MASWALI YA KUJADILI: RUTHI 1:1-24
- Je lilikuwa wazo jema kwa Elimeleki na Naomi mkewe kwenda nchi ya wapagani ya Moabu kwenda kuhemea chakula? Unadhani wangebaki kwenye nchi yao Mungu asingewaponya kwa njaa? Kulikuwa na jinamizi gani linawaandama hata mume na watoto wawili wakafariki na kubaki wajane 3 wasio na waume?
- Dhana ya Naomi kuwa Mungu alikuwa amemkasirikia kutokana na vifo vilivyotokea (Ruthi 1:13,21) ina ukweli wowote au ni mawazo yatokanayo na uchungu wa kufiwa? Ungekuwa unatakiwa kumfariji Naomi na wakweze ungewapa neno gani la faraja juu ya upendo wa Mungu? Je lilikuwa wazo sahihi kwa Naomi na mumewe kuwaoza watoto wao kwa binti wa kipagani wa Moabu?
- Kwa nini mabinti hawa wa kipagani (na hasa Ruthi) waling'ang'ania kuandamana na Naomi na kuwa sehemu ya jamii ya Israeli? Wajane hawa watatu walifarijiana kulingana na machungu yanayofanana wanayoyapitia. Unadhani ipo haja ya wajane kujiundia umoja wa kufarijiana? Unadhani familia na jumuiya za kidini zinafanya wajibu wao wa kutosha kusaidia wajane?
MASWALI YA KUJADILI: RUTHI 2:1-23
- Ruthu alikuwa binti mwenye upendo wa kweli, mchapakazi, na mwaminifu asiye na majivuno. Mabinti wenye tabia za namna hii ni rahisi kupata ajira na wachumba. Ungekuwa mshauri wa vijana ungewashauri nini wasichana wanaotafuta kazi na wachumba? Umuhimu wa Ruthu kuandamana na mkwewe unaonekana baada ya Ruth kuwa mtafuta riziki ya familia. Nini kinakosekana leo kwa wakwe kushindwa kuishi vizuri na wakwe zao?
- Tatizo la ukosefu wa ajira na ugumu wa maisha linazidishwa na tabia ya vijana wengi kuchagua kazi za kufanya. Unadhani Ruthu alikubali kufanya kazi ye yote kwa kuwa hakuwa mwenyeji wa nchi ile au kwa kuwa alikuwa na njozi ya maisha? Boazi ni mfano bora wa matajiri wenye kuwafikiria wale waliokuwa nacho?
- Unadhani Mungu anawafikiria wanyonge wanaofanya kazi katika mazingira magumu ili kujikimu kimaisha? Je unatoa mchango gani kusaidia watu hao? Mara nyingine tumeshuhudia ndugu wa karibu wakiwa wagumu kujihisisha na shida za ndugu zao kuliko watu baki. Unajifunza nini kutoka kwa Boazi kuhusiana na hali hii?
MASWALI YA KUJADILI: RUTHU 3:1-18
- Naomi alifanya sehemu yake kulipa ukarimu wa mkwewe kwa kuntengenezea mazingira ya kupata mchumba. Unadhani wazazi wana nafasi ye yote katika kuwatafutia vijana wao wachumba wanaofaa? Unadhani mpango wa uchumba wa Ruthu na Boazi ulitoka kwa Mungu? Je ikiwa binti anasukumwa kutoka kuolewa na mvulana aliyekidhi vigezo vyake atafanyaje kufikisha ujumbe huo kwa njia nzuri kwa yule mvulana?
- Je tofauti ya umri ni sababu ya watu waliopendana kutooana? Tofauti kubwa ya umri kati ya wanaooana ina athari gani katika ndoa? Je ni jambo linalokubalika kwa wachumba kutembeleana hali wakiwa wanaishi peke yao? Kuna faida na hasara gani ikiwa watafanya hivyo? Ni sahihi kumpa mchumba zawadi? Je uchumba ukifa una haki ya kuidai zawadi hiyo?
- Boazi alikuwa muungwana maana hakumwingilia kingono Ruthu walipokuwa peke yao usiku. Una maoni gani kwa vijana wanaofanya ngono wakati wa uchumba? Kuomba ili Mungu akupe mchumba peke yake hakutoshi. Jitihada za kujiweka katika mazingira ya kuchumbiwa kama alivyofanya Ruthu ni za muhimu. Una jambo gani ulilojifunza kutoka kwa Ruthu linalofaa kuigwa na vijana wa leo?
MASWALI YA KUJADILI: RUTHI 4:1-22
- Boazi alimpa mkubwa wake fursa ya kuamua juu ya urithi wa ndugu yao Elimeleki.n Unazungumziaje wale ambao kutoka na uwezo wa kiuchumi huwadharau wakubwa wao na kujitwalia madaraka ya kuongoza koo na familia zao isivyo halali? Ndoa ni jambo nyeti linalostahili kuhusisha viongozi wa dini. Unatoa maoni gani juu ya ndoa Hza kimila na kuchukuana bila utaratibu zinazozidi kushamiri leo?
- Ukoo wa Elimeleki walitambua za wajane Naomi na Ruthi na kupitia baraza la wazee wakaweka utaratibu wa kuwasadia. Kwa nini katika familia zingine wajane wananyanyaswa na kunyimwa haki zao? Je kanisa linaweza kufanya nini kuwasaidia wajane wasinyanyasike? Ndoa zinazofungwa kanisani zina faida gani ukilinganisha na zile za kienyeji?
- Unadhani ni furaha ya kiasi gani alikuwa nayo Ruthi - mwanamke mjane na ambaye hakubahatika mtoto alipoolewa na kupata mtoto. Hii inatufundisha kutokata tamaa katika maisha? Kuolewa kwa Ruthi na kuzaliwa kwa mtoto katika ukoo wa kifalme waYuda kulileta faraja gani kwa Naomi katika uzee wake? Unadhani alipata kitu cha kutuliza maumivu ya kufiwa?
- Iliwezekanaje Ruthi Mmoabi awe katika ukoo wa Yesu? Unadhani Orpa (mjane mwenza wa Ruthi) kwa kurudi kwake Moabu kulimpotezea fursa ya kuwa miongoni mwa jamii ya Israeli?