Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

HUDUMA ZA WASHIRIKI

SEMINA YA VIONGOZI WA HUDUMA ZA WASHIRIKI

CHIMBUKO LA HUDUMA ZA WASHIRIKI:

Idara katika kanisa la Mungu huanzishwa kutegemeana na mahitaji yanayojitokeza katika kipindi husika. Uanzishwaji wa Idara unakusudia kuliweka jukumu fulani muhimu mikononi mwa watu wachache watakaolishughulikia kwa umakini zaidi badala ya jukumu hilo kusimamiwa na kanisa lote kwa ujumla. Kabla idara ya mashemasi haijaanzishwa inaelekea kanisa zima lilisimamia shughuli za kulihubiri Neno au shughuli ya uinjilisti. Baada ya kuoneka haja ya kuwepo kitengo kinachojishughulisha na utatuzi wa migogoro yaani mashemasi ndipo na watu wengine maalumu wakawekwa kusimamia shughuli za uenezaji wa Neno au Uinjilisti.

“Hata siku zile wanafunzi walipokuwa wakiongezeka hesabu yao, palikuwa na manung'uniko ya Wayahudi wa Kiyunani juu ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahauliwa katika huduma ya kila siku. Wale Thenashara wakawaita jamii ya wanafunzi, wakasema, Haipendezi sisi kuliacha neno la Mungu na kuhudumu mezani. Basi ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho, na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili; na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile Neno”. (Matendo 6: 1-4)

SIFA ZA VIONGOZI WA HUDUMA ZA WASHIRIKI

Kiongozi wa huduma za washiriki ni mtu anayetwishwa jukumu la kusimamia mipango ya Uinjilisti ya kanisa katika mwaka husika na katika eneo lote la kanisa husika. Mtu huyu ni lazima awe ameshuhudiwa kuwa na karama za uinjilisti, kuwa na shauku ya kuona roho nyingi zikiokolewa, na mwenye juhudi na moyo usiokata tamaa.

WAJIBU WA VIONGOZI WA HUDUMA ZA WASHIRIKI

Idara ya huduma za washiriki huhusisha idara zote zilizopo kanisani isipokuwa idara ya mashemasi. Idara hii ina viongozi wakuu wawili. Mmoja huitwa Kiongozi wa Huduma na mwingine huitwa Katibu wa huduma. Viongozi hawa wote ni wajumbe wa Baraza la Kanisa.

MAJUKUMU YA IDARA YA HUDUMA

Kama nilivyosema awali idara hii hushughulikia kuona kama idara na washiriki wote wameingizwa katika shughuli za uinjilisti katika mwaka husika. Jambo la kwanza wanapoanza kazi mwanzo wa mwaka ni kuitisha kikao kitakachojadili idadi ya roho zilizolengwa kuongolewa katika mwaka husika, mbinu zitakazotumika kuzileta roho hizo, maeneo mapya yatakayopewa kipaumbele, tarehe na mahali ambapo matukio mbalimbali ya uinjilisti yatafanyika, gharama za uendeshaji wa shughuli hizo za uinjilisti; upatikanaji wa vyombo vya kuhubiria, Biblia, Vijizuu,  masomo ya Sauti ya Unabii na Biblia Yasema, chakula cha wanatimu, vibali vya mikutano na Bima, wahubiri, Kwaya na malazi yao, zawadi mbalimbali na matangazo yatakayohitajika.

Mbinu kuu zinazotumika kupata roho makanisani kwa sasa ni Mikutano ya hadhara (Effort), Huduma za Utabibu, Shule na Vyuo vyetu, Vitabu vyetu kupitia wainjilisti wa vitabu, Runinga na Radio na Sabato za Wageni. Njia hizi kwa kawaida hutumika kama hatua ya kuvuna kile kilichopatikana kutokana na madarasa ya Biblia Yasema yaliyokuwa yanaendelea katika kipindi kinachotangulia matukio hayo. Uamuzi wa kujitoa kwa ubatizo katika matukio hayo ya uinjilisti kwa sehemu kubwa hutokana na vijizuu vilivyokuwa vikigawanywa kwa nyakati mbalimbali, mahusiano ya kifamilia, kirafiki, kiukoo, kiujirani, na kikazi na pia kama matokeo ya kufuatilia hotuba za mikutano iliyopita iliyofanyika sehemu mbalimbali ambayo iligusa mioyo yao. Ili kufanikisha shughuli zake idara hii inapaswa kufanya yafuatayo:

KUCHUKUA NA KUTUNZA TAKWIMU MUHIMU ZA WATU ZA ENEO  ANALOLISHUGHULIKIA:

Takwimu hizi ni zile zinazoonesha eneo lake lina vijiji na vitongoji vingapi, idadi ya wakazi wote wa eneo hilo kwa mujibu wa sense iliyopita ni wangapi, na kati ya wakazi hao wanaume, wanawake na watoto ni idadi gani, Waadventista na wasio Waadventista ni kiasi gani. Takwimu hizo zitamsaidia kujua ukubwa wa jukumu lake la kupeleka injili lilivyo. Lengo la idara ya huduma ni kuona wote walioko kwenye eneo lake wanafikiwa na ujumbe wa malaika watatu na wanaupokea.

