka ni nyoka? Tufanyeje ili watoto wetu wasirithi tabia zetu mbaya? Ni muhimu kwa kiongozi wa kiroho kujua historia ya taasisi anayoiongoza na jinsi Mungu alivyoivusha katika nyakati ngumu huko nyuma. Unadhani Yeftha alipatia wapi uelewa huu?
 4. Hiyo inakuambia nini juu ya umuhimu wa viongozi leo kuijua historia ya kanisa na uwezo wa Mungu wanayemtumikia? Yeftha alitoa ahadi yake kwa kukurupuka lakini akawa mwaminifu kuitimiza. Hii inatufundisha nini kuhusu kutoa ahadi au nadhiri? Binti wa Yeftha alikuwa na tabia njema hata kuliko baba yake wakati alipokuwa mtoto ambaye aliungana na mabaradhuli. Hii inapingana na ukweli kuwa mtoto wa nyoka ni nyoka? Tufanyeje ili watoto wetu wasirithi tabia zetu mbaya?

 
MASWALI YA KUJADILI: WAAMUZI 12:1-15     

 1. Unawachukuliaje watu wanaopendelea kulalamika kutoshirikishwa waonapo mafanikio lakini ambao katika kipindi chote cha mapambano walikaa mbali bila kujihusisha? Je mafanikio yaweza kuongeza idadi ya maadui maishani mwako? Ufanye nini ili hali hiyo isitokee? Magomvi ya wanandugu hutokana na ubinafsi na kutafsiri vibaya mienendo ya wengine huku kukiwa na nia ovu ya kutaka kushika uongozi kinyume cha aliyepo madarakani kwa uhalali?
 2. Unadhani hali hiyo inajidhihirisha kwenye kisa hiki? Je, hali hiyo ipo kwenye familia au kanisani kwako? Yapo mambo yanayowatofautisha hata ndugu wa jamaa moja na hivyo ni jambo lisilowezekana kufikiria kuwafanya watu wote wafanane maana ni Mungu aliyeruhusu tofauti hizo ziwepo kwa nia ya kuimarishana na kutoshelezana. Katika kisa hiki shetani alitumiaje tofauti za ndugu kwa faida yake?
 3. Je tofauti zenu katika familia na katika kanisa zinawafanya mgombane na kuangamizana au zinawaleta pamoja? Unajifunza nini kwa Tanzania yenye makabila mengi yasiyogombana wala kuchukiana ukilinganisha na majirani zetu? Kama hilo limewezekana katika nchi linashindikanaje kwenye familia yenu na kwenye jumuiya yako ya kidini?


MASWALI YA KUJADILI: WAAMUZI 13:1-25

 1. Je, umekata tamaa na taarifa kuwa ugonjwa au hali mbaya uliyo nayo utadumu nayo siku zote? Habari njema ni kuwa Mungu aweza kubadilisha hali yako kama alivyobadilisha utasa wa mke wa Manoa. Je, unaamini hilo? Malezi bora ya mtoto huanzia akiwa tumboni na hutokana pia na vyakula na vinywaji anavyotumia mama na mahusiano ya wazazi.
 2. Unadhani tabia mbaya za watoto tunazozishuhudia leo zinatokana na kukosa mambo hayo wakiwa hawajazaliwa? Kwa nini katika kizazi cha leo inaonekana zuio la kunywa vileo na kula wanyama najisi ni kama halitokani na agizo la Mungu? Au ni kwa sababu ya kuelemewa na ulevi na ulafi kama Luka 21:34 isemavyo? Mungu akitaka kuokoa familia au kikundi cha watu humuandaa mtu atakayewaongoza ambaye humwezesha kwa vipawa kadhaa na kumfanya kuwa tofauti na wengine?
 3. Unadhani umeandaliwa kuwa nani katika siku za usoni? Je unauthamini mpango huo wa Mungu? Ujenzi wa tabia za watoto hukamilika katika miaka minane ya mwanzo na huendelezwa hata atakapokuwa mtu nzima. Kama mzazi au kiongozi wa kiroho unatumia muda gani kumuomba Mungu akuwezeshe kuwalea watoto wako? Je kwenye kanisa lako kuna utaratibu nzuri wa malezi ya watoto?
 4. Unafahamu mwanao atakuwa nani katika siku za usoni? Umefanya sehemu gani kumwezesha kuwa vile anavyotaka au vile Mungu alivyompangia kuwa? Unazungumziaje wazazi wanaolazimisha watoto wao kuwa vile wanavyotaka wao? Manoa na mkewe walikuwa watu wa kiroho kwa kuwa walikuwa wakitimiza taratibu za ibada za wakati huo na Mungu akaruhusu Samsoni - Mwamuzi mashuhuri wa Israeli kuzaliwa kwao. Hali ya ibada nyumbani kwako ikoje?