MKAKATI WA KULIFIKIA ENEO LOTE KWA INJILI:

Mkuu wa Idara na msaidizi wake wataweka mipango ya muda mfupi, muda wa kati, na muda mrefu wa namna ya kulifikia eneo lote la kanisa lake na Injili ya Milele. Ataainisha maeneo yaliyofikiwa na injili na yale mapya, na kila mwaka ataonesha mipango aliyonayo kwa ajili ya maeneo mapaya na ya zamani. Kila mwaka atachagua eneo moja kwenye maeneo mapya na eneo jingine kwenye maeneo ya zamani ambako kanisa litaweka msisitizo wake wa uinjilisti.

KUZIGAWIA IDARA MAJUKUMU YA KIUINJILISTI KWA MWAKA HUSIKA:

Viongozi wa idara hii watazigawia idara zilizopo kanisani maeneo ya kufanyia kazi na roho wanazotakiwa kuzivuna kama matokeo ya kazi yao ya uinjilisti kwa mwaka husika. Idara hizo katika vikao vyao zitatakiwa zioneshe mbinu mbalimbali watakazotumia kufikia lengo hilo na kuwaridhisha viongozi wa idara ya huduma kama kweli mbinu hizo pekee zinatosha kufikia malengo hayo. Mchana wa Sabato ya kwanza ya mwezi kwa kawaida hutumika kwa ushuhudiaji na kutoa taarifa ya kazi. Kama katika mbinu zilizopendekezwa kuna Effort na Sabato za Wageni, uongozi wa idara utaratibu ili kuhakikisha shughuli hizo haziingliani na shughuli zingine za aina hiyo hiyo za idara au kanisa zinazofanywa wakati huo huo na mahali hapo hapo.

BARAZA LA MALENGO YA UINJILISTI YA MWAKA:

Idara ya Huduma za washiriki itafanya kikao chake cha pili kitakachopokea mipango yote ya kiuinjilisti ya maidara kwa mwaka na kuifanyia marekebisho pale yanapohitajika na kisha watayaunganisha pamoja ili kuyawasilisha kwenye baraza la kanisa. Mipango hiyo itaonesha kinachokusudiwa kufanyika, tarehe kitakapofanyika, wahusika wa tukio, gharama zitakazotumika, na zitakavyopatikana gharama hizo. Vyanzo vya mapato kwa kawaida ni Bajeti ya Kanisa, michango ya washiriki, Harambee, Wafadhili wa ndani na nje, na Miradi.

VITENDEA KAZI VYA INJILI:

Idara ya huduma inatakiwa kujua mahitaji ya vitendea kazi vya kanisa vinavyohitajika kwa ajili ya shughuli za uinjilisti na kuhakikisha vitendea kazi hivyo vinapatikana kwa wakati ama kwa kuvinunua ama kwa kuviazima. Vitendea kazi hivi vimegawanyika katika makundi mbalimbali kama ifuatavyo;

Vyombo vya electronic vya kuhubiria ambavyo ni Generator, Projector, Amplifier, Mixer, Speakers (box na horn), Microphone za nyaya, Microphone zisizo na waya (Wireless Microphone) na receiver zake, Stabilizer, Extension cables na nyaya za umeme na za spika, DVD au Video Receiver, Laptop n.k.

Vitendea kazi vya mfumo wa karatasi ambavyo ni Biblia Yasema, Masomo ya sauti ya Unabii, Masomo ya mgunduzi, Masomo ya Sauti ya Unabii, Vijizuu, Matangazo ya kubandika na ya kugawa, Kadi za mialiko, magazeti, vitabu, Picture rolls, Biblia, Vibali vya mkutano, Bima n.k.

Vitendea kazi vya mfumo wa samani ambavyo ni Jukwaa la wahubiri na waimbaji, jukwaa la box na horn speaker, Viti vya wahudumu na vya mkutano, Vibanda vya kukaa wasikilizaji kuwakinga na mvua au jua na gharama zote za ujenzi.

Huduma za Malazi na chakula ni eneo jingine ambalo linahitaji kuwekewa mipango kamili. Ni lazima ijulikane idadi ya watu watakaohitaji chakula, malazi na huduma zingine muhimu. Ni jukumu la wakuu wa idara husika wakishirikiana na viongozi wa huduma kuona kuwa chakula cha kutosha kinakusanywa mapema kabla ya tukio na malazi ya wanatimu, kwaya na mhubiri vinajulikana mapema. Washiriki binafsi waombwe kusaidia wawezavyo kwenye eneo hili ili kupunguza gharama.

MAFUNZO

Jukumu lingine la idara ya huduma za washiriki ni kutoa mafunzo ya namna ya kufanya uinjilisti. Mafunzo haya yamegawanyika katika maeneo mbalimbali. Eneo la kwanza ni mafunzo ya namna ya kuhubiri kwenye mikutano ya hadhara na mikutano ndani ya kanisa. Mafunzo haya hutolewa kwa washiriki wote na baada ya kupimwa wale watakaooneka wamemudu wataorodheshwa ili kutumika katika maeneo husika. Eneo jingine la mafunzo ni mafunzo ya kuingia nyumba kwa nyumba yatakayofuatiwa na mafunzo ya kuendesha madarasa ya Biblia Yasema na mbinu za kukatisha shauri. Wakuu wa idara pia wataendesha mafunzo ya Walei na Wamishionari ili kuongeza idadi yao maana ni watu muhimu kwa kazi ya uinjilisti. Pamoja na mafunzo haya viongozi wa idara wanaweza kuendesha semina ya kujadili mafungu tata na kuyapatia ufumbuzi.

 HUDUMA KWA JAMII

Idara ya huduma za washiriki itawahamasisha washiriki kufanya huduma mbalimbali za kusaidia wenye mahitaji wanaopatikana kwenye jamii wanayokusudia kuipelekea injili. Huduma hizo ni pamoja kutoa nguo, fedha, chakula, matibabu, ushauri wa afya, ndoa, na msuala ya uchumi, kujenga au kukarabati nyumba, choo, visima, kulima shamba, kushona nguo zilizotatuka, kuunga kandambili, kurepea viatu, majembe, sufuria, miavuli, kunoa majembe, mapanga, na mashoka, kufundisha tuition watoto n.k. Shughuli hizi hujenga mahusiano mema  na kufungua njia kwa ajili ya Injili.

WALEI KABLA NA BAADA YA MKUTANO:

Viongozi wa idara hii wataorodhesha Walei na Wamishionari waliopo kwenye kanisa lao ili kuwatumia kwa ajili ya maeneo mapya yaliyokusudiwa kufanywa mikutano ya injili mwaka huo. Walei wapelekwe kwenye eneo la tukio miezi mitatu kabla na waendelee kubaki angalau miezi mitatu baada ya mkutano kwisha. Gharama za walei na wamishionari hawa zitolewe na kanisa au wafadhili wa ndani na nje. Washiriki wote wahimizwe kutoa vyakula, samani, na nguo kwa ajili ya walei watakaojitolea kulea waumini wapya.

TAARIFA YA SHUGHULI ZA KUONGOA ROHO

Kila baada ya mkutano wa Injili kwisha na mwishoni mwa robo katibu wa Huduma ataandika taarifa inayoonesha mikutano ya injili iliyofanyika, watu waliosikia ujumbe huo (utafanya makisio kulingana na umbali ambao vyombo vyenu vilimudu kurusha mahubiri na idadi halisi waliohudhuria), waliopokea Ujumbe (hapa utachukua jumla ya watu walijitoa kutaka kuendelea kujifunza), na idadi ya waliojitoa kwa ubatizo. Taarifa itaonesha pia gharama zilizotumika na kama makdirio mliyojiwekea yalifikiwa au hayakufikiwa na utapendekeza kwa nini yalifikiwa na kwa nini hayakufikiwa.

MIIKO YA VIONGOZI WA HUDUMA ZA WASHIRIKI

Viongozi wa idara ya huduma hawaruhusiwi kuwatumia kwa kazi ya Injili watu waliozuiwa na uongozi wa Konferensi au wenye msimamo unaokwenda kinyume na kanisa. Hawaruhusiwi kualika mhubiri au kwaya yoyote bila taarifa na idhini ya mchungaji. Mialiko yoyote kutoka au kwenda nje ya mtaa ni lazima ipitie kwa mchungaji na kasha Konferensi na bima ya dola moja (sawa na Tshs 1,700/= kwa sasa) kwa mtu mmoja ni lazima ilipwe kwa ofisi ya Konferensi majuma mawili kabla ya safari. Ni mwiko kwa mikutano yetu kuvuka muda tuliopangiwa au kukiuka masharti tuliyopewa isipokuwa kama kuna haja hiyo basi viongozi waonane na uongozi wa mahali pale mapema.