MASWALI YA KUJADILI: WAAMUZI 14:1-20

 1. Kuchagua mwenzi wa maisha kunahitaji umakini na muda wa kutosha wa kumchunguza. Unadhani uchaguzi wa Samsoni ulizingatia vigezo hivyo? Katika nyakati hizo kulikuwa na faida gani ya kuoa mke kutoka katika jamaa ya karibu? Je sababu hizo zina mashiko kwa leo? Wazazi wana nafasi gani katika kupendekeza mke au mume anayefaa kwa watoto wao katika siku tunazoishi? Ni kweli kuwa jambo hili halihitaji ushauri wa wazazi?
 2. Unadhani Samsoni alipendezwa na nini kwa yule binti wa Wafilisti ambao ni maadui wa taifa lake? Je katika kuoa au kuolewa swala la kupendezwa au kuvutiwa na yule unayetaka kuoana naye ni la muhimu? Je unadhani Samsoni alikuwa amefikia hatua ya kuoa au alikuwa bado ana mambo ya ujana yakimsumbua? Dalili ya kijana aliyefikia umri unaostahili kuoa au kuolewa ni zipi?


MASWALI YA KUJADILI:
WAAMUZI 15:1-20   

 1. Je, ubabe usioandamana na uadilifu unafaa katika kuwakomboa watu na ukandamizaji wa maadui. Vitendo vya Samsoni vinaashiria kuwa ni mtu aliyetumwa na Mungu? Katika kufanya kazi ya kuwatumikia watu kuna uwezekano wa kuingiza ubinafsi? Je shida aliyoipata Samsoni kwa mkwewe ilitokana na kufungiwa nira na wasio na imani?
 2. Uharibifu wa mazao ya Wafilisti uliofanywa na mbweha wa Samsoni ulikuwa wa lazima? Je, ulileta faida ye yote kwa Waisraeli? Jitihada za Samsoni za kuwakomboa Waisraeli ziliwaletea usumbufu mkubwa kutoka kwa maadui zao kiasi cha kutamani Samsoni alegeze misimamo yake. Unadhani katika hatua hii ni nani alikuwa sahihi kati ya Samsoni na watu wake?
 3. Mungu aweza kutumia chochote kilicho mkononi mwako kukuletea ushindi na mafanikio ikiwa utakitoa wakfu kwake. Unadhani iliwezekanaje taya la punda liue watu elfu tatu? Unaridhika na namna Samsoni alivyoanza kuwaokoa Waisraeli?


MASWALI YA KUJADILI: WAAMUZI 16:1-31

 1. Samsoni alikuwa na nguvu za kung'oa malango lakini hakuwa na nguvu za kushinda tamaa. Kipi kilikuwa muhimu kwake ili kufanikiwa kuwaokoa Waisraeli kikamilifu? Je, kuna uwezekano wa kuutosheleza moyo ili usijisikie kutamani tena? Suleimani, Daudi, Samsoni, na hata Ibrahimu pamoja na matendo makuu waliyofanya walitamani. Nini kilimsaidia Yusufu asitamani mke wa Potifa? Unadhani inawezekana kuishinda dhambi hiyo leo?
 2. Wakati Samsoni akitamani wanawake, Delila alitamani fedha alizoahidiwa ili kumsaliti mumewe. Ni nani kati ya hao anafanya dhambi zaidi? Je, ni halali kuwalaumu wanawake zaidi pale tabia za zinaa na uasherati zinaposhamiri? Je, unadhani Samsoni alitambua makosa na udhaifu wake wakati anatoa siri ya nguvu zake? Je aliamini kwamba angeweza kukamatwa?
 3. Kwa nini Wafilisti walimtumia mwanamke kumnasa Samsoni na si mwanaume Mfilisti mwenye nguvu kama Samsoni? Hii inakuambia nini juu ya uwezo wa wanawake kama ukitumiwa vizuri? Kwa nini Wafilisti baada ya kumkamata Samsoni walihimidi miungu yao? Je hii ilikuwa ni vita ya kiroho baina ya Mungu wa mbinguni na Shetani chini ya kivuli cha miungu ya kipagani? Kwa hatua hii ni Mungu yupi alikuwa ameshinda?
 4. Je, kuishiwa nguvu za kiroho ni dalili kuwa Mungu anakuacha au wewe unamwacha Mungu? Je, ukigundua nguvu zako zimepungua unaweza kumuomba Mungu akakurejeshea nguvu zako za awali?


MASWALI YA KUJADILI: WAAMUZI 17:1-13   

 1. Kuna hatari ya kung'ang'ania uelewa binafsi wa mambo ya kiroho na kupuuzia ule uelewa wa pamoja wa kundi la waumini katika siku tunazoishi. Unadhani hii inatokana na kila mmoja kujifanyia aonavyo kuwa ni mema machoni pao? Mtu mwenye misimamo inayopingana na uelewa wa kundi la waumini afanyweje? Apuuzwe, asikilizwe, au aadhibiwe?
 2. Kuna watu ambao hawaoni haja ya kuwa na viongozi wa kiroho waliopo unadhani wanafahamu madhara ya kutokuwa na viongozi? Unadhani lengo la msimamo wao huo ni kutaka wao ndiyo wawe viongozi? Inawezekanaje mtu aliyewahi kumuamini Mungu wa kweli arudi nyuma hadi kuabudu vinyago? Hii inakuambia nini juu ya hatari ya kupoa kiroho? Kama unamnua mtu wa namna hiyo unapangaje kumsaidia?
 3. Kuna watu wenye tamaa ya kutaka kuwamiliki na kuwatumia  viongozi wa kiroho kama mali yao na kuwashinikiza kufanya maamuzi wanayoyapenda kwa sababu ya jeuri ya pesa. Una maoni gani juu ya watu hao?

 
MASWALI YA KUJADILI: WAAMUZI 18:1-31

 1. Unadhani mpango wa kuuteka mji wa Laisha ulio katika nchi ya vilima vilima ya Efraimu ulifanana na utekaji wa mji wa Yeriko? Je unadhani uliratibiwa na Mungu? Kama haikuwa halali kwa kuhani kutumika kwa nyumba ya mtu mmoja ilikuwa halali kutumika kwa kabila moja la Wadani?
 2. Huyu kuhani alikuwa na wito wa kufanya kazi yake alikuwa sawa hawa watumishi walioenea leo wanaopenda kufanyia kazi penye malisho mazuri na kutoa utabiri wa kufurahisha wateja wao? Kwa nini hata leo sanamu za kuchonga zinatumika kwa makusudi ya ibada licha ya Mungu kupiga marufuku kwenye amri ya pili?
 3. Watu wa Laisha hawakuwa na mwokozi huashiria kuwa hawakujishughulisha kutafuta usalama wao kutoka kwa Mungu ili alinde mafanikio yao. Ni nini uhakika wa usalama wa mwanadamu kando ya kumtegemea Mungu? Unachukua hatua gani kutorudia makosa ya watu wa Laisha?
 4. Katika kisa hiki tunashuhudia maisha yaliyojaa ubabe na ukiukwaji wa haki za msingi kwa mujibu wa miongozo ambayo watu wamejiwekea na maagizo ya Neno la Mungu. Je unaishuhudia hali hiyo katika mahali unapoabudu? Unachukua hatua gani? Wapo wanadamu wanaofanana na Wadani ambao hufanikisha mambo kwa utundu wao na kudai yametokana na Mungu ili kuyapa uhalali. Je hali hiyo Mungu anaikubali?


MASWALI YA KUJADILI: WAAMUZI 19:1-30 

 1. Hali ya kukaa bila mfalme ni mfumo wa maisha usiozingatia sheria na maadili. Maelezo yanayopatikana katika sura hii yanafanana na maelezo yanayoripotiwa katika vyombo vya habari siku hizi. Hii inaashiria tumepuuzia sheria na maadili? Kiongozi wa kiroho hakuwa makini katika kuchagua mwenzi wa maisha? Muda wa miezi 4 aliosubiri kabla ya kumfuata mkewe unadhihirisha uzembe au kukerwa na tabia ya ukahaba ya mkewe?
 2. Kwa nini walio kwenye ndoa wamekosa uaminifu katika ndoa zao? Mzazi wa mke wa kuhani alikuwa na lengo gani kuwachelewesha kuondoka wageni wake? Hakutaka waondoke au alitaka kuwafanyia ukarimu? Tabia za watu Gibea zilifanana na watu wa Sodoma maana hawakuwapenda wageni na walikuwa hawana maadili. Unadhani ilikuwa busara kulala katika mji huo? Je chanzo cha tabia hii ni nini na nini kifanyike kuiondoa?
 3. Kwa nini ili kujisalimisha walipendekeza wawatoe wanawake walionao ili wawatendee unyama? Je kama yule mwenyeji na Mlawi wangekuwa na upendo wa kweli wangependekeza nini badala yake? Kitendo Mlawi alichomtendea mkewe kwa kumkatakata kwa mapanga kinadhihirisha alivyokuwa na roho mbaya au anavyochukia tabia ya ukahaba?
 4. Kisa hiki kinatukumbusha jinsi baadhi ya ndoa zinavyopitia changamoto na manyanyaso wayapatayo wanawake? Je unadhani alichofanyiwa mwanamke kahaba alikistahili?


MASWALI YA KUJADILI: WAAMUZI 20:1-48  

 1. Dhambi ya watu wachache isiposhughulikiwa ifaavyo na kwa wakati hugharimu maisha ya wengi au kundi zima. Unadhani kwa nini Benjamini walikataa kuwatoa mabaradhuli waliohusika na uovu uliotendeka? Je hiyo ingeepusha vita iliyotokea? Je muda unaotumika kulumbana na kupigana vita katika familia na jumuia za kidini unapunguza muda wa kujiletea maendeleo na kumkabili adui yetu halisi?
 2. Je kulipiza kisasi kama walikofanya Waisraeli kulikiwa kwa lazima? Iliwezekanaje Waisraeli washindwe vitani hata baada ya kumuomba Mungu? Inawezekana kuna wakati tunamlazimisha Mungu  kufanya tunachotaka? Katika kipindi kinachotajwa makabila yote ya Israeli hayakuwa katika mahusiano mazuri na Mungu. Je unayachukuliaje mazoea ya kumkimbilia Mungu wakati wa shida pekee?
 3. Unadhani mataifa ya kipagani yaliyowazumguka Waisraeli yalitamani kuwaona wakigombana au wakipatana? Unadhani maovu yanakemewa kwa kiwango cha kuridhisha makanisani?


MASWALI YA KUJADILI: WAAMUZI 21:1-25   

 1. Waisraeli walijutia kuangamiza ndugu zao Wabenjamini kwa kuwa lengo lao lilikuwa kukomesha uovu usienee katika taifa zima. Je kuna umuhimu wa kupima adhabu tunazotoa kwa wakosaji ili zisivuke mipaka? Viapo au nadhiri ni jambo linalopaswa kutolewa kwa uangalifu maana Yeftha katika Waamuzi 11:30 alitoa nadhiri iliyomgharimu. Unadhani kiapo walichotoa Waisraeli kutowapatia Benjamini wake wa kuoa kilikuwa cha lazima?
 2. Waisraeli walilia sana walipogundua wamefanya kosa. Je toba ya kweli ni lazima wakati wote iandamane na kulia? Je kuna uwezekano wa mtu anayedai analia kwa sababu ya kujutia dhambi afanye hivyo kwa kuigiza? Kwa nini ilikuwa lazima kabila moja ya Benjamini iliyopungua itafutiwe uwezekano wa kurejeshwa kwa namna ye yote ile? Je njia iliyotumika kuwapatia wake wa kuoa ilikuwa sahihi